Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Haji Khatib Kai (5 total)

MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kupata maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imeshauri wananchi kuzitambua na kuzitumia fursa za soko la Afrika Mashariki na kwa kuwa Serikali na Wizara husika, ina wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi wa Tanzania kuhusiana na soko la Pamoja la Afrika Mashariki. Ni kwa nini na ni lini Serikali au Wizara husika itatoa elimu kwa wananchi wa Kaskazini Pemba hasa Jimbo langu la Micheweni ili waepukane na tabu ambazo wamekuwa wakizipata kila mara?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema, endapo matatizo yatatokea au vikwazo vitatokea wananchi wawasiliane na Wizara yake au Balozi zetu. Binafsi wananchi hawa au Watanzania hawa wapatao 130 wanaotoka Jimbo langu na Majimbo mengine, waliposhikwa nchini Kenya waliwasiliana na mimi na mimi nikawasiliana na Balozi zetu zote mbili Nairobi na Mombasa kwa ajili ya msaada, msaada ambao ulishindikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifuata utaratibu wa kwenda Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje kwa msaada zaidi na nilikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara na tulikubaliana kilichofanyika si sahihi. Kwa bahati mbaya, naomba kumwuliza swali Mheshimiwa Waziri, hadi sasa sijapata mrejesho wowote, je, atakubaliana nami kwamba Watanzania hawa ambao hawakupata msaada si ni wazi kwamba, kutokana na itikadi yao ya kisiasa ndilo jambo ambalo lilipelekea kushindwa kupatikana msaada wowote? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi. Ningependa nimjibu Mheshimiwa Kai, Mbunge wa Micheweni maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pengine kwa upande wa Tanzania nimekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki kwa mwaka mzima. Hili suala analolieleza hapa ndiyo nalisikia kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, ningeomba tu Mheshimiwa Mbunge hilo analolisema ni kitu kizito sana, itabidi tukae chini na Wizara husika tuweze kuelewa kilitokea kitu gani hata kama alikwenda Ubalozi wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi, naomba kutoa wito kwa wananchi wa Tanzania wanaofanya biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, ukipata matatizo kama Naibu Waziri alivyosema kwenye jibu la swali la msingi, hakikisha unakwenda Ubalozi, ukishindwa nenda Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, ukishindwa nenda TCCIA (Tanzania Chamber of Commerce and Industrial and Agriculture), ukishindwa nenda Tanzania Exporters Association (TEA).
Kwa hiyo, taasisi zote hizi zitakusikiliza lakini hakikisha Wizara inapata taarifa kwa sababu tuna miundombinu tayari ya kulalamika.Wenzetu wanajua sana kulalamika, Watanzania tunalalamika chini kwa chini.
La pili, lini tutatoa elimu kwenye Jimbo lake? Elimu tunatoa kuanzia hii Wizara ilipoanzishwa, tunatoa kupitia vipindi vya redio, television, pamphlets, kupitia mikutano, hatuwezi kufanya specifically kwa Jimbo moja, lakini naomba niwahakikishie Watanzania kwamba biashara Afrika Mashariki sasa hivi imeongezeka kwa kasi na Watanzania tunachangia kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito tu kwa wafanyabiashara wa Kitanzania, tutumie hii fursa ya kupeleka bidhaa katika nchi za Afrika Mashariki kwenye bei nzuri, hulipi chochote kwa bidhaa zote ambazo zina uasilia wa Afrika Mashariki, unachotakiwa tu ni kupata hiyo certificate ya origin pale unapofika mpakani hasa kama bidhaa yako haizidi dola 2,000 na kwa wafanyabiashara wakubwa wao wanapata kutoka TCCIA.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumejengeka dhana ya askari wa KMKM kule Zanzibar kujiona wao peke yao ndio wenye haki ya kufanya doria baharini, jambo ambalo hupelekea askari hawa ambao ni askari Marine ambao wamepata mafunzo maalum kujiona wametelekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi kwamba sasa ni wakati muafaka wa askari wa Police Marine - Pemba kupata boti ili aweze kufanya doria ya haraka ambayo itaweza kuokoa usalama kwa Pemba lakini kwa Watanzania kwa jumla? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wa Jimbo langu la Micheweni, raia wema na raia wenye kupenda amani idumu nchi hii wamewahi kushika boti za Kisomali zaidi ya mara mbili; na boti hizi zinapofanyiwa upekuzi zimegundulika na maganda ya risasi.
Je, kwa kuwa askari wa Marine Pemba wanasema kila mwezi hutolewa mafuta lita 500 kwa ajili ya doria baharini, utakubaliana na mimi sasa kwamba ni vema Police Marine - Pemba kuwa na boti ya doria ili kuweza kuimarisha ulinzi wa baharini, lakini pia kuweza kunusuru usalama wa nchi hii na raia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge juu ya umuhimu wa Police Marine - Pemba Micheweni kuwa na boti yake. Ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilizungumza kwamba azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba Wilaya zote ambazo zinapaswa kuwa na boti, polisi wanapatiwa kadri hali ya kibajeti itakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo ndiyo azma ya Serikali na pale ambapo bajeti itakapokuwa inaruhusu, tutafanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na askari wa KMKM, Jeshi la Polisi kutokana na kutokuwa na vifaa vya kutosha ikiwemo uchache wa boti zilizomo katika maeneo mballimbali nchini, hufanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vingine vya usalama nchini ikiwemo Kikosi cha KMKM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme Mheshimiwa Mbunge ana bahati kwamba katika Wilaya yake ajue kwamba Jeshi la Polisi limekosa boti kwa wakati huu, lakini zipo boti za KMKM ambazo zinasaidiana na Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa pamoja kusimamia ulinzi katika upande wa bahari.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya ufafanuzi wa Mheshimiwa Waziri naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amekiri katika jibu la msingi kwamba askari wa jeshi sasa hivi wanalipwa posho ya shilingi 10,000 kwa siku hela ambayo kwa maisha ya sasa ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali itawaongezea askari hawa posho kutoka shilingi 10,000 angalau hadi 20,000 kwa siku?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jeshi letu la Tanzania limekuwa likipata sifa kitaifa na kimataifa kutokana na weledi na utendaji wake wa kazi, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba Jeshi hili halitoi malalamiko kwa posho wanazolipwa, hasa ukizingatia kazi wanazozifanya? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba posho zinaongezwa kadri ya uwezo wa Serikali unavyoruhusu. Katika hili nimetoa mifano, kwamba tulianzia na shilingi 5,000 ikapanda mpaka shilingi 7,500 ikapanda mpaka shilingi 8,500 sasa ni shilingi 10,000; kwa hiyo, tutaendelea kuzipandisha posho hii kwa kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la pili kuhusu malalamiko unayoyazungumzia; nataka nikueleze Mheshimiwa Mbunge ni kwamba kwa kiwango kikubwa posho zinazotolewa sasa kwa askari na maafisa wetu zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa. Mimi nataka nikuhakikishie kwamba wengi wanafurahia posho hizi zinazotolewa. Kama nilivyosema hakuna kinachotosha, mara zote kutakuwa kunaupungufu tu. Kwa hiyo, kwa kadri uwezo utavyoruhusu tutaendelea kuwa tunazi-review kila mwaka posho zote kuangalia uwezekano wa kuzipandisha kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri katika maelezo yake amekiri kwamba tatizo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara; na kwa kuwa katika maelezo yake amejiridhisha kwamba wavuvi kutoka Pemba wamekuwa wakivua katika mwambao wa Bahari ya Hindi upande wa Kenya kutoka mwaka 1960; na vilevile katika maelezo yake amejiridhisha kwamba mwaka 1976 Serikali ya Kenya na Tanzania ilifanya makubaliano juu ya wavuvi wa nchi hizi mbili:-
Je, ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi kukaa na Serikali ya Kenya kupitia mkataba ambao niliuwasilisha hapa Bungeni ili kulipatia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wavuvi hawa kabla hawajaenda kuvua katika bahari ya Kenya wamekuwa wakienda kukutana na Maofisa Uhamiaji, Fisheries pamoja na BMUs za sehemu ambazo wamekuwawakienda kuvua.
Je, ni kwa nini Serikali hii au ni kwa nini Serikali hii au Mheshimiwa Waziri asiwaambie wavuvi hawa leo ili wawe na matumaini kwamba tatizo hili litakuwa halijirudii tena mara kwa mara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema na kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, nimesema kwamba Serikali sasa imechukua hatua ya kuwasiliana na sekta husika ikiwemo Wizara za kisekta kwa maana ya upande wa Tanzania na upande wa Kenya na Balozi ikihusishwa ili kuweza kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto hiyo, siyo tu tunakaa, lakini pia katika kujadiliana ni pamoja na kupitia mkataba ule. Mkataba huu tunajua kwamba ulifanyika mwaka 1976 kabla ya kuvunjika kwa Umoja Jumuiya ya Afrika, kabla ya wa sasa hivi kuundwa upya. Ulikuwa ni wa zamani sana. Kwa hiyo, tumeona hii changamoto na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi kama Serikali tumesema tumeanza mazungumzo baina ya wadau wote wanaohusika ikiwemo Serikali ya Kenya, Tanzania kwa maana ya Wizara za Kisekta pamoja na Ubalozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba wavuvi hawa kabla hawajaenda kuvua katika upande ule wa Kenya huwa wanakutana na Maofisa Uhamiaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba wamekwenda kuwaona Maofisa Uhamiaji, nimesema kwenye jibu langu la msingi kwamba sisi kama Wizara na tukiwakilishwa na Ubalozi wetu, tunapokuta hawa wametendewa ndivyo sivyo, tunashughulikia jambo hilo. Ila tunawaasa wale ambao wanakwenda kule bila kutumia uratatibu wa kisheria; na ndiyo hao ambao kwa sehemu kubwa wanapata matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nawaasa kwamba sheria na kanuni zifuatwe kwa sababu suala la kushughulikia uvuvi, kwa maana ya uvunaji wa mazao ya uvuvi hasa samaki, ni masuala ambayo ni makubaliano kati ya nchi husika yaani nchi mbili Tanzania na Kenya. Na sisi tutaendelea kusimamia kuona haki inatendeka kama wavuvi wetu wamefuata utaratibu.
MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo masuala mawili ya nyongeza. Mkoa wa Kaskazini Pemba una Wilaya mbili za Kipolisi kwa maana ya Wilaya ya Wete na Wilaya ya Micheweni. Ma-OCD hawa walikaimu au wamekaimu zaidi ya miaka mitatu katika nafasi za OCD mwaka 2016 hadi mwaka 2019 na kwa OCD ya Wilaya ya Wete alikaimu nafasi hiyo hadi pale muda wake wa kustaafu ulipomfikia bila kupata maslahi yoyote ya cheo cha OCD. Mheshimiwa Naibu Waziri je, ni utaratibu gani wa Serikali kupitia Wizara yako inaweza ikafidia ma-OCD kama hawao kaimu bila kupata maslahi ya kazi hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa kukaimu nafasi ya OCD kuna changamoto za kiutendaji na si tu changamoto za kiutendaji hata changamotoza kimazingira. Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa kiasi kidogo sana cha mafuta kwa mwezi shilingi 1,000,000 jambo ambalo linamfanya OCD anayekaimu kutumia fedha zake za mfukoni kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani na unajua umuhimu wa mafuta kwa Polisi, umesimamiaje Serikali kuhakikisha kwamba inaongeza mafuta ili kuondoa tatizo la mafuta kwa Jeshi la Polisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimefarijika kuona Mheshimiwa Kai leo amekuwa mtetezi wa Askari wetu na hii inadhihirisha kwamba kumbe Askari wetu wanafanya kazi vizuri sana kule Pemba, wanashirikiana vizuri sana na Mheshimiwa Kai pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine ambao kwa Pemba tunajua asilimia kubwa Wabunge wanatoka Chama gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo nataka nimjibu kama ifuatavyo. Kwanza hakuna fidia katika kukaimu niseme tu labda nishee pamoja na yeye masikitiko yake kuhusu kukaimu kwa muda mrefu bila kupandishwa cheo. Maana kama amekaimu miaka mitatu maana anaiweza hiyo nafasi lakini nimthibitishie kwamba ili mtu aweze kupanda cheo kuna taratibu ambazo nimezieleza katika jibu la msingi. Na moja katika mambo ambayo yanapelekea vilevile kupandishwa cheo kwa Askari ni kutokana na kuwepo kwa hizo nafasi, sasa inawezekana kwa bahati mbaya katika kipindi hiki ambacho wanakaimu hakukuwepo na fursa za kuweza kupandishwa cheo kwa Askari wahusika. Na kama unavyojua kwamba mahitaji ya Askari ambao wanahitaji kupandishwa cheo ni wengi na wengi vilevile wana sifa, kwa hiyo nafasi ni chache lakini wenye sifa ni wengi na ndio maana tunapandisha kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na bajeti ya mafuta nimuhakikishie kwamba tutajitahidi kadri ya miaka inavyokwenda kulingana na hali ya ukuaji wa uchumi wetu kuongeza bajeti katika Jeshi la Polisi ikiwemo bajeti ya mafuta. Tunatambua kwamba bajeti ya mafuta katika maeneo mengi bado haikidhi lakini tutaendelea kuizidisha katika maeneo yote ikiwemo katika Wilaya ya Micheweni na Wilaya ya Wete ili hatimaye tuweze kuhakikisha kwamba Askari wetu wanafanya kazi zao vizuri na kwa ufanisi.