Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Haji Khatib Kai (4 total)

MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Tanzania ni mwenyeji mkubwa kati ya nchi zilizounda Umoja wa Afrika Mashariki, hivyo basi, hupelekea au hupaswa Watanzania kufaidika na soko la Afrika Mashariki:-
(a) Je, Serikali inawashauri nini wananchi wake wanapokwenda kibiashara kwenye nchi zinazounda umoja huo?
(b) Je, pindi wanapopata matatizo au vikwazo katika nchi husika ni wapi watapeleka malalamiko?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni, napenda kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimendoleana ushuru wa forodha mipakani, hatua ambayo inapanua soko la bidhaa za Tanzania kufikia Wanaafrika Mashariki takribani milioni 143 katika nchi tano Wanachama wa Jumuiya za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Hivyo ni dhahiri kuwa, endapo soko hilo litatumika kikamilifu litachangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Taifa na kupunguza umaskini wa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inawashauri wananchi kuzichangamkia fursa za kibiashara, ajira, uwekezaji na kadhalika zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kujiharakishia maendeleo.
Pili, Serikali inawashauri wananchi kuzitambua taratibu za kufuatwa katika kuzitumia fursa za kibiashara zilizopo katika Jumuiya kama nchi wanachama zilivyokubaliana ikiwa ni pamoja na kuwa na cheti kinachobainisha kuwa bidhaa imezalishwa ndani ya Jumuiya yaani cheti cha uasili wa bidhaa- EAC certificate of Origin na vibali/nyaraka kutoka mamlaka husika kutegemeana na aina ya bidhaa mfanyabiashara anazotaka kuuza au kununua.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa katika kufanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, vikwazo visivyo vya kiforodha hujitokeza kwa wafanyabiashara wetu kinyume na makubaliano ya nchi wanachama. Napenda kutoa rai kwa wafanyabiashara kuwasiliana na Wizara yangu pindi wanapopata matatizo au vikwazo vya kibiashara katika Jumuiya, Balozi zetu au Vyama vya Wafanyabiashara kama vile Tanzania Chamber of Commerce Industry and Agriculture (TCCIA), Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Tanzania Exporters Assosiation (TANEXA) na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Wizara imeweka mabango makubwa yani double sided billboards yenye ujumbe wa taratibu za kufuatwa na wafanyabiashara wadogo, wa kati, wa kuuza au kuagiza bidhaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mipaka ya Horohoro, Rusumo, Kabanga, Namanga, Sirari na Mtukula na vilevile imeweka Maafisa wake katika mipaka ya Rusumo, Mtukula, Namanga na Sirari kwa ajili ya kuwasaidia au kutatua changamoto za wananchi wanapofanya biashara na nchi wanachama.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuwahamasisha wananchi katika Majimbo yao kuzitumia fursa zitokanazo na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
MHE. ALLY SALEH ALLY (k.n.y. MHE. HAJI KHATIB KAI) aliuliza:- Arusha International Conference Center ni miongoni mwa taasisi ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya hiyo mwaka 1977, hivyo hii inaonyesha kwamba taasisi hiyo ina sura ya Muungano. Je, ni kwa nini taasisi hii haionyeshi ushiriki wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), kilianza shughuli zake rasmi tarehe 1 Julai, 1978 kufuatia kuvunjika kwa Jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1977. Kituo hicho kilianzishwa kwa kuzingatia Sheria mama ya Mashirika ya Umma ya mwaka 1969 kwa kupitia establishment order iliyotolewa kupitia notice ya Serikali Na. 115 ya tarehe 25 Agosti, 1978. Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hicho pamoja na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere vimemilikishwa kupitia Notisi ya Serikali Na. 84 ya tarehe 4 Aprili, 2014, ambapo vituo vyote vipo chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kituo kilianza shughuli zake kikiwa na madhumuni makubwa mawili ambayo ni kuendesha biashara ya mikutano na upangishaji wa nyumba na ofisi. Mheshimiwa Mwenyekiti, kimuundo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Wajumbe wa Bodi huteuliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa Zanzibar katika uendeshaji wa kituo kama taasisi ya Muungano, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki huwa wakati wote anamteua Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Zanzibar ili kuhakikisha ushiriki wao katika kituo hicho. Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo kinafanya kazi chini ya Bodi ya Wakurugenzi na shughuli za uendeshaji za kila siku zinasimamiwa na Mkurugenzi Mwendeshaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile pale inapotokea fursa ya ajira katika nafasi za utendaji, nafasi hutolewa kwa ushindani na hutangazwa kupitia magazetini ambapo pande zote mbili za muungano huchangamkia nafasi hizo na washindi hupatikana kulingana na uwezo wao katika nafasi walizoomba.
MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeimarisha kwa kuweka boti kwa ajili ya Police Marine maeneo mengi ya mito, maziwa na hata baharini ili kuzuia au kudhibiti ajali zinapotokea.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma hiyo katika Mikoa au Wilaya ambazo hazijapata huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, Mbunge wa Micheweni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa kupeleka huduma za boti kwa ajili ya Polisi Wanamaji ili kuzuia, kudhibiti ajali kwa awamu katika mikoa yote na Wilaya ambazo hazijapata huduma pale uwezo wa kibajeti utakapoimarika.
Aidha, muda huu ambapo Serikali inaendelea kutafuta fedha ili huduma hizo ziweze kupatikana, huduma hiyo ya Polisi Wanamaji itatolewa na vituo vya Wanamaji waliopo karibu kwa kufanya doria kwenye maeneo husika.
MHE. HAJI KHATIB KAI aliuliza:-
Serikali imeandaa utaratibu wa kuliwezesha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kufanya shughuli zake kwa kuwapatia posho mbalimbali ikiwemo ration allowance.
Je, ni lini Serikali itaongeza posho hiyo iendane na maisha yalivyo sasa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Haji Khatib Kai, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inao utaratibu wa kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kufanya shughuli zake kwa kuwapatia maafisa na askari posho za aina mbalimbali ikiwemo ration allowance. Serikali imekuwa ikiboresha maslahi na stahiki mbalimbali kwa maafisa na askari kwa kuzingatia hali ya maisha ya wakati husika na uwezo wa Serikali kifedha kumudu kulipa stahiki hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ration allowance inalipwa kwa maafisa na askari wote. Serikali ilipandisha kiwango cha posho ya chakula (ration allowance) kwa nyakati tofauti. Kwa mfano, mwaka 2011 ration allowance ilikuwa shilingi 7,500, mwaka 2014 ration allowance ilipanda kufikia shilingi 8,500 na mwaka 2015 ilipandishwa kufikia shilingi 10,000, kiasi ambacho kinaendelea kutolewa hadi hivi sasa. Kwa hivyo, Serikali itaendelea kuboresha posho ya chakula na posho nyinginezo kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.