Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mary Pius Chatanda (28 total)

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Walimu wamekuwa wakinyanyasika sana katika suala la upandishwaji wa madaraja na hata wanapokuwa wamepandishwa hayo madaraja, bado malipo yao kulingana na madaraja waliyopewa hawapewi kwa wakati, inawachukua muda mrefu kulipwa kulingana na madaraja waliyopewa. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya jambo hili?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwamba tumekuwa tukilipa malipo haya na ni kweli mengi yamekuwa hayalipwi kwa wakati, lakini kuna sababu zake. Hata hivyo, pia ukiangalia uwezo wa Kiserikali wa bajeti, tumekuwa tukijitahidi, tunafanya uhakiki na mara tunapothibitisha kwamba kweli madai hayo ni ya halali, tumekuwa tukijitahidi kufanya jitihada za ziada kuweza kuyalipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama nilivyomjibu Mheshimiwa Masoud Serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha madeni haya inakuwa ni historia.
Vilevile tunachokifanya pamekuwa na tatizo kubwa katika mfumo ambao tunautumia wa human capital, ukiangalia namna ambavyo wanakokotoa, kuna namna inakokotoa kupitia automatic system, lakini vile vile wale ambao unakuta wameajiriwa baada ya tarehe kumi na tano, unafanyaje? Inabidi waje wasubiri mpaka mwezi unaofuata. Kwa hiyo, ni dhahiri kabisa madeni haya yataendelea kuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya sasa ni kuangalia ni kwa namna gani tutaweza kuufanyia mapitio mfumo wetu wa malipo na taarifa za kumbukumbu za watumishi ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaondokana na malimbikizo haya.
Vilevile kuhusiana na wanaopandishwa madaraja, niseme tu kwamba majukumu ya kupandisha watumishi especially walimu ni Kamati mbalimbali za Ajira kupitia Wilaya zao na kama ambavyo nilijibu juzi kupitia swali la Mwalimu Kasuku, nilieleza changamoto ambayo walikuwa nayo Idara ya Walimu walikuwa na changamoto ya watumishi, lakini pia walikuwa na changamoto ya kibajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini suala hili litakuwa historia baada ya Tume ya Utumishi ya Walimu itakapoanza kazi rasmi mwaka huu, mwezi Julai. Niseme tu kwamba kwa upande wa walimu hawa, ukiangalia katika quarter tu ya kwanza ya Julai mpaka Oktoba mwaka huu takriban walimu 10,716 tayari walikuwa wameshapandishwa vyeo vyao. Vilevile tulikuwa tunasubiri kupata taarifa mbalimbali kupitia Kamati hizi za Ajira na mamlaka mbalimbali za ajira katika Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mary Chatanda, sasa hivi tunafanya kila jitihada kupitia TAMISEMI na tunatarajia kumalizia Wilaya 90 zilizobaki pamoja na Mikoa 12 ili kuweza kuwapandisha Walimu hao madaraja yao.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa amesema kwamba umeme umeunganishwa katika Gridi ya Taifa kule Hale; na kwa kuwa Korogwe imekuwa umeme unakatika mara kwa mara. Je, ni lini umeme utakoma kukatika ili kusudi wananchi wa Korogwe Mjini waweze kufanya shughuli zao za biashara pamoja na shughuli nyingine bila kuwa na kukatika kwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mary Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Mkoa mzima wa Tanga umeme unakuwa ukikatika mara kwa mara na suala la kukatika umeme mara kwa mara siyo kwa Mkoa wa Tanga peke yake, lakini sasa hivi tunachofanya, tunafanya marekebisho ya miundombinu yote katika Mikoa karibu yote. Kati ya mikoa yote, Mkoa wa Tanga tumeupa kipaumbele. Tunafanya marekebisho ya transfoma pamoja na chanzo cha umeme cha Hale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii inayokuja, tuombe sana Waheshimiwa Wabunge, tunadhani mtaipitisha; tumetenga pesa kwa ajili ya kurekebisha mitambo hiyo. Kwa hiyo, Mkoa wa Tanga na Korogwe mtapata umeme wa uhakika baada ya bajeti hii.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Waziri, amesema kuna wawekezaji ambao wanakusudia kuwekeza pale Kwamsisi, natoa pongezi kwa sababu kiwanda kile kinakuja katika Mkoa wetu wa Tanga. Kwa kuwa ndiyo wanatarajia kuanza kulima hayo mazao ambayo yatalisha kiwanda hicho, je, haoni ni wakati muafaka kwa matunda yaliyopo sasa na hasa ikizingatiwa kwamba Serikali imeshasema itafufua kwanza viwanda vilivyokuwepo hasa kiwanda kilichokuwepo pale Korogwe, ni kiwanda kidogo lakini kinaweza kutengeneza juice kikafufuliwa hicho kwanza wakati tunasubiri kiwanda kikubwa?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, waambie wanipige taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mary Chatanda ameuliza maswali mawili katika moja. Ubora wa matunda au matunda tuliyonayo na hii kampuni ya Kwamsisi ambayo itachukua miezi 18 mpaka ianze kutengeneza juice, jibu lake ni hivi, kuna kampuni nyingine inaitwa Sayona inajenga kiwanda sehemu ya Tanga karibu na Chalinze, itachakata tani 25,000 za matunda yoyote, hii itakuwa inakidhi haja wakati sisi tunasubiri hiki kiwanda cha SASUMUA. Kwa nini SASUMUA hawezi kuanza, yeye analenga kuanza na mananasi na wanasema wataalam kwamba nanasi litakapopandwa linahitaji miezi 18 kuweza kukomaa. Kwa hiyo, yeye ana masharti yake na utaalamu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la Korogwe kwamba kiwanda kipo na bahati nzuri ameuliza swali siku nzuri, namuagiza Mkurugenzi Mkuu wa SIDO aende Korogwe na mtaalam wa TIRDO watathmini ni kitu gani kinahusika halafu Halmashauri yake ambaye yeye ni Diwani tuje tuangalie ni namna gani ninyi mnaweza kuhamasisha Wanatanga ili muweze kukiendesha, viwanda vingine siyo vya Serikali. Ni nini tatizo, hiyo ni kazi yangu nitabaini, spare atanunua wapi wataalam wangu watamwambia, ni viwanda vya shilingi milioni 60 au 80, halmashauri mnavimudu.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona. Naomba niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri, Korogwe ilikuwa na mradi wa World Bank ambapo ilikamilisha miradi yake Kwa Msisi, Ngombezi na Kwa Mndolwa na ikabakiza mradi wa Rwengela Relini, Rwengela Darajani na Msambiazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha miradi hiyo ambayo imebakia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Korogwe kuna mradi wa maji, lakini naomba nitoe maelezo kwamba si Korogwe peke yake isipokuwa kuna miradi ya maji mingi sana hivi sasa, hata Wabunge wengi wanaweza wakasimama. Miradi hii ni kwamba mingi ambayo wakandarasi walikuwa site, lakini baadaye wakafanya mpaka waka-demobilize vifaa kutokana na kushindwa kulipwa fedha. Nadhani hata mradi wa Korogwe ndiyo tulipata changamoto hiyo, lakini siyo mradi wa Korogwe peke yake isipokuwa ni miradi mingi.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana, tulipoanza katika Serikali ya Awamu ya Tano jukumu lake kubwa, lilikuwa ni kuangalia jinsi gani itakusanya fedha za kutosha. Wakati tunaingia tulikuwa na outstanding payment ambapo deni tunalodaiwa lilikuwa karibu bilioni 28, lakini kutoka na makusanyo mazuri yaliyofanywa hivi sasa deni lile lote limeshalipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naamini sasa hivi ukiangalia hata Waziri wa Fedha hapa atakapokuja katika bajeti yake ataeleza kwamba hivi sasa tuna uwezo hata certificate zikija watu wakaweza kulipwa. Kwa hiyo, mradi wa Korogwe sawasawa na miradi mingine ambayo imesimama. Naamini Halmashauri zingine hivi sasa watasema bado hawajapokea fedha, lakini mchakato huu sasa nawasisitiza Wakurugenzi wote na ma-engineer wote wa Wilaya, wale wakandarasi ambao certificate zao hazijapelekwa, haraka zipelekwe Wizara ya Maji ilimradi kuhakikisha kwamba, wakandarasi wanarudi site kazi ziweze kufanyika. Hii ni kutokana na umakini uliyofanyika katika ukusanyaji wa kodi. Hapa naomba niwasistize ndugu zangu Wabunge, wote tushikamane na Serikali yetu ili kodi ziweze kulipwa, miradi iweze kutekelezeka.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mji wa Korogwe unapitiwa na Mto Pangani katikati ya mji, je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kwa kuutumia mto ule kuwapatia watu wananchi wa Mji wa Korogwe maji hasa ikizingatiwa kwamba wana shida ya maji, wanaangalia mto lakini maji hawayapati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza mradi wa HTM na tayari tumeshaahidiwa fedha kwa wafadhili na usanifu wa mradi huo umekamilika. Bahati nzuri ni kwamba usanifu huo utachukua maji kutoka Mto pangani tena karibu kabisa na eneo la Korogwe.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nakuahidi kwamba wakati tunachukua maji kutoka katika Mto wa Pangani hatuwezi kuacha kupeleka maji sehemu yenye chanzo. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba eneo la Korogwe pia litapatiwa maji kutokana na huo mradi wa HTM.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sambamba na suala la madawati, wananchi wameitikia wito wa uandikishaji wa watoto shule za awali pamoja na darasa la kwanza. Je, Serikali iko tayari sasa kupeleka Walimu wa madarasa haya ya awali kwa sababu madarasa hayo hayana Walimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba tuweke rekodi sawa, katika utekelezaji wa ahadi ya Chama cha Mapinduzi na Ilani yake lakini azimio la Mheshimiwa Rais kuhakikisha watu wote wanakwenda shuleni, tumepata mafanikio makubwa sana na ni kweli tumepata ongezeko la wanafunzi na shule zingine zime-burst. Shule ambayo ilikuwa inatarajia kusajili wanafunzi 500 wamesajili mpaka wanafunzi 1,000, haya ni mafanikio makubwa katika Taifa letu hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa utaratibu uliopo sasa Walimu wote wanaosoma ngazi ya certificate wanakuwa na component ya elimu ya awali. Kwa hiyo, imani yangu kubwa ni kwamba katika ajira ambazo tunatarajia kuzitoa mwaka huu ambapo siyo muda mrefu ujao, suala hilo la kuzingatia Walimu ambao watakwenda kufundisha masomo ya awali litapewa kipaumbele bila mashaka ya aina yoyote.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa walimu wamejiunga na PSPF lakini walimu hawa wanapoomba mikopo watu wa PSPF wanachelewa sana kuwapa majibu na kuwakamilishia haki yao ya msingi ambapo wengine wanakuwa wamekaribia kustaafu wanataka wajiandae. Je, Serikali inawaelezaje walimu hawa ambao wanakaribia kustaafu na wanahitaji wapate huo mkopo wanawacheleweshea kuwapa mkopo huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni haki ya walimu waliojiunga katika mfuko wa PSPF kupata mkopo pale ambapo wamekidhi yale masharti yanayohitajika, kwa maana umri ule wa kustaafu ambao kwa mujibu wa taratibu za sasa za mfuko ule, tayari wamekwishakuanza kutoa mikopo kwa walimu ambao wamekaribia umri wa kustaaafu kuanzia miaka 55 wakishapeleka maombi yamekuwa yakifanyiwa kazi.
Nichukue tu fursa hii kuwaomba walimu wote ambao watakuwa wamekidhi masharti na vigezo vya kupata mkopo basi wafike katika ofisi zao kwa ajili ya kuweza kupata huduma hiyo.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Wilaya ya Korogwe ina Halmashauri mbili na Halmashauri ya Mji wa Korogwe haina hospitali, wananchi wake asilimia 60 wanatibiwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya na kusababisha msongamano mkubwa katika hospitali hiyo. Halmashauri ya Mji tuna zahanati ipo Kata ya Majengo ambayo vilevile inalaza akina mama wajawazito wanajifungulia pale.
Je, Serikali sasa kwa maana ya Wizara ya Afya hasa ikizingatiwa kwamba hatuna hospitali itakuwa tayari kutusaidia kujenga jengo la upasuaji ili kusudi wa kina mama wale wajawazito wasiende kule kwenye hospitali ya Magunga ambako kuna msongamano mkubwa?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumbukumbu zangu kama sikosei na Mama Mary Chatanda atanisahihisha, mwezi wa Machi tulikuwa pamoja kutembelea Hospitali ya Korogwe pale, lakini tulivyoenda pale nilichokishuhudia ni umati mkubwa wa watu waliojaa katika hospitali ile, sikujua kwamba umati ule ni kutokana na congestion kutoka katika hizi Halmashauri mbili.
Nimshukuru Mbunge kwa sababu siku ile tulivyoondoka nimekuta kwa mara ya kwanza mashuka yaliyowekwa katika makabati siku hiyo wametandika katika vitanda, Mbunge alinisaidia sana tukatoa maagizo mazito kuhakikisha kwamba makabati wataalamu suala la shuka ziwekwe katika vitanda siyo watu walalie vitenge vyao. Kwa hiyo Mbunge nikushukuru katika lile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wana hiki kituo cha afya naomba niseme wazi umati mkubwa tuliouona pale naomba kwa sababu bajeti ya mwaka huu tumeshaipanga, katika bajeti inayokuja naomba tuweke mkakati wa pamoja katika kikao chetu cha Baraza la Madwani. Tutenge bajeti na Ofisi ya TAMISEMI itasimamia hilo kuhakikisha tunajenga theater ili hiki kituo cha afya tukipandishe tukipandishe hifikie hadhi inayokusudiwa, mwisho wa siku ni kwamba katika hii Korogwe Mji iwe na Hospitali yao inayojitegemea kupunguza umati wa watu katika Hospitali ya Halmashauri ya Korogwe.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa niulize swali la nyongeza. Wafanyakazi wamekuwa wakikatwa fedha zao na kupelekwa kwenye huu mfuko wa PSPF. Lakini wafanyakazi hawa wanapokuwa wamemaliza huo muda wanacheleweshewa kupewa mafao yao. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuona kwamba, wafanyakazi hawa wanapomaliza muda wao wawe wanaandaliwa cheque zao mapema ili kusudi ziweze kuwasaidia katika kufanya shughuli zao wanazokuwa wamejipangia kuliko hivi sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, je, Mheshimiwa Waziri amejibu amesema wameshaanza kulipa; anaweza sasa akanisaidia mimi orodha ya Mkoa wa Tanga, hususan Korogwe, wale ambao wamekwishalipwa ili wasiendelee kunieleza kwamba wanadai? Nipate ile orodha ili iweze kunisaidia.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa swali lake la kwanza alilouliza kuhusu kucheleweshewa malipo, kama ambavyo Serikali imekuwa ikitoa majibu humu Bungeni ni kwamba kucheleweshewa huku hakutokani na Serikali, kunatokana na waajiri ambao wanachelewesha kufikisha nyaraka za wastaafu hawa katika Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii. Hivyo, nitoe tu wito wangu kwa waajiri wote wajitahidi kupeleka nyaraka zote zinazostahili kwa wastaafu miezi mitatu au sita kabla mstaafu hajastaafu ili tuweze kulipa mapema iwezekanavyo. Wakiweza kufanya hivyo, Waheshimiwa Wabunge tunaweza kabisa mstaafu anapokuwa amestaafu nyaraka zake zimekamilika na cheque yake itaweza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, Mheshimiwa Mbunge naomba nifanye kazi mimi na wewe kuhusu wastaafu wote wa Wilaya ya Korogwe wanaolipwa na Mfuko wetu wa PSPF, tunapomaliza Kikao hiki cha Bunge naomba tushirikiane ili upate orodha halisi ya waliostaafu na orodha halisi ya waliolipwa katika kipindi hiki. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi ndicho kilichoshinda katika uchaguzi mkuu uliokwisha hivi karibuni mwaka 2015; na kwa kuwa Serikali iliyoko madarakani sasa inatakiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi iliyojinadi kwa wananchi wake; na kwa kuwa ziko nchi ambazo uchaguzi ukishamalizika vyama vya siasa vingine havipaswi kwenda kufanya mikutano ya hadhara, je, hatuoni sasa ni wakati muafaka wa kufanya marekebisho ya sheria ili chama kilichoko madarakani kiweze kuachiwa nafasi ya kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kuendelea kuwakumbusha wanasiasa kwamba madaraka ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa yako kwa mujibu wa Katiba na waendelee kutii madaraka na pale wanapovunja sheria, sheria zitaendelea kuchukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mary Chatanda ameleta ushauri kwa Serikali na ninachoweza kusema kwa niaba ya Serikali ni kwamba, kwa kuwa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria mbalimbali zilizowekwa ndizo zinazofuatwa kwa sasa kuongoza misingi ya utawala bora na hasa pale chama kinaposhinda kuendelea kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi, hivyo ndivyo ilivyo sasa. Kwa hiyo, kama nchi hii itaona kwamba kunatakiwa kufanya mabadiliko na michakato ya Katiba inaendelea, basi mambo hayo mengine mapya yanaweza kuzingatiwa katika michakato ya Katiba inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunaendelea kuwakumbusha Watanzania wote chama kilichoshinda na kushika hatamu ya kuendesha nchi hii kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ni Chama cha Mapinduzi na Watanzania
wote wataendelea kushughulikiwa kupitia Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi, sheria na Katiba iliyopo sasa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa usalama barabarani ni pamoja na kusimamia kuhakikisha kwamba ajali hazitokei mara kwa mara.
Je, Korogwe kutoka Chalinze hadi Same ni kilometa kama 370 na kitu, je, Serikali kwa maana ya Wizara ya Mambo ya Ndani, askari wa Korogwe Mjini wao ni mara nyingi ndiyo ambao huwa wanashughulikia ajali kutoka kwenye maeneo hayo niliyoyasema hizo kilometa zote hizo. Watakuwa tayari kuwapatia gari askari wa barabarani ili waweze kufanya patrol ili waweze kupunguza ajali zinazotokea barabarani?

MHE. MARY P. CHATANDA: Korongwe Mjini.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mary Chatanda, Mbunge wa Korogwe Vijijini?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tupo tayari kupeleka gari la nyongeza hapo cha msingi ni kuyapima mazingira hayo, kwa hiyo, nawalekeza Jeshi la Polisi kulipitia ombi la Mheshimiwa Chatanda na kuangalia uwezekano wa kuongeza gari moja pale litakapokuwa limepatikana.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwenye taarifa ya Waziri wa Fedha aliyoiwasilisha hii ya bajeti, imezungumzia tu suala la milioni 50, kwamba zitakwenda kwenye vijiji, haikuzungumzia Mitaa, kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan walizungumza walipokuwa wakipita kwenye kampeni kwamba watahakikisha Mitaa na Vijiji vinapata mikopo ya milioni 50. Je, Serikali inatuambia nini juu ya wananchi wanaoishi mijini, ambao wana mitaa badala ya vijiji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Mary Chatanda, Mbunge mwanamke wa Jimbo pia kwa kazi nzuri za uwakilishi anazozifanya na nina imani kule Korogwe Mjini wako salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa najibu katika swali langu la msingi, kwamba kazi kubwa ambayo tunaendelea kuifanya sasa hivi ili kufanya maandalizi mazuri ya Mfuko huu, kuweza kutumika kwa Watanzania wote. Kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ni pamoja pia na kutafsiri maana ya Mitaa na Vijiji kwa kuzingatia Sheria ya Local Government kama ilivyoweka mipaka katika maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Wabunge wawe na amani, watulie. Serikali yao inafanya kazi na utaratibu utawekwa wazi na tunahakikisha kwamba Watanzania hawa watanufaika na fedha hizi kama vile tulivyoainisha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Wakuu wa Wilaya ndiyo Watendaji Wakuu ambao wanakutana na wananchi kwa karibu zaidi. Je, Waziri anaweza sasa kufanya mabadiliko badala ya kupeleka OC kwa RAS wakapeleka moja kwa moja kwa DAS ili kusudi waweze kufanya kazi zao vizuri zaidi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba jambo hili tumeliona na pengine liko dhahiri sana. Kwa sababu kule kuna Mkuu wa Utawala katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Pia kuna Mkuu wa Utawala katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye ndiye RAS na huku anaitwa DAS ambao kazi yao na majukumu tofauti ni maeneo tu. Kwa hiyo, sidhani kama kuna ubaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema wakati wa majumuisho yangu siku ya bajeti yangu kwamba tunaangalia namna ya kuhakikisha kwamba OC hizi kwenye Wilaya zinapelekwa moja kwa moja, nasi tumekubaliana. Katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/2017, OC hizi kwenye Wilaya zitapelekwa moja kwa moja kwenye Ofisi za Ma-DAS ili na wenyewe waweze ku-manage pale kama wanavyoafanya Mkoani. Kusema ukweli tunalichukua wazo hili, ni zuri nasi tulishawekea mkakati wake, tutalitekeleza, ni jambo zuri sana.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa, Bunge lililopita kuna fedha zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya ile miradi 10 ya World Bank katika Vijiji Mji vya Mji wa Korogwe ikiwemo Lwengela Relini, Lwengela Darajani na Msambiazi. Je, Serikali ina mpango gani kwa sababu kwenye bajeti hii sijaona hiyo fedha? Safari iliyopita hawakupewa zile fedha, safari hii wana mkakati gani kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinachimbiwa vile vile visima virefu kama ambavyo ilikuwa imepangwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya Miradi ya World Bank ambayo haikukamilika, kama ambavyo nimeshajibu awali kwamba, katika bajeti tuliyoitenga mwaka huu, basi tuhakikishe kwamba tunakamilisha kwanza ile miradi ambayo haikukamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, natambua pia, kwamba, eneo la Korogwe lina matatizo makubwa ya maji, baadhi ya vijiji bado havijapata. Kupitia mradi wa HTM ambao chanzo chake nacho kinatoka katika ule Mto Ruvu tutahakikisha kwamba, sehemu ya maji hayo yanapita kwenye Vijiji vya Korogwe ili kuhakikisha kwamba, wananchi wote wa eneo la Korogwe wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo hayatafikiwa na mradi tuhakikishe kwamba tunashirikiana na Halmashauri kwa ajili ya kuchimba visima au kujenga mabwawa. Kama fedha haipo katika Mwaka wa Fedha 2016/2017 basi wahakikishe wanaharakisha kuleta maombi, ili katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tunatoa fedha. Katika hiki kipindi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutatembelea hilo eneo, tutatembea kuja kujionea hali halisi.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa suala la mashamba ya mkonge kwa upande wa Korogwe Vijijini inafanana na Korogwe Mjini, na kwa kuwa Korogwe Mjini tayari ilishaingia kwenye mpango kabambe wa masterplan, na kwa kuwa mji huu una mashamba ya mkonge nayo ambayo hayaendelezwi na tayari tulishaleta mapendekezo ya kuomba mashamba hayo yafutwe.
Je, Serikali inatuambiaje na hasa ikizingatia kwamba tupo kwenye ule mpango kabambe wa masterplan kuhakikisha kwamba mashamba hayo yanafutwa ili maeneo hayo yaweze kutumika katika huu mpango kabambe ambao umeandaliwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba hayo mashamba ambayo tayari wao wameleta mapendekezo kwa Waziri ili na yeye aweze kumshauri Rais ayabatilishe ni yale pia katika mchakato ambayo pengine tunasema kwamba kuna maeneo mengine ambapo wamekopea pesa benki.
Kwa hiyo, mchakato unafanyika ili kuweza kujua, na pale pale tunaangalia ile ilani ambapo kama imekwenda sawasawa kisheria, kwa sababu mashamba ni mengi na yote yanahitaji pia umakini katika kuyabatilisha.
Kwa hiyo, tusingependa kutoa ushauri ambao pengine unaweza ukampotosha Mheshimiwa Rais akaja akalaumiwa, tunataka kujiridhisha na masharti yote yaliyopo pale kama yamezingatiwa lakini pia na kuangalia fedha za Umma zisije zikapotea kwa sababu tu hawa watakuwa wamebatilishiwa umiliki wao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hilo tunalifanyia kazi na nimwahidi Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuiangalia orodha ya mashamba ambayo anayasema tuweze kuona yamefikia katika utaratibu gani ili hatua nyingine ziweze kuendelea.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwanza, naishukuru Wizara ya Elimu iliweza kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Chuo cha Ualimu pale Korogwe ambapo kilileta wanachuo karibu 800 na kitu kwa ajili ya mafunzo pale. Hata hivyo, naiomba Serikali, kwa kuwa chuo kile kina maktaba ndogo na sisi wananchi tumeweza kujenga maktaba kubwa ambayo ingeweza kuwasaidia wanachuo ambao ni wengi sasa pale chuoni, pamoja na wananchi wa Korogwe kwa ujumla: Je, Serikali itakuwa tayari kutupa fedha ili tuweze kukamilisha lile jengo la maktaba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Chatanda kwa kufuatilia masuala ya kielimu na Mheshimiwa Mbunge anapofanya jitihada kama hizo sisi Serikali tunao wajibu wa kusaidia. Kwa hiyo, tutachukua hilo jukumu la kusaidiana nao kuhakikisha maktaba hiyo inakamilika vizuri.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kama ambavyo Naibu Waziri amesema kwamba chuo kile kina uwezo wa kudahili wanachuo 1,200 na ameeleza mwenyewe kwamba 2015/2016 kilidahili wanachuo 234. Kutokana na miundombinu na rasilimali iliyopo pale, kuwa na wanafunzi 234 kati ya 1,200 hatuoni kwamba hatukitendei haki chuo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna utaratibu ule wa kuwadahili kupitia mtandao na huko vijijini hakuna mitandao kwa nini isirejee utaratibu wa kuandika barua pamoja na kutumia hizo internet kwa wenzetu walioko mijini ili watoto wa wanavijiji na wenyewe waweze kupata hizi nafasi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, zamani utaratibu ulikuwepo wanafunzi ambao wako shuleni walikuwa wakiomba nafasi za ualimu wakiwa shuleni. Je, kwa nini wasirudishe utaratibu huo mtu aweze kuomba akiwa shuleni ili tuweze kupata wanachuo wa kutosha kuliko kuwa na chuo ambacho kinataka wanafunzi 1,200 halafu wanadahili wanachuo 234?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli baada ya kuboreka kwa miundombinu hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba chuo hicho kinachukua wanafunzi wanaostahili kuwepo. Ieleweke kwamba baada ya kubadilisha hizo sifa kwanza hali ya ufaulu wa wanafunzi katika shule zetu ulikuwa uko chini lakini pia kutokana na mambo ambayo yalikuwa yanachangiwa humu Bungeni juu ya sifa za Mwalimu, kwa sababu ilikuwa inaonekana kwamba ualimu anapelekwa mtu mwenye sifa hafifu, kwa hiyo, Wizara ilifanya marekebisho na kuona kwamba sasa sifa ziwe mwisho ni daraja la III.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo, kwa mwaka wa kwanza tulikuwa na wachache lakini kwa sasa hali ya ufaulu imeboreka kutoka katika shule zetu za Serikali na zisizo za Serikali kwa hiyo, tunao wanafunzi wengi ambao wanaweza kupelekwa huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika niseme tu kwamba katika suala la udahili tunaliangalia na Kamati yetu ya Huduma ya Jamii imelizungumza sana. Tunaangalia namna bora ya kudahili bila kupoteza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa ubora unalindwa. Kwa hiyo, tutafikia maamuzi baada ya tafiti zinazoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuwapeleka wanafunzi moja kwa moja kutoka shuleni ni kwamba wanafunzi hao ni mpaka wawe wameshafanya mitihani na wengine wanachukuliwa kutoka katika ngazi mbalimbali za uombaji, kwa hiyo, matokeo yao ndiyo yanayowapeleka huko siyo tu ilimradi yuko pale shuleni na aanze kujaza. Kwa hiyo, suala ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaopelekwa katika Chuo cha Korogwe na vyuo vingine vyote ni wale wenye vigezo vya ubora unaohitajika.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nitaongea kwa kifupi. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na napenda tu kuongezea jambo dogo kwamba, suala hili la vyuo vya ualimu kuwa na wanafunzi wachache kuliko uwezo wake lilitokana na uamuzi wa kuwapeleka wanafunzi UDOM ambapo ilisababisha mlundikano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulihakikishia Bunge lako Tukufu yale mambo yaliyokuwa yanasemwa kwamba Serikali iliwaondoa wanafunzi UDOM ili ipate nafasi siyo kweli kwa sababu iliona ni vizuri, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba Vyuo vya Ualimu vichukue wanafunzi kulingana na uwezo wake. Nashukuru.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri, alipotembelea Wilaya ya Korogwe aliweza kuona hali halisi ya tatizo la maji lililopo katika mji wetu wa Korogwe. Hata hivyo aliahidi kutuletea shilingi bilioni mbili ili angalau tatizo la maji lile liweze kuondoka pale, swali; kwa kuwa
wameshatuletea milioni 500 kwa ajili ya kutoa maji kutoka kwenye Mto Ruvu, je, sasa Serikali zile fedha wameshaziingiza kwenye bajeti ili kusudi ziweze kutusaidia katika kutengeneza miundombinu ile ambayo ni mibovu maana yake
tutakapokuwa tumejenga matenki au tumejenga ule mkondo wa maji bila ya kuwa na matenki ya maji makubwa bado tatizo la maji litakuwa lipo pale Korogwe. Je hizi fedha shilingi bilioni mbili alizosema zimetengwa katika bajeti hii? Nashukuru.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tulitenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha maji katika Mji wa Korogwe na tulitoa maelekezo kwamba usanifu ukikamilika tunatangaza tender kwa hiyo ikishatangazwa tender na wakianza kufanya kazi tutakuwa tunalipa kwa certificate jinsi zinavyokuja. Kwa hiyo, naomba nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi ule utatekelezwa na fedha zipo kwenye bajeti. Ahsante sana.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti nashukuru kunipa nafasi ili na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti tatizo la Karatu linafanana
na tatizo la Korogwe Mjini. Korogwe Mjini haina hospitali, kwa maana ya Halmashauri ya Mji, na Wilaya yetu tumeamua kwa makusudi kabisa kujenga kwanza kituo cha afya ambacho tutakifanya kiwe hospitali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweza kutusaidia kutupiga jeki kwa sababu tunajenga kituo cha afya chenye ghorofa tatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niweke kumbukumbu sawa ni kwamba nipende kumshukuru Mama Mary Chatanda, Profesa Maji Marefu pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ambapo nimetembelea mara kadhaa katika eneo lile. Nilivyofika pale nimekuta initiative mbalimbali wanazozifanya hasa katika suala zima la sekta
ya elimu na sekta aya afya na bahati nzuri wanatumia hospitali ya ndugu yangu Profesa Maji Marefu, iko vijijini lakini obvious kijiografia iko mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa sababu
mmeanza harakati za ujenzi, na kile kituo cha afya ni kituo cha afya makini inaonekana kuna viongozi makini eneo lile, Serikali itachukua wazo lile jema kuangalia wapi mmeishia, tukishirikiana nanyi kwa pamoja tufanyeje, kwa kuangalia resource tulizo nazo tusukume ili eneo la pale ambalo ni katikati; watu wanaotoka Arusha hata ikipatikana ajali
lazima watakimbizwa pale, tuweze le tuweze kushirikiana kwa pamoja tujenge Hospitali ya Wilaya pale.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Wizara ya Utumishi ina watumishi wanaofanya kazi vizuri, hawajatumbuliwa, Serikali kwa maana ya Chuo cha Ualimu, kutokana na swali langu namba 81 ambalo nilijibiwa kwamba suala la upandishaji madaraja na likizo za Watumishi wamelipwa kwa kiasi kile ambacho walikuwa wamekitaja.
Je, watakuwa tayari sasa kutoa orodha ile ya wale waliokwishalipwa kwa Chuo kile cha Korogwe cha
Ualimu ili kusudi Walimu waweze kujitambua kwa sababu huwa kama wanawalipa, wanaingiza moja kwa moja kwenye mishahara, watakuwa tayari kuitoa hiyo orodha ili iende kwa Mkuu wa Chuo kila mtu aweze kutambua kile alichoweza kulipwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Chatanda. Nimelifuatilia swali hili, nadhani wiki iliyopita lilijibiwa na Mheshimiwa Stella Manyanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema kwamba nitafuatilia na Wizara ya Elimu kwa karibu ili kuona waliolipwa ni akina nani na orodha iweze kutolewa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nampongeza Waziri wa Elimu na Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kufuatana nami ili aweze kuangalia lile jengo ili kusudi waweze kutoa kitu ambacho kinalingana na kazi ambayo inakusudiwa kumaliziwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni ndiyooo! (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sikubaliani na majibu ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, hayaridhishi kabisa. Ukiangalia kwa mtiririko ulioko kwenye majibu haya imesema wazi mwaka 2006/2007 walifanya upembuzi na kugundua kwamba shilingi bilioni kumi na tatu ilihitajika kwa ajili ya mradi huu lakini wakafanya upembuzi tena mwaka 2014/2015 ikaonekana shilingi bilioni 1.54 zilitakiwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hili lakini bado wakafanya mwaka 2015/2016 wakatenga milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najenga hoja naomba utulie. (Kicheko) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]
Mheshimiwa Mwenyekiti, walitenga fedha hizi shilingi milioni 800 hazikutoka, halafu mwaka 2016/2017 hawakutenga fedha…
… 2017/2018 hawakutenga fedha, sasa ni kwa nini wanazungumza uongo? Kwa nini hawakutenga fedha katika miaka miwili hii ambayo imo mpaka bajeti ya safari hii wanazungumza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mtu ambaye amekamilika, ulimi inawezekana umeteleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni sasa kwamba kutokutekeleza mradi hii hawawatendei haki wananchi wa Wilaya ya Korogwe hususan Manga Mkocheni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya shemeji yangu Mheshimiwa Mary Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeonyesha taratibu mbalimbali zilizofanywa na Serikali na kwamba utendaji lazima tufuate tathmini ya wataalam. Sisi kazi yetu ni kutunga sera na kupitisha bajeti, lakini utekelezaji unazingatia taarifa za wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi nimesema kwamba utafiti wa awali ulionesha kwamba bwawa lingejengwa kwa shilingi bilioni 13; lakini tathmini ya kimazingira ikaonyesha kwamba bwawa hilo lingejengwa lingezamisha baadhi ya maeneo na vijiji vya wananchi wa Manga, tusingeweza kufanya hivyo. Kwa hiyo, Tume ya Umwagiliaji kupitia Mkoa wa Kilimanjaro wakafanya tathmini nyingine upya ambayo kama ingetekelezwa basi hayo maeneo ambayo yangeathirika na bwawa yasingekuwemo, ndiyo maana bajeti sasa ikaja shilingi bilioni 1.5, hilo ndilo jibu la msingi. Lakini bado tumetenga shilingi milioni 800 mwaka uliofuata 2014/2015 lakini kwa bahati mbaya bajeti haikutoka ndio maana utekelezaji haukufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba malengo yetu ni kuhakikisha tunajenga hili bwawa na ndio maana Serikali ya Chama cha Mapinduzi...
...imeunda Tume ya Umwagiliaji ambayo sasa kazi yake itakuwa ni kusimamia moja kwa moja suala la utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi hakuna haja ya hasira kazi hii tutaifanya na wananchi wa Manga watapata huduma wanayoihitaji. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa niulize swali la nyongeza. Katika jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Teaching Allowance ipo kwenye mshahara. Sasa tunapata tabu sana tukikutana na Walimu wanapotuambia juu ya kurudisha Teaching Allowance. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutamka ndani ya Bunge hili ili waweze kutambua kwamba Teaching Allowance yao iko kwenye mshahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa tulilokuwa nalo ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi sana hapa leo wanalizungumza ni suala zima la maslahi mapana ya watumishi. Ndiyo maana hata hicho kilichokuwepo kama kidogo au kikubwa hakioneshi vizuri ni kwa sababu huenda lile fungu lenyewe, purchasing power imekuwa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma, juzi juzi kulikuwa na kikao maalum kinafanyika kwa sababu kunaundwa bodi maalum ya kuja kupitia maeneo yote hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha Teaching Allowance, kuna mambo mengine; kuna suala la haki za watu wanaofanya kazi katika mazingira magumu. Kwa hiyo, jambo hili tutakuja kulitamka rasmi sasa baadaye kuhusu mchakato huu unavyokwenda. Hiyo Bodi iliyoundwa sasa kupitia mishahara, siyo kwa Walimu peke yake, isipokuwa watumishi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaona jinsi gani kila mtumishi atapata stahili yake na nyongeza kwa kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili tutakuja kulitoleaa tamko rasmi hapa baadaye Bungeni likiwa katika utaratibu mzuri baada ya kutoa hii documentation vizuri.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza, niipongeze Wizara hii kwa maana ya MSD kwa kuwa sasa wanatoa dawa za kutosha katika hospitali zetu. Hata hivyo, kwa kuwa hospitali hizi zinapokuwa zinakosa hivi vifaa tiba, kama ambavyo amezungumza kwenye jibu lake la msingi, kwamba wanaruhusu kwenda kununua kwa wazabuni, haoni kwamba kitendo cha kwenda kununua kwa wazabuni bei ni kubwa mara mbili zaidi ya vile vifaa ambavyo wanakwenda kuvinunua kama vile dawa za amoxicillin pamoja na vile vifaa vya theater. Hawaoni kwamba sasa inakuwa ni gharama kubwa zaidi kuwahudumia hao wagonjwa ambao wanaokwenda kwenye hizi hospitali? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa anasema kwamba mteja apewe ndani ya siku moja ili kwenda kununua kwenye haya maduka ya watu binafsi. Kwa nini isiwe ndani angalau ya wiki moja kuliko ile siku moja ili mtu apate nafasi nzuri ya kuweza kwenda kununua hizo dawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza, ni kweli kwamba bei kwenye sekta binafsi zinaweza zikawa kubwa ukilinganisha na bei zilizopo kwenye maghala ya MSD. Sababu ni nyingi, mojawapo ikiwa ni kwamba kwenye MSD kwa sasa kwa sababu tunanunua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji tumeshusha gharama ya manunuzi ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa asilimia takribani 40 na kwa hiyo bei ya dawa MSD iko chini sana ukilinganisha na kwenye sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, lakini kinachosababisha tushindwe ku-take advantage ya bei ya MSD kuwa chini ni kujaribu kuongeza ufanisi kwamba pale ambapo hatuna dawa kwa kiasi fulani tusicheleweshe wananchi kupata huduma ya dawa kwa sababu tu tunataka vituo vyetu vipate dawa kutoka MSD, basi tuwape fursa Halmashauri waende wakanunue dawa kwenye sekta binafsi ili dawa zisikosekane kwa wateja pale kwenye kituo cha kutolea huduma za afya. Haya yalikuwa ni malalamiko ya muda mrefu, kabla hata sisi hatujateuliwa kwenye nafasi hizi malalamiko ya dawa yalikuwa mengi sana na Waheshimiwa Wabunge wengi walitamani Halmashauri zao ziruhusiwe kwenda kununua dawa kwenye sekta binafsi, kwa sababu kisheria hairuhusiwi kabisa lakini tumeamua kufanya maboresho ambayo yanaongeza tija na ufanisi wa MSD ili kuhakikisha tunaharakisha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakati ambapo Halmashauri zina pesa na MSD haina stock ya dawa fulani.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niwathibitishie na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla kwamba baada ya kuongeza ufanisi wa MSD, kwa sasa upatikanaji wa dawa umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 80. Kwenye Halmashauri nyingine ambazo natembelea nakuta upatikanaji wa dawa umekuwa mpaka katika kiwango cha asilimia 90, asilimia 95, dawa zote muhimu zinapatikana.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tunatoa saa 24 kile kibali cha Out of Stock (OS) kwa sababu tunataka kuongeza ufanisi kama nilivyosema. Kuliko kusema tutoe wiki nzima ndiyo tutoe kile kibali cha Halmashauri kwenda kununua dawa, maana yake tutakuwa tumewachelewesha wananchi kupata dawa kwa wiki nzima.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii kwenda kwenye 24 hours maana yake tunataka ufanisi uwe ni wa hali ya juu na wananchi wasikose dawa.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwanza napongeza TARURA kwamba wameanza kazi vizuri hususani katika Mji wangu wa Korogwe, lakini napenda kujua je, Wizara ina mpango gani sasa wa kuwawezesha hawa TARURA hususani kwenye hizi Halmashauri za Miji pamoja na kwamba wanawapa fedha za kujenga barabara zile kwa kiwango cha changarawe, sasa wapewe fedha za kutengeneza ile mifereji kwa kiwango cha kutumia mawe ili kusudi wasiweze kurudia mara kwa mara kutengeneza zile barabara? Wana mpango gani wa kuwatengea fedha ili Miji hii iweze kuwa na barabara zilizo imara kwa kupitia kuweka mawe misingi yao? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri yote ya msingi ya mwanzo yaliyoweza kutolewa. Naomba nimpongeze mama Mary Chatanda ni miongoni mwa Wabunge ambao tulipambana sana katika ujenzi wa barabara na stendi yake ya pale Korogwe Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa utengenezaji katika Halmashauri za Mji kwanza tunatumia mradi wa UGLSP ambao tunagusa takribani Manispaa na Halmashauri zote za Mji. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie Wabunge wote ambao wako katika Halmashauri za Miji na Manispaa mpango wetu mkakati ni kuhakikisha maeneo haya tunayabadilisha kwa ajili ya ujenzi katika maeneo haya kwa tabaka la lami. Huu ndiyo mpango wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika ile Miji Mikuu Saba ambayo nimezungumza tutaaendelea kuboresha suala la mifereji, suala la barabara kwa kiwango ambacho tunajua kwamba barabara zetu tunataka guarantee ya miaka 20 ndiyo tuweze kuzifanyia service, ndiyo maana hatuko katika supervision ya hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nikiri kwamba TARURA tuna mtandao wa barabara takribani kilometa 108,000 ambao ni matandao mkubwa sana, lakini ukiangalia kutokana na suala la kisera la mgawanyo wa Mfuko wa Barabara ambao asilimia 30 inakuja TARURA na asilimia 70 inaenda TANROAD, eneo hili ndilo lina changamoto kubwa. Baadaye tutaangalia nini cha kufanya, lengo letu kubwa ni kwamba Halmashauri zote ziweze kupitika kwa sababu wananchi huko ndiko uchumi unapojengeka. (Makofi)
MHE. MARY P.CHATANDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kwa kutukumbuka Korogwe, Kilindi na Mkinga kwamba mwaka huu wa fedha watatupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Swali la nyongeza, kwa kuwa vile vile Mahakama hizi zimekuwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi hususan Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutupelekea Mahakimu Mahakama za Mwanzo Korogwe Mjini na Vijijini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU:
Mheshimiwa Spika, kabla sijamjibu swali lake napenda nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kwa hatua madhubuti ambayo wameianza ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo ya Mnyuzi na hivi sasa najua wanasubiri tu ramani kuanza ujenzi huo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu lini tutawapelekea watumishi kwa maana ya kada ya Mahakimu, nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pale ambapo tutakuwa tuna uwezo wa kibajeti wa kuweza kufanya kazi hiyo tutafanya, kwa sababu tumeanza na ukarabati wa miundombinu, basi jambo hili likikamilika pia tutaona namna ya kuweza kuongezea watumishi katika Mahakama za Korogwe ili nao waweze kupata huduma hii ya Kimahakama. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sikubaliani na majibu ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, hayaridhishi kabisa. Ukiangalia kwa mtiririko ulioko kwenye majibu haya imesema wazi mwaka 2006/2007 walifanya upembuzi na kugundua kwamba shilingi bilioni kumi na tatu ilihitajika kwa ajili ya mradi huu lakini wakafanya upembuzi tena mwaka 2014/2015 ikaonekana shilingi bilioni 1.54 zilitakiwa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hili lakini bado wakafanya mwaka 2015/2016 wakatenga milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walitenga fedha hizi shilingi milioni 800 hazikutoka, halafu mwaka 2016/2017 hawakutenga fedha…

… 2017/2018 hawakutenga fedha, sasa ni kwa nini wanazungumza uongo? Kwa nini hawakutenga fedha katika miaka miwili hii ambayo imo mpaka bajeti ya safari hii wanazungumza…

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali haioni sasa kwamba kutokutekeleza mradi hii hawawatendei haki wananchi wa Wilaya ya Korogwe hususan Manga Mkocheni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya shemeji yangu Mheshimiwa Mary Chatanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeonyesha taratibu mbalimbali zilizofanywa na Serikali na kwamba utendaji lazima tufuate tathmini ya wataalam. Sisi kazi yetu ni kutunga sera na kupitisha bajeti, lakini utekelezaji unazingatia taarifa za wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu la msingi nimesema kwamba utafiti wa awali ulionesha kwamba bwawa lingejengwa kwa shilingi bilioni 13; lakini tathmini ya kimazingira ikaonyesha kwamba bwawa hilo lingejengwa lingezamisha baadhi ya maeneo na vijiji vya wananchi wa Manga, tusingeweza kufanya hivyo. Kwa hiyo, Tume ya Umwagiliaji kupitia Mkoa wa Kilimanjaro wakafanya tathmini nyingine upya ambayo kama ingetekelezwa basi hayo maeneo ambayo yangeathirika na bwawa yasingekuwemo, ndiyo maana bajeti sasa ikaja shilingi bilioni 1.5, hilo ndilo jibu la msingi. Lakini bado tumetenga shilingi milioni 800 mwaka uliofuata 2014/2015 lakini kwa bahati mbaya bajeti haikutoka ndio maana utekelezaji haukufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba malengo yetu ni kuhakikisha tunajenga hili bwawa na ndio maana Serikali ya Chama cha Mapinduzi...

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: ...imeunda Tume ya Umwagiliaji ambayo sasa kazi yake itakuwa ni kusimamia moja kwa moja suala la utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi hakuna haja ya hasira kazi hii tutaifanya na wananchi wa Manga watapata huduma wanayoihitaji. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa niulize swali la nyongeza. Katika jibu la msingi la Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba Teaching Allowance ipo kwenye mshahara. Sasa tunapata tabu sana tukikutana na Walimu wanapotuambia juu ya kurudisha Teaching Allowance. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kutamka ndani ya Bunge hili ili waweze kutambua kwamba Teaching Allowance yao iko kwenye mshahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo kubwa tulilokuwa nalo ambalo Waheshimiwa Wabunge wengi sana hapa leo wanalizungumza ni suala zima la maslahi mapana ya watumishi. Ndiyo maana hata hicho kilichokuwepo kama kidogo au kikubwa hakioneshi vizuri ni kwa sababu huenda lile fungu lenyewe, purchasing power imekuwa ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma, juzi juzi kulikuwa na kikao maalum kinafanyika kwa sababu kunaundwa bodi maalum ya kuja kupitia maeneo yote hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha Teaching Allowance, kuna mambo mengine; kuna suala la haki za watu wanaofanya kazi katika mazingira magumu. Kwa hiyo, jambo hili tutakuja kulitamka rasmi sasa baadaye kuhusu mchakato huu unavyokwenda. Hiyo Bodi iliyoundwa sasa kupitia mishahara, siyo kwa Walimu peke yake, isipokuwa watumishi wote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tutaona jinsi gani kila mtumishi atapata stahili yake na nyongeza kwa kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili tutakuja kulitoleaa tamko rasmi hapa baadaye Bungeni likiwa katika utaratibu mzuri baada ya kutoa hii documentation vizuri.