Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yussuf Haji Khamis (5 total)

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 Serikali ilikamata Meli ya Uvuvi MFV TAWARIQ, nahodha wake Tsu Chin Tai pamoja na watu wengine 36 walishtakiwa Mahakama Kuu kwa kesi ya Jinai Na. 38 ya mwaka 2009. Kwa amri ya Mahakama samaki tani 296.3 wenye thamani ya sh. 2,074,000,000/= waligawiwa bure. Aidha, meli hiyo ilizama ikiwa inashikiliwa kama kielelezo. Tarehe 23 Februari, 2012 watuhumiwa wawili walihukumiwa kifungo na walikata rufaa Mahakama ya Rufaa ambapo tarehe 25 Machi, 2014 waliachiwa huru na sasa ni miaka saba tangu meli hiyo ikamatwe.
Je, Serikali itarudisha lini sh. 2,07,000,000/= ambazo ni thamani ya samaki na fedha ambazo ni thamani ya meli kwa Mawakili wa Nahodha wa Meli hiyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 8 Machi,
2009 kikosi kazi kilichokuwa kikifanya doria katika ukanda wa kiuchumi wa Bahari Kuu ya nchi yetu (Exclusive Economic Zone) katika Bahari ya Hindi kilifanikiwa kukamata meli ya uvuvi iitwayo Na. 68 BU YOUNG ikivua katika bahari yetu bila kibali. Meli hiyo ilikuwa ikiongozwa na nahodha aitwaye TSU CHIN TAI, raia wa Jamhuri ya Watu wa China na alikuwa pamoja na wenzake 36. Pamoja na kuwa jina la meli hiyo ni No. 68 BU YOUNG, meli hiyo ilikuwa inatumia pia jina la TAWARQ 1 na TAWARIQ 2 ili kuficha jina halisi na kuendeleza kufanya uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahodha wa meli hiyo, yaani
TSU CHIN TAI na wenzake walishtakiwa Mahakama Kuu katika kesi ya jinai Na. 38/2009 ambapo nahodha Tsu Chin Tai na ZHAO HANQUING aliyekuwa wakala wa meli hiyo, walitiwa hatiani. Wawili hawa waliomba rufaa Mahakama ya Rufani ambapo mwaka 2014 Mahakama hiyo ilibatilisha na kufuta mwenendo mzima wa kesi baada ya kubaini kuwa kulikuwa na kasoro katika taratibu za kuwafungulia mashtaka. Kwa ufupi, hawakuwahi kushinda kesi na Mahakama ya Rufani haikuwahi kutamka kuwa wako huru kwa sababu hawana hatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi wa Mashtaka alifungua mashtaka upya katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye kuondoa mashtaka dhidi yao tarehe 22/8/2014. Baada ya miaka miwili, yaani 2016 Wakili Captain Bendera alifanya maombi namba 108/2016 katika Mahakama Kuu akimwakilisha Bwana Said Ali Mohamed Al Araimi ambaye hakuwa mmoja kati ya washtakiwa katika kesi ya msingi akiomba apewe meli au USD 2,300,000.00 kama thamani ya meli hiyo na sh. 2,074,249,000/= kama thamani ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, ilikubaliana na hoja za Jamhuri na kutupilia mbali maombi hayo. Katika uamuzi wake, Mahakama ilitamka yafuatayo, naomba kunukuu: “this application was uncalled for, superfluous and amounts to abuse of court process, thus devoid of any merit.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala la kisheria na wahusika wanaweza kuendelea kulishughulikia kupitia Mahakamani.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-
Kituo cha Polisi cha Mkokotoni kiliungua mnamo tarehe 27/12/2010 na ujenzi wake ulianza mara moja.
Je, ni lini ujenzi huu utakamilika na kituo hicho kuendelea na shughuli zake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa kituo cha polisi cha Mkokotoni kilipata ajali ya moto mwaka 2010. Baada ya kuungua kwa kituo hichi, wananchi wa eneo husika waliendelea kupata huduma za kipolisi kupitia jingo lililokuwa pembeni na kituo kilichoungua moto. Serikali kupitia Jeshi la Polisi ilitafuta mkandarasi ambaye alianza kujenga upya kituo hicho na kwa sasa ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 80. Aidha, shughuli za Kituo cha Polisi cha Mkokotoni zitaanza katika jengo jipya baada ya kukamilika kwa ujenzi wake.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeongeza idadi ya Majimbo ya Uwakilishi kutoka 50 hadi 54, kabla ya ongezeko hilo Majimbo ya Uwakilishi na Ubunge yalikuwa sawa kwa ukubwa, mipaka na idadi ya wapiga kura. Ongezeko hili limefanya Majimbo mawili ya uwakilishi kufanywa Jimbo moja la Ubunge:-

Je, ni lini Tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya uhakiki wa Majimbo ya Ubunge Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepewa jukumu la kuchunguza mipaka ya kiutawala na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Majimbo ya Uchaguzi wa Ubunge. Kwa kuzingatia Ibara tajwa, Tume imepewa jukumu la kuchunguza na kugawa Majimbo ya Uchaguzi ya Ubunge mara kwa mara; na angalau kila baada ya miaka kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya uhakiki wa Majimbo ya Uchaguzi wa Ubunge mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Baada ya uhakiki, jumla ya Majimbo 26 yalianzishwa kutokana na maombi 77 yaliyowasilishwa Tume kutoka Halmashauri 37 na Majimbo ya Uchaguzi 40. Hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuhakiki tena Majimbo ya Uchaguzi wa Ubunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar baada ya kutangaza kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS Aliuliza:-

Kumekuwa na matukio ya watoto kuokota mabomu wakidhani ni vyuma chakavu na kisha kuwalipukia na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo. Hivi karibuni watoto watano wamepoteza maisha na zaidi ya watoto 40 kujeruhiwa katika Shule ya Msingi Kihanga iliyopo Ngara Mkoani Kagera.

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti na kukomesha tatizo hili?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi duniani yanakabiliwa na changamoto ya kutapakaa kwa kwa silaha ndogo ndogo yakiwemo mabomu ya kutupwa kwa mkono. Pamoja na Tanzania kuwa ni nchi yenye amani, baadhi ya nchi zinazotuzunguka zimejikuta zikitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hali hiyo imesababisha baadhi ya wakimbizi kukimbia na silaha yakiwemo mabomu ya kutupwa kwa mkono na kuyatekeleza baada ya kujiona wapo salama au kuwauzia wahalifu jambo ambalo limechangia kuwepo kwa mabomu hayo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya vita vya Kagera, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilitoa elimu kwa wananchi kutookota vitu vinavyong’ara, vifaa vya chuma na pindi wanapoona vitu hivyo watoe taarifa Vituo vya Polisi au kwenye Kambi za Jeshi iliyo karibu. Kwa maeneo yaliyotiliwa mashaka wananchi walipewa tahadhari ya kutolima, kutopita au kulisha mifugo. Aidha, Jeshi la Wananchi lilipeleka Wahandisi wa Medani kukagua maeneo hayo na kujiridhisha kama yapo salama kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za kawaida. Hivyo, inashauriwa wananchi katika mkoa huo na mingine kuendelea kuchukua tahadhari wanapoona vitu vyenye asili ya chuma.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-

Upimaji wa Afya za Wanamichezo ni jambo muhimu kwa ajili ya kulinda na kuhakikisha afya zao kabla ya kushiriki michezoni kwani kumekuwa na matokeo mbalimbali ya Wanamichezo kupoteza maisha wakiwa uwanjani. Mathalani, Ismael Mirisho wa Timu ya Mbao FC, Marc Vivien Foe wa Cameroon na Cheikh Tiote wa Ivory Coast:-

Je, Serikali kupitia Vyama vya Michezo vimeweka utaratibu gani kuhakikisha upimaji wa afya za wanamichezo ni jambo linalopewa kipaumbele?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri, wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia na kuwa na uelewa sahihi kuhusu umuhimu wa afya za wachezaji wetu wakiwa michezoni. Matukio ya wanamichezo kupata matatizo ya kiafya na hata wakati mwingine vifo kutokea uwanjani, yamekuwa yakitokea mara kwa mara Tanzania na imeshuhudiwa matukio kama hayo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ukweli huo, Wizara yangu kupitia kitengo chake cha Kinga na Tiba kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Michezo Nchini, imeendelea kutoa elimu ya afya kwa wanamichezo na Viongozi wa Mashirikisho ya Vyama vya Michezo kwa lengo la kuwawezesha kuelewa umuhimu wa huduma za afya kwa wanamichezo muda wote wawapo viwanjani kwa mazoezini au katika mashindano.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo huo, vilabu vyote vya soka vya ligi kuu ya Tanzania kwa mfano, vimeelekezwa kuwa na Daktari mwenye sifa na ambaye muda wote atakuwa tayari kutoa huduma ya matibabu kwa wachezaji.

Mheshimiwa Spika, Kitengo cha Kinga na Tiba cha Wizara, mbali ya kutoa elimu ya afya kwa wanamichezo pia kina jukumu la upimaji wa afya na kutoa Huduma ya Kwanza kwa wanamichezo kila wanaposhiriki michezo au mashindano mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, suala la huduma za afya kwa wanamichezo ni suala la kisera. Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995 sehemu ya 10.1 imeelekeza kuwa ni lazima mchezaji achunguzwe afya yake na kuwekewa kumbukumbu zote za kiafya kwa kipindi chote awapo kambini na ahudumiwe na Daktari kwenye taaluma ya tiba kwa wanamichezo.

Aidha, utaratibu wa matibabu kwa wanamichezo ujumuishe mafunzo juu ya athari za kutumia madawa ya kuongeza nguvu kwa wanamichezo. Wizara yangu inashauri na kuelekeza Vyama na Mashirikisho yote ya Michezo Nchini kuwa na utaratibu wa mara kwa mara wa kutoa elimu ya afya kwa wadau wake pamoja na kutoa elimu kinga kwa wanamichezo ili kulinda afya zao. Wizara yangu iko tayari kutoa ushirikiano katika jitihada hizo kwa kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuimarisha afya za wanamichezo.