Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hassanali Mohamedali Ibrahim (1 total)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. IBRAHIM HASSANALI MOHAMMEDALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya nzuri kusimama hapa mbele ya jengo hili na niweze kusema kwamba ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili. Nawashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Kiembe Samaki kwa imani yao kwa kunileta katika jengo hili, nawaambia ahsanteni sana wananchi wa Jimbo la Kiembe Samaki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwa kweli ameonyesha kwamba anataka kuibadilisha Tanzania katika sekta zote za uchumi na hususan Tanzania yenye viwanda. (Makofi)
Katika kipindi kifupi Mheshimiwa Rais, ameweza kweli kuleta mabadiliko na matumaini kwa Watanzania wanyonge ambayo sisi Wabunge lazima tumuunge mkono kwa asilimia mia.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza vilevile ndugu yangu Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba yake nzuri. Kwa kweli naweza kusema Mheshimiwa Waziri ambaye kapata hii Wizara ni kweli Mheshimiwa Rais hakufanya makosa kumchagua ndugu yangu. Nina imani ni mtu ambaye amebobea, ni mtu ambaye anajua, nasi tumuunge mkono katika kufanikisha yale ambayo yeye amejipanga, na sisi tuwe nyuma yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara. Kwanza nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri kwamba hawa TIC wawe serious kidogo katika hao wawekezaji ambao wanakuja Tanzania kutaka kuwekeza. Kwa sababu Serikali inategemea TIC na kama TIC hawatakuwa serious katika suala hili kwa kweli tutawavunja moyo wafanyabiashara ambao kwa nia moja nzuri kabisa wanataka kuja kuwekeza Tanzania, kwa sababu Tanzania ni kisiwa cha amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri katika jengo la TIC pawepo na One Stop Centre ambayo mambo yote yanaishia kwenye jengo lile. Mfanyabiashara, tena mwekezaji asihangaike kwenda katika masuala mengine ya kutafuta vibali ambayo mwisho tunamvunja nguvu mwekezaji na huondoka hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa nataka Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara aweke vivutio maalum kwa wale wawekezaji ambao wanataka kwenda kuwekeza Mikoani, kwa sababu sasa hivi wawekezaji wengi sana wanawekeza katika Mkoa wa Dar es Salaam. Kwa hiyo, pawepo na vivutio maalum kwa wale ambao wanataka kwenda kuwekeza Tanga, Mtwara au mikoa mingine ya Kigoma. Kuwe na vivutio vizuri vya kuwawezesha waje hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwa ruksa yako ni kuhusu soko. Kwa kweli sisi Tanzania tuna nafasi nzuri sana ya kuzalisha mambo mengi sana. Mungu ametupa ardhi yenye rutuba nzuri sana, lakini hatuitumii ile ardhi, hatukitumii kile ambacho Mwenyezi Mungu aliyetupa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara awaangalie katika kutafuta masoko. Tanzania leo hii tuna mananasi mpaka yanaoza yanatupwa. Leo Tanzania hii tuna embe mpaka yanaoza yanatupwa na matunda mengine, kwa kweli soko lipo nje, lakini hao ambao wanazalisha mashambani upeo wao mdogo kwenda kutafuta soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kusema kwamba embe hapa Tanzania ukiuziwa shilingi 500 au shilingi 700 unaona nyingi sana, lakini embe hii hii ikipelekwa nchi za Arabuni, basi tunanunua kwa dola moja au dola moja na nusu. Kwa hiyo, naweza kusema kwamba soko lipo lakini hawa wakulima bado hawajasaidiwa katika kutafuta masoko ya nchi za nje.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, kwa kweli Tanzania tumejaliwa kuwa na ardhi na matunda tunayo ya kutosha, kwa hiyo, tuwasaidie wakulima wetu katika kuwatafutia masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine tuje katika hawa ndugu zetu Watanzania waliowekeza katika Kiwanda cha Saruji. Kwa kweli wanajitahidi kuzalisha saruji katika kiwango kizuri ambapo sasa hivi tunafurahi tofauti na siku za nyuma tulikuwa tunanunua saruji kutoka nchi nyingine lakini ilikuwa haina quality. Leo wenzetu ambao wamewekeza Tanzania katika viwanda vya saruji wanatupa saruji nzuri na tuwapongeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio chao hawa viwanda vya saruji wanakuwa wanalipa ten percent ya clinker. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Viwanda na Biashara iwaangalie katika hiyo kulipa ten percent kama kuna uwezekano wa kutolipa au wa wapunguziwe hiyo ten percent ili saruji tupate kwa bei nzuri ambayo sisi Watanzania wengi ambao sasa hivi tuko katika kujenga majumba, hata tukitembea mikoani huko vijijini, watu sasa hivi hawajengi tena kwa udongo, wanatumia saruji, Tanzania hii inabadilika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri aliangalie na suala hili. Vile vile nami niko tayari kumsaidia Mheshimiwa Waziri kama atataka nimtafutie masoko, kwa sababu mimi ni mfanyabiashara, ninakwenda nchi mbalimbali. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri niko tayari kufanya kazi na Wizara yako, niko tayari kukutumikia na Inshallah tutafika mahali ambapo Mwenyezi Mungu atatusaidia, Tanzania hii itakuwa ya viwanda na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, namshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii adhimu katika jengo hili Tukufu na ninamwombea dua Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mungu ampe nguvu, kutekeleza yale ambayo yeye mwenyewe, sisi tunayajua na tunayaona na nataka kumthibitishia Mheshimiwa Rais kwamba tutamuunga mkono kwa asilimia mia moja, wapinzani wetu wataisoma namba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, kwa heshima zote, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu na naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara.