Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tundu Antiphas Mughwai Lissu (4 total)

MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kuuliza swali dogo la nyongeza kuhusiana na tatizo la Madawati. Mwaka 2015 tuliletewa taarifa na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kwamba kila Halmashauri ya Wilaya ya nchi hii imepelekewa madawati siyo chini ya 708 yaliyotokana na chenji ya rada iliyotoka Uingereza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yangu ya Wilaya ya Ikungi haijapata dawati hata moja. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atueleze, madawati 708 ya Halmashauri ya Ikungi yalipelekwa wapi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua upungufu wa madawati hasa zaidi kwenye Shule za Msingi na hata Sekondari. Serikali katika jitihada hiyo, tulianza kuamua kama Taifa kuhakikisha kwamba tunaondokana na tatizo la watoto wetu kukaa chini. Pia tukapata fursa inayotokana na fedha ya chenji ya rada ambayo Mheshimiwa amejaribu kuuliza na madawati yametengenezwa na baadhi ya Halmashauri nchini zimepata. Nakumbuka nina shule zangu kama mbili ikiwemo Shule ya Msingi Malolo, imepata.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. GEORGE B. SIMBACHAWENE): Sasa kwa sababu Mheshimiwa ameitoa hii taarifa, tutajaribu kuangalia tupitie tuweze kuona kwa nini kama alikuwa yupo kwenye mgawanyo wa yale madawati katika Jimbo lake, hayakuweza kufika na yako wapi? Siyo rahisi kupata jibu la moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo Serikali tunatambua hili na tumejipanga. Tunataka kuhakikisha kwamba ndani ya muda mchache sana ujao tunakuwa na madawati kwa nchi nzima. Nitakuja na Mpango na Maelezo, nitaomba Waheshimiwa Wabunge wote mniunge mkono.
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba niulize swali la nyongeza. Mwaka 2013 nilitembelea Kumbukumbu ya Vita ya Majimaji, iko Songea na ni vizuri sana kwamba angalau tumeweka kumbukumbu ya mashujaa waliopigana Majimaji; isipokuwa katika Kumbukumbu ya Mashujaa wa Majimaji kuna watu mle ambao wamepewa heshima kwenye kumbukumbu ambao hawakuwa wamezaliwa wakati Majimaji inapiganwa. Chumba kikubwa kabisa kwenye Kumbukumbu ya Maji Maji kinamhusu Laurence Mtazama Gama ambaye hakupigana Majimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumejenga Kumbukumbu ya Majimaji ili kumkumbuka Laurence Gama au kukumbuka waliokufa kwa sababu ya Majimaji?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni ya kumbukumbu za mashujaa ni kuwakumbuka wale walioshiriki katika vita husika. Kwa hiyo, hii taarifa ya kwamba kuna mtu ambaye amewekwa kama kumbukumbu wakati hakushiriki, pengine imetokana na kwamba kumbukumbu hiyo inajumusiha zaidi ya mashujaa wa Majimaji. Inawezekana kuna mashujaa wengine ambao wanajumuishwa. Kwa hiyo, naomba nipate fursa hii tuliangalie vizuri suala hili ili tuweze kulitolea jibu la uhakika zaidi.
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali la nyongeza linalofanana na swali ambalo ameuliza Mheshimiwa John Heche.
Mheshimiwa Naibu Spika, jimboni kwangu kuna eneo lina dhahabu na kampuni moja inaitwa Shanta Mining imeingia na kupewa eneo hilo tangu mwaka 2004. Leo ni miaka 13 haijaanza kuchimba madini, haijajenga mgodi na kwa taarifa za kitaalam ambazo nimeziangalia, hizo deposits za dhahabu siyo kubwa sana za kuweza kupewa kampuni ya kigeni. Namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri alieleze Bunge lako kama Serikali ina mpango wa kulitwaa hilo eneo na kuwarudishia wananchi ili wachimbaji wadogo wadogo wenyeji wachimbe kwa sababu baada ya miaka 13 hawachimbi, hawa wawekezaji inaelekea hawana mpango au uwezo wa kuchimba dhahabu kwenye hili eneo la Mang‟oni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, kwanza namshukuru Mheshimiwa Tundu. Nimekuwa nikiwasiliana naye mara kwa mara kuhusiana na kumpatia eneo. Niseme tu, ni kweli kabisa Kampuni ya Shanta Mining ilipewa leseni ya utafiti tangu mwaka 2004. Nieleze kidogo, muda wa kufanya utafiti kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, awali ya kwanza ni miaka minne, baada ya miaka minne anapewa tena miaka mitatu ya kuendelea na utafiti na hatimaye anamalizia miaka mitatu. Kwa hiyo, ni kweli kabisa shughuli za utafiti zinachukua muda mrefu. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, baada ya kukamilisha utafiti, kampuni inatakiwa ianze shughuli za uchimbaji, hivi sasa kama ambavyo Mheshimiwa Tundu anasema haijaanza, matarajio ya mgodi ni kuanza shughuli za uchimbaji kati ya Juni, 2018. Kwa hiyo, baada ya shughuli za uchimbaji kuanza, basi maeneo mengine yata maeneo mengi yatashughulikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia yapo maeneo ambayo Kampuni ya Shanta Mining tunazungumza nayo. Hivi sasa tumezungumza na Kampuni ya Shanta Mining, inatarajia kuwa na maeneo ya hekta kama 200 ambayo inaweza ikawaachia wananchi wa Singida ili wachimbe kwa ajili ya uchimbaji mdogo kwa sababu yanaweza kuonekana siyo manufaa kwa kampuni hiyo. Baada ya taratibu hizo kukamilika, Mheshimiwa Tundu Lissu basi wananchi wako watawasiliana na Serikali tu na watapewa maeneo hayo.
MHE. TUNDU A. M. LISSU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na huo mgodi unaopangwa kujengwa wa Kabanga Nickel, Serikali itapata asilimia ngapi kama mrahaba kwa mujibu wa Sheria za Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Tundu Lissu, Mbunge mashuhuri kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimueleza Mheshimiwa Tundu Lissu; Mrabaha unaotozwa kwa sasa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 madini yote ya ujenzi ikiwa pamoja na madini ya chumu na iron ambayo ni nickel ni asilimia tatu, lakini madini mengine ya dhahabu ni asilimia nne na madini mengine ni asilimia moja, madini ya almasi ni asilimia tano. Kwa hiyo, asilimia tutakazopata kutoka kwenye mgodi ni pamoja na hiyo. (Makofi)