Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tundu Antiphas Mughwai Lissu (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa sababu muda nitazungumzia masuala mawili tu na yote yanahusu mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza linahusu masuala ya kinidhamu ya Majaji. Tarehe 30 Novemba, 2014, Bunge hili lilipitisha Azimio kwamba Rais aunde Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza Majaji wa ESCROW. Majaji wawili ambao kwa ripoti maalum ya uchunguzi ya Kamati ya Kudumu ya Bunge hili iliwakuta wamechukua mamilioni ya fedha kutoka kwa yule bwana wa ESCROW James Rugemalira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Majaji wawili Aloysius Mujulizi na Profesa Eudes Ruhangisa. Bunge lilipitisha Azimio, baadae Mheshimiwa Rais Kikwete alipozungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, tarehe12 Disemba mwaka huo alisema kwamba, suala la nidhamu ya uchunguzi wa Majaji hao linapelekwa kwa Tume ya Utumishi wa Mahakama lianzie huko, halafu baadaye ndiyo liletwe kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapema mwaka jana na baadaye mwishoni mwa mwaka jana Mheshimiwa Jaji Mkuu aliviambia vyombo vya habari kwamba uchunguzi wa Majaji hawa wawili ulikuwa umeisha kamilika! Leo ni mwaka mmoja na nusu, tangu Azimio la Bunge, kuhusu Majaji wa ESCROW pamoja na wengine litolewe, taarifa iko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tafadhali Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujumuisha, utuambie Majaji waliochukua shilingi milioni mia nne, mia nne kutoka kwa Rugemalira na Bunge hili likapitisha Azimio kwamba washughulikiwe kwa mujibu wa Katiba, kitu gani kinatokea na huu ukimya ni wa nini?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala la nidhamu ya Majaji ni suala muhimu sana, mahakama zetu zimechafuka, tunapenda kulalamika Mahakimu, Mahakimu, Mahakama zetu katika ngazi zote zimechafuka! Kitu cha ajabu kabisa ni kwamba tumekuwa tunachukua hatua dhidi ya Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo once in a long while, Majaji hawaguswi! Hatuna malaika wala watakatifu katika Mahakama Kuu, hatuna malaika wala watakatifu katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania, kitu cha ajabu ni kwamba mara ya mwisho na hii ni muhimu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania amechukuliwa hatua ilikuwa mwaka 1991, Mheshimiwa Jaji Mwakibete alipoundiwa Tume ya Uchunguzi akaondolewa madarakani. Miaka zaidi ya 25 Mahakama ni rushwa tupu na kila mtu analalamika hapa! Lakini ikifika kuchukua hatua, kila mtu anaogopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hili ambalo liko wazi kabisa la waliokutwa wamechukua mamilioni ushahidi wa nyaraka upo, tuambiwe imekuwaje? Tusinyamaziwe tafadhali, mahakama zetu kama tunakubali kwamba kutumbua majipu ya muda mrefu ni kitu muhimu, haya ya wazi haya, tusiyaache hilo la kwanza.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha pili ambacho kinasemwa sana ni hiki kinachoitwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Mafisadi. Mara nyingi ninapoona watu ambao wanaonekana onekana kama wana akili hivi, kama wamesoma hivi, kama wanajua sheria hivi, halafu wanazungumza vitu vya ajabu kabisa, nakuwa nafedheheka sana.
Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa na Mahakama ya Mafisadi tangu mwaka 1984; kwa miaka 32 leo tuna Mahakama ya Mafisadi. Sasa haiitwi jina hilo inaitwa kwa kiswahili maarufu inaitwa Mahakama ya Wahujumu Uchumi. Ilianzishwa wakati wa crackdown ya Sokoine wa wahujumu uchumi na walanguzi. Mahakama Kuu inaposikiliza kesi zote za rushwa, Mahakama Kuu inaposikiliza kesi zote za kutakatisha fedha haramu, Mahakama Kuu inaposikiliza kesi zote za hujuma ya uchumi, makosa kwa mfano yanayohusiana na Sheria za Wanyamapori, Sheria za Dawa za Kulevya and so on and so forth, inakaa kama Mahakama ya Mafisadi, imeanzishwa kwa mujibu wa sheria. Sasa unashangaa watu wanaoonekana kama wanafahamu wanazungumza, tunampongeza Mheshimiwa Rais sana, ameamua kutuanzishia Mahakama ya Mafisadi nonsense!
Mheshimiwa Naibu Spika, nani aliyewaambia hakuna Mahakama ya Mafisadi? Kama mnataka kuibatiza tu semeni, halafu ukiuliza eehe! huo Muswada uko wapi? Aah tutaianzisha tu kama Division ya Mahakama Kuu, nonsense! Division ya Mahakama Kuu inahitaji Sheria, kuna Division ya Mahakama Kuu ya Ardhi, imeundwa kwa sheria. Division ya Mahakama Kuu ya Ajira Kazi, imeundwa kwa Sheria, Division ya Mahakama Kuu ya Biashara, imeundwa kwa sheria, hii Division ya Mahakama Kuu ya Mafisadi, sheria yake iko wapi? Hii ambayo mnasema mtaianzisha sijui mwezi Julai!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mambo haya, ambayo tunaambiwa tuna wataalam wa sheria wanaofahamu fahamu, why are they allowing these nonsense to go on. Kwa nini watu wenye utaalam wa sheria, madaktari hapa na wengine maprofesa, kwa nini wanaacha ujinga huu unaendelea kusambaa? Nafahamu na kwa sababu nimeshughulikia haya masuala kwa miaka mitano Bunge lililopita, kwamba kuna matatizo makubwa kuhusiana na uendeshaji wa kesi za ufisadi, nayafahamu, lakini kusema kwamba hakuna mahakama ya kuyashughulikia ni kuthibitisha ujinga tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka kupigana sawa sawa na tatizo la ufisadi, tuzungumze kuna tatizo gani katika Mahakama ya Economic and Organized Crimes Court iliyoanzishwa na Marehemu Sokoine mwaka 1984. Tusijifanye tunatengeneza mambo, hakuna kitu kipya hapa, Mahakama hii ipo for the past 32 years, ina matatizo yes, tuyazungumze hayo matatizo. Lakini tusizungumze as if hakuna kitu, tunaanzishiwa kitu kipya na Rais John Pombe Magufuli. Akizungumza Rais, namsamehe siyo mwanasheria, akizungumza Daktari wa Sheria nafedheheka sana kwa sababu anajua kama hajui anapaswa kujua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa vile muda hakuna, hivi umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu ni miaka mingapi? Hivi huyu Jaji Mkuu wa kwetu hajafikisha huo umri wa kustaafu? Wenzake wote aliokuwa nao darasa moja, Jaji Msofe, Jaji Masati, Dkt. Steven Bwana, walishastaafu miaka mingi, Jaji Mkuu wetu umri wake wa kustaafu ni lini? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. TUNDU A.M. LISSU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, naomba majedwali ya marekebisho ambayo tumeyapeleka Ofisi ya Katibu asubuhi hii yaingizwe kwenye mjadala huu kwa sababu Kanuni ya 86(11) ipo wazi. Kama tunataka kutunga sheria basi tufuate Kanuni za utungaji wa sheria, majedwali yetu yote tuliyoyapeleka yaingizwe ili sheria hii tuijadili na tuipitishe kama inavyotakiwa na Kanuni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kufafanua mambo kadhaa ambayo yamezungumzwa utafikiri ni mambo mapya lakini siyo mambo mapya hata kidogo. Naomba sana Mwalimu wangu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe anisaidie kama nitakuwa nakosea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, inazungumzwa hapa kwamba suala la accreditation ya waandishi wa habari ni jambo jipya kwamba hatuwezi tukaachia holela tasnia hii, ni kitu kipya, ni kitu muhimu na kadhalika. Siku ambayo Sheria ya Magazeti ilitungwa mwaka 1976 siku hiyo hiyo ilitungwa Sheria ya Shirika la Habari la Tanzania (SHIHATA) na sheria ile pamoja na mambo mengine iliipa SHIHATA mamlaka ya kuandikisha waandishi wa habari na kuwapa vitambulisho. Kwa hiyo, kwa muda wa miaka 24 ambayo Shirika la Habari Tanzania lilikuwepo kwa mujibu wa sheria, moja ya majukumu yake ilikuwa accreditation ya waandishi wa habari. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe kama nakosea naomba aniambie Mwalimu wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mwaka 2000 ilipopitishwa Sheria ya Kufuta Shirika la Habari Tanzania, sheria ile ilikasimu mamlaka yaliyokuwa ya SHIHATA kwa Idara ya Habari Maelezo isipokuwa mamlaka ya ku-accredit waandishi wa habari yaliondolewa. Mamlaka ya kusajili waandishi wa habari yaliondolewa kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Kufuta SHIHATA. Kama nakosea Mwalimu wangu nisahihishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kitu muhimu ni kwa nini mamlaka ya accreditation yaliondolewa mwaka 2000 na Sheria ya Kufuta SHIHATA. Sababu ipo kwenye taarifa ya Tume ya Rais ya mfumo wa Chama Kimoja au Mfumo wa Vyama Vingi maarufu kama Tume ya Nyalali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1991 Tume ya Nyalali ilipotoa taarifa yake pamoja na mapendekezo mengi mengine ilisema kwamba Sheria ya Magazeti, Sheria ya SHIHATA iliyokuwa inaweka utaratibu wa waandishi wa habari kuandikishwa, asipoandikishwa hafanyi kazi, sheria hiyo inakwenda kinyume na matakwa ya Katiba ya uhuru wa habari na uhuru kwa vyombo vya habari. Ndiyo maana accreditation ya waandishi wa habari iliondolewa kwa sheria iliyofuta SHIHATA. Kama nakosea Mwalimu wangu naomba unisahihishe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuulizane kama accreditation ya waandishi wa habari iliondolewa kwa sababu inapingana na Katiba kwa sababu inazuia uhuru wa habari kwa nini inarudishwa sasa hivi? Tukijibu hilo swali tutakwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, masharti haya ambayo yako kwenye Muswada huu, masharti ya udhibiti wa magazeti yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika sheria inayoitwa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1928 (Newspapers Ordinance 1928). Ndiyo iliweka utaratibu huu ambao umepigiwa kelele tangu mwaka 76 ilipotungwa hii Sheria ya Magazeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kudhibiti magazeti kwa kutumia mamlaka ya usajili …
Umeelezewa vizuri sana na mwandishi wa kitabu hiki, The Media History of Tanzania.
Lengo la sheria ya kikoloni, lengo la Sheria ya Magazeti ya mwaka 1928 ilikuwa kuhakikisha kwamba an indigenous press haikui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya usajili wa magazeti ya mwaka 1928 yaliingizwa kama yalivyo na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Sasa kwa wasiofahamu, naomba mkaangalie mjadala wa Bunge wa mwaka 76, Edgar Maokola Majogo alizungumza kitu gani. Edgar Maokola Majogo alisema sheria hii tunayopitisha ina harufu nyingi ya kasumba za kikoloni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii masharti ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1928 yaliyoingizwa kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, miaka 40 baadaye yameingizwa kama ilivyo katika Muswada huu. Maana yake ni kwamba tangu mwaka 1928 utaratibu wetu wa udhibiti wa magazeti, wa udhibiti wa habari falsafa haijabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, vifungu vyote vya uchochezi vilivyopo katika Muswada huu vimeingizwa kama vilivyo kutoka kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Sasa hapa ni muhimu tujue vilitoka wapi kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1952 miaka miwili kabla TANU haijaanzishwa wakoloni wa Kiingereza walileta sheria, iliingizwa katika Kanuni yetu ya Adhabu kwenye Penal Code sheria ambayo iliingiza makosa yote ya uchochezi kama yalivyo katika Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na kama yalivyo katika Muswada huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mjadala wa Baraza la Kutunga Sheria LEGCO la mwaka 1952, wakati vifungu hivi vinaingizwa walikuwa wanasema kuna haja ya kudhibiti wanaopinga Serikali, kuna haja ya kudhibiti wachochezi. Ndiyo maana, Mwalimu wangu naomba anisaidie, watu wa kwanza kupatikana na hatia ya uchochezi kwa mujibu wa sheria hii walikuwa watatu. Wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, wa pili alikuwa Robert Makange, Mhariri wa Gazeti la ...
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2016
MHE. TUNDU A. LISSU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia vile vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia kwa kiasi kikubwa katika Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana za Serikali na kama bado muda utatosha nitazungumza kidogo kuhusu marekebisho ya Sheria ya Wanyamapori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa kiingereza unasema unaosema the road to hell is paved with good intentions (njia ya kwenda jehanamu imepambwa kwa nia njema). Sasa nia njema peke yake haiwezi ikatosha tunapotunga sheria. Lazima tuangalie potential consequences za hiyo sheria tunayoitunga. Kwa hiyo, kutuambia kwamba lengo la muswada ni zuri kwa hiyo tupitishe ni kutuelekeza jehanamu kwa kutegemea tu nia njema. Hatuwezi tukafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu unapendekeza hivi; Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iwe mdeni wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Serikali ya Jamhuri ya Muungano inakopa pesa say kutoka Benki ya Dunia au kutoka Mabenki ya Kibiashara ya Kimataifa au nchi za kigeni, masharti ya mkopo huo yanadai kwamba ulipwe kwa muda fulani, kwa riba fulani, kwa fedha za kigeni. Halafu kwa Muswada huu, Serikali ya Zanzibar tunaikopesha sisi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano inaikopesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa masharti yale yale ambayo tumepewa sisi na Benki ya Dunia au Mabenki ya Biashara au Taasisi zingine za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tuulizane tu. Tusitegemee tu nia njema, what if they do not pay? What if they are unable to pay, for whatever reasons. Itakuwaje Serikali ya Zanzibar ikishindwa kulipa huo mkopo kwa masharti yale yale ambayo sisi tumekopa nje (Serikali ya Jamhuri ya Muungano) itakuwaje? Tutakamata mali zao? Tutawashtaki? Tutafanyaje? Wakishindwa kulipa itakuwaje? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, muswada unapendekeza vilevile kwamba Serikali inakopa pesa nje kwa masharti hayo, masharti ya mikopo ya kimataifa sio marahisi sana, inakopa nje halafu linakuja Shirika la Umma kwa mfano UDA au Shirika la Elimu Kibaha au National Insurance Corporation au Air Tanzania, Serikali inaikopesha kwa masharti yale yale ambayo imekopa nje ilipe kwa dola, ilipe riba, ilipe kwa muda fulani; ndiyo masharti yanayozungumzwa kwenye muswada huu. Tusizungumzie nia njema, nia njema itatupeleka kuzimu.
Mheshikmiwa Mwenyekiti, itakuwaje Air Tanzania wakishindwa kurudisha hiyo hela Serikalini? Itakuwaje Shirika la Elimu Kibaha wakishindwa? Itakuwaje Halmsahauri ya Wilaya ya Ikungi, imekopa pesa Serikalini kwa utaratibu huu ikishindwa kulipa? Kwa sababu Halmashauri za nchi hii karibu zote zinaitegemea Serikali kwa karibu asilimia 90, zimenyang‘anywa vyanzo vya mapato, hazitozi kodi za majengo na mapato mengi zimenyang‘amywa, zikishindwa kulipa itakuwaje? Kwa hiyo, haitoshi tu kuwaambia watu nia njema, nia njema, tunaunga mkono nia njema ya Serikali, tutaenda kuzimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye suala la utaratibu huu kwa Serikali ya Zanzibar kwa sababu watu hawaelewi matatizo makubwa ambayo yanakabili Muungano wetu kwa sababu ya matatizo kama haya. Kumekuwa na mgogoro kwa wasiofahamu (mwalimu wangu anafahamu vizuri sana) kumekuwa na mgogoro nchi hii kwa zaidi ya miaka 40 juu ya mapato ya Muungano, zaidi ya miaka 40. Jumbe aling‘olewa madarakani mojawapo kwa sababu ya hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar wamekuwa wanadai kwamba pesa zinazokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano hawazipati. Tukatengeneza utaratibu unaosema wapate asilimia 4.5 ya fedha zinazokuja kama misaada ya kibajeti. Kwa misaada ya bajeti wapate asilimia 4.5; hawajawahi kupata hata hiyo, haijawahi kutokea. Kwenye misaada ile ambayo sio ya kibajeti, hela za basket fund na hizo tunawapa kwenye budget support na budget support wazungu wameiondoa, hiyo general budget support imeondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Zanzibar miaka yote wanasema hatupati mgao wetu halali na ndiyo maana iliundwa Tume ya Pamoja ya Fedha mwaka 1984 wakati Jumbe anaondolewa madarakani. Ndiyo maana Katiba iliingizwa maneno kwamba kutakuwa na A Joint Account (Akaunti ya Pamoja) ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar ili kutatua hili tatizo la Zanzibar kutopata mgao wake miaka yote, tangu mwaka 1984 halijashughulikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Pamoja ya Fedha ilipendekeza tangu mwaka 2006 ikarudia tena mwaka 2010, tutatue matatizo ya mgawanyo wa mapato ya Muungano, haijatokea. Na kama kuna sababu kubwa ya resentment juu ya Muungano ya Wanzanzibari ni hii. Sasa badala ya kutibu magonjwa hayo, badala ya kutibu matatizo hayo, tunapendekeza hivi, wawe wadeni wetu wa kudumu. Wakitaka hela za maendeleo waje tuwakopeshe. Tuwakopeshe sawa na UDA, tuwakopeshe sawa na ATCL, tuwakopeshe sawa na Halmashauri ya Wilaya ya Newala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza utaratibu ambao utazaa matatizo makubwa zaidi ya Muungano na hatuwezi tukafanya hivi tukiwa; we can only do this if we are blind. Tunaweza tukafanya hivi kama ni vipofu, na kama hatujui lakini kama tunafahamu matatizo ya mgawanyo wa mapato ya Muungano this is not the way to go. Tafadhali sana tusitegemee nia njema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna chombo cha Kikatiba kimeundwa tangu mwaka 2003 lakini kilitungiwa sheria mwaka 1996, miaka 20 iliyopita. Tume ya Pamoja ya Fedha, chombo cha Kikatiba, hiki ndicho kinatakiwa kifanye maamuzi juu ya masuala haya; mikopo, misaada na dhamana za Serikali ya Muungano kwa fedha za Muungano kwa ajili ya mambo ya Muungano; haijawahi kufanya kazi, badala yake tunaletewa vitu kama hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mimi sijui nisemeje, lakini naomba niwaambieni Waheshimiwa Wabunge tunatengeneza bomu, na tunalitengeneza tukiwa na macho meupe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho la mapendekezo ya Sheria ya Wanyamapori. Ni hivi, muswada huu unapendekeza kwamba mtu akituhumiwa kwa nyara ya Serikali, amekamatwa na nyamapori, kabla hajapelekwa mahakamani, kabla hajashtakiwa, hakimu atoe kibali, hiyo nyamapori iuzwe au ipikwe iliwe au iwe otherwise disposed. Halafu hakimu akishaamua kumbuka kesi haijafunguliwa, kibali cha hakimu tayari ni ushahidi kamili wa jambo litakalobishaniwa, endapo hiyo kesi itafunguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sijawahi kuona ni mwanasheria kidogo, wanasheria waliomo humu ndani hebu nisaidieni hiyo ni ya wapi ambapo ushahidi unakubaliwa kabla kesi haijafunguliwa? Ni ya wapi hiyo? Mwanasheria Mkuu wa Serikali seriously unatuletea hii, nani atakayepona? Maana utafungwa tayari hakimu ameshakubali ushahidi, kabla mwenyewe hujashtakiwa, nani atakayepona? Kuna safeguard zipi dhidi ya watu watakaosingiziwa? Nchi hii kama hamfahamu magereza yamejaa, yamefurika kwa watu wanaosingiziwa kesi za ajabu ajabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunahalalisha mambo hayo Waheshimiwa kwa kuleta mapendekezo kama haya. Nyamapori, hakimu anasema eeh nimeshaona hii ni ushahidi tayari, kabla kesi haijafunguliwa umekwenda na maji.
Waheshimiwa Wabunge, hili si tatizo la CHADEMA, sio tatizo la UKAWA, tunawatengenezea Watanzania mazingira ambayo watakandamizwa sana, tusikubali. Tusikubali kuambiwa nia njema itawaumiza watu wetu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.