Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jamal Kassim Ali (3 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia, nitumie nafasi hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Magomeni kwa kunichagua kuja kuwa mwakilishi wao katika Bunge letu hili Tukufu. Ni imani yangu ya kwamba tutashirikiana pamoja katika kuleta maendeleo ndani ya Jimbo letu na Taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, niwapongeze Watanzania kwa kuendelea na kuwa na imani na Chama cha Mapinduzi na kukipa fursa kuongoza nchi yetu kwa kipindi kingine. Naamini hivyo hivyo kwa Wazanzibari wenzangu wataendelea kukipa fursa chama chetu kuiongoza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wachangiaji waliotanguliwa kumpongeza Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania; Waziri Mkuu na timu yote ya Serikalini kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameanza kuifanya kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu. Nimpongeze Dkt. Mpango na timu yake yote kwa kuwasilisha Mpango mzuri kabisa ambao umekwenda kujibu au kutafsiri ile dhana ya Rais wetu ya kusema anataka kuipeleka nchi yetu kuwa nchi ya viwanda. Niwapongeze sana Wizara kwa kuandaa mpango wetu huu mzuri na kuwasilisha vizuri katika Bunge lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo nitayagusia, eneo la kwanza, ni eneo la kodi. Nimpongeze Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenyewe kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuweka mikakati kuona namna gani tunaendelea kukuza makusanyo yetu ili tuweze kumudu mahitaji yetu ya maendeleo katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejionea ongezeko kubwa kabisa la ukusanyaji wa kodi ambalo taasisi yetu ya TRA kwa kipindi hiki cha miezi miwili ambayo imefikia. Niwapongeze sana na juhudi hizo waziendeleze ili kukuza makusanyo, kwa sababu tunaamini kabisa makusanyo hayo ndiyo yatafanya Mpango wetu utimie na yale maendeleo ambayo tunakusudia kuwapelekea wananchi yafikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la kodi, kwa kipindi kirefu kabisa, kumekuwa na masikitiko au malalamiko yanayohusu masuala ya bidhaa na vitu ambavyo vinatoka Tanzania Zanzibar kuja Tanzania Bara. Mfumo wetu wa kodi uliokuwepo hivi sasa kwa bidhaa hizi zinazotoka Tanzania Zanzibar kuja Tanzania Bara kunakuwa na tozo la kodi ambalo linaitwa difference.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati tunajiuliza, iweje tufikie hapo? Tuna Taasisi moja ya kodi ambayo ni TRA, Taasisi hii na Zanzibar ipo, inatumia sheria moja na mwongozo huo huo mmoja, wa Kamishna huyo huyo mmoja wa Forodha. Tumekwenda kutengeneza mfumo ambao umetengeneza urasimu, manung‟uniko na baadhi ya wakati hata ukokotoaji wa kodi hizi hauko wazi, wananchi wetu hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu ana television yake tu akifika pale Bandarini Dar es salaam anaambiwa alipie kodi hajui alipie kodi vipi na ile TV ameinunua Zanzibar. Kwa hiyo, mambo kama haya, are very peanut, lakini huko mtaani tunakwenda kutengeneza bomu ambalo wananchi wetu wanalinung‟unikia lakini Serikali yetu inachukua muda mrefu kabisa kulipatia majawabu mambo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi najiuliza, TV ili itozwe kodi ya forodha maana yake lazima mkadiria kodi aijue CIF yake, aliijuaje? Kwa hiyo, hizi kodi hazina base yoyote, tumekuwa tunatengeneza fursa ya maafisa wetu kujiamulia tu haya mambo na kwa asilimia kubwa yametengeneza urasimu na mifumo ya rushwa. Kwa hiyo, nimwombe kabisa Mheshimiwa Waziri, hili jambo linawezekana, halihitaji mshauri mwelekezi, yeye mwenyewe anatosha kulielekeza, kulifuta, hao wananchi basi wa-enjoy fursa ya Muungano wetu, Wabara waende Zanzibar na bidhaa zao bila tabu, Wazanzibari wakija bara, waje bila taabu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nitalizungumzia, eneo la viwanda. Tumeona kabisa Mheshimiwa Rais, toka alivyokuwa katika kampeni zake na alivyozindua Baraza lake la Mawaziri alikuwa anazungumza sana kuhusu suala la viwanda. Lengo lake ni kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Nampongeza na namuunga mkono katika hilo na naamini kabisa, viwanda ambavyo tutavianzisha ndiyo vitakwenda kujibu matatizo ambayo nchi yetu inayakabili kwa sasa, viwanda hivi hivi ndiyo vitaenda matatizo ya ajira kwa vijana wetu, viwanda hivi hivi ndiyo vitaenda kujibu matatizo ya masoko kwa wakulima wetu, wafugaji na wavuvi. Viwanda hivi hivi ndiyo vitakwenda kujibu tatizo letu…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha. Hiyo ni kengele ya pili nimeshauriwa hapa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote, napenda kuwashukuru Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa kunichagua kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Nawaahidi kwamba nitaitumikia nafasi hii kwa maslahi yetu na maslahi ya chama chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa bajeti nzuri kabisa ambayo imetafsiri ile dhana ya Mheshimiwa Rais ya kwenda kwenye Tanzania ya viwanda, Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo nakupongeza sana. Hao wanaokubeza, naamini kabisa ndani ya nafsi zao wanajua kwamba katika viongozi wenye dira wewe ni miongoni mwao. Naweza kudiriki kusema kwamba wewe sio wa Kitaifa, bali wewe ni wa Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja, kwenye upande wa umeme. Tumeona jitihada za Mheshimiwa Waziri na wataalam wake katika kuipeleka Tanzania kuondokana na changamoto mbalimbali za umeme ambazo ilikuwa inakabiliwa nazo huko nyuma. Tumeona coverage ya umeme ilivyoongezeka, upungufu wa bei, ongezeko la install generation capacity, kwa hiyo, nawapongeza sana. Naamini bado tuna changamoto kubwa katika sekta hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumshauri Waziri na Wizara na sekta husika kwamba kuna maeneo inabidi tuzidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kwamba ile dhamira ya kuwa na umeme wa uhakika na wenye kutosheleza inafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye mpango wetu wa miaka kumi hadi mwaka 2025 tunatarajia kuwa na umeme usiopungua megawatts 10,000 na sasa tupo kwenye megawatts 1461. Kwa hiyo, tunatakiwa kwa hesabu za haraka haraka, kwa wastani kila mwaka tuongeze install generation capacity isiyopungua megawatt 948.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema ukweli Megawatts hizi ni nyingi sana na kwa kuiachia TANESCO peke yake hawataweza. Ninachokusudia kusema ni kwamba kuna haja ya kufanya reform katika sekta yetu ya umeme. Tunajua TANESCO imekabiliwa na changamoto nyingi katika muda mrefu. (Makofi)
Kwanza, shirika letu hili la umeme kwa kipindi cha takriban miaka minne sasa limeshindwa kuzalisha faida, linaendeshwa kihasara, kwa hiyo, halina mtaji wa kwenda kuwekeza kwenye uzalishaji wa umeme wote ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hata ukiangalia vitabu vyao vya mahesabu, pia wana-operate katika deficit working capital. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kabisa wakati umefika kwenda kufanya reform ya sekta ya umeme nchini mwetu. Serikali ifungue milango, wawekezaji binafsi waingie katika uzalishaji na katika usambazaji wa huduma hii muhimu kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itatufanya kwanza kupata ongezeko kubwa la umeme kwa sababu tutafungua mwanya kwa wazalishaji wengi kuingia, lakini tutapata nafasi ya mashirika haya ambayo yanafanya usambazaji wa umeme ku-compete na kushusha bei ya umeme; na yenyewe yata-compete kwasababu yatakuwa katika business oriented. Naamini kabisa yataendeshwa kibiashara na yatazalisha faida tofauti na sasa ambavyo TANESCO inavyoenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa East Africa wote walikuwa na matatizo kama ya kwetu, wenzetu Wakenya walikuwa na kama ya kwetu au kuzidi ya kwetu; Waganda hali kadhalika, lakini walifanya reform kubwa kabisa katika sekta hii muhimu ya umeme, lakini hatimaye leo mashirika yao yanazalisha faida, hayaendi kwa ruzuku na pia wanapata wasaa wa kuchangia pato kwa Serikali kama sehemu ya gawio la Serikali. Kinyume na hapa kwetu ambapo Shirika letu la TANESCO mara zote limekuwa kila mwaka likiendeshwa kwa ruzuku ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kabisa Mheshimiwa Profesa nia hii unayo, dhamira unayo na uwezo unao. Kwa hiyo, ni wakati sasa wa kufanya reform kubwa ya kuhakikisha tunaenda katika uzalishaji ambao ile dhamira ya kufikia kwenye Tanzania yenye viwanda tunafikia. Kwa sababu bila kuwa na umeme wa kutosha na uhakika, suala la viwanda litabakia kwenye vitabu vyetu na mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huo, niende kwenye upande wa EWURA. Nimepitia kitabu cha bajeti, ukurasa wa 80 kuna jedwali lile la bei elekezi za EWURA za umeme. Katika jedwali lile kuna vitu nimebaini niweze kusema ni changamoto ambazo naomba Mheshimiwa Waziri uzifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia upande wa tariffs hizi za bei ya mahitaji ya juu (demand charges); mteja ambaye yuko katika T3HV (high voltage) wanachajiwa shilingi 16,550 kama tozo lao la bei ya mahitaji ya juu, wakati logic hapa hawa waliokuwa kwenye transmission line, cost ya kuupeleka umeme kwenye transmission line ni ndogo compared na cost ya kuupeleka umeme kwenye T3MV na T2, lakini wamebebeshwa mzigo mkubwa ambao hata najiuliza EWURA walipoweka hii bei walikusudia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wateja waliokuwepo hapa ni watatu tu waliokuwepo kwenye T3HV. Kuna Shirika la Umeme la Zanzibar, Bulyankhulu na Twiga Cement. Kwa mfano, kwa upande wa Shirika la Umeme la Zanzibar, ni bulk purchaser ambao waliingia mikataba na TANESCO ya Purchase Power Agreement ambayo sasa baada ya kuja EWURA ile mikataba imekuwa haina nguvu tena. Huyu ni bulk purchaser ambaye mwenyewe anatarajia huu umeme auze kwa wateja wake wa kati na wadogo. Sasa kama tunam-charge katika bei hii tunatarajia yeye auze kwa shilingi ngapi? Kusema ukweli katika kipindi kirefu kumekuwa na mlundikano wa madeni ambayo ZECO inadaiwa na TANESCO. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huenda moja ya sababu ya madeni haya naweza kusema ni appropriate tariff ambayo ZECO imekuwa ikitozwa kama ambavyo tunavyoona katika mwongozo huu wa bei ambao EWURA wameutoa mwezi Aprili. Kwa sababu wao wanachukua umeme katika transmission level ambapo gharama za depreciation, gharama za maintenance katika level hiyo ukilinganisha na wanaochukua T3MV na T2 ni ndogo lakini wamepewa…
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo kuchangia katika bajeti hii ya Serikali. Kwanza, nikupongeze kwa umahiri ambao umeuonesha ndani ya Bunge hili na kwa Watanzania wote katika kuendesha vikao vya Bunge kwa uimara na ujasiri mkubwa kwa kufuata kanuni na taratibu ambazo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kwenda, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mipango na timu yake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya kuhakikisha kwamba Serikali inakusanya pesa za kutosha kwenda kugharamia gharama mbalimbali za maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwenye suala la VAT. Mheshimiwa Dkt. Mpango katika mawasilisho yake ya mapendekezo ya bajeti, katika marekebisho ya Sheria ya VAT amesema kwamba sasa VAT baina ya pande hizi mbili za Muungano yaani Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara zitatozwa at a point of destination.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Waziri, biashara baina ya pande hizi mbili za Muungano zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa ya kodi mpaka sasa bado hatujaweza kuzitatua. Kuruhusu utaratibu huu ni sawasawa na kwenda na kijinga cha moto kwenye petrol, tunakwenda kuongeza matatizo ya kodi ambazo wafanyabiashara wetu wamekuwa wakizilalamikia, wale ambao wanafanya biashara zao baina ya pande mbili za Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Afrika Mashariki tumeona wameingia makubaliano ya redemption, kodi zikusanywe at a point of entry, na kule mzigo unapofika basi atakuwa remitted ile kodi yake iliokusanywa. Na mfumo huu ndio uliokuwa unatumika hapo kabla ya mabadiliko ya Sheria mpya VAT ya mwaka 2015. Nimwambie Dkt. Mpango, katika utaratibu huu mpya, kwanza tunaenda kutengeneza mgogoro wa kikodi kwa wafanyabiashara wetu, lakini pia tunaenda kusababisha au kutengeneza loophole ya watu kukwepa kodi. Kwa mfano leo hii, mtu akinunua mabati yake hapa Dar es Salaam akasema anayapeleka Zanzibar hatotozwa VAT. Lakini yale mabati yanaweza yasifike Zanzibar yakaishia hapa hapa Dar es Salaam, kwa hiyo, tutakuwa tunapoteza kodi yetu. Kwa hiyo, nikuombe kabisa katika hili tunaomba utaratibu ule ambao ulikuwa unatumika hapo awali uzidi au uendelee kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye mabadiliko ya Sheria ya Kodi ya Mapato, niungane na baadhi ya Wabunge wenzangu ambao hawakuunga mkono hoja ya kutozwa kodi Wabunge katika gratuity, niunge mkono hilo. Nilivyopitia Sheria Namba 11 ya mwaka 2004 ya Kodi ya Mapato katika jedwali la pili nilikuta kwamba watu na taasisi ambazo zinasamehewa kodi si Wabunge peke yake. Wapo watu wengine, zipo taasisi zingine ambazo zinasamehewa kodi. Kwa hiyo, Dkt. Mpango katika hiyo hoja yako ya kusema unataka ujenge mazingira ya usawa naona kwa hapo itakuwa haina mashiko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikuombe kabisa, kama ambavyo umeona kuna hoja na haja ya wale wote wengine waendelee kusamahewa kodi za mapato kwa mujibu wa sheria yetu ile kama ilivyo katika jedwali lake la pili basi, hoja na haja hizo bado ipo kwa Wabunge; Wabunge waendelee kusamehewa kodi katika gratuity zao ambazo wanalipwa baada ya kumaliza kipindi chao cha Ubunge. Hoja na haja hiyo ipo, wenzangu wengi wamezungumza na mimi nikuombe kabisa, niombe Serikali yangu sikivu katika hili itufikirie sana. Kwa vile muda ni mdogo sitaki kuzungumza mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine kwanza nikupongeze na niwapongeze wafanyabiashara wa Tanzania kwa kuutikia wito wako wa kuanza kutumia mashine za kielekitroniki yaani hizi za EFDs katika kutoa risiti pale ambapo wanauza bidhaa zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ningependa kujua kwa sasa ukuaji wa sayansi na teknolojia umepelekea mabadiliko makubwa kabisa hata katika transaction zetu hizi za mauzo. Kumekuwa na ukuaji mkubwa katika e-commerce na naamini Wabunge wenzangu mnashuhudia hilo. Leo hii kuna miamala inayofanywa kupitia moja kwa moja baina ya benki zetu kwenda kwa wauzaji. Kuna miamala ambayo inafanywa kupitia simu zetu, mfano mdogo tu asilimia kubwa leo ambao wanatumia ving‟amuzi, hawalipi cash dirishani wanatumia simu zao kulipia gharama mbalimbali za ving‟amuzi hivyo vya televisheni. Katika eneo hili Mheshimiwa Dkt. Mpango tunaomba uje utuambie basi Serikali kupitia TRA imejipangaje, ku-track records zote za mauzo hayo kuhakikisha kwamba na wao basi, wanachangia au wanakuwa sehemu ya kuchangia katika kodi ya Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwa upande wa CAG. Ofisi yetu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali imefanya kazi kubwa na nzuri sana kwa Taifa letu. Imefanya kazi kubwa na nzuri kwa Taifa letu na sote mashahidi, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali imekuwa ikitoa mapendekezo ya maboresho mbalimbali ambayo yameisaidia Serikali yetu hii kutokuingia katika hasara au upotevu mbalimbali wa fedha za umma. Lakini ofisi hii hii imesaidia Serikali kurudisha pesa mbalimbali ambazo aidha, watu walikwepa kulipa au watu walifanya ubadhirifu na kuwa sababu ya watu kuchukuliwa hatua kisheria kwa makosa hayo. Nimuombe Mheshimiwa Waziri katika Bajeti ya mwaka jana, ofisi hii tuliitengea shilingi bilioni 74; katika bajeti ya mwaka huu tumeitengea shilingi bilioni 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini maana yake? Maana yake tunaenda kumfunga miguu CAG asiende kukagua tunaenda ku-reduce ile scope yake ya ukaguzi na hii athari yake ni nini kwa Taifa letu? Kwanza kwa vile mwaka huu tumeona asilimia 40 ya pesa za bajeti ya Serikali zinaenda kwenye miradi ya maendeleo tutatengeneza mianya ya watu ambao hawana nia nzuri na Serikali yetu kwenda kuzitumia hizi pesa kutokidhi yale malengo ambayo yamewekewa kwa sababu ambayo watajihakikishia kwamba, hakutokuwa na ukaguzi wa kutosha ambao unaweza ukabaini huenda ubadhirifu au wizi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika nimepitia ripoti ya CAG ya Taarifa za Ukaguzi kwa Mwaka wa Fedha 2015, ukisoma tu katika preamble ripoti ile inabainisha kwamba CAG amefanya kazi kubwa na nzuri. CAG katika ripoti yake ile ile ameweza kutubainishia kwamba Serikali imepoteza takribani shilingi bilioni 100 katika eneo la ukwepa wa kodi.
Baada ya kusema hayo, naamini Mheshimiwa Waziri atakuja na hoja ya haya niliyoyaibua. Ahsante sana.