Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Masoud Abdalla Salim (6 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Hali ya maisha ya wastaafu wetu ni mbaya sana na Serikali imeshindwa kuongeza pensheni zinazolingana na gharama halisi za maisha kwa sasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha pensheni za wastaafu hao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni kwa ajili ya kuwapunguzia wastaafu makali ya ongezeko la gharama za maisha. Ili kukabiliana na changamoto za ugumu wa maisha kwa wastaafu, Serikali imekuwa ikiongeza pensheni kwa wastaafu pale ambapo hali ya uchumi inaruhusu.
Kwa mfano, mwaka 2004 pensheni ilikuwa shilingi 21,606.05 ambayo iliongezwa hadi shilingi 50,114.43 kwa mwezi wa Julai, 2009 sawa na ongezeko la 132%. Mwezi Julai, 2015 Serikali imeongeza pensheni hadi kufikia Sh. 100,125.85 sawa na ongezeko la 100%.
Mheshimiwa Spika, pamoja na changamoto za kiuchumi zilizopo kuanzia mwaka 2004 hadi 2015 kiwango cha pensheni kimeongezeka mara tano na Serikali itaendelea kuboresha pensheni za wastaafu kwa kadiri uchumi wa nchi utakavyokuwa unaimarika.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:-
Kumekuwepo na malalamiko mengi ya walimu kulipwa mishahara midogo ambayo hailingani na gharama halisi za maisha:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha maslahi ya walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Jimbo la Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mshahara wa Watumishi wa Umma wakiwemo walimu hailingani na gharama halisi za maisha. Hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa nyongeza ya mishahara kila mwaka kwa kadri hali ya uchumi inavyoruhusu. Aidha, wakati wa kutoa nyongeza hiyo ya mishahara walimu hupewa nyongeza kubwa kuliko watumishi wengine wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2015/2016, mshahara wa walimu wenye cheti au astashahada uliongezeka kutoka shilingi 163,490/= hadi kufikia shilingi 419,000/= kwa mwezi ambayo ni sawa na asilimia 156.28.
Kwa upande wa mwalimu mwenye stashahada, mshahara uliongezeka kutoka shilingi 203,690/= hadi shilingi 530,000/= ambayo ni sawa na asilimia 160.20.
Kwa upande wa mwalimu mwenye shahada mshahara uliongezeka kutoka shilingi 323,900/= hadi kufikia shilingi 716,000/= sawa na asilimia 121.05.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inafanya tathmini ya kazi au job evaluation katika utumishi wa umma ili kubaini uzito wa kazi kwa watumishi wa umma wakiwemo walimu ili kupanga upya mishahara kwa kulingana na uzito wa kazi. Kazi hii imeanza mwezi Oktoba, 2015 na inatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 15 ijayo.
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM aliuliza:- Ajira iliyotarajiwa kuongezeka kutokana na ukuaji wa sekta ya viwanda haijafikiwa hasa baada ya viwanda vingi kubinafsishwa na kuachwa bila kuendelezwa:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu hili?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nia njema kabisa Serikali ilibinafsisha viwanda na mashirika ya umma ikiwa na matumaini kuwa sekta binafsi ingeliweza kuendesha taasisi hizo kwa faida na kulipa kodi kwa Serikali, kuzalisha bidhaa au huduma na kutoa ajira kwa wananchi. Pamoja na malengo hayo Serikali ililenga kuachana na shughuli za biashara ikielekeza nguvu zake katika shughuli zake za msingi za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Masoud, makampuni mengi yaliyobinafsishwa hayakufanya vizuri, ikiacha mfano wa makampuni machache yakiwemo Tanzania Breweries, Morogoro Polister ambayo inaitwa Twenty First Century na Tanzania Cigarette Company.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathimini inayoendeshwa na Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina juu ya viwanda, mashamba na mashirika ya Serikalil yaliyobinafsishwa kuanzia mwaka 1992 inadhihirisha ukweli tunaoujua kuwa wengi kati ya waliyopewa taasisi hizo hawakutekeleza mikataba ya mauziano kikamilifu. Hivyo tunawafuatilia kwa karibu wale wote waliopewa mashirika ya umma kwa utaratibu wa ubinafsishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuhakikisha makampuni yote haya yanazalisha kwa tija ili tupate bidhaa, kodi ya Serikali na ajira kwa wananchi wa Tanzania. Wale wote watakaobainika kukiuka makubaliano yaliyomo katika mikataba ya awali, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvitwaa viwanda au mashirika hayo na kutafuta Wawekezaji mahiri wa kuviendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutimiza adhma ya kutoa ajira kwa Watanzania, Wizara inafanya yafuatayo chini ya viwanda vidogo na vya kati unaoshirikisha SIDO na Halmashauri za Wilaya na Mikoa tunahamasisha shughuli za ujasiriamali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao na kilimo, uvuvi na ufugaji huku Mikoani.
Pia kupitia mamlaka zetu za EPZA, TIC na NDC tunakaribisha na kuwaongoza wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika shughuli za kutoa ajira zaidi. Serikali kupitia Wizara yetu inaboresha mazingira ya uwekezaji hali itakayowajenga imani wawekezaji na kupelekea kupanua shughuli zao zaidi za kibiashara kupitia njia hii ajira zaidi itaongezeka.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Moja ya majukumu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mujibu wa Ibara ya 130(c) ya Katiba ya nchi ni kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora:-
Je, ni kwa kiasi gani Tume imefanikiwa kutekeleza jukumu hilo kwa kipindi cha mwaka 2010 - 2016?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah Salim, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika majukumu yake kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 - 2016 ilipokea na kuyachunguza jumla ya malalamiko 13,709. Kati ya malalamiko hayo, malalamiko 6,169 yalihitimishwa na malalamiko 7,540 yanaendelea kuchunguzwa. Mchanganuo wa malalamiko ni kama ifuatavyo:-
(i) Migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wawekezaji, wakulima na wafugaji, wananchi wa maeneo ya hifadhi;
(ii) Matumizi mabaya ya madaraka kwa watendaji;
(iii) Ukatili dhidi ya wanawake na watoto;
(iv) Ucheleweshwaji wa haki kwa mahabusu na wafungwa; na
(v) Matumizi ya nguvu kwa vyombo vya dola.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na taarifa hiyo, katika kipindi cha mwaka 2010 - 2016 Tume ilifanya tafiti kuhusu haki za watoto, ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, kutembelea magereza na kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA (K.n.y. MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM) aliuliza:-
Kumekuwepo na ajali nyingi zinazosababisha vifo na majeruhi barabarani, baharini na kwenye maziwa.
Je, ni ajali ngapi zimetokea barabarani, baharini na kwenye maziwa kuanzia Januari, 2015 hadi sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdalla Salim, Mbunge wa Mtambile, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Kakunda Joseph, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha Januari, 2015 hadi Februari, 2016 jumla ya ajali zilizotokea ni 9,864 ambazo zimesababisha vifo 3,936 na majeruhi 9,868 katika Mikoa yote ya Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kama hicho jumla ya ajali 15 za baharini na kwenye maziwa zilizotokea, ambapo tisa zilitokea baharini na sita zilitokea katika maziwa. Katika ajali hizo, jumla ya watu 24 walipoteza maisha na watano walijeruhiwa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:-
Uvuvi ni miongoni mwa sekta inayochangia Pato la Taifa, lakini Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuboresha sekta hii wakati tukielekea katika Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuboresha sekta ya uvuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masoud Abdallah, Mbunge wa Mtambile, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kutengeneza zana za uvuvi. Hadi sasa jumla ya viwanda vitatu vya kutengeneza boti aina ya fibre glass na viwanda viwili vya kutengeneza nyavu vimeanzishwa. Aidha, viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi 48 vinavyojumuisha viwanda vikubwa 15 na vidogo 33 pamoja na maghala ya kuhifadhi mazao ya uvuvi 38 yameanzishwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Sambamba na hilo Serikali ikishirikiana na sekta binafsi inafanya juhudi ya kutafuta wawekezaji wa kujenga viwanda vya kuchakata samaki aina ya jodari katika huu Ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, hili likifanikiwa litawezesha wavuvi kuongeza thamani ya mazao ya samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imedhamiria kuongeza uzalishaji wa Samaki kupitia ufugaji wa samaki (aquaculture) kutoka metriki tani 10,000 mpaka metriki tani 50,000 ifikapo mwaka 2020. Aidha, Serikali ina dhamira ya kuanzisha vituo vipya vitatu na kuboresha vituo vingine 15 vya uzalishaji wa mbegu bora za samaki, kushirikisha sekta binafsi na taasisi za kitafiti katika kuboresha teknolojia na uzalishaji wa mbegu na chakula bora cha samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hatua zake za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu, Serikali imekamilisha mazungumzo kati yake na Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam ambapo gati namba sita litatumiwa na meli zinazovua katika ukanda wa uchumi wa bahari, ili kushusha samaki. Aidha, juhudi za ujenzi wa bandari ya uvuvi zinaendelea ambapo tayari mtaalam elekezi wa kufanya upembuzi yakinifu amepatikana.