Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Lazaro Samuel Nyalandu (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. LAZARO S. NYALANDU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi iliyowasilishwa kwa umahiri na Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeleta mpango kabambe na wa makini wenye lengo la kuinua kilimo nchini na kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi. Nashauri Wizara iendelee kuimarisha na kuboresha ulinzi wa rasilimali za samaki katika Bahari Kuu eneo la kiuchumi la Tanzania (Strategic Economic Zone); na kudhibiti wavuvi haramu ambao wanatoka Mataifa kama vile Japan, China, Greece, Korea na kwingineko.
Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya samaki wanaovuliwa nchini ikidhibitiwa na kuhakikisha kodi halali inalipwa, sekta hii itachangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa Pato la Taifa na kuwaendeleza wavuvi wazawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vishirikishwe na Wizara hii katika kuweka ulinzi kabambe wa ufukwe wote wa Pwani tokea mpaka wa Tanzania na Kenya na Mozambique kwa kutumia vyombo vya kisasa ikiwa na pamoja na satellite connectivity unmanned vehicles (drones), helicopters na boats zenye uwezo wa kwenda kasi na kuzikamata manowari za wavuvi haramu. Aidha, napendekeza kuwepo kwa chombo maalum ndani ya Wizara kitakachosimamia mapato ya uvuvi wa Bahari Kuu, kwa kuweka mtandao wa internet unaoruhusu meli za nje kulipia leseni na kuhakikiwa mizigo yao kabla ya kuondoka ukanda wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika kwa kuwa taarifa kadhaa zimeonesha kuwa Tanzania imepoteza dola milioni 50 kutokana na uvuvi haramu, naamini wazo la kuweka regime ya usimamizi itasaidia Serikali kudhibiti na kuongeza matumizi endelevu ya rasilimali za samaki/uvuvi nchini Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima naomba kuunga mkono hoja hii ya Serikali.