Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Magdalena Hamis Sakaya (43 total)

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba niulize swali moja dogo kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba ugonjwa huu siyo hatari, lakini kwa sasa hivi hapa Tanzania tunalo tatizo kubwa sana la uzazi. Ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu akinamama hawapati mimba na inasemekana kwamba hiki ni chanzo mojawapo cha kuzuia akina mama kupata mimba. Pamoja na kuwa anasema kwamba siyo ugonjwa hatari lakini haoni kwamba tatizo la familia kutokupata watoto ni tatizo kubwa hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nashukuru kwa swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua na nitalijibu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tunaposema ugonjwa fulani ni hatari tunaangalia ni kundi kubwa kiasi gani linapata ugonjwa huo. Hatusemi tu ni hatari kwa sababu ameupata mmoja na ameathirika, hizi ni taratibu za kitaalam, za epidemiology na labda niseme tu hili ndilo eneo nililobobea kitaaluma, epidemiology and public health.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi, kwa ugonjwa huu wa uterine fibroid, kiwango cha akinamama wanaoathirika na ugonjwa huu hakifiki 20%.
WABUNGE FULANI: Aaaah.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Hakifiki 20% ya akinamama wote na kwa maana hiyo hatuwezi kuweka programu maalum ya ugonjwa huu wakati tuna vipaumbele vingine vya magonjwa yanayowasibu akinamama kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tatizo la akinamama kupata shida ya kujifungua, ni kweli linahusiana na ugonjwa wa fibroid lakini sababu siyo ugonjwa wa fibroid, actually, akinamama wanapochelewa kushika mimba ndiyo wanaingia kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa fibroid. Kwa sababu ugonjwa wa fibroid unawapata akinamama wakiwa wanakaribia kipindi cha menopause yaani kati ya miaka 35 na kuendelea na siyo chini ya hapo...
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Inatarajiwa kibaiolojia akinamama wengi zaidi wawe wameshika mimba katika kipindi hicho.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kusema kwamba Daktari amejibu siyo tu kama ni Naibu Waziri bali amejibu kama mtaalam.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Kwa hiyo, amejibu na anajua anachokisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niahidi kitu kimoja, tutafanya semina kwa Wabunge ili kueleza suala hili na tuwape takwimu halisi ugonjwa huu unaathiri wanawake kiasi gani na tunayo maelezo hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nilitaka kuliweka hilo vizuri.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza swali, jibu lililotolewa kwenye swali namba (b) siyo kweli kwamba Wilaya ya Kaliua imepewa asilimia 70; Wilaya ya Kaliua ina vijiji 101, vilivyopewa ni 54 tu. Kwa hiyo, ni chini ya asilimia 70 kama asilimia 55. Kwa hiyo, kama lengo ni asilimia 70, Kaliua haijapata asilimia 70 kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali namba moja, mchakato mzima alioeleza Mheshimiwa Waziri, kuhusiana na namna ya kuweza kupata hizi kaya maskini ni kinadharia zaidi kuliko hali halisi kule kwenye vijiji. Kama ilikuwa inafuatwa kama ilivyoandikwa hapa, isingewezekana kwamba leo hii baadhi ya Watendaji familia zao zimewekwa kwenye mpango, wenye uwezo mzuri wamewekwa kwenye mpango, maskini kabisa wameachwa.
Kwa hiyo, naomba kujua Serikali kwa kuwa hapa imeandika vizuri, imeweka utaratibu gani basi, mpango mzuri kuhakikisha haya yaliyoandikwa kwenye suala namba „A‟ yanakwenda mpaka chini kwenye ground ili wale walengwa waweze kunufaika na mradi huu wa TASAF III. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; TASAF III inalenga zaidi kutoa fedha kuliko kuweka mfumo ambao utakuwa endelevu; na kwa kuwa mpango wowote kwa kuwa ni mradi, una muda wake; naomba kujua Serikali imejiandaa vipi baada ya Mradi wa TASAF III, zile familia ambazo zinapewa fedha cash haziwekewi utaratibu wa kuweza kujiendeleza, ziweze kuwa endelevu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Magdalena Sakaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na kipengele (b) kwamba wamenufaika na vijiji 54 wakati wana vijiji 101. Kwa mujibu ya taarifa za Mratibu na barua ninayo ya Machi, 2015, alieleza vimesalia vijiji 17 na nitaomba tu-share pamoja kukupa orodha hiyo na baadaye tufuatilie kwa nini visiwe ni vijiji 47 na yeye alete vijiji 17?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la kwanza kwamba katika mchakato au hatua ambazo nimeelezea za upatikanaji wa fedha za TASAF, kwamba ni wa kinadharia zaidi kuliko uhalisia; ni kweli changamoto zipo, nami naomba kupitia Bunge lako Tukufu, ukiangalia mchakato mzima wa Mpango huu wa TASAF III na awamu nyingine ambazo zilitangulia unabuniwa na jamii yenyewe. Wanachokifanya TASAF kupitia uwezeshaji wa Kitaifa wanaenda tu pale kusaidia katika kutoa elimu, kuwasaidia wananchi wa eneo husika waweze kujua ni namna gani wanaibua miradi yao.
Mheshimiwa Maibu Spika, tatizo kubwa tumegundua linajitokeza katika vijana wetu ambao siyo waaminifu ambao wanapita katika kila kaya kufanya madodoso; kwa hiyo, naomba tushirikiane, mtakapoona kuna udanganyifu wowote, ziko taratibu za malalamiko. Iko fomu Na. HU1 ya malalamiko na madai. Basi wakati wowote wanakijiji wahudhurie mikutano hii inapoitishwa, lakini vile vile wanapoona kuna kaya ambayo imeorodheshwa na siyo kaya masikini sana, basi pale pale wao kupitia Mkutano wa Kijiji waweze kuchukua hatua na mtu huyo aweze kuondolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile inapokuwa orodha hii imefikishwa TASAF Makao Makuu, wanapoanza kufanya uchambuzi kupitia kompyuta, ni uchambuzi ambao unaangalia vigezo vya umaskini kwa mujibu wa Household Survey ambayo inatolewa na National Bureau of Statistics. Wakati mwingine unakuta kaya zinazofanyiwa dodoso majumbani, hawaelezi ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mara nyingi kaya ambazo zinastahili kufuatwa ni zile kaya ambazo unakuta hazina hata mlo mmoja kwa siku; ni zile kaya ambazo haziwezi kumudu gharama za matibabu; ni zile kaya ambazo haziwezi kumudu huduma mbalimbali za kijamii, lakini vilevile zina watoto wengi na zinashindwa kuwapeleka shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kupitia Bunge hili tuelimishe wananchi wetu, lakini na sisi kama TASAF, tutaendelea kuto elimu hii. Wananchi wetu kwenye zile kaya wanapofanyiwa madodoso, basi waweze kutoa taarifa zenye ukweli ili waweze kunufaika. Vilevile kupitia uongozi wa vijiji, katika mikutano ile, wanapoona mara moja kuna mtu ambaye hastahili kuingizwa, basi mara moja waweze kumtoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu tulizonazo, unajikuta katika mikutano mingine wale viongozi wa vijiji wote wanawaogopa, wanajikuta hawawezi kubainisha upungufu uliopo. Kwa hiyo, naomba sana tushirikiane kwenye hili, wakati wowote nitakuwa tayari na sisi tutafanya uhakiki na kuhakikisha kwamba hatua zinachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshaanza kuchukua hatua. Mfano, kwa upande wa Karagwe tulichukua hatua katika Kijiji cha Kibondo lakini vile vile kwa Wilaya ya Kalambo na kwenyewe tulichukua hatua dhidi ya watumishi ambao wamefanya ubadhirifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili kwamba tumejiandaa vipi kuhakikisha sasa fedha hizi zinakuwa endelevu? Ukiangalia programu hii imeanza mwaka 2000 na hii ni awamu ya tatu; mara nyingi wale wanufaika au walengwa wanatakiwa wapate huduma hii kwa miaka mitatu. Baada ya miaka mitatu tunafanya tathmini kuangalia kama wameweza kuondokana na hali ya umaskini. Kwa kweli kwa msingi mkubwa wengi takribani asilimia 52 ambao wamekuwa wakinufaika, wameweza kunufaika na kuondokana na umasikini.
Kwa hiyo, tujitahidi tuendelee kuelimisha, waweze kunifaika, maana wako wengine wamekuwa wakitisha watu kwamba fedha hizi ni za Freemason, fedha hizi sijui ni za kitu gani; na unakuta wanufaika wengine wamekuwa hawajitokezi kunufaika nazo.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana tangu tarehe 18 Septemba, 2014 mpaka leo ni miaka miwili; taarifa ilikabidhiwa na mpaka leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa za kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kuendelea kuchelewa kuchukua hatua kwenye masuala ya msingi kama haya yanayohusu masuala ya kilimo wakati tunasema kilimo ni uti wa mgongo; inazidi kudidimiza kilimo ambacho ndio hasa sehemu kubwa ya uchumi wetu na hivyo Serikali ipo tayari sasa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha wale wote waliohusika wanafilisiwa kwanza mali zao wakati hatua za kuwafikisha mahakamani zinafuata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili hakuna kilimo chenye tija bila kuwa na ushirika wenye nguvu; COASCO ambayo imepewa jukumu la kukagua vyama vya ushirika Tanzania imeshindwa kabisa kutimiza wajibu wake. Serikali sasa haioni sababu kuweza kukabidhi jukumu la ukaguzi wa Vyama vya Ushirika kwa Ofisi ya CAG ili watimize wajibu huu? Fedha zinazoibiwa ni fedha za Watanzania, ni fedha za wakulima lakini pia ni fedha za Serikali. Ili jukumu hili likaguliwe na Ofisi ya CAG na hivyo kuweza kusaidia kilimo na wananchi kwa ujumla. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba hatua za kuwachukulia wahusika kuwapeleka mahakamani imechukua muda mrefu. Hata hivyo, nimueleze tu kwamba ni changamoto ya jumla katika sekta yetu ya kutoa haki na ndio maana kuna hatua mbalimbali zinaendelea ndani ya Serikali ili kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya kuona kwamba baada ya kuona kwamba utaratibu wa kuwatumia wanasheria wanaotoka kwa DPP; Wizara yangu kwa kupitia Tume ya Ushirika tayari imeandika barua ya kuomba ruhusa ya kuwatumia wanasheria waliopo kwenye Tume ya Ushirika ili wao waweze kuhusika katika kuendesha kesi za ushirika. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi ombi letu hilo litakapokubalika na tunalifuatilia kwa karibu sana; wanasheria wetu watahakikisha kwamba kesi hizo zinaendeshwa kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu COASCO; napenda vilevile kukubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbungekwamba COASCO imekuwa ikituletea matatizo na changamoto katika ukaguzi wa Vyama vya Ushirika. Badala ya kutumia Ofisi ya CAG kwa sasa Wizara yangu inafanya utaratibu wa kurekebisha kasoro za kiutendaji zilizopo ndani ya COASCO ili iendelee kutoa huduma za ukaguzi kwa haraka kwa sababu wao ndio wanatambuliwa kwenye Sheria ya Ushirika Namba Sita ya mwaka 2013 kama ndio wakaguzi wa vyama hivi vya ushirika. Tunatambua changamoto tunaifayia kazi, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru kwa nafasi, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa utendaji mbovu na kutokuwajibika kwa watendaji wa ardhi waliopo kwenye Halmashauri kunachangiwa pia na muundo mzima kwamba watendaji wale hawapata order wala maelekezo kutoka kwenye Serikali Kuu kwa maana ya kwenye Wizara, na hasa wanapokosea inakuwa ni vigumu kwa Waziri kutoka juu kumchukulia hatua kwa sababu anasikiliza sana kwenye Halmashauri.
Je, Serikali haioni umuhimu sasa, kwa unyeti wa Wizara hii na kuondoa migogoro ndani ya nchi yetu kuhakikisha kwamba watendaji wote wa ardhi wanapokea order kutoka juu na hata wanapokosea waweze kuchukuliwa hatua kutoka juu ili kuondoa migogoro ndani ya nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, utendaji mbovu wa watumishi hasa kwenye sekta ya ardhi nadhani siyo suala tu pia la kujua kwamba anapokea order kutoka mamlaka ipi. Ni kweli katika ule mlolongo uliopo pengine unaweza ukaliona hivyo, lakini nia ya Serikali kugatua madaraka na kusogeza huduma katika Halmashauri zetu ilikuwa ni nia njema na dhamira ya dhati ya kutaka kuona kwamba huduma zile zinafanyika kwa wakati mahali ambapo watu wanahitaji.
Mheshimiwa Spika, lakini hili kama limekuwa ni tatizo, nadhani suala la msingi ni ndani ya Serikali kuweza kuona namna ya kuweza kudhibiti udhaifu huu au utendaji huu mbovu uliopo ili tuweze kujua kwamba hapa kinachotakiwa kufanyika, kama mtumishi ambaye anafanya utendaji wake katika viwango visivyostahili na akitarajia tu kabisa kwamba mamlaka yenye sauti kwake ni mamlaka fulani, hilo halimfanyi yeye asamehewe katika kosa alilolifanya.
Kwa hiyo tunachosema, ugatuaji wa madaraka ilikuwa ni kusogeza huduma, lakini kama suala la kitaaluma au suala la kitendaji linaonekana lina ugumu katika namna ya kudhibiti watendaji hawa, nadhani ni suala la kuongea kati ya Wizara zote mbili husika tukajua ni jinsi gani watu hawa tutaweza kuwasimamia vizuri zaidi ili wafanye kazi zao kwa weledi.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali inatambua mchango wa zao la tumbaku kwenye uchumi wa Taifa hili na hivi tunavyoongea makampuni kwenye Vyama vya Ushirika hawajatoa makisio kabisa maeneo mengine na maeneo mengine wametoa makisio madogo sana, kiasi kwamba wakulima wengi mwaka huu wanashindwa kwenda kulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweke commitment hapa, itafanya utaratibu gani wa haraka kuhakikisha makampuni haya yanatoa makisio kwenye Vyama vya Msingi ili wakulima ambao wanalima miaka yote waweze kulima kwa sababu ndiyo sehemu ya maisha hayo? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika msimu unaokuja, makisio yamekuwa ni ya kiasi kidogo kuliko msimu uliopita. Makisio ya msimu unaokuja ni kilo milioni 55.9 wakati msimu uliopita ni kilo milioni 60. Kwa hiyo, maana yake ni tumbaku kidogo itanunuliwa ukilinganisha na msimu uliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, shida hii imetokea kwa sababu kulikuwa na kutoelewana katika bei ya dira kati ya makampuni na Vyama Vikuu. Kwa hiyo, Serikali inachojaribu kufanya ni kuweka mikakati ili makubaliano ya bei yaweze kufanyika mapema ili katika msimu mwingine tusije tukapunguza hizi kilo, ila ziongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachoweza kusema kwa sasa ni kwamba, tayari makubaliano yameshatokea, sisi tunaangalia huko mbele kuhakikisha kwamba tunaongeza kilo ambazo zitanunuliwa.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na maagizo mbalimbali na matamko mbalimbali yanayotolewa hapa Bungeni na hata nje ya Bunge na Serikali kuhusiana na kutoa huduma bure kwa makundi haya muhimu, bado tumeshuhudia akina mama wanaojifungua hospitali wanazuiliwa na vichanga vyao kwa sababu tu wameshindwa kulipa gharama za kujifungua.
Je, Serikali inasemaje kuhusiana na haya yanayofanywa na uongozi wa hospitali kama Muhimbili, hospitali kubwa kumzuia mwanamke ndani ya hospitali zaidi ya wiki kwa sababu ameshindwa kulipa huduma za kujifungua. Serikali haioni kwamba inakwenda kinyume na sera zake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa kuna matukio ya baadhi ya vituo vya kutolea huduma nchini kukiuka utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007. Nakiri kuwepo kwa mapungufu hayo, lakini tayari kwa kuwa tulipata taarifa tulikwisha kutoa maelekezo na hapa Bungeni katika Bunge lililopita nilieleza na kufafanua wazi kwamba Sera ya Afya inaelekeza wakina mama wajawazito wote na watoto wote chini ya miaka mitano watibiwe bure, pamoja na makundi mengine mabayo nilitaja kwenye jibu la msingi.
Mheshimiwa Spika, ninaagiza kwa mara nyingine tena, ninaagiza watoa huduma wote wa afya wa Serikali ama wenye mikataba na Serikali watoe huduma hizi bure kama Sera ya Afya inavyosema. Nikikuta ama nikipata taarifa kituo chochote kile cha kutolea huduma hakifuati misingi hii inayoagizwa na sera nitachukua hatua kali dhidi ya viongozi wa taasisi husika.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Kaliua na Jimbo la Kaliua wana adha kubwa ya maji na ardhi ya Tabora nzima ikiwepo na Kaliua visima vikichimbwa vinatoa maji kidogo sana. Namna pekee ya kusaidia wananchi wa Kaliua na Wilaya nyingine ni kuweza kupata maji kutoka mto mkubwa wa Malagarasi. Je, ni lini mradi mkubwa wa kutoa maji Malagarasi kwenda Kaliua mpaka Urambo utaanza na utakamilika lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imekamilisha mradi wa upembuzi yakinifu wa kutoa maji kutoka Mto Malagarasi kupeleka Kaliua na Urambo. Sasa hivi mkandarasi anaendelea na usanifu wa kina wa mradi huo. Baada ya kukamilisha usanifu wa kina Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya mradi huo kukamilika sasa tutakuwa na chanzo cha uhakika kutoka Malagarasi kuleta maji Kaliua, Urambo na hatimaye kupeleka Tabora. Ni kweli kabisa ulichosema chini ya ardhi katika Mkoa wa Tabora maji ni kidogo sana.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni kwa nini Serikali inaruhusu na kutoa vibali kujengwa kwa hoteli za kitalii kuzunguka rim ya Ngorongoro Crater hali inayoharibu mandhari ya Ngorongoro lakini pia ni vyanzo vya maji kwa ajili ya hifadhi hii?
Swali la pili, wakati Ngorongoro inaanzishwa mwaka 1959 ilikuwa na wakazi 8,000 lakini kwa takwimu za mwaka 2013 hifadhi hii ina wakazi elfu 87.7 kwa hivyo leo tunavyozungumza ni zaidi ya laki moja. Lakini kuongezeka kwa watu maana yake ni kuongezeka kwa mifugo lakini pia kuongezeka kwa mahitaji na huduma mbalimbali.
Naomba Serikali iliambie Bunge, wakati Hifadhi
inaanzishwa, master plan ya Ngorongoro Crater inasemaje juu ya uwepo wa idadi gani ya watu ambao wanaweza kuhudumiwa kikamilifu wakapata huduma zote, lakini pia hadhi ya hifadhi ikaendelea kubaki kama ambavyo tunategemea? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Magdalena Sakaya kwa kuwa kwanza yeye ni Mhifadhi kitaaluma lakini pia amekuwa miongoni mwa Wajumbe wa
Kamati ya Maliasili na Utalii ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kuishauri Serikali kuhusiana na masuala ya maliasili na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza ni kweli ukienda Ngorongoro leo utakuta kuna hoteli zimejengwa kandokando ya crater kwenye eneo linaloitwa rim ya crater. Lakini uwepo wa hoteli hizi ni ambao umetokana na mabadiliko mbalimbali tangu sheria ilipokuwa imeandikwa kwa mara ya kwanza mwaka 1952.
Sheria hii ilifanyiwa marekebisho ya kwanza mwaka 1963 lakini baadae sheria hiyo ilifanyiwa marejeo mwaka 2002. Katika vipindi hivyo mabadiliko mbalimbali yametokea, sasa tangu
amri ilivyotolewa kutokana na sheria kwamba sasa hakuna kuanzisha hoteli kandokando ya crater na hasa kwenye eneo la rim hakuna hoteli nyingine yoyote imeanzishwa katika kipindi hicho. Nyingi zilizopo ni zile ambazo zilianzishwa katika
kipindi cha nyuma.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili ni kweli kwamba mwaka 1959 wakati sheria hii inapitishwa kulikuwa na takribani watu 8,000 katika eneo la hifadhi na kwamba ni ukweli ulio wazi takwimu zinaonesha mwaka 2013 tayari idadi ya watu ilifikia 87,851. Ukifanya hesabu ni kama vile ongezeko la wakaazi 1500 takriban kwa kila mwaka. Hili ni ongezeko linaloashiria kwamba leo tukifanya takwimu kweli tunaweza kupata wakaazi wanaokaribia laki moja, hii ni idadi kubwa sana na ni tishio kwa shughuli za hifadhi katika eneo hili la Hifadhi la Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, hatua ambazo Serikali inafanya kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni uwepo wa sheria peke yake utakaoweza kutoa mwongozo na mwelekeo namna gani tunaweza kukabiliana na changamoto za hifadhi katika eneo la Ngorongoro. Sasa sheria iliyopo ina mapungufu ni kweli na ndiyo maana nimesema katika jibu la msingi kwamba katika kipindi cha muda mfupi ujao mchakato wa kufanya marekebisho ya sheria ili iendane na matakwa ya sasa ya uhifadhi katika eneo linalohusika utaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, mara Serikali itakapoleta sheria hii mbele ya Bunge hili baada ya kukamilisha michakato ya awali, wote tuwe na spirit ya kutaka uhifadhi uimarishwe katika eneo la
Ngorongoro ili tuweze kupata faida zote za urithi na kiuchumi na faida nyingine zote zinazotokana na uhifadhi kupitia utalii.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika majibu yake ya msingi amesema kwamba ziko fedha ambazo zimelipwa kwa madai ya walimu lakini ni kidogo sana kuendana na madai halisi ya walimu wa Tanzania kwa miaka karibu mitatu iliyopita. Kwa Wilaya ya Kaliua tu walimu wa sekondari wanadai shilingi 221,347,561 kwa mwaka 2015/2016 tu. Ni lini sasa madai haya ya walimu kwa Wilaya ya Kaliua yatalipwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kimsingi tunatambua kwamba kuna madeni ya walimu lakini naomba pia mnikubalie kwamba kweli kuna baadhi ya madeni sio madeni halali. Uzoefu unaonesha kwamba baada ya uhakiki kuna baadhi ya madeni yanashuka mpaka kufikia moja ya tatu kitu ambacho kinasikitisha na kimekuwa kikichelewesha kuwalipa walimu kwa wakati pamoja na watumishi wengine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni rai yangu kwa watumishi wote waone jambo la kulipwa ni haki yao lakini vilevile ni vyema madai yakawa halali ili kuepusha usumbufu usio wa lazima. Haipendezi sana mtu umedai halafu baadaye unaambiwa hayo madai hayastahili kwa sababu taratibu na kanuni zetu tunazijua na hivyo unaweza ukajua ni kipi unastahili na kipi hustahili.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa maneno ya Mheshimiwa Mbunge tutajitahidi kufuatilia katika Wilaya au Jimbo lako kuona kwamba hawa watumishi wanaostahili kulipwa waweze kulipwa kwa wakati baada ya uhakiki.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tatizo kubwa ni kwamba Halmashauri zetu hazina uwezo wa kutosha wa kupima maeneo yao ili kugawa viwanja na hivyo kuwepo na makazi bora, Serikali sasa ina mpango gani mahususi wa kutoa fungu maalum kwa ajili ya Halmashauri iwe kama revolving fund, wakishapima maeneo waweze kuyauza then warudishe ile fedha na hivyo kuhamishiwa kwenye Halmashauri nyingine ili Halmashauri zote hapa nchini ziweze kupima maeneo yao na hivyo kuwa na makazi bora kwa wananchi wetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, suala alilolizungumza Mheshimiwa Sakaya, ni kweli, Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kufanya kazi hiyo, lakini ndani ya Wizara tulikuwa tumeanzisha mfuko huu kwa ajili ya kuwezesha Halmashauri mbalimbali kuweza kupima na kuuza viwanja na baadaye kurejesha madeni yao.
Mheshimiwa Spika, lakini kumekuwa na mfano mbaya ambapo Halmashauri nyingi hazirejeshi na mpaka sasa tunadai zaidi ya Halmashauri saba ambazo zimechukua na hazijarejesha na wengine wamerejesha kiasi, na ninadhani kama Mjumbe pia anayo taarifa, tulishawasilisha wale ambao wanadaiwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tusingependa pia kuendeleza kuwa na madeni haya na ndiyo maana Serikali inahimiza makusanyo ya ndani ya Halmashauri zenyewe zinazohusika. Pia wanayo fursa ya kupata mikopo kutoka katika mabenki mbalimbali ambayo yanaweza kutumika katika zoezi hilo. Ndiyo maana pia tumeruhusu wataalam mbalimbali wa kutoka kwenye private sector kufanya zoezi hilo la upimaji. Katika kupima, siyo lazima ulipe cash, kuna ile barter trade tunayosema wanaweza wakafanya.
Kwa hiyo, kuna maeneo mengine ambayo wameshaanza; ukiangalia Mkoa wa Katavi, kuna maeneo mengi wanafanya kwa kukubaliana mpimaji na Halmashauri, wanaachiana asilimia kadhaa, hawalipi cash isipokuwa vile viwanja anavyopima anauza anapata hela yake na Halmashauri inaachiwa vingine kwa ajili ya kuweza kutengeneza miundombinu.
Mheshimiwa Spika, hata yule mmiliki wa kiwanja, kama ana kiwanja kikubwa kimetoa viwanja labda vitano, wanakubaliana asilimia kadhaa; anaachiwa viwanja vyake vingine wanachukua Halmashauri wanauza wanatengeneza miundombinu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, siyo lazima kuwe na cash, ni namna ambayo unaweza ukaifanya na hasa kwa maeneo ya vijijini. Kwa mijini inaweza ikawa ngumu kidogo, lakini vijijini inawezekana kwa kufanya barter trade na bado zoezi la upimaji likafanyika vizuri.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imejidhatiti kukusanya mapato kwa kupitia mashine hizi za EFD, lakini kuna matatizo makubwa ya kutokuwepo kwa mtandao au mawasiliano tunapoenda kwenye vituo vya manunuzi, vinavyosababisha wanunuzi kukaa kwenye vituo kwa muda mrefu wakisubiri risiti au wakati mwingine tunakata tamaa tunaondoka bila kuwepo na risiti.
Je, Serikali ina mpango gani makini kuhakikisha kwamba inaboresha mfumo wa kukusanya kodi pamoja na kupata huduma kwa muda unaotakiwa ili kuhakikisha kwamba kile walichokikusudia kinaliletea Taifa mapato kwa maendeleo yetu? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba lipo hili tatizo kwa baadhi ya wauzaji na wafanyabiashara ndani ya nchi yetu. Tatizo la kimtandao halipo kwa kiwango ambacho wafanyabiashara wanakisema, nitoe wito kwa Wabunge kama viongozi kwenye maeneo yetu tushikamane na Serikali yetu kwa sababu hakuna maendeleo bila kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tushirikiane katika kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia mashine hizi kwa pamoja, lakini TRA wanafanya jitihada kubwa za kupita maeneo ya wafanyabiashara wetu kuhakikisha kwamba mashine hizi zinatumika na zinafanya kazi. Ni wito wangu kwenu Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kuhakikisha hili linaweza kufanyika ndani ya nchi yetu.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kaliua - Ulambo ambayo inakilometa 34 ilishafanyiwa upembuzi yakinifu, ishapata fedha, tender ilishafunguliwa na ilitakiwa ianze ujenzi mwezi wa pili mwaka huu. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri ni nini kinachozuia ujenzi wa barabara hii kuanza wakati sasa hivi ni mbovu sana na wananchi wa Kaliua wanateseka sana kwenda Urambo na maeneo mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Magdalena Sakaya ni matatizo tu ya procurement ni kweli process zilianza mapema lakini bado hazijakamilika na nikuhakikishie kwamba barabara hii itajengwa muda sio mrefu kwa sababu tayari tumepata idhini ya kuanza ujenzi wa hiyo barabara.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba na mimi nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, umeme wa REA unatarajiwa kuwa
ni tegemeo kubwa sana kwa wananchi, lakini pia kuinua uchumi kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo, lakini Kaliua umeme wa REA umekuwa unakatika mara kwa mara, Mheshimiwa Waziri nimeshakuja kwako mara nyingi tu kuhusiana na suala hili. Kwa siku zaidi ya masaa nane, masaa manne unawaka, masaa nane hauwaki, kwa hiyo lile tegemeo halipo tena kwa wananchi wale. Mheshimiwa Waziri aliahidi kujenga substation pale Kaliua alivyotembelea mwaka 2015.
Naomba kujua sasa Serikali ina mpango mkakati gani kuhakikisha kwamba inajenga substation pale Kaliua ili umeme wa REA uweze kuwa na tija na kuinua uchumi wa wanachi wa Kaliua? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, Mheshimiwa Sakaya nilipokuja kwako nilitembea na wewe sana na naomba niendelee kutembea na wewe nikija tena. Lakini pia … (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ni kweli alivyosema Mheshimiwa Mbunge, umeme unaosafiri kwenda Kaliua ni ule unaotoka Tabora - Urambo, - Kaliua hadi Uvinza, kwa hiyo, ni umbali mrefu sana. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mbunge anavyosema, transfoma ya kusafirisha umeme iliyopo Tabora ndiyo inayohusika kusafirisha umeme katika Majimbo ya Kaliua, Urambo mpaka Uvinza, umbali wa kilometa 372. Mkakati madhubuti wa kumaliza tatizo hili la kukatika kwa umeme ni kuwa Serikali sasa inajenga substation katikati ya Kaliua pamoja na Urambo katika eneo la Gologolo.
Kwa hiyo, utaratibu umeanza na wakati utekelezaji
wa REA utakapoanza basi wananchi watapata umeme huo lakini katika jibu langu litakalofuata kwa swali la msingi nitaeleza kwa upana zaidi lakini nimpe uhakika Mheshimiwa Mbunge utaratibu fedha zimeshatengwa na survey imekamilika na ujenzi utaanza hivi karibuni.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa huu ni mwaka wa nne tangu Serikali ilivyokuja na mpango wa kutoa maji Malagarasi lakini bado mradi uko kwenye upembuzi yakinifu na hata fedha iliyotengwa, shilingi bilioni mbili mwaka huu ni kwa ajili ya upembuzi yakinifu, wakati huohuo wananchi wa Kaliua wanaendelea kuteseka kupata maji na akina mama wanateseka na watoto hawaendi shule kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa huu ni mpango wa muda mrefu, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuwapatia wananchi wa Kaliua maji ya uhakika na masafi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Kampuni ya GTI imefanikiwa kuchimba kisima cha maji kwenye Kata moja ya Usindi na ikapata maji mengi pamoja na kuwa ardhi ya Kaliua haina maji kwenye water table, Serikali sasa ina mpango gani wa kupeleka wataalam wenye uwezo mkubwa Kaliua waweze kugundua maeneo yenye maji ya uhakika kwenye ardhi ili angalau tupate visima vyenye maji ya kutosha wananchi wapate maji ya kutosha waache kuteseka na adha kubwa ya maji Jimbo la Kaliua? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Sakaya alikuja ofisini na tukazungumza matatizo ya maji katika Wilaya yake na nikamueleza kwamba nitapeleka wataalam kupitia TUWASA ili wakasaidiane na Mhandisi wa Wilaya, inaonekana kidogo Mhandisi wa Wilaya hana uwezo wa kuweza kufanya usanifu wa miradi maana mpaka sasa ametengewa shilingi milioni 692 anataka azitumie zote kufanya usanifu, nimekataa kwamba haiwezekani ukatumia shilingi milioni 600 kwa usanifu, tunataka tupate matokeo.
Kwa hiyo, napeleka wataalam ili wakashirikiane angalau hata hicho kisima anachokizungumza tuweze kukiendeleza wananchi wa pale waweze kupata maji.(Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi tunaowapa elimu kwa ajili ya ufugaji wa samaki katika maeneo mbalimbali, wamekuwa wanahamasika na wanajenga mabwawa ya samaki lakini wanakosa vifaranga kwa muda mrefu, zaidi ya miaka miwili mpaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango gani kuhakikisha maeneo yote ambayo tunatoa elimu ya ufugaji wa samaki, tunanunua mashine za kutosha za kutotoa vifaranga vya samaki ili wananchi wale waweze kupata vifaranga kwa urahisi, lakini kwa bei nzuri waweze kunufaika na ufugaji wa samaki maeneo wanayokaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge lako Tukufu nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna ukosefu wa vifaranga vya samaki. Kwa sasa kama kuna mtu yeyote ambaye anataka vifaranga, awasiliane na Wizara. Kimsingi vifaranga vya samaki mbalimbali wanazalishwa katika vituo vyetu vya uvuvi.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama wananchi wake wanataka kuwekeza katika ufugaji wa samaki, anione nimwelekeze namna ya kupata vifaranga vya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimfahamishe
Mheshimiwa Mbunge kwamba hata kwenye Ziwa Victoria Serikali imejipanga, kuna mradi ambao tunauanza katika mwaka huu wa fedha unaokuja wa kuwekeza vifaranga vya zaidi ya milioni 50 katika Ziwa Victoria ili kuendelea ku-boost uzalishaji wa sangara na sato. Kwa hiyo, kama kuna upungufu wowote Mheshimiwa Mbunge anaweza akaniona.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, suala la ajali hizi kutokana na jibu la msingi imekuwa ni hatari kubwa na ukiangalia idadi ya watu waliopoteza maisha, waliopata ulemavu na majeruhi ni wengi. Vilevile ajali hizi zinasababisha kuwepo kwa walemavu, wategemezi, wajane na wagane wengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua ambazo zinachukuliwa na Wizara na Serikali kuona kwamba ajali zinapungua lakini bado ajali zinaongezeka.
Je, Serikali haioni sababu kubwa ya ajali hizi ni kwamba madereva wa bodaboda hawafuati sheria za barabarani ikiwepo ku-overtake kushoto badala ya kulia? Serikali haioni sababu ya kuendesha masomo au mafunzo maalum kila Wilaya kwa bodaboda wote waweze kuelewa kanuni na sheria za barabarani na hivyo kuweza kupunguza ajali za barabarani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, baadhi ya maaskari barabarani badala ya kuwaelimisha bodaboda wamefanya bodaboda ni vyanzo vya mapato, kila wakiwaona wanakimbizana nao barabarani matokeo yake wao wanakuwa ni kisababishi cha ajali badala ya kupunguza ajali. Serikali inafanya nini na inachukua hatua gani kwa wale maaskari wote ambao wanakimbizana na bodaboda barabarani hajali amebeba abiria au hajabeba abiria ili kupunguza ajali hizi na kuokoa maisha ya Watanzania wanaopoteza maisha? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mbunge kwamba jambo hili linamgusa na ameongea kwa hisia kama mama na kama mwakilishi wa vijana wetu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Serikali imefanya jitihada kubwa kama ambavyo nimeelezea, jambo ambalo limesalia ni familia zetu kuanzia ngazi za familia na ngazi za vijiwe, kuliongea jambo hili kama moja ya jambo linalomaliza maisha ya vijana wetu. Kila tunapokaa tuambizane kwamba ukienda mwendo kasi, usipofuata taratibu za uendeshaji wa vifaa hivi vya moto, madhara yake ni kupoteza maisha ya mwendeshaji mwenyewe ama yule aliyebebwa. Kwa hiyo, hili jambo likienea elimu yake itakuwa kubwa kuliko hii tu ambayo mpaka sasa tunaendelea kuifanya ya kutoa semina Wilaya kwa Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu vijana hawa kukimbizwa na askari, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge ukichukulia kwenye sura moja unaweza ukaona kama vijana wanaonewa sana lakini niseme kuna utaratibu ambao unakuwa unakosewa. Moja, vijana wanakuwa wameshapewa leseni lakini inatokea wanapokuwa kule vijiweni wanakabidhiana bodaboda hizi kwa mtu ambaye hana leseni, mtu ambaye hana mafunzo yaani amejaribisha tu akaona pikipiki inatembea naye anabeba abiria, hili ni kosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimewaelekeza viongozi wa vijiwe vile vya bodaboda kwamba na wenyewe watimize majukumu ya kiuongozi kwamba akitokea mwenzao aliyekosea na wenyewe wawe tayari kumwambia unatakiwa uripoti kistaarabu polisi ili uweze kumaliza jambo lako la kisheria. Kama hawatafanya hivyo, polisi itakuwa haina njia nyingine zaidi ya kumtafuta kwa nguvu na kuweza kumkimbiza popote pale ambapo yupo aweze kufikishwa katika mkono wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tunawapenda sana vijana wetu lakini mapenzi yetu kwa vijana wetu ni kuhakikisha tunaokoa maisha yao. Kwa hiyo, huruma tunayoweza kufanya ni kuhakikisha tunadhibiti jambo hili na hamna njia mbadala zaidi ya kuweza kuhakikisha tunachukua hatua za kisheria kwa yule ambaye anaonekana anakiuka sheria. Kwa wale ambao kwenye vijiwe vyao watatimiza maelekezo haya, tumeelekeza askari wasikimbizane nao bali wamalize kistaarabu mambo ambayo yanahusu sheria.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmshauri ya Kaliua ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 76, waliopo ni asilimia 24 tu. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kuna mkakati gani wa dharura kuhakikisha kwamba angalau kwa Kaliua kabla hata ya kuandika barua maana nasema hapa wanapatiwa watumishi wa afya ili akina mama waache kuteseka kwa kukosa huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):Mheshimiwa Naibu Spika, umenisaidia kwa sababu majibu aliyotoa Mheshimiwa Waziri wa Nchi na Mheshimiwa Sakaya yuko hapa, sidhani kama itakuchukua muda mrefu kuandika barua kuainisha huo upungufu ili hili jambo liweze kufanyiwa kazi kwa mara moja.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kumuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza Halmashauri ya Kaliua hatujafikiwa kuwa asilimia 70 tumefikiwa kwa asilimia 50 tu; kati ya vijiji 102 ni vijiji 54 tu. Katika vijiji ambavyo vilipata miradi kuna baadhi ya makosa ambayo yalifanyika katika kuanisha wale ambao walikuwa ni walengwa na baada ya kulalamika wakaambiwa waandike rufaa kwa sababu kuna wazee ambao wanastahili kupata mradi hawakupewa mradi wakaenda kupewa watu ambao wana uwezo. Leo ni mwaka wa pili waliambiwa waandike rufaa na mpaka leo rufaa haijarudi wala majina yao hayajaingizwa kwenye mradi, jambo ambalo limeleta manunguniko makubwa na masikitiko kwa sababu wanashindwa kuishi lakini wenzao ambao wana hali nzuri wanaendela kupata mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba zile rufaa ambazo ziliandikwa na walengwa zinarudi ili waingizwe kwenye mradi waendelee kunufaika na mradi huu wa kunusuru kaya maskini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili mradi huu umeanza mwaka 2013, lakini kwa baadhi ya wilaya ikiwemo Kaliua tumeanza mwaka 2015, Januari. Naomba kuuliza Serikali kwa zile wilaya ambazo zilichelewa kupata mradi kwa miaka miwili, je, wataendeleza mradi kwa miaka 10 kama ilivyo kawaida au wataenda kufanya evaluation kama wanavyokwenda nchi nzima na kusahau kwamba sasa hivi mradi ni mwaka wa tatu wakati wengine ni mwaka wa tano? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Sakaya kwa jinsi anavyofuatilia kunusuru kaya maskini katika jimbo lake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza kwamba kwake tumefikia asilimia 50 sio 70 kama katika maeneo mengine mimi kama Waziri ninayesimamia masuala ya TASAF nitafuatilia nione nini kimesababisha wao wawe chini kulingana na wilaya nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, anasema makosa yalifanyika katika kuwabaini walengwa na naomba nichukue nafasi kulieleza Bunge lako Tukufu, Watendaji wa TASAF hawana kauli juu ya nani asaidiwe. Wenye kauli juu ya nani asaidiwe ni watu katika mtaa, shehia, wao ndio wanaokaa wanasema hapa kijijini fulani bin fulani hali yake si nzuri. Kwa hiyo kwa yale maeneo ambayo makosa haya yamefanyika ni makosa ya wanavijiji na hasa viongozi wa vijiji kule Kaliua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale ambapo mmetuletea watu ambao hawakuhusika wamelipishwa fedha. Juzi nilikuwa Singida vijijini, watu walilipishwa milioni tatu laki tisa ambao hawahusiki, wamesharudisha milioni tatu bado laki tisa; na kila mahali wanarudisha. Katika maeneo mengine tumewawajibisha watendaji wa TASAF ambao walishiriki katika udanganyifu huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zile wilaya ambazo zilichelewa nalo siwezi kuwa na jibu la moja kwa moja hapa, nitalifanyia utafiti nijue walichelewa kwa sababu gani na nitachukua hatua stahiki.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Dodoma sasa hivi ni Makao Makuu ya nchi na Manispaa wameongezewa jukumu lingine la ardhi ambalo lilikuwa la CDA, lakini kuna upungufu mkubwa wa vitendea kazi pale Manispaa hasa ile Idara ya Ardhi pamoja na watendaji ni wachache kiasi kwamba ukienda pale bado kuna watu wengi wanakaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
Serikali sasa kwa kutambua kwamba Dodoma ni Makao Makuu, imejipangaje kuhakikisha kwamba Manispaa ya Dodoma inawezeshwa kwa vitendea kazi, miundombinu pamoja na watendaji wa kutosha ili wafanye kazi kwa weledi na kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupata nguvu kazi ya kutosha kutoka kwenye ile iliyokuwa CDA, ni kweli kwamba bado kuna mahitaji ya watumishi na baadhi ya vitendea kazi na hivyo vinafanyiwa kazi mpaka mwezi wa sita, matatizo mengi yatakuwa yamekamilika.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wapo watoto walemavu wa aina mbalimbali wanaokosa kupata elimu kutokana na uchache wa shule maalum kwa watoto hawa na hasa kwa Mkoa wa Tabora ambao una shule moja tu ya mission; kwa hiyo, watoto wengi wa Kaliua na maeneo mbalimbali wanakosa kupata elimu kutokana na kwamba kile kituo kina idadi maalum ya watoto walemavu.
Je, Serikali ina mpango gani maalum wa kuhakikisha kwamba kila mkoa, hasa Mkoa wa Tabora kunajengwa shule maalum ili watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali waweze kupata elimu sawa na watoto wengine? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli swali hili ni la msingi sana na Serikali tumeliona hili. Ndiyo maana katika Ofisi yetu ya Rais, TAMISEMI hivi sasa tuna Mkurugenzi maalum anayehusika na Dawati la Ulemavu. Lengo kubwa ni kuhakikisha tunafanya hilo vizuri. Hata hivyo, nataka nilijulishe Bunge lako hili Tukufu leo hii, Mheshimiwa Waziri Mkuu leo hii anapokea vifaa mbalimbali vikiwemo vya maabara, sambamba na vifaa vyote vya kielimu katika makundi ya walemavu. Tukio hilo linafanyika pale Lugalo na Shule moja ya Uhuru Mchanganyiko itaenda kupatiwa majira ya saa 7.00 mchana, kuona commitment ya Serikali katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nini tunatakiwa kukifanya? Maana tutaelekeza katika Mikoa yetu. Lengo letu ni kwamba watu wenye ulemavu waweze kupata elimu kama watu wengine kwa kadri inavyokusudiwa. Kwa hiyo, ni commitment ya Serikali na hili tunaweza kulifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba dada yangu Mheshimiwa Magdalena Sakaya wala asiwe na shaka katika hilo, ni commitment ya Serikali kwamba sasa tunaenda kwa kasi katika suala zima la sekta hiyo hasa kwa watu wenye mahitaji maalum.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru Mheshimiwa Dada Magdalena Sakaya kwa swali lake zuri, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 ambayo ndiyo inatupa mwongozo wa namna nzuri ya kuwashirikisha wenzetu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania ili waweze kupata haki zao zote, inatupa pia maelekezo kwamba msingi wa elimu tutakaouweka katika kuwahudumia wenzetu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania kwa sasa tunaupeleka katika mtazamo wa ujumuisho. Shule zote zitakuwa inclusive. Hatutataka kuwa na shule ambazo zitawatenga wenye ulemavu wasome wao peke yao tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana hiyo tumeona kwamba haiwasaidii, inawafanya wajisikie ni watu wasiojiweza. Kwa hiyo, tunapotengeneza mfumo huu sasa wa elimu jumuishi kwa kuzingatia Sheria Namba 9 ya mwaka 2010, unawasaidia na wao kujiona wana uwezo, wanaweza kushindana na wanaweza wakafanya mambo kama wanavyofanya watu wengine ambao hawana ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia Sheria hiyo Namba 9 ya mwaka 2010 tutajitahidi kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kuboresha miundombinu, vifaa vyao kwa ajili ya kujifunzia kama vile programu nzito sana ya leo ya kukabidhiwa vifaa, inayofanywa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kule Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuwe pamoja kuhakikisha wenye ulemavu wanakuwa ni part ya maisha ya kawaida ya Watanzania wote.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kaliua haina Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya anatumia Ofisi ya Tarafa ambayo ina hali mbaya na ni chumba kimoja kidogo wanajibana pale. Ofisi ya Wilaya imeanza kujengwa tangu mwaka 2012 na imesimama mwaka 2014 mpaka leo haijaendelezwa. Naomba kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa fedha ya kutosha ili Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ikamilike na Mkuu wa Wilaya aweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, alichosema Mheshimiwa Sakaya ni kweli na ndiyo maana nimesema kwamba sasa hivi tunajitahidi kupeleka fedha na hata katika Halmashauri yake anafahamu tumeshapeleka milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Halmashauri Kaliua. Hiyo ni commitment ya Serikali kwa Kaliua. Angalia kipindi hiki cha muda mfupi tumepeleka shilingi milioni 700 lakini najua Ofisi ya DC bado haijakamilika. Hii tunalichukua kuangalia jinsi gani tumefanya allocation ya funds niangalie kama Kaliua katika suala la jengo la Mkuu wa Wilaya hali ikoje halafu tutasukuma ili jengo liweze kukamilika. Ofisi hizi zilisimama muda mrefu na sasa hivi nimetoa commitment kubwa ya Serikali kupeleka kwa ajili ya umaziaji wa majengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo usiwe na mashaka Dadangu tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imejidhatiti kukusanya mapato kwa kupitia mashine hizi za EFD, lakini kuna matatizo makubwa ya kutokuwepo kwa mtandao au mawasiliano tunapoenda kwenye vituo vya manunuzi, vinavyosababisha wanunuzi kukaa kwenye vituo kwa muda mrefu wakisubiri risiti au wakati mwingine tunakata tamaa tunaondoka bila kuwepo na risiti.
Je, Serikali ina mpango gani makini kuhakikisha kwamba inaboresha mfumo wa kukusanya kodi pamoja na kupata huduma kwa muda unaotakiwa ili kuhakikisha kwamba kile walichokikusudia kinaliletea Taifa mapato kwa maendeleo yetu? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakiri kwamba lipo hili tatizo kwa baadhi ya wauzaji na wafanyabiashara ndani ya nchi yetu. Tatizo la kimtandao halipo kwa kiwango ambacho wafanyabiashara wanakisema, nitoe wito kwa Wabunge kama viongozi kwenye maeneo yetu tushikamane na Serikali yetu kwa sababu hakuna maendeleo bila kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tushirikiane katika kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia mashine hizi kwa pamoja, lakini TRA wanafanya jitihada kubwa za kupita maeneo ya wafanyabiashara wetu kuhakikisha kwamba mashine hizi zinatumika na zinafanya kazi. Ni wito wangu kwenu Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kuhakikisha hili linaweza kufanyika ndani ya nchi yetu.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa, wananchi wa Kata ya Usinge Wilaya ya Kaliua wanakwenda Nguruka kwa sababu Kata ya Usinge ambayo ni kubwa sana ina wananchi wengi na ni center ya biashara haina kituo cha afya, ina Zahanati moja ndogo kiasi ambapo inasababisha watu waende kule Nguruka ambapo ni mbali sana karibu kilometa 40 kwenda pale Nguruka. Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha ule mpango wake wa kujenga kituo cha afya Kata ya Usinge unaanza haraka ili kupunguza msongamano wa wananchi wanaokwenda kuhudumiwa katika Kata ya Nguruka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kata ya Usinge ina changamoto kubwa na ukiangalia population pale ni kubwa sana, wakati ukitoka Kigoma pale ukipita unaona kweli kuna haja. Naomba niseme kwamba Serikali tumelichukua hili, tutahakikisha tunafanya kila liwezekanalo eneo lile kujenga kituo cha afya ili wananchi waweze kupata huduma.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwepo sera ya kudhibiti ongezeko la watu ya mwaka 1992 na kufanyiwa maboresho mwaka 2006, bado kwa maeneo ya vijijini wazazi na familia nyingi wamekuwa wanazaa watoto wengi kwa madai kwamba kila mtoto anakuja na riziki yake. Matokeo yake watoto wanaishi katika hali ya mazingira magumu na wengi wao wanaishia kuwa watoto wa mitaani kwa sababu wanakosa huduma zote muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hii ambayo ni hali halisi, Serikali sasa iko tayari kutangaza ukomo wa watoto katika familia angalau tano au saba ili watoto wanaozaliwa kila mtoto apate elimu inayotakiwa, apate huduma za afya, apate mambo yote ambayo anastahili katika maisha yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; njia mojawapo inayotumiwa na Serikali kudhibiti ongezeko la watu ni kuwepo kwa uzazi salama. Maeneo ya vijijini bado wanaopata uzazi salama ni wachache kwa sababu vituo vya afya ni vichache, zahanati ni chache hakuna mobile clinic, kwa sababu wengi wao hawapati hii huduma jinsi inavyostahili hali ambayo wanaendelea kuzaa bila kuwepo na mpango. Serikali sasa iko tayari pamoja na juhudi zote ambazo zimeelezwa kwenye jibu la msingi kuhakikisha kwamba kule ambako hakuna zahanati, hakuna vituo vya afya, kuwepo mobile clinic za kutosha na wapelekwe watalaam, pikipiki za kutosha…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio swali, kuhakikisha kwamba elimu ya uzazi salama inawafikia kina mama wote vijijini na mijini? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza kwamba Serikali kutangaza ukomo wa idadi ya watoto, napenda kumwambia Mheshimiwa Sakaya na Bunge lako Tukufu kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba suala hili la ongezeko la idadi ya watu nchini ni suala mtambuka na ni suala la kijamii. Kusema Serikali iweze kutoa tamko la watu kupata idadi ya watoto naamini haitokuwa sahihi kijamii na kulingana na tamaduni za Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili kuhusu kutokuwa na vituo katika baadhi ya vijiji vyetu tunaona jitihada za Serikali kuhakikisha kwamba vituo hivi vinajengwa katika kila Kata yetu pamoja na zahanati katika kila Kijiji. Pia kuna ongezeko kubwa la mobile clinic katika vijiji vyetu ambayo Serikali imeanza kutekeleza na ni imani yangu akinamama watapata huduma ya uzazi salama kwa wakati muafaka.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa vifaa vya bandia kwenye maduka sasa hivi siyo siri tena, hata ukienda wanakwambia kuna hiki hapa ambacho ni dhaifu, kuna hiki hapa na bei pia ni tofauti. Kwa hiyo si kwa njia ya vichochoroni hata madukani vipo na vinauzwa halali kabisa.
Je, Serikali haioni, kuruhusu kuwepo kwa bei aina mbili/tatu kwenye kifaa kimoja dukani ni kuruhusu kuwepo kwa vifaa bandia kihalali kitu ambacho tunapiga marufuku katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI):
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri ni kweli, unakwenda dukani unakutana na hiyo hoja. Na hoja yenyewe inakuwa kwenye kukata mapato kwenye TRA, na ndio maana juzi juzi hapa, kama umeongea na wafanyabiashara TRA imeendelea kuweka sheria ngumu ikiwepo pamoja na kila duka hata kama ni dogo lazima liwe na ile mashine ya EFD kwa ajili ya kupata zile recept ili waweze kulipa kodi.
Mheshimiwa Spika, lakini Wizara ya Fedha inaendelea kuweka sheria kali na ukaguzi mkubwa sana katika bidhaa. Suala moja ambalo ni zuri kwa sisi Waheshimiwa Wabunge ndugu zangu tuendelee kuwaelimisha wananchi wetu. Sasa kama wewe unapewa hiyo kauli, kwamba ukitaka bidhaa hii itakuwa na shilingi kadhaa lakini hii itakuwa na bei chini zaidi, wewe mwenyewe lazima ujiulize kwamba kwa nini hii ni chini?
Mheshimiwa Spika, kama ningelikuwa ni mimi ningeweza nikasema basi naomba uniuzie hiyo hiyo ya bei ambayo ni kubwa lakini unipe receipt. Kwa sababu hiyo moja kwa moja ameshakwambia hii haina ubora, sasa wewe kwa nini uende ukanunue.
Mheshimiwa Spika, lakini nakiri pia kwamba, si wananchi wote wa Tanzania hasa vijijini wenye elimu ambayo naweza nikawa nayo mimi au unaweza ukawa nayo Mheshimiwa Sakaya. Sasa ni suala letu sisi Waheshimiwa Wabunge na Madiwani na Serikali kwa pamoja tuendelee kuwaelimisha wananchi ili waweze kukwepa haya na ndiyo maana Serikali sasa inaweka viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hiyo kama alivyozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba hata viwanda vya ndani nao wanaweza wakafanya vitu vya namna hiyo. Ndugu zangu tunayo kazi kwa hiyo tuendelee kuelimisha jamii na kutunga sheria zilizo kali na tuzisimamie ili haya yaweze kuondoka.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi naomba nimuulize Mheshimiwa naibu Waziri swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa mfuko huu wa kina mama na vijana unatakiwa uchangiwe na maeneo mawili kwa maana ya Serikali Kuu itoe fedha kwa ajili ya ule mfuko lakini pia Halmashauri zetu zitoe asilimia 10 kwa ajili ya ule mfuko. Kwa baadhi ya Halmashauri ikiwepo Kaliua tunajitahidi sana kutenga ile asilimia 10 lakini Serikali haitoi ile sehemu yake.
Je, Serikali haioni kwamba kutokutenga ni kuendelea kudumaza wanawake na vijana kutokupata mikopo kwa kiasi kinachotakiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la msingi lilivyo ni juu ya Halmashauri kuhakikisha kwamba wanatenga asilimia 10 na yeye katika Halmashauri yake anasema wamekuwa wakitenga hii asilimia 10 kwa uzuri zaidi.
La kwanza ambalo naomba tuhamasishe na kuagiza Halmashauri zote ni kuhakikisha kwamba wanaiga mfano mzuri kama ambavyo Halmashauri ya Kaliua inafanya ili kwanza tuwe na uhakika katika hii asilimia 10 ambayo inatengwa, je, inawafikia akina mama na baada ya hapo tukiwa na uhakika na mfumo ambao ni rasmi unatumika Serikali haitasita kwa sababu lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba inawakomboa wanawake na vijana na ndio maana sheria ilipitishwa ili kuhakikisha kwamba tunawawezesha wanawake na vijana katika suala zima la uchumi.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii muhimu sana. Kutokana na mvua ambazo zinaendelea kunyesha barabara nyingi za Jimbo la Kaliuwa zimekatika na hazipitiki kabisa, zikiwemo barabara ambazo zinatoa magari Kahama kwenda Kaliuwa na kwenda vijiji mbalimbali. Barabara ya Kahama kwenda Ugaza imekatika, Kahama kwenda Usinge imekatika, Usinge kwenda Lugange Mtoni imekatika na Kahama kwenda Mpanda Mloka imekatika.
Mheshimiwa Spika, TARURA waliomba bajeti ya dharura ili waweze kufungua barabara hizi ambazo sasa hivi hazipitiki kabisa, wananchi wametengeneza mitumbwi ya kupita. Naomba Serikali ituambie mpango wa haraka wa kuweza kuwapa fedha kwa TARURA, Wilaya ya Kaliuwa ili waweze kutengeneza barabara hizi ziweze kupitika kwa sababu ni barabara kubwa za uchumi? Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kuhusu suala la barabara nyingi kukatika kwa sababu ya mvua zinazonyesha, naomba nimhakikishie na itakuwa vizuri mimi nikishatoka baada ya hapa tukafanya mawasiliano ili tuhakikishe haraka kabisa barabara hizo zinatengenezwa ili ziweze kupitika. Kwa sababu ni lengo la Serikali kuhakikisha kwamba barabara zote zinapitika kwa vipindi vyote.
Mheshimiwa Spika, ametaja barabara nyingi, itapendeza kama tutawasiliana halafu tuone jambo gani la haraka linaweza likafanyika ili wananchi wasije wakakwama katika shughuli zao.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kutokana na jibu la msingi tumeona namna gani ambavyo migogoro ni mingi hapa nchini. Migogoro hii inapoteza maisha ya Watanzania, migogoro hii inapoteza mali za Watanzania, watu wanafilisiwa mifugo yao, wanaharibiwa nyumba zao, wanachomewa vitu vyao, lakini pia migogoro hii inadumaza uchumi kwa kuwa watu wana - concentrate kwenye migogoro wanashindwa kufanya masuala ya maendeleo.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa nategemea Mheshimiwa Waziri baada ya kubaini matatizo haya aje na mpango mkakati, namna gani za haraka kutatua migogoro hii, tofauti anavyosema hapa wataendelea kushirikiana na wadau. Wakati timu zinaendelea kufanya kazi kubaini migogoro hii, bado Watanzania wameendelea kunyanyasika, wakati huu tunapoongea bado watu wanaendelea kunyanyaswa kwenye maeneo ya hifadhi, mipaka, mifugo yao inaendelea kupigwa mnada, vyanzo vinazidi kuharibiwa, nilitegemea wakati Serikali haijaja na mpango wa kutatua matatizo haya, wangesitisha kuendelea kunyanyasa watu ili wenyewe wafanye kazi yao, ndiyo waendelee kushughulikia watu ambao wako ndani ya hifadhi ambapo wamesajiliwa kisheria?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2012/2013, Wizara ya Maliasili na Utalii ilinyang’anya vijiji 26 vyeti vya usajili kutoka Wilaya ya Kaliua kwa madai kwamba vimesajiliwa kinyume na utaratibu wakati walisajiliwa kisheria chini ya Wizara ya TAMISEMI, suala ambalo sasa hivi limeenda kuumiza uchumi wa wananchi wale kwa sababu makampuni ya tumbaku yamesema hayataingia mikataba ya biashara kununua tumbaku kwenye vijiji 26 kwa sababu havina vyeti vya usajili wa vijiji.
Mheshimiwa Spika, naomba Wizara ya Maliasili ituambie itarudisha lini vyeti vya usajili kwa vijiji 26 ambavyo leo wanaenda kuathirika kiuchumi kwa kuwa walisajiliwa kisheria, wanaishi kisheria, kama lilifanyika kosa ni suala la Serikali? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitoe taarifa kwamba siyo lengo la watumishi wetu walioko kwenye hifadhi kuwanyanyasa wananchi, kwa mujibu wa kanuni na taratibu hawaruhusiwi kufanya hivyo, kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanalinda hifadhi na siyo kuwanyanyasa wananchi wanaozunguka katika maeneo hayo. Kwa hiyo kama kuna kesi kama hizo naomba tuwasiliane na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kuwachukulia hatua stahiki hao ambao wanawanyanyasa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kuhusu mpango mkakati nimeeleza kwamba timu hiyo baada ya kukamilisha hilo zoezi Wizara zote zinazohusika zimepewa hii taarifa kwa ajili ya kuanza kuweka mkakati wa makusudi kabisa wa kutekeleza na kutatua migogoro ya namna hiyo. Hiyo kazi imeshaanza na kila Wizara ina mpango wake inatekeleza, sisi kama Maliasili na Utalii tumejipanga kwa ajili ya hiyo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, Mheshimiwa Waziri Mkuu alituagiza kuweka mipaka katika maeneo yote yenye migogoro, mipaka ile baada ya kuwekwa sasa Serikali inatathmini ni maeneo yapi yana migogoro, yapi yapo ndani ya hifadhi, yapi tunaweza kuyaachia, yapi lazima tuwape fidia wananchi na yapi tuwaondoe wananchi. Baada ya hiyo yote kukamilika, hatua stahiki zitafanyika na Mheshimiwa Mbunge atapata ule mpango wa Serikali kwa ujumla katika maeneo yote.
Mheshimiwa Spika, kuhusu wananchi ambao Mheshimiwa Mbunge anasema walinyanga’anywa vyeti vyao wa usajili wa vijiji, hiyo taarifa naomba niseme bado sina lakini nitaifuatilia, nitashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba angalau tunapitia na tuone tunashirikiana pamoja na Wizara zingine ili katika hivi vijiji 366 ambavyo viko ndani ya hifadhi tuone kama na hivyo navyo vipo ili kusudi tuone hatua itakayochukuliwa na Serikali, basi itahusu maeneo yote hayo pamoja na vijiji alivyovisema. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dunia ya leo ya utandawazi mawasiliano ni uchumi, ni kilimo, ni kila kitu. Maeneo yote ambayo nimeyataja Mpanda Mlohoka, Usinga, Kombe, Shela, Mwamashimba, Ibumba, Mkuyuni na vingine vingi ni maeneo ambayo wanalima sana zao la tumbaku ambalo linaingiza kipato kikubwa. Serikali imekuwa na speed ndogo sana ya kupeleka mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye jibu lake hapa la msingi anasema kwamba kuna baadhi ya maeneo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali, kwenye jibu la swali la msingi Mheshimiwa Waziri anasema maeneo mengine itategemea upatikanaji wa fedha, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali, kwa kuwa kuna makampuni ambayo pia yanapeleka mawasiliano maeneo ya Vijijini, wakati wanasubiri kupata fedha Serikali kwenye mpango wa Serikali wanaweza kuongea na haya makampuni ili baadhi yaanze kupeleka mawasiliano maeneo hayo kuliko kusubiri mpaka Serikali ipate fedha? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kumekuwepo na migongano mikubwa kwenye masuala ya ulipaji wa minara ya simu kwenye maeneo mbalimbali ya vijijini, Serikali za Vijiji zikiona kwamba minara ile ni vipato kwa ajili ya Serikali lakini pia wananchi ambao wametoa yale maeneo wakiona ni haki yao wao kulipwa. Serikali inasemaje juu ya minara ambayo imewekwa vijijini ambapo imeleta migongano hawajui kwamba hela ziende wapi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Magdalena Sakaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ni taasisi ya Serikali ambayo inahusika kupeleka mawasiliano katika vijiji vyote au sehemu zote ambazo hazina mvuto wa kibiashara. Haya makampuni ya simu yanafanya biashara, ili yaweze kuweka mnara sehemu mojawapo ni lazima pawe na mvuto wa kibiashara. Kuepuka hilo, ndiyo maana Serikali ilianzisha Mfuko wa Mawasialiano kwa Wote kuhakikisha kwamba hata zile sehemu ambazo hazina mvuto wa kibiashara zinapata mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na vijiji vya Mheshimiwa Sakaya, nashukuru sana kwamba kuna barua yake ambayo imeanisha vyote hivyo na nimeshaipokea pamoja na barua za Wabunge wengine wengi tu. Namuahidi baada ya kipindi cha Bunge hili la bajeti nitafanya ziara ya mwezi mzima na wataalam wangu kutoka TCRA na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha tunaanisha maeneo yote nchi nzima ambayo hayana mvuto wa kibiashara tutangaze tenda ili makampuni ya simu yaweze kuweka minara wananchi waweze kuwasiliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu malipo, kwanza kabisa kuna masuala kama mawili. Suala la kwanza ni malipo kwa mtu ambaye anatoa eneo lake mnara uwekwe, mara nyingi huwa ni mapatano kati ya mwenye ardhi na makampuni ambayo yanaweka mnara. Wakati mwingine tunashauri sana vijiji ndio viwe vinatoa maeneo kwa ajili ya kuweka mnara ili kuhakikisha kwamba pesa inarudi kwa wananchi lakini inapotokea kwamba ni mtu binafsi amepata hiyo fursa hatuwezi kumuingilia sana japo tunatamani sana halmashauri iweze kuwa inaingilia. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora na Kanda ambazo tunalima tumbaku kwa miaka zaidi ya 10 tumekuwa tunaomba kiwanda cha tumbaku kijengwe Mkoa wa Tabora na ikithibitika kabisa kwamba asilimia 60 ya tumbaku ya Tanzania inalimwa Mkoa wa Tabora, lakini mwaka jana tu Serikali imeruhusu kiwanda cha pili kujengwa Mkoa wa Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa kiwanda cha Tumbaku Mkoa wa Tabora kwanza kumewanyima ajira vijana wetu wa Tabora, lakini kubwa zaidi ni kwamba wakulima wa tumbaku wanachajiwa gharama za kusafirisha tumbaku kutoka Tabora kupeleka Morogoro, kwa hiyo wanaongezewa maumivu. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali iliruhusu sasa mwaka jana kiwanda kipya kujengwa Mkoa wa Morogoro ambako hakulimwi tumbaku, iko tayari sasa kushawishi kile kiwanda kimoja kihamishiwe Mkoa wa Tabora ili wakulima wa Tabora nao pia waweze kunufaika na zao lao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwenye jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kawmba uzalishaji umepungua, ni kweli umepungua lakini umepungua kutokana na wakulima hawapewi makisio na kampuni. Wana lengo la kulima, wanakopa hata msimu huu wenyewe tu Kaliua peke yake zaidi ya Vyama vya Msingi sita vimekosa makisio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao hili ni zao la uchumi wa Taifa na Mkoa wa Tabora, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha kwamba Vyama vya Msingi ambavyo vimekosa makisio mwaka huu vinapatiwa makisio? Kwa sababu uchumi wa Tabora unategemea tumbaku na uchumi wa familia unategemea tumbaku? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na dhamira nzuri ya Serikali na wananchi wa Tabora kupenda kujenga Kiwanda cha Kuchakata Tumbaku Tabora lakini pia Muwekezaji huwa anaangalia mazingira ya yanayoweza kumuwezesha kupata faida zaidi na kufanya shughuli zake vizuri zaidi. Kwa hiyo kama tulivyosema awali tutaendelea kuhamasisha lakini pia kuwakatisha tamaa wale ambao wameamua kuwekeza Morogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu kutoa makisio; kwa kweli kama kuna zao ambalo linapambana na changamoto ni pamoja na hili la tumbaku. Fikiria mteja anaanza kwanza kuhamasishwa “uvutaji wa sigara ni hatari kwa maisha yako” lakini pia uweze kufanya biashara. Kwa hiyo kwa misingi hii unakuta hata kampuni wakati mwingine zinashindwa kufikia malengo kutokana na mazingira kama hayo. Hata hivyo, nizidi kuwaomba wananchi wa Tabora, wote kwa pamoja tutaendelea kufuatilia na kuona kwamba hali ya bei yanzuri kwa upande wa wakulima inapatikana. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru sana kwa kuniona; naomba niulize swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kaliua Mjini pale Mheshimiwa Rais aliahidi kilometa tano za lami ndani ya Mji wa Kaliua, na mwaka jana wakati amekuja kwenye ziara yake pia tulimkumbusha akasisitiza kwamba ahadi hiyo itekelezwe kwa wakati. Naomba kujua Serikali itaanza lini utekelezaji wa kilometa tano za lami ndani ya Mji wa Kaliua Center? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi, ahadi zote za viongozi wakuu wa Kitaifa zitatekelezwa. Kwa kuanzia naomba niwaagize TARURA mkoani kwake na hasa Wilaya ya Kaliua wahakikishe kwamba wanatenga katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili ahadi ya Mheshimiwa Rais ya Ujenzi wa kilometa tano ianze kutekelezwa mara moja.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, zipo sheria nyingine ambazo kuchelewa kuletwa Bungeni zina-cost maisha ya watu moja kwa moja. Kwa mfano, Sheria hii ya Usalama Barabarani, suala la sasa hivi Bodaboda ku-overtake kushoto linasababisha ajali nyingi sana na watu wengi wanapoteza maisha. Sheria inasema overtake kulia, lakini wewe una- overtake kushoto na ajali nyingi zinatokea kwa utaratibu huo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maisha ya watu yanapotea kila siku, Serikali haioni haja ya kuleta sheria hii kwa fast-track Bungeni ili kuokoa maisha ya watu wanaoteketea kila siku kwa sababu ya Sheria ya Barabarani kuwa imepitwa na wakati?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama ndani ya Bunge hili tukufu nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, nichukue fursa hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuniamini kwamba ninatosha na ninaweza kumsaidia kazi hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Pia nakushukuru wewe kwa ushirikiano ambao unanipatia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Mavunde namna ambavyo amejibu swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika kupambana na ajali za barabarani, na sisi tunajua kabisa bodaboda kama alivyosema Mheshimiwa Sakaya limekuwa ni tatizo kubwa. Tayari hivi tunavyozungumza, majibu mazuri kabisa ya Mheshimiwa Mavunde ni kwamba marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani yako katika hatua za mwisho. Aiamini Serikali kwamba tutaileta hapa Bungeni kwa ajili ya Bunge hili kuweza kuipitisha. Ahsante. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa; Serikali imetoa matangazo na kuweka vibao kuhalalisha masoko ya mazao ya misitu maeneo ambayo hakuna mashamba ya misitu, wakijua kabisa kwamba misitu inayovunwa wale wavunaji wanavuna visivyo halali. Kwa mfano, ukitoka Dodoma ukiwa unaelekea Morogoro kuna vibao kwamba kuna masoko halali, lakini wale watu kule hakuna mashamba ya misitu, wanavuna kwenye maeneo ambayo siyo halali na hawana namna nyingine, hawajaelimishwa namna gani wapande misitu ili wavune mazao ya misitu kwenye maeneo ambayo yamepandwa. Je, Serikali haioni kwamba, kuweka masoko ya mazao ya misitu maeneo ambayo hakuna mashamba ya misitu ni kuhalalisha kuendelea kuhakikisha kwamba misitu iliyopo ya asili inateketea?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la la pili; kwa kuwa kwenye majibu ya msingi Mheshimiwa Waziri anasema kwamba misitu imepandwa. Kuna baadhi ya misitu ya uoto wa asili imepandwa lakini tumeshuhudia kazi wanayofanya Maafisa Misitu maeneo yetu, ikiwepo Kaliua ni kupiga mihuri magogo, kupiga mihuri mbao na kutoa vibali kwa ajili ya uvunaji usio halali kiasi kwamba speed ya kuvuna misitu baada ya kuwepo kwa TFS imeongezeka tofauti ya ilivyokuwa mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza, je, Serikali haioni kwamba kuna sababu ya kukaa na Maafisa wao wa Misitu ili sasa waanze kazi ya uhakika ya kurejesha uoto wa asili ikiwepo maeneo mbalimbali kwa sababu Kaliua kuna misitu mingi lakini hakujapandwa mti hata mmoja kuhakikisha kwamba tunarejesha uoto wa asili maeneo ambayo yameharibika? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba nikiri kabisa kwamba kweli kumekuwa na matumizi mabaya ya misitu yetu katika maeneo mengi na vituo vingi vipo katika maeneo ambayo kwa kweli hakuna misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuwepo kwa sehemu ya kituo hata kama hakuna msitu siyo tatizo, tatizo ni kwamba ule mkaa unaouzwa katika lile eneo je, una kibali na umepatikana katika taratibu zilizowekwa. Kama haujapatikana kwa mujibu wa utaratibu hilo ndilo linakuwa tatizo kubwa lakini kama vibali vipo na mkaa umesafirishwa kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine maadam una vibali hilo linakuwa siyo tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo tutaendelea kulifuatilia pale ambapo watu wanafungua vituo wanaweka masoko bila vibali maalum Serikali itachukua hatua zile zinazostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu hawa Maafisa Misitu ambao wapo maeneo mengi na wamekuwa hawatekelezi labda majukumu yao sawasawa na kama ulivyosema wamekuwa labda wanagonga mihuri tu zile mbao, kwa kweli naomba nitumie nafasi hii kuwaagiza Maafisa Misitu wote kuhakikisha wanasimamia hifadhi zetu zote zilizoko katika maeneo yao, mihuri inayotakiwa kutolewa ni pale ambapo wale wavunaji wamevuna katika ile misitu wanayoisimamia, kwa mujibu wa taratibu kwa mujibu wa sheria na kanuni tulizojiwekea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wakiwa wamefuata hizo taratibu na wakigonga haina shida, shida inakuwa pale wanapopita njiani humu halafu wanagonga hiyo mihuri wakati wao wenyewe hawajui hizo mbao zimetoka sehemu gani. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua zinazostahili, kwa wale ambao watakuwa wanakiuka hizi taratibu ili kusudi hifadhi zetu ziendelee kuwepo hapa nchini. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekondari ya High School ya Kaliua inapokea watoto kutoka Tanzania nzima na ina watoto wegi sana lakini kuna upungufu mkubwa sana wa mabweni ya wasichana na wavulana. Pamoja na juhudi za halmashauri za kuendelea kujenga bado mahitaji ni makubwa sana. Serikali iko tayari sasa kupeleka nguvu katika Sekondari ya High School ya Kaliua ili watoto wale wapate mabweni ya kutosha kwa sababu hivi tunavyoongea baadhi ya wavulana wanakaa kwenye madarasa kwa kukosa mabweni ya kulala?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sakaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo tayari kuangalia uwezekano wa kusaidia kujenga miundombinu katika shule aliyosema. Kama nilivyosema kwenye maswali mengine tunahitaji kupata maombi, ni lazima halmashauri yenyewe ituletee maombi ili tuangalie ni namna gani tanaweza kusaidia. Kwa hiyo, tuko tayari kujenga miundombinu, tumeshajenga mingi katika nchi nzima lakini tunaangalia vilevile na bajeti. Kwa hiyo, alete maombi yataangaliwa pamoja na maombi mengine.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza moja la nyongeza. Mkandarasi aliyepewa barabara ya Urambo – Kaliua kilometa 28 tu ameonesha udhaifu mkubwa kuanzia mwanzoni sasa hivi ni karibu miezi 10 kazi iliyofanyika ni ndogo sana. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri anaweka vyombo kwenye site, Waziri akiondoka anaondoa vyombo. Serikali haioni sasa sababu ya kubadilisha mkandarasi huyu ili wananchi wa Kaliua na Urambo waweze kupata barabara ambayo ni kubwa sana kwa ajili ya uchumi wa Kaliua na Urambo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hizi taarifa nizipokee kama ni taarifa mpya kwangu kwa maana kwamba tutafanyia kazi ili tuone kama kuna huu mchezo unafanyika wa kuweka vifaa site wakati wa ukaguzi halafu baadaye vinaondolewa ili tuweze kuangalia na tuchukue hatua. Kwa sababu ujenzi wa barabara hii na mkandarasi kuwepo site ni kwa mujibu wa taratibu na pia iko mikataba na kama kuna mchezo huu tutaona rooms zilizoko kwenye mkataba wetu ili tuweze kuchukua hatua stahiki na mwenyewe nitahakikisha nalifuatilia hili mguu kwa mguu. (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Watumishi wanaofanya kazi kwenye njia ya reli kwenye vituo vidogo (gangs) wanafanya kazi ngumu, kwenye mazingira magumu, lakini wamekuwa hawalipwi fedha zao kwa wakati. Kwanza ni vibarua lakini kuna wakati wanakaa wanapewa baada ya miezi miwili mitatu, wanaishi katika hali ngumu sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba watumishi hawa wanalipwa fedha zao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Magdalena Sakaya kwa sababu ni mdau mkubwa sana wa reli, amekuwa akiitumia miaka mingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba gangs zetu nyingi sana zimekuwa chakavu na nyingine tumezifunga kutokana na uchakavu huo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Shirika la Reli lipo kwenye mchakato wa kuanza kuzirekebisha gangs zote nchini, kwa sababu kutokuwepo kwa gangs kumesababisha hata hujuma mbalimbali kwenye reli yetu na kusababisha upotevu wa mali na wakati mwingine hata maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tutahakikisha kwanza tunazirekebisha gangs zetu, lakini tumeomba kibali kwa ajili ya kufanya ajira nyingine zaidi kwa sababu hata waliokuwepo wameshafikia umri wa kustaafu lakini tumeamua kuwa-hold. Tutakapofikia hatua hiyo hali itabadilika na utaona kabisa kwamba wale nao wataanza kulipwa kwa wakati. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mradi wa barabara hii ya Kaliua-Urambo wa kilomita 28 ambao unatekelezwa na fedha ya Tanzania shilingi bilioni 37 ulitakiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2019 ambapo ni sasa hivi lakini mpaka leo wakati mradi unatakiwa ukabidhiwe una asilimia 37 tu kwa hiyo huu ni udhaifu wa hali ya juu.

Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wakati wakandarasi hawa watatu wanaomba zabuni mpaka wanapewa walikuwa watatu na ndiyo maana walikidhi vigezo lakini wengine walikuwa ni kama mwavuli sasa hivi ni mkandarasi mmoja tu ambaye ni Jossam ndiyo anatekeleza mradi huo na hana uwezo wa kutosha ndiyo maana anakwenda speed ndogo sana na barabara hii ni muhimu kwa uchumi na haiwezi kukamilika kwa wakati. Kwa kuwa wakati wanapewa kazi walikuwa makampuni matatu na sasa hivi amebaki mmoja ambaye ni Jossam na udhaifu unaonekana, kwa nini Serikali isielekeze wale wote watatu ambao waliomba tenda waungane pamoja na kwa kuwa wameomba kuongezewa muda waweze kukamilisha barabara hii kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kigezo kwamba mvua ilikuwa nyingi ndiyo maana barabara haiendi kwa wakati nakikataa kwa sababu majira ya kanda mbalimbali Tanzania za mvua na jua yanajulikana lakini hata wakati wa jua barabara hii bado haitengenezwi. Unaona wakati wa jua kabisa wamelala usingizi na mvua ikija wanasema ni mvua. Toka mwezi wa Julai na Agosti tuko kwenye jua karibu miezi tisa hapa imekwenda lakini bado speed ni ndogo. Kwa hiyo, tunaomba kisingizio kwamba majira hayajulikani kiondoke lakini pamoja na muda walioongezewa Serikali inatuambie barabara hii itakamilika lini kwa viwango vinavyotakiwa? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Mheshimiwa Magdalena Sakaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, barabara ya kutoka Tabora – Urambo - Kaliua - Uvinza - Kigoma yote sasa hivi itakamilika kwa sababu vipande vitatu vilivyobaki, kimojawapo hicho anachokizungumzia Mheshimiwa Magdalena Sakaya cha kutoka Urambo - Kaliua ambacho kina mkandarasi lakini pia Kazilambwa - Chagu tumetangaza tenda na wakati wowote tutatangaza tenda ya Malagarasi – Uvinza. Kwa hiyo, barabara nzima itakamilika na fedha tunayo kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, nimetembelea kule na nimewakuta wale wakandarasi wote watatu na msingi wa wakandarasi watatu ulianzishwa na Mheshimiwa Rais akiwa Waziri. Unakumbuka kule Mbutu aliwaunganisha wakandarasi 10 wakafundishwa na hao sasa hivi ndiyo wanakuwa wakandarasi wazuri. Kwa Urambo - Kaliua nimemtembelea yule mkandarasi nikaona changamoto zilizokuwepo, tumekaa, tumezungumza na tumekubaliana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Magdalena Sakaya mwenyewe ni shahidi, wamenunua mtambo mkubwa sana kwa ajili ya kusaga kokoto, kwa hiyo, barabara itakamilika kwa muda uliowekwa. Hakuna haja ya kuwasimamisha, tayari nimeshakwenda kule nikaongea na Mhandisi Mshauri na wale wakandarasi watatu wote wamerudi sasa wanaendelea na kazi, kwa hiyo, mradi huo utakamilika kwa muda walioongezewa. Nimhakikishie Mheshimiwa Sakaya na wananchi wa Urambo kwamba hapana shaka mradi huo unakamilika pamoja na barabara yote kuelekea Kigoma.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 Serikali ilitenga eneo la hekari zaidi ya 30 katika Kata ya Ushokora kwa ajili ya kujenga Gereza la Wilaya lakini kwa miaka sita (6) sasa wananchi wa Pozamoyo pale Ushokora hawajawahi kuambiwa chochote na waliondolewa kwenye makazi na mashamba yao wameenda kujibanza kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani sasa angalau kufidia wananchi wale iliyowahamisha pale ambao wamepanga maeneo mbalimbali waweze kwenda kutafuta makazi sahihi na wakati huo huo Serikali iweze kujenga hilo gereza maana ni muda mrefu sasa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mhehimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mbunge wa Kaliuwa na Naibu Katibu Mkuu mpya wa Chama cha CUF, kama ifuatavyo:- (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nimeelewa vizuri swali lake anazungumzia wananchi ambao wametakiwa kuhamishwa kwa ajili ya ujenzi wa gereza na ambao pengine anadhani wanahitaji kulipwa fidia. Kama hivyo ndivyo kwa sababu swali lake hili ni mahsusi naomba nilipokee na tuweze kulifanyia kazi na nitampatia mrejesho.
MHE. MAGDALENA HAMIS SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa Bungeni leo, hayaoneshi dhamira ya dhati kupiga marufuku mifuko ya plastiki hapa nchini. Ukiangalia majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba, inadhamiria siku zijazo, siyo kesho wala mwakani, hatujui. Hivi tunavyoongea, kwenye masoko yetu wajasiriamali wengi wanauza mifuko mizuri, mifuko ambayo ni rafiki kwa mazingira, mifuko ambayo ni vikapu vya ukili na mifuko mingine ambayo inaweza kutumika isiharibu mazingira. Mifuko hiyo haina masoko, hainunuliwi kwa sababu mifuko ya plastiki inatolewa bure masokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali haioni kwamba tatizo siyo kukosekana kwa mfuko mbadala, tatizo ni Serikali kuendelea kulinda viwanda vinavyotengeneza mifuko hii inayoharibu mazingira?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hakuna Mtanzania yeyote au mdau yeyote asiyejua madhara ya mifuko ya plastiki hapa nchini. Serikali hioni kuendelea na makongamano, sijui na vikao vya wadau ni kupoteza muda na gharama na Serikali sasa ichukue hatua za haraka kupiga marufuku mifuko hii hapa nchini kama ambavyo wenzetu wamefanya, Zanzibar wameweza, Rwanda wameweza, Kenya wameweza, maeneo mengine yote wameweza. Sisi tatizo nini? Naomba majibu ya uhakika.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana sana Mheshimiwa Sakaya kwa kuongea kwa uchungu kabisa na kuonesha ni mwanamazingira kabisa fasaha. Naomba nimhakikishie kwamba, katika hotuba yetu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ambayo itakuja tarehe 16 kwa mujibu wa ratiba ya mwezi huu, tunaweza kutangaza hatua hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu wiki hii mimi nimeelekezwa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kasim Majaliwa Majaliwa, nikutane na Taasisi za Serikali zinazohusika na jambo hili, NEMC, TBS, TRA, Uhamiaji, Polisi na Customs ili kuweka utaratibu wa namna tunavyoweza kupiga marufuku. Hapa nilipo, tayari ninazo kanuni nimeshazitengeneza ambazo zinangoja kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali. Kwa hiyo, kama tutakubaliana katika vikao vya wiki hii na vinayokuja, basi tarehe Mosi, Julai, inawezekana kabisa ikawa ndiyo mwisho wa matumizi ya plastiki hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo ambalo Serikali inalichukulia kwa uzito na tunalifanyia kazi. Ni kweli kabisa tumeongea na wadau wote, hakuna sababu yoyote ya kuendelea kutumia plastiki hapa nchini. Mimi kama Waziri wa Mazingira nakubali hilo. Mbadala upo na inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tukubaliane kwamba tutakapopiga marufuku, basi tuwe tumejiandaa kufanikiwa. Kwa sababu zipo nchi ambazo zimeamua kuchukua hatua hii, lakini hazikujipanga kwenye kufanya lile zoezi; mkajikuta kwamba mmetoa tangazo tu, lakini kitaasisi hamjajipanga, kiuratibu hamjajipanga, kwa hiyo, inakuwa ni bure tu. Kwa hiyo, tunataka tukitangaza tulifanye zoezi hili kwa namna ambayo tutafanikiwa. Tunaamini kabisa kwamba hatua hii itaibua ajira nyingine nyingi zaidi kuliko hata zile zilizopo kwenye mifuko ya plastiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tuko pamoja kwenye hili.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja dogo.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango gani wa makusudi kuweza kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Kaliua ili vijana wa Kaliua ambao wanakua haraka sana ni wengi wanaokosa nafasi za kuingia masomo ya juu waweze kupata stadi za kazi na ujuzi waweze kujiajiri na tunapoelekea kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kulieleza Bunge lako tukufu na ningeshukuru kama Waheshimiwa Wabunge wote watasikiliza kwa sababu jibu nitakalotoa linafanana kwa kila Jimbo kwa sababu jibu ni hilo hilo.

Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kujenga VETA katika kila Wilaya na Mkoa. Kwa sasa tunavyoongea kuna ujenzi unaendelea katika Wilaya 17 Vyuo vya VETA lakini vilevile kuna VETA tano zinaendelea kujengwa. Sasa mpango wetu ni kwamba nikuhakikisha kila Wilaya inapata VETA kwa hiyo tutaendelea kujenga nyingi iwezekanavyo kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ushauri wa ujumla ambao ningependa kutoa kwa Waheshimiwa Wabunge, ukiweza kujiongeza na kwenda mbele zaidi katika kujenga sehemu inakuwa ni rahisi Serikali kuleta fedha kwa sababu hata hivyo tunachotaka ni kuongeza nafasi za udahili kwa wengi nchi nzima.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekiri changamoto kubwaya utekelezaji wa Sera hii ya kutoa huduma bure kwa makundi haya maalum ikiwemo wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee wanaozidi umri wa miaka 60 ambao hawana uwezo lakini pia makundi ya watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii makundi haya yanateseka sana kupata huduma maeneo mbalimbali na wengi kiukweli wanapoteza maisha. Leo maeneo ya vijijini, Wilayani huko wanaandikiwa barua kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya watembee mitaani wanaomba misaada ili waweze kutibiwa kwahiyo Serikali ione changamoto kubwa hii iliyopo.

Mheshimiwa Spika, napenda kujua, Serikali imekuja na mkakati wa kuweza kuwepo hii huduma ya kuweza kutoa bima kwa wote sasa hawajasema specific ni lini itakamilika. Wanasema mpaka mchakato wa Serikali kutoa maamuzi. Hebu muone umuhimu ni lini sasa, naomba commitment hapa Bungeni ni lini mchakato huu utakamilika ili mfuko huu uweze kuwa na fedha ya kutosha makundi haya yatibiwe yaweze kupona kwa kuwa wengi wanapoteza maisha?

Mheshimiwa Spika, lakini tangu Serikali imetoa agizo kwenye Halmashauri zetu ni miaka zita sasa na Mheshimiwa Waziri kwenye majibu yake ni asilimia 40 tu wametekeleza, kwa hiyo bado wazee wengi hawajapewa vitambulisho, hawapati huduma za fya kwenye madirisha maalum.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali, siyo kutoa tu rai, Serikali sasa naiomba leo iweze kutoa tamko hapa Bungeni, itoe deadline ni lini ambapo vitambulisho hivi vikamilike na wale Halmashauri ambazo hazijakamilika kwa wakati waweze kupewa adhabu ili wazee hawa ambao wametumikia Taifa hili wapate huduma za afya bure waweze kuishi. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Magdalena Sakaya alitaka commitment ya Serikali kwamba ni lini utaratibu au mchakato huu wa Bima ya Afya kwa wananchi wote utakamilika; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ifikapo Bunge la Septemba Serikali tutaleta Muswada wa Bima ya Afya kwa wananchi wote ndani ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, lakini ameuliza swlai la pili kuhusiana na wazee na lini mchakato huu tuweze kutoa tamko; mimi naomba niseme tu kama ifuatavyo; nchi yetu sasa hivi inaendelea kupata neema na wastani wa Matanzania sasa hivi kuishi ni iaka 64 kwamba tunategemea kwamba na tunatarajia kama kila mtu atatunza afya yake vizuri tunatarajia tu kwamba atafika miaka 64, kwa hiyo umri huu unazidi kuongezeka na iddai ya watu hawa wanazidi kuongezeka ambao wanazidi miaka 60. Kwa hiyo, hatuwezi tukasema wkamba tutatoa ukomo kwamba ifikapo kesho wazee wote wa miaka 60 wawe wamepata vitambulisho.

Kwa hiyo mimi niendelee kusisitiza tu kwamba Serikali imeshatoa maagizo kwa Halmashauri zote na hili ni agizo la Serikali wanatakiwa waendelee kuwatambua wazee na waendelee kuwapatia vitambulisho wale wazee ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeahidi kujenga barabara ya Kaliua - Chagu (km 48) na walituambia kwamba tayari walishapata mfadhili wa kuijenga barabara hiyo. Ni lini sasa ujenzi wa barabara wa hiyo km 48 tu utaanza? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza barabara hiyo siyo kilometa 48 ni kilometa 36, tenda tumeshatangaza wakati wowote tunasaini mikataba. Baada ya kusaini mikataba kuanzia tarehe ile tuliyosaini tutakwambia sasa tunaanza lini na tunakamilisha lini.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na kuwepo kwa wataalam watafiti wenye uwezo na weledi, taasisi nyingi za utafiti zinakabiliwa na changamoto kubwa za miundombinu mibovu lakini pia ukosefu wa rasilimali fedha pamoja na madawa kwa ajili ya kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba kushindwa kutenga asilimia moja ya bajeti kwenda kwenye utafiti inasababisha Serikali kushindwa kuhudumia taasisi hizi na hivyo kusababisha magonjwa kuendelea kutesa mimea na wananchi kuendelea kuathirika kwa kulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali ina mkakati wa kuweza kusambaza mbegu bora na miche bora ambazo zinahimili magonjwa wakati huo huo zinapandwa maeneo ambapo pambeni yake kuna mazao yaliyoathirika, kuna mimea iliyoathirika. Kwanini Serikali isije na mkakati sasa na program maalum ya kuondoa mimea iliyoathirika yote na kuwezesha wakulima kupata mbegu nzuri na miche bora ili kuhakikisha kwamba miche mipya inayopandwa haiathiriki na hivyo kusaidia wakulima kuinua uchumi wa familia na uchumi wa Taifa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sakaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni maamuzi ya Kikanda na Kimataifa kwamba tutenge asilimia moja ya pato letu kwa ajili ya research na development lakini vilevile ni ukweli usiopingika kwamba bado mapato ya nchi na vipaumbele na matatizo yanayotukabili kama nchi ni mengi. Kwa hiyo, uwekezaji katika research pamoja na kuwa ni muhimu lakini hatujafikia lengo ambalo tumejiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tulichoamua kama Wizara ya Kilimo ni kwamba all resource zinazokuja kutoka kwa development partners na tarehe 19, Wizara ya Kilimo tutakuwa na kikao na development partners wanaowekeza katika sekta ya kilimo, fedha zote tutaelekeza katika research na seed multiplication program ili uwekezaji katika vyuo na taasisi za utafiti uweze kupata resource inayotosheleza. Tuondoe uwekezaji unaofanywa katika capacity building ambao unatolewa na taasisi za Kimataifa zinazowekeza katika sekta ya kilimo. Kwa hiyo, focus yetu katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu ni uwekezaji mkubwa wa fedha zote za donors na development partners zinazokuja katika sekta ya kilimo pamoja na uwekezaji wetu wa ndani kuwekezwa katika maeneo ya research na uzalishaji wa mbegu bora ambazo zitakabiliana na matatizo yanayotukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna changamoto pale ambapo ardhi imekumbwa na tatizo halafu tunapeleka mbegu mpya. Kama Wizara tumeamua kufanya mapping na tumeanza programu katika Mkoa wa Dodoma, Wilaya ya Kondoa ambao wameathiriwa na sumukuvu. Maeneo yote haya sasa hivi tunaanza utaratibu wa kwenda kwa wananchi katika kata zilizoathirika kuondoa mbegu walizohifadhi kwa ajili ya msimu ujao na kuanza utaratibu wa kuwapatia mbegu mpya na ku-treat ile ardhi ili tatizo hilo lisiweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu wa kufanya mapping na kuelewa wapi kumeathirika na nini unaendelea ndani ya Wizara. Tunaamini kwa mpango mpya wa miaka mitatu wa Wizara ya Kilimo wa kuwekeza katika research na development katika taasisi hizi, tutaondoka katika matatizo haya yanayotukabili sasa hivi kama nchi.