Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu (15 total)

MHE. HUSSEIN M. BASHE (K.n.y. MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU) aliuliza:-
Kifungu na 97(1)(b) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kinamtaka mwekezaji kabla hujaanza shughuli za kujenga mgodi ili kuzalisha madini ni lazima ahakikishe kwamba anawasilisha na kutekeleza mpango wa fidia, ujenzi wa makazi mapya na kuwahamishia wananchi waliopisha ujenzi huo kwenye makazi mapya yaani “compensation, reallocation and resettlement plan” kulingana na matakwa ya Sheria ya Ardhi.
Je, ni lini Serikali itarekebisha Sheria ya Ardhi ili iendane na matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Namba103 la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi yenye madini pamoja na kutawaliwa na Sheria ya Madini Na. 14 ya mwaka 2010 pia hutambuliwa na Sheria mama za sekta ya ardhi. Kwa kutambua hilo, kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Madini kinatoa tafsiri ya mmiliki halali wa ardhi (lawful occupier) kuwa ni mtu ambaye anamiliki ardhi chini ya Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999. Hivyo, ni wajibu wa wamiliki wa migodi kuhakikisha kwamba wanatekeleza masharti ya Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi Na. 4 na 5 za mwaka 1999 kifungu cha 3(1)(f) vinabainisha kwamba ardhi ina thamani na kwamba thamani hiyo inazingatiwa wakati wowote katika mapatano yoyote yanayoathiri maslahi hayo. Sheria hizi zinasisitiza kwamba lazima ardhi ilipwe fidia kamili kwa bei ya soko, haki na kwa wakati kwa yeyote ambaye ardhi yake imetwaliwa. Aidha, katika Kanuni za Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, Kanuni ya 10 ya “The Land (Compensation Claims) Regulations” ya mwaka 2001, inaelekeza kuwa fidia lazima iwe ya fedha lakini Serikali inaweza kutoa fidia katika muundo wa kitu kimoja kati ya hivi au vyote kwa pamoja:-
(a) Kiwanja kinacholingana na kile kilichotwaliwa;
(b) Jengo au majengo yanayolingana na yale yaliyotwaliwa;
(c) Mimea au mbegu; na
(d) Kutoa nafaka na vyakula vya msingi kwa wakati maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999, imezingatia matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010. Hivyo, kwa sasa hakuna sababu ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi ili iendane na Sheria ya Madini katika suala la ulipaji wa fidia.
MHE. HUSSEIN M. BASHE (K.n.y. MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU) aliuliza:-
Mji wa Igunga unakabiliwa na tatizo kubwa la maji kutokana na kupanuka kwa kasi wakati miundombinu ya maji ni ile ile na pia imechakaa sana na haitoshelezi mahitaji ya maji kwa wakazi wake:-
Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Mji wa Igunga maji ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya maji ili kupunguza tatizo la maji katika Mji wa Igunga ambapo kwa sasa hali ya huduma inayotolewa ni asilimia 60 ya wakazi wote. Mahitaji ni lita za ujazo milioni 3.5 wakati huduma inayotolewa ni lita za ujazo milioni 2.5. Hii ni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mtambo wa kusafisha na kutibu maji mwezi Januari, 2013. Hata hivyo Serikali inakusudia kuboresha hali ya huduma ya maji kwa mji huo na imeshaanza mchakato wa kutoa maji Ziwa Viktoria kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo umbali wa kilometa 12 kila upande kutoka bomba kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za kupata Wakandarasi wa ujenzi wa mradi huu zinaendelea ambapo mradi unategemewa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017. Kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na ulazaji wa bomba kuu, ujenzi wa matenki mapya kwa Vijiji na Mji wa Igunga, ulazaji wa mabomba mapya ya usambazaji na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji. Hivyo, kukamilika kwa mradi huu kutaongeza huduma ya maji kufikia asilimia mia moja.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Mbuga ya Hifadhi ya Wembere ni mbuga iliyotelekezwa na Serikali na kupoteza sifa za kuendelea kuwa hifadhi na sasa inatumika na wafugaji kulisha mifugo na wakulima kulima alizeti na mpunga kwenye eneo hilo.
Je, ni kwa nini Serikali isibadilishe matumizi ya mbuga hiyo badala yake ipimwe na kutumika kwa wafugaji na wakulima na kuondoa migogoro inayoendelea kati ya wakulima na wafugaji ambayo wakati mwingine inasababisha mauaji na uharibifu wa mali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mbuga ya Wembere ipo ndani ya mipaka ya mikoa ya Tabora na Singida. Umuhimu wa eneo hili ni pamoja na kuwa chanzo cha maji yanayokwenda katika maziwa Eyasi na Kitangire. Mbuga hiyo pia ni maarufu kwa aina (species) za mimea na wanyamapori mbalimbali na muhimu kwa mazalia ya ndege mbalimbali wenye sifa za Kitaifa na Kimataifa. Eneo hilo linatambuliwa Kimataifa kama mahsusi kwa kundi muhimu la uhifadhi wa ndege duniani tangu mwaka 2001.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa eneo hilo linakabiliwa na changamoto ya uvamizi kwa shughuli za kilimo na ufugaji kama alivyobainisha Mheshimiwa Mbunge, bado Serikali haijaitelekeza mbuga hiyo na kinyume chake eneo hilo linatumika kwa shughuli za uwindaji wa kitalii ambapo linaliingizia Taifa fedha za kigeni na kutoa ajira kwa wananchi waishio kando ya eneo hilo. Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 2013/2014 hadi 2015/2016 Serikali imepata kiasi cha dola za Kimarekani 142,450 kutokana na shughuli za uwindaji katika vitalu vilivyoko ndani ya eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu kiikolojia wa eneo hilo Kitaifa na Kimataifa Wizara yangu itaendeleza majadiliano na Serikali ya Mkoa wa Tabora na Singida ili kuona uwezekano wa kupandisha hadhi eneo hilo ili kuwa na uhifadhi endelevu wa bioanuai zilizopo.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Moja kati ya jukumu la Benki Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 51(2)(a) cha Sheria ya Benki Kuu, 2016 ni kutunza dhahabu safi.
Je, kwa nini Serikali imekataa kutunza dhahabu safi katika Benki Kuu wakati Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazozalisha dhahabu safi na kwa wingi Afrika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, jukumu la msingi la Benki Kuu ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuwa na utulivu wa bei kwa ajili ya ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa. Ili kufanikisha azma hii, Benki Kuu inadhibiti ongezeko la ujazi wa fedha kwa kutumia nyenzo mbalimbali zikiwemo kuuza dhamana na hati fungani za Serikali na kushiriki katika soko la jumla la fedha za kigeni kati ya mabenki ambayo ni Interbank Foreign Exchange Market.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza jukumu lake la msingi, Benki Kuu hutunza hazina ya rasilimali za kigeni zinazotosha kuagiza bidhaa nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne. Hazina ya rasilimali za kigeni inaweza kuwa dhahabu-fedha yaani monetary gold au fedha za kigeni. Uamuzi kuhusu hazina itunzwe vipi unazingatia vigezo mbalimbali vikiwemo vile vya kudumisha thamani, wepesi wa kubadilisha yaani convertibility na faida inayopatikana kwa kuwekeza hazina hiyo.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu kwa muda mrefu haijaweka dhahabu kama sehemu ya hazina ya rasilimali za kigeni kutokana na bei ya dhahabu katika soko la dunia kutokuwa tulivu na hivyo kusababisha uwezekano wa kupunguza thamani ya hazina ya rasilimali ya nchi. Mfano, tumeshuhudia bei ya dhahabu ikishuka kutoka dola 1,745 za Kimarekani kwa wakia moja Septemba, 2012 hadi dola za Kimarekani 1,068 Disemba 2015. Aidha, ununuzi na uuzaji wa dhahabu unahitaji ujuzi maalum ambapo kwa kuzingatia jukumu la msingi la Benki Kuu ambalo tumelieleza hapo juu, Benki Kuu haijajijengea uwezo katika eneo la biashara ya dhahabu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali isidhibiti matumizi holela ya dola nchini ili kupunguza
utakatishaji wa fedha na kuimarisha ukuaji wa uchumi kama zinavyofanya nchi
nyingi duniani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa
Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti matumizi holela ya fedha za
kigeni, Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza
usimamizi katika maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ambapo taarifa za kila
muamala wa fedha za kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa. Hatua
zimechukuliwa pia kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa
na mabenki ni ile inayohusu shughuli za kiuchumi tu ili kulinda thamani ya shilingi
yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tamko na mwongozo uliotolewa na
Serikali mwaka 2007, ulieleza kuwa bidhaa na huduma zinazowalenga watalii au
wateja wasio wakazi wa Tanzania, bei zake zinaweza kunukuliwa kwa sarafu mbili
yaani shilingi ya kitanzania na sarafu ya kigeni na malipo kufanyika kwa sarafu
ambayo mlipaji atakuwa nayo. Pia, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe
kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa kuruhusu soko huru la fedha za kigeni
hapa nchini ni hatua ya makusudi ambayo ilichukuliwa na Serikali yetu ili
kuiwezesha nchi kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha za kigeni. Mfano,
kufikia Desemba, 2015 akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni
4,093.7 wakati amana za fedha za kigeni za wakazi wa Tanzania zilikuwa dola za
Kimarekani milioni 2,933.1 na rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi
cha dola za Kimarekani milioni 1,021.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, utulivu wa urari wa biashara ya nje umetokana
na sera huru ya fedha za kigeni ambayo imechangia kuimarisha uchumi kwa
zaidi ya miaka 10 iliyopita. Wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita ulikuwa ni asilimia saba ikiwa ni wastani wa juu sana
ikilinganishwa na nchi zingine duniani. Mfano, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 5.4 katika kipindi hicho, wakati
ule wa nchi zinazoibukia kiuchumi ulikuwa ni asilimia 5.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, njia zinazotumika kutakatisha fedha ni pamoja
na kuziingiza fedha haramu kwenye taasisi za fedha na kuziwekeza katika
rasilimali halali kama ardhi na nyumba. Baadhi ya mambo yanayowapatia
wahalifu fedha haramu ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya, rushwa,
ujangili, ujambazi, ukwepaji kodi na kadhalika. Fedha zinazotokana na shughuli
za kihalifu zinaweza kuwa shilingi za Kitanzania, dola za Kimarekani au fedha
nyingine yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kanuni ambazo zinafuatwa na vyombo vya
fedha ili kuzuia utakatishaji wa fedha zote zilizopatikana kutoka vyanzo haramu
na siyo dola tu. Benki Kuu kupitia jukumu la usimamizi wa taasisi za fedha
hufuatilia mabenki ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinafuatwa.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH (K.n.y. MHE. DKT. DALALY
P. KAFUMU) aliuliza:-
Wilaya ya Igunga ni miongoni mwa Wilaya zinazolima pamba kwa wingi nchini:-
Je, ni lini Serikali itajenga au kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na nguo na hata mafuta ili kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga nchi ya viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mweyekiti, Serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi nchini (mass consumption), zinazotoa ajira kwa wingi na zinazotumia malighafi za ndani ya nchi kama inavyojieleza kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano. Bidhaa hizo ni pamoja na nguo zitokanazo na pamba inayolimwa maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Igunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha uzalishaji katika mnyonyoro mzima wa thamani katika zao la pamba unaofanyika, Serikali iliandaa mkakati wa kuendeleza zao la Pamba, Nguo hadi Mavazi (Cotton to Clothing Strategy –C2C) uliozinduliwa mwezi Mei, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huo ambao utekelezaji wake unaendelea, unahamasisha uendelezaji wa zao la pamba na uongezaji wa thamani wa zao hilo kuanzia kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na nguo na hata kuongeza thamani ya mafuta ya kula yatokanayo na mbegu za pamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza kasi ya uwekezaji katika Sekta ya Viwanda, Wizara yetu imendaa mkakati wa kuharakisha ujenzi wa viwanda (Fast Tracking Industrialization in Tanzania) na imekamilisha utafiti juu ya vikwazo zinavyochelewesha uwekezaji nchini. Ni imani yangu kuwa utekelezaji wa maandiko tajwa hapo juu na juhudi za uongozi wa Mkoa wa Tabora zitatuwezesha kuvutia uwekezaji Wilaya ya Igunga.
DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Zaidi ya asilimia 70 ya eneo la Jimbo la Igunga lilikuwa limefunikwa na maji ya Ziwa Victoria lakini baada ya Ziwa hilo kukauka, eneo hilo limebaki kuwa ni mbuga inayojaa maji wakati wa masika hivyo kufanya ujenzi wa barabara za vijiji kuwa wa gharama kubwa sana na Halmashauri ya Wilaya ya Igunga haina uwezo wa kifedha kujenga barabara hizo.
Je, kwa nini Serikali isiandae mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara za vijijini katika Wilaya ya Igunga na Wilaya nyingine nchini zenye tatizo kama hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua tatizo la udongo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini yaani TARURA imepanga kufanya utafiti wa udongo huo ili kuona kama unafaa baada ya kuongezewa kemikali (additive) badala ya kuondoa na kuleta udongo mwingine na hivyo kupunguza gharama za ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Halmashauri ili ziweze kupitika kwa kipindi chote. Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga shilingi milioni 336.8 ambazo zilitumika kufanya matengenezo ya barabara kilometa 119.3, madaraja 8 na kalvati 10. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/18 Hamashauri hiyo imetengewa shilingi bilioni 1.26 ambapo hadi tarehe 30 Septemba, 2017 fedha zilizopokelewa ni shilingi milioni 241.9. Taratibu na kumpata mkandarasi zinaendelea.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Kutokana na wananchi wa vijijini kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya sheria na haki zao, Watendaji wa Vijiji na wa Kata wakishirikiana na Mahakama za Mwanzo na Mabaraza ya Ardhi huwaonea na kuwadhulumu kwa kuwabambikizia kesi na kuwanyang’anya ardhi:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua za kukomesha tabia hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba yapo malalamiko dhidi ya baadhi ya Watendaji wa Kata na Vijiji ambao wamekuwa wakilalamikiwa na viongozi na wananchi kuwabambikizia kesi na kushirikiana na Mahakama za Mwanzo na Mabaraza ya Ardhi kuwaonea na kuwadhulumu ardhi wananchi hao kwa kuwanyang’anya ardhi yao. Serikali inakemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi wa umma wasio waaminifu na ambao wanakiuka maadili ya utumishi wa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukomesha tabia hii, Serikali inaelekeza kwa viongozi na watendaji mambo yafuatayo ya kuzingatia:-
• Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wahakikishe wanasimamia uzingatiaji wa maadili ya watendaji walio chini yao.
• Watendaji wote katika ngazi zote za mamlaka za Serikali za Mitaa wanatakiwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miiko na maadili katika utekelezaji wa majukumu yao.
• Serikali haitasita kumchukulia hatua Mtendaji yeyote atakayekiuka sheria, kanuni, taratibu na maadili ya kazi yake, ikiwemo kujihusisha na tabia ya ubambikiziaji kesi wananchi na kuwanyang’anya ardhi;
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha inasimamia kikamilifu maadili ya watumishi wa umma ili kuongeza nidhamu katika utumishi wa umma na haitasita kuchukua hatua mara moja dhidi ya Mtendaji yeyote wa Kata au Kijiji atakayethibitika kutumia vibaya madaraka yake ikiwemo kubambikia kesi wananchi kwa lengo la kuwanyang’anya ardhi. Nitoe wito kwa viongozi na wananchi wote nchini kuhakikisha wanafichua utendaji na watumishi wa umma wenye tabia kama hii ili waweze uchukuliwa hatua stahiki.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Mwaka 2015 Serikali ilianzisha Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga kwa lengo la kusogeza karibu huduma kwa wananchi na kuleta maendeleo, lakini tangu wakati huo hadi leo hii, Mamlaka hiyo haijapatiwa fedha za kujiendesha na kutoa huduma kwa wananchi:-
(a) Je, ni lini Mamlaka hiyo itatengewa bajeti ili iweze kujiendesha na kufanya kazi zake kwa ufanisi?
(b) Je, ni lini Mamlaka hiyo itapatiwa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mji huo na kujenga barabara za lami kilometa nne zilizokuwa zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais wakati wa Kampeni za Uchaguzi za mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mji Mdogo huanzishwa kwa mujibu wa Sheria za Serikali za Mitaa, Sura ya 287, kifungu 13 - 21. Pamoja na vyanzo vya mapato vya Mamlaka ya Mji Mdogo kuainishwa katika Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kifungu cha (8), Mamlaka hizo siyo Mamlaka kamili na hufanya kazi chini ya usimamizi wa Halmashauri za Wilaya husika. Hivyo, Mamlaka ya Mji Mdogo Igunga imekuwa ikiandaa mipango na bajeti zake kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na imekuwa ikipata mgao wa fedha kama zipatavyo Halmashauri nyingine nchini kutokana na upatikanaji wa fedha.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliahidi kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 4 na katika mwaka wa fedha 2016/2017 barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 0.67 ilikarabatiwa kwa gharama ya Sh.287,068,098. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali itajenga barabara yenye urefu wa kilometa 1.164 kwa kiwango cha lami katika Mji Mdogo wa Igunga, Sh.406,664,816 zimeshapelekwa na mkandarasi amefikia 5% ya utekelezaji wa mradi. Serikali itaendelea kujenga barabara za lami Wilayani Igunga kupitia TARURA kwa kadri fedha zinavyopatikana.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU) aliuliza:-
Gereza la Wilaya ya Igunga linakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa ngome, hakuna Ofisi za Mkuu wa Gereza na Utawala, hakuna nyumba za askari lakini pia gereza hilo ni dogo na linahudumia wafungwa na mahabusu wa kiume tu, wafungwa na mahabusu wa kike hupelekwa Gereza Wilaya ya Nzega.
Je, ni lini Serikali itajenga Gereza la Wilaya ya Igunga ili liweze kutoa huduma bora kwa wafungwa mahabusu Wilayani Igunga?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa gereza la mahabusu Wilaya ya Igunga ulianza mwaka 2003 ili kuwapokea na kuwahifadhi mahabusu na wafungwa kutoka Wilaya ya Igunga ambao walikuwa wakipelekwa na kuhifadhiwa katika Gereza la Nzega ambalo nalo ni dogo na hivyo kusababisha msongamano mkubwa. Ujenzi huo bado haujakamilika kwani unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa gereza hilo utakapokamilika kutakuwa na maeneo yote muhimu yanayotakiwa kwenye gereza kama vile ngome, ofisi, mabweni ya wafungwa na mahabusu, jiko, bwalo la chakula na litakuwa na uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu wa jinsia zote.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati na Madini wamepungua sana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita:-
(a) Je, ni nini kimesababisha hali hiyo?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa Wawekezaji wanaendelea kuja ili kukuza uwekezaji kutoka nje (Foreign Direct Investment] (FDI)?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vichocheo vikuu vitatu vya uwekezaji katika Sekta ya Madini katika nchi yoyote, cha kwanza ni jiolojia inayoashiria uwezekano wa uwepo wa madini (prospective geology). Pili ni mwenendo wa bei ya madini husika kwenye Soko la Dunia na tatu Sera za Uchumi Mkuu (Macroeconomics) za nchi husika. Ilani ya CCM tunayoitekeleza hivi sasa ilizingatia vigezo hivi kwa kuhimiza kujenga uwezo wa Geological Survey of Tanzania ili waweze kugundua mashapo ya madini, kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuboresha miundombinu na kuongeza thamani ya madini ili yawe na bei nzuri kwenye soko la dunia na kubadili Sheria ya Madini ili kuongeza uwazi na manufaa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miaka mitano nchi yetu imeendelea kupokea wawekezaji kwenye sekta ya madini. Jumla ya leseni 102 za uchimbaji mkubwa (Special Mining Lenience) na wa kati (Mining License) zimetoelewa kati ya mwaka 2012/2013 hadi 2016/2017, ikiwa ni wastani wa leseni 20 kwa mwaka. Aidha, mwaka wa fedha 2012/2013 hadi 2016/2017 leseni 3,136 za utafutaji wa Madini (Prospecting License) zilitolewa, hii ikiwa ni wastani wa leseni 627 kwa mwaka. Mwaka 2017/2018, tumepokea maombi 26 ya Special Mining License na Mining License, yaani uchimbaji wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepokea maombi 818 ya leseni za utafiti wa madini (Prospecting License). Tume ya Madini iliyoundwa hivi karibuni inaendelea kupitia maombi hayo na iwapo yatabainika kukidhi vigezo vya kisheria leseni hizi zitatolewa na hivyo kuendelea kuchangia kuongezeka kwa Foreign Direct Investment (FDI). Kwa takwimu hizi, bado wawekezaji wanaonesha nia ya dhati kuwekeza nchini kwani nchi yetu inakidhi sifa tatu nilizoainisha hapo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuandaa mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji na kutangaza fursa zilizopo nchini. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile ujenzi wa barabara, reli, kupanua bandari, kujenga miundombinu, maji, umeme, gesi na mawasiliano kuelekea maeneo yanayotazamiwa kuanzishwa migodi. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kuwapatia wataalam vitendea kazi ili kuwawezesha kuongeza kasi ya kufanya tafiti za kina za maeneo yenye madini nchini. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE.DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Katika Ilani ya CCM kuhusu huduma za afya nchini ni kujenga zahanati katika vijiji na kituo cha afya katika kila kata; kwa sasa Jimbo la Igunga lina vituo vya afya viwili tu katika kata 2 kati ya 17 na zahanati kwenye vijiji 19 tu kati ya vijiji 68:-

(a) Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya kwenye kata 15 zilizosalia?

(b) Je, ni lini Serikali itajenga zahanati kwenye vijiji 49 vilivyosalia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa NaibuSpika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 kwa ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya kote nchini kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo. Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ilipokea shilingi milioni 800 kwa mwaka wa fedha 2018 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya Igurubi na Simbo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kituo cha Afya cha Simbo ambacho ujenzi wake upo asilimia 97, fedha hizo zilitumika kumalizia majengo mawili ambayo ni jengo la upasuaji, nyumba ya mtumishi pamoja na ujenzi wa majengo mapya manne ambayo ni maabara, jengo la uzazi, jengo la kufulia na jengo kuhifadhi maiti. Aidha, kituo hicho kimeanza kupokea vifaa tiba kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Kwa upande wa Kituo cha Afya Igurubi, ujenzi unaendelea na umefikia asilimia 70. Jumla ya majengo manne mapya yamejengwa ambayo ni maabara, jengo la uzazi, jengo la kufulia na jengo la kuhifadhi maiti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya kwa awamu katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha. Ahsante.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Madini ya Tanzanite yanapatikana nchini Tanzania pekee, juhudi za kufanya madini haya kuchimbwa na Watanzania pekee kwa Kanuni za Madini za mwaka 2004 na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 hazijaweza kuzaa matunda:-

(a) Je, kwa nini Tanzania isiyatangaze madini ya Tanzanite kuwa ni Nyara za Taifa itayovunwa na Serikali pekee ili kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa Taifa letu?

(b) Je, kwa nini Serikali isiende kujifunza nchini Zimbabwe kuona jinsi ilivyofanikiwa kuyafanya madini ya Almasi kuwa Nyara ya Serikali na hivyo kuleta manufaa makubwa sana kwa nchi hiyo?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatambua upekee na umuhimu wa madini ya Tanzanite. Kwa muktadha huo, ilipelekea tarehe 20/9/2017 kuliamuru Jeshi la Wananchi wa Tanzania kujenga ukuta wenye urefu wa kilometa 24.5 kuzunguka eneo hilo. Lengo likiwa ni kudhibiti utoroshwaji wa madini ili kupata manufaa stahiki ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, eneo la Mirerani ambako Tanzanite inapatikana lilitangazwa kuwa eneo lililodhibitiwa (Mirerani Controlled Area) kwa GN 450 ya mwaka 2002. Lengo la hatua hiyo ni pamoja na kuthamini upekee na umuhimu wa madini hayo na kudhibiti upotevu wa mapato yanayotokana wa Madini ya Tanzanite ili kuongeza manufaa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Madini ya Tanzanite yanachimbwa na Watanzania katika Vitalu A, B, C na D-extension. Aidha, kitalu C kimekuwa kikichimbwa kwa ubia kati ya Shirika la STAMICO na Kampuni ya kigeni ya TanzaniteOne Mining Limited (TML). Hata hivyo, tarehe 23 Desemba 2019, STAMICO na TML waliachia eneo hilo na kupewa surrender certificate ya leseni yao na sasa eneo hilo limerudishwa kwenye usimamizi wa Serikali. Baada ya kuachiwa kwa eneo hilo, utaratibu maalum unaandaliwa wa namna bora ya kuligawa kwa kutoa leseni za uchimbaji wa kati kwa Watanzania wenye uwezo wa kulichimba na kuongeza mchango katika uchumi wa madini.

Mheshimiwa Spika, ushauri wa kuyafanya madini ya Tanzanite kuwa Nyara za Taifa na kwenda kujifunza katika nchi kama Zimbabwe, ushauri huo tunaupokea.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Asilimia 70 au zaidi ya maeneo ya Kata za Isakamaliwa, Mbutu, Igunga, Nguvumoja, Lugubu na Itumba katika Jimbo la Igunga na Kata za Igoweko katika Jimbo la Manonga yapo ndani ya Mbuga ya Wembere ambayo kwa sasa imekosa sifa ya kuwa hifadhi ya wanyama na wananchi katika Kata hizo wameongezeka na kufanya kukosekana kwa maeneo ya makazi, kilimo na ufugaji na kwa kutokuwepo mipango mizuri ya matumizi bora ya ardhi kwa sababu ya hifadhi hiyo na kusababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji na kuleta mauaji:-


Je, ni lini Serikali italitenga na kulipima eneo la Hifadhi ya Wembere hususan katika maeneo ya Kata hizo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Pori Tengefu Wembere, Serikali inakusudia kulibadilisha hadhi pori hili kuwa Pori la Akiba. Katika zoezi hili alama za mipaka ya hifadhi na maeneo yanayopakana zitapitiwa na kuhakikiwa upya.

Mheshimiwa Spika, aidha, mipango ya matumizi bora ya ardhi hufanyika katika maeneo ya vijiji na husimamiwa na Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Wizara yangu iko tayari kushirikiana na mamlaka hizi na wadau wengine pale itakapohitajika.

Mheshimiwa Spika, mbuga ya Wembere ina ukumbwa wa kilimeta za mraba 8,784 na ilitambuliwa kisheria kuwa Pori Tengefu kwa Tangazo la Serikali Na. 269 la mwaka 1974, pori linapatikana katika Mikoa ya Singida (Wilaya ya Manyoni) na Mkoa wa Tabora (Wilaya za Igunga, Sikonge na Uyui).

Mheshimiwa Spika, Pori Tengefu Wembere ni ardhi oevu (Chepechepe) ambayo ni muhimu Kitaifa na Kimataifa kwa kuwa ni chanzo cha maji dakio na chujuo la maji ya Ziwa Kitangiri na Eyasi. Pori hili ni mazalia na ushoroba wa wanyamapori ambao ni kiunganishi pekee cha mfumo wa ikolojia wa Hifadhi za Taifa ya Ruaha na Serengeti, mapori ya akiba ya Rungwe, Kizigo, Muhezi na Ugalla. Aidha, pori ni makazi na mazalia ya ndege wahamao ambapo mwaka 2001 utafiti wa Kimataifa ulibaini uwepo wa zaidi ya spishi 12 za ndege walio hatarini kutoweka.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa, pori hili linatumika kwa uwindaji wa kitalii na utalii wa picha ambapo fedha inayopatikana hutumika kwa ajili ya uboreshaji wa huduma za jamii kupitia Halmashauri za Wilaya husika.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-

Mwaka 2018 ulikuwa msimu wa mvua nyingi sana zilizosababisha kubomoka kwa mabwawa ya maji kwenye Kata za Kinungu, Nguvumoja, Mwamashimba, Nanga, Bukoko na Mbutu na kuwaacha wananchi wa vijiji zaidi ya 24 bila maji; maeneo haya ni mbuga na hayana maji chini ya ardhi hivyo wananchi hutegemea mabwawa hayo tu. Aidha, Halmashauri ya Igunga haina uwezo wa kifedha kuyakarabati mabwawa hayo mara moja:-

Je, ni kwa nini Serikali isilete mradi mkubwa wa kukarabati miundombinu ya maji katika kata hizo kuwaondolea wananchi hao tabu ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Jimbo la Igunga kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mwaka 2018 kulikuwa na mvua nyingi zilizonyesha na kuharibu miundombinu ya malambo katika Kata za Kinungu, Nguvumoja, Mwamashimba, Nanga, Bukoko na Mbutu na kuwaacha wananchi wa vijiji zaidi ya 24 bila ya huduma ya maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari inaendelea na ujenzi wa mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka bomba kuu la KASHWASA kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Wilaya ya Uyui, ambao unatekelezwa kwa gharama za dola za Marekani milioni 268.35, fedha ambazo mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India. Katika mradi huo vipo vijiji mbalimbali vya Kata Nanga na Mbutu zitapata huduma ya maji kupitia mradi huo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kukarabati miundombinu iliyoharibiwa na mvua hizi kwa Kata za Kinungu, Nguvumoja, Mwambashimba na Bukoko kwa kadri fedha zinavyopatikana ili kuhakikisha wananchi hawa wanapata huduma ya maji kama ilivyokuwa awali.