Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Othman Omar Haji (3 total)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Kwa kuzingatia usalama na utulivu wa nchi yetu, viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa kauli zenye msisitizo kwa wananchi kuepuka kuhubiri siasa katika nyumba za ibada na kuchanganya dini na siasa katika mikutano.
Je, ni kifungu gani cha Katiba au Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kinafafanua juu ya kauli hizo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza katika utangulizi wake kuwa Tanzania inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia, ujamaa na isiyokuwa na dini.
Aidha, Ibara ya 3(1) ya Katiba hiyo hiyo inaeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa isiyokuwa na dini na yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ibara ya 19(1), (2) na (3) inaeleza kuwa kila mtu anastahili kuwa na uhuru wa mawazo, imani na uchaguzi katika mambo ya dini pamoja na uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ibara ya 3(2) inaeleza kuwa mambo yote yanayohusu uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya Katiba na sheria iliyotungwa na Bunge kwa ajili hiyo. Hivyo basi, sheria ya vyama vya siasa Sura ya 258 inaeleza bayana katika kifungu cha 9(2) kuwa chama cha siasa, hakitastahili kusajiliwa endapo katiba yake au sera zake zina mwelekeo wa kuendeleza maslahi ya imani ya kidini au kundi la kidini.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI Aliuliza:-
Moja kati ya kazi za Polisi ni ulinzi na usalama wa raia na mahali zao, uzoefu unaonesha kila zinapotokea kampeni za Uchaguzi Jeshi la Polisi hutumika kama Taasisi ya Chama Tawala hivyo husababisha ulinzi na usalama (hasa Wapinzani) kutoweka mikononi mwa Polisi:-
Je, Serikali haioni kwamba inalitumia Jeshi la Polisi kwa lengo la kudhoofisha Upinzani na kurahisisha kukipatia ushindi Chama chake cha CCM?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwa ni pamoja na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO) ambazo zinatoa mwongozo kwa shughuli za Askari.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ifahamike kwamba Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya Ulinzi wa raia na mali zao na siyo kwa ajili ya chama fulani cha siasa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anasema. Ni Jeshi linalowatumikia Watanzania wote pasipo kujali vyama vyao, kabila zao, dini zao ama rangi zao. Hata hivyo, ikitokea Askari wamekiuka taratibu za kiutendaji tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali za kinidhamu dhidi ya wale ambao Wizara yangu inapata malalamiko rasmi kupitia dawati la malalamiko.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI aliuliza:-
Moja kati ya maeneo yaliyomo kwenye mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba (1986) ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya.
Je, ni kwa kiasi gani Tanzania imefaidika na utekelezaji wa mkataba huo katika sekta ya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Othman Omar Haji, Mbunge wa Jimbo la Gando, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Cuba katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya tangu 1986, ambapo mkataba ulisainiwa kati ya Serikali hizi mbili. Kupitia mkataba huo, Serikali ya Tanzania imekuwa ikipokea Madaktari Bingwa kutoka Cuba ambao wamekuwa wakifanyakazi katika hospitali za Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Hospitali ya Tumbi na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Madaktari hawa wamekuwa wakitoa huduma mbalimbali za Kibingwa kwa wananchi na kuwajengea uwezo madaktari wanaofanya nao kazi katika hospitali hizo. Aidha, kwa kushirikiana na kampuni ya Labiofarm ya Cuba, Serikali imeweza kujenga kiwanda cha kutengeneza viuadudu vya kibaiolojia yaani biolarvicides kwa ajili ya kuua viluilui vya mbu waenezao malaria. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iligharamia ujenzi wa kiwanda hicho na Serikali ya Cuba ilitoa msaada wa wataalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, matarajio yetu ni kuwa, wataalamu hao watawajengea uwezo Watanzania ili waweze kutengeneza bidhaa hizo bila kutegemea wataalam kutoka nje ya nchi kwa siku zijazo. Viuadudu hivyo vimeanza kutengenezwa kuanzia mwezi Disemba 2016, na kwa sasa uhamasishaji wa Halmashauri mbalimbali nchini kununua bidhaa hizo umeanza. Endapo viuadudu hivyo vitatumiwa vizuri vitasaidia kupunguza mbu waenezao malaria na hivyo kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria nchini.