Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Ali Salim Khamis (1 total)

Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii kuweza kutoa mchango wangu. Kwanza nitangulie kwa kusema kwamba kutenda inatoka moyoni na haitoki mdomoni. Sasa nijikite katika huu Mpango na nimsaidie Kaka yangu hapa Waziri wa Fedha pengine inaweza ikasaidia ili kulivusha Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyoangalia katika kulinyanyua Shirika la Ndege la Air Tanzania, Waheshimiwa Wabunge Shirika la Air Tanzania ni Shirika la mwanzo Afrika Mashariki na nchi zote za Afrika Mashariki zinalitegemea shirika hili. Hatujui kilichosibu ni nini mpaka leo tumekuwa wa mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Shirika hili kufa, sijui hawa ambao walishiriki kulisababishia shirika hili kufa walichukuliwa hatua gani na mpaka leo hii inaonekana kwamba upo umuhimu wa kulihuisha shirika hili tena jambo ambalo mimi siamini kama tuna uwezo kwa sasa hivi kulihuisha Shirika la Ndege la Air Tanzania eti tu kwa sababu tutanunua ndege tatu siyo kweli. Ikiwa hakuna hatua ambazo tumezichukua wakati shirika limekufa, leo hii tuchukue hatua ya kulifufua shirika hili siamini mpaka sasa hivi na sijui kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha wataalam wako wamekushauri sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, ukiangalia leo Ethiopian Airline hawakukurupuka tu kuanzisha Shirika la Ndege, walitafuta wataalam ambao ni wazoefu wa kuanzisha Mashirika ya Ndege. Ukiangalia Emirates Air hawakuanzisha tu shirika kwa sababu walikuwa na pesa, lakini walitafuta wataalam ambao wana fani ya kuanzisha mashirika ya ndege, ndiyo maana leo wamefanikiwa. Leo tunakwenda katika ushindani wa kujenga shirika la ndege, majirani zetu Ethiopia ambao tumewasaidia siku nyingi mpaka mwaka jana wana ndege 76 na wame-order ndege mpya 46 ili kulihuisha shirika zikiwemo ndege za Air Bus.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui manufaa ya hizi ndege ambazo zitanunuliwa na Serikali zije ziwanufaishe wananchi, imani yangu kukuomba Mheshimiwa Waziri ungerudi tena ukafanya utafiti kabla ya fedha hizi za umma hazijapotea.
Leo ukiangalia shirika hili lina madeni chungu nzima, na ikumbukwe kwamba shirika hili ni Shirika la Tanzania, ikiwemo na Zanzibar, Zanzibar imechangia asilimia kubwa ya shirika hili na ukiangalia katika takwimu ndege ambazo zilikuwa zikimiliki shirika la Air Tanzania nyingi zimenunuliwa na Serikali ya Zanzibar, lakini matokeo yake fedha hizi zote zimepotea na hakuna hatua ambazo zimechukuliwa, sasa tusitegemee kwamba shirika hili litahuika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba fedha za wananchi zisitumike kununua ndege, watu wakafanya haraka kununua ndege, watafutwe wataalam ambao wanaweza kushauri ili kuanzisha shirika litakalokuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa shirika la Precision Air, tulitegemea kwamba lile shirika litakuwa ni Shirika la Tanzania japo kuwa la wazalendo, lakini matokeo yake lilipoanza kufanya kazi vizuri Kenya Airways wameanza kulimiliki hili shirika, asilimia 51 sasa hivi iko Kenya Airways badala ya Precision Air, matokeo yake ni nini? Hili shirika maana yake tena sasa haliendi kuwa Shirika la Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo namwomba Mheshimiwa Waziri ungetafuta watu ambao wana fani hii ya kuanzisha mashirika ya ndege ili zikitumika fedha za umma, zitumike kwa mantiki ambayo imekusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niongelee katika masuala ya utalii. Mheshimiwa Waziri umetuletea kitabu chako hiki cha Mpango. Ukija kwenye ukurasa huu wa 14, unaelezea suala zima la utalii. Kutoka mwaka 2010 mpaka 2014, kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka 784,709 na mpaka mwaka 2014 tumepata watalii 1,142,217, maana yake ni ongezeko la watalii 357,508 kwa muda wa miaka minne. Kwa hiyo, ukigawa hii kwa ratio ya miaka minne maana yake Tanzania tunapata watalii 89,000 kwa wastani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tujiulize vivutio vya utalii tulivyonavyo, hivyo kweli sisi tulileta watalii 89,000 kwa mwaka mzima? Hii Wizara inafanya shughuli gani, Bodi ya Utalii inafanya kazi gani. Ikiwa leo hii inaonesha pato la nchi hapa lilivyoongezeka kupitia hawa watalii, 357,000 kutoka dola milioni 1,254,600 mpaka kufikia dola 2,006,000, ni tofauti ya dola 1,880,599, hili ni ongezeko la pesa za kigeni kwa watalii 357,000. Je, Mheshimiwa Waziri hukuliona hili, kwamba hili ni eneo ambalo lingeweza kusaidia nchi yetu kuweza kupata mapato zaidi na kuweza kwenda huko tunakotaka kujitegemea katika huo uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la bandari, Mheshimiwa Waziri bandari ndiyo uchumi nchi, Dubai, Hongkong wanafanya jeuri ya fedha kwa sababu ya bandari. Leo bandari zetu ukienda katika hii bandari ambayo unaambiwa inaimarishwa ya Dar es Salaam bado, bandari ambayo inaweka msongamano wa mizigo mpaka inakuwa watu kuchukua mizigo yao badala ya kwenda kufanya biashara wapate faida, sasa wanakula hasara kwa sababu ya mizigo inayorundikana katika bandari moja ya Dar es Salaam na kuchelewa kutoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia hiyo Reli ya Kati, imeanzia katika Bandari ya Tanga lakini Bandari ya Tanga haishughulikiwi imeachwa hivi tu na wala haimo katika Mpango. Bandari ndiyo shingo na roho ya uchumi wa nchi, leo inaachwa Bandari ya Tanga inakufa na Bandari ya Mtwara tunaenda kujenga Bandari ya Bagamoyo. Hivi tutegemee kweli huu uchumi wa viwanda utakua na wakati bandari ya Tanga ina miundombinu ya reli kutoka bandarini kwenda sehemu nyingine, leo tumeua kila kitu!
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sijui, napata mashaka kwamba kweli tunaweza kufanikiwa kwenda katika uchumi wa kati kupitia viwanda ambavyo tunategemea kwamba viwe mkombozi wa nchi hii. Nina imani kama kweli unajenga ile dhana ya kiuchumi, basi naomba ufahamu kwamba bandari ndiyo uti wa mgongo wa nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la uvuvi, miaka iliyopita michache tu, Mheshimiwa Rais wa sasa alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alikamata meli hapa, meli ile ilikamatwa ina samaki wa bahari watupu, baada ya kuwakamata hao watu na meli kukamatwa kupelekwa Mahakamani haikuonekana kwamba kuna umuhimu, kwa kuwa bahari yetu ina samaki wa kutosha, sasa tuwekeze katika uvuvi ili pato la nchi yetu liongezeke. Ndiyo maana nimetangulia kusema kwanza kwamba kutenda inatoka moyoni siyo kwa mdomo, sasa ikiwa hali hii tutakwenda nayo hivi, tutazungumza haya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nimesafiri nimepitia uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kulikuwa na mvua, uwanja wa International Airport unavuja, sijui kama Waziri mhusika kama ameenda kutembelea pale, nenda ushuke pale eneo la abiria mtu anashuka kwenye ndege ya Emirates au Etihad, ama Qatar eneo la kushukia abiria hakuna feni, hakuna air condition, watu wanatoka majasho sasa ni impression gani ambayo unampa mgeni anaingia ndani ya nchi yako, anakuona wewe ni mtu wa aina gani? Hii ndiyo taswira ambayo tunawapa watu wanaoingia hapa kwamba hawa watu wenyewe ni wa hovyo hovyo tu, kila kitu chao wameweka hovyo hovyo tu, lazima wewe atakudharau mwanzo tu anapofika akiona hali kama ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo International Airport inavuja, wageni wanafika pale airport, maana yake ingekuwa angalau kuna mafuriko, uwanja umejaa maji sawa, Lakini leo mvua ya kawaida tu uwanja unavuja! Sijui kama Waziri amewahi kwenda kwenye eneo la abiria wanaposhuka kwenye uwanja wa ndege, kutoka katika safari zao nchi za nje ili aende akashuhudie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.