Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Stephen Hillary Ngonyani (15 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipo. Kwanza nianze kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Korogwe Vijijini kwa kuniamini na leo nipo hapa kwa mara ya pili Mungu awabariki sana, sitawaangusha, nitafanya kazi kwa jinsi walivyonituma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nataka nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Mawaziri, safari hii wametupa nguvu ya kuonesha kabisa kwamba safari hii hapa ni kazi tu. Naomba kazi hii isiishie mijini iende vijijini ikaangalie kero za
wananchi.
Mimi nitajikita katika mambo matatu au manne makubwa. Sasa hivi Serikali ya Mheshimiwa Pombe Magufuli imeamua kufanya kazi, lakini naomba sana Serikali ihakikishe inamaliza kwanza zile ahadi za nyuma ambazo zilitolewa kwa wananchi. Kwa mfano, sasa hivi
watu wana mpango wa kujenga Bandari ya Bagamoyo, wangeacha kwanza Bandari ya Bagamoyo wangezijenga Bandari za Tanga pamoja na Mtwara ili iwe kiegesho kikubwa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiyafanya haya Watanzania watatuelewa vizuri sana. Hatuwezi kila siku kuwa tunaanzisha vitu halafu vinaishia njiani. Kwa mfano, suala la reli, reli ni kitu muhimu sana kwa Watanzania, lakini inaangaliwa sana reli ya kati, inaachwa reli ya kutoka Tanga kwenda Arusha kwenda Musoma. Huko pia kuna maeneo ambayo wananchi wanafanya biashara, wananchi wana mizigo wanataka kubeba, wananchi wanataka kuona na wao wanapanda treni kama wanavyopanda wenzetu wa kati. Hii Tanzania ni moja, Watanzania ni wamoja, wakati wakiwa nje tunakuwa tofauti, lakini tukiwa hapa ndani wote tunatetea haki za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nataka tuzungumzie mambo ya viwanda. Sasa hivi tunasema kwamba Tanzania ya viwanda, lakini kuna viwanda vingi vimekufa hakuna mpango wa aina yoyote ambao unaweza kuanzishwa naomba tusijenge viwanda vingine tuanze kwanza kuvifungua viwanda vya Mponde ambavyo vimefungwa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawapati chai, chai hakuna mahali pa kuipeleka, Watanzania wamekosa kabisa kuamini. Naomba kwanza tuhakikishe tunawafungulia viwanda Watanzania, vile vilivyokuwa vimefungwa kule Tanga, kwa mfano, Kiwanda cha Chuma,
Kiwanda cha Omo, Kiwanda cha Mbao na viwanda vingi mpaka Kiwanda cha Blanketi kimefungwa. Sasa leo tukisema tunataka kuanzisha viwanda, wakati vya zamani bado, naomba kwanza Serikali yangu Tukufu, naipenda sana na safari hii imetupa nguvu sisi Wabunge, tunafanya kazi kwa kujiamini, wahakikishe kwanza vile viwanda vya zamani vyote vinaamshwa na Watanzania wengi wanapata kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la mama ntilie na vijana. Serikali ya Mheshimiwa Pombe Magufuli iliamua kwamba, mama ntilie na hawa wanaofanya biashara ndogo ndogo wasishikwe ushuru. Sasa hivi inashangaza sana, watu badala ya kushika ushuru
mkubwa mkubwa katika maeneo, wanawakimbiza watu wa bodaboda na mama ntilie na wale akinamama ambao wanauza hata vitu vidogodogo, nyanya pia mtu analipa risiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye Jimbo langu aliwahakikishia Watanzania wanaoishi Korogwe kwamba ushuru mdogo mdogo utafutwa, lakini cha kushangaza watu wanauona huo ushuru mdogo mdogo wa kuwasumbua Watanzania wa hali ya chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali hii, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mchezaji wangu wa mpira, anajua kabisa kero hizo kwa sababu huko kote tulizunguka naye na hata kwenye Jimbo langu alifika kunifungulia shule. Naomba sasa wale wanaoshika ushuru
mdogo mdogo waache, kwa sababu wakifanya hivyo na sisi Wabunge tuna nguvu sana ya kujenga hoja hapa ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara ni suala muhimu sana. Kuna barabara ambayo toka mwaka 2010, Serikali ya CCM tulisema kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami, naomba iangaliwe sana hii barabara ya kutoka Korogwe kupitia Bumbuli kwenda mpaka Soni ili
iwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile katika suala la maji, tusianzishe miradi mingine, kuna mradi mkubwa wa kutoka Kilimanjaro kuja mpaka Mkoa wa Tanga kupitia Kata ya Mkomazi na Tarafa ya Mombo. Naomba Waheshimiwa Mawaziri mliopo, ni majembe ambayo tunayaamini kabisa, safari hii hakuna tena lelemama ni kazi, naomba mradi ule umaliziie ili Watanzania tuendelee kuipenda, maana sasa hivi Watanzania wote wanaipenda Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa nini? Kwa sababu ya Jembe Magufuli. Sasa kwa haya naomba pia tuhakikishe kwamba tunakamilisha bila tatizo la aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme ni muhimu sana. Mheshimiwa Profesa mwenzangu Muhongo umeshaniahidi leo hapa, nimekufuata kwako umeniambia vile vijiji vyangu vyote vilivyokosa umeme, safari hii vinapata umeme vyote. Sasa isiishie tu katika
mazungumzo yetu ya mimi na wewe, maana hapa tupo maprofesa wawili tu tuliohitimu kama wewe, naomba unikamilishie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niyaseme haya kwa sababu, leo hapa tumekuja kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Pombe Magufuli. Naamini kabisa Watanzania wanataka kuona Tanzania ile ya juzi
siyo Tanzania ya kesho. Nikiongea mpaka kesho sitakuwa na lolote la maana la kuwasaidia ila ni kuiomba Serikali yangu kwamba yale yote yaliyoahidiwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, tuyatekeleze kwa kipindi ili mwaka 2020, tuteremke tu maana safari hii tumepata shida kweli kweli. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kuniona. Vile vile naanza kwa kuwapongeza Wabunge wenzangu kwa kazi nzuri ya kutoa michango katika hii hoja ya Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyokuwa Dar es Salaam nilisema huu Mpango wa Serikali ni mzuri sana. Ni mzuri sana kwa Watanzania wote! Nilivyokuwa Dar es Salaam nilisema sitaunga mkono hoja. Ni kwa nini sitaunga mkono hoja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango umeelekeza kwa Tanzania nzima jinsi itakavyopanga Serikali yetu ambayo tunaipenda sana ya Awamu ya Tano. Nataka tu Mawaziri watakapokuja waniletee majibu ya sehemu hizi ninazotaka kujua. Maana ya viwanda, maana ya reli na maana ya bandari. Unaposema kwamba tutaimarisha Bandari za Tanzania, moja ya bandari ni bandari ya Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Tanga toka nimeanza kuisikia kwenye vyombo vya habari na toka nimeanza kuisikia hapa ndani ya Bunge hili kwamba kutajengwa Bandari ya Mwambani, tutarekebisha bandari zilizopo sasa hivi, lakini cha kushangaza, inayong‟ang‟aniwa ni Bandari ya Dar es Salaam peke yake. Hizi bandari nyingine zina matatizo gani? Fedha inayotumika ni ya Serikali, siyo kwa ajili ya Bandari ya Dar es Salaam peke yake! Ni bandari zote za Tanzania zirekebishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukaa meli sana Dar es Salaam siyo faida! Kuna Bandari ya Mtwara ambayo unaweza kupeleka meli na ikatoa mizigo ya aina yoyote. Kuna Bandari ya Tanga unaweza kutoa meli ukatoa mizigo yote, lakini tunang‟ang‟ania tu Bandari ya Dar es Salaam, meli zinakaa pale mwezi, wakati kuna bandari nyingine zenye kina kirefu, hakuna chochote kinachoendelea! Hii hatutendewi haki! (Makofi)
Tunapozungumzia reli, reli zote ni kwa faida ya Watanzania, lakini unaponiambia kwamba barabara zitatengenezwa na zitaimarika; zitaimarika namna gani kama reli zenyewe ambazo tumeanza kuziongolea toka sijaingia Bunge hili mpaka leo hii hazitengenezwi? Hiyo barabara itakayokuwa nzuri ambayo mabasi yatakuwa yanapita na magari madogo bila kuumia ni ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu Tukufu, sikivu, hebu jaribu kuiangalia na reli inayotoka Tanga, kupitia Kilimanjaro, kupitia Arusha na kwenda mpaka Musoma. Mwaka 2012 tumeijadili hii reli kwamba itajengwa lakini tunashangaa zinajengwa reli ya kati tu, lakini huku kwingine zikikorofisha kidogo zinarekebishwa. Reli hii ya Tanga mpaka Arusha mpaka Musoma, hata kuisikia kwenye vyombo vya habari, hatuisikii! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania haijengwi na reli ya kati peke yake, Tanzania haijengwi na mikoa ya kati pekee, Tanzania inajengwa na mikoa yote ya Tanzania ili mtutendee haki. Serikali hii ambayo ni sikivu inayoendelea kutumbua majipu, hebu angalieni na mikoa hii mingine ambayo mlituahidi wenyewe na tukaunga mkono kwa dhati kwamba tunachohitaji ni maendeleo. Maendeleo haya hayatapatikana kwa reli ya kati peke yake! Barabara zinazotoka Arusha kwenda Dar es Salaam, kila siku zinakarabatiwa, kwa nini? Kwa sababu reli ya Tanga haifanyi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri katika mipango yake yote, hebu jaribuni kurekebisha hizi reli nyingine ambazo hamzipi kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye viwanda. Siku za nyuma, mikoa mitatu ndiyo ilikuwa na viwanda vingi sana hapa Tanzania; Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na Tanga. Cha kushangaza, tunasema tutajenga viwanda vipya, hatukatai. Ni mambo mazuri ya Serikali kwa sababu ya kuwasaidia Watanzania ili wapate kazi. Je, viwanda ambavyo vimekufa mnaviweka wapi? Kwa mfano, kuna kiwanda cha General Tyre Arusha, Kiwanda cha Kahawa pale Moshi na viwanda vilivyoko katika Mkoa wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga kulikuwa kuna viwanda vyenye msimamo! Kuna Kiwanda cha Chuma, Kiwanda cha Mbolea, Kiwanda cha Foma, Kiwanda cha Mablanketi, Kiwanda cha Mashati, kulikuwa na Kiwanda vilevile cha kutengeneza Mbao, Sikh Saw Mills, kulikuwa na kiwanda pale Mkumbara cha kutengeneza chipboard, kulikuwa kuna Viwanda vya Chai ambavyo mpaka leo hii havijafunguliwa. Serikali imeahidi itavifungua, kwa mfano kiwanda cha Mponde, lakini hakuna! Sasa tukifanya haya mambo, tunafanya mambo tu, halafu sisi tukirudi huko nyuma ndiyo tunahukumiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hapa leo tunaongea sana lakini Wabunge wakirudi nyuma watakiona chamoto. Naomba Serikali sikivu, mviangalie hivi viwanda. Leo hii tunaambiwa Kilimo Kwanza, nimekubali lakini nataka mniambie hawa wananchi wa Mkoa wa Tanga watalima wapi, wakulima wa Moshi watalima wapi, wakulima wa Morogoro watalima wapi; kwa sababu maeneo mengi yamehodhiwa na watu wachache na hao watu wachache waliohodhi hayo mashamba hawayaendelezi badala yake ni ya kukopea mikopo kwenda kununua magari ya kisasa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama watu wanakopa mikopo kwa ajili ya kununua magari ya kisasa na wamekopa kwa ajili ya kuendeleza kilimo, kilimo hicho hakiendelezwi, wananchi wanaambiwa kilimo kwanza, wakati mashamba yale ambayo wangeyategemea wananchi wa chini kulima, yamehodhiwa. Ukilima pale, mtu anakuja nyuma yake, anakupeleka Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ni rafiki yangu na nampenda, anafanya kazi kwa dhati. Bahati nzuri Mawaziri wote mlioingia safari hii, hakuna Waziri mwenye shida. Wote mmeamua kumsaidia Mheshimiwa Magufuli. Haya mambo tunayoyaongea ni ya msingi sana ili kuiona Tanzania siyo tegemezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumzia masuala ya umeme, ni kitu muhimu sana kwa Watanzania, lakini nataka niulize, huu umeme wa mafuta wenye gharama kubwa tunaoukazania, kwa nini msiendeleze kituo cha Hale, Kihansi na pale Achemka ambapo ni umeme wa maji? Maji yapo! Ni lini mmesikia Mto Ruvu umekwisha maji? Kama tatizo ni maji, Mto Ruvu ni lini umekauka maji? Kwa sababu tunategemea tu kwamba tutumie mabilioni ya pesa! Hawa watu wa Symbion wanaokuja kutupa masharti magumu, tumshukuru Mheshimiwa amesema safari hii hatutegemei wafadhili, tunajitegemea sisi wenyewe. Sasa kama tunajitegemea sisi wenyewe tujaribu kupunguza gharama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hivi vituo vya nguvu za umeme ambavyo vinatoa nguvu za umeme kwa kutumia maji ambayo gharama yake ni nafuu. Tungeviongezea engine. Kama ni mashine, basi ziongezewe mashine kuliko kutumia umeme unaotokana na mafuta ambapo hao watu wanatupiga bei mara mbili. Watanzania wanakaa katika wakati mgumu kwa kuwalisha watu wachache ambao wanataka kuja kutuhukumu leo kwamba hawatatupa misaada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, vitu muhimu sana ambavyo tunaweza kufanya; wananchi wa Tanzania wanategemea sana kilimo, lakini hivi leo ninavyokwambia, hakuna sehemu ambayo Watanzania wanaweza kulima. Siyo kwamba nchi hii haina ardhi, ipo; lakini ardhi hii inakuwa ya masharti kama tuko Kenya. Imehodhiwa na mtu kwa manufaa yake. Nashukuru safari hii Waziri wa Ardhi, unafanya kazi nzuri sana, lakini usiangalie mikoa ya huko tu, angalia na Mikoa ya Mashariki yako. Anza Morogoro, njoo Pwani, nenda Tanga, nenda Kilimanjaro, nenda mpaka Arusha, ili ukitoa maamuzi, utoe maamuzi! (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, wengine wakati wa nyuma walikuwa hata ukiwapigia simu hawapokei, lakini wewe unapokea. Sasa kama unapokea, umefanya kazi nzuri kwa muda mfupi. Njoo uangalie mashamba, misitu ya kule Tanga ambayo wananchi wanalalamika sana kwamba, hawana mahali kwa kulima, lakini mashamba hayo yamekopewa fedha. Ukienda ukilima, kesho mtu anakuja kupanda zao lake, anakwambia hapa siyo kwako. Sasa kama siyo kwangu, nimekaa miaka 50 hapa siyo kwangu kivipi? Eti kwa sababu ni mtu ambaye ana uwezo. Sasa hawa waganga wa kienyeji wasiokuwa na uwezo watalima wapi? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuangalie, naamini kabisa Serikali ya safari hii ni sikivu. Mawaziri mnafanya kazi nzuri sana nami naendelea kuwapongeza. Ukimwona mtu anamsema vibaya Waziri ana matatizo ya akili, kwa sababu Mawaziri mko wachache na nchi ni kubwa, hamwezi kwenda kila kona kwa muda mfupi. Kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba, tushirikiane nasi Wabunge hapa wote, usijali itikadi ya mtu; twendeni mkaone mazingira ya Majimbo yetu na mtoe maamuzi kama anavyotoa Mheshimiwa Lukuvi pale kwa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme hili, kwa sababu sisi kule Tanga na Mikoa ya Mjini huku tunapata shida sana. Kama tunapata shida sana, hakuna mahali kwa kuongelea masuala haya ila ni hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu Mheshimiwa Waziri wa Barabara ajue kwamba Jimbo langu barabara zote zimefungika, watu wamekaa kwenye visiwa na maji yameingia kwenye nyumba za watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali Tukufu hii iende ikaangalie Mkoa wa Tanga ulivyopata mafuriko makubwa. Wabunge usione tumekaa hapa, tumekaa kwa ajili ya kuchangia hoja hii tusije tukaonekana Wabunge wa Mkoa wa Tanga ni watoro. Siyo watoro lakini kwetu huko kumeingiliwa, hakuna mahali kwa kuwatetea Waheshimiwa Wakulima wetu, pamoja na Wajumbe wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu awasaidie sana na amsaidie sana Spika wa Bunge hili kwa kazi nzuri aliyotufanyia safari hii. Meza tunayokaa utafikiri tupo Ulaya, kumbe tupo Tanzania. Ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa neno la ahsante na vilevile sitafanya vizuri kama sitawashukuru Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mjumbe wa NEC. Nataka niwaambie, siendi kufuata riziki, naenda kuwatetea ninyi wana-CCM wenzangu, hakuna kukatwa Mbunge wa aina yeyote. Niko tayari kutoa chozi la mwisho kwa ajili ya ninyi Wabunge kuwatetea kule. Tulikuwa tunafanywa kama wanyonge lakini nataka niwaahidi, siendi kwa ajili ya biashara, naenda kwa ajili ya kuwatetea ninyi ndugu zangu Wabunge, Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nianze kuwashukuru wapiga kura wangu kwa kuniamini. Pamoja na kwamba nilikuwa nafanya kazi katika mazingira magumu, nilikuwa naumwa lakini waliniamini na leo hii nimekuwa mwakilishi wao tena, naomba Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya, Naibu Waziri wake pamoja na Naibu Waziri wa TAMISEMI. Nawashukuru sana kwa kazi nzuri mnayoifanya. Usiposhukuru kwa kidogo, hata kikubwa ukipewa hutashukuru. Nawashukuru kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wameweza kuja kwenye Jimbo la Mkoa wa Tanga mara chungu nzima na kujua kero za wananchi na wakaamua kuzifanyia ufumbuzi wake. Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru sana viongozi wa Wizara ya Afya; bila ninyi Wizara ya Afya, leo hii hapa ndani ya Bunge hili asingekuwepo Stephen Ngonyani, mlinitetea sana, mkanipeleka India na leo nimerudi. Pamoja na kwamba naumwa, lakini Wizara ya Afya ni Wizara mama sana, inatakiwa tuiangalie kwa macho yote. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu ambavyo vinatakiwa viangaliwe kwa macho yote ni Wizara ya Afya. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu Wizara ya Afya, hata kama utakuwa unafanya kazi ya aina yoyote, bila kuwa na afya njema hakuna chochote cha maana ambacho utaweza kufanikiwa nacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza Serikali, zile hospitali za Mtwara, Tarime na Dar es Salaam ambazo hazijakwisha, kwanza itengwe pesa ili Serikali ihakikishe zile zahanati au vituo vya afya au hospitali zinakwisha, kwa sababu tutaendelea kujenga hospitali nyingi lakini ziko ambazo wananchi wenyewe waliamua kuzianzisha, lakini hospitali hizo zimefika ukingoni, hazipati msaada wa aina yoyote, hasa kule kwa ndugu yangu Mheshimiwa Matiko, naomba ziangaliwe sana ni vitu muhimu sana hivyo. (Makofi)
Ndugu zangu, kumekuwa kuna mchezo hapa, ambapo mtu akishaanza kuchangia anataka kujifananisha na Waganga wa Kienyeji. Why!
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma hapa nataka niwaambie ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hakukuwa na hospitali hata moja; mlikuwa mnatumia tiba asili, tiba mbadala. Leo hii kila atakayefanya makosa; jana Askari Polisi, hapa Askari wa Magereza na Askari wa Jeshi mmewafananisha kwamba wakikosa kazi watakuwa Waganga wa Kienyeji. Hii ni biashara kweli mnafanya hapa? Ndicho kilichowaleta kuchangia! jaribuni kubadilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganga wa Kienyeji ni fani kama fani nyingine. Msiwaweke Waganga kama ni watu dhaifu sana. Niliyeko hapa nina hospitali Nairobi. Hulazimishwi kumtibu mtu. Mtu anakuja kwa kupenda kwake. Ninyi mnakuja kututolea mifano hapa! Wakati wa uchaguzi mpo milangoni kwetu! Inakuaje? Wakati wa uchaguzi mko milangoni kwetu, leo hapa mnakuwa ndio watu wa kuwatolea mifano Waganga wa Kienyeji, kwa nini! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msiwadharau watu ambao usiku mko majumbani kwao. Nashangaa! Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili, Tiba Mbadala Tanzania. Hatuwezi kukaa hata siku moja tukaja kusema ni namna gani tunaweza kutatua tatizo la tiba asili, tiba mbadala! Badala ya kutaja kwamba hospitali zenu zinakosa dawa, ninyi mnaona fani kutaja Waganga wa Kienyeji. Inawasaidia? Hivi ninyi hakuna aliyekwenda kutibiwa hapa! Msiseme haya mambo ya kininii hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanzia leo, msitufananishe. Mkichangia, changieni hoja zenu. Msiwafananishe watu ambao usiku mko majumbani kwao mnakwenda kutibiwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yamepita jamani, yamepita. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina hospitali nyingi sana ambazo zinahitaji zipatiwe upembuzi na tiba. Leo hii kuna matatizo ambayo yanakwenda katika mahospitali. Kuna hospitali nyingi Madaktari wenyewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini kuna watu ambao sio Madaktari, wakifika pale wanaharibu kabisa taaluma ya Madaktari wetu.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atuambie kuhusu wale watu ambao wanavaa nguo za manjano ambao sio Madaktari, lakini wanajifanya ni Madaktari, wanachukua pesa za wapiga kura, pesa za walalahoi halafu dawa hawapati, matokeo yake fani yote ya Madaktari wanapewa majina mabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo Muhimbili, nilitibiwa vizuri na Madaktari mabingwa wa pale, lakini kuna watu wamevaa vinguo vya manjano eti wasaidizi wa Madaktari ukifika pale wanakupokea wao, hao watu waandikeni namba kwenye mashati yao ili tuwajue. Mkifanya namna hii mtafanikiwa sana na hamtakuwa mnapata matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ndugu zangu tusiendelee tu kuangalia, mwangalie dawa. Dawa ni kitu muhimu sana kwa Watanzania. Leo hii hospitali nyingi hazina dawa na tatizo ni kwamba siyo ninyi, huko nyuma watu walikuwa wanapeana uongozi. Huo uongozi walivyokuwa wanapeana, imefika mahali mtu anakwenda kuchukua dawa feki ilimradi hela zinaingia mfukoni mwake halafu tunakuwa hatupati chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aangalie kabisa; anapasua majipu, amepasua majipu vizuri sana, lakini aangalie watu wengine, wanunuzi wa madawa hawa; wanunua dawa zinakwenda wapi? Dawa zinaonekana zimetoka MSD zimekwenda mikoani, mikoani hazijafika, ziko kwa akina nani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niyaseme hayo, lakini naomba kitu kingine. Hospitali yangu ya Korogwe ni hospitali kubwa sana, ina mikoa karibuni mitatu, Mkoa wa Pwani, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Kilimanjaro. Kila ajali inayopatikana barabara kubwa wagonjwa wote wanaingia pale Magunga Hospitali, lakini inatengwa sana hii hospitali. Ni kwa sababu gani? Kama Tumbi imekuwa hospitali teule, kwa nini Korogwe isiwe hospitali teule na kila kigezo kiko tayari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuangalie na sisi watu wa Tanga; Mheshimiwa Waziri anatoka Tanga. Yeye anafanya mambo makubwa sana kwenye mikoa mingine, hata Mkoa wake! Amekuja kwangu mara tatu na amefanya kazi kubwa, ametoa madawa, ametoa mashuka hebu apandishe hadhi. Mheshimiwa Simbachawene yupo. Nilikuwa niombe hilo na kwa sababu ana Makamu wake makini na anafanya kazi kwa kujitolea sana, hebu fanyeni kazi mhakikishe kwamba Tanzania hii kwanza mwongezewe pesa, mlizotengewa hapa ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufatana na mazingira ya sasa, miaka ya nyuma watu walikuwa milioni 12 wakaja kuwa milioni 25 sasa hivi ni milioni 48, milioni 48 kwa mabilioni haya mnayoyatenga, watu watatosheka kiasi gani? Hebu tubadilike! Kama kweli tunataka kuisaidia hii Wizara ya Afya, bajeti hiyo ni ndogo, iongezwe ili dawa ziende na mashuka yaende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta hospitali nzuri haina vitanda, haina shuka, haina Madaktari. Madaktari pia ni watu wa kutakiwa waonekane sana.
Wengine mnafika mnawatukana Madaktari. Mnawatukana kwa lipi, wakati mgonjwa umekuja pale, umemkuta Daktari ana mgonjwa mwingine; unataka atolewe mgonjwa mwingine aingizwe babu yako eti kwa sababu ni ndugu yake na Maji Marefu. Naomba hili tatizo Mheshimiwa Waziri aliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha yupo hapa, hebu bwana mipango rafiki yangu, ongezeni pesa pale. Mnasema kilimo, maji, umeme, lakini hakutakuwa na umeme bila kuwa na afya; hakutakuwa na elimu nzuri bila kuwa na afya; hebu tuyamalize haya. Tukiyamaliza haya, mambo mengine yote yatakuja. Tufanye vitu vichache ambavyo vitasaidia, watu wataviona kwamba, vimekamilika kuliko… (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja

iliyoletwa hapa mezani na aliyoyaongea yote Mheshimiwa Waziri Mkuu nimpongeze sana kwa kazi nzuri wanayoifanya Serikali hii ya Awamu ya Tano. Vile vile nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba kumbe inawezekana. Amefanya mambo makubwa na yameanza kuonekana ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania. Mungu ambariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa suala la reli. Reli ni kichochea kikubwa sana cha uchumi Tanzania, lakini niombe, sitashika shilingi tena kama mwaka jana; mwaka jana nilishika shilingi kwa ajili ya reli ya kutoka Tanga-Arusha
– Musoma ila nataka Waziri husika katika suala la reli ahakikishe safari hii hakuna haja ya kushikiana shilingi atuambie; tunahitaji standard gauge lakini huwezi kujenga zote kwa wakati mmoja, lakini ni namna gani reli ya kutoka Tanga kupitia Kilimanjaro, Arusha na kwenda Musoma itaanza kazi ili na sisi mizigo yote ambayo ilikuwa inatoka katika bandari ya Tanga ifanye kazi nzuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Bomba la Mafuta, tumshukuru sana Rais. Bomba la Mafuta lingeweza kwenda mkoa wowote lakini limeletwa Tanga kutoka Uganda. Naomba sana Serikali hii sikivu wajaribu sana Watanzania wapate kazi pale, ule mtaji wa kwamba Watanzania wanalishangilia bomba la mafuta wanaokuja kufanya kazi ni Wakenya uwe sasa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kawaida ya watu wanatengeneza biashara kama hizi vijana wa Kitanzania hasa wa Mkoa wa Tanga na jirani na wanakopita Bomba la Mafuta hata kuchekecha zege watolewe watu Kenya, hata kushika lile toroli mtu atoke Kenya! Safari hii haiwezekani, wakija kwetu watu wa namna hiyo tutawafukuza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu msikivu sana, kuna Watanzania waliamua kujenga shule za kata; shule za kata zimejengwa maabara nyingi na Watanzania wenyewe kwa nguvu zao wenyewe. Naiomba sana Serikali, kwa sababu tunataka watoto wetu
wasome tuangalie ni mazingira gani watatengewa fedha, zile sehemu zote ambazo wananchi walitumia nguvu kubwa sana kujenga maabara za kata katika shule za sekondari watenge fedha ambazo watamalizia nguvu za wananchi wenyewe walioamua kujitolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nimeona niliseme kwa sababu wananchi waliamua wenyewe kujenga shule za kata lakini mpaka leo hii kuna magofu ya ajabu sana katika shule za kata, hakuna mahali ambapo utaenda utakuta maabara, na vijana wengi lazima waingie kwenye maabara kujifunza sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la REA ni suala la msingi sana katika Tanzania. Tunategemea sana kwamba umeme utakwenda vijijini, lakini cha kusikitisha utashangaa kuona REA tulipewa taarifa kwamba katika kila wilaya kutakuwa na vijiji ambavyo vitapata REA na tukashukuru sana. Hata hivyo, hatua ya mwisho unakuja kuambiwa vijiji vile vimekatwa, wananchi wanaanza kulalamika kwamba Waheshimiwa Wabunge hatuwatendei haki, kwa nini vijiji fulani vimekatwa na ni kwa nini mlituambia kwamba vijiji hivi vitapata REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye simu yangu hapa, ukinunua bando unaambiwa umekatwa shilingi fulani za kwenda kwenye REA. Ukiwauliza watu wanaosimama kujenga au waliopata contract za kusambaza umeme wanakwambia hatujalipwa. Sasa najiuliza hii hela inayokatwa kwenye simu hii ambayo inaonesha kabisa inaenda kwenye REA, sasa inakwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri husika, Mheshimiwa Waziri Mkuu vijana wake wamekuja Jimboni kwangu Mawaziri zaidi ya kumi (10) na nawashukuru sana wamenifanyia kazi nzuri sana. Wamekuja wametoa fedha nyingi sana; na kwa sababu katika Tanzania Korogwe ni wilaya ya kuigwa kwa sababu tukipewa hela chache tunafanya kazi kubwa na chenchi inabaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mziangalie zile wilaya ambazo zina uchungu na fedha ya Serikali kwa macho yote ili mtusaidie kutengeneza zile sehemu ambazo zimeanza. Leo tunajenga kule vituo vya afya, kuna vituo vya afya vizuri na kuna shule za sekondari nzuri ambazo hata Waziri wa Elimu, Waziri wa Nishati, Waziri wa Ardhi, Waziri wa Kilimo, Waziri wa Maji, Mawaziri karibu wote wamekuja pale na wameona. Naomba sasa ...

T A A R I F A . . .

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Tena nimeipokea kwa mikono miwili ahsante sana ndugu yangu.

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Naipokea, tena kati ya watu ambao wamenisaidia sana Wizara ya Nishati ni huyo Naibu Waziri.

Alifika akafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kwenye upande wa Maji. Taarifa zote nimezipokea, ya huyu niliipokea kwa vizuri na Mheshimiwa Waziri kwa sababu amefika mpaka jimboni kwangu na amelizungukia jimbo lote na ameona haya matatizo, zote nazipokea na ninaomba Serikali izifanyie kazi. (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana unilindie muda wangu, umeona wengine hapa, haya. (kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la REA nafikiri wenzangu wamenisaidia na Waziri amenisaidia, tuje kwenye upande wa TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili TARURA ni kama jipu, tulilipendekeza sisi hapa kwamba TARURA itufanyie kazi sasa ipewe kazi ya kutengeneza barabara lakini mpaka leo hii kwangu hawajatengeneza barabara hata moja. Kuna daraja limekatika kutoka Kwa Sunga kwenda Mswaha darajani, miezi tisa daraja halijajengwa hata kujengwa tunaambiwa kuna TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Korogwe unategemea sana Mji wa Mombo kupata fedha ya kuendesha Wilaya ya Korogwe, lakini leo hii mtu aende mpaka Mombo akaangalie barabara zilivyo leo tunaambiwa kuna TARURA, hawa TARURA ni mtu binafsi? Kama ni chombo ambacho kimeundwa kwa ajili ya kusaidia Serikali ina tatizo gani kwenda kutengeneza barabara ambazo zimekufa? Ni nini kinazuia wakati kuna fedha tayari wameshatengewa na Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii TARURA naomba ieleweke kabisa kwamba TARURA pamoja na kwamba wanadai kwamba wametengewa fedha hizo fedha ziko wapi? Kama zipo kwa nini hawatengenezi barabara za vijijini? Tumeziondoa kwenye Halmashauri kwa sababu walikuwa wanataka sana ten percent, tukawapa TARURA ambao hawaingiliwi na mtu yeyote. Sasa kama hawaingiliwi na mtu yeyote, fedha zikae mifukoni mwao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la maji, suala hili ni kigezo kikubwa sana kwa sisi Watanzania, Mbunge yeyote atakayefika jimboni kwanza unaulizwa maji. Kuna maji toka mwaka 2010 ambayo yanatoka Mkoa wa Kilimanjaro, Bwawa la Nyumba ya Mungu, hili mpaka leo hatujui yameishia wapi. Tunasikia tu mradi unaendelea, mradi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi ya Benki ya Dunia, tangu mwaka 2010 mimi naingia Bungeni mpaka leo imesimama. Leo tunasema maji vijijini haya maji vijijini wanapata kina nani? Naomba sana Serikali ile miradi yote ambayo imeanzishwa na baadhi ya viongozi wamepita na kui-support naomba ikamaliziwe kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata shida sisi Wabunge, unafika mahali unawaambia maji yanakuja, unakwenda siku ya pili wanakwambia maji yako wapi? Unafika mahali unawaambia barabara ya lami kutoka Korogwe kwenda Lushoto kupitia Bumbuli itatengenezwa, mwaka wa 10 huu mtu anakuangalia anakwambia barabara ichongwe. Unafika barabara za vijijini zimekufa; unafika suala la vituo vya afya; tunawashukuru sana Serikali hii imetenga fedha taslimu kwenda kwenye madawa kwenda kwenye vituo vya afya, lakini kuna vituo vya afya vingine vimeshaanza kuleta nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Hospitali ya Magunga ya Korogwe, ndiyo hospitali kubwa katika barabara kuu hii, haina gari. Magari yalikuwepo yamekufa na ndiko kwenye ajali kubwa zinazopatikana barabara ya kutoka Chalinze kwenda Kilimanjaro, wanapitia pale, hakuna gari. Naomba Serikali iiangalie Korogwe kwa macho ya ukunjufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la katani. Katika mazao makuu ya biashara katika Tanzania yamewekwa manne, naomba liwekwe na katani. Katani ni zao kubwa ambalo limeingiza fedha, sisi wengine Tanga tumekwenda mwaka 1961 tukiwa manamba tumefuata Katani. Katani ilikuwa inaingiza fedha kuliko zao lingine lolote, lakini cha kushangaza mpaka sasa hivi katani hii wanaoendeleza ni watu wachache wakulima binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa ambao wanajiita Bodi ya Mkonge wameyajaza mashamba. Katika Tanzania eneo lenye mashamba makubwa ya Mkonge ni Korogwe Vijijini, nina mashamba zaidi ya 18; watu hawaendelezi, wanaoendeleza ni watu walioshika mashamba binafsi akina Mohamed Mo, Mura, Luhinda pamoja na Gai; lakini ukiangalia mashamba ambayo yameshikwa na hawa wenzetu wa Bodi ya Mkonge hakuna shamba hata moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi si kwamba tunakataa katani, tunaipenda sana katani hata juzi Waziri wa Kilimo amefika pale na kuwakemea sana, lakini yale mashamba ambayo hayaendelezwi wapewe wananchi walime Mkonge. Tunakuwa tukisema mkonge, mkonge, mkonge wenyewe kwa mkulima mdogo kwenye katani ananunua kwa shilingi elfu nne wakati watu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Serikali pamoja na Waziri wa Viwanda kwa hotuba yake nzuri ambayo inaleta changamoto na watu wote tunaipongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wana msemo wao, wanasema: “asiyesikia la mkuu, badala yake, huvunjika mguu.” Kwa nini nimesema hivyo? Nimesema hivyo kufuatana na mazingira ya maongezi. Tunapokaa hapa, ni kwa ajili ya kuchangia mawazo ya wananchi waliotutuma. Kwa hiyo, usiposikiliza mawazo ya wananchi waliotutuma, matokeo yake ni kwamba tutakuja kuvunjika miguu, utakaporudi kwenye uchaguzi unakuwa huna la kwenda kuongea kwa wapiga kura wako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la viwanda. Bahati nzuri Wizara ya Viwanda ina Waziri makini na Watendaji wake makini. Tunasema hivyo kwa nini? Kwa muda mfupi tumeona Katibu Mkuu pamoja na Waziri wamezunguka sana katika maeneo kuangalia viwanda gani vimekufa na vipi viamshwe. Naomba sana na nataka nirudie kauli yangu ambayo niliitoa wakati ule wa mipango, hapa hatupo kupendezana, tupo kwa ajili ya kujenga nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kwamba mwaka huu tunataka Tanzania ya Viwanda, sikatai, naiunga mkono mia kwa mia; lakini naomba nirudie Mheshimiwa Waziri. Tunaposema viwanda, tunaviangalia viwanda vilivyokufa; na kama tunaangalia vilivyokufa, ni namna gani tutavianzisha viwanda vilivyokufa ili vije vijengwe viwanda vingine? Leo hii kiwanda cha General Tyre Arusha kingekuwa kinafanya kazi, Watanzania wengi wangekuwa wanaingia pale kufanya kazi, badala yake tunasema tunajenga viwanda. Tufufue Arusha General Tyre.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kiwanda cha kutengeneza magodoro Dodoma, kilikuwa kiwanda kikubwa na wananchi wa Dodoma walikuwa wanakitegemea sana, badala yake kiwanda hiki kimehamishiwa Dar es Salaam. Wale wafanyakazi ambao wangeweza kusaidia au wangeweza kupata kazi hapa, Dodoma watapata kazi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanga nimemsikiliza mchangiaji mwenzangu pale, katika mikoa ambayo ilikuwa ni mikoa ya viwanda; ilikuwa kama mikoa mitano au minne; Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Morogoro, Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha. Sasa hivi ndiyo imekuwa mikoa maskini kuliko mikoa mingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Kiwanda cha Foma kimeondoka Tanga kinakwenda Dar es Salaam. Kwani Tanga hakuna wananchi? Leo hii Kiwanda cha Chuma, kilikuwepo Tanga, hakuna! Leo hii hata Viwanda vya Mkonge, wanafanya kuungaunga maskrepa ili kufungua viwanda vya mkonge ambapo mkonge mmeweka katika zao la biashara. Leo hii ninapokwambia, kuna viwanda vya mkonge, acha viwanda ambavyo vinataka kujengwa, wafanyakazi wake wanayanyaswa kama watoto wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii shamba la Kwa Shemshi, kuna Kiwanda cha Mkonge ambacho wafanyakazi wametoka bara; imagine kama mimi Maji Marefu, nimetoka Songea, nilikwenda kule kama Manamba; na wengine wametoka Kigoma, wengine wametoka Usukumani, wamekwenda kule kama Manamba; lakini Manamba yake ilikuwa ni kwenda kufanya kazi. Leo hii shamba hilo linabadilishwa na watu zaidi ya watatu; wametumia kigezo gani? Wametumia sheria gani? Hatua ya mwisho, wafanyakazi wanafukuzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninapomwambia Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, shamba la Kwa Shemshi wafanyakazi wamefukuzwa na wanaambiwa hawalipwi na shamba hilo limeingiwa na Mwarabu, alipotoka hajulikani; kwa mkataba gani, haujulikani. Sasa mnaposema kwamba Watanzania wanatakiwa wakafanye kazi, watafanya kazi gani? Sina maana kwamba Mwarabu ni wewe Mheshimiwa Keissy, hapana, naona unaanza kujitutumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani naona huyu ananisumbua kwenye message zangu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nairidhia sana Serikali yetu hii, naomba sana tuangalie kwa mfano Kiwanda cha Urafiki Dar es Salaam, kilikuwa kina wafanyakazi chungu nzima, wako wawekezaji wa Tanzania wana uwezo, kama akina Mheshimiwa Bakhresa, Mheshimiwa Mengi, na Waheshimiwa wengine ambao wanafanya kazi vizuri, hakuna upungufu. Leo tunaleta Wachina, tunawaambia waje wafanye biashara. Badala ya kufanya biashara, wanafanya ni kiwanda cha kutengeneza mbao. Kilikuwa kiwanda cha kutengeneza nguo, kinabadilishwa kinakuwa kiwanda cha kutengeneza mbao. Ndiyo mikataba yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana ya kuendeleza viwanda vyetu ni nini? Maana yake ni kwamba viwanda ambavyo havifanyi kazi, ambavyo vilikuwa vimekufa vipewe watu ambao ni wazawa wenye uwezo wa kufanyia kazi, badala ya kutegemea majitu yanayotoka nje, yanakuja hapa kuchukua viwanda vyetu kwa ajili ya kukopa pesa zetu, wanapeleka huko, halafu wanatuambia Watanzania ni walalahoi. Nani mlalahoi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga kulikuwa kuna Kiwanda cha Saruji, hakipo; kulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, hakuna; kulikuwa na Kiwanda cha Sabuni ambao ni Gardenia, hakuna; kulikuwa kuna Kiwanda cha Foma, kimehamishiwa Dar es Salaam; kulikuwa kuna Kiwanda cha Chuma, hakuna; kulikuwa kuna Kiwanda cha Matunda Korogwe, mpaka scraper zimetolewa; kulikuwa kuna kiwanda cha kutengeneza ceiling board kipo Mkumbara, lakini cha kushangaza kiwanda kile sasa kimekuwa cha kuchoma mkaa. Maskrepa yameondolewa yamepelekwa sehemu nyingine. Morogoro kulikuwa kuna viwanda chungu nzima, badala yake vinakuwa ni nyumba za kufugia mbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ndugu zangu, Mheshimiwa Waziri yupo makini na bahati nzuri safari hii Mawaziri wote wapo makini. Mnafanya kazi kwa kujituma bila kuangalia itikadi ya Vyama. Naomba sana, tusianze kusema tunajenga viwanda vingine, nendeni Bagamoyo mkaanzishe Kiwanda cha Sukari. Hizi kesi tunazopata za sukari, hatutazipata. Nendeni kule APZ, nendeni Kigoma, kaangalieni Kiwanda kile cha Mawese, kimefikia wapi? Kaangalieni viwanda vya kutengeneza samaki, hebu tuangalieni ukanda huu wa Pwani, ni wapi kuna kiwanda cha kutengenza samaki? Vipo kule ziwani, Mafia hakuna.
Hebu tufanyeni. Tusifanya kazi kwa mazoea. Tufanye kazi kulingana na mazingira ya Watanzania, wanatakaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niyaseme haya kwa sababu naipenda sana Serikali yangu na ukimkuta mtu hapa kazi yake ni kuja na kuiponda Serikali na kuitukana, nafikiri ana upungufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacholilia sana ni kwamba tuifanye kazi yetu, wote tuungane, tusiangalie itikadi ya Vyama, tujaribu kukupa mawazo mazuri. Mheshimiwa Waziri, mtu anapokupa mawazo mazuri, usiangalie Chama chake, angalia huko tunakotoka, tuna matatizo gani? Tukisema tuangalie kwamba huyu anatoka sehemu nyingine, hatutapata nafasi nzuri ya kuwa na viwanda vizuri na bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kama kuna tatizo kubwa, Mheshimiwa Waziri anza kuangalia Mkoa wa Tanga ambao ulikuwa ni Mkoa wa viwanda. Viwanda ambavyo vipo, vinaweza kupokea vijana zaidi ya 20,000 badala ya kujenga viwanda vipya ambavyo havitakuwa na maana, havitatusaidia lolote wakati viwanda vya zamani vipo na majengo yake yapo. Hapa kwanza inapunguza gharama ya watu kuanza kutafuta utaratibu mwingine. Una viongozi wazuri ndani ya Wizara yako, wote ni watu watendaji. Nimewapitia kupitia Kamati yangu ya PAC, tumewaona ni wazuri. Naomba tuzitumie nguvu zetu kwa kushirikiana na sisi Wabunge ili mwone tutafanyaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muheza kuna matunda, kiwanda hakuna. Kiwanda cha Gossage Tanga kimekufa; Sumbawanga huko ndiyo usiniambie, walikuwa na Kiwanda cha Maziwa, hakuna kitu. Sasa niliona niyaseme haya kwa sababu Kilimanjaro kulikuwa na Kiwanda cha Kahawa, hakipo tena; kulikuwa kuna Kiwanda cha Magunia hakuna; leo tunataka tujenge vingine. Tuanze vya magunia Kilimanjaro, tuanze kile cha Kahawa Kilimanjaro, tukimaliza hivyo ndiyo tunajenga viwanda vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, sitaki kupoteza muda sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja asilimia mia moja. Hii Serikali yetu wote, tunatakiwa tuwaunge mkono kwa kila kona katika matukio yote wanayoyafanya kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Ila nilete kwako masikitiko yangu makubwa kutokana na kitendo alichonionesha Mheshimiwa Naibu Waziri asubuhi. Sikutarajia kama ningepata majibu ya namna ile, lakini nataka nimwambie kwenye siku ya Wizara yake, shilingi yangu hataiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona nimeleta maneno hapa Bungeni, maana yake ni kwamba kule Wakurugenzi, watumishi wa Halmashauri wameshindwa kuyafanya yale mambo, ndiyo maana nayaleta hapa ili nipate msaada zaidi. Kuna lugha nzuri za kuweza kutufanya sisi ambao tunatumwa na wananchi tuyalete hapa ili mtuelekeze ni namna gani ya kwenda kuongea na wananchi watusikie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu, Wakurugenzi zaidi ya tano; toka nimeingia Bungeni, Wakurugenzi kwangu wanakaa miezi sita sita, hii taarifa ya ardhi wao wataipata wapi? Muda wa kukusanya habari, wao watazipata wapi? Mkurugenzi akikaa miezi sita kaondolewa; akikaa mwaka mmoja, kaondolewa! Kuna watumishi wengine wanakaa miaka, hawaondolewi! Sasa narudi kwenye hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye upande wa TAMISEMI. Naomba kwanza wafanye marekebisho ya Sheria ya Manunuzi. Hapa tutakuwa tunadanganyana, hakuna Mbunge anayeingia hapa kuangalia kwenye ile Kamati ya Sheria ya Manunuzi, Wabunge wote tunakaa nje. Wanayojadili mpaka kununua vitu, wananunua watumishi wa Halmashauri, sasa sisi Wabunge tunakwenda pale, tunaambiwa Jimbo lako halifanyi kazi. Kama leo kujenga nyumba inaandaliwa na watumishi wa Halmshauri, unaambiwa shilingi milioni 35, wewe Mbunge hushirikishwi, halafu tunakuja huku tunaambiwa sisi ni mafisadi, ufisadi wetu unaletwa na nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuangaliane kwamba Sheria ya Manunuzi ikirekebishwa na sisi Wabunge tunaingia pale tunatoa hoja zetu. Tukiona mahali hapaendani na jinsi ilivyo, tunapinga. Sasa sisi Wabunge tunakuja kulalamikia Bungeni, kule hakuna mahali tunaingia. Eti wataalam ndio wanakaa, wanamtafuta mkandarasi, wanamweka pale, ananunua vitu; nyumba ya kujenga shilingi milioni 30 anajenga kwa shilingi milioni 90, wewe Mbunge utalalamikia wapi? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nasikitika, tunaletewa hela sana na Serikali, lakini zinaletwa siku za mwisho mwisho. Ikifika siku ya mwezi wa saba tarehe 1, hela zinatakiwa zirudi huko. Kwa nini hizi hela kama mnatuamini mnatuletea, zisibaki Halmashauri ili wananchi wakaendeleza ile miradi ambayo ilikwama kwasababu hela zilikuwa hazipatikani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaashangaa hela zinakuja; Serikali haiwezi kukusanya hela kwa wakati mmoja na ikagawa kwa sehemu moja. Hela ni lazima igawanywe kwa kila sehemu. Wanasema kakondoo kadogo kanaliwa na kila mtu, sasa lazima kila sehemu zipewe lakini inafika mahali kwamba tunaletewa pesa zile, baada ya siku mbili unaambiwa hela zinatakiwa zirudi Hazina; hazijafanya kazi yoyote, hatujapanga mikakati ya aina yoyote, halafu leo tunakuja kulaumiwa kwamba Wabunge hatusimamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili suala Mheshimiwa waziri utakapokuja tueleze; kama hela mnaamini; mimi naamini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli hakuna mahali mtu atapita kuchukua hata thumni kwa jinsi mlivyojipanga safari hii Mawaziri wetu. Mmnejipanga vizuri, mnafanya kazi vizuri na watendaji wenu ni wazuri. Sasa kama Watendaji ni wazuri, mna wasiwasi gani hela zisibaki Halmashauri? Mimi kwangu zilikuja hela za maji, Benki ya Dunia, mabomba yametengenezwa, hayakwisha, lakini hela zinatakiwa zirudi, zinakwenda kufanya kazi gani? Kama zililetwa kwa ajili ya Watanzania na Serikali ya Tanzania itazilipa fedha zile, kwa nini zisibaki pale ili tukijua kwamba zimebaki pale, ziendeleze miradi mingine ya maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme kwasababu sasa hivi kuna hospitali, tuna zahanati nyingi ambazo tuliziahidi kwamba zitaboreshwa, mpaka sasa hivi hatujaboresha. Tulikuwa tunaomba vilevile maabara, wananchi wamechangishwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu tukufu tuongeze mtaji ili zile maabara ambazo wananchi walijitolea kwa nguvu ili mwongeze hata ka-percent kidogo wananchi waone Serikali yao inavyofanya kazi, kwasababu Serikali hii ni sikivu na kama Serikali ni sikivu, lazima tuwe kwa kila kona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Kuna suala la Mombo. Mombo toka mwaka juzi ilikuwa iwe Halmashauri, lakini kila siku naomba katika Ufalme wako Mheshimiwa Waziri na hilo naomba uliangalie sana. Niko chini ya miguu yako, Mombo. Katika vitu ambavyo vinaumiza kichwa wananchi wa Korogwe Vijijini, Mombo, iweke iwe Halmashauri ya Mji. Watu tumezunguka kila kitu tumefanya tumefanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye utawala bora. Ukimkuta mtu anawasema watu wa TAKUKURU akili yake kidogo imepungua, wanafanya kazi sana. Ukimkuta mtu anasema watu wa Kamati ya Maadili, wanafanya kazi sana. Naomba tuboreshe ofisi zao, naomba tuwape nguvu, naomba badala ya kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, wapewe ruhusa, wao wenyewe wapeleke watu mahakamani. Tunaogopa nini? Kama mtu huna tatizo ambalo umelifanya, wao mpaka kesi waichukue, waijadili, waichunguze wakishaichunguza halafu inapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka. Sasa kama hamwaamini, mliwapa kazi za nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maadili wanafanya kazi. Juzi nilikwenda Kibaha, nimeangalia Ofisi ya Maadili ya Kibaha, utafikiria ni nyumba ya Mganga wa Kienyeji, tena ni nyumba ya kukodi na wakati watu wanafanya kazi kuhusu maadili yenu kuwa mazuri! Kwa nini tusiwaboreshee ofisi zao na kila Mkoa kukawa na ofisi? Wanapokuwa wanafanya kazi na ukiwawekea ofisi nzuri, nao wanakuwa nguvu ya kufanya kazi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa usalama. Leo hii Usalama wa Taifa tunatakiwa tuwaongeze posho, kwa sababu wanapofanya kazi ni kwa ajili ya maslahi ya Watanzania. Ninyi hamjakaa Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekaa Kenya miaka 15. Kuna wakati Mtanzania analala saa 6.00, kwa nini? Kwa sababu usalama wao ni mdogo. Leo hapa Tanzania watu wa usalama wanafanya kazi vizuri, tunawaangalia, hatuwapi matumaini, tena tukiwaona tunawadharau. Tusifanye kazi kwa mazoea. Tufanye kazi kama Mheshimiwa Pombe Magufuli anavyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niyaseme haya kwasababu hii ndiyo demokrasia yetu. Mheshimiwa Lukuvi ni rafiki yangu, siondoi shilingi hata siku moja, wala siwezi kuipinga Serikali yangu. Kwa hiyo, kukwambia kwamba nitakuja kuondoa shilingi, siondoi tena naunga mkono moja kwa moja.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mtuunge mkono sisi Wabunge. Tunakaa katika mazingira magumu sana huko vijijini. Mnapokuwa katika Bunge hili, mjue kwamba ninyi wote ni Wabunge kama sisi. Angalieni kauli za kutujibu. Itafika mahali na sisi tutaonekana kama watu ambao tumetoka nje ya Bunge hili; na hatupendezewi, hatufurahishwi tuonekane kama Wabunge tumekuja hapa kujipendekeza au kupendeza baadhi ya watu, tuonekane tunaiponda Serikali yetu. Serikali yetu ni sikivu, inafanya kazi vizuri, Mawaziri safari hii ni Wazuri, naomba muendelee kutujali na kututhamini katika majibu yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape nafasi wengine; nakushukuru kwanza wewe binafsi kwa kukuomba ombi langu kwamba naumwa sana mguu niasidie na umenikubalia, Mungu akubariki sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Mimi nianze kwa kuunga mkono hoja, naomba niunge mkono hoja asilimia mia moja kwa sababu Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wa kazi wanafanya kazi vizuri na Mungu awabariki muwe hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa na wazo moja tu, nianze na Mkoa wangu wa Tanga. Wabunge wenzangu wa Mkoa wa Tanga wameongea sana na mimi nataka nirudie, kwani Tanga ni Upinzani? Tanga haikutoa kura nyingi ndani ya Chama cha Mapinduzi? Na kama tumetoa, mbona tunaachwa? Naomba sana Mheshimiwa Waziri wewe ni mtu msikivu, pamoja na Wizara zako zote mbili uchukuzi pamoja na ujenzi, naomba muangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano katika Wilaya ya Korogwe, mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne aliahidi kutengeneza barabara ya lami kutoka Korogwe kwenda Kwa Shemsi kupitia Bumbuli na kutokea Soni. Leo ukiangalia katika kitabu hiki ukurasa wa 51, haikutengewa hata thumni, maana yake ni nini? Zile sehemu ambazo ni nyeti, ambazo zinategemewa, ambazo zilikuwa ni ahadi, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano amesema, hazikutengewa hata thumni. Mnatutendea haki kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la Mji wa Mombo. Mji wa Mombo uliahadiwa na Marais wawili na leo narudia kwamba Mji wa Mombo itajengwa kwa kiwango cha lami kilometa 1.5 na ikaahidiwa kwamba, kazi hiyo ifanyike. Mpaka leo hii hakuna chochote ambacho kimeweza kuwekwa. Naomba Serikali yangu tukufu, msikilize kilio cha Wanatanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bandari kavu. Suala la bandari kavu ilikuwa toka Awamu ya Kwanza, ilikuwa kwamba, Korogwe Mjini kutakuwa sehemu ya Old Korogwe, kwamba kutakuwa na eneo la kujenga bandari kavu, lakini kwenye kitabu hiki hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la reli kutoka Tanga mpaka Arusha, mpaka Musoma ni kitu muhimu sana kwa Watanzania wa Kusini. Watanzania wanategemea kuona safari hii kazi inaendelea, lakini cha kushangaza inayoangaliwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, eeh Kaskazini, sawa sawa, lakini kinachoangaliwa ni reli ya kati peke yake na reli ya TAZARA, kwa nini? Hii reli ya Kaskazini haina maana, haifanyi kazi, hakuna watu, hakuna biashara na hakuna viwanda? Naomba Serikali yetu hii muangalie!
Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari ni kitu muhimu sana, lakini leo…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. STEPHEN J. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na tabia ya kusahau barabara ya Korogwe – Dindira – Bumbuli - Somi kwa kiwango cha lami tangu mwaka 2010 hadi leo wakati barabara hii imo ndani ya Ilani Uchaguzi ya Cham cha Mapinduzi ya mwaka 2010. Kila siku inasahaulika na cha kusikitisha mwaka huu wa fedha 2017/ 2018 imetengewa kiwango kidogo cha fedha cha sh. 130,000,000/=, hii haina msaada wowote. Pili, Mji Mdogo wa Mombo uliahidiwa kuweka kiwango cha lami tangu mwaka 2014 hadi leo hakuna msaada wowote ambao umefanyika, kila kukicha maneno tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara za mkoa hadi leo zinajengwa chini ya kiwango kiasi ambacho fedha zinatengwa lakini utengenezaji wake si wa kuridhisha. Fedha zinahamishwa bila sababu yoyote, kwa mfano barabara ya Korogwe – Magoma – Maramba – Mabokwemi kuna sehemu hazikumaliziwa kabisa. Barabara ya Korogwe – Mnyuzi – Maguzoni kuna kama kilometa 15 zilitakiwa heavy grading lakini hata kilometa tisa hazikufanyika. Sasa Serikali iliangalie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara zinatakiwa kupandishwa hadhi kutoka za Wilaya kuwa za Mkoa. Hadi leo hakifanyiki chochote wakati DCC imepitisha RCC imepitisha. Barabara hizo ni hizi zifuatazo:-
(a) Barabara ya kutoka Mombo hadi Mzeli inaunganisha wilaya mbili na Mkoa kwa ujumla;
(b) Barabara kutoka Makuyuni hadi Mpakani Bumbuli; na
(c) Barabara ya kutoka Msambiazi hadi Bungu na kuunganisha Wilaya Bumbuli haijafanyiwa chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mawasiliano. Kuna Kata ya Kizara mawasiliano hakuna, kuna Kata ya Kalalami katika Kijiji cha Kigwasi (wachimbaji wa madini) na inapakana na Mbuga ya Wanyama ya Mkomazi hakuna mawasiliano. Serikali isiangalie tu mjini na huku wapo wananchi wenu. Nategemea Mheshimiwa Waziri atakuja na majibu mazuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Aaah tumekuwa watatu sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Wizara ya Nishari na Madini kwamba sisi wengi Wabunge tuliorudi safari hii ni heshima yako Mheshimiwa Profesa. Nasema hivyo kwa sababu sehemu zote ulizoweka umeme ndiyo watu wamepata neno la kuongea na leo hii Wabunge tumeingia hapa. Tunamshukuru sana yeye pamoja na taasisi zako zote na tunaomba waendelee na moyo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze kwa neno dogo. Katika utaratibu wa umeme kuna sehemu vimejitokeza vitu ambavyo vinatakiwa vifanyiwe kazi haraka sana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mita zetu za LUKU Watanzania wengi wamekuwa wanakatwa ikifika mwisho wa mwezi. Kama ni kukatwa pesa ni afadhali mtu awe anataarifiwa kwamba katika kuwekewa LUKU yako LUKU hiyo imekutwa na matatizo, huko nyuma ulikuwa una deni na kama ni deni tujue kwamba, ilikuwa ni kiasi gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Lakini kumekuwa na taratibu ndani ya TANESCO mtu anatarajia katika simu yake ana shilingi 20,000; anaweka LUKU lakini ikifika pale anaambiwa pesa yako haitoshi, wakati hana pesa nyingine na anahitaji msaada wa umeme. Unaweka shilingi 30,000 unaambiwa pesa yako haitoshi. Sasa kama haitoshi kwanini vitu hivi mtu asikuambie mapema kwamba, unawekewa LUKU lakini siku za nyuma ulikuwa una deni kiasi fulani unatakiwa ulipe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mnawangoja walala hoi inafika siku ya mwisho wa mwezi mtu analipia LUKU yake kwa misingi kwamba nyumba yake ipate umeme, unakatwa pesa yako. Mheshimiwa Waziri naomba sana kama utaratibu huu huufahamu tunataka tukuambie kuna tatizo hili kwa Watanzania wa chini ambao hawajui kwamba maisha yao ya baadaye yanakuaje wanakatwa pesa zao hovyo hovyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, watu wanaowekewa REA waliambiwa kwamba wanawekewa umeme kwa shilingi 27,000. Na Watanzania wengi walipata nguvu kubwa sana kwamba sasa tunawekewa umeme kwa shilingi 27,000. Lakini kunatokea mabadilika, mtu anakwenda kutafuta pesa hata kwa kukopa kwa mtu, anaweka line katika nyumba yake, siku anayotarajia anaambiwa kwamba leo REA imekiuka sio hii tena shilingi 27,000 inapanda bei kiasi ambacho Mtanzania wa chini anashindwa wakati nyumba yake tayari imekuwa na LUKU tayari ameshaifanyia kila kitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kama umeme wa REA ameufanyia jitihada kubwa sana kwa Watanzania, wameupata, lakini sasa inafika mahali wanabadilishiwa viwango vya kuweka umeme, hatuwatendei haki kwa sababu umeme huu umeletwa na Watanzania na hii pesa ya Watanzania na ni kodi ya Watanzania. Kama kweli tunataka kuwasaidia Watanzania basi wawekewe kiwango kile kile kiwasaidie Watanzania wa chini na wao wawe na umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuja umeme. TANESCO wanafanya kazi nzuri sana usiyemkuta mtu anayemshukuru mtu wa TANESCO au watu wote wa TANESCO basi mwangalie huyu mtu ana mapungufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila nataka niwashauri kitu kimoja Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi. Umeme tunao utumia sasa hivi ni wa gharama kubwa sana kwa sababu unatumia mafuta na vitu vingine, na wengine mnakodi mitambo. Lakini kuna vituo vya nguvu vya umeme ambavyo vinatumia maji. Vituo hivi ndivyo vinavyofanya leo Uganda wanakuwa na umeme ambao haukatiki mara kwa mara, na umeme huo wa Uganda umefika mpaka Tanzania kwa kutumia maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini eneo la Hale, Kihansi, Bwawa la Nyumba ya Mungu na Bwawa la Mtera tusiyaendeleze kwa kuweka mitambo ya kisasa badala ya kutegemea hawa watu wanaotoka nje ya nchi kuja kutuibia Watanzania? Wanatuongezea bills zisizokuwa na maana, matokeo yake wanataka watupeleke mahakamani? Hawa watu walikuja kwetu kuchuma au walikuja kuwasaidia Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kuna uwezekano, haya meneo ambayo tuliyaanzisha sisi; Watanzania walikuwa wanategea sana umeme wa nguvu za maji leo Zimbabwe na Zambia wanategemea nguvu ya maji tu. Na hii nguvu ya maji inasaidia haina gharama kubwa kama hizo wanazotupa hawa wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba sana Mheshimiwa Waziri, yeye ni msikivu sana, tena ni Profesa mwenzangu naomba aliangalie suala hili ambalo mimi bila yeye nisingerudi pale jimbo la Korogwe Vijijini. Alifanya kazi ya ziada kulisambazia umeme, lakini pamoja na umeme ule ambao ameusambaza namshukuru na uendelee na jitihada zake. Lakini swali ambalo ninajiuliza, kuna baadhi ya maeneo ambayo hayana umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo la Korogwe katika Mkoa wa Tanga, Jimbo la Korogwe Vijijini ndiko kwenye nguvu za umeme aina mbili, iko Hale, iko Chemka. Lakini nguzo nyingi za umeme zimepita kwenye nyumba za watu zimekwenda kwenye mashamba ya mkonge ambayo leo hii hayaendelezwi.
Sasa badala ya kuchukua nguzo nyingi kupeleka kwenye maeneo, na kuna vijiji ambavyo vimepitiwa na maeneo yale, kwa nini wasipeleke nguzo moja badala ya kupeleka nguzo 50?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusitumie vielelezo hivi? Kwa mfano nina kata pale toka Uhuru umeme wanausikia kwenye redio, kata ya Kizara, kata Vugiri katika vijiji vya Mlalo, kata ya Mpale katika kijiji cha Mpale na Mali hakuna kitu cha aina yoyote. Kata ya Mkalamo, Mswaha hakuna umeme, sasa na ndio umeme umetokea huko kwangu. Mheshimiwa Waziri, naomba ulivyonisaidia wakati nikiumwa, nikiwa India ukanipelekea na watu wako wa REA wamefanya kazi nzuri sana hebu nimalizie hili na mimi nijijue kwamba mwaka 2020 basi tunakuwa watu wa kupeta tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la madini. Madini ni kitu muhimu sana kwa Tanzania. Mimi kwenye jimbo langu kuna sehemu kubwa tu za kutoa madini, lakini watu wa madini hawapati faida yoyote ya madini yale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma Serikali iliahidi kwamba itakwenda kule kuwapelekea wachimbaji wadogo wadogo, watakwenda kuwafungulia SACCOS zao za kupata pesa kwa ajili ya wao kuendeleza miradi yao ya madini, lakini cha kushangaza mpaka leo hii katika Jimbo langu kule Kalalani hakuna hata mtu mmoja ambaye amesaidiwa. Sasa hawa wachimbaji wadogo wadogo kwanini hatuwathamini wakati wao ndio wanaoonesha njia kwamba, hapa ndiko kwenye madini na ndipo wanapoonesha njia na Serikali inakuja kuchimba inapata faida kubwa, wawekezaji wanakuja; lakini sio kwa Serikali peke yake bila kushirikiana na hawa wachimbaji wadogo wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni msikivu na Wizara yake ni sikivu. Mimi nimeiita kwenye Kamati yangu, tumeona matatizo yake na mmejaribu kuyarekebisha. Katibu wako Mkuu, anafanya kazi vizuri, Katibu Mkuu wa REA anafanya kazi vizuri. Naomba sana hii shughuli hebu imalizie kwa sababu wengine hatuwezi kusimama hapa kila siku kupinga wakati Serikali imefanya. Si mimi tu hata upinzani kuna majimbo mengi yamepewa umeme na kama yamepewa umeme ni kwa ajili yako na ndio maana wengine hapa leo hata kusema yale maneno makubwa makubwa hatuwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia, Mungu akubariki sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru wewe binafsi kwa kuniona na vilevile nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli kwa safari hii kutuchagulia Mawaziri majembe. Mheshimiwa Lukuvi wewe ni jembe na Mawaziri wote waliochaguliwa safari hii na Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli wote ni majembe, mnafanya kazi kwa kujitolea sana, Mungu awabariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Shirika la Nyumba. Shirika la Nyumba linaendeshwa na Mkurugenzi mzuri asiyekuwa na majivuno, mchapakazi mzuri asiyekuwa na makundi. Mungu ambariki sana pale alipo. Nataka kutoa maoni yangu, kwamba katika Shirika la Nyumba kuna matatizo makubwa ambayo inatakiwa Serikali hii ya sasa yashughulikiwe sana. Kuna nyumba ambazo zimejengwa kwa gharama nafuu na kuna nyumba ambazo zimejengwa kwa gharama nafuu ambazo haziwasaidii Watanzania maskini, zinawasaidia watu matajiri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hayo kwa sababu leo hii Wabunge tuliopo hapa ndani ni asilimia 70 ambao wamekuja wapya na kuna asilimia 30 tu ya Wabunge waliokuwepo Bunge lililopita. Waheshimiwa Wabunge wengi walikuwa wanakaa kwenye nyumba za Shirika la Nyumba. Leo hii nyumba zile kuwapa Wabunge wapya waingie hawataki, wanakodisha kwa watu. Naomba mlishughulikie suala hili. Kama umeshakuwa Mbunge na umetoka, ukishatoka hapa huna mkataba wa kurudi Bungeni. Ni kwamba mkataba wako umekwisha na ulipewa nyumba na Shirika la Nyumba ili ukae kwa muda ule utakaokuwa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge leo anakaa Guest au hotelini wakati kuna majumba hapa yamekodishwa kwa watu, wanafanyia biashara ambazo hazina mbele wala nyuma! Naomba Mheshimiwa Waziri hebu fuatilia Shirika lako la Nyumba hasa kule walikotoka Wabunge wa zamani. Zile nyumba ambazo walikuwa wanakaa wenzetu, wapewe Wabunge wapya, wakae na wao waone faida ya hili Shirika. Tunalitetea Shirika hili, lakini halina msaada kwa Wabunge. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni kwamba, nyumba nyingi zilizoko Dar es Salaam zimechukuliwa na matajiri. Badala ya kuwasaidia maskini, wanawapangisha matajiri wenzao, wao wanakaa kwenye nyumba zao, zinakuwa ni nyumba tu ambazo zimekaa hazina faida yoyote kwa Watanzania. Sasa maana ya kusema tunajenga nyumba kwa ajili ya Watanzania, faida yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kuna maeneo ambayo wenzetu wa Shirika la Nyumba wamebomoa; maana ya kubomoa maeneo haya ni kwa ajili ya kujenga nyumba mpya. Nashangaa zinakwenda kujengwa nyumba nyingine leo hii Dar es Salaam, Magomeni, kumekuwa pori. Wezi wakiiba usiku, wanakwenda kujificha pale. Si muanze kujenga lile eneo pale ambalo mlibomoa kwa ajili ya kujenga nyumba nyingine!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo pale Tanga. Tanga wamekuja wamebomoa ambazo wazee wa kimaskini walikuwa wanakaa, wakaambiwa kunajengwa nyumba mpya. Leo mwaka wa nne karibuni, nyumba hazijajengwa. Sasa maana yake ni nini? Kama tunataka kujenga nyumba, basi anzeni kutakasa kwenye miji mikubwa ili ile miji mikubwa iwe mizuri halafu mnarudi huku katika maeneo ambayo mnafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja katika suala la ardhi. Mheshimiwa Waziri, ni msikivu. Tumekuja hapa kuleta malalamiko kwa ajili ya ardhi, siyo kwamba kule kwetu Wakurugenzi wanashindwa kufanya kazi. Kwenye Jimbo langu nimebadilishiwa Wakurugenzi mara sita. Huyo Mkurugenzi atakayefanya kazi ya kuchunguza ardhi hii mpaka aorodheshe alete hapa, akitaka kuleta hapa anaambiwa ahame. Sababu za kuhamisha Wakurugenzi hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika Tanzania nzima, Jimbo ambalo linaongoza, ambalo lina mashamba makubwa ambayo hayaendelezwi ni Korogwe Vijijini. Nashangaa maeneo mengine yanagaiwa. Watu wanapewa maeneo, wanaambiwa hapa Serikali imechukua, Korogwe Vijijini kuna tatizo gani? Kwani haya maeneo kule ni ya nani ambayo Serikali inashindwa kuyatoa kwa wananchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati alikuja Waziri wa Kilimo wakati ule, alikuja akatoa hati kwamba wananchi wachukue Shamba la Chavda. Leo hii shamba la Chavda limekaa zaidi ya miaka 15 kuwapa watu wa Korogwe waendee hata kulima ni masharti. Leo hii kuna mashamba ya mkonge. Mashamba ya Mkonge ilikuwa ni kuendeleza mkonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kushangaza, badala ya kuendeleza mkonge, watu wanafanya biashara zao. Wanaleta watu wengine wanakuja kufanya kazi, wanakuja kupanda mkonge; tena afadhali watengeneze wao. Wanachofanya wao ni kwamba wanangoja wakulima wadogo wadogo wamelima, wao wanakuja kupanda mkonge. Maana yake nini, kama siyo dharau? Serikali sikivu kama hii!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri, mara ya kwanza niliuliza swali hili na nikaomba kwamba nitoke na Mheshimiwa Waziri aende kule Korogwe akaangalie haki inavyotendeka. Leo hii watu wa Magoma hawana mahali pa kuzikana, shamba wamezungukiwa. Leo hii kuna mgogoro wa kijiji na kijiji, Kata ya Mkomazi; Kata ya Mnyuzi haina mahali, Kata ya Mswaha haina mahali; Makalamo na maeneo mengi. Mashamba 18 mtu mmoja kwenye shamba lao, halafu tunasema wakati huu ni wa Kilimo Kwanza. Watalima wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana na namwamini sana. Tusifanye kazi kwa mazoea. Yeye hafanyi kazi kwa mazoea, ndiyo maana leo hapa kila Mbunge wa Upinzani, kila Mbunge wa CCM anamuunga mkono. Siyo tunakuunga mkono kwa sababu ya sura, bali kwa muda mfupi ambao smekaa katika Wizara hiyo, smeifanyia kazi nzuri kiasi ambacho hata sisi Wabunge tukimpinga ni kama tunajipinga wenyewe. Nimeona nimwambie suala hili hasa katika Mkoa wa Tanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga ulikuwa ni mkoa wa zao la mkonge, lakini baadaye mkonge hamna. Leo hii nenda Morogoro, kuna watu wamezuia mashamba makubwa, yasiyokuwa na faida, mtu anakwambia huyu alikuwa ni Waziri. Waziri wakati watu wanakosa ardhi? Kama Waziri alikuwa amechukua shamba, haliendelezi, watu wa Morogoro wanalalamika, wanagombana kila siku kwa sababu ya ardhi na mtu mmoja huyo huyo ana eneo zaidi ya hekta 1,000 na hajapanda hata mahindi; Serikali mna ugumu gani kuyachukua maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nenda Kilimanjaro, watu wanapata shida kama Ndugu yangu Mheshimiwa Selasini alivyosema hapa. Leo hii nimetoka Bukoba, watu wana ardhi nzuri, watu waende kule wakaendeleze ile ardhi kuwasaidia watu wa Bukoba wapande vitu, vionekane. Tusiangalie tu mji mkubwa wa Dar es Salaam, Arusha na Mbeya, angalieni na mikoa midogo midogo ambayo Watanzania wengi wako huko ambapo kuna ardhi ya kutosha lakini hawana mahali pa kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukijenga nyumba pale Bukoba Kijijini kwa rafiki yangu Rweikiza unaweza kupata wapangaji wengi tu, lakini watu wanang‟ang‟ania tu Dar es Salaam, Tanga na sehemu nyingine. Hizi sehemu nyingine kama Wilaya ya Korogwe, hizi Wilaya ndogo ndogo kwa ndugu yangu kule Mheshimiwa Nassari, kuna eneo kubwa kule ambapo nimemsikia hapa, naomba sana Serikali yangu sikivu, kama kweli mnataka kuwasaidia Watanzania, kwanza zichukueni zile nyumba za Wabunge wote ambao hawakurudi ili Wabunge hawa wapate.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunaomba sana, ile ardhi ambayo imechukuliwa na watu ambapo wanakaa, watu hawana faida yoyote, hawaleti faida yoyote kwa Watanzania, Watanzania maskini wanalalamika kila wakati, hawapati msaada wa aina yoyote, tena ukienda ukiingia unapelekwa Mahakamani na ukifika kule unanyimwa dhamana. Sasa hii biashara ni kuoneana au ndiyo ubinadamu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri ambayo ameionesha kwa muda mfupi ambao ameingia madarakani. Nataka tuwaambie kwamba hatutawaangusha, tutawaunga mkono kwa dhati.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa mambo ambayo yameongelewa juzi pamoja na Waziri, ameongelea sana kwamba ataimarisha Bandari na Viwanja vya Ndege na ataimarisha Reli. Nimeshangaa sana katika mambo ya kuimarisha reli yeye anaizungumzia tu reli ya kutoka Dar es Salaam mpaka nyumbani kwake Kigoma, hajawahi kuitaja reli ya Tanga – Moshi - Arusha mpaka Musoma. Hapa pana tatizo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati uliopita nilizungumzia sana suala la reli, nikazungumzia suna kama tunataka kuimarisha biashara ni lazima muiangalie reli ya Tanga. Reli ya Tanga kutoka Tanga kupitia Moshi kwenda Arusha mpaka Musoma ingesaidia sana katika uchumi wa nchi yetu. Nashangaa rafiki yangu ambaye ni Dkt. wangu Mpango, ameangalia sana reli inayokwenda nyumbani kwake ameisahahu ile ya Tanga. Naomba atakapojumuisha aiangalie hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, ni suala la Mkaguzi Mkuu. Kiwango cha pesa ambacho amemtengea, Serikali hapa hamuwezi kwenda kila mahali kukagua na mkapata wale mafisadi, lazima Mkaguzi Mkuu wa Serikali awakagulie, awaambie huyu ndiye fisadi, anatakiwa kupelekwa Mahakamani, leo mnapowapunguzia pesa watakwenda kukagua hiyo miradi na nini? Naomba Serikali iliangalie sana suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamepunguza bei ya mafuta ya petroli kwamba bei ya mafuta ya petroli imeachwa kama ilivyo, naomba Serikali ipandishe kwa sababu bei ya petroli haimsaidii Mtanzania, maana kupunguza bei ya mafuta maana yake ni kwamba wasafiri wapunguziwe gharama, lakini toka wamepunguza bei ya petroli hakuna Mtanzania yeyote ambaye anapanda nauli kwenye gari kwa kupunguziwa gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa waiongeze, tujue kabisa kwamba kwa sababu hatufaidiki lolote Watanzania wa hali ya chini. Kwa hiyo, kwa sababu ni kitu muhimu na wameona kwamba ni vizuri, basi tunaomba wapandishe petroli, watupunguzie sukari. Sukari hawajaiongelea hapa, lakini sukari ni kitu muhimu sana kwa Watanzania. Naomba hiyo Mheshimiwa rafiki yangu Waziri wa Mipango, Mpango yeye ni rafiki yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji ni muhimu sana na barabara; wamezungumzia masuala ya barabara kuna mikoa wameshaanza kuionesha kwamba ni mikoa matajiri sana, lakini mbona wanashindwa kuwaambia hii mikoa maskini kama mikoa ambayo wamenyima hata kuwatengenezea Bandari, mtawapa kiwango kiasi gani kwa sababu tuna bandari ya Tanga pale, tuna Bandari ya Mtwara pale, tuna Bandari ya Bagamoyo, katika Mpango walisema hizi Bandari wataziongeza lakini hatuoni chochote kinachoendelea eti Tanga kwa sababu kunajengwa bomba la mafuta kutoka Uganda ndiyo isahaulike? Haikubaliki!
Hili bomba la mafuta linakuja kwa ajili ya nchi mbili! Haliji kwa ajili ya Tanga! Kama Tanga linakuja ni kama bandari nyingine. Naomba hapa iongezewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Kambi ya Mbadala, tunazungumzia suala hili kwa masikitiko makubwa. Kwa niaba ya Kambi Mbadala, wenzetu wa Kambi ya Upinzani walisema kwamba sitting za Wabunge zifutwe, nasi tunasema hata per diem pia zifutwe kama tunataka kuisaidia Serikali, si Waheshimiwa Wabunge wote tulikuja kwa ajili ya kuwatetea wanyonge? Kama tumekuja kwa ajili ya kuwatetea wanyonge, wenzetu wamesema sitting mwondoe, sisi Kambi Mbadala tunasema hivi, hata ile per diem inayotegemewa na hawa, kama kweli tumekuja kuwasaidia watu, zote ziondolewe ziende kwa maendeleo ya wananchi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo ni uti wa mgongo sana, lakini kwangu kulitakiwa kujengwe bwawa la maji toka miaka ya nyuma sana. Bwawa hili lilikuwa linagharimu shilingi bilioni 13, lakini fedha zile ziliondoka zikaenda Kilimanjaro. Sasa hii bwawa ambalo lilikuwa lijengwe katika Jimbo langu; mmesema safari hii ni wakati wa kilimo, naomba hili bwawa liendelee kujengwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni viwanda. Katika Tanzania, mikoa ambayo ilikuwa inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi ni mikoa mitatu au minne. Ni Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Tanga na Arusha. Hebu niambieni leo, tunazungumzia viwanda. Rafiki yangu Waziri wa Viwanda, best wangu hapa ana hakika kabisa kwamba atafanya; hela za kuanzia hivyo viwanda zitapatikana wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, Serikali yangu sikivu, nampenda sana Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli na Mawaziri mlioko hapa, mnafanya kazi kubwa sana kwa kujituma na hata leo tutamwombea dua Naibu Spika ili aendelee kukaa mpaka Bunge la mwaka 2020 kwenye jukwaa lile pale. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema haya kwa sababu tuna uchungu. Sisi tunaotoka kule Majimbo tunapokuja hapa, tunaonekana kama Waswahili. Mnaposema kwamba maendeleo yanakwenda vijijini, mtuambie maendeleo haya ni ya namna gani, siyo kusoma vitabu. Leo hii hakuna dawa mahospitalini, hakuna elimu ya kutosha, Walimu wanadai haki zao hawapewi, Madaktari hospitalini hawaongezewi posho; leo tunasema kwamba tunataka kufanya mambo, hebu tumalize haya madeni tunayodaiwa na watu ambao tunawatumia muda mwingi mpaka wakati wa uchaguzi hawa ndiyo tunaowatumia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tunawatumia watu mpaka wakati wa uchaguzi tunawapenda, leo hii madeni yao hatuwalipi, eti tunategemea tu kukaa; inakuwa siyo nzuri. Naomba kabisa Mheshimiwa tuanze na madeni ya ndani. Tukishamaliza madeni ya ndani tutakuwa tumefanya kazi za msingi sana kwa wananchi, Watanzania ambao wanaipenda sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Ukimwona mtu anaipinga Serikali ya Chama cha Mapinduzi, basi ujue ni fisadi. Ukimwona mtu yeyote leo anakuja kulalamika kwa bajeti yenu, ni fisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Mahakama naomba muianzishe mapema, kwa sababu tumechoka kuonekana Wabunge…
TAARIFA.......
MHE. STEVEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei, mimi sio Kambi ya Upinzani. Mimi ni mmoja kati ya Wabunge wa CCM ambao tumekuja hapa kuweka chachu ya michango yetu kufuatana na hawa wenzetu waliokimbia eneo hili. Kwa hiyo, mimi bado ni Mbunge wa CCM, hiyo taarifa yake siisikii. Ninaposema Kambi Mbadala ni kambi ambayo imekamilika kwa ajili ya kujenga hoja za msingi ya kuisaidia Serikali yetu. Sisi sio Upinzani, kwa hiyo taarifa yake siikubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya, nimeipenda sana bajeti hii, naiunga mkono kwa asilimia mia moja, siungi mkono taarifa yake huyo.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nianze kwa kurudia tena kuwashukuru Wabunge wenzangu wote ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile nirudi tena kuwashukuru kwa msaada mkubwa ambao Wabunge walinipatia nikiwa hospitalini nikiwa nimelazwa. Sitaacha kulisema hili kwa sababu wala sikutarajia, wala sikutegemea kama Wabunge wangejitokeza na kunipa misaada mbalimbali, Mungu awabairiki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimshukuru sana Waziri wa Afya pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu pamoja na Daktari wa Muhimbili, wamefanya kazi kubwa sana ya ziada. Sitaacha kulisema hili kwa sababu unapopata nafasi lazima uliseme. Bila Waziri wa Afya kulisimamia kidete kunipeleka mpaka ofisini kwake na kunihakikishia barua yangu inapita, nisingefika na leo hii nikaja kusimama na Wabunge wenzangu ili nitoe neno la shukurani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisimamie suala moja tu la insurance, Bima ya Afya. Katika muda ambao nimekaa hospitalini nikiangalia bima ya afya inatakiwa iboreshwe kwa hali ya juu sana; kwa sababu kama sisi tunapewa vile vitambulisho vya V.I.P halafu kuna wengine wakulima ambao hawana vitambulisho vya V.I.P; lakini sisi tuliopewa vitambulisho vya V.I.P tunaambiwa tukanunue dawa nje za kutibiwa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba unapokatwa hela yako ni kwamba utibiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jubilee walikuwa wanatukata hela hapa, tulikuwa tunasafiri mpaka India. Tunakwenda tunatibiwa wala hatupati shida ya aina yoyote. Leo tumesema haya mambo yote yarudi katika upande wa Serikali, lakini cha kushangaza leo hii mtu ameugua Mombasa, ameumia, anakwenda na insurance yake anaambiwa hii haitambuliki hapa, basi matokeo yake inafika mahali anafika mwingine anawekwa dhamana kwa sababu ya mtu. Kitendo hiki kimetudhalilisha sana sisi Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa hospitalini, nimetibiwa kwa muda wa karibuni siku 27 katika Hospitali ya Mikocheni, nimehudumiwa kila kitu lakini vipimo vya gharama kubwa nimelipiwa na insurance. Kipimo kidogo cha gharama ya 30,000 naambiwa nikanunue nje, sasa nini maana ya Bima ya Afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bima ya Afya sisi Wabunge ambao tunazipitisha hapa yanafanyika haya, je huyo Mtanzania wa chini ambaye hana uwezo kabisa atakuwa amefika wapi? Naomba Wenyeviti, mmetuletea hili jukumu, kwa kweli Serikali tunataka waiboreshe sana Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiini cha matatizo ni Wizara ya Afya kutengewa hela ndogo ndogo ambazo hazina msingi; kwa sababu Wizara ya Afya peke yake; nimetoka India juzi, kule Wizara inadaiwa zaidi ya bilioni 37 na bado wanatakiwa Wizara ya Afya itusaidie sisi Watanzania tulioko ndani ya nchi. Sasa hivi kule watu wanaanza kukata tamaa kutuhudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo; hatukatai kwamba Serikali imejitolea sana kwa hali na mali na mimi naishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inafanya kazi ya ziada sana; tunapofanya mambo haya tuangalie na utaratibu kwamba hii Wizara tunaisaidia kiasi gani. Hakuna kitu kibaya kama mtu; afadhali ukose chochote, lakini upate elimu na upate afya bora. Bila Wizara ya Afya kunisimamia kidete, bila Bunge kunisimamia kidete, bila ya Rais kunisimamia kidete, leo hii nilikuwa nakatwa mguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba sana; Wenyeviti wa Kamati wametuletea mapendekezo lakini hii Wizara ya Afya inapata hela lakini hela zake hazitoshelezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika vijiji, wananchi wameamua kujenga zahanati lakini wameamua kujitolea wenyewe, kwangu wamejitolea kujenga zahanati lakini zahanati hizo hazisaidii chochote kwa sababu ukienda Wizara ya Afya unakuta watu wanakaa pale kusaidia lakini inafika mahali watachukua wapi hela ili ziende kule vijijini zipeleke dawa? Dawa zipo kweli, lakini namna zile dawa zitakavyotumika vijijini lazima na sisi tuwaunge mkono hawa, lazima na sisi Wabunge safari hii tuhakikishe hii Wizara inapatiwa hela ya kutosha ambayo itatusaidia ili kuboresha mambo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko. Kwa kweli Wizara ya Afya ni kiungo muhimu sana kwa mwili wa binadamu. Leo hii angekuwa ameugua mtu mwingine ningesema labda wanatutania, nimekaa siku 27 Mikocheni, nimekwenda Muhimbili kwa Mkurugenzi wa mifupa nimeona shida wanayoipata. Nimeenda Wizarani nimeona wanavyohangaika, wanahangaika kweli kweli kutusaidia lakini hela hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wenyeviti mfanye mambo yenu yote lakini hebu jaribuni kumsaidia Dada Ummy. Yeye kama Ummy ni Waziri, yeye kama yeye hawezi kupitisha chochote lazima ninyi Wenyeviti na nyie mtilie mkazo. Sasa mnapotilia mkazo baadhi ya mambo wakati mnafikiria kwamba yeye atakwenda kutafuta hela sehemu nyingine tunakuwa tunamuumiza na Serikali hii tusitarajie kila kitu watufanyie Serikali na sisi wenyewe tujitume ili tufanye mambo mazuri ili tufanikiwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hii insurance; na Mwenyekiti akija aje na jibu Jubilee ilifanya makosa gani na kwa nini iliondolewa? Kwa nini ilikatwa? Kama ilikatwa tukaamua kuliweka Shirika la Bima la Serikali ni tatizo gani lisiwe linafanya kazi katika nchi hizi tatu za Afrika Mashariki ili itusaidie hata wengine badala ya kwenda mbali zaidi; hata Afrika ya Mashariki unaweza kupata huduma ya kutosha tukashughulikiwa na insurance.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya nirudie kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu, walinipa matumaini makubwa sana, hawakujali vyama vyao, hawakujali mimi ni nani, walinifanya nikawa najisikia kwamba si mnyonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nisiache kumshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, nisiache kumshukuru Naibu Spika, nisiache kumshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Kashilillah, walikuwa wananipa moyo wa dhati. Hatua ya mwisho nilikuwa nakaa ofisini kwa Naibu Spika akiniambia subiri subiri na leo subiri hii nimeweza kuja hapa, Mungu awabariki sana Waheshimiwa Wabunge, Mungu awabariki sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa na mengi ya kuongea ila nilikuwa tu nataka nikazie hii insurance kwa sababu ikifika mahali hospitali nyingine ukienda hutibiwi bado hatujasaidia Watanzania. Kama umepewa insurance basi kila hospitali unayokwenda unatakiwa utibiwe kwa kutegemea ile kadi uliyopewa. Leo hii unachaguliwa baadhi ya hospitali, hospitali nyingine wakikuona wanakuona vile kama kituko, sasa kituko maana yake ni nini? Tunakatwa hela, wanazichukua halafu kwenye huduma unaambiwa dawa nyingine ukanunue wewe mwenyewe wakati umekaa hospitalini….
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya Mungu atubariki, naunga mkono hoja ya viongozi hawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja ya Bajeti ya Waziri Mkuu, vilevile nitoe pole sana kwa familia ya Dkt. Macha kwa msiba mkubwa ambao umewapata. Nawapa pole.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niendelee kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuilinda nchi hii. Wote sasa tumekuwa kitu kimoja na wote tumekuwa sawa.
Vilevile nisiache kumshukuru Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge pamoja na Wizara ya Afya pamoja na Wabunge wote bila kujali Vyama vyao kwa msaada mkubwa walionipitia wakati naumwa pale, hawakujali vyama wala itikadi za vyama vyao, walikuja wakaniona na walinipa faraja sana. Nawashukuru sana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, haya mambo msiyafanye kwangu tu, myafanye kwa kila Mbunge msijali vyama vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nianze kwanza kwa kuongelea Mfuko wa Jimbo. Mfuko wa Jimbo toka tumeanza kuupata Mfuko huu wa Jimbo toka mwaka 2009 haujafanyiwa marekebisho ya aina yeyote. Mfuko wa Jimbo umekuwa ni kichocheo cha Wabunge katika kila Wilaya na kila Jimbo ili pale wananchi wanapojitolea sisi tunaongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko huu umekuwa hauwasaidii sana Wabunge kwa sababu unakuwa na mlolongo mrefu kiasi ambacho Mbunge hana uwezo nao, yeye kazi yake ni Mwenyekiti tu, lakini inapofika kutoa fedha kwa ajili ya kusaidia maendeleo yaliyoanzishwa na wananchi,
Mfuko huu unakuwa ni mgumu sana kama vile ni mfuko ambao tumepewa kama mtego. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, huu Mfuko wa Jimbo usiishie tu kwa Wabunge wenye Majimbo. Hata hawa Wabunge wa Viti Maalum wangekuwa wanapewa kiwango kiasi kwa sababu wengi wa Viti Maalum hawakai katika Majimbo peke yake,
wanazunguka katika mikoa yote. Wanapozunguka katika mikoa wanafika mahali akinamama wanawaambia tuna shida, utatoa wapi hela? Hela yenyewe ndiyo hii ya kuchanganya changanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeomba nao hawa Wabunge wa Viti Maalum watengewe kiwango kidogo kisilingane na cha kwetu lakini kiwasaidie kuzunguka katika mikoa yao ili itusaidie Wabunge wa Majimbo ili iwe inatupa nguvu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua Mheshimiwa Waziri Mkuu akija atuambie sisi sasa hivi tuko wapi, kwa sababu mara nyingi tulikuwa tunaambiwa vifaa vya Wabunge katika Majimbo hasa zile furniture tunapewa na Ofisi ya Bunge, jambo la kushangaza hii taarifa kwa Waraka
wa mwaka 2010 inaonesha kabisa kwamba Mfuko huu uko chini ya Mkuu wa Mkoa, toka Wakuu wa Mikoa wamepewa huu mfuko kwa ajili ya kuwasaidia Wabunge, hakuna hata Mbunge mmoja ambaye amejengewa ofisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja kwenye Ofisi ya Bunge tunaomba vitendea kazi lakini tunaambiwa viko kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Mikoa hawatuelezi ukweli. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja kutoa hitimisho lake atuelekeze vizuri Wabunge tusisumbue Bunge. Tukisumbua Bunge wakati kitu hiki kishatengwa kwamba kwenye Waraka wa Rais wa mwaka 2010 unaonesha kwamba Mfuko huu uko chini ya Mkuu wa Mkoa na sisi tukija hapa tunaendelea kuwasumbua wenzetu ili tuonekane kwamba tunafanya kazi nzuri lakini kule vijijini watu hawajui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tusijitetee sisi tu. Hapa tuko katika mazingira mazuri kufuatana na utendaji mzuri wa Rais wetu, lakini kuna Watendaji ndani ya Bunge hili wanafika wakati wao wenzetu ambao wanatusaidia kwa kila kitu hata mishahara wakati mwingine wanakaa miezi mitatu hawapati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge hakuna Mbunge ana mazingira magumu. Tulizoea raha sana ndiyo leo tunaona kwamba kuna ukata. Watu wanakwenda kwenye vyombo vya habari kusema kwamba kuna mazingira magumu, mazingira magumu hakuna. Ukiangalia bajeti yetu
ni ile ile, ila siku za nyuma Wabunge tuli-relax sana tukajisahau ndiyo maana inafika mahali mtu anakimbilia kwenye Vyombo vya Habari kusema Bunge baya, Bunge gumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mazingira ya mwaka 2010 hakuna kilichopungua ila utendaji wetu, raha zetu, maisha yetu, ndiyo tunakimbilia kusema kwamba maisha magumu. Hela tunapata kwa wakati, hela ni ile ile. Tulikuwa tunapata sh. 80,000, lakini sasa hivi tunapata karibu sh. 120,000 na tunapata sh. 200,000. Sasa tukianza kuyasema haya hatutendi haki. Naomba tuwe wawazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapana! Niacheni niseme, kila mtu anasema kwa wakati wake, kila mtu yuko huru kusema. Tusiwe tu watu wa
kulalamika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niyaseme haya mapema kwa sababu inafika mahali tunakimbilia vyombo vya habari, tukae wenyewe, tuna uongozi wetu, tukae chini, tuangalie upungufu uko wapi, turekebishe kuliko kukimbilia kulalamika, kama sisi tunalalamika na wapiga kura nao watamlalamikia nani? Nimekosea eeh? Kumbe imefika mahali pake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kwenye suala la matibabu ya Wabunge. Tungeomba ikiwezekana Waziri Mkuu amshauri Rais, matibabu ya Wabunge yarudi kwa Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu yalikuwa….
Taarifa....
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei, kama yeye alikuja kufuata maslahi...
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, sasa sipokei taarifa kutoka upande wowote.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachojua kilichotuleta hapa siyo maslahi ya Wabunge ni maslahi ya wapiga kura waliotuchagua kuja kutetea Bunge hili. Kama watu walifuata maslahi basi wakabadilishe kazi ambayo itakuwa na maslahi juu yao lakini ninachokumbuka kilichotuleta hapa ni kutetea wanyonge waliotuchagua ili tuwape maslahi mazuri waendelee kutuchagua kwa namna
yoyote ile. Kwa hiyo, taarifa yake siipokei akatafute sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala la matibabu ya Wabunge, naomba mzigo mkubwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu, naona kuna mahali nimewagonga kidogo ndugu zangu. Kama kuna mahali nimewakosea ndugu zangu Wabunge basi kawaida ya mtu huwa tunasameheana basi tugange yanayokuja, ahsanteni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na suala la matibabu. Siku za nyuma suala la matibabu yalikuwa yanapitia Ofisi ya Spika na yeye alikuwa
anajua huyu anaumwa au huyu haumwi, inategemea sasa hivi tumeona kwamba Rais anafanya kazi nzuri sana lakini baadhi ya watumishi wake wanaweza kuchelewesha kitu kwa makusudi na kumfanya mgonjwa azidiwe. Hapa ningeomba Mheshimiwa Rais ambakishie madaraka Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kutusaidia katika kututibu au kwenda kuzungumzia suala la aina yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nizungumzie mambo machache naona taarifa zinakuwa nyingi kwa sababu nimegusa maslahi ya Wabunge, nilichokuwa nataka kujali ni kwamba kauli aliyosema Mheshimiwa Simbachawene kwamba hakuna tunachokidai mambo yote yako sawa, kwa hiyo naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hoja zangu zote alinisaidia kunisafirisha India kwa kunilipia watu zaidi ya wawili. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa msaada wako mkubwa, usifanye kwangu tu, fanya na kwa hawa wengine ambao
maslahi yao wanaona kama yamebanwa banwa, Mungu awasaidie sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayofanya, vilevile nisiache kumpongeza Waziri wa Wizara hii, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Mameneja wa Mikoa hasa Mkoa wangu wa Tanga kwa kazi nzuri wanazozifanya. Usiposhukuru kwa kidogo, hata kikubwa utakachopewa hutashukuru. (Makofi)

Vilevile Mheshimiwa Waziri wangu naomba nikwambie kitu kimoja ambacho kiko ndani ya msingi wangu mkubwa kwamba safari hii nitashika Mshahara wako, nasema haya kwa sababu zifuatazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, toka mwaka 2010 Barabara ya kutoka Korogwe kwenda Bumbuli hadi Soni, iko ndani ta Ilani ya Uchaguzi, barabara hii ilitengewa kwamba itawekwa lami, lakini mpaka mwaka jana barabara hii haikutengewa pesa ya aina yoyote, mwaka huu imetengewa milioni 130 tu. Mheshimiwa Waziri hata bubu wakati mwingine ukimzidia anasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatupendi sana kuwa tunaongea sana humu ndani, kubishana na viongozi, lakini inapofika mahali tunaponyamaza sana tunaonekana watu wengine hatusemi. Sasa kwa mtazamo huu safari hii nataka niwaambie ukweli kwamba nitashika shilingi ya Waziri. Kwa sababu tumevumilia mno, mahali pengine kote kunatengenezwa barabara, lakini barabara yangu miaka saba. Na miaka saba hii sioni sababu yoyote ambayo inazuia, kila kitu kimefanyika! Niliona niliseme hilo mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya lami ambayo iliahidiwa na Serikali ya Awamu ya Nne, kilometa
1.1 katika Mji wa Mombo, lakini barabara hii mpaka leo wala sijui kwamba mawazo yao hasa ni nini. Mpaka leo hii haioneshi kwamba inaweza kujengwa kiwango cha lami na vilevile awamu zote mbili zimesema itajengwa kiwango cha lami. Naomba Waziri mhusika muiangalie, sisi hatupendi sana tuwe watu wa kubishana, sisi ndiyo wenye Serikali, tunataka tuisaidie Serikali, pale mahali ambapo tunaona inakwenda tofauti tuunge mkono ili mtusaidie. Sasa tukinyamaza na ninyi wenzetu mnatuona kwamba hatuongei haileti maana nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni bandari ya nchi kavu; katika awamu iliyopita tulikuwa tunasema kwamba katika Mkoa wa Tanga kutakuwepo na bandari ya nchi kavu pale Korogwe, hili mpaka leo imekuwa kama kizungumkuti, haioneshi dalili wala hakuna dalili yoyote, tunayoisikia hapa ni reli ya kati tu na bandari nyingine, Bandari ya Tanga na Mtwara tunaziona kama vile zinasahaulika. Mkifanya namna hii tunakuwa wanyonge kwa sababu ukitaka kuichukua Tanga lazima utaje Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Mwanza pamoja na Manyara hii ukiijumlisha inatoa neno la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika reli, reli ambayo ni ya mwanzo kabisa, mojawapo ni reli ya Mkoa wa Tanga. Nashangaa inakuwa ni vitu tofauti, tunapigwa chenga tu, sijui kwa sababu hatuongei au kwa sababu tumenyamaza sana. Naomba Serikali ituangalie, unaposema kwamba mpango wa biashara, uchumi, uchumi hauletwi na Mikoa ya Kati peke yake ni Tanzania nzima lazima kuwe na uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu hizi barabara za mkoa. Barabara za Mkoa Mameneja wa Mikoa wanafanya kazi nzuri sana, lakini wakandarasi wanatuumiza.

Kuna sehemu inakuwa heavy grading ambayo ni lazima uchimbue barabara halafu ushindilie, lakini cha kushangaza kuna sehemu hawafanyi hizo kazi na hela wanapewa, halafu kibaya zaidi ni kwamba, hela ambazo zinatengwa na Serikali baadae unaambiwa zimechukuliwa tena kwenye Wizara zinapelekwa sehemu nyingine. Hivi maana yake mnaposema hela zinakwenda kwenye mikoa, halafu Wizara inakuja inazipunguza pesa zile na barabara zinakuwa zinaharibika, hivi mkifanya namna hii tutakuwa tunafika mbali? Naiomba Serikali kama tatizo hili lipo naomba litekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwenye barabara yangu ya kutoka Korogwe kwenda Maguzoni - Muheza imeondolewa hela. Barabara ya kutoka Korogwe kwenda Maramba – Daruni mpaka njia panda ya kwenda Mombasa, wameondoa fedha. Sasa hivi mvua imenyesha barabara ilijengwa vizuri, lakini imefumuka yote kwa sababu malengo ya kutengeneza barabara hayakufanyika. Naomba sana Serikali iangalie suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo linatusumbua sana ni mawasiliano. Katika Tanzania sehemu ambayo inatoa madini nyeti sana ni katika kata ya Kalalani katika kijiji cha Kigwasi lakini sehemu nyingine zote kuna mawasiliano, hapa pia ni Mbuga ya Mkomazi na hapa pia ndipo kunakotoka madini ya aina mbalimbali. Tumeongea, nimekuja nimeongea hapa Bungeni, yanaingia kwenye sikio hili yanatokea sikio hili. Sasa sipendi sana kubishana na Serikali kwa sababu kazi kubwa mmeshatufanyia, hizi ndogo ndogo ni kurekebishiana tu ili tuone kwamba namna gani mtatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wachangiaji wenzangu wameongea sana, lakini ukweli mnatuonea sana watu wa Tanga hasa Bandari ya Mwambani. Kila mwaka mnaongelea suala la bandari, mtu anatoka Tanzania anakwenda kutoa mizigo Mombasa anaacha kwenda Tanga kwenda kutoa mizigo wakati ni bandari nzuri. Mtu anaondoka anakwenda anaacha Bandari ya Mtwara yenye kina kirefu, mtu anakwenda Mombasa. Kwa nini jamani? Tuna makosa gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mkigawa, hata kama kasungura kadogo kama alivyoongea Mbunge mwenzangu wa Mwanza lakini tugawane kidogo, mnapotugawia kidogo nasi tunakuwa na nguvu. Mkinyamaza sana mwisho wake tutakuwa tunasema kwamba hawa labda hatuna imani, lakini mimi nina imani sana na Serikali ya Awamu ya Tano kwa haya mnayofanya, kwa sababu leo pia Rais amenifurahisha sana baada ya kusema yeye hataki vyeti feki, anataka mtu elimu yake aiseme ile. Mimi elimu yangu ni ya darasa la saba na ninaomba muendelee kuichunguza hivyo hivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna minara pale kwangu kwa Mkole katika kata ya Chekelei, kijiji cha Bagai, mnara huo umefungwa toka mwezi wa kwanza mpaka leo hii haujafunguliwa sijui sababu ni nini? Kuna kata ya Kizara mmejenga mnara mzuri sana lakini mawasiliano yake yanakuwa ni hafifu.

Naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako, mmenisaidia sana katika mambo yangu ya kimsingi katika Jimbo langu hasa nilipokuwa naumwa. Mmefanya kazi kubwa sana ya kunipelekea fedha kwa kupitia Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Tanga na barabara zangu zinapitika vizuri, sitapenda kuwaangusha, lakini msituangushe mahali ambapo tunawaamini kwamba ni watendaji wazuri wa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache naunga mkono hoja, ujue usipokuja na majibu mazuri hiyo siku ya kuidhinisha ninatoa shilingi yangu mpaka uniambie barabara ya kutoka Korogwe - Kwashemshi - Dindila - Bumbuli - Soni, sasa ijengwe kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, nataka nirudie suala langu la jana naomba nishukuru watu wafuatao. Nimshukuru Mheshimiwa Spika, Katibu wa Bunge, Ofisi ya Uhasibu, Wabunge wote wa Mkoa wa Tanga kwa msaada walionipatia, Wizara ya Afya chini ya Mheshimiwa Waziri Ummy, pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na rafiki yangu Ndassa kila wakati alikuwa anakuja kumuona mgonjwa pale Muhimbili. Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanayoifanya. Leo ilikuwa nichangie makubwa sana lakini kufuatana na hotuba na gawiwo walilokuwa wamelipata, Wabunge wenzangu tujaribu kuwaunga mkono hawa mabwana. Kwa sababu tulikuwa tunatarajia kwamba Serikali au Hazina ingetupatia fedha nyingi ili itusaidie katika suala la umeme lakini cha kushangaza ni kwamba hela zile nyingi hazikupatikana na Waziri anafanya kazi katika mazingira magumu na amekuja kwangu mara nyingi na amesema yale aliyokuwa anataka kuyafanya hayafanyiki kwa sababu hana fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuwashukuru sana wenzetu wa REA wanafanya kazi katika mazingira magumu. Hata hivyo, tuna mtihani Wabunge wote tuliokuwa hapa ndani, bila kukaa vizuri na Hazina wakatupa fedha hawa Wabunge hapa wameweka Ubunge wao rehani. Wakati wa mwanzo tulipewa orodha ya vijiji ambavyo vitapata umeme wa REA na Wabunge wakafurahia wakapeleka katika majimbo yao na kuonyesha kwamba umeme huu utafika kwa wakati fulani. Cha kusikitisha vijiji ambavyo vilipewa majina na Wabunge tukaenda tukavisemea na Madiwani wakaenda wakavisemea vimekatwa vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nina kata ishirini na tisa, kuna kata saba ambazo toka Uhuru hazijapata umeme. Mwaka huu ziliingizwa kwenye mpangilio wa kupata umeme, leo hii naambiwa zile kata hazina umeme, nina kwenda kuwaambia nini wapiga kura? Inasikitisha sana, nina Kata za Kizara, Kalalani, Mpale, Mswaha, Mkalamo na Folofolo toka Uhuru umeme wanausikia. Ukizingatia Wilaya ya Korogwe ina viongozi wakuu wanatoka pale. Kwa mfano, kata ambayo anatoka Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu, Kata ya Mkomazi haina umeme. Huyo Assad ambaye anawakagua hapa anatoka kwenye jimbo langu lakini kwake hakuna umeme. Ukienda Kata ya Mtindiro, Kijiji cha Mtindiro hakina umeme, ukienda vijiji vingine zilivyoko pale havina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Askofu Mkuu wa Anglikana anatoka kwenye Jimbo langu, Mheshimiwa Mndolwa lakini leo hii umeme umepita nyumbani kwake, wameruka, wanakwenda kuangalia sehemu nyingine, mnatuweka wapi? Wabunge tutasema nini kwa wapiga kura? Keshokutwa mnataka tuwachague Wenyeviti wa Serikali za Vijiji watakwenda kusema nini kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi simlaumu kabisa Mheshimiwa Waziri, wala siwalaumu watu wa REA, wanafanya kazi katika mazingira magumu lakini huko Hazina kuna nini kibaya? Leo mnatuandikia hapa kwamba tunapokwenda kulipa bili TANESCO, REA wanakata asilimia 3, Ewura wanakata asilimia 1, nani anachukua hela hii? Leo hii kila tukisema hela, makandarasi wanasema hela hawajapewa, unaangalia ukienda kwenye mafuta tunakatwa hela, ukienda kwenye kulipia umeme tunakatwa hela, maji tunakatwa hela ya umeme leo hii tukikulaumu Mheshimiwa Waziri tunafanya makosa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wabunge wenzangu tuungane tumsaidie hizi fedha ambazo zilikuwa zinazungushwa apatiwe tumaliziwe miradi yetu. Mheshimiwa umezunguka nchi nzima hii unawasha umeme lakini cha kushangaza katika vijiji vyote watu wamerundika nguzo tu ukiuliza wanasema hatujapewa fedha. Sasa tunaipeleka wapi hii nchi, tunapeleka wapi wapiga kura wetu? Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama hizi hela zilikuwa haziendi REA au TANESCO, basi naomba tuondoeni hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wananchi wanatulalamikia wanasema Wabunge wanakwenda kulala, Wabunge wanaonyesha nia kwamba tunatetea umeme, umeme huo tunautetea ni upi? Kama umeme haupatikani, umeme haufiki, Waziri amekuja kwenye Jimbo langu wakati wa kampeni akasema sehemu ambazo zilikuwa hazina umeme upatikane. Kinachoshangaza sana Mheshimiwa Waziri, vile vijiji ambavyo ulisema vipate umeme havipati tena umeme kinapata kijiji kimoja eti hela hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kwenye Jimbo langu kuna mradi wa maji, kuna nguzo zimewekwa na TANESCO toka 2004 mpaka leo waya hazijawekwa. Tumekwenda na viongozi wa TANESCO wa Mkoa, viongozi wamekwenda pale wamenisemea, wananchi wamesikia leo wanakwambia umeme haufiki, mimi mnaniweka wapi na Wabunge wengine tunawaweka wapi? Hii ipo ndani ya Ilani ya Uchaguzi, kwa nini tusitekeleze haya mambo? Mheshimiwa Dkt. Kalemani ni mchapakazi wa hali ya juu sana, hebu tujaribu Bunge hili kuhakikisha pale mahali ambapo fedha za EWURA na REA, zilipokwamia zijaziwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mweyekiti, suala la pili ni la bomba la mafuta. Tuna kawaida mabomba ya mafuta au kitu chochote kizuri kinapokuja wananchi wanakuwa hawatengewi sehemu badala yake wanachukuliwa watu kutoka nje Watanzania tunabaki hivihivi. Mheshimiwa Waziri bomba la mafuta umekuja, umeliona, umetathmini, umetupa hamasa, watu hawa wote wanaopitiwa na bomba la mafuta naomba Watanzania wawe wa kwanza kupewa kazi. Kuna taratibu watu wanakuja na watu wao, Watanzania ambao watalilinda bomba lile hawapati kazi. Naomba Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu sana na ni rafiki yangu sana lakini kwa leo naomba uhakikishe kwamba bomba la mafuta linalopita katika ile Mikoa yote Watanzania wa nchi hii wapate kazi kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nisisitize katika vijiji ambavyo mlikuwa mna-support kwamba vipate umeme Tanzania nzima, kwa kupitia mpango wa REA naomba virudishwe kwenye orodha. Mkurugenzi wa REA Maganga anakaimu, unafikiri atatoa maamuzi gani? Huyo Bwana Msofe ni mtu mmoja mzuri ukimpigia simu hata saa nane za usiku anakupokea, ukienda Mwenyekiti wa Bodi wa REA ni watu wasikivu, wapewe fedha ili hii kazi iishe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, kwa sababu naumwa niliomba tu niwe mtu wa kwanza, naomba niwahi Muhimbili lakini naunga mkono asilimia mia kwa mia Waziri apatiwe fedha afanye kazi. Mungu awabariki sana, ahsanteni sana.