Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Othman Omar Haji (5 total)

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, iwapo itatokea kiongozi wa Umma atazungumzia masuala ya kisiasa ndani ya nyumba ya ibada; je, ni kifungu gani cha katiba au sheria kinachoweza kumtia hatiani kiongozi huyu? (Makofi)
Swali la pili, iwapo katika matamshi yake aliyoyazungumza katika nyumba hiyo inakwaza jamii moja katika Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.
Je, ni adhabu gani amestahiki Kiongozi kama huyu? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilishaeleza katika jibu langu la swali la msingi kwamba mtu yeyote ambaye atafanya kinyume na ambacho Katiba inaelekeza na vilevile sheria, atakuwa amefanya makosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize tu hapa kwamba, Katiba ya nchi ndiyo inayozaa sheria. Kwa hiyo, siyo siyo tu mtu, hata chama cha siasa ambacho kinaendekeza masuala ya kidini nacho kinakuwa kimekosea, lakini siyo suala la mtu mmoja kuamua kuwa umekosea, kuna utaratibu wa kuweza kulifikisha hilo suala mbele ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hatua za kisheria kuweza kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kwa viongozi wa Kiserikali, anaingia kwenye Kanisa au Msikitini, siyo Serikali iweze yenyewe kuwa kila sehemu, lakini ijengwe hoja na wananchi ambao wamefika pale na huko ndiko kulinda utawala wa sheria katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. OTHMAN OMAR HAJI:Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza madogo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tarehe 20 Machi, 2016 ambapo vyombo vya dola vilikamilisha kusimamia zoezi la uchaguzi wa Zanzibar, ambao uliiweka madarakani Serikali
haramu inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein jambo ambalo wakati huo palitokea tuhuma dhidi ya wafuasi wa CUF kwamba wanapita wakiharibu mali za wafuasi wa CCM, shutuma ambazo ziliwapelekea wafuasi wa CUF kukamatwa, kupigwa, kuwekwa mahabusu……
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matokeo hayo ambayo yalitokea katika Kisiwa cha Pemba, katika Kisiwa cha Unguja maeneo ya Tumbatu kulitokea nyumba za wafuasi……
Mheshimiwa Naibu Spika, najenga hoja.
Nyumba za wafuasi wa CUF kuchomwa moto na wafuasi wa CCM, kwa kuthibitisha majibu ya Mheshimiwa Waziri Je, kwa nini wafuasi hawa walioshutumia na CUF katika Kisiwa cha Tumbatu, kwa nini mpaka leo hawajakamatwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, inapotokea Wapinzani wanataka kufanya mikutano, Jeshi la Polisi wanasema wana taarifa za kiintelijensia kwamba hakuna usalama. CCM wanapofanya mikutano yao, Jeshi la Polisi linakusanyika pote ili kulinda mikutano hiyo. Je, kwa nini Jeshi la Polisi linailinda mikutano ya CCM lakini pale ambapo Upinzani wanafanya mikutano hawataki kuilinda?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nataka nimthibitishie pamoja na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa ujumla kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ni halali ambayo imechaguliwa na wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kauli kama hizi katika Bunge lako Tukufu ambazo zinapotosha umma siyo tu kupotosha na kudhalilisha Serikali halali na maamuzi sahihi ya wananchi ziendelee kupingwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili anauliza swali kwamba baada ya uchaguzi kuna wafuasi wa CUF ambao walishutumiwa kwa tuhuma mbalimbali ambao walikamatwa na akatolea mfano wa Kisiwa cha Tumbatu kuna wafuasi ambao hawakuchukuliwa hatua nadhani alikusudia wa vyama vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu baadhi ya Vyama vya Upinzani ikiwemo chama chake, viongozi walijitokeza kuhamasisha wananchi kufanya mambo ambayo yanakiuka sheria za nchi yetu. Kuna matukio mbalimbali ambayo yamejitokeza ikiwemo kuchomwa moto kwa nyumba, kuchomwa mashamba, kurusha mabomu ikiwemo nyumba ya Kamishna Mkuu wa Polisi wa Zanzibar ambayo kwa uchunguzi uliofanyika mpaka sasa hivi tunavyozungumza watu ambao wamekamatwa kuhusika na urushaji bomu katika nyumba ya Kamishna ni Viongozi Waandamizi wa Chama cha CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Polisi imeshakamilisha uchunguzi wake na suala lipo kwa DPP na linahitajika kupelekwa Mahakamani ili hatua za kisheria zichukuliwe. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba, watu hawa ambao wamefanya matukio ya ukiukwaji wa sheria wapo wengi, mpaka sasa hivi zaidi ya watu 24 wameshapelekwa katika vyombo vya sheria na wengine wapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi. Kwa hiyo, siyo sahihi kwamba Jeshi la Polisi linafumbia macho uvunjifu wa sheria. Iwe Tumbaktu, Pemba, Unguja ama sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yeyote ambaye anakiuka sheria za nchi atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusiana na hoja ya kwamba mikutano ya CCM inaruhusiwa na Polisi lakini mikutano ya CUF hairuhusiwi. Naomba nikuthibitishie pamoja na Wabunge na wananchi wote kwa ujumla, kwamba hakuna ubaguzi kama nilivyojibu katika swali langu la msingi katika kuhakikisha kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, halibagui chama cha siasa. Tunapozungumza sasa hivi mikutano ya hadhara imezuiliwa kwa vyama vyote ikiwemo Chama cha Mapinduzi. Hakuna sehemu yoyote ambayo Chama cha Mapinduzi kinaruhusu mikutano ya hadhara zaidi ya Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa katika Majimbo yao. Mikutano ya ndani inaruhusiwa kwa vyama vyote na haijawahi kuzuiliwa kwa chama chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge kama ana uthibitisho wa mikutano halali ya chama chake ambayo imezuiliwa basi atuletee taarifa ili tufuatilie tuweze kuchukua hatua stahiki.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa mujibu wa Msajili wa Hazina, Benki ya Kilimo inawajibika kutoa huduma zake Tanzania nzima. Napenda kumuuliza Naibu Waziri, ni kwa nini benki hii haijafikisha huduma zake kule Visiwani Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la Msingi, katika utekelezaji wa mpango wa biashara wa Benki hii ya Maendeleo ya Kilimo, imepanga kufungua ofisi sita za kikanda na Zanzibar ikiwemo. Ni imani yangu baada ya kufungua Ofisi ya Kikanda Dodoma, Ofisi ya Kikanda ya pili itakayofunguliwa ni Ofisi yetu ya Visiwani Zanzibar.
MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswala mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, pamoja na kuhamasishwa Halmashauri mbalimbali kununua dawa hizi zinazotengenezwa na kiwanda hiki, Wizara ya Afya ni mteja mkuu ambaye alitegemewa kununua dawa hii inayozalishwa na kiwanda hicho, lakini wameshindwa kutokana na kukosa pesa, jambo ambalo limepelekea kiwanda kutafuta wateja kutoka nchi za nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Naibu Waziri atueleze hapa imekuwaje Wizara kutokutenga pesa kwa ajili ya kuwanusuru Watanzania ambao wanasumbuliwa na ugonjwa huu wa malaria hapa nchini?
Swali la pili,kwa sababu teknolojia hii ya kuzalisha viuadudu vya kuulia viluilui vya mbu ni mpya hapa Tanzania na Bara zima la Afrika, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutueleza ni maeneo gani katika Jamhuri yetu ya Tanzania wamewahi kuchukua angalau sampuli ya kiwanda kile na kuweza kuifanyia majaribio ili kuweza kujua ubora wa dawa hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba arudie swali la pili walikuwa wanapiga makofi, sikumsikia vizuri.

MHE. OTHMAN OMAR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimemuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwa sababu teknolojia hii ya kuzalisha viuadudu vya kuulia viluilui vya mbu wanaoeneza malaria ni mpya hapa Tanzania na Bara zima la la Afrika.
Je, Wizara imewahi angalau kwenda kuchukua sampuli kule kiwandani na kuweza kuifanyia majaribio na kuweza kujua ubora wa hii dawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nitaanza na swali la pili kwamba je, Wizara imewahi kwenda kuchukua sample kwenye kiwanda kile na kuzifanyia utafiti?
Kwanza naomba nimhakikishie kwamba teknolojia
ya biolarvicides kuingia hapa nchini na kukubalika kutumika kuna mchakato mrefu wa kisayansi ambao umefuatwa.
Kwa hivyo, katika hatua hii ambapo inazalishwa kwa wingi wala hakuna haja ya kufanya utafiti wa majaribio, kwa sababu pale mwanzoni wakati ugunduzi wa teknolojia unafanyika zilifanyika tafiti ambazo kisayansi zinajulikana kama clinical tries za kubaini efficacy ya biolarvicide ambayo inatumika lakini pia kubaini kama kuna any emergency ya resistance yaani usugu dhidi ya biolarvicide yenyewe ambayo inatumika na hatimaye ikafikiwa kuthibitishwa kwamba ni teknolojia ambayo ni effective.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano walipoanza kufanya tafiti hizi miaka hiyo ya zamani walitumia bacteria ambaye anajulikana kama bacillus sphaericus katika hatua za awali mpaka wakafikia mwisho wakakamilisha uchunguzi na ikaonekana kwamba bacillus sphaericus ana-develop resistance kiurahisi sana, wakahama wakaweka bacillus thuringiensis vara israelensis ambayo ni second generation.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumuweka huyu bacillus wa aina ya pili yaani kwa kifupi BTI ikaonekana kwamba yeye ni effective zaidi kuliko yule wa kwanza. Kwa hivyo, ikaonekana kwamba sasa tutumie generaly BTI kwa ajili ya biolarvicide. Kwa hivyo ni teknolojia ambayo imethibitishwa na haina shaka, na sisi Tanzania tunapaswa kujivuna kwa kuwa tuna kiwanda hicho hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza kiwanda kile kitazalisha full capacity yake biolarvicides lita milioni sita. Malengo hasa ya kuanzisha kiwanda kile sio kwa ajili ya Tanzania peke yake, ni kwa ajili ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika na dunia ambazo zitakuja kununua biolarvicide hapa nchini. Kwa mfano mpaka sasa tayari tuna nchi za Serbia, tuna nchi ya Cuba, yenyewe tuna nchi za Sweden, tuna nchi ya Niger ambazo zimenunua biolarvicide kutoka Tanzania, kwa sababu kuanzia hiyo mwezi Desemba, 2016 mpaka sasa tumezalisha lita milioni mbili na tumeuza kwenye hizo nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hapa Tanzania Halmashauri takribani tano zimeonesha nia ya kununua, Halmashauri mbili zimekwisha nunua japokua kwa kiasi kidogo na zimekwishatumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niwapongeze Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe na Halmashauri ya Wilaya ya Geita ambao wao walikuwa ni wa kwanza kwa Halmashauri za hapa nchini kununua biolarvicide. Kwa hiyo swali lake la msingi linasema kwamba Wizara ya Afya tungepaswa tununue si sahihi kwa sababu malengo ni sisi kuwezesha kiwanda kile kuwepo na baada ya hapo Halmashauri ziweke kwenye bajeti zao wao wenyewe waweze kununua pale kadri ambavyo wanahitaji. Ndiyo maana tunaendelea na uhamasishaji wa Halmashauri zote nchini kununua biolarvicide kwa ajili ya control ya malaria.