Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Haji Khatib Kai (5 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameweza kuniamsha salama siku ya leo nikiwa na afya tele na kuweza kutoa mchango wangu katika hoja iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ambayo Rais John Pombe Magufuli akilihutubia Bunge na kulifungua, aliwajengea wananchi wa kawaida matumaini makubwa kwa kule kusema kila alipokuwa akizungumza kwamba anawaomba wananchi na kuwataka wamuunge mkono kwa
kazi kubwa ambayo ataifanya ya kutumbua majipu ili nchi yetu iweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya game ilizunguka, majipu yaliyotumbuliwa yaliwagusa wananchi hawa kwa kuvunjiwa makazi yao, wananchi hawa wanyonge hawajui kwa kwenda hadi sasa, hawajui la kufanya na vilevile kusababisha maafa na kusababisha vifo
kwa watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niseme kwamba Mheshimiwa Rais amewatelekeza wananchi ambao alisisitiza kila alipokuwa akizungumza kwa kutaka wamuunge mkono na kwa kutaka wamwamini kwa kazi kubwa ambayo amekusudia kuifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie hali ya kisiasa Zanzibar. Wakati Rais John Pombe Magufuli siku ya tarehe 20/11/2015 akilifungua Bunge hili alimtanguliza Mungu mbele kwa kusema kwamba atautatua mgogoro wa Zanzibar kwa utulivu na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kusema kwamba baada ya yote hayo, Mheshimiwa Rais kumtanguliza Mungu mbele na wakati Mheshimiwa Rais akienda kwenye maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 2016 Mheshimiwa Rais alikwenda kutangaza
kurudia Uchaguzi wa Zanzibar. Nimeamua kusema hili kwa sababu kiongozi yeyote wa chini kiprotocol anapozungumza jambo mbele ya Kiongozi Mkuu, basi kauli ile inakuwa siyo ya kiongozi wa chini bali ni ya kiongozi wa juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar siku zote tumekuwa tukisikia kauli aina mbili ambazo zikitolewa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kauli zinazosema kwamba Serikali ya Mapinduzi haiwezi kutolewa kwa makaratasi, hatutoi, hatuitoi, hatuitoi labda wapindue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kauli ya pili ambayo imekuwa ikitolewa na Chama cha Mapinduzi inasema kwamba Serikali ya Mapinduzi haiwezi kutolewa kwa kura, hilo wasahau.
Masuala ya kujiuliza ni kwamba, kwa nini Zanzibar iendelee kufanya chaguzi ikiwemo hiyo ya marudio. La pili, milioni ngapi zinatumika kugharamia chaguzi ambazo majibu yake yanajulikana? Nini tija ya kufanya hivyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, chaguzi ngapi zimefanyika huko nyuma ambazo zimekuwa zikilalamikiwa lakini hazijawahi kurudiwa? Seuze chaguzi huu wa mwaka huu ambao matatizo yake yamekuwa madogo na yangeweza kushughuhulikiwa kwa gharama ndogo sana. Yote haya ya kulazimisha kurudia uchaguzi ni kwa sababu ya watu wachache kwa maslahi yao binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashindwa kuelewa ni kwa nini Serikali ya CCM na viongozi wa CCM hawawezi kujifunza kwa yanayotokea duniani kama vile Somalia, Afghanistan, Misri, Libya na kwingineko. Raia wa nchi hizi hawakutaka kufikia hapa walipo, lakini walisababishwa kufikia
hapo walipo na uongozi dhalimu wa nchi zao kama vile uongozi dhalimu wa CCM na viongozi wao ambao wamekusudia na wamepanga sasa kutupeleka ambako siko, kule Zanzibar.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM na viongozi wa CCM wamekuwa wakitudhulumu kule Zanzibar; mwaka 1995 walitudhulumu, mwaka 2000 walitudhulumu, mwaka 2010 walitudhulumu na mwaka 2015 wanapanga kutudhulumu!
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokuwa nakizungumza hapa ni hali ya kisiasa Zanzibar, kwa hivyo sioni sababu kusema kwamba kuzungumzia chaguzi zilizopita ili tujue nini tufanye.
Nilichokuwa nasema, Serikali hii ya CCM na viongozi wake ambao wamekuwa wakituonea, wakitudhulumu, siku zote haikubaliki. Serikali ya CCM na viongozi wake walitudhulumu 1995, wakatudhulumu 2000, wakatudhulumu 2005, wakatudhulumu 2010, na 2015 mmepanga kutudhulumu! Haikubaliki, inauma sana, Mheshimiwa Waziri mkuu inauma sana hii. (Makofi)
MHE. HAJI K. KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimalizie kwa kusema, endapo suala la Zanzibar halitapatiwa ufumbuzi wa haraka, nchi inakokwenda siko. Tumevumilia Wazanzibar vya kutosha vya kutosha na sasa mazungumzo yanakwenda, mazungumzo mnatudanganya, mnamdhalilisha kiongozi wetu, mnampeleka huku na kule, kumbe hamna nia njema na mazungumzo.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, hili limeonekana kwamba linagusa hisia za watu…
MBUNGE FULANI: Wewe mbishi.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Basi niseme tu kwamba kwa hapo nilipofikia, nasema ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fikra za kuchangia kwa maandishi. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuteuliwa tena kuongoza Wizara hii muhimu ili aweze kutimiza azma yake kwenye sekta ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu napenda niuelekeze kwa Mheshimiwa Waziri na nitamtaka wakati wa kufanya majumuisho nipate majibu ya maswali yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, Bunge la mwaka 2010 akiwa Waziri wa Wizara hii alisimamia Kamati ya Ardhi, Maliasili kwenda nchini Uganda kujifunza ni namna gani Uganda wamefanikiwa katika sekta ya ardhi. Pia Kamati ilijifunza ni namna gani na muda gani wananchi wa Uganda wanapoanza mchakato wa kumiliki ardhi na jinsi zoezi hilo linavyokwenda haraka yaani si zaidi ya wiki moja mwananchi wa Uganda anakuwa amemiliki ardhi. Kamati ya Ardhi iliyopita nikiwa mmoja wa Wajumbe tulishauri Serikali kupitia Wizara hii kufanya jambo hili. Je, kwa sisi Tanzania na ili jambo hili liweze kupunguza kero na msongamano kwenye ofisi za ardhi limefikia wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati iliyopita ilienda nchini Dubai kujifunza kwenye Shirika lao la Nyumba. Kamati ilishauri Shirika la Nyumba lipewe mamlaka yake, lijitegemee na lijiendeshe. Je, suala hili hadi sasa limefikia wapi ili Shirika la Nyumba lifanye shughuli zake kwa ufanisi zaidi? Ahsante sana.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia, kwa kuniwezesha siku ya leo kuamka salama na afya tele na kuweza kusimama mahali hapa na mimi kuweza kutoa mchango wangu kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi ni muhimu kwa Taifa lolote duniani, kwani bila ya ulinzi ulio imara, Taifa haliwezi kuwa salama. Nianze ku-declare interest, kwanza mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Kati ya miradi ambayo Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ilikwenda kuyatembelea ni mradi wa ukarabati wa majengo na miundombinu. Mradi huu ulitengewa na Bunge likaidhinisha shilingi bilioni nane kamili, lakini hadi Februari, 2016 hakuna fedha yoyote iliyotolewa kwa ajili ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko na niaibu kubwa. Ni masikitiko kwa sababu Kamati tulipofika kwenye mradi huu, kwa kweli binafsi sisi Wajumbe wa Kamati tuliogopa hata kuingia hata katika majengo ambayo yalitarajiwa kufanyiwa ukarabati katika pesa ambazo ziliidhinishwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika miundombinu hiyo ambayo kuna mess ambayo wanajeshi hawa wanakuwa wanaitumia, kwa bahati mbaya sana wanajeshi hawa ni waungwana na ni waadilifu sana, lakini bahati mbaya sana mess hii inavuja. Ni aibu!
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine ambao tuliutembelea katika Kamati yetu ni mradi wa ulipaji wa fidia katika maeneo ambayo yalichukuliwa na Jeshi. Mradi huu ulitengewa na Bunge shilingi 7,390,000,000. Hadi kufikia mwezi Februari, 2016 fedha zilizopelekwa ni shilingi milioni 180, wananchi wa Tanzania walikuwa na imani na vyombo viwili vya nchi hii, moja likiwa ni Bunge na la pili likiwa ni Jeshi wa Wananchi wa Tanzania. Kwa bahati mbaya sana Watanzania kupitia chombo chao cha Bunge, wameshakata matumaini kwa sababu ya kukatishwa kuoneshwa matangazo ambayo waliona kwamba wanasaidiwa na wanatetewa na Bunge lao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa chombo cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kuwachonganisha na wananchi kwa kutopeleka fedha ambazo zilitegemewa kulipia fidia kwa maeneo ambayo yalichukuliwa na Jeshi, hii ni aibu, ni tatizo na mnasababisha kuwachonganisha wanajeshi ambao walikuwa na imani na wananchi, lakini leo imani hiyo itakuwa imetoweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie uchaguzi wa marudio Zanzibar. Ni mara kadhaa nimemsikia Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akisema kwamba Jeshi la Wananchi wa Tanzania halijapelekwa Zanzibar. Nasema hili siyo kweli, kwa sababu Mheshimiwa Waziri anasahau kwamba wanajeshi hao wanapokwenda Zanzibar hawapitii mbinguni. Wanajeshi hawa wanapokwenda Zanzibar wanapitia baharini, tunawaona wanavyokwenda, lakini pia tunawaona wanaporudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nadhani Mheshimiwa Waziri atafute maneno mengine ya kutuambia, lakini siyo kwamba Wanajeshi hawajapelekwa Zanzibar kwa madhumuni mamoja tu ya kisiasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri huyo huyo amekuwa akisema kwamba wanajeshi waliopelekwa Zanzibar au waliopo Zanzibar, kazi yao ni kulinda amani na usalama wananchi. Nasikitika kusema kwamba hivi wananchi wanapolindwa kwa usalama au Jeshi linapolinda usalama ni kuwatisha wananchi ambao wametulia? Hii haileti maana kwamba ni kuwasaidia na kuwalinda wananchi walioko Zanzibar. (Makofi)
Nasikitika kusema kwamba Makamu Mwenyekiti wangu wa Kamati namheshimu sana, lakini kwa bahati mbaya au bahati njema alisema kwamba watu wamekuwa wakisimama hapa wakizungumza kwamba Zanzibar kulipelekwa vifaru katika uchaguzi wa marudio.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwambie tu Mheshimiwa Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama, sawa hata kama vifaru hatuvijui, kwa sababu hatujaenda jeshini lakini tunaona. Kwa hiyo, suala la kusema kwamba watu hawajui, sawa hatujui, lakini tunaona. Kwa hiyo, tunapoona, tunajua hiki ni kirafu. Tumeona na tumeshuhudia wakati wa uchaguzi wa marudio, wanajeshi wakizunguka na vifaa vya kivita mpaka kwenye vijiji. Sasa tunaposema kwamba jeshi lilikuwa limeingilia shughuli za kisiasa Zanzibar, msituelewe vingine. Tunasema kwa jambo ambalo tumeliona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la malalamiko ambayo yapo kwa wanajeshi wa rank ya chini. Wanajeshi wa rank ya chini na ninaomba Mheshimiwa Waziri hapa atakapokuja atoe ufafanuzi, inawezekana hawafahamu lakini pia inawezekana kwamba hawajajua kwa sababu pengine wameingia juzi juzi au hawajakuwa wazoefu katika Jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanajeshi hawa wa rank ya chini wanasema kwamba kwa kawaida ration allowance inakuwa ni sawa kwa wanajeshi wote, lakini kwa bahati mbaya wamekuwa wakiona kwamba mwanajeshi wa rank ya chini kabisa amekuwa akilipwa shilingi 180,000, lakini kuanzia Koplo, nyota moja hadi nyota mbili wamekuwa wakilipwa kiwango kikubwa ambacho ni tofauti kabisa na difference inakuwa ni kubwa. Kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja alitolee ufafanuzi ili wale ambao pengine hawafahamu, waweze kufahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri tu kwa hili, ni vyema basi, ili kuondoa malalamiko na mambo ambayo yanaweza yakaleta tofauti kwa wanajeshi wetu, basi naomba labda itafutwe njia nyingine ya kuweza kuweka hii tofauti ambayo inaonekana ni kubwa kwa wale askari waliopo rank ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nimalizie kusema kwamba siyo jambo la busara na siyo jambo jema kwa Wizara kama ya Ulinzi na Usalama kwamba inapopangiwa bajeti ambayo itasaidia usalama wa nchi hii, vinginevyo leo bajeti inakuwa haipelekwi na inapelekwa ambavyo Bunge halikuidhinisha. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri usimamie hili, kwa sababu na wewe upo Serikalini upo kwenye Baraza la Mawaziri, utie lobbying yako ili uhakikishe kwamba Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kama ilivyopangwa ndivyo inavyopelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, nasema ahsante kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunirudishia dakika zangu tano kwa vile umetumia busara kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pale ambapo nilibakiza. Nilisema ili kumaliza matatizo ambayo wavuvi wetu wamekuwa wakiyapata kule nchini Kenya, basi ni vyema Serikali hizi mbili zikarudi kwenye mkataba ambao Serikali hizi mbili Mawaziri wetu wa Mambo ya Nje walikubaliana na kusaini. Kwa hiyo, ninao hapa naomba Watendaji wachukue ili wampatie Mheshimiwa Waziri ili jambo hili liweze kumalizika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, mimi nikiwa mmoja ambaye niliteuliwa kwenda nchini Afrika Kusini, Pretoria, tulipofika Ubalozi tulipatiwa taarifa ya majengo nane ambayo tulienda kuyakagua. Katika jengo moja ambalo tulilikagua na kupewa taarifa yake ni jengo ambalo linamilikiwa na SMZ yaani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jengo hili kunataka umakini mkubwa sana. Katika Serikali ya SMZ kuna chombo cha kutunga sheria kama vile Bunge la Jamhuri ya Muungano na katika Baraza la Wawakilishi ziko Kamati za Kisekta ambazo zimekuwa zikizungukia miradi na kuona miradi ambayo inamilikiwa na SMZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasiwasi wangu hapa ni kwamba Mheshimiwa Waziri atutoe wasiwasi hapa wakati wa ku-wind up: Je, kuna utaratibu wowote au kuna makubaliano yoyote ya jengo hili ambalo linamilikiwa na SMZ ambalo sasa hivi linataka kuingizwa katika Jamhuri ya Muungano? Je, endapo litakuwa hivyo, hakuna maneno yoyote? Hakuna malalamiko yoyote ambayo yanaweza kuleta shida huko mbele?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la pili ambalo tulienda kulikagua ni jengo la Tanzania House ambayo ni Ofisi ya Ubalozi. Jengo hili unapoliangalia katika sura ya mbele utaliona ni zima, lakini ukweli ni kwamba jengo hili limeshafanya crack au nyufa. Jengo hili utashangaa kwamba nyumba ya Balozi na Maofisa ziko vizuri, ziko salama, lakini unapokuja katika jengo la Ofisi ya Ubalozi maisha ya Maafisa Ubalozi wetu tunayaweka rehani. Tusiombe litokee tetemeko la aina yoyote. Endapo kutatokea tetemeko la aina yoyote, basi tunaweza kupoteza Maafisa Ubalozi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jengo ambalo linakaliwa na Afisa Ubalozi wetu ambaye anaitwa Rose Jairo. Jengo hili kwa bahati mbaya sana na hali halisi ya nchi ya Afrika ya Kusini na usalama wa nchi…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya muda wangu ambao haukutosha, nimeona nimalizie kwa maandishi. Ili kumaliza tatizo la wavuvi wetu na hata wengine kufikia kufungwa jela nchini Kenya, ni vema Serikali zetu mbili yaani Kenya na Tanzania zikarudi kwenye mkataba uliosainiwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje, nchi hizi mbili Tanzania na Kenya Desemba 17, 1975.


Mheshimiwa Mwenyekiti, copy ya Mkataba pamoja na kwamba nilikuambatanishia Mheshimiwa Waziri na barua niliyomwandikia hapa nilipo copy ninayo. Akiitaka nitampatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.