Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Masoud Abdalla Salim (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-wa-ta‟ala amenijalia uzima na afya njema, nikapata nafasi au fursa ya kuchangia machache kwenye hotuba hizi mbili; hotuba ya Mheshimiwa George Boniface Simbachawene na Mheshimiwa Angellah Kairuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nataka nimkumbushe ndugu yangu Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, wakati akitoa maelezo kwamba Bunge lililopita tulipitisha sheria kwamba Bunge hili lisioneshwe live, watu waliokwambia walikudanganya. Siyo kweli, ulikuwa ni uongo wa mchana kweupe bila giza. Hakuna mahali iliyopita hata mara moja kwamba ilifika wakati sisi kuna taarifa hiyo ilipita, hilo la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nashukuru sana kwa mujibu wa kitabu cha Mheshimiwa George Boniface Simbachawene ukurasa wa 74, ameelezea mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ufuatiliwaji wa taarifa za fedha juu ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali; pili, Utawala Bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti...
KUHUSU UTARATIBU....
MWENYEKITI: Sawa. Mheshimiwa Masoud tuendelee, utatoa baadaye uthibitisho huo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kutokana na tabia hiyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo kwenye kitabu cha Mheshimiwa George, Waziri huyu ameelezea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna tatizo kubwa ukiangalia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; Serikali Kuu ukurasa wa 304 imeelezea kilio, deni ambalo Tanzania tunatakiwa tulipe la shilingi bilioni 90 juu ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kulipa kampuni ta China ya Wallys.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jipu la kwenye kichogo au kisogo, kwa maana nyingine jipu hili halionekani. ATCL iliingia mkataba na kampuni ya Sonangol kutoka China katika miaka iliyopita kwamba ingeleta ndege saba, tano zikiwa aina ya airbus na ndege mbili ndogo. Baadaye kampuni hii ya Kichina ya Sonangol ilimtaarifu kampuni mwenzake ya Wallys kwamba iweze kuleta ndege hapa Tanzania, lakini nini ambacho kilitokea? Ndege iliyofika ilikuwa moja tu aina ya airbus na ndani ya hapo ndege hiyo ilipofika hapa Tanzania ilikaa kwa muda wa miezi sita kwa sababu ndege hiyo ilikuwa ni mbovu. Baadaye hiyo ndege ikachukuliwa mkaipeleka Ufaransa; kufika Ufaransa ndege hiyo mpaka leo haijarudi. Ndege hiyo iko wapi Serikali? Mtuambie ndege hiyo mpaka leo iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi kufika Ufaransa ndege hiyo ilipakwa rangi nyingine kwa nchi ya Guinea na rangi tunaambiwa iliyopakwa hatuelewi kama ilikuwa ni ya kijani au manjano, hatuelewi. Baadaye mtatuambia; lakini ndege hiyo ilipakwa rangi nyingine na ndege hiyo mpaka leo haikurudi, lakini cha kujiuliza ni kitu gani? Ni kwa nini kulikuwa na uharaka mkubwa kupita kiasi katika mikataba hii? Ina maana tunadaiwa shilingi bilioni 90 hivi sasa. Hilo ni jipu kubwa, kwa nini mnalifumbia macho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaposema sisi upande huu wa pili tunaambiwa kwamba ninyi mnapinga hiyo ndiyo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 30, 2015 kwenye Serikali kuu ukurasa wa 304. Hilo ni jipu, tumbueni au ni upele hamwezi kuukuna. Wahusika wapo, Mheshimiwa Waziri Simbachawene kwa nini hadi leo walioko Hazina, walioko ATCL hakuna hata mmoja aliyeulizwa? Kwa nini? Tunaambiwa tulipe sisi shilingi bilioni 90.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hilo halitoshi, nenda kwenye ukurasa wa 282 ambapo inaelezea juu ya wizi, ubadhirifu na ufisadi mkubwa kabisa. Ripoti inaeleza kwenye Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma ambapo mwenyewe Mheshimiwa Waziri ndipo anapotoka, kuna ufisadi, wizi na ubadhirifu wa shilingi bilioni 912 kwa mambo yafuatayo; hilo ni jipu au ni upele au ni uvimbe? Mtasema wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, sikiliza kwa makini sana; kuna salio ya shilingi 571,498,633 la vifaa vya dawa, mafuta na vifaa vingine vinavyotumika mara kwa mara havikuingizwa kwenye taarifa za fedha; ufisadi wa kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wa pili, kuna mali zenye thamani ya shilingi 209,809,780 zilizidishwa kwa taarifa za fedha na hakuna marekebisho yaliyofanywa; ubadhirifu wa pili Mkoa wa Dodoma kwenye Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi, hapa hapa mchana kweupe.
La tatu, kuna matumizi yaliyolipwa zaidi kwa shilingi 131,049,085 kama madai ya mwaka 2014/2015 yameingizwa kwa malipo mengineyo; ufisadi mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaosema sisi tunapiga kelele, tunapinga kila kitu, hatupingi kila kitu, tuna ushahidi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, inaonesha kuna wizi, kuna ubadhirifu, ufisadi wa kutisha na hii ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sisi tukasemee wapi wakati Serikali ndiyo ninyi? Tutasema hapa hapa kweupe wala hatuvumilii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine haya yamekuwa ni mazoea. Mimi nikiwa Mbunge wa Bunge la Nane kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2005 jumla ya fedha ambazo zilisababishwa na wizi, ubadhirifu na ufisadi ilikuwa shilingi bilioni 4,403; watu waliopelekwa mahakamani ilikuwa ni 321; lakini cha kustaajabisha walipofika mahakamani waliambiwa kwamba wahusika hawa hawana kesi, wametoroka. Aliwatorosha nani? Walitoroka kwenye vyombo vya dola. Sasa hili ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2006 shilingi bilioni 2.3; mwaka 2007 shilingi bilioni 3.5; mwaka 2008 shilingi bilioni 3.1; mwaka 2009 shilingi bilioni 11.1; mwaka 2010 shilingi bilioni 12.9; wote huu ni ufisadi wa kutisha unaofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sisi tukayaseme wapi haya? Leo tunapoelezea mambo kama haya watu hawako serious, umakini wa Serikali uko wapi? Lazima tuyaseme haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala bora uko wapi? Tumekuwa tukisema mambo mengi ya msingi; leo hii ukiangalia manyanyaso ambayo yanatokea kwa watu wetu kule Tumbatu; na naomba nisome kwenye Ibara ya 13; “Watu wote ni sawa mbele ya sheria na wanayo haki bila ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.” Wananchi wa Tumbatu makosa yao ni nini? Unguja wamekuwa nyumba zao zikitiwa moto, hawana pa kushitaki. Lolote wanalolifanya wao kwao ni baya. Tatizo la Tumbatu ni kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ni lazima nao walindwe. Inakuwaje leo watu wetu hawa wa Tumbatu kila siku wananyanyaswa na baadhi ya watu ambao wanajulikana lakini hakuna hatua. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, fanya ziara yako uende Tumbatu. Hali hairidhishi. Hili ni jambo kubwa sana na nadhani Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani utalichukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tuje kwenye mafao. Ni mara kadhaa ambapo inaonekana kwamba mafao ya wastaafu wakati wa kupata haki zao wanapunjwa na hili ni tatizo kubwa. Sasa inakuwaje leo mnasema kwamba kwa mujibu wa ripoti iliyomaliza juzi mwaka 2015 kati ya majalada 1,683 wastaafu 200 wamepunjwa shilingi 385,304; je, hamjui kukokotoa? Angalieni ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ukurasa wa 99, kwa nini mwapunje na kwa nini msiwazidishie?
Mheshimiwa Kairuki, kwa nini msiwazidishie? Sasa huu ni ufisadi au siyo ufisadi? Mnawapunja, lakini watakapokufa wastaafu wale wengine ambao wana heshima zao mnakwenda pale na risala ya kutoa machozi ya uongo mtupu kweupe mchana, Marehemu alikuwa hodari, shupavu, jasiri mwaminifu na mtiifu; yeye atakumbukwa, atathaminiwa, mbona walipokuwa hai hamkuwathamini mliwapunja ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ufisadi wa kutisha ni wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kama hata wastaafu hamwathamini pia mnawapunja...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Masoud muda wako umeisha, naomba ukae.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwanza nataka Watanzania ambao wanatusikiliza waelewe kwamba sisi kama Kambi ya Upinzani tutaendelea kushikilia misimamo yetu dhidi ya ukandamizaji wa demokrasia na sisi tuko makini kweli kweli, hiyo ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wakati alipokuwa akitoa hotuba yake alisema miongoni mwa taasisi ambazo anaziongoza tatu ni APRM (African Peer Review Mechanism) mpango ni wa kujitathmini wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa huu mpango Tanzania inajitathmini yenyewe ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri atueleze, kwa sababu huu ni mpango wa utawala bora, huu mpango wa Bunge kutooneshwa live mmejitathmini kiasi gani? Mpango huu wa Bunge kutooneshwa live ni kiasi gani mmejitathmini ninyi wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, viongozi wetu kukatwa katwa mapanga na kupigwa na kuumizwa na wengine kuuawa kama kwa kamanda Alphonce Mawazo ambaye yeye ni Mwenyekiti wa Mkoa wa CHADEMA, kiasi gani mmejitathmini na nani waliohusika katika mpango huu wa utawala bora? Pia sambamba na hilo ningependa kuelewa kupigwa na kukatwa katwa na kuuawa kwa Diwani wetu kule Muleba, Faustine Mlinga, Kata ya Kimwani, kiasi gani mmejitathmini na kujua nini cha kufanya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuelewa kuvamiwa kwa viongozi mbalimbali wa dini kule Mwanza juzi na kupigwa. Je, katika mfumo huu wa utawala bora ni kiasi gani mmejitathmini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuuawa kwa vikongwe, walemavu, wale albinism, kiasi gani mpango huu wa kujitathmini wenyewe mmeweza kukaa kitako na mkaona njia gani mbadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya ili tuelewe sasa kiasi gani APRM, kwa sababu haina vote yake yenyewe hampewi fedha, kwa hivyo sasa ionekane kiasi gani katika kujitathmini ninyi wenyewe kama uwezo wenu ni mdogo, hamna fedha, mimi naishauri Serikali, APRM (African Pear Review Mechanism) ipewe vote yake yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna masikitiko makubwa, Watanzania ambao wanataka kwenda Uingereza viza zao zamani walikuwa wanazipata Kenya, sasa mpaka Afrika ya Kusini. Mheshimiwa Waziri, tuambie tatizo gani la figisu figisu baina ya Tanzania kutoaminiwa na Uingereza mpaka viza hizi kutoka sasa kwenda kutoa Kenya sasa unazipata Afrika ya Kusini, tatizo ni nini? Mna tatizo gani la kidiplomasia na hawa wenzetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni diplomasia ya kiuchumi. Nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri ingawa anaongea ongea pale, katika kuongeza kasi hii ya diplomasia ya kiuchumi baadhi ya nchi zimeweza ku-present credentials, kupeleka hati za utambulisho hapa kwetu, na sisi inaonekana bado kuna nchi mbalimbali hatujaweza kuwasilisha hati za utambulisho. Tanzania hapa Balozi wa Namibia na Botswana wako Tanzania lakini sisi Balozi wetu kule Botswana na Namibia naona kama sisi hatuna Balozi.
Lakini tarehe 05 Januari, 2016 kuna nchi tatu ambazo waliweza ku-present credentials hapa. Jamhuri ya Korea, Jumuiya ya Ulaya na Taifa la Palestina. Je, sisi tumejipanga vipi? Wakati wao tarehe tano walileta hiyo hati ya utambulisho kwa Rais John Pombe Magufuli, sisi je, kwa nchi ambazo nimezitaja. Jamhuri ya Watu wa Korea, Jumuiya ya Ulaya na Taifa la Palestina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba Mheshimiwa Waziri ukija unieleze, ni kwa nini sisi tunachelewa kuwasilisha hati za utambulisho? Mfano Balozi wetu pale Berlin, Ujerumani, nchi ambazo anaziwakilisha ni Ujerumani, Uswiss, Jamhuri ya Czechoslovakia, Poland, Hungary, Bulgaria, Romania, Australia na Vatican, lakini hati ambazo zimewasilishwa na Ujerumani, Uswiss, Austria na Vatican, nyingine zote mpaka leo hatujawasilisha hati za utambulisho, tatizo ni nini na hii ni diplomasia ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo Cairo, pale Misri Balozi wetu nchi ambazo anaziwakilisha ni Misri, Israel, Lebanon, Palestina, Libya, Iraq, Syria na Jordan. Lakini hati ambazo zimewasilishwa ni Misri peke yake, nyingine zote bado hatujawasilisha hati za utambulisho na hapa uchumi wetu utakuwa ukiendelea kudorora siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri, utakapokuja uniambie…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Masoud, dakika tano zako zimekwisha.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhana Wataala kwa kunijalia uzima na afya na kuniwezesha kuchangia taarifa hizi mbili muhimu, ile ya LAAC ambayo imetolewa na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale Mwiru, mtoto wa Kingunge, hongera sana kwa kazi nzuri na Mheshimiwa Kaboyoka, taarifa zao ni za kina kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za CAG ndizo ambazo wenzetu hawa wanazifanyia kazi. Taarifa zote hizi mbili ni nzuri, lakini tatizo la kutopatikana kwa fedha kwa viongozi wa Kamati hizi mbili kwenda katika maeneo mbalimbali kujionea uhalisia wa miradi ya maendeleo, kuangalia value for money, jinsi gani fedha zilivyotumika, limekuwa ni kubwa kweli. Kazi ambayo wameifanya Wenyeviti hawa wawili ni kubwa lakini kama hawapewi fedha za kwenda katika maeneo mbalimbali kuangilia uhalisia na kile kitu kinachoitwa value for money ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi nimpongeze Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, naye vilevile nimwonee huruma kidogo baada ya kumpongeza, kama alihitaji shilingi bilioni 62, Serikali imekwenda kumpa shilingi bilioni 18 atafanya kazi vipi? Huu ni upungufu mkubwa sana! Kila mtu aliyepewa dhamana na Serikali atengewe fedha ya kutosha ili atakapotoa mapendekezo yake basi yawe ni kweli. Kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaomba shilingi bilioni 62 anaenda kupewa shilingi bilioni 18 kuna jambo, tatizo kubwa. Kwa mara nyingine naishauri Serikali iandae mpango madhubuti, mpango makakati, ulio mzuri na mahsusi wa kuweza kutoa fedha hizi kwa wahusika hawa. Hiyo ili kuwa ni chombeza ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wachangiaji wenzetu waliopita walisema kwamba moja ya tatizo kubwa hapa ni Hazina kuchelewesha kutoa fedha za maendeleo katika Halmashauri au kutopeleka kabisa. Utekelezaji wa miradi ambayo tumepanga sisi Waheshimiwa Wabunge na ikumbukwe kwamba asilimia 70 ya fedha za maendeleo zinakwenda kwenye Halmashauri, kama Serikali haitaki kutoa fedha kwa wakati, inachelewesha au haitoi kabisa ina maana sisi Wabunge ni kama danganya toto tu. Tatizo ni nini kwa Serikali? Ni lazima Serikali ikumbuke kwamba sisi Wabunge tunapopiga kelele na kuandaa mazingira mazuri basi hizi fedha waweze kuzitoa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya upungufu mkubwa unaonekana ni suala zima la Wakurugenzi wengi katika Halmashuri kutokuwa na sifa na ndiyo maana miradi mingi ya maendeleo huwa inakwama. Wenyeviti wetu na Kamati kwa ujumla waliwaita baadhi ya Wakurugenzi kuja kutoa taarifa, unaona jinsi wanavyojikanyaga kanyaga, hawana sifa. Wakurugenzi hawa wanachukuliwa kwenye NGOs, ni vyema Wakurugenzi hawa watoke katika utumishi na wajulikane wana sifa fulani lakini wapi, tatizo nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati ya kuziboresha hizi Halmashauri zetu ni kwamba yale makusanyo ya ardhi ambapo fedha hizi zinakwenda moja kwa moja Serikalini inatakiwa asilimia 30 zirudi kwenye Halmashauri lakini hawapewi. Kwa hiyo, Halmashuri zinadhulumiwa, zinanyanyaswa, zimekuwa maskini na Serikali imekaa tu, tutafika kweli? Sijui. Niiombe sana Serikali iandae mpango mkakati na mzuri kabisa ili Halmashauri iweze kupata hizi asilimia 30 kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa katika lile la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye katika taarifa hizi ni jicho la kuona. Nitaanza na taarifa moja moja na naomba niende kwenye ukurasa wa 141 ambapo kuna ubadhirifu wa fedha ambao umefanywa. Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni, 2005 kuna suala zima la Kivuko cha Kigamboni ambacho kinatoka Kigamboni kwenda Dar es Salaam. Kivuko hicho kilifanyiwa majaribio ni kibovu na kwa mujibu wa ripoti kilinunuliwa kwa dola za Kimarekani 4,980,000 karibu shilingi bilioni 10 lakini hakikufanya kazi, ni tatizo kweli, ina maana hapa Serikali imeingia hasara wakati tuliambiwa kivuko hiki ni kizuri, ni bora lakini hapa pametokea matumizi mabaya ya fedha za umma.
Niishauri Serikali kwa kuwa aliyekuwa Waziri katika Wizara hii sasa ni Mtukufu mwenyewe wa heshima, kiongozi wetu, ni vema ashauriwe kwamba watu wote waliompelekea Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika mkataba huu mbovu wa shilingi karibu bilioni 10 kununua kivuko kibovu ambacho ni cha kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam na hakifanyi kazi, watu hawa Mheshimiwa Rais awatumbue. Yeye mwenyewe anawajua, yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais awatumbue watu hawa ambao walituingiza katika mkataba mbovu na Ujerumani kwa dola za Kimarekani 4,980,000 karibu shilingi bilioni 10 na kivuko hiki kikawa hakina sifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ikasema kwamba hati ya makabidhiano haikutolewa. Kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano jambo ambalo ni baya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote sifa ya kiwango cha kutembea ni tatizo. Ukiangalia kivuko cha Bakhresa kinatoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ambacho kimenunuliwa shilingi bilioni nne, kinatumia saa moja na nusu lakini kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam saa tatu. Ni vema kwa kuwa kiongozi mkuu yeye mwenyewe alikuwa ndiyo wakati huo ana dhamana mumshauri wale wote waliotuingiza katika mkataba huu awatumbue alfajiri mapema ili wananchi wapate imani nao, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la wastaafu. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko, ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimekuwa zikizungumzia jinsi gani wastaafu wanavyoonewa, wanavyopunjwa na wanavyodhulumiwa. Ukiangalia ripoti zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, nianze na inayoishia mwaka 2015, kati ya majalada 4,683 ya wastaafu yaliyokaguliwa majalada 200 yalipunjwa jumla ya shilingi milioni tatu themanini na tano laki tatu na mia nne themani na moja. Utetezi wa Serikali na kinachoonekana tatizo ni kukokotoa, mnakokotoa jambo gani jamani? Majalada 200 wastaafu wamepunjwa, wamedhulumiwa na ndiyo maana wakawa maskini. Wastaafu hawa wakishakufa risala nzuri na mnatoa machozi, machozi ya nini wakati mliwaonea alfajiri mapema? Roho mbaya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwaje leo ripoti inayoishia 2014, majalada 4,764 ya wastaafu yaliyokaguliwa majalada 283 yamepunjwa shilingi 481,456,311, jamani! Kila siku wakati wa kustaafu hawataki kuwatendea haki wastaafu. Wastaafu hawa na wao walikuwa ni wafanyakazi wetu, wameshastaafu jambo gani kubwa la msingi mnashindwa kukokotoa mkawapa haki zao. Kila siku ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaonya kwamba wakati wa kukokotoa basi Serikali iwe makini au hakuna wataalam? Jamani, aibu si aibu, ni shida kweli. Kila mmoja ni mstaafu mtarajiwa kuna Wabunge wastaafu na watu wengine mbalimbali, lakini wastaafu hawa ni vema kwa vyovyote iwavyo waangaliwe kwa jicho la huruma ni jinsi gani wanavyodhulimiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo lingine, nikuombe habari zifike kunakohusika, kwa sababu Serikali hapa ipo, inakuwaje sisi kila siku tunaingia kwenye mikataba mibovu? Tumeingia mkataba na Shirika la Ndege kipindi kile la South Africa na Shirika letu la Ndege la Tanzania (ATCL) tukakodi ndege (Airbus 320) na baadaye ndege hiyo ilikuwa ni mbovu, ikapelekwa Ufaransa kwa matengenezo, ikasuasua, ikaondolewa ikapelekwa Guinea, ikapakwa rangi, tumepata hasara ya shilingi bilioni 91 nani katumbuliwa? Mnatumbua maskini za Mungu waliokuwa hawana kitu, tumbueni hawa, hawa ndiyo wa kutumbuliwa. Wameiingizia hasara Serikali ya shilingi bilioni 91 mbona hawa hawatumbuliwi? Muwatumbue na hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anapotoa maelezo yake kwamba kuna wizi, ubadhirifu na ufisadi mkubwa kama huu, Serikali lazima mtilie maanani, muone kwamba hili jambo ni la msingi sana vinginevyo ni shida kweli! Hata ukichangia kiasi gani, Serikali inasema ni sikivu, inasikia kilio chetu lakini usikivu uko wapi? Sisi wengine tunapata shida kweli Serikali ukiishauri haikubali. Kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali lakini Serikali haikubali kusimamiwa ni shida na inavyoonekana Serikali haitaki kusimamiwa, wanataka watusimamie sisi tutakubali wapi, hatukubali. Tutachombeza hivi hivi kidogo kidogo kuna siku mambo yatawaingia vizuri muweze kutufanyia yale ya haki na hasa kwa wananchi. Haiwezekani shilingi bilioni 91 ziende, ndege mbovu, muiondoshe Ufaransa muipeleke Guinea muipake rangi, lakini hakuna aliyekamatwa, ni shida kweli, tutafika sisi kweli? Sijui, kwa sababu ameingia Trump inawezekana akatusaidia pengine anasikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, mimi sitaki nichombeze chombeze sana, naomba jicho hili la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mumpatie fedha aende katika maeneo mbalimbali. Haiwezekani anaomba shilingi bilioni 62 anapewa shilingi bilioni 18. Mheshimiwa Kaboyoka na Mheshimiwa Ngombale nao hawakupewa fedha za kutembelea maeneo mbalimbali kujionea wenyewe, value for money iko wapi, hamna kitu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe wao ripoti walitumiwa moja kwa moja kwenda site hakuna. Bunge ndiyo…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana nashukuru na naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kunipa nafasi ya kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Awali ya