Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Khamis Mtumwa Ali (2 total)

MHE. KHAMIS M. ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza je. La kwanza, je Serikali haioni utaratibu huu wa askari au wakuu wa vituo kujaza fomu na kupeleka risiti unaonesha urasimu, na inapelekea hadi askari anastaafu kutokulipwa pesa zake hizi za kulipa umeme?
Lakini la pili kwa upande wa askari wadogo ambao si maafisa kwa nini wasiwekewe pesa zao za posho za umeme na maji katika mishahara yao kama wanavyofanya JWTZ? Nashukuru.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Khamis Mtumwa, Mbunge wa Kiwengwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali lake la pili, ukweli ni kwamba sio askari wote ambao wanalipwa posho kuna askari ambao hawalipwi posho, kuna askari ambao wanaishi katika nyumba binafsi ambao ndio wengi. Kama unavyofahamu Waheshimiwa Wabunge sasa hivi tuna changamoto ya makazi kwa askari, ambao hawa kiutaratibu wanalipwa posho ya pango ni asilimia 15 ya mshahara. Kwa hiyo hawa hawana shida. Tatizo lilipo ni kwa wale askari ambao wanaishi kwenye nyumba za askari ambapo wakati mwingine kuna tatizo la kuchelewa kwa posho zao. Hata hivyo Serikali Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na swali lake la kwanza ambapo alizungumzia kuchelewa kwa malipo hayo hadi kufikia wakati askari wanastaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha ucheleweshwaji wa malipo ya madeni haya. Moja kama ambavyo mnafahamu wakati mwingine kunakuwa na ucheleweshaji wa kupata fedha za bajeti ama wakati mwingine zinakuja kidogo. Lakini pia wakati mwingine hata ambapo zinapokuja kuna matukio ambayo mara nyingi hatuyatarajii, ambayo yanajitokeza yanafanya matumizi yale yaweze kuhamishiwa na kutekeleza yale matumizi ya dharura, ikiwemo ya ujambazi, migogoro ya kijamii, hata operesheni za baadhi ya wanasiasa zisizokuwa na tija. Haya mambo na mambo mengine yanachangia wakati mwingine kufanya fedha hizi zitumike kwa matumizi mengine ya dharura na kuchelewesha malipo yale.
MHE. KHAMIS MTUMWA ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa taasisi hizi za Ubalozi ni taasisi za Muungano je, haoni ipo haja sasa ya kushirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar katika kukagua taasisi hizo?
Pili, kwa kuwa tuna mahusiano mazuri katika taasisi hizi za Muungano, yeye Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hajaona ulazima; je, haoni sasa imefika wakati wa kushirikiana na kuonesha Muungano wetu huu unadumu na kuondosha kero ndogo ndogo ambazo zinatokezea kama hizi za kutokushirikishana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali yetu na lengo lake kwa Muungano ni kuudumisha Muungano wetu katika kila nyanja, kama alivyosema Mheshimiwa Rais wetu katika sherehe za Muungano za mwaka huu 2017 kwamba Serikali yetu inaupenda Muungano na tutaulinda kwa ngazi zote na nguvu zote, hiyo itabaki hivyo. (Makofi).
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mwanzo jukumu hili la ukaguzi ni la Kikatiba na Kisheria. Ofisi zote za Muungano hukaguliwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini akiona inafaa Mkaguzi huyu anaweza kumshirikisha Mkaguzi yule. Tuelewe tu kwamba kikatiba na kisheria siyo lazima, lakini kimahusiano anaweza akafanya hivyo. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS,
(MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongezea katika majibu mazuri kabisa yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha, kwamba pamoja na mgawanyo wa majukumu ya kikatiba na kisheria kuhusu mamlaka za ukaguzi maeneo na taasisi zinazopaswa kukaguliwa, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wakaguzi hawa na Wadhibiti Wakuu wa Serikali zote mbili wanashirikiana kwa karibu sana katika kubadilishana uzoefu, pia kujenga uwezo wa kitaasisi hasa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa upande wa Zanzibar. Hilo ndilo ambalo tunalihimiza na tunalisisitiza lamahusiano na ushirikiano wa taasisi za pande zote mbili hata katika masuala ambayo siyo ya Muungano.(Makofi)