Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Masoud Abdalla Salim (13 total)

MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni aibu na fedheha kwa Serikali kwa jinsi ilivyowatelekeza wastaafu wake. Ukiangalia nchi ya Kenya na Rwanda, wastaafu wana hali nzuri. Serikali mmepandisha pensheni kutoka shilingi 50,000/= mpaka shilingi 100,000/=, wastani wa shilingi 3,300/= kwa siku, fedha ambayo hata chai haitoshi! Serikali inasemaje sasa? Kuna mkakati wa ziada angalau kuwaongezea pensheni wastaafu kwa shilingi 250,000/= kwa mwezi? Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, la pili, kwa mujibu wa Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, miaka kadhaa, miaka mbalimbali, imekuwa ikiripoti kupunjwa, kudhulumiwa kwa mafao ya wastaafu na Serikali imekuwa ikisema kwamba wataalamu wake ndio wanaokosea. Tunataka tuelewe, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweza kutoa mafao stahiki kwa wastaafu wetu?
Pale ambapo wastaafu wanafariki, Serikali imekuwa ikitoa risala za kutoa machozi na kulia, uwongo mtupu! Tabia hii mbaya lini mtaacha? (Kicheko/Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba niseme, siyo sahihi kwamba imekuwa ni fedheha kwa Serikali. Kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya swali la msingi ni kwamba tumekuwa tukiongeza kiwango hiki cha pensheni kwa wastaafu kulingana na uchumi unavyoimarika na tumekuwa tukiliangalia kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati wa wazi wa kuongeza shilingi 250,000/= kwa mwezi kama pensheni; kama nilivyosema mwanzo, tunaangalia kiwango cha uchumi wetu, uchumi utakakaa vizuri kuturuhusu kulipa shilingi 250,000/= tutalipa hiyo shilingi 250,000/=.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mkakati wa kutoa mafao sahihi kwa wastaafu kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge katika swali lake la pili; naendelea kusisitiza kwamba uchumi utakapokuwa umeimarika vizuri; na kama mlivyoona kwa speed ya Serikali ya Awamu ya Tano, tunakusanya mapato kwa kiasi kikubwa na tunatarajia kuongeza tax base ya kukusanya kodi ambayo tunazingatia. Moja ya watu wa kuwaangalia ni Wastaafu wetu, wamelitumikia Taifa na tuna uhakika tutaweza kuwahudumia. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Katika azma ya kuboresha maslahi ya walimu, katika sherehe ya siku za walimu duniani katika awamu iliyopita, Rais mstaafu aliwaahidi walimu kuwapatia posho ya kufundishia yaani teaching allowance, lakini hadi leo posho ya kufundishia (teaching allowance) hawajapatiwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba ahadi ambayo aliitoa Rais inatekelezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kumekuwa na tabia ya kutolipa madeni ya walimu kwa wakati unaostahili na mara nyingi madeni ya walimu hulipwa hasa wakati wa kukaribia uchaguzi, hii ni tabia mbaya. Ni lini na Serikali ina mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba walimu wanalipwa madeni yao kwa wakati unaostahili? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na posho ya kufundishia niseme tu kwamba ni kweli kwamba Rais mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, wakati huo alipokwenda katika sherehe za walimu alielezea kwamba suala hili litafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba sisi kupitia Baraza Kuu la majadiliano katika utumishi wa umma tutaliangalia na kila mwaka tunakaa mara moja. Kwa hiyo, tusubiri tutakapokaa na vyama hivyo vya wafanyakazi katika Baraza hili Kuu la Majadiliano tuone tutasemaje. Tunaweza tukapanga viwango lakini tukajikuta vinakuwa ni viwango ambavyo Baraza Kuu kupitia Vyama vya Wafanyakazi wakawa hawajaviridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa madeni ya walimu, kwa upande wa Serikali inaweka mkazo mkubwa sana kuhakikisha kwamba walimu wanapata stahiki zao, lakini si kwa walimu tu na kwa watumishi wote mbalimbali wa umma. Ukiangalia katika mwaka huu peke yake, tumeshalipa takribani bilioni 3.7, lakini vilevile kwa mwaka jana tu peke yake tulilipa takribani shilingi bilioni 27.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya hivi sasa tunahakikisha tunakamilisha kulipa na kuhakiki, maana huwezi ukalipa tu. Wapo wengine vilevile wanafanya madai ambayo si ya kweli. Kwa hiyo, niseme tu kwamba sisi kama Serikali tupate nafasi tuendelee na uhakiki lakini wakati huo huo tukiendelea kulipa kwa kadri inavyowezekana. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na malalamiko mengi ya muda mrefu kwa wafanyakazi viwandani kupewa mishahara midogo lakini zaidi maneno ya kuudhi kwa wamiliki wa viwanda jambo ambalo halikubaliki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuunda Tume Teule ya kufuatilia malalamiko ya wafanyakazi hawa?
Swali la pili, katika jibu la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wale wote watakaobainika kukiuka makubaliano yaliyomo katika mikataba ya awali hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvitwaa na kutafuta wawekezaji mahiri wa kuviendeleza hivyo viwanda.
Kwa kuwa viwanda vya korosho vilivyobinafsishwa miaka 1970 na 1980 ambapo Serikali ilikopa kutoka Italia na Japan dola milioni 20 na viwanda hivyo hadi leo haviendelezwi wamiliki wake wanajulikana. Sasa tatizo nini kwa Serikali mnaelewa kila kitu tumekuwa tukisema muda mrefu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Je, nini mkakati wa ziada wa kuhakikisha kwamba viwanda vya korosho vimebinafsishwa kule Mtwara na Serikali mkatoa kwa vigogo wengine mnaowajua kwa bei chee! Je, viwanda hivyo ni lini vitarudi kwa wananchi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika viwanda kuna malalamiko na kama mnavyojua tunao ndugu zetu wanafanya kazi viwandani, sioni haja ya kuunda Tume, Wizara yetu ikishirikiana na Wizara ya Ajira tumeanza kazi ya kufuatilia masuala haya na Kamishna wa Kazi yuko ana kazi maalum ambapo tutahakikisha kwamba wafanyakazi wetu wanatendewa haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaeleze wawekezaji, sisi tunatengeneza viwanda kutengeneza ajira, kuzalisha bidhaa na kuwafanya mlipe kodi hatutengenezi viwanda kusudi waje kuteseka watu katika nchi yao, huo ndiyo msimamo wa Serikali na tunawahakikishia tushirikiane Waheshimiwa Wabunge, ninyi ndiyo macho yetu mtushauri na mtuelekeze. Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutoa viwanda, viwanda vile viliuzwa kisheria, nimeshasema mara tatu bei waliyolipa ni pamoja na masharti ya kuzalisha bidhaa kwa tija, kutoa ajira na kulipa kodi.
Kwa hiyo, kama ulimuuzia kisheria utamnyang’anya kisheria na niwahakikishie watu wanaotoka kwenye ukanda wa kulima korosho hakuna tatizo viwanda vitafanya kazi. Pamoja na hivyo wako wawekezaji wako tayari kuwekeza kwenye kutengeneza korosho, yaani korosho inatoka pale kiwandani inaingia mikononi mwa mteja tuna-add value, na tutatoka hapa tunakwenda kuuza Ulaya siyo tunatoka hapa tunauza India, India ipeleke Ulaya. Tunakwenda moja kwa moja sokoni na kazi hiyo naiweza tushirikiane. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Spika, na mimi nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri katika jibu la muuliza swali la msingi (b) alieleza kwamba yuko tayari kukarabati kituo cha polisi husika ambacho kimetajwa, lakini kituo cha polisi cha Kengeja ni kibovu, chakavu, kinavuja na kuta zake zimeanza kudondoka na ni athari sana kwa polisi na kituo hicho mmerithi kutoka kwa wakoloni.
Je, hamuoni kwamba ni aibu na fedheha kwamba hamuwezi kukikarabati na inawezekana kikapelekea askari hawa kupoteza maisha? Hamuwezi kukarabati hata lile ambalo mmerithi kwa wakoloni!?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nakiri kabisa kwamba kituo cha Kengeja hali yake siyo nzuri, hata mimi niliwahi kufanya ziara pale, lakini siyo Kengeja tu, ni maeneo mengi ndani ya nchi yetu vituo vya polisi haviko vizuri sana. Kwa mfano, Mkoani ni zaidi! Nadhani Kituo cha Mkoani kina hali mbaya zaidi kuliko Kengeja.
Mheshimiwa Spika, kama alivyozungumza mwanzo Mheshimiwa Mbunge, ni kwamba tuna mkakati wa kuvifanyia ukarabati vituo hivi na utaratibu huo utakuwa unaenda hatua kwa hatua kulingana na hali ya fedha itakavyoruhusu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Masoud uvute subira.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nina maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, uvunjwaji huu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora inaathiri sana usalama wa raia na mali zao. Katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amekiri na amesema kwamba mambo yaliyochunguzwa ni matumizi mabaya ya madaraka ya watendaji na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola.
Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kile kinachoitwa Uchaguzi wa Marejeo kule Zanzibar na kubadilika kuwa Uchafuzi wa Makusudio, ni kwa kiasi gani Serikali ilifanya uchunguzi ikagundua udhalilishaji huu wa watu kupigwa bila hatia na kule Tumbatu nyumba zao kuchomwa moto? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wametembelea magereza na kufanya uchunguzi wa kina. Naomba Mheshimiwa Waziri aniambie katika kutembelea magereza, wamefanya uchunguzi kiasi gani, wakafuatilia kiasi gani na wakagundua jambo gani pale ambapo Mashehe waliotoka Zanzibar waliopelekwa Tanzania Bara, waliofanyiwa vitendo vibaya, viovu, vichafu, vya kikatili na vya kishenzi walipolawitiwa. Tarehe 28 mimi nilikwenda kwenye Gereza la Segerea na wakasema kwamba hali yao ni mbaya na kinyesi chao hakizuiwi wanavuja mavi. (Makofi)
Je, tuambie Serikali hii, katika misingi ya uvunjaji wa haki za binadamu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud hilo ni swali la tatu sasa.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Hilo ni la pili.
NAIBU SPIKA: La pili umeshauliza…
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Sijauliza swali la pili.
NAIBU SPIKA: Kwa namna gani, kwa namna gani mara tatu, sasa hayo ni maswali mengi already. Kama unafuta hilo la pili basi uliza sasa hili lile la katikati ulifute. (Makofi)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Waziri wakati unajibu umesema kwamba mlikwenda kwenye magereza na kufanya uchunguzi, ni kiasi gani mmegundua malalamiko yaliyoko kwenye magereza na hasa pale ambapo kuna malalamiko ya muda mrefu ya Mashehe waliotoka Zanzibar ambapo walilawitiwa, vitendo vichafu, viovu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masoud, tafadhali uliza swali, umeanza na je, malizia. Uliza swali tafadhali, hayo maelezo tumeshayasikia.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Waziri, ni kwa kiasi gani malalamiko haya ya vitendo hivi viovu, vichafu, vibaya, vya kishenzi na vya kinyama walivyofanyiwa Mashehe wetu mtavifuatilia kwa kina?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kazi yake kubwa ni kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi. Mheshimiwa Mbunge anaposema kumetokea udhalilishaji wa haki za binadamu za kupindukia, napenda kujua kama hayo masuala malalamiko yalipelekwa kwenye Tume kwa sababu nachozungumzia hapa ni Tume ya Haki za Binadamu na jinsi ninavyojibu ni malalamiko ambayo yametolewa na wananchi. Kama nilivyosema kati ya mwaka 2010 mpaka mwezi huu ninapoongea Tume imepokea na kushughulikia zaidi ya 13,709. Sasa kama hiyo ni mojawapo taarifa ya Tume nitaletewa na nitakuja kuiweka hapa Mezani kama Katiba inavyonitaka chini ya Ibara ya 131(3).
MHE. MASOUD ABDALLA SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, kuna mkakati wa kupeleka Polisi
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
18
kwenye Kisiwa cha Tumbatu siku hadi siku kukabiliana na matatizo ya usalama, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri bado hujatueleza ni mkakati gani wa ziada wa kuweza kuwabaini na kuwakamata wale ambao walifanya uhalifu wa kuchoma moto nyumba za watu kule Tumbatu, ambapo hadi sasa watu wengine wamekosa makazi. Je, kuna mkakati gani wa Waziri na Serikali kuhakikisha kwamba, matatizo yale hasa yanaepukwa na hayatokei tena na yanakoma na wahusika wanakamatwa? Naomba maelezo!
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, siku zote Jeshi la Polisi limekuwa likichukua hatua kadri ya matukio ya uhalifu yanapotokea ikiwemo tukio la uhalifu ambalo limetokea Tumbatu. Kuna mambo mawili makubwa ambayo tumefanya tayari, la kwanza, ni kuhakikisha kwamba, tunachukua hatua kwa wale ambao tumewakamata, watuhumiwa kwa ufupi kwa kuwapeleka katika vyombo vya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili, ni kudhibiti hali ile isijitokeze tena, ndiyo maana katika jibu langu la msingi nilizungumza kwamba kumeongezeka doria na sasa hivi nadhani kwa kipindi kirefu kidogo, matukio yale ya uhalifu ya kuchomeana moto nyumba yamepungua ama yamesita Tumbatu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nina swali moja dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vilivyobinafsishwa ni kikwazo cha maenedeleo katika maeneo mengi. Katika hotuba ya Mheshimiwa alisema kuna viwanda 34 ambavyo vilibinafsishwa na Serikali ina mkakati wa kuweza kuvifufua. Pia kwenye majibu yako Mheshimiwa Naibu Waziri umesema kwamba mnapitia upya mikataba. Je, katika mikataba hiyo, mna mkakati gani wa ziada kuhakikisha kwamba mikataba ya Viwanda vya Korosho vya Lindi na Mtwara ambavyo vilibinafsishwa na hadi leo kuna tatizo kubwa la kupatikana kwa maendeleo katika mikoa hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ya ziada ambayo Serikali inaifanya, cha kwanza kabisa, viwanda vingi vilikufa kwenye miaka ya 1990 na 1998. Jambo la pili, viwanda vingi vilikufa kwa sababu ya kukosekana kwa malighafi au kuwepo kwa malighafi lakini kupungua kwa soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha tatu ni Sera ya Ubinafsishaji. Sasa mikakati ya kikatiba, kisheria na kimkataba, kwanza ni kutazama sasa hali halisi ya soko la dunia lakini hali halisi ya viwanda vingine na ku-review mikataba hiyo ya kiuwekezaji. Hatua ya pili, ni kutazama sera yetu sasa ya uchumi ambapo tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda na kutazama sasa mikataba yetu iwe namna gani ili kuvifufua viwanda hivyo.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza mimi nasikitika kwa sababu Serikali inaonekana haina nia njema juu ya jambo hili. Mimi nikiwa Mbunge mwaka 2004 Serikali ilitoa majibu haya haya, mwaka 2008 Serikali ikatoa majibu haya haya, mwaka 2012 Serikali ikatoa majibu haya haya. Mimi ni Mbunge kwa kipindi cha nne sasa, nasikitika sana juu ya majibu yenu ambayo … (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa swali kwa ufupi naomba tafadhali.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu, uzee na kuzeeka nani ataukwepa, hakuna na kila mmoja ni mzee mtarajiwa. Serikali ituambie sasa ina mkakati gani wa ziada na kama mlivyosema kuwa hatua chache zimebakia, hizo hatua chache ni zipi? Je, ndani ya miezi mitatu mnaweza kumaliza suala hili ili wazee wapate pensheni zao hasa ukizingatia na wale baadhi waliopigana Vita vya Kagera?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, lakini nikiendelea kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya jambo hili na ndiyo maana katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 jambo hili limewekwa na kutafsiriwa vizuri sana. Kipindi cha nyuma jambo hili halikuwa limechukua picha ya kutosha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Hiyo tu kwanza ni nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha jambo hili linatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ameeleza vizuri sana na naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba suala hili sio la kulala na kuamka ndani ya miezi mitatu halafu ukasema unaanza tu kulipa pensheni, hapana.
Narudia kusema Serikali imeshaanza kutengeneza miundombinu ya kulifanya jambo hili liweze kutekelezeka.
Sheria inayompa mamlaka Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kifungu cha 5(1)(e), kimemuagiza na kumwelekeza Mdhibiti kuhakikisha anasimamia suala zima la kuona namna gani Watanzania wengi wanafikiwa na sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo wazee.
Kwa hiyo, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu Serikali inalifanyia kazi suala hili na mara litakapokamilika litaanza kuchukua nafasi yake na wazee watapata pensheni.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Serikali mwaka 2006 (miaka kumi iliyopita), Serikali iliahidi kuyapima, kutathmini na kutoa fidia maeneo kadhaa na ndani ya maelezo hayo maeneo yote mliyaeleza mkaainisha katika kitabu ambacho mlitupatia.
Swali linakuja, inakuwaje leo ndani ya muda wa miaka kumi Serikali haijaona umuhimu, ahadi zenu ambazo mlituambia maeneo hayo mtayapima, kutathmini na kutoa fidia na baadhi ya wameshakufa katika maeneo hayo; je, Serikali ina nia njema kulipa fidia wananchi hao? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali na kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba tumeorodhesha maeneo yote yenye migogoro na tumeyaorodhesha maelezo ya nini kinachohitaji kufanyika. Yapo maeneo ambayo yanahitaji kwanza kufanyiwa tathmini ya fidia, yapo yanayohitaji kupimwa, yapo yanayohitaji kutolewa fidia lakini yako vilevile kama nilivyosema awali yale ambayo wananchi walivamia na hawastahili kuwa hapo. Na ukweli wa mambo ni kwamba fedha zinazohitajika ni nyingi, kila mwaka tumekuwa tukitenga katika bajeti yetu, fedha kiasi fulani ili kupunguza awamu kwa awamu mpaka tumalize. Kwa bahati mbaya sana kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge ni kwamba fidia ni gharama kubwa. Mheshimiwa Spika, maeneo mengi wananchi wamejenga na kila nyumba ina thamani yake, kwa hiyo kuweza kulimaliza hili tatizo haraka ni vigumu kwasababu ya uwezo wenyewe wa kifedha. Tunachoweza kuendelea kusema ni kwamba kila mwaka, mwaka huu wa fedha tumetenga shilingi bilioni 12, zikipatikana tutaanza sehemu moja baada ya nyingine ili kuweza kuondoa hili tatizo la muda mrefu. Mara nyingi nimekuwa nikisimama hapa nikijibu suala la migogoro ya ardhi kati ya Jeshi na Wananchi lakini ningependa kutoa wito vilevile kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba tusaidiane.
Mheshimiwa Spika, zamani Jeshi lilikuwa lina maeneo makubwa sana. Kwa sababu ya uhaba wa ardhi, wananchi sasa hivi wamekuwa wakivamia maeneo hayo. Kwa hiyo, yale maeneo yote ya Jeshi yaliyovamiwa ambayo wananchi hawastahili kuwa hapo ni vema wakatoka katika maeneo hayo na sisi kama Serikali, wale ambao wanastahili ya kulipwa fidia tutaendelea kuwalipa kadri uwezo utakavyokuwa unaruhusu.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza nina masikitiko kwamba majibu ambayo ametoa Mheshimiwa Waziri, ama wataalam wake hawaijui sekta ya uvuvi na wanaelekea zaidi kwenye shughuli za mifugo au itakuwa kuna danadana za hapa na pale. Nina maswali mawili ya nyongeza yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia mkakati wa Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati, Serikali imekuja na majibu wanasema wanataka kuanzisha viwanda vitatu vya kutengeneza boti aina ya fibre glass. Tanzania ya viwanda
kuelekea uchumi wa kati wanataka kutengeneza boti sasa ndogo (fibre glass), Serikali ituambie ina mkakati gani wa kuweza kununua meli za uvuvi za kisasa kwenda kwenye bahari kuu ambapo watavua samaki ambao wanavuliwa na nchi nyingine? Hiyo, tunataka mkakati wa ziada, sio mnasema mnataka kununua fibre glass? Fibre glass kwenye uchumi wa kati, Tanzania ya viwanda? Maajabu makubwa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wanasema Serikali kwamba sekta ya uvuvi hii wanataka kuboresha maisha ya wavuvi, wametenga wana shilingi milioni 400 kwa ajili ya kuboresha ruzuku za uvuvi na mambo mengine. Shilingi milioni 400 Mheshimiwa! Wavuvi ni maskini, shilingi milioni 400 ndio kitu gani? Kwenye bahari na kwenye maziwa? Serikali ituambie mna mkakati gani wa ziada kuboresha maisha ya wavuvi hasa wadogo wadogo sio shilingi milioni 400. Ndio Tanzania ya viwanda kuelekea uchumi wa kati hiyo? Tupe majibu ya uhakika, Serikali inasemaje juu ya kuboresha maisha ya wavuvi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Masoud kama ifuatavyo:-
Kuhusu uwekezaji wa ununuzi wa meli kwa ajili ya uvuvi katika bahari kuu nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yenyewe haina nia ya kununua meli, lakini kinachofanywa ni kuweka mazingira wezeshi na kuhamasisha sekta binafsi iweze kuwekeza katika ununuzi wa meli pamoja na uvuvi katika bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Shilingi milioni 400, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba hiyo ni sehemu ndogo tu shilingi milioni 400 zilizotolewa kwa ajili ya kuwawezesha wavuvi ni sehemu ndogo tu ya jitihada mbalimbali zinachokuliwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza sekta ya uvuvi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya walimu yasiyo ya mshahara ni pamoja na deni la walimu kwa Serikali juu ya posho na kufundishia yaani teaching allowance ambayo ni ahadi ya Serikali tangu mwaka 2012 ambayo ilitolewa kule Mtwara siku ya Walimu Duniani.
Je, Serikali ina mkakati gani wa ziada kuweza kuwalipa na kuwapatia fedha zao walimu hawa deni wanalolidai, posho la kufundishia yaani teaching allowance kwa haraka inavyowezekana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, kwa hali ya sasa tunachokifanya ni kuhakikisha kwa kadri iwezekano kusaidia sekta ya elimu. Ndio maana kabla sijajibu hili swali sasa hivi ukiangalia Serikali yetu kwa kazi kubwa waliyoifanya sasa hivi, mwanzo ukiangalia Walimu Wakuu, hata Waratibu wa Elimu mwanzo walikuwa hawalipwi hizi allowances.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali hivi sasa toka mwaka jana kuanzia Waratibu wa Elimu, Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari hivi sasa wote wanalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama kuna madeni mengine yoyote Serikali iko katika michakato mbalimbali kuyalipa madeni haya yote. Naomba niwahakikishie ndugu zangu Wabunge kwamba Serikali yetu jukumu letu kubwa ambalo tunalilenga sasa hivi, kwa sababu tunataka kuhakikisha ubora wa elimu lazima madeni haya yote yatalipwa na kama nilivyosema madeni yote ambayo yamehakikiwa kupitia Hazina yatalipwa madeni hayo. Tunataka walimu wetu wawe na morali ya kufanya kazi katika mazingira yao ya kazi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza. Nami naishukuru Kampuni ya Azam Marine kwa kurahisisha usafiri kutoka Tanga kwenda Pemba. Swali langu ni moja dogo lifuatalo:-
Kwa kuwa kuna malalamiko ya muda mrefu ya kutokupatikana kwa usafiri wa uhakika kutoka Dar es Salaam kuelekea Bandari ya Mtwara; na Serikali imekuwa ikiahidi mara kadhaa kwamba wako katika mkakati kabambe wa kuhakikisha kwamba usafiri kwa njia ya baharini kutoka Dar es Salaam kwenda Mtwara utapatikana kwa haraka; Serikali ituambie, ahadi hii ya muda wa miaka saba iliyopita, ni lini Serikali itaandaa mikakati ya kurahisisha usafiri huu? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tu humu Bungeni nilisema kwamba Serikali inaangalia uwezekano wa kutatua tatizo la usafiri kwenye Bahari ya Hindi, kwa sababu maamuzi yetu ya nyuma yalilenga kutoa fursa hii kwa wawekezaji binafsi. Ndiyo maana tulipotoa hizo fursa, wawekezaji kama Azam Marine walijitokeza na wengineo kuwekeza. Ni kwenye Maziwa Makuu tu ndiyo Serikali tuliendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuhamasisha wawekezaji binafsi lakini pale itakapoonekana kwamba wawekezaji binafsi, hawawezi kabisa kutoa huduma hiyo, Serikali itaangalia uwezekano wa kurudisha TACOSHILI ya zamani ili iweze kutoa huduma katika Bahari ya Hindi. Nimhakikishie tu kwa sasa hivi watu wa Mtwara wanasafiri kwa raha sana kwa njia ya barabara.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jengo la Polisi la kituo cha Kingeja ni bovu, chakavu, linavuja na jengo hili Serikali walinyang’anya kutoka kwa hao wanaitwa Wakoloni. Kwa bahati mbaya sana wamenyang’anya kutoka kwa hawa wanaitwa wakoloni wakawa wameshindwa kueliendeleza na linahatarisha maisha ya polisi na Naibu Waziri amefika kituo cha Polisi cha Kingeja huku akiwa na ahadi lukuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka utuambie leo Mheshimiwa Waziri, una mikakati gani ya ziada kuhakikisha kwamba kituo cha polisi cha Kingeja ambacho mlinyang’anya kwa wakoloni, jengo lile sasa hivi linapatiwa ukarabati wa hali ya juu ili polisi wale wasipate madhara yoyote? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokizungumza Mheshimiwa Masoud ni sahihi, binafsi nilifanya ziara katika Jimbo hilo la Mtambile na nilikitembelea hiki kituo, kwa kweli hiki kituo kiko katika hali mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujakaa kimya wala hatujadharau. Tunatambua changamoto kubwa ya ubovu wa kile kituo kama ambavyo vituo vingine vingi katika nchi yetu na kama ambavyo nimezungumza mwanzo kwamba pale ambapo tutapata fedha za ujenzi na ukarabati wa vituo hivyo tutafanya hivyo haraka sana.