Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ally Abdulla Ally Saleh (15 total)

MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Hivi karibuni ulifanyika Mkutano wa Dunia wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Mazingira (COP21) ambapo Katibu Mkuu wa UN alisema Mkataba uliofikiwa ni momental triumph for people and our planet aimed at ending poverty, strengthening peace and ensuring life of dignity and opportunity to all:-
(a) Je, Serikali ya Tanzania ilishiriki vipi katika Mkutano huo?
(b) Je, Serikali itatekelezaje maazimio ya Mkutano huo kisera, kisheria na kiutendaji?
(c)Je, Serikali ina mikakati gani ya kupambana na umaskini, kuimarisha amani, heshima na fursa sawa kwa kila mtu?
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Mkutano wa 21 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi ulifanyika Paris, Ufaransa tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba, 2015. Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Begum Karim Taj, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, wataalam kutoka Ofisi ya Makamu Rais, Kilimo na Zanzibar walishiriki pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huu ulilenga kutekeleza msimamo wa Tanzania katika majadiliano ikiwa ni pamoja na:-
(i) Upatikanaji wa fedha na teknolojia za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi;
(ii) Upunguzaji wa gesijoto kwa ajili ya nchi kwa kuzingatia historia ya chanzo cha mabadiliko haya na uwezo wa nchi husika kukabiliana na tatizo hilo;
(iii) Kuweka kipaumbele katika uhimili wa mabadiliko ya tabianchi kwa sekta zote; na
(iv) Kushiriki katika miradi ya kupunguza gesijoto na nchi zilizoendelea kuendelea na jukumu la kutoa feda na tekinolojia kwa nchi zinazoendelea.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itatekeleza maazimio ya Mkutano huo kisera, kisheria na kiutendaji kwa kufanya yafuatayo:-
(i) Tanzania inatarajia kutia saini Mkataba wa Makubaliano ya Paris kati ya tarehe 22 Aprili, 2016 na 21 Aprili, 2017. Hatua hii itaimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012.
(ii) Serikali pia itahakikisha kuwa Tanzania inanufaika na fursa zilizo chini ya Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund), unaofadhili shughuli za Mkataba wa Makubaliano ya Paris.
(iii) Aidha, Serikali itaendelea kuzibana nchi zote zenye kuzalisha hewa ya ukaa ili zipunguze uzalishaji huo kulingana na misingi ya utekelezaji wa Mkataba huo.
(iv)Zaidi ya hayo, Serikali itaendelea kuwasiliana na washirika wa maendeleo ili kuanzisha maeneo ya ushirikano kwa muktadha wa utekelezaji wa Mkataba wa Paris.
(v) Mwisho Serikali itaimarisha juhudi na kujenga uwezo wa elimu kwa umma kuhusu athari za mazingira ya tabianchi na namna ya kukabiliana nazo ili kuimarisha juhudi za kuhimili athari za mabadiliko haya.
(c)Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kupambana na umaskini, kuimarisha amani, heshima na fursa sawa kwa wote. Mikakati hiyo ni kama MKUKUTA, MKUZA, MKURABITA, na matumizi ya Mifuko mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hili kama vile; Mfuko wa Mazingira, Mfuko wa Jamii chini ya Ofisi ya Rais TASAF, Benki ya Wakulima, Benki ya Wanawake na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, juhudi kwa sasa za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na ufisadi, kuimarisha utawala bora, uadilifu na uwajibikaji, zitatoa mchango mkubwa katika kuleta amani na maendeleo kwa wananchi wote. Kujenga uwezo na kuimarisha ushirikishwaji wa Serikali za mitaa katika utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi unazingatiwa ili fursa zinazopatikana ziwafikie Watanzania wengi zaidi kadri iwezekanavyo.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Yamekuwepo malalamiko mengi ya kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu wa kupiga watu, kuwatesa, kuchoma mali na kutishia amani katika Kisiwa cha Unguja Wilaya za Magharibi na Mjini na kwamba wahusika wamekuwa hawajulikani:-
(a) Je, ni kwanini hali hiyo imeachwa kuendelea kwa muda mrefu?
(b) Je, ni kwa nini Jeshi la Polisi limeshindwa kuwakamata wahusika?
(c) Je, wananchi hao wategemee lini vitendo hivyo kutoweka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwepo na ongezeko la matukio saba ya uhalifu katika Wilaya ya Magharibi na Mjini kwa mwaka 2015 ambapo jumla ya matukio 139 yaliripotiwa katika Vituo vya Polisi ikilinganishwa matukio 132 ya mwaka 2014. Hata hivyo pamoja na kuwepo kwa ongezeko hilo takwimu zinaonesha kuwa vitendo hivyo vya makosa ya jinai kwa ujumla Visiwani Zanzibar vinapungua kwa kasi ya kuridhisha. Mathalani, kwa mwaka 2015 jumla ya makosa 1,673 ya jinai yaliripotiwa katika Kituo cha Polisi, ikilinganishwa na makosa 3,227 yaliyoripotiwa mwaka 2014. Hii ni pungufu ya makosa 1,554, sawa na wastani wa asilimia 51.8.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo vya uhalifu Zanzibar havijafumbiwa macho hata kidogo kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, kwani kutokana na takwimu zilizoainishwa awali, ni dhahiri kuwa uhalifu Zanzibar sio tu wa kutisha na unaendelea kudhibitiwa. Jeshi la Polisi linao wataalam wa kupambana na wahalifu wa aina mbalimbali na litaendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote wanaovunja sheria.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Wavuvi kutoka Ukanda wa Uvuvi wa Kisiwa cha Unguja na wale wa Ukanda wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani wamekuwa wakifanya uvuvi kwenye maeneo yanayoingiliana, lakini hivi punde wavuvi wa Unguja wameanza kusumbuliwa na kuwekewa vikwazo vya kuvua maeneo ya Tanzania Bara:-
(a) Je, kwa nini wavuvi hao wasumbuliwe na kuwekewa vikwazo?
(b) Je, wavuvi hao hawana haki ya kuvua maeneo hayo?
(c) Je, ni kwa nini Serikali isiwaelimishe juu ya wanachotakiwa kufanya au wasichotakiwa kufanya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli za uvuvi kwenye maji ya kitaifa na maji baridi si moja ya suala la Muungano. Hivyo uvuvi katika maji hayo husimamiwa kupitia Sheria ya Uvivi, Na. 22 ya 2003 kwa upande wa Tanzania Bara na Sheria ya Uvuvi, Na. 7 ya 2010 kwa upande wa Zanzibar. Uvuvi katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu, husimamiwa na Serikali zote mbili kupitia Sheria ya Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu, Na.1 ya 1998 na marekebisho ya 2007.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwa wavuvi, Serikali zetu zimeweka utaratibu unaoitwa Dago au uvuvi wa makambi ambao unatoa fursa au ruhusa kwa wavuvi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara kuvua bila kusumbuliwa. Kupitia utaratibu huu, wavuvi wanatakiwa kuwa na utambulisho kutoka maeneo yao na kuwasilisha maeneo wanayokwenda kuvua ambao pia huainisha taarifa za uvuvi, zana anazotumia na muda atakaotumia kukaa kwenye Dago.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia majibu ya kipengele (a), wavuvi wa pande zote za Muungano wana haki ya kuvua kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kuzingatia maelezo ya Sheria ya Uvuvi katika eneo husika.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa elimu kwa wavuvi kuhusu uvuvi endelevu, kwa mfano, kupitia Ofisi za Uvuvi za Halmashauri ambapo mvuvi kabla hajapewa utambulisho, huelimishwa kuhusu utaratibu wa Dago. Vilevile Wizara imeandaa mwongozo wa makambi ambao uko wenye hatua za mwisho kama hatua mojawapo ya kutatua matatizo yanayojitokeza. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tuendelee kuwaelimisha wavuvi kufuata sheria na taratibu zilizopo kwa ajili ya uvuvi endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Hivi karibuni Tanzania imetangaza kufungua Ubalozi wetu nchini Israel, ambapo Tanzania ilikataa uhusiano hapo nyuma.
(a) Je, ni sababu gani zilizosababisha kubadilika kwa mtazamo wa nchi na kurudisha uhusiano wa Kibalozi?
(b) Ni upi msimamo wa Tanzania katika suala la uhuru wa Palestina ambayo ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya kukataa uhusiano na Israel hapo nyuma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka kuwa Tanzania na Israel zilikuwa na mahusiano mazuri ya kidiplomasia mara tu baada ya Tanzania kupata uhuru, ambapo Israel ilikuwa na Ubalozi wenye Makazi yake Dar es Salaam na Tanzania ikiwakilishwa na Ubalozi wake wenye Makazi Cairo, nchini Misri. Hata hivyo, mahusiano haya yaliingia dosari kuanzia mwaka 1973 hadi 1995 kufuatiwa na maamuzi ya Umoja wa Afrika kuitenga Israel kwa sababu ya sera zake juu ya watu wa Palestina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka huo wa 1973 hadi leo mabadiliko makubwa yametokea katika medani ya Kimataifa ukijumuisha kumalizika kwa vita baridi, kusambaratika kwa Muungano wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Kisoviet, kuanguka kwa Ukuta wa Berlin na kuungana kwa Ujerumani Mashariki na Magharibi. Pia katika suala la mgongano kati ya Israel na Palestina kumekuwa na hatua kadhaa zinazochukuliwa kulekea kumaliza mgogoro huo pamoja na kutiwa saini kwa Mkataba wa kwanza wa Oslo wa mwaka 1995 na ule wa pili wa mwaka 1993 na 1995 na uwepo wa Mpango wa Amani wa Palestina.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1995 Tanzania ilichukua hatua ya kwenda na mabadiliko ya dunia na kuamua kuhuisha mahusiano ya kidiplomasia na Israel, ambapo kukawa na ubalozi wa Israel Tanzania mwenye makazi yake Nairobi, Kenya na Tanzania ikiwa na Balozi wa Tanzania Israel mwenye makazi yake Cairo, Misri. Aidha, mahusiano yameendelea kukua hususan baada ya Tanzania kuwa na Sera Mpya ya Mambo ya Nje ile ya mwaka 2001 inayosisitiza diplomasia ya uchumi. Kwa kutambua hatua kubwa iliyopigwa na Israel katika nyanja za kilimo, sayansi na teknolojia Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhuisha mahusiano baina yetu ikiwa ni pamoja na kufungua Ubalozi Nchini Israel.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kufungua Ubalozi wa Tanzania Israel, msimamo wa Tanzania katika kutetea haki za wanyonge Duniani, wakiwemo watu wa Palestina, bado uko pale pale kama tulivyoachiwa na muasisi wetu wa Taifa hili. Hivyo basi, msimamo wa Tanzania katika suala la Israel na Palestina ni kumaliza mzozo huu kwa amani, kwa kuwa na nchi mbili yaani Israel na Palestina huru. Kwa muktadha huo Tanzania itaimarisha mahusiano na Israel, hususan katika mambo ya kiuchumi pamoja na kuendelea kutetea haki ya Taifa la Wapalestina kuwa huru.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Wapo askari polisi kadhaa ambao wamestaafu kwa zaidi ya miaka 20 sasa na wametumikia nchi kwa uadilifu na uzalendo, lakini hawajalipwa stahili zao; Serikali kwa mara ya mwisho iliwasiliana nao kupitia barua CAB/336/394/01/70 ya tarehe 28 Julai, 2015:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali haijawajibu barua yao zaidi ya miezi sita?
(b) Je, ni kwa nini suala hili halimalizwi kwa miaka yote ili wahusika wapate haki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wizari ya Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, (a) siyo kweli kwamba wastaafu hawa hawajajibiwa kwa zaidi ya miezi sita, bali kumbukumbu zinaonyesha kuwa Jeshi la Polisi limeshawaandikia barua ya kuwajibu askari hao tangu tarehe 12/10/2015 yenye kumbukumbu namba PHQ/C.10/8A/VOL.9/90.
Mheshimiwa Naibu Spika, (b) suala hili halina utata wowote kwani wastaafu hawa hawana wanachodai Jeshi la Polisi kwani haki zao walishalipwa kulingana na mikataba yao, kwani walikuwa chini ya mkataba wa bakishishi (gratuity) ambao ulikuwa ni uchaguzi wao.
MHE. ALLY SALEH ALLY Aliuliza:-
Tanzania imekuwa ikipeleka vikosi vya kulinda amani ndani ya Afrika na sehemu nyingine duniani kadri mahitaji na hali inavyoruhusu na kutimiza dhima ya duniani.
(a) Je, mazoezi kama haya yanaimarisha jina la Tanzania kiasi gani katika jukumu hili?
(b) Kama miaka kumi iliyopita Tanzania imepeleka vikosi maeneo gani na kwa misingi gani?
(c) Changamoto gani zinakuwepo katika kukusanya vikosi hivyo kabla havijapelekwa nje ya nchi kwa kzi kama hizo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na inatimiza wajibu wake wa kuzisaidia nchi zenye migogoro ili kuleta amani pale inapoombwa kufanya hivyo. Ushiriki wetu umetuletea heshima kubwa duniani kwa mara zote kuonesha utayari wetu wa kutoa msaada kwa ulinzi wa amani pamoja na kazi nzuri unayofanywa na jeshi letu katika kutekeleza jukumu hili.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka kumi iliyopita Tanzania imepeleka vikundi vya ulinzi wa amani katika maeneo yafuatayo;
(i) Lebanon, kombania mbili toka mwaka 2008;
(ii) Darfur, Sudan, kikosi kimoja toka mwaka 2009; na
(iii) DRC zaidi ya kikosi kimoja toka mwaka 2013.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizopo katika kukusanya vikundi kabla ya kupelekwa nje ya nchi kwenye majukumu ya ulinzi wa amani ni zifuatazo:-
(i) Gharama za kuvihudumia vikosi hivyo vikiwa kwenye mafunzo;
(ii) Gharama ya vifaa vya wanajeshi vitakavyotumika eneo la uwajibikaji; na
(iii) Ugumu wa kupata mafunzo ya uhalisia wa maeneo wanakokwenda kwa mfano jangwani, misituni na kadhalika.
MHE. JAMES F. MBATIA (K.n.y MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Bunge lilipitisha Mpango wa Maendeleo na katika utekelezaji wake kasi ya Serikali kukopa imekuwa kubwa na bila shaka matokeo yake ni kuongezeka kwa Deni la Taifa:-
(a) Je, Serikali inaweza kuliambia Bunge hili ni kiasi gani kimekopwa hadi sasa ndani na nje ya nchi?
(b) Je, Serikali inajipangaje kulipa deni hilo pamoja na deni ambalo tayari lipo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango wa Pili wa Maendeleo (2016/2017 – 2020/2021) ulipitishwa na Bunge lako Tukufu na kuidhinishwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli mwezi Juni, 2016. Serikali ilianza utekelezaji wa mpango huo mwezi Julai, 2017.
Katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji, Serikali ilitarajia kukopa jumla ya shilingi bilioni 9,653 kutoka katika soko la ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 5,374.30 zilitarajiwa kukopwa kutoka soko la ndani shilingi bilioni 2,177.8 mikopo yenye masharti nafuu na shilingi bilioni 2,101.0 ni mikopo ya masharti ya kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi 31, 2017, Serikali ilifanikiwa kukopa jumla ya shilingi bilioni 6,893.4 sawa na asilimia 71.4 ya lengo la kukopa shilingi bilioni 9,653.0. Kati ya kiasi hicho shilingi bilioni 4,715.6 zilikopwa kutoka soko la ndani na shilingi bilioni 2,177.8 ni mikopo nafuu kutoka nje. Aidha, hatukuweza kukopa kutoka katika chanzo cha masharti ya kibiashara katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na takwimu hizi napenda kulifahamisha Bunge lako tukufu kuwa, si kweli kwamba tangu tupitishe Mpango wa Maendeleo Juni, 2016 kasi ya kuongezeka kwa Deni la Taifa imekuwa kubwa. Hata hivyo, hatuwezi kupima kasi ya ongezeko la Deni la Taifa ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, madeni yote ya Serikali yakijumuisha mtaji pamoja na riba yanalipwa kupitia mfumo wa kawaida wa bajeti ya Serikali. Katika mwaka 2016/2017, Serikali ilitenga shilingi bilioni 4,866.3 kwa ajili ya kulipa mtaji na riba ya deni la ndani na shilingi bilioni 1,586.6 kwa ajili ya kulipa mtaji na riba ya deni la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi 31,2017, shilingi bilioni 3,657.74 zilitumika kulipa mtaji wa deni la ndani, shilingi bilioni 796.16 zilitumika kulipa riba ya deni la ndani, shilingi bilioni 766.02 zilitumika kulipa mtaji wa deni la nje na shilingi bilioni 436.56 zilitumika kulipa riba ya deni la nje. Hadi sasa Serikali inahudumia au kulipa deni lake (ndani na nje) kwa mujibu wa masharti ya mikopo husika na kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 7,830.0 kwa ajili ya kuhudumia deni la Serikali litakaloiva kati ya Julai, 2017 na Juni 2018. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 5,973.8 zimetengwa kwa ajili ya deni la ndani na shilingi bilioni 1,856.1 ni kwa ajili ya deni la nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuimarisha mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, kutafuta mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa uchumi wa Taifa letu na hivyo kuhakikisha kuwa Deni la Taifa linaendelea kuhudumiwa kwa wakati na kwa mujibu wa masharti, sheria, kanuni na taratibu za mikopo.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Tanzania imesajili michezo kadhaa ambayo huingia kwenye medani ya Taifa kiushindani lakini kote huwa ni mashamba yanayozaa visingizio.
(a) Je, Serikali haioni haja sasa ya kujipinda katika michezo michache kiushindani Kimataifa?
(b) Je, kama kukiwa na uamuzi huo inaweza kuwa michezo ipi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imesajili michezo mbalimbali kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Aidha, ili timu au mchezaji aweze kushiriki katika mashindano ya kimataifa kama vile michezo ya Olympic na michezo mingine, lazima awe amefikia viwango vilivyowekwa na mashirikisho ya kimataifa. Serikali inatoa mwanya kuibua na kukuzwa kwa vipaji katika michezo mbalimbali bila upendeleo. Suala la kufanya vizuri katika mashindano linategemeana na viwango vya uelewa, mazoezi, mafunzo na uzoefu katika mchezo husika.
Aidha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali inatoa msaada wa hali na mali kufanikisha timu ama mchezaji aliyefikia viwango kushiriki michezo ya Kimataifa ikiwa taarifa na taratibu zinazingatiwa tangu ngazi za awali. Kitendo cha kuchagua michezo kadhaa kinaweza kupelekea kupoteza vipaji ambavyo havijavumbuliwa na kukuzwa kufikia kushiriki mashindano kitaifa na kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo Serikali itaendelea kuhamasisha michezo yote kupitia vyama vya michezo kwa sababu kila mchezo unaweza kushiriki kiushindani. Hii inasaidia kutoa fursa kwa wanamichezo wenye vipaji tofauti kuweza kushiriki katika michezo ya kimataifa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya Mheshimiwa Mbunge ni mazuri kwa maana ya kujikita katika michezo ile ambayo tunadhani itaweza kusaidia Taifa kufanya vizuri katika ushindani kimataifa, hili litawezekana kwa kusaidia timu ama mchezaji aliyefuzu, kwani katika hali halisi huwezi kuamua kuwa huu ndio mchezo unaoweza kufanya vizuri bila kupata viwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, niseme kuwa kwa sasa bado utaratibu huu hatujaanza kuutumia na kwa hiyo sio rahisi kujua ni michezo gani kwani kila mchezo unaandaliwa kwa kufuata taratibu na viwango husika na matokeo mazuri yanapatikana kwa kuibua na kukuza vipaji. Kwa kuchagua michezo kadhaa tutakatisha tamaa ukuaji wa vipaji katika michezo mingine. Lakini bado iko fursa kama wadau kufanya upembuzi wa kina na kuja na maoni juu ya michezo gani tuipatie kipaumbele kwa manufaa ya Taifa.(Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) yenye soko la watu milioni 200 na rasilimali lukuki katika mtawanyika wa nchi 15 wanachama, zikiwemo fursa kubwa za madini, petroli, gesi, ufundi, elimu na utalii.
(a) Je, Tanzania imefaidikaje na soko hili kwa kipindi cha miaka ya uanachama wake?
(b) Je, ni maeneo gani ya ushirikiano yameonekana zaidi kuwa na maslahi na Tanzania?
(c) Tanzania inapakana na majirani ikiwemo Zambia, Msumbiji, Congo DRC na Malawi. Je, tuna miradi au ushirikiano wa kiuchumi na nchi hizo kupitia SADC?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inajivunia kuwa moja ya nchi waanzilishi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo pamoja na mambo mengine imekuwa ikifaidika sana na fursa za masoko zinazotolewa na nchi 15 wanachama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha miaka 10, mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenye nchi za SADC yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani milioni 301 mwaka 2007 hadi Dola za Kimarekani bilioni 1,017 mwaka 2016. Bidhaa ambazo Tanzania imekuwa ikiuza kwa wingi katika Soko la SADC zinajumuisha madini mbalimbali yakiwemo Tanzanite na dhahabu, bidhaa za kilimo kama chai, pamba, kahawa, bidhaa za viwandani kama vile vifaa vya plastic, sigara, neti za mbu, vipuri vya magari na simenti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ambayo Tanzania ina maslahi nayo ni pamoja na maendeleo ya viwanda kwa lengo la uongezaji wa thamani katika mazao ya kilimo na madini, afya, usafirishaji, nishati, pamoja na ajira katika sekta mbalimbali. Maeneo haya yatachangia katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa kanda kutoka wastani wa 4% kwa sasa hadi 7%. Utaongeza mchango wa sekta ya viwanda katika uongezaji wa thamani ya Pato la Taifa kufikia 30% ifikapo mwaka 2030. Utaongeza uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na teknolojia ya kati na ya juu kutoka kiwango cha sasa ambacho ni chini ya 15% hadi kufikia 30% inapofika mwaka 2030 na kuongeza mchango wa mauzo nje ya bidhaa za viwandani hadi kufikia 50% kutoka wastani wa 20% hivi sasa ifikapo mwaka 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inanufaika pia na miradi ya ushirikiano inayoendelezwa katika nchi za SADC hususan miradi inayounganisha nchi jirani, kama vile mpango kabambe wa maendeleo ya miundombinu ya Kanda ya SADC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo ni pamoja na miradi ya maendeleo ya nishati ya umeme kama vile Mradi wa Zambia – Tanzania – Kenya wenye kilovoti 400 ambayo ni (400Kv Transmission Line) unaounganisha kutoka Tunduma, Makambako, Iringa, Singida – Arusha – Namanga, kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan; mradi wa vituo vya pamoja vya mipakani kati ya Tanzania na Zambia, Tunduma, Nakonde, mradi wa maendeleo ya maji na uendelezaji wa Bonde la Mto Songwe; mradi wa kuendelea Kanda ya Mtwara ambao unahusisha nchi za Tanzania, Msumbiji, Malawi na Zambia, ujenzi wa Daraja la Umoja kati ya Tanzania na Msumbiji, ujenzi wa reli na bandari, ujenzi wa vituo vya forodha kati ya Tanzania na Msumbiji, Zambia na Malawi na mradi wa maendeleo ya skimu ya umwagiliaji kwenye Bonde la Mto Ruhuhu, Bwawa la Kikonge.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Tanzania inaonekana kupanua uwanda wake wa kidiplomasia kwa kuanzisha Balozi mpya maeneo kadhaa, lakini pia kumekuwa na malalamiko ya makazi ya Wanabalozi wa nchi hii huko ughaibuni.
• Je, Serikali haioni haja ya kuwekeza katika eneo hili kwa kujenga ofisi ambazo pia zinaweza kuwa kibiashara?
• Kama hilo linafanyika, je, limefanyika wapi na wapi hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Wziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Tanzania imeendelea kufungua Balozi zake mpya katika nchi mbalimbli duniani ili kuimarisha mahusiano na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika nchi hizo. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya Balozi mpya sita zimefunguliwa katika nchi za Sudan, Algeria, Israel, Korea Kusini, Qatar na Uturuki.
Mheshimiwa Spika, halikadhalika Serikali inatambua umuhimu wa kuendelea kujenga majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini na imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa kutumia fedha za bajeti ya maendeleo zinazopangwa kwa kila kipindi cha mwaka wa fedha. Hadi hivi sasa Serikali inamiki jumla ya majengo 106 yalipo katika nchi mbalimbali ambayo yanatumika kama makazi ya watumishi na ofisi za Balozi zetu.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali inatambua kuwa na majengo ya vitega uchumi katika Balozi zetu ni muhimu ili kuwezesha kupatikana kwa fedha zitakazokuwa zikitumika kuziendesha Balozi hizo na hatimaye kuipunguzia mzigo Serikali. Kwa mfano, Serikali inamiliki majengo ya Ofisi ambayo pia yanatumika kama kitega uchumi katika Balozi zetu za Tanzania Maputo, Msumbiji; New York, Marekani na Paris, Ufaransa. Aidha, Serikali imeanza kushirikiana na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na taasisi za fedha zilizopo nchini kwa ajili kujenga majengo ya vitega uchumi katika viwanja vya Serikali vilivyopo Abuja, Nigeria na Lusaka, Zambia.
Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa Wizara ya miaka 15 wa ujenzi, ununuzi, ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini ulioanza kutekelezwa mnamo mwaka wa fedha 2002/2003, Wizara imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali kwenye Balozi zetu kama vile kufanikisha ujenzi wa jengo la ofisi ya Ubalozi New Delhi, India; ununuzi wa jengo la Ofisi ya Ubalozi Washington D.C, Marekani; ununuzi wa jengo la ofisi ya Ubalozi New York, Marekani; ununuzi wa jengo la ofisi ya makazi ya Balozi Paris, Ufaransa; ukarabati wa jengo la makazi ya Balozi Nairobi, Kenya; ukarabati wa makazi ya ya Balozi wa Tanzania Tokyo, Japan; na ukarabati wa jengo la ghorofa tisa la ofisi na makazi lililopo Ubalozi wa Tanzania Maputo, Msumbiji ambalo litatumika kama ofisi ya Ubalozi na kitega uchumi cha Serikali nchini humo.
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Wizara imeandaa mpango mwingine wa miaka 15 wa ujenzi, ununuzi, ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi ya watumishi Balozini ulioanza kutekelezwa mwaka huu wa fedha 2017/2018. Baadhi ya miradi inayotekelezwa ni ukarabati wa jengo la ofisi na makazi ya watumishi kwenye Balozi za Tanzania Harare, Zimbabwe; Kampala, Uganda; Beijing, China; Pretoria, Afrika Kusini; Cairo, Misri; ukarabati wa nyumba za Ubalozi wa Tanzania Lilongwe, Malawi; Kinshasa, DRC; ukarabati wa jengo la zamani la ofisi ya Ubalozi lilipo Washington DC; ujenzi wa makazi ya Balozi wa Tanzania Addis Ababa, Ethiopia na ujenzi wa ofisi ya Ubalozi wa Tanzania Muscat, Oman.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. ALLY SALEH ALLY) aliuliza:-
Utaratibu wa kutunga Sheria wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unahusisha maslahi ya nchi zote tano wanachama wa EAC kuelekea fungamano la kiuchumi na siasa.
(i) Je, hadi sasa ni sheria ngapi zimeshatungwa na kwa mgao wa maeneo yapi?
(ii) Je, hatua gani huchukuliwa unapotokea mgongano baina ya sheria ya ndani na ile ya Jumuiya?
(iii) Je, kuna utaratibu gani wa kutoa elimu ya umma kuhusu Sheria za Jumuiya?
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwa Bunge la Afrika Mashariki mwezi Novemba, 2001 hadi hivi sasa jumla ya sheria 78 zimeshatungwa. Kati ya hizo, sheria 20 zimesharidhiwa na Wakuu wa Nchi na Wanachama na nyingine zipo katika hatua mbalimbali za kusainiwa na kuridhiwa. Sheria zilizotungwa zimelenga katika kuimarisha biashara, kukuza uchumi baina ya nchi wanachama na Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuwezesha taasisi na vyombo vya jumuiya kutekeleza majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya sheria hizi ni Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004, Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kusimamia Uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiushuru ya mwaka 2017, Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2013 na Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Uanzishwaji wa Vituo vya Utoaji Huduma kwa Pamoja Mipakani ya mwaka 2013.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 8(4) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sheria za Jumuiya zina nguvu kuliko za nchi wanachama. Hivyo basi, ikitokea mkingano baina ya Sheria za Jumuiya na zile za nchi wanachama, nchi wanachama hazina budi kuzifanyia marekebisho sheria hizo ili ziendane na Sheria za Jumuiya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Tanzania sheria mbalimbali za kodi zilifanyiwa marekebisho, ili ziendane na utekelezaji wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi wa Forodha ya mwaka 2004 ambayo ndiyo sheria inayotumika kwa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, ili kuendana na makubaliano yaliyofikiwa katika Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Tanzania imefanya marekebisho katika Sheria ya Masoko na Mitaji na Dhamana, Sura ya 79; Sheria ya Kubadilisha Fedha za Kigeni Sura ya 271; pamoja na Kutunga Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Nchini Na. 1 ya mwaka 2015. Vilevile Serikali inaendelea na mapitio ya sheria mbalimbali ili kuainisha na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zinazotokana na mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa ni pamoja na kuwapatia uelewa wa sheria zilizopitishwa na Bunge la Afrika ya Mashariki. Elimu hii hutolewa kupitia vyombo vya habari, tovuti ya Wizara, makongamano, vikao vya wadau, warsha, blog za kijamii na mitandao ya kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalani mwezi Julai Wizara iliratibu kampeni ya kuhamasisha vijana wa Kitanzania kutumia fursa za biashara zitokanazo na mtangamano wa Afrika Mashariki iliyojulikana kama Chungulia Fursa, iliyolenga kuwahamasisha vijana kufanya biashara za kuvuka mipaka ya Tanzania iliyofanyika katika mikoa ya Dodoma, Mwanza, Manyara na Arusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ilitoa elimu ya faida na fursa za mtangamano kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Wajumbe wa Baraza la Vijana wa Zanzibar. Mafunzo hayo yalifanyika mwezi Machi, 2018 na yaliongozwa na kaulimbiu iliyosema Vijana na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-
Mchezo wa chess au sataranji unakuza akili, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi na ni mzuri sana kwa vijana ambao wanakulia na kuingia hasa katika masomo ya sayansi na ufundi.
(a) Je, mchezo huo umejikita kiasi gani hapa nchini hadi sasa?
(b) Je, kunaweza kuwa na mipango ya kufanya juu ya mchezo huo kuwa wa lazima na sehemu ya mtaala kwa kuiga hasa nchi za Ulaya ya Mashariki?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Ally Saleh Ally kama ilivyo kwa michezo mingine, mchezo wa chess au saratanji unakuza akili, hilo tunakubali, uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Hata hivyo, mchezo huu bado haujaenea sana hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa michezo ikiwemo mchezo wa chess inaimarika nchini. Wizara, kupitia Baraza la Michezo la Taifa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo - Malya kwa kushirikiana na wadau wa mchezo huu itaangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa lengo la kuueneza mchezo huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali itaendelea kuhamasisha wananchi katika maeneo mbalimbali kushiriki katika mchezo huu kama inavyofanya katika michezo mingine ili kuueneza mchezo huu kwa manufaa ya jamii kwa ujumla, kwani tayari umeshasajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa sasa Serikali haina mpango wa kuufanya mchezo huu kuwa wa lazima kufundishwa kwenye shule kwa kuuingiza kwenye mitaala yetu. Pia suala la kuingiza mchezo kuwa sehemu ya mtaala linahusisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara mbalimbali na hasa baada ya kujiridhisha kwa kufanya tafiti za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali, Waheshimiwa Wabunge na wadau wote wa Sekta ya Michezo waendelee kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kuwa michezo, ikiwemo mchezo wa chess inasonga mbele. (Makofi)
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-

Chuo cha Diplomasia kimekuwa na umuhimu mkubwa katika masuala ya kidiplomasia na uwakilishi wa Tanzania nje ya nchi.

(a) Je, Chuo cha Diplomasia kimetoa wahitimu wangapi na mgawanyiko wake ukoje hadi sasa?

(b) Je, wahitimu wangapi hadi sasa wamepanda na kuwa Career Diplomats?

(c) Diplomasia inaenda sambamba na mawasiliano, je, Serikali haijafikiria kuongeza lugha zinazofundishwa chuoni hapo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali namba 118 kutoka kwa Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Chuo cha Diplomasia mwaka 1978 hadi hivi sasa, chuo kimetoa jumla ya wahitimu 3,421, kati ya hao, wahitimu katika ngazi za Shahada ni 72, Stashahada ya Udhamili katika Menejementi ya Uhusiano wa Kimataifa ni 503, Stashahada ya Udhamili katika Diplomasi ya Uchumi ni 341, Shahada ya kawaida ni 2,084, ngazi ya Cheti ni 347 na wahitimu 74 ni wa Mafunzo Maalumu ya Maafisa Waandamizi wa Mambo ya Nje.

Mheshimiwa Spika, katika idadi hiyo ya wahitimu wa Chuo cha Diplomasia, wanawake ni 1,060 na wanaume ni 2,361. Wanafunzi hao walitoka nchi za Afrika Kusini, Algeria, Angola, Botswana, Burundi, Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Guinea, Kenya, Komoro, Libya, Malawi, Msumbiji, Namibia, Palestina, Rwanda, Sudan, Zambia, Zimbabwe pamoja na hapa kwetu Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa chuo hiki mwaka 1978, zaidi ya wahitimu 500 kutoka Tanzania wameweza kuwa Career Diplomats na kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, chuo kinatambua umuhimu wa lugha katika nyanja za masuala ya mahusiano ya kimataifa na diplomasia. Chuo kimeongeza idadi ya lugha za kigeni zinazofundishwa, mpaka hivi sasa chuo kinafundisha lugha saba (7) ambazo ni Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Kihispania, Kingereza, Kikorea na Kireno. Halikadhalika, chuo kimetayarisha mtaala wa kufundishia lugha ya Kiswahili kwa wananfunzi wa kigeni ili kueneza lugha hiyo kimataifa. Mafunzo hayo yataanza kutolewa kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-

Moja ya misingi mikuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ni utawala bora, haki za binadamu na demokrasia sambamba na kukuza uchumi za Nchi sita Wanachama:-

(a) Je, hilo linatimizwa kwa kiasi gani ndani ya Jumuiya na Wanachama?

(b) Je, kuna mfumo gani wa kukosoana ndani ya Jumuiya katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally, Mbunge wa Malindi, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 6 ya Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeainisha misingi mikuu ya kuzingatia ili kuiwezesha Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi Wanachama kufikia malengo yake. Katika kutekeleza matakwa ya Ibara hiyo, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimegawanya madaraka katika mihimili mitatu yaani Bunge, Mahakama na Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mihimili hii inajiendesha kwa kanuni na taratibu zake ambapo Wakuu wa Nchi kupitia Baraza la Mawaziri husimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo maelekezo na maamuzi ya Wakuu wa Nchi; Bunge limepewa mamlaka ya kuwakilisha wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutunga sheria, kusimamia utekelezaji wa miradi na programu za Jumuiya pamoja na kupitisha bajeti ya Jumuiya; na Mahakama ina mamlaka ya kutafsiri Sheria za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhamira hiyo ya kusimamia misingi mikuu ya Utawala Bora na Demokrasia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nchi Wanachama hupokezana Uenyekiti wa Jumuiya. Aidha, uendeshaji wa shughuli za Jumuiya hufuata vikao rasmi ambavyo ni shirikishi kuanzia ngazi ya Wataalam, Makatibu Wakuu, Baraza la Mawaziri na Wakuu wa Nchi, hivyo maamuzi yanayofikiwa ni yaliyokubalika na nchi zote sita (consensus). Mathalani, nchi hizo zimekubaliana kutuma waangalizi wa uchaguzi kwenye chaguzi kuu za nchi wanachama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Jumuiya ya Afrika Mashariki hutoa fursa kwa Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia kuwasilisha hoja na masuala mbalimbali ambayo hufanyiwa maamuzi kupitia vikao rasmi. Pia, wananchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Mabunge ya nchi zao hufanya uchaguzi wa Wabunge wanaowawakilisha nchi hizo katika Bunge la Afrika Mashariki. Halikadhalika, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ina mamlaka ya kusikiliza mashauri mbalimbali kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa ukosoaji katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanyika kupitia Bunge na Mahakama ya Afrika Mashariki. Bunge hilo limepewa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuandaa ripoti mbalimbali zinazowasilishwa na kujadiliwa ndani ya Bunge.

Hatua hii imewezesha Bunge hilo kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na Baraza la Mawaziri. Vilevile, kupitia Mahakama ya Afrika Mashariki wananchi hupeleka mashauri mbalimbali na Mahakama hiyo imeweza kufanya maamuzi ya kesi mbalimbali dhidi ya Serikali za nchi wanachama.
MHE. ALLY SALEH ALLY aliuliza:-

Katika masuala ya Haki za binadamu Tanzania ina wajibu wa ndani na nje na kila wajibu unahitaji kuonekana wazi ili kujenga imani kwamba haki za Binadamu zinatekelezwa katika viwango vya Kisheria, Kikatiba na Kimataifa?

(a) Je, Serikali itatimiza vipi matakwa haya ya ndani na nje?

(b) Je, ni kiasi gani Serikali imekuwa ikijenga misingi ya usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa Haki za Binadamu ndani ya nchi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Saleh Ally (Malindi) lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria zetu za nchi, Mikataba ya Kimataifa na Kikanda, Serikali ina wajibu wa kuheshimu na kulinda haki za binadamu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza wajibu huo, ndani ya nchi, Serikali imeweka mfumo wa Kisheria na Kitaasisi ili kuhakikisha kuwa masuala ya haki ya za binadamu nchini yanalindwa, yanatekelezwa na kuheshimiwa ipasavyo. Kwa kufanya hivyo, Serikali ilianzisha Chombo mahsusi, kitakachosimamia masuala ya haki za binadamu nchini ambacho ni Tume ya haki za binadamu na Utawala Bora iliyoanzishwa kwa mujibu wa Katiba na imewekwa ikifuatilia utekelezaji wa misingi ya haki za binadamu na Utawala bora na kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha utekelezaji wa wajibu wake ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, ambazo zimeridhia Mikataba mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda, inayohusu haki za binadamu imekuwa ikijenga misingi ya usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa haki za binadamu ndani ya nchi kwa kutunga Sheria mbalimbali na kuanzisha Taasisi na mfumo inayosaidia utekelezaji wa misingi iliyowekwa kwa mkataba ya Kimataifa na Kikanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania, imekuwa ikiwasilisha taarifa zake kuhusu utekelezaji wa haki za binadamu nchini katika vyombo mbalimbali vya Kimataifa na Kikanda. Taarifa hizo hujadiliwa na mapendekezo ya kuboresha haki za binadamu nchini hupokelewa na kutekelezwa kwa kuzingatia Sheria za nchi, mila na desturi za Watanzania pia.