Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Magdalena Hamis Sakaya (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa mwelekeo wa bajeti uliowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi alisema Serikali inataka Tanzania kuwa nchi ya viwanda, kuelekea uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwenye hotuba hii imesema itawavutia wawekezaji waje kujenga viwanda hapa nchini, kwa mwendo wa kusubiri wawekezaji waje wajenge viwanda hatuwezi kwenda na kufikia malengo ya Taifa tuliojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda wa miaka 10 sasa kila hotuba ya Viwanda na Biashara inaeleza kuwaita wawekezaji wa kujenga viwanda, ni kwa kiasi gani tumefanikiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeeleza Mkoa wa Tabora kunajengwa kiwanda cha Tumbaku ili kutoa ajira kwa vijana na ku-process tumbaku ambapo asilimia 60 ya tumbaku inalimwa Tabora. Tuelezwe ni mipango gani ya awali iliyofanywa ili kufanikisha azima hii ya Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Makaa ya Mawe kwa wingi sana kule Namtumbo-Songea. Kuna Malori zaidi ya 80 hadi 100 yanabeba makaa yale kila siku na kupeleka Kenya na kwingineko. Serikali itueleze, makaa hayo yanapelekwa huko kwa utaratibu gani, tunanufaikaje na makaa hayo ili kutuongezea nishati na kuokoa misitu yetu inayoteketea kwa uchomaji wa mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora tuna misitu na mbao zenye thamani kubwa. Mbao zile zinasafirishwa kwenda nje na Mikoa mingine kutengeneza Furniture (Samani). Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha tunapata kiwanda cha mbao Mkoa wa Tabora ili vijana wa Tabora wapate ajira na mbao ya Tabora iweze kuwa na thamani zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imekuwa ni dampo la bidhaa ambazo hazina viwango kwa kila kitu, vifaa vya umeme, nguo, viatu, vifaa vya ujenzi na kadhalika. Kwa nini Serikali imeshindwa kuweka sheria za bidhaa hapa nchini? TBS wameshindwa kabisa kudhibiti bidhaa duni hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mpango gani wa kuhakikisha bidhaa feki, duni na dhaifu haziingii hapa nchini? Sheria ya Uwekezaji inamtaka mtu anayekuja hapa nchini kuwekeza anatakiwa kuwa na mtaji wa kuwekeza na kutoa ajira kwa wazawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itueleze, Wachina na Wahindi wanaozagaa Kariakoo na maeneo mengine wakiuza maua, karanga, mitumba na kadhalika wanaruhusiwa na nani? Serikali imeruhusu ajira za wananchi wake zichukuliwe na watu wa nje ambao wanaitwa wawekezaji, tunakwenda wapi? Ni lini Serikali itahakikisha biashara ndogondogo zote hapa nchini zinafanywa na wazawa na hivyo kuwaondoa Wachina wote waliopo Soko la Kariakoo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vilivyobinafsishwa wawekezaji wamebadilisha matumizi na kufanya magodauni, vingine havijalipiwa fedha ya kununuliwa na vingine vimeng‟olewa mashine zote zilizokuwepo. Serikali inasema nini kuhusu viwanda hivi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ihakikishe mazao yote yanachakatwa ndani ya nchi na hivyo kuongeza thamani tofauti na sasa ambapo mazao mengi yanasafirishwa ghafi na hivyo kukosesha mapato mengi Taifa na kupoteza ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itaacha kuagiza samani za maofisini kutoka China na hivyo kununua samani ndani ya nchi kutokana na mbao ya Tanzania. Hii ni aibu kubwa!
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge ni chombo cha uwakilishi. Ndani ya Bunge hili kila Mtanzania anawakilishwa kwa Mbunge waliyemchagua wao wenyewe. Wananchi wana haki Kikatiba kuona live nini wawakilishi wao wanakifanya na nini kinaendelea ndani ya chombo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zote zilizotolewa na Mheshimiwa Waziri kuhusu kuzuia matangazo ya Bunge Live hazina mashiko hata moja.
Mheshimiwa Waziri akiwa Mwanza alipohojiwa sababu hasa alisema Bunge la Kumi 2010 – 2015 lilifanya maamuzi hayo jambo ambalo ni uongo wa mchana kweupe. Sisi tuliokuwepo wakati huo hatukuwahi kujadili suala hilo wala kutoa maamuzi ya kipuuzi kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali leo ieleze Watanzania sababu hasa ya kuzuia matangazo ya Bunge live kwa Watanzania. Kitendo cha TBC kurudia matangazo ya Bunge usiku kuanzia saa 4.30 usiku baada ya kuchuja na kuondoa wasiyotaka yaonekane wakati ambapo watu wamechoka na kazi za kutafuta kipato mchana kutwa na wanatakiwa kupumzika ili wapate nguvu ya kufanya kazi siku inayofuata, ni manyanyaso kwa Watanzania, ni matumizi mabaya ya kodi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaji vya michezo hujengwa kuanzia primary school, secondary school ndipo tunaweza kupata wanamichezo wazuri wenye weledi na wanaoweza kujiajiri kwenye michezo na kuleta heshima kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za michezo zinazotolewa kwa shule zetu kwa watoto wetu huko shuleni ni kidogo sana; hakuna vifaa vya michezo, hawapati mazoezi ya kutosha na walimu wa michezo hawawezeshwi. Serikali imejipanga vipi kuhakikisha michezo shuleni inawezeshwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wanacheza wakiwa shuleni na hata wakiwa majumbani kwao. Viwanja vya michezo kwenye mitaa mingi maeneo mbalimbali hapa nchini yamevamiwa na kujengwa nyumba na shughuli nyingine. Watoto wanacheza barabarani na kila leo wanagongwa na magari, pikipiki na vyombo vingine vya usafiri. Serikali ina mpango gani mahususi kuhalalisha inafanya uhakiki wa viwanja vya watoto wetu vilivyoporwa, kuvamiwa ilimradi kutumiwa na watoto kwa malengo ya michezo na kukuza vipaji vya watoto wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipiga marufuku kuwatumia watoto wadogo kwenye maigizo na kutengeneza mikanda ya sanaa za maigizo. Tumeendelea kuona watoto wadogo wakitumika kwenye maigizo na hivyo kuathiriwa kisaikolojia na kushindwa kufikia ndoto zao. Watoto wenye ndogo za kuwa madaktari wanapoingizwa kwenye maigizo wakati akili zao hazijaweza kuamka, automatically tunawahamisha mwelekeo wa ndoto zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ieleze Bunge, kwa nini watoto bado wanaendelea kushirikishwa kwenye maigizo? Umri wa mtoto unajulikana ni miaka 18 kushuka chini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye hotuba iliyoko mbele yetu na kwa sababu ya muda nienda straight kwenye hoja zangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu tumekuwa tunatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya kujenga miundombinu ya barabara, nyingine za nchi na nyingi pia za jasho la walipa kodi. Kwa bahati mbaya sana barabara hizi zimekuwa zikichukua muda mfupi sana kwa sababu kwanza viwango vya ujenzi ni dhaifu, utunzaji wake ni dhaifu lakini pia tunatumia makandarasi ambao baadhi yao hawana viwango vya kuweza kujenga barabara kwa uhakika. Badala ya kutengeneza barabara angalau tumalize miaka kumi ili tuhame kutoka eneo moja twende eneo lingine tunarudi mle mle huku maeneo mengine hayana barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Wabunge wanazungumzia juu ya kubandua barabara za lami kujenga nyingine wakati mikoa mingine wako kwenye udongo. Miaka 54 ya uhuru tunabandua lami na kurudisha lami pale pale wakati wengine wako kwenye udongo hawajui ni lini watapata barabara za lami. Kwa hiyo, tatizo kubwa ni kwamba hatusimamii vizuri barabara zetu. Ifike mahali tuwe na standards za ujenzi wa barabara nchi nzima. Tuamue kwamba mkandarasi ambaye anashindwa kukidhi vigezo vya matengenezo tunayoyataka asipate kandarasi. Kwa sababu ya kubeba wakandarasi mtu anaharibu huku anapelekwa kule, matokeo yake tunaingiza hasara kubwa kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye barabara nyingi, niseme kabisa barabara zilizotengenzewa ndani ya miaka kumi ya uongozi wa Awamu ya Nne zote ziko kwenye hali mbaya. Nyingi zina mashimo mengi, nyingi zina migongo, nyingi zinaanza kuchimbika kuanzia pembeni, Awamu ya Nne barabara zote zimeharibika. Pamoja na kuwa anasifika kwamba alitengeneza barabara nyingi lakini kaziangalieni, nimefanya utafiti barabara nyingi za uongozi wa Kikwete ziko kwenye hali mbaya kwa sababu usimamizi ulikuwa mbovu. Hatuwezi kuwa na barabara za lami za kutosha kama tunashindwa kuweka standards kwa ajili ya barabara zetu za lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, tumekuwa tunatoa fedha kidogo kidogo kwenye ujenzi wa barabara matokeo yake tunaweka vyombo vya ujenzi barabarani kwa muda mrefu na tunalipa wakandarasi waelekezi kwa muda mrefu, tunapoza fedha nyingi sana za walipa kodi kwa kitu ambacho hakitakiwi. Tunapotengeneza barabara miaka minne, mitano haijakamilika lakini vyombo vinalipiwa, mkandarasi mwelekezi analipwa, how much are we wasting? Ni pesa nyingi sana tunapoteza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe na utaratibu, tunapopanga kutengeneza barabara tuitengee muda, ndani ya mwaka mmoja, miwili ikamilike ili tuokoe fedha na faini tunazolipa kwa ajili ya kuweka vyombo barabarani wakati huo hatutoi fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara zile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la reli. Suala hili ni uchumi wa Taifa. Ni jambo la ajabu kwa nchi inayotegemea kilimo kwa zaidi ya asilimia 80, leo tuna reli kwanza sio za standards, zinabomoka kila siku, lakini kwa kiwango kidogo, ni aibu mpaka leo. Sambamba na kwenda kwenye uchumi wa viwanda, sambamba na kwenda kwenye uchumi wa kati, suala la reli halikwepeki. Kwa hiyo, katika mawazo yote ya Serikali ili tuweze kwenda pamoja lazima suala la reli lipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nilianza kuumizwa na Waziri wa Fedha. Kwanza alikuja na mpango wa kwanza kwamba lazima tutengeneze reli ya kati kwa standard gauge, tulipokwenda Dar es Salaam kwenye semina anasema kwamba tunatafuta wabia na nchi ambazo tuna-share matumizi ya reli hiyo, hatuwezi kutegemea watu wa nchi nyingine, pengine kwao reli si priority lakini ndani ya nchi yetu reli ni priority. Kwa hiyo, ni lazima tujipange sisi wenyewe kuhakikisha kwamba tunajenga reli zetu? Leo tunategemea Burundi, Burundi kwake pengine reli si priority, au Rwanda, it is not their priority, au Kenya, sisi kama sisi tunafanyaje?
Kwa hiyo, suala la reli ya kati na matawi yake ina-cover karibu mikoa 15 ya nchi hii. Wengi wamezungumza kwa msisitizo tunaomba wakati wa ku-wind up kesho tuambiwe tarehe ya kuanza na kumaliza kujengwa reli ya kati na kwa standard gauge, halikwepeki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la upungufu wa mabehewa. Kuna shida kubwa ya upungufu wa mabehewa ya abiria. Reli yote hii ya kati mabehewa ni machache sana matokeo yake imeleta matatizo makubwa. Leo Wabunge walikuwa wanazungumzia suala la bei kwenda juu pamoja na kuwepo kwa walanguzi, shida kubwa ni mabehewa machache. Leo ndani ya Wilaya ya Kaliua kwenye stop station ya Kaliua kwa siku moja, kwanza treni ni siku mbili tu kwa wiki, lakini hiyo siku mbili eti siku kumi, can you imagine? Watu kumi kwenye kituo kwa wiki mara mbili! Reli iko kwenye wilaya yao, wengi hali ya uchumi ni mbaya, hawana uwezo wa kutumia 50,000, 60,000 kwa basi angalau reli ndicho chombo chao wanaambiwa siti kumi. Matokeo yake watu ambao si wasafiri na wanakwenda na vitambulisho wananunua wanakwenda kuziuza mitaani kwa wale wasafiri. Matokeo yake mtu badala ya kununua tiketi shilingi 23,000 ananunua shilingi 40,000 na huwezi kuzuia kwa sababu mabehewa ni machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba ya Waziri, amesema ameongeza mabehewa, lakini mengi ni ya mizigo, mabehewa ya mizigo kutoka 530 mpaka 704, lakini suala la mabehewa ya abiria ni shida kubwa. Pia tuongeze angalau route. Kwa kweli ni jambo la ajabu kuambiwa kwamba Wilaya ya Kaliua reli yote ya kati kituo kimoja, kwa wiki moja wasafiri watu 20, kwa kweli inasikitisha sana. Hatuwezi kukwepa suala la kuendelea kulanguliwa kwa tiketi kama hatuongezi mabehewa lakini pia kama hatuongezi angalau routes za treni tuweze kusaidia wananchi ambao treni pia ni tegemeo lao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, suala lingine ni la mafao ya watumishi wa iliyokuwa TRC waliohamia RITES. Mwaka 2007 walipohama kutoka TRC kwenda TRL waliambiwa watalipwa mafao yao leo ni karibu miaka kumi hawajawahi kulipwa. Tunaomba Waziri wakati ana-wind up atuambie wale watumishi waliohamishwa kutoka TRC kwenda TRL mwaka 2007 mpaka leo hawajalipwa haki zao wanalipwa lini haki zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye barabara za Tabora. Mkoa wa Tabora mpaka tunapoongea umeunganishwa na mkoa mmoja tu, Mkoa wa Singida. Mwanza moja kwa moja mpaka Tabora bado, Mbeya bado, Shinyanya bado, Kigoma bado. Tunaomba sana, kuna barabara hii ya Nyahuwa – Chanya, ni kipande kidogo tu pale, kilometa 85.4 imetengewa fedha kidogo. Ni yale yale ninayoyasema, tukitenga fedha kidogo kidogo tunaleta gharama zaidi. Hebu tuhakikishe kwamba tunaweka fedha za kutosha barabara hii ikamilike ili angalau tuunganishe Dodoma na Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini barabara nyingine ni barabara ya Urambo - Kaliua. Ni barabara muhimu kweli kweli, imetengewa shilingi bilioni tano tu, sasa hizi ni za uchambuzi au za kufanya nini? Barabara ile ni fupi, kilometa 28, tunaomba Mheshimiwa Waziri aweke fedha ya kutosha angalau ikamilike. Leo ukienda pale una mimba changa inatoka, barabara hali ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni ya Kazilambwa - Chagu. Tunashukuru angalau kwa kipande kidogo imekamilika, kutoka Kazilambwa kuja Kaliua tayari, Kazilaumbwa kwenda Chagu kwa maana ya kuunganisha Tabora na Kigoma bado. Fedha iliyowekwa ni kidogo sana labda ni kwa ajili ya uchambuzi, sijui. Naomba barabara hii na yenyewe iweze kutekelezwa ndani ya bajeti hii ili angalau tuunganishe Mkoa wa Tabora na Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni ya kuunganisha kutoka Mpanda – Ugala – Kaliua, Ulyankhulu – Kahama. Ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Kaliua, Mpanda na Kahama. Barabara hii imewekewa fedha kidogo ya uchambuzi, tunaomba kwa bajeti ya mwaka wa kesho ihakikishe inajengwa kwa lami, ni barabara nzuri sana kwa ajili ya uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la viwanja vya ndege. Kiwanja cha Tabora ni matatizo, leo ni mwaka wa nne tangu kimetengewa fedha ya ukarabati, hakikamiliki kwa nini? Nashangaa Wabunge wanaosema kwamba ndege ni anasa, ndege siyo anasa, tunataka uchumi wa kati, tunataka wawekezaji. Leo unamtoa Mchina kutoka Dar es Salaam aingie kwenye makorongo afike Tabora saa ngapi? Angetaka apande ndege straight afike Tabora aangalie eneo la kuwekeza, arudi kwenye shughuli zake. Kwa hiyo, viwanja vya ndege ni uchumi wa nchi hii. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija atuambie kiwanja cha Tabora lini kitakamilika kwa gauge kubwa, kipanuliwe kiweze kuwa kiwanja ambacho kinaingiza ndege kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanja kile ndege kubwa haziingii. Ndege ndogo, nauli kutoka Dar es Salaam mpaka Tabora ni shilingi 450, 000 nani mwenye uwezo huo? Gharama ni kubwa, wananchi wengi hawawezi. Kuna Mbunge kasema hapa tukiweza kuwa na viwanja vikubwa, ndege nyingi zikatua, zenye upana mkubwa hata gharama zinapungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kidogo kuhusiana FastJet, Wabunge wanasema kwamba FastJet ni rahisi, FastJet ni gharama kuliko maelezo, ni aibu. Kwanza mimi niseme FastJet ni wezi, ni wezi kabisa. Leo unachangishwa begi shilingi 200, 000, maji nusu lita shilingi 3,000 hii ni aibu, ni wizi wa hali ya juu. Anakwenda kuchukua maji kwa jumla jumla shilingi 300 kwa nusu lita anakuja kuuza shilingi 3,000 huu ni wizi, hakuna gharama ya unafuu wa aina yoyote.
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Magdalena.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini Serikali inaruhusu Shirika la ndege la FastJet hutoa huduma kwa kuwaibia wateja/abiria kwa kiasi kikubwa hivyo? Ndani ya ndege, maji nusu lita wanauza shilingi 3,000 wakati wanachukua kiwandani kwa bei ya jumla, nusu lita shilingi 300.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikata tiketi ya go and return, ukipata dharura ukashindwa kusafiri tarehe ya tiketi hata ukiwapa taarifa saa 24 kabla ya safari, hela yako inakufa na tiketi imekufa. Begi hata kama lina nguo za mtoto, likizidi kilo moja unalipishwa kuanzia shilingi 100,000 mpaka shilingi 200,000; huu ni wizi mtupu wakati Serikali ipo na inaona. Tunaomba majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawasiliano ya simu; katika Wilaya ya Kaliua kuna maeneo ambayo hakuna minara ya simu na hivyo, wananchi hupata shida kubwa ya mawasiliano. Kata ya Igwisi, kijiji cha Upele na vitongoji vyake vyote, kata ya Tugimlole mpaka kijiji cha Igombe. Kata ya Ulambi, Sigaga mpaka vijiji vya Usinga na Kotonko. Kata ya Igagala mpaka vijiji vya Wachawasome na vitongoji vya Kona Nne, Ukumbanija, Ufulaga. Kata ya Ugunga mpaka vijiji vya Mpilipili na vitongoji vya Kanyanya. Maeneo yote ya Kaliua kuanzia pale mjini mtandao wa Tigo ni wa shida sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninakushukuru kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba ya Wizara ambayo iko mbele yetu. Kwa sababu ya muda nichangie moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka zaidi ya 15 sasa tumekuwa tunashuhudia tunajadili hapa Bungeni suala la makaa ya mawe, tangia sijawa Mbunge alikuwepo Profesa alikuwa anaitwa Profesa Mwalyosi ndani ya Bunge hili, kila akisimama ndani ya Bunge nilikuwa nasikia anazungumzia Mchuchuma, Liganga, makaa ya mawe miaka iliyopita, alikuwa ni Profesa wa mimea na mazingira. Leo nimeingia ndani ya Bunge miaka 10 tunazungumza makaa ya mawe, ni kwa nini tunashindwa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya nishati ya matumizi ya nyumbani? Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija atueleze kuna tatizo gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inaenda kuwa jangwa, hatuna means, kwa sababu umeme haushikiki, hata Mheshimiwa Waziri hawezi kupikia umeme. Mafuta ya taa hayashikiki, gesi haishikiki, tunachemshia vitu vidogovidogo tu, asilimia 80 tunatumia mkaa, nchi inakuwa jangwa. Kama kwa mwezi mmoja Dar es salaam peke yake wanatumia magunia 200,000 kwa takwimu za Waziri can u imagine nchi nzima tunatumia gunia ngapi kwa mwezi mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipoangalia tunaenda kuwa jangwa, lakini tunashangaa tumepewa makaa ya mawe ndani ya nchi yetu, kuna tatizo gani Mheshimiwa Waziri, tunaomba kesho utujibu hapa, kwa nini hatuoni umuhimu wa kutumia rasilimali hii tuliyopewa ndani ya nchi yetu tutoe nishati kwa ajili ya kuitumia, naomba sana Mheshimwa Waziri atuambie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikwenda Likuyu - Namtumbo mwaka juzi, nilikaa pale Namtumbo karibu siku tatu, jambo la kushangaza niliona malori zaidi ya 100 kila siku yanabeba makaa ya mawe, kwanza napenda kujua yanapelekwa wapi cha kwanza, Mheshimiwa Waziri uniambie, yale makaa ya mawe, yanayotoka Namtumbo, malori 100 kila siku yanapelekwa wapi, kwa sababu kwa takwimu ambazo nilijaribu kuuliza wananchi pale wanasema wanakwenda Uganda nan mengine yanakwenda Kenya. Nikawa nashangaa kama malori 100 yanabeba makaa ya mawe kutoka Namtumbo, rasilimali ya nchi yetu, leo tunaendelea kuteketeza misitu yetu, are we serious?
Naomba uje utuambie yanakwenda wapi, na wale wananchi pale wananufaikaje na sisi kama Tanzania tunanufaikaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Wizara ya Madini na Nishati kutoa leseni za kutafuta madini kwenye maeneo ya hifadhi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilindie muda wangu, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na utaratibu ambao kunakosekana coordination kati ya Wizara ya Madini na Nishati na Wizara ya Maliasili. Wizara ya Nishati na Madini inatoa leseni za utafutaji wa madini ndani ya maeneo ya hifadhi, kwa hiyo imeleta migogoro mingi sana. Kuna baadhi ya maeneo ya hifadhi ambayo mpaka sasa hivi kuna migogoro mikubwa sana mojawapo ni Hifadhi ya Manyara. Wamepewa leseni ndani ya hifadhi, hakuna coordination matokeo yake leo kuna migogoro ambayo haiishi. Kwa hiyo, tungependa wakati Wizara inatoa leseni za kutafuta madini kuwepo na coordination kati ya Wizara hizi mbili ili kuondoa migogoro ambayo inatokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nimeangalia kitabu cha Mheshimiwa Waziri, tuna madini ya Uranium ambayo tunachimba maeneo mengi sana ya Tanzania, napenda kujua haya madini ya Uranium maeneo gani yameanza kuchimbwa, maeneo gani yanafanya kazi, maeneo gani na tunanufaikaje na madini hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nilitembelea Mgodi ule wa Uranium kule Likuyu Namtumbo, tuliona jinsi ambapo kuna Uranium nyingi iko nje, tulitembea pale wanaita yellow cake, iko peupe ni ya kukusanya. Kwanza ningependa kujua ule mgodi umeshaanza kufanya kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, tunanufaikaje kama Watanzania na lingine wananchi wa eneo lile wananufaikaje na ule mgodi kama umeshaanza kufanya kazi. Maana naona kimya, nilikuwa nategemea angalau tuone huku kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri, sioni chochote ambacho kimeandikwa huku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la REA, kiukweli kwenye sula la REA kwa kiasi fulani limesaidia sana umeme kusambaa, lakini bado changamoto zake ni kubwa sana. Suala la REA kila Mtanzania anashiriki kwa fedha ya REA, hata bibi wa kule kijijini kabisa akinunua lita moja ya mafuta ya taa tayari kasaidia mchango wa REA kuendelea kuwepo kwa kukatwa shilingi 150. Jambo la kushangaza kwa nini fedha zile hazielekezwi zote maeneo yaliyopangiwa?
Mheshimiwa Waziri hebu kesho utuambie, zile fedha ambazo hazikutumika kwa hii miaka mitatu hazikupelekwa kwenye REA zimeelekezwa wapi na ni kwa sababu gani? Kwa sababu kupanga ni kuamua, kama tumeamua kutengeneza mradi wa kusaidia umeme vijijini, tumeamua kama Watanzania, tunawakata kwenye mafuta, kwanye diesel, petrol, na kwenye mafuta ya taa. Tuwe na nidhamu basi ya matumizi ya hizi hela.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kama Wabunge wengine walivyosema, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja kwenye Jimbo langu la Kaliua, namshukuru Mheshimiwa Waziri, kiukweli alikuta hali ni mbaya. Wakati anakuja katika Jimbo la Kaliua tulikuwa na asilimia moja tu ya usambazaji wa umeme wa REA katika Wilaya nzima mpaka alishtuka.
Nashukuru baada ya kuwepo kwake alisukuma watendaji wake angalau shughuli zimeanza kwenda lakini Mheshimiwa Waziri uliagiza tarehe 30 mwezi wa nne, umeme wa awamu ya kwanza na ya pili uwake, mpaka leo ni kijiji kimoja tu kinawaka umeme, hivyo, bado tunayo changamoto nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA inahitaji ufuatiliaji wa hali ya juu, siyo suala kwamba watendaji wa TANESCO wanawaachia wale makandarasi hapana. Nimeona mfano mmoja Kaliua, Mameneja walikuwa wamekaa ofisini hawafanyi kazi, walivyonyanyuka kutoka ofisini kuwafuata makandarasi leo kazi inafanyika.
Kwa hiyo, watu wa TANESCO watoke maofisini waende kwa makandarasi wahakikishe kwamba wanawasimamia, makandarasi wale wanapoachiwa peke yao wanafanya wanavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia nguzo zinazopelekwa kwenye maeneo ya vijiji ni chache sana, wanasambaza barabarani mwa kijiji au makao makuu ya kijiji, vitongoji vyote hakuna umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali na Watanzania ni kila Mtanzania anayetaka kutumia umeme atumie umeme, siyo maeneo ya barabarani, ni lazima pia umeme uende mpaka maeneo ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni migodi mikubwa ya dhahabu kutolipa Kodi ya Mapato. Leo nimesikia kauli ya ajabu, eti wanasema watu wa migodi wamekuwa wanapata hasara endelevu. Sijawahi kusikia hasara endelevu. Hakuna mfanyabiashara yeyote duniani, hata kama ni mama ntilie akubali kupata hasara endelevu. Kama wanapata hasara endelevu, kwa nini waendelee kuwepo? Kama wanapata hasara endelevu, kwa nini waendelee ku-run? Wanakuwaje na watumishi? Wanakuwaje na kila kitu? Hapa ni wizi mtupu. Tunataka migodi yote ilipe kodi. Tumekuwa tunayabeba sana makampuni. Leo kama Tanzania hatunufaiki sana na migodi yetu ya madini kwa sababu wanabebwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati, wametuambia kwamba kuna makampuni yanayodaiwa shilingi bilioni kadhaa. Makampuni ambayo hayakulipa Kodi ya Zuio yanadaiwa shilingi bilioni 89 lakini kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema Acacia wamelipa almost karibu shilingi bilioni 13. Sasa hebu tujue, Mheshimiwa Waziri utuambie, kwanza haya makampuni mengine ambayo hayakulipa, umesema kuna makampuni matatu hapa ambayo hayakulipa, wamelipa tu Acacia kidogo, yale mengine tunayafanyaje, ikiwepo Mantra na hao wengine Tanzania One?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini hawakulipa na ni kwa sababu gani? Kwa nini Mheshimiwa Waziri hajatueleza kwenye kitabu chake kwamba wanafanywaje? Kwa sababu ametuambia tu wamelipa Acacia kiasi kidogo. Kwanza Acacia hawajamaliza, tunataka walipe kodi yetu yote, lakini yale ambayo hawajalipa, tunawafanyaje? Mheshimiwa Waziri, tuache kuwabeba, wanatunyonya, hii rasilimali ni yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la wachimbaji wadogo wadogo. Kwenye Jimbo langu ninayo machimbo ya madini ya dhahabu kwenye eneo la Ulyankulu, machimbo ya Silambu. Tulikubaliana hapa Bungeni Serikali iwezeshe wachimbaji wadogo wadogo, kuwapatia maeneo lakini pia wapatiwe mitaji, pamoja na vitendea kazi. Bado halitekelezwi kama tulivyokuwa tumekubaliana, bado wana hali ngumu ya utendaji wao wa kazi, bado wanahangaika hapa pale, wamekuwa ni watu wa kufanyia kazi kama za utumwa, wanatumika tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaomba sana, Serikali inajua na Mheshimiwa Waziri anajua, anawajua wote wako wapi na vitalu vyao, hebu wekeni utaratibu wa kuwawezesha, waweze kunufaika na ile kazi yao wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, ndani ya Wilaya yangu ya Kaliua, Kata ya Igwisi, Kijiji cha Twende Pamoja, kuna machimbo ya madini ya mawe, yanachimbwa na kampuni ya CHICO. Kampuni ya CHICO imechimba pale karibu miaka mitatu wanatengeneza kokoto, hawajawahi kulipa chochote kwenye kata ile wala kwenye kijiji kile, lakini kikubwa kuliko yote, kuna nyumba zaidi ya 25 hazijalipwa, baruti zinapasuliwa usiku na mchana, wananchi wale wengine wanateseka, wengine wanazimia, hawajaweza kuhamishwa, lakini wapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipofuatilia kwa CHICO anasema, sisi tuna-deal na watu wa madini. Sasa Mheshimiwa Waziri utusaidie, pale kampuni inapopewa mlima, pale ni mlima wamesambaratisha mlima wote umekwisha, wananchi wanateseka. Hakuna hata coin moja ambayo wamewahi kulipa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri ukija kujibu utuambie, wale kampuni ya CHICO ambao mmewapa mlima wa pale Twende Pamoja, Igwisi, wamechimba miaka mitatu, wanatengeneza kokoto, kwa nini hawalipi ushuru unaotakiwa kwa kijiji husika na kwa Halmashauri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kwa nini mpaka leo hawalipi watu haki zao? Wawaondoe pale. Nilishawahi kukuta mwanamke amezimia pale, mpaka kijiji kwa huruma, wakamhamisha wakampeleka sehemu nyingine. Wananchi wa kawaida, lakini Serikali ipo na sheria iko wazi kwamba pale unapotaka kutumia eneo kwa ajili ya matumizi mengine, lazima watu wapewe haki zao waondoke. Makanisa, mawe yanadondoka mpaka ndani ya kitanda cha mtu. Makanisa...
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango wako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara kwa kuandaa hotuba na kuileta hapa Bungeni. Kwa dhati nampongeza Waziri kwa mipango mizuri, utendaji mzuri na mikakati mizuri ya kuhakikisha ardhi ya nchi hii inatumika vizuri na kuwepo kwa mpango miji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo tabia ya wananchi kuanzisha miji midogo midogo kiholela pembezoni mwa barabara kuu kila kona. Ukipita barabara kuu kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma kuna miji midogo mingi isiyokuwa na ramani yoyote. Naomba Waziri aeleze Bunge hili ni mikakati gani inapangwa kudhibiti uanzishaji miji kiholela halafu wanadai huduma za jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kaliua, Kata ya Ushokola wananchi walichukuliwa mashamba yao ya asili kwa lengo la kupimwa viwanja kwa ajili ya makazi na huduma nyingine tangu mwaka 2000 mpaka leo hawajalipwa haki zao. Mashamba hayo yamepimwa viwanja na watu wanauziwa lakini wamiliki hawaambiwi hatma ya haki zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2011 watendaji wa TANROARDS waliweka mawe ya alama za barabara kwenye viwanja na miji ya watu. Mpaka leo hakuna lolote linaloendelea wala hawaambiwi lolote kuhusiana na mawe hayo yaliyowekwa. Maeneo yaliyowekwa mawe ni Kata ya Ushokola na Zugimlole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro mingi ya ardhi inasababishwa na watendaji wabovu, wala rushwa katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya na Manispaa. Maafisa Ardhi ndiyo chanzo cha matatizo kwani ndiyo wanauza viwanja mara mbili mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa migogoro ya ardhi. Afisa Ardhi Mteule pale Manispaa ya Morogoro ni chanzo cha matatizo kwa muda mrefu yupo pale na hachukuliwi hatua yoyote. Kwa nini Serikali inashindwa kuchukua hatua za nidhamu kwa watu kama hawa na kuwaacha kuendelea kuwatesa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Ardhi kwa ngazi ya Kata na Wilaya ni muhimu sana kusaidia kutatua migogoro ya ardhi kwa gazi za Wilaya. Serikali ihakikishe Mabaraza ya Ardhi yanaundwa katika wilaya zote hapa nchini. Aidha, Wajumbe wa Mabaraza haya wapewe posho yenye tija ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na waache utaratibu wa sasa wa kudai fedha kwa wale wenye matatizo ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya migogoro ya wafugaji na wakulima itakwisha kwa Serikali kuhakikisha kwamba makundi haya yanatengewa maeneo ya mifugo na maeneo ya kilimo. Maeneo hayo yakishatengwa yaheshimiwe na kulindwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Uwekezaji inaeleza wazi kuwa wawekezaji wote wanaofika nchini na kuhitaji ardhi kwa lengo la kuwekeza watapata ardhi kwa kufika Kituo cha Uwekezaji (TIC) lakini wapo wanaokwenda moja kwa moja vijijini wanawapa viongozi wa vijiji fedha, wanawapa ardhi ya wananchi tena bila kutumia mkutano na wananchi. Serikali itoe mwongozo wa maandishi kwa ngazi za vijiji, kata na wilaya kuhakikisha sheria zinafuatwa ili kuondoa migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi na nyumba bora ni vyema sasa Serikalii ikaondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi kwa Shirika la NHC. Pia Serikali ipeleke miundombinu ili kupunguza gharama za nyumba ili wanyonge au wananchi wa kawaida waweze kuzimudu/kuzinunua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Serikali inapoona wananchi/mwananchi anajenga nyumba eneo ambalo siyo sahihi mara moja asimamishwe na sio kusubiri akamilishe ndiyo abomolewe. Suala la kubomoa linaathiri sana familia, watoto na kusababisha mzigo mkubwa wa mawazo na watu kupoteza maisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kulipongeza Shirika la Hifadhi la TANAPA na Ngorongoro kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhifadhi rasilimali hapa Tanzania. Imekuwa ni kawaida pale ambapo Serikali inashindwa kuhifadhi maeneo mbalimbali kimbilio lake ni shirika lake ambalo linawapelekea na kwa kiasi kikubwa kwa kweli wameonekana wanajitahidi sana kulinda rasilimali zetu na vituo vyetu hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo tetesi kwamba Serikali inataka kuhodhi mashirika haya, kuyarudisha mikononi mwake kwa hili napinga kwa asilimia zote. Kama ni kweli kwamba ziko taarifa Serikali inataka kuhodhi mashirika haya irudishe kwenye mikono yake, wawe wanaendesha wao ni uhakika kabisa kwamba tunakwenda kuua uhifadhi hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mashirika mengi hapa nchini yalikufa kwa sababu Serikali imeshindwa kuyasimamia. Yale machache ambayo iliamua kuyapa full authority yajiendeshe yenyewe ndiyo bado yapo. Leo TANAPA na Ngorongoro wanajiendesha wenyewe kwa asilimia 100 na bado wanapeleka ruzuku Serikalini na ni mashirika pekee ambayo Serikali haiweki ruzuku hata senti moja. Leo kama wanataka kuyarudisha ndani ya mikono yao tunakwenda kuua uhifadhi hapa nchini. Naomba kama mpango huo upo ufe kabisa haufai kuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana pekee TANAPA imetoa shilingi bilioni 10 kama ruzuku Serikalini na bado inajiendesha. Tumekuwa tunalia kilio hapa kwamba Serikali ijenge angalau miundombinu ya kwenda kwenye vivutio, barabara kutoka Iringa kwenda Ruaha kwa miaka 10 Serikali imeshindwa kujenga, leo tunanyang‟anya mashirika haya mamlaka ya kujisimamia tunakwenda kuua uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa nimeona tunayo mapori ya akiba zaidi ya 28, tunayo mapori tengefu zaidi ya 42, tunazo hizi hifadhi za TANAPA 16. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri haya mapori ya akiba 28 na mapori tengefu 42, mengi yapo taabani na mengine hayapo, yapo kwenye vitabu kwenye ground hayapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapori haya yana hali mbaya, tumekuwa tunalia hapa, mapori haya mengine yamevamiwa miaka 35 iliyopita huko nyuma na wamejenga ndani ya hifadhi vijiji, hospitali na barabara. Tumekuwa tunalia hapa mapori haya yalivamiwa miaka mingi iliyopita Serikali haikuchukua hatua, wamesajili vijiji kisheria, wanapeleka huduma, leo Mheshimiwa Waziri anatuambia tuna mapori ya akiba 28, yako kwenye hali mbaya, mengine hayapo katika ground, yapo kwenye karatasi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Tabora peke yake tuna vijiji zaidi ya 50 ndani ya hifadhi vina vyeti vya usajili na kila kitu kipo mfano shule na hospitali. Ninayo taarifa hapa kamili ya Kiserikali, Mkoa wa Tabora wenyewe vijiji zaidi ya 50, Wilaya ya Kaliua peke yake tuna vijiji 21 vimesajiliwa kisheria ndani ya hifadhi. Wananchi hawa wamekaa kwa hofu miaka mingi, Serikali tunaiambia hapa miaka 10, lakini hakuna hatua inayochukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea hatua ya leo Mheshimiwa Waziri angekuja na mpango kamili namna gani watu hawa wanashughulikiwa ili waache kuishi kwa hofu, waache kunyanyaswa, wanauliwa mifugo yao, wanaharibiwa mashamba yao, ni shida, ni matatizo makubwa. Watu wa hifadhi wanachokifanya kwa watu ambao wamesajiliwa kisheria siyo halali ndani ya nchi ambayo tunaishi kwa kufuata Katiba na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umuhimu naomba nitaje tu kwa ufupi vijiji ambavyo vimeathirika na suala hili. Tuna Vijiji vya Ukumbi Kakonko, Lumbe, Usinga, Ukumbi Siganga, Kombe, Kashishi, Uyowa, Seleli, Nyasa, Mwendakulima, Sasu, Kiwakonko, Nsimbo, Mpanda Mlowoka, Mwahalaja, Chemkeni, Kanoge, Ulanga, Mwendakulima, vijiji 21 miaka yote watu wanaishi kwa hofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa atueleze nini hatma ya watu hawa na nini hatma ya shule ambazo zimejengwa kule? Hatuwezi kuacha wananchi waendelee kuishi kwa hofu miaka yote, wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo, lakini Serikali ipo tu imetulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye suala la TFS. Tulianzisha Wakala wa Misitu (TFS) kwa maana ya kuokoa rasilimali ya misitu inayopotea na ndiyo lengo letu kama Watanzania, Wizara na Wabunge. Watu wa TFS wamekuwa ndiyo chanzo kikubwa cha kuangamiza misitu kuliko tulivyokuwa mwanzoni. Leo watu wa TFS hawana mpango wowote makini wa kuja kuokoa misitu, wao wanakaa wanasubiri wachukue mbao, wagonge muhuri mbao isafirishwe. Serikali imeweka utaratibu, imefunga kabisa kutoa magogo kwenye miti ya asili pamoja na mbao kutoka kwenye misitu ya asili. Kwa nini Serikali inaweka malengo kwenye TFS? Kwa nini Maafisa Misitu wanapewa malengo ya makusanyo? Leo misitu yetu inateketea kwa kasi kubwa ya ajabu kuliko ilivyokuwa TFS haipo. Labda hawakupewa malengo, labda Serikali haikuwa na mipango, labda hawajaambiwa wanatakiwa wafanye nini. Hili ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chain saws zilizopo ndani ya maeneo ya misitu ya asili nyingi ni za watu wa TFS. Wao ndiyo wananunua chain saws wanawapa watu wao wanaenda kuweka kule kwenye misitu, kwa hiyo, hakuna tunachokifanya. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa kuhitimisha atuambie nini hasa kazi na wajibu wa TFS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, TFS walikuja Kaliua, wamekuja kufyeka mahindi ya wananchi kwenye Jimbo langu, tena leo naomba njaa ikija, muwe wa kwanza kuja kuwalisha chakula wananchi wa Kaliua. Mahindi yalishafikia karibu kuzaa, wanakuja wanaweka beacon ndani ya nyumba za watu. Nimeongea nao kwenye simu hamfanyi kazi kwa weledi? Hamna mpango shirikishi, Wilaya haijui, Mbunge hajui, Mkurugenzi hajui, wanakuja wenyewe wanakwenda kufyeka mahindi ya watu, hawana weledi wa kufanya kazi. Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atujibu nini kazi ya TFS. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ikija hapa itujibu, kuna Tume ya Kimahakama iliundwa na Mheshimiwa Rais wa awamu iliyopita, kutokana na ripoti ya Operesheni Tokomeza kwenda kuangalia madhara makubwa waliyopata wananchi nchi nzima, leo ni mwaka wa tatu iko wapi ripoti ile? Iko wapi? Wananchi wanateseka, watu waliuawa, watoto wananyanyasika, mifugo iliteketea, operesheni tokomeza ilikuwa ya kutokomeza watu. Tunaitaka ripoti ya Mheshimiwa Rais hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Bunge lako liagize tupate ripoti ya Tume ya Kimahakama ya Mheshimiwa Rais ili tuweze kuangalia namna gani ya kuwasaidia wale watu waliopata madhara makubwa sana na wengine walipoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni tozo kwenye hoteli za kitalii ambazo ziko ndani ya hifadhi. Kwa miaka mingi tumekuwa tunazungumzia suala hili la tozo. Tozo zinazotozwa sasa hivi na TANAPA ni za miaka 10 iliyopita wakati vitanda vikiwa vinatozwa dola 50 - 100, leo kitanda kimoja dola 300 - 500, tozo ni zile zile huu ni wizi, haiwezekani! Kwa nini concession fee iwe ya miaka 10 iliyopita? Leo maisha yamepanda, gharama zimepanda, vitu vyote vimepanda Serikali imenyamaza kimya kuna nini hapa? Naomba Mheshimiwa Waziri akija hapa atuambie, Mahakama imeshatoa rulings wale wafanyabiashara walishindwa kwa nini hatuletewi tozo nyingine zinazoendana na hali ya sasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wetu kwenye EAC utakuwa na tija kwa Taifa hili na watu wake ikiwa tutatambua na kuzitumia fursa zilizopo ndani ya umoja huo. Pamoja na Ibara ya 10 ya Itifaki ya Soko la Pamoja kuwahakikishia raia wanachama uhuru wa kupata ajira nchi zote za umoja wa EAC. Serikali itupatie takwimu ya Watanzania wangapi wameajiriwa kwenye ajira rasmi za Serikali katika nchi za Umoja wa Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imekuwa ni masoko kwa bidhaa zinazotoka kwenye nchi za Kenya na Uganda. Hata kwa bidhaa ambazo tunatengeneza kwa wingi hapa nchini kama vyombo vya plastic, viatu vya plastic na kadhalika bado vinavyotoka nje ni vingi kiasi cha bidhaa za viwanda vyetu kukosa soko ndani ya chini. Serikali ieleze ni kwa namna gani tukalinde viwanda vyetu ndani ya nchi, kuna udhibiti wowote wa uingizaji bidhaa hizi ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nchi yetu kuwa na vivutio vingi ya utalii bado hatujaweza kuvitangaza kikamilifu ili tuweze kunufaika vizuri. Ni kwa namna gani tunatumia Balozi zetu zilizoko katika maeneo mengi kutangaza utalii na vivutio vyetu huko waliko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwezesha Balozi zetu ni muhimu sana ili ziweze kutekeleza vizuri majukumu yao. Ni aibu kwa Maafisa wa Ubalozi kushindwa kulipia nyumba za kuishi na kubaki wakilalamika mara kwa mara kila tunapokwenda nje. Maofisa hawa wanalalamikia shida, tabu na kutelekezwa na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuelekea kwenye kutumia sarafu moja kwa nchi zote za EAC. Tumejiandaa kiasi gani? Kwa sasa hiyo shilingi ya Tanzania ndio yenye thamani ndogo sana tofauti na fedha za wenzetu. Tusikubali mambo ambayo yatakuja kutuumiza kama hatujajipanga vizuri ndani ya nchi. Tusije tukawa wasindikizaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nchi yetu kuwa na vyuo vinavyotoa mafunzo ya fani za utalii na customer care; bado mahoteli mengi makubwa na madogo watumishi wengi ni kutoka Kenya na wanatoa huduma nzuri sana na wanaipenda kazi yao. Naomba Serikali itueleze nini kinakosekana ndani ya vyuo vyetu hapa nchini au kwa vijana wetu wanaosoma fani hiyo kiasi cha kutokubalika kwenye hoteli zetu. Je, Serikali imefuatilia mitaala ya vyuo vya utalii vya Kenya na kuona upungufu wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lipange utaratibu wa Wabunge wa EAC wawe wanatoa semina na mafunzo kwa Wabunge kuhusu yale wanayofanya ndani ya Bunge la EAC ili tupate uelewa mpana na up to date yanayoendelea kuliko kusubiri hotuba wakati wa bajeti ya Serikali.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo kwenye mapendekezo ya mpango ambayo yako mbele yetu. Kwa sababu mengi yamezungumzwa na wengi sitazungumza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba pato la wastani la kila Mtanzania kwa mwaka 2015 ilikuwa ni Sh.1,918,928. Nimekuwa najiuliza kwamba takwimu kama hizi zimechukuliwa kutoka katika maeneo gani? Kwa sababu kwa sisi ambao tunaishi na wananchi wetu vijijini wale ambao hawana uwezo wa kupata hata laki kwa mwezi, hawana uwezo wa kupata milo miwili ya uhakika kwa siku, unaambiwa kwamba kila Mtanzania ana uwezo wa kupata milioni moja na laki tisa, nadhani ni lazima Serikali inapochukua takwimu ichukue takwimu vijijini ambapo asilimia 80 ya watu wanaishi kule. Wakichukua takwimu za mjini hawawezi kupata hali halisi ya maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea hali ni mbaya kwelikweli, ni matatizo matupu, ukiambiwa kwamba kila mtu ana milioni moja na laki tisa, unapata mashaka makubwa sana. Kwa hiyo, naomba kwenye takwimu nyingi za Serikali chukueni maeneo ambapo percent kubwa ya Watanzania inaishi kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la ongezeko la watu na nimekuwa nashangaa Serikali imekaa kimya sana kutokana na ongezeko kubwa la watu Tanzania. Ukiangalia kwenye sensa mwaka 2012 tulikuwa watu milioni 45 japokuwa wengine hawakuhesabiwa. Kwa takwimu za Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake 2016 tuko watu milioni 50.1, prediction 2025 tutakuwa watu milioni 63.
Mheshimiwa Mwenyekiti, spidi ya ongezeko la watu haiendani na spidi ya Serikali kutoa huduma muhimu, ni jambo ambalo liko wazi, haiendani kabisa. Ndiyo maana unaona leo wanafunzi wanagoma, mikopo haitoshi, huduma za afya hazitolewi kwa uhakika, elimu bado ni matatizo, Serikali inaogopa nini kuanza kuweka mikakati ya udhibiti wa ongezeko la watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa nchi nyingine, China walivyoweka kwamba mwisho watoto wawili kuna factor waliziangalia na maeneo mbalimbali wanaweka idadi kwamba angalau mtu awe na watoto watatu mpaka wanne ili kuweza kutoa huduma. Haifai na haileti tija watu wazaliwe mshindwe kutoa huduma, ni kama sehemu ya familia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mzazi ukiwa na watoto kumi huwezi kuwapa elimu nzuri, huwezi kuwavalisha vizuri, huwezi kuwapa huduma nzuri, unawatesa. Simple applied kwa Tanzania kuendelea kuona idadi ya watu inaongezeka kwa spidi kubwa lakini Serikali hatuzungumzi chochote ni kuendelea kuwafanya watu wateseke bila sababu. Watu tuwe na watoto ambao tunaweza kuwahudumia vizuri angalau kila mwananchi apate huduma anazostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye suala la kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu litekelezwe kikamilifu kwenye bajeti ijayo. Nikianza na mpango wa elimu, Serikali kweli imeanza na mpango wa kutoa elimu bure, tunatembea kwenye shule zetu bado fedha inayotolewa kwa retention haitoshi, changamoto ni lukuki katika shule zote. Kila unapokwenda ni kilio, Walimu wanalia wanafunzi wanalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumetengeneza madawati, madawati maeneo mengi yako kwenye maturubai, yamewekwa shade kwa kutumia majani hakuna madarasa ya kutosha, lakini pia hakuna miundombinu ya nyumba za Walimu, hakuna vyoo, ukienda kwenye shule zetu bado changamoto ni nyingi sana. Kwa hiyo, kwenye bajeti ijayo lazima Mheshimiwa Waziri aje na mpango mkakati wa kuongeza miundombinu ya madarasa, nyumba za Walimu kwenye shule zetu za primary na secondary. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala la kujenga vyuo vya elimu ya mafunzo, kwa spidi ambayo tunaongezeka nayo na kwa sasa hivi Serikali ambapo inasema division one na two ndio inaenda vyuo vikuu wengine wanaenda vyuo vya kawaida, vyuo vya mafunzo, wanafunzi wengi wanabaki vijijini, tunaulizwa maswali hatuna majibu. Tunaomba mpango ujao Mheshimiwa Waziri aje na mpango maalum kuhakikisha tunajenga vyuo vya VETA kwenye Wilaya zetu na atueleze ni vingapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye mpango huu hapa amesema mpango ni kumalizia chuo kinachojengwa Mahenge, haitoshi! Tunataka Wilaya zote ambazo hazina vyuo vya ufundi ni lazima vipate vyuo hivyo. Hii iende sambamba na kuweka karakana zinazoeleweka na miundombinu yote ili wanafunzi wetu wapate angalau stadi za kazi waweze kujitegemea kule vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la afya. Njia pekee ya kuondoa vifo vya akinamama na watoto, wazee na makundi mengine Tanzania ni kusogeza huduma karibu na walipo. Tulikubaliana na Serikali karibu miaka kumi sasa kujenga zahanati kila kijiji, kituo cha afya kila kata mpaka sasa hivi mpango huo bado unakwenda taratibu. Kwa hiyo, kwenye mpango ujao Mheshimiwa Waziri tunataka atuambie zahanati ngapi zitajengwa, za kutekelezwa siyo za kwenye vitabu, ngapi zitajengwa Tanzania nzima? Ni vituo vya afya vingapi vitajengwa kwenye kata zipi, zianishwe na zitekelezwe kwenye mpango ujao ionekane. Pia kuhakikisha kwamba tunapata watumishi wa kutosha na huduma zote muhimu zipatikane na vifaa tiba na dawa ziwepo za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni la maji. Watu wanaongezeka changamoto ya maji inaongezeka kila siku. Tunaomba kwenye mpango ujao lazima Waziri atuambie namna gani ya kuondoa changamoto za maji kuendana na ongezeko la watu. Tusingependa mwakani tuanze kushika hotuba ya mwaka huu na ya mwaka kesho hatutaki kama ambavyo Serikali zilizopita. Tunataka tujue yaliyopangwa kwenye bajeti ya mwaka huu yawe yamepita ya mwakani tuwe na mipango mipya inayotekelezeka, tunaomba sana hilo. Kwa hiyo, lazima mipango mikakati ya maji ya kutekelezeka iweze kuletwa ndani ya Bunge, ianishe wazi na ikatekelezwe siyo kuja kubaki kwenye vitabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo ya elimu ya juu. Nimeangalia hotuba ya Waziri anasema kwa mwakani wanategemea kutoa ruzuku kwa wanafunzi kama 124,243 hata wanaoomba mwaka huu ni wengi zaidi ya hao. Inawezekana Serikali haifanyi tathmini ya kutosha kuanzia sekondari, vyuoni kujua idadi ya wanafunzi wanaohitaji kupata ruzuku kwa ajili ya elimu. Tumekubaliana kwamba kila Mtanzania awe maskini awe tajiri, mtoto wa maskini asome wa tajiri asome. Kama wengi hatuwapatii mikopo wanapataje uwezo wa kusoma mpaka kufika vyuo vikuu na hao ni Marais watarajiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri ahakikishe wanafanya tathmini ya kutosha mwakani wawe na uhakika kwamba watoto kadhaa wanakwenda kupata mikopo na wapate mikopo yao kwa ukamilifu. Mtoto wa maskini unampa asilimia 10 au 20 haimsaidii kitu, anaishi maisha magumu kweli shuleni, wanaishi kwa kula mihogo na magimbi. Tunaomba itengwe fedha ya kutosha kuendana na mahitaji ya watoto maskini ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hakuna mikakati mizuri ya kusimamia…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hakuna mikakati mizuri ya kukusanya marejesho ya fedha za mikopo. Mimi nilisoma kwa kutumia mkopo wa Serikali, nimelipa miaka mitano iliyopita na nimekamilisha, juzi mwezi Agosti napata barua nadaiwa. Hii ikanipa picha kabisa kwamba hakuna mikakati ya kufuatilia mikopo, kama mtu amelipa miaka mitano iliyopita leo unampa barua anadaiwa, it seems kwamba hafuatilii mikopo inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kidogo kwenye mkataba ambao upo mbele yetu. Kwa sababu mengi yameshazungumzwa na wenzangu, nitazungumza machache sana.
Mheshimiwa Spika, kwanza linapokuja suala la maslahi ya Taifa lazima tusimame kama Taifa. Japokuwa tuna Umoja wa East Africa, lakini kila nchi ina levels zake za maendeleo ambayo ime-move. Kwa hiyo, tunapoenda kuangalia suala la maslahi ya Tanzania tuasianze kusema kwa nini fulani kasaini, kwa nini Uganda kasaini, kwa nini Kenya kasaini? Yapo mambo ambayo yamemvutia yeye kusaini huo mkataba. Kwa hiyo, kwenye masuala ya maslahi ya Taifa tusimame kama Taifa kuangalia maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kusikitisha kwamba mkataba ambao upo mbele yetu ukiusoma vizuri unaturudisha nyuma karibu miaka 50 tuliyotoka. Unakwenda kutupangia masharti wakati tumepigana angalau miaka 50 tunaanza kuweka sera za uchumi, sera za mapato na sera mbalimbali nzuri, inatuambia sasa kwamba tuache sera zote pembeni tufuate masharti ya EU, hatukubaliani na hilo.
Mheshimiwa Spika, leo tunazo sera ambazo sahihi jinsi ya kukusanya mapato. Mkataba unachambua, zipo changamoto na hasara ambazo tutazipata kutokana na kuingia mkataba huu.
Mheshimiwa Spika, nasema ili muweze kuondokana na hasara hizo, lazima mkae mrekebishe sera za mapato ndani ya nchi zenu, hivi kweli tupo sawa sawa? Cha kusikitisha sana, pia wanatuambia ili muweze kufidia hasara zitakazotokana na kuruhusu biashara free kuingia nchi yetu bila ushuru muweze kukaa muongeze VAT kwenye bidhaa ndani ya nchi yenu ili muweze kufidia hasara.
Mheshimiwa Spika, tukiongeza VAT kwenye bidhaa zetu, tunamuumiza nani? Tunawaumiza wananchi wetu, kwa sababu vyote wanaenda kulipa wananchi wetu. Kwa hiyo, tunalazimishwa sasa kwenda kuwabana zaidi Watanzania kwa sababu tu ya kukidhi matakwa ya Mkataba nchi za Ulaya.
Mheshimiwa Spika, kwenye suala kama hili kiukweli ni lazima tuwe makini, tuwe makini sana jamani. Juzi tulikuwa na bajeti mwezi wa sita, tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda; ni nchi gani duniani ambayo imeweza ku-move kwenda kwenye industrialization bila kulinda viwanda vya ndani? Hakuna. Hata hao Ulaya ambao leo tunaona wame-move, walilinda viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Spika, kwanza sisi mpaka hapa tulipo bado ni soko la bidhaa za wenzetu, ni soko la pamba-stick, ni soko la Wachina, ni soko la Wakenya, ni soko la wengine. Haitoshi tu tukafungue wazi, sisi tuwe kazi ni kuzalisha na kupeleka.
Mheshimiwa Spika, kama tunataka ku-move na mikataba kama hii na mikataba mingine naomba, kama Taifa lazima tuje tuwe na watu ambao tunapokuwa na mikataba kama hii waende ku-negotiate; negotiators wenye uwezo mkubwa. Kwa sababu mkataba kama huu haukutakiwa hata sisi kuja kuujadili; ulitakiwa uishie huko huko! Baada ya kuona kwamba hatuna maslahi nao, wanapiga pembeni, tunasonga mbele kwenda na mambo mengine ambayo yana maslahi kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima sisi Wabunge tuisimamie Serikali vizuri, tuje tuwe na watu wenye uwezo, capacity thinking nzuri ya kuweza kuwa negotiators kwenye mikataba kama hii hasa ya kitaifa ambayo tusipoiangalia vizuri, kipengele kimoja tu kinaweza kutu-switch tunajikuta kwamba tunaenda kuwa watumwa wa nchi nyingine badala ya ku-move kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, naungana na wenzangu Wabunge wengine wote kwamba mkataba kama huu hautufai na hata kama utatufaa, ni huko mbeleni. Pengine miaka 50 ijayo tuwe tume-move kidogo tumekuta wenzetu. Kama Wakenya, leo Kenya ni nchi ndogo, lakini kila nchi pia ina factors zake. Leo Tanzania tupo karibu milioni 50. Wakenya wenyewe ni wachache, lakini pia sera zinatofautiana. Kwa hiyo, lazima tuangalie factors nyingi nyingi kuhakikisha kwamba mikataba ya Kimataifa kama hii tunaipitisha. Kila mkataba unaopitishwa, tuangalie maslahi yetu, tusiangalie East Africa kwa sababu kila mmoja anapambana kwenye uwanja wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunajadili mapendekezo ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2017/2018 huku Serikali ikiwa haijatoa fedha za maendeleo kwa ajili ya miradi kwenye halmashauri na wilaya kwa sehemu kubwa na hivyo kusababisha miradi kudorora.
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Waziri wa Fedha inaonesha wastani wa pato la kila Mtanzania ilikuwa sh. 1,918,928/= sawa na USD 96.5 mwaka 2015.
Hizi takwimu haziendi na hali halisi ya wananchi wengi zaidi ya 809 wanaoishi vijiji ambao hawana uwezo wa kupata hata 100,000 kwa mwezi. Wengi wanapata mlo mmoja tu kwa siku. Serikali itueleze ni maeneo gani ya nchi yetu ambapo takwimu hizi zinatolewa/zinachukuliwa ambapo hazitoi hali halisi za maisha ya watu wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ongezeko la watu ndani ya nchi yetu ni kubwa sana haliendani na uwezo wa Serikali kutoa huduma muhimu na za uhakika. Ikiwa sensa ya mwaka 2012 tulikuwa watu milioni 45 mwaka 2016 tunakadiriwa watu milioni 50.1 na mwaka 2025 tutakuwa milioni 63 hii ni hatari kwa ustawi wa watu wa Taifa letu. Kwa mikakati gani ya Serikali kudhibiti ongezeko na kasi kubwa ya ongezeko la watu kwa nini Serikali inanyamaza kimya wakati inaona hatari iliyoko mbele?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Serikali ihakikishe kipengele cha kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu kinatekelezwa kikamilifu; mpango wa elimu bure umesaidia kupunguza machungu kwa wazazi na watoto wengi kuandikishwa mashuleni, bado fedha inayotolewa ni kidogo haitoshelezi mahitaji ya watoto na shule zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mpango ujao lazima Serikali iongeze fedha ya capitation zinazopelekwa mashuleni baada ya kufanya tathmini na kutambua mahitaji ya wanafunzi ili wapate elimu nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwenye mpango ujao ilete mpango kamili wa kujenga vyuo vya mafunzo ya ufundi (VETA) kwenye Wilaya zote hapa nchini ambazo hazina mahitaji ya vyuo vya VETA, ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga stadi za kazi kwa watoto wanaofeli wanaokosa nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vingine vya mafunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka mpango ujao uoneshe mikakati ya kujenga zahanati kila kijiji na vituo vya afya kila kata ili kuokoa maisha ya watu yanayopotea kwa sababu ya huduma za afya kuwa mbali na watu. Njia pekee ya kupunguza vifo vya watoto na wanawake, wazee na makundi mengine ni kutotekeleza mpango wa kupeleka huduma hizi jirani na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa maji safi na salama; tatizo la ukosefu wa maji ni kubwa sana linazidi kukua kutokana na ongezeko kubwa la watu. Mpango wa mwaka 2017/2018 lazima Serikali ioneshe mkakati wa kuondoa tatizo la maji, miradi mikubwa ya maji, Mkoa wa Tabora kutoa maji Ziwa Victoria, mradi wa maji kutoka Malagarasi kwenda Kaliua na Urambo na miradi yote ya kimkakati katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikopo ya elimu ya juu; mpango ujao kwanza tathmini ya uhakika ifanyike kuanzia mashuleni na vyuoni ili kubaini mahitaji halisi/wanafunzi wanaohitaji kunufaika na mikopo hiyo ili kutenga fedha za mikopo ya elimu ya juu kuendana na mahitaji na kuwezesha watoto wa maskini kupata elimu mpaka vyuo vikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa mapato yote ya Serikali kuingizwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kufuta utaratibu wa retention uangaliwe kwa mapana. Lisipoangaliwa vizuri kuna taasisi na mashirika ya Serikali yataathirika sana – mashirika yanayojiendesha yenyewe bila ruzuku ya Serikali na yanalipa kodi zote stahiki na asilimia zilizoelezwa na Serikali mfano mashirika ya uhifadhi mfano TANAPA, Ngorongoro, TAWA, TFS, NHC.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Taarifa zilizoko mbele yetu. Awali niwashukuru sana watoa hoja wote, Kamati zote mbili kwa taarifa zao nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda nitakwenda straight kwenye hoja. Naomba nianze kwa kusema kwamba, tunayo hifadhi moja tu Tanzania yenye urithi wa kipekee, hifadhi ambayo ina vivutio ambavyo haviko sehemu nyingine Tanzania, Afrika na hata Dunia nzima na ni Hifadhi yetu ya Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ambayo imekuwa inatuingizia kipato kikubwa sana kwa Taifa hili, lakini kwa karibu miaka 10 sasa, hifadhi hii isipoangaliwa kwa makini inakwenda kupotea ndani ya Tanzania. Hifadhi hii imewekwa ndani ya Urithi wa Dunia, imeingia kwenye Maajabu saba ya Dunia na imewekwa chini ya UNESCO, Shirika la Uhifadhi la Dunia, lakini Watanzania ambao tumepewa hadhi ya kuwa na hifadhi hii tumeshindwa kuitunza na sasa hivi hali ya hifadhi hii inakwenda kupotea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Ngorongoro inakabiliwa na tatizo kubwa la watu kulima ndani ya hifadhi, Ngorongoro inakabiliwa na watumishi kutafuna fedha za hifadhi, inakabiliwa pia na kuongezeka kwa mifugo. Jana nilikuwa nasoma vyombo vya habari, tayari Ngorongoro hata watumishi wanahamishwa wanakataa wanakwenda Mahakamani kushtaki. Najaribu kuelewa kwamba, miaka mitano ijayo tunayo Ngorongoro?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, hadhi ya Hifadhi ya Ngorongoro iendelee kubaki kama Urithi wa Dunia kwa vizazi vya leo na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeunda Tume hapa Tanzania kwa ajili ya kupitia migogoro ya wakulima na wafugaji na kuweza kuondoa mauaji yanayotokea ndani ya nchi yetu. Hata hivyo napenda kujua, Tume hii imeshaanza kazi, itamaliza lini? Tume hii ambayo inahusu Wizara nne na wataalam kutoka Wizara nne wakati bado inaendelea na kazi bado kuna wataalam na watendaji wanaopita kwenye maeneo ya hifadhi na kuweka alama katikati ya nyumba za watu bila kushirikisha Ofisi za Wilaya, Wakurugenzi hata Wabunge kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tujue, Serikali imeamua kuunda Tume, itekeleze kwanza jukumu la Tume. Tume ije na mpango kamili utakaoweza kutoa suluhu ya kutosha kuondoa migogoro ya wafugaji, kuondoa migogoro ya wakulima na migogoro ambayo watu wanapoteza maisha yao hapa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba, Wizara ya Ardhi wamefanya kazi nzuri; wamefungua kanda nne ndani ya Tanzania kuweza kurahisisha huduma za ardhi. Pamoja na kufungua Kanda nne ndani ya nchi yetu bado kuna tatizo kubwa katika Halmashauri zetu, manispaa zetu pamoja na majiji la kutokuwa na fedha za kutosha kuweza kupima maeneo. Tunayo shida kubwa sana Waheshimiwa Wabunge, nchi yetu haijapimwa, maeneo mengi hayajapimwa, migogoro inaongezeka kwa sababu pamoja na kwamba Wizara inajitahidi; na namshukuru Mheshimiwa Lukuvi anafanya kazi nzuri, lakini bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie namna ya kuweza kutoa fedha kama revolving fund kwenye manispaa zetu, kwenye halmashauri zetu pamoja na kwenye majiji, wapewe fedha wapime maeneo, wakishayapima wayauze wapate fedha, warejeshe fedha. Hiyo kazi ilianza kama miaka mitano iliyopita kwenye Manispaa za Dar-es-Salaam; Temeke, Ilala na Kinondoni, sikujua ule mpango uliishia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba, ule ulikuwa ni mpango mzuri, tuliusapoti lakini umeishia katikati. Ni mpango mzuri, Serikali iwezeshe, ipeleke watalaam wa kutosha kwenye halmashauri, ipeleke vifaa kwenye manispaa, kwenye majiji na halmashauri, lakini pia, itoe fedha waweze kupima kuhakikisha kwamba, nchi yetu inapimwa. Kutegemea Wizara peke yake tutachukua miaka mingi sana kuweza kupima maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo kubwa sana la makazi holela. Mimi kila nikiongea juu ya ardhi nazungumzia makazi holela. Tumekuwa kama Serikali hatujipangi. Leo kila ukienda watu wanaanzisha miji miwili, mitatu, baada ya miezi mitano, baada ya mwaka ni mji tayari. Tayari wanahitaji huduma za maji, barabara, na umeme. Serikali kwa nini isiwe na mpango? Watu waambiwe kajengeni pale? Kwa nini inasubiri wananchi wajiamulie wenyewe wakakae wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukianza kutembea kuanzia Dodoma, elekea Morogoro unaenda Dar-es-Salaam, vijiji vinaanzishwa kidogo, kama utani. Serikali ipo, viongozi wapo, wataalam, lakini wanaona wananyamaza kimya. Leo tumekuwa na nchi ambayo haijapimwa maeneo mengi, miji yake ni ya kiholela na bado inazidi kuanzishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ifike mwisho kuwa na mji usiopimwa, usiopangwa, miji ambayo ni ya kiholela. Nchi nzima tunakuwa na vichuguu, hatutaki kuwa na nchi yenye vichuguu. Kwa hiyo tunaomba, Wizara inafanya kazi nzuri lakini haijaweza kudhibiti ujenzi holela kwenye maeneo mbalimbali ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala pia, la National Housing. Nishukuru kwamba, wanafanya kazi nzuri, tatizo kubwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata makazi bora. National Housing inafanya kazi kwa niaba ya Serikali, ni kwa nini Serikali haiwezi ku-subsidize nyumba za National Housing ili wananchi wa hali ya chini waweze kukaa na kuishi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini National Housing inunue simenti bei ileile, mchanga bei ileile, vifaa vya ujenzi bei ileile utegemee wakauze nyumba rahisi? Haiwezekani! Pia, wanapeleka huduma za maji wenyewe, umeme wenyewe, miundombinu wenyewe. Serikali inatakiwa iweze kutoa baadhi ya vitu kupunguza gharama, nyumba za National Housing zinufaishe wananchi wote wenye hali ya kawaida na wenye hali ya chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasahivi nyumba za National Housing zinakaliwa na kununuliwa na watu wa hali ya juu, watu wa chini hawanufaiki kabisa. Kwa hiyo, hata ile maana ya kuwepo kwa National Housing yenyewe inakuwa haina tija kwa wananchi wa hali ya chini. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba National Housing inakuwa na nyumba nzuri, lakini za standard ambazo mwananchi yeyote yule anayetaka kumudu anaweza kumiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo, TANAPA inajitahidi inafanya kazi nzuri. Naomba Serikali ihakikishe inafungua, inaweka miundombinu kwenye maeneo ya hifadhi za Kusini, tuweze kufungua hifadhi za Kusini. Leo ukiangalia Tanzania National Park inajitahidi lakini ni upande mmoja wa Kaskazini. Huku maeneo ya Iringa kuna vivutio vizuri, Kitulo, Mbeya, maeneo mengi. Serikali ni wajibu wake iweke miundombinu kwenye National Parks nyingine zilizoko nje na Kaskazini ili tuweze kuwa na utalii nchi nzima. Vivutio vipo, tatizo ni kwamba, maeneo hayo hayawezi kufikika kwa sababu hakuna miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo tatizo lingine. Tumekuwa tunazungumzia suala la concesion fees kwenye National Park. National Park wame-introduce concesion fees kwa maana ya tozo ya vitanda kwa hoteli ambazo ziko ndani ya hifadhi kwa miaka zaidi ya 10 sasa. Wanatumia zilezile za miaka 20 iliyopita, Dola tano mpaka Dola saba, wakati huo imewekwa hii tozo Dola tano mpaka Dola saba tulikuwa tunalipa kitanda Dola 150 mpaka Dola 200, leo kitanda kimoja National Parks ni Dola 500 mpaka Dola 1,000 lakini tozo iko palepale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba, Bodi haikuwepo, sasa Bodi imeshateuliwa tayari, naiomba Serikali mapema iwezekanavyo tozo mpya za National Parks ziweze kuwa introduced ili National Park ipate fedha za kutosha kuboresha miundombinu, lakini pia kuweza kusimamia utalii ndani ya hifadhi zetu za TANAPA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la Loliondo. Tumeona migogoro mingi ndani ya Loliondo. Naiomba Serikali; kwa taarifa ambazo tumezipata ni kwamba, sehemu ambayo inagombaniwa mpaka Mkuu wa Mkoa Mheshimiwa Mrisho Gambo wametofautiana yeye na Mheshimiwa Waziri ni eneo la chanzo cha maji. Katika eneo lile wanaokuja kufuga kule ni watu wa kutoka nje ya nchi, wameleta mifugo kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaomba kwenye masuala ya uhifadhi na hasa kulinda vyanzo vya maji tusiweke siasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia juu ya vyanzo vya maji. Nimesema eneo linalogombaniwa ni eneo ambalo linaonekana lina chanzo cha maji. Suala la kuwepo kwa chanzo cha maji haliangalii hifadhi au si hifadhi, ni chanzo cha maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mingi tumeshuhudia mifugo Loliondo inakufa wakati wa ukame kwa sababu maji yanakosekana. Leo hata wale wa Loliondo wenyewe wakishindwa kutunza vyanzo vyao vya maji wakati wa ukame mifugo itakufa tu. Kwa hiyo, nasema kwamba, tuangalie interest ya Taifa lakini pia, interest ya wafugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni chanzo cha maji kilindwe iwe nje ya hifadhi iwe ndani ya hifadhi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Muswada ulioko mbele yetu na mchango wangu utajikita kwenye Muswada wa kuanzisha Taasisi ya Utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Muswada huu nilipoenda kwenye lile jedwali namba tatu, nikaangalia maeneo ya utafiti nikaona almost tume-cover mambo mengi sana, ukiangalia karibu kila kitu, kwenye uboreshaji wa mazao, afya ya mimea, utafiti, mavuno, matumizi ya ardhi kilimo, usimamizi, mambo mengi yamekuwa covered. Nilipokuja kwenye namba 26 namna ya kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza yote haya yaliyoko hapa karibu mambo 11 sioni dalili za kutekelezwa kwa mambo hayo kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia source za fedha ni hiyo mikopo, ruzuku ya Serikali, kuangalia ruzuku itakayopangwa, posho, sheria hii tunataka ituambie namna gani fedha zitapatikana kutekeleza hapa. Mimi nina imani kwa kupitia sheria hii kama kweli tutapata fedha za kutosha, tumekuwa na magonjwa ya mimea ya muda mrefu, tuna magonjwa ya migomba kule Bukoba zaidi ya miaka 20 utafiti hautoi majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna magonjwa ya machungwa leo hatusafirishi machungwa nje kutokana na kwamba magonjwa hayapatiwi majibu. Tuna magonjwa ya mihogo, tuna magonjwa ya nazi, hatuwezi kama hatuna namna ya kupata fedha za kutosha. Kwa hiyo, shida kubwa ya Muswada huu hakuna namna ya kupata fedha kutekeleza haya yaliyoainishwa yote kwenye hili Jedwali Namba Tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na Vyuo vyetu vingi tu vya utafiti hapa nchini vyuo vilikuwa 16 vyote leo tunaambiwa vitakuwa chini ya hii Taasisi ya Utafiti, Vyuo hivi siyo kama vilikuwa havina wataalam, vilikuwa na wataalam wa kutosha, wana majengo yao mazuri, tatizo ni financial support. Kuna wataalam wenye uwezo, kuna Madokta lakini tatizo hakuna fedha, hakuna vitendea kazi, hakuna madawa ya maabara, matokeo yake vimekuwepo kama ni picha. Kwa hiyo ni lazima kwanza sheria hii ituambie namna gani tunapata fedha za kutosha kuweza kuendesha Taasisi ya Utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliweka utaratibu ndani ya nchi yetu kuhakikisha kwamba angalau asilimia moja ya mapato ya nchi ndani ya mwaka yanakwenda COSTECH hatujaweza kufika hata hapo. Kwa hiyo, hata tungekuja na sheria nyingi kiasi gani, kama hatutoi fedha, hakuna utafiti usiokuwa na fedha, hakuna mafanikio ya utafiti ambao haujawekezwa, kuwa na utafiti ni kuwekeza vya kutosha. Nimeona hiyo ndiyo kwanza shida kubwa sana kwenye Muswada wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na maoni yaliyotolewa kwamba lazima tuje na Mfuko Maalum wa Utafiti, tuwe na nidhamu nao na uwe ring fenced tuhakikishe kwamba fedha inakuwepo. Leo hii tunaposema tunaingiza mpaka mambo ya mazingira, nimeshukuru sana kwamba angalau sasa tunaanza kuoanisha hata kilimo na mazingira, kilimo na mabadiliko ya tabianchi, kilimo na matumizi bora ya ardhi, ni mambo mengi lakini kwa namna gani? Naomba sana sheria hii ingeanza kwanza namna gani tunapata fedha, hapo ningejisikia burudani kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Mheshimiwa Waziri hapa atuambie namna gani tunapata fedha ya uhakika, siyo tunasema tu kwenye bajeti ya Bunge, kwani miaka yote hatutengi, tunatenga lakini haiendi! Mara tozo haziendi, hivyo kwanza ni financial support namna gani tunawekeza kwenye taasisi hii iweze kuwa na mafanikio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nikienda kwenye Muswada wenyewe sasa kwenye baadhi ya vifungu, kwenye Kifungu cha nne (4), kinasema kuhamasisha matumizi ya uzalishaji mbegu. Hapa ni kweli tumekuwa na shida katika nchi yetu kwa muda mrefu, asilimia 60 ya mbegu za Tanzania zinatoka nje na ni makampuni ya nje, mbegu zetu nyingi zimedumaa, leo ukienda kwenye maduka ya mbegu za mazao wanakwambia kabisa tunataka mbegu fulani kwanza zile za nje ni expensive, watu hawawezi kuzimudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pamoja na hiyo wafanyabiashara wale wanakwenda mpaka vijijini kwenda kuhamasisha zinanunuliwa. Kwa hiyo ni expensive halafu nyingine zinafanyiwa majaribio kwa kuwa hakuna utafiti ambao unatangulia. Ningeshukuru sana, kwa kupitia Muswada huu nina imani sasa tutakuwa na uhakika tunazalisha mbegu ndani ya nchi yetu za kutosha, lakini pia wananchi wetu wahamasishwe watumie mbegu za ndani ya nchi yetu na hivyo tuhakikishe kwamba tunajitosheleza vya kutosha kwa kutumia mbegu za mazao kutoka ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha tano (5) napendekeza wale Wajumbe wa Bodi lazima kuwepo angalau Mwakilishi kutoka kila Kanda, hii kusema kwamba Mwakilishi mmoja awakilishe wakulima sikubaliani nayo! Kwa sababu wawakilishi wa kila Kanda watasaidia, leo mkulima wa korosho kule Kanda ya Kusini hawezi kujua changamoto za mkulima wa tumbaku kule Tabora. Mkulima wa mahindi kule Mbeya hawezi kujua changamoto za mtu anayelima mwani labda yuko upande wa Pwani. Kwa hiyo, lazima kila Kanda itoe Mwakilishi wanapokaa kwenye Bodi kila mmoja aainishe changamoto za Kanda yake na mazao yanayozalishwa kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha saba (7) posho za Wajumbe. Huwezi kusema kama Wajumbe wapendekeze posho, Waziri aende aidhinishe hapana! Wanajipendekezea posho kwa nini? Lazima kuwepo chombo kinachopendekeza posho, leo Mjumbe wa Bodi hawezi kujipendekezea posho mwenyewe, lazima kuwepo na chombo kinachopendekeza washauriane na Waziri wakubaliane tusitoe loophole. Wanaweza wakasema kila mmoja milioni mbili kwa siku siyo wao wenyewe? Tusiwape loophole hiyo tunataka fedha nyingi ziende kwenye kazi husika siyo kwenda kulipana posho kwenye vikao mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 10(4) pia napendekeza kwenye Baraza la Taasisi lazima kuwepo Wajumbe kutoka kila Kanda tofauti na wanavyosema hapa ni Mjumbe mmoja wa kuwakilisha Wakulima kwa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 22 kusajili miradi utafiti wa kilimo na utoaji wa huduma. Kifungu hiki ndicho kitakachosaidia sasa kuweza kupata watoaji wa huduma ya kilimo wenye uelewa na weledi. Leo tumekuwa na watu wanaosambaza mbegu za kilimo, wanasambaza mbolea ni business oriented, ni wafanyabiashara, hajasoma kilimo, hajui kilimo, hajui msimu, hajui ni madhara namna gani unavyochelewesha mbolea unaathiri nini, unapeleka mbolea muda ambao siyo unaathiri nini. Unapeleka mbegu muda umepita, unaathiri nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia Muswada huu na kifungu hiki, lazima tuainishe sasa watu wenye uwezo wenye weledi, wenye elimu kuweza kutoa huduma za mazao, huduma za kusambaza mbegu, mbolea, hata kwenye manunuzi, mtu ambaye anaona hiyo ni fani yake, tofauti na sasa hivi ambapo mara nyingi tumekuwa tukiwatumia watu ambao ni wafanyabishara, hawanufaishi wakulima, tunaishia kupata hasara, mwisho wa yote wakulima wetu wanakuja kuwa ni maskini wa kutupa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 26 ningependa sana kuhusiana na namna gani, tuna vituo vingine kwa mfano pale Sokoine University, kuna taasisi ya TOSCI inayoshughulika kuhakikisha kwamba mbegu zinakuwepo za kutosha na ubora wa mbegu, sijaona imeguswa kabisa humu, namna gani sheria hii inashirikisha taasisi nyingine tofauti na vyuo kuweza kufanyakazi kwa pamoja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima waone ni namna gani wanafanya kazi kwa pamoja kwa sababu kama mmesema sasa ni kama umbrella, taasisi nyingine zote lazima zishirikishwe na wataalam wale washirikishwe kuhakikisha kwamba mwisho wa siku tunaweza kuwa na tija nzuri kwenye sheria hii ambayo imekuja mbele yetu leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 29(7)(a) kwa idhini ya kimaandishi ya Waziri anaweza kutumia fedha bila kujali kwamba matumizi hayo hayapo kwenye bajeti yoyote. Naomba kifungu hiki kiondolewe, tumekuwa tunasema hatuna nidhamu ya matumizi ya fedha, fedha tunaipeleka kwenda kwenye shughuli fulani, inatoka inaenda sehemu fulani, haiendi kwenye lengo, leo tunaweka sheria kwamba kwa maandishi ya Waziri anaweza kuagiza Bodi itumie fedha tofauti na bajeti iliyokuwepo. Lazima tuwe na nidhamu ya matumizi ya fedha, hapa tunaweka mwanya tunaweka upenyo namna gani Bodi itumie fedha za miradi bila kuwa na utaratibu wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kifungu hiki kiondoke kwa sababu hakitatusaidia, kwanza tutaleta matatizo, fedha zitaenda kutumika sehemu ambapo haikupangwa kwenda kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tumeambiwa kwamba pale mtu anaomba usajili akinyimwa aende kwa Waziri na Waziri awe ni namba ya mwisho. Hapa naomba Waziri asiwe namba ya mwisho. Inawezekana ikatokea figisu au utaratibu fulani wakamnyima tu huyu mtu kwa makusudi, akienda kwa Waziri na yeye asimsikilize. Kwanza ni muda mrefu wanasema siku 21 anaomba, Waziri ndani ya siku 30 hapo tayari miezi miwili imekwisha mtu anaomba usajili, siku 30 anasubiri majibu, miezi miwili imekwisha kwanza ni muda mrefu, lakini pia Waziri asiwe ni namba ya mwisho. Waziri ni binadamu. Naomba kiwepo chombo kingine.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 20 (2) kabla ya Mwandishi wa Habari kuondolewa au kukoma kuwa Mwanahabari kwa kosa lolote atakuwa amekiuka sheria hii, ni lazima kuwepo chombo huru kitakachothibitisha pasipo shaka kuhusu adhabu hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 20(3) Mwanahabari aliyepatikana na kosa apewe fursa ya kukata rufaa pia apate fursa ya kujitetea kwenye chombo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 14(1) maneno kwa idhini ya Waziri yaondoke na badala yake yawekwe maneno kwa kushauriana na Waziri wa Habari. Ni vizuri sana na muhimu Bodi ya chombo hiki ikawa huru bila kuingiliwa majukumu yake, wala kuamuliwa nini cha kufanya ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ianishe wazi kwenye Bodi uwiano wa wajumbe wanawake na wajumbe wanaume ili mawazo yanayowagusa wanawake yapate nafasi kwenye Vyombo vya Habari na kwenye jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 7(2) ni vizuri habari zinazoandikwa zisihatarishe usalama wa nchi. Swali muhimu hapa ni chombo gani kinachothibitisha kwamba, habari iliyoandikwa inahatarisha usalama? Isije kutokea mtu mmoja tu akaibuka na hoja itakayokandamiza uhuru wa habari. Hivyo, ni vizuri sheria iainishe wazi chombo kinachothibitisha habari na kiwe huru.