Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khamis Mtumwa Ali (2 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MTUMWA ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia, aidha napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Kiwengwa kwa kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mbunge wa Jimbo hili tiketi ya Chama cha Mapinduzi. Pia napenda kuwashukuru Watanzania kwa kumchagua Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Mheshiimwa Dkt. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba niguse mambo mawili, matatu ambayo yamezungumzwa katika hotuba ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wapinzani katika hotuba yao wamezungumza kwamba wana hofu ya kuvunjika kwa Muungano, mimi napenda kusema kwamba hofu hii wataendelea kuwa nayo lakini Muungano huu hauvunjiki utaendelea kuwepo, kwa maslahi ya Watanzania wakiwemo Wazanzibari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli Muungano huu umeleta faida nyingi kwetu, wengine tunaozungumza hapa tumekuwepo kwa tiketi ya Muungano kama siyo Muungano maana yake tusingekuwemo humu na tusingefika hapa kuzungumza na kuchangia mambo mbalimbali ambayo yanahusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wameendelea kusema eti Muungano huu unalindwa na CUF na Maalim Seif, kama siyo wao Muungano huu usingekuwepo. Nataka niwahakikishie kwamba, Muungano huu unalindwa na Watanzania wote, Watanzania wa Zanzibar na Watanzania wa Tanganyika ndiyo wanaoulinda Muungano huu, siyo Maalim Seif na wana-CUF. Kusema ukweli Upinzani Muungano huu hawautaki, iweje leo waulinde, sisi tutasema Serikali ya CCM ndiyo itaulinda Muungano huu na tutahakikisha kwamba unadumu kwa maslahi ya Tanzania na kwa maslahi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba yao hii, wamezungumzia haki za binadamu, eti wamesema Serikali ya Muungano imeivamia Zanzibar kijeshi na Polisi kwenye uchaguzi wa marejeo. Hivi Zanzibar ina Serikali yake ivamiwe kijeshi kivipi, wao wanachotaka kufanya wanataka kufanya vurugu, lakini nafasi hiyo hawakuipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalipongeza Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kusimamia uchaguzi wa marudio, kurejewa kwa hali ya ukimya, hali nzuri ya ulinzi na usalama wa hali ya juu. Wananchi wote walipewa fursa ya kushiriki katika uchaguzi ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ambao wamekataa wenyewe wasisingizie kwamba Zanzibar imevamiwa, waseme ukweli kwamba walishindwa kushiriki kwa sababu wanajua kwamba hawawezi kurejea katika uchaguzi ule kwa sababu CCM tutawashinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njama zao za kuiba kura tulizibaini na bahati nzuri Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kupitia Jecha alwatan akafutilia mbali uchaguzi ule na hatima yake tukarudia uchaguzi ambao halali na hatimaye wameshindwa kuingia uwanjani wametia mpira kwapani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nawaambia zile pesa za posho na mshahara wanaopata wawasaidie wale wenzao waliouza mashamba yao ya mikarafuu kwa ajili ya kugombea baadaye wakakaa nyumbani wakaambiwa eti wapumzike sasa hivi wanajuta kwa nini hawakuingia katika uchaguzi ule. Iliyobaki ni kelele na kuwapa matumaini mabovu Wazanzibari kwamba kesho eti Jumuiya ya Madola itamtangaza Maalim Seif itakuja kumuapisha, yaguju. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wamekaa wanasema eti wapewe nafasi wapumue, sasa hivi ndiyo wakati mzuri tumeshawapa nafasi wapumue nje ya Serikali. Kwa sababu walikuwepo ndani ya Serikali hakuna walichokifanya, walikuwa wanaijejea Serikali, hawana maendeleo waliyoyaleta. Wamepewa Wizara ya Afya wameshindwa kuleta hizo huduma walizokuwa wanasema, maana walikuwa wanasema hata panadol hakuna, hatimaye wameshindwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, hawa bora wakae nje waone sasa hivi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein ikifanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika kutoa mawili, matatu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri. Kwanza nampongeza kwa hotuba yake nzuri na mwonekano mzuri ambao aliusema hasa kwa nia ya kuyarekebisha yale mambo ambayo yanahusiana na Muungano yanayohusu masuala ya kifedha. Huu mgao wa fedha ni vyema sasa ukaangaliwa kwa makini.
MHE. MTUMWA KHAMIS ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mgao huu ukiangaliwa kwa makini utasaidia zaidi kudumisha Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika naomba nizungumzie Mfuko wa Jimbo. Mfuko huu unakuja Zanzibar kama ulivyo na ni vyema ukapangiwa utaratibu mzuri ili tuweze kuupata katika wakati mzuri kama wanavyoupata wenzetu huku Bara. Kwa sababu pesa zikifika kule zinakuwa zinachelewa, kwa hiyo, tunamuomba Mheshimiwa Waziri afuatilie na apange utaratibu mzuri wa fedha hizi ziweze kupatikana kwa wakati mzuri ili kuweza kuhakikisha maendeleo ya wananchi wetu yanapatikana kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira za Muungano, ni jambo muhimu sana kuangalia ajira hizi zinapatikana kwa usawa. Tukiwa tunapata ajira hizi kwa usawa hata wale vijana ambao wana mihemko na hawaelewi kuhusiana na suala la Muungano wataweza kuelewa. Ikiwa kuna utaratibu mzuri wa upatikanaji wa ajira hizi katika hizi taasisi za muungano itasaidia sana kuhakikisha kwamba Muungano wetu huu unadumu kwa sababu upungufu mdogo mdogo uliokuwepo ukifanyiwa kazi utaweza kusaidia kuhakikisha kwamba Muungano wetu huu unaimarika na unadumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mazingira, naomba nimpongeze Waziri kwa jitihada ambayo ameichukua kwa kuanza kwa kasi mpya kuhakikisha kwamba masuala ya mazingira yanafanyiwa kazi vizuri. Napongeza pia hatua anazozichukua sasa hivi kwa kutembelea Zanzibar kwa kwa kuwa Kisiwa cha Zanzibar…
MHE. MTUMWA KHAMIS ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KHAMIS MTUMWA ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba mbingu na ardhi kwa kuniwezesha kuwa mzima wa afya na kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Mama Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kazi nzuri ya kusimamia Taifa letu hili. Pia napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya katika kusimamia amani ya nchi hii. Kwa kweli bila amani hatuwezi kufanya jambo lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linakabiliwa na changamoto mbalimbali nitaanza kuzungumzia makazi ya askari. Kwa kweli makazi ya askari ni duni sana pamoja na Mheshimiwa Waziri kuelezea kwamba wana mpango mzuri wa kujenga nyumba za askari. Hata hivyo, kiuhalisia ukiangalia zile nyumba za askari ambazo zipo hivi sasa zinatisha. Ukienda central tu hapo utakuta nyumba za askari zina mabati, ndani hazina ceiling board hata yule askari akinunua mayai akayaweka ndani baada ya wiki utaona yameshatoa watoto yaani zile nyumba zimegeuka incubator. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo hizo nyumba za askari zilizopo ambazo hazina hata ceiling board, zimejegwa kwa udongo ambapo siku za mvua ukipata maji zinaporomoka. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri ni lazima aangalie hali hii kwani mazingira wanayoishi askari wetu si mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifika wakati wa usiku baridi iliyokuwemo ndani ya nyumba zile ni kama wapo katika mafriji. Wale ni binadamu, wanataka nyumba nzuri ili waishi kama binadamu wengine ili waweze kufanya kazi vizuri. Naomba sana Serikali kupitia Wizara hii waweze kuangalia hizi nyumba wanazojenga na hizi ambazo zipo ili kuziboresha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea posho za askari wetu hawa. Kwa kweli inasikitisha sana, askari wadogo hawapati posho stahiki na kwa wakati na hali hii inapelekea kuwa na imani potofu na duni. Ikiwa kama kuna matabaka ya kupata hizi posho stahiki au kucheleweshewa kupelekwa posho hizi kwa wakati itapelekea askari hawa kuvunjika moyo na hatimaye kutofanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana hapa wakati wa bajeti tulimwambia Mheshimiwa Waziri kwamba askari wanalipia umeme kwenye mifuko yao wenyewe kutoka katika mishahara yao. Mheshimiwa Waziri akasema hili atalisimamia lakini inafika hatua wanastaafu pesa za umeme ambazo wametumia kutoka kwenye mifuko yako hawajalipwa hadi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana sana Mheshimiwa Waziri na hili aliangalie aweze kuhakikisha askari hawa wanapewa posho zao straight kama ilivyo kwa Jeshi la Wananchi (JW). Kwa sababu wakipewa hivyo itapunguza malalamiko wakati wa kustaafu ya kutopewa posho au pesa ambazo wanazitumia kwa ajili ya kulipia nyumba au umeme. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja aweze kutuelezea vizuri mkakati huu kafikia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kuhusu mafunzo mbalimbali ya Jeshi la Polisi. Ni ukweIi usiopingika kwamba bila mafunzo Jeshi la Polisi haliwezi likafanya kazi vizuri. Ikiwa mafunzo haya yanatolewa kwa askari wa headquarter tu bila kuwashirikisha wale askari wadogo wadogo waliopo mikoani itakuwa ni vigumu askari hawa kufanya kazi kwa weledi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aweze kuhakikisha kwamba askari wadogo nao wanakwenda mafunzo siyo waliopo headquarter tu mikoani mafunzo hamna, hivi sasa mafunzo yamepungua kabisa. Kama kutakuwa na upungufu wa bajeti basi Serikali ipeleke fedha kikamilifu ili mafunzo haya yaweze kupatikana vizuri zaidi kwa askari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa Vituo vya Polisi kama alivyosema Mhesimiwa Raza pale vipo katika hali ngumu. Katika Jimbo langu kuna Kituo cha Polisi kimoja tu, unapotokea uhalifu inakuwa ni shida sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba katika Shehia yangu ya Kilombero tungepata Kituo kimoja cha Polisi kwa sababu anapotokea mhalifu inakuwa ni vigumu kumfikisha Kituo cha Mahonda ambapo ni mbali zaidi kutoka eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekuja hapa akasema kwamba viatu vyake vizuri sana kuliko vya wengine, ni kweli. Hata hivyo, askari wake viatu wanavyotumia ni vile vya UN! Namwomba sana Mheshimiwa Waziri ajitahidi viatu vya askari wake viwe kama vyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naunga mkono hoja. Ahsante sana.