Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mohamed Juma Khatib (2 total)

MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Swali la kwanza naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri, yeye mwenyewe amekiri hapo kwamba ajali hizi zinasababishwa na uzembe na wahusika kutofuata sheria. Lakini pamoja na kuelewa hivyo bado ajali zinaendelea kutokea na bahati mbaya sana ni kwamba ajali hizi zinawahusu nguvu kazi vijana wadogo sana wa Taifa letu.
Je, Serikali inafikiria njia gani nyingine ya kuwabana hawa kuhakikisha kwamba suala hili halitokei?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine, Mheshimiwa Waziri hamuoni kwamba inawezekana hawa vijana mbali na uzembe wanapata hizi leseni kwa njia ya rushwa? Kwamba wanafanya kazi hii bila ya ujuzi lakini ukiwafuata unakuta kwamba leseni wanazo. Je, Serikali itahakikisha vipi kwamba hawa vijana wote wanapata leseni kwa njia inayostahili?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake kwa sababu ni kweli jambo hili linagharimu maisha ya vijana wenzetu. Lakini niseme tu njia mbadala ambayo tumekuwa tukisisitiza ni kila familia na kila rika na kila vijiwe vya bodaboda kuchukulia kwamba jambo hili wana wajibu nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili si la Serikali peke yake kwa sababu Serikali imeweka taratibu zote hizi. Lakini ambacho huwa kinatokea kwa vijana wenzetu hawa anaweza akawepo mmoja anayemiliki leseni au anayemiliki pikipiki kwa taratibu zote, lakini anavyotoka na anavyokuwa kituoni, wanatokea wengine kirafiki wanapeana unakuta yeye hata mafunzo ya kuendesha bodaboda hiyo amejifunza ziku hiyo hiyo mpaka saa 4 asubuhi na inapofika mchana anabeba abiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu abiria anayepanda hamuulizi kwanza leseni yako iko wapi yeye anaona tu yuko na chombo mambo haya yanajitokeza. Na ndio maana tunapoona hayo yamejitokeza tunachukua hatua kali. Lakini msisitizo tunaofanya na tunapotoa mafunzo, tunaelekeza kila mmoja atambue kwamba hiki ni chombo cha moto na ukikiuka utaratibu wa matumizi yake una hatari ya kupata majeraha ama kupoteza maisha wewe mwenyewe pamoja na wale uliowabeba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu taratibu za leseni, kwa kiwango kikubwa tunafanya hivo. Sasa hivi kwenye kila Mikoa tumeelekeza taratibu za namna ya kuweza kupunguza hata athari za ajali zinapokuwa zimetokea kwa vijana wetu hawa kwa kuzingatia mahitaji yanayotakiwa katika matumizi ya vyombo hivyo vya moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimewaelekeza hata wale viongozi wa vijiwe hivi vya bodaboda kuchukua wajibu wa kiuongozi kuelekezana kwamba hili jambo ni jambo linaloua, lakini vilevile wazingatie matumizi bora ya mahitaji ambayo yanatolewa katika uendeshaji wa vifaa hivo vya moto.
MHE. MOHAMMED JUMA KHATIB: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai pamoja na Kanuni za Utendaji wa Jeshi Polisi bado jambo hili linaendelea na ni sugu sana.

Je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kubadili mfumo wa utendaji kazi wa Polisi likaingizwa suala la haki za binadamu ili kuwa-conscientious Polisi katika utendaji wao wa kazi wakazizingatia hizo haki za binadamu?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, kwa kuwa Katiba yetu inakataza uteswaji na pia kwa kuwa kuna Mkataba wa Kimataifa wa Convention Against Torture, je, Serikali haioni kwamba iko haja ya kuridhia Mkataba huu ili hawa watu wanaoteswa wakapata fursa ya kwenda kushtaki katika Mahakama za Kimataifa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mohamed Khatib, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na pendekezo lake la kuubadili mfumo, tunadhani tatizo siyo mfumo, mfumo wa Jeshi letu la Polisi uko vizuri kwani Askari Polisi kabla hajaajiriwa tuna utaratibu mzuri wa kutoa mafunzo. Moja katika mambo ambayo tunayazingatia kuwaelimisha kuhusiana na sheria na kanuni pamoja na kutenda kazi zao kwa uadilifu kwa kufuata sheria na kanuni hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inapotokea changamoto ambazo zinahusu ukiukwaji wa sheria, ni matatizo ya baadhi ya Askari mmoja mmoja. Kama nilivyojibu katika swali lake la msingi kwamba tunapogundua kwamba kuna Askari ambaye anafanya vitendo hivyo vya kunyanyasa raia huwa tunachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwashtaki na kuwafukuza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi kwa maelezo hayo naona nimejibu maswali yake yote mawili kwa pamoja.