Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stephen Hillary Ngonyani (12 total)

MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Katika Jimbo la Korogwe Vijijini yako mashamba ambayo tangu yabinafsishwe hayajaendelezwa:-
(a) Je, ni lini mashamba hayo yatagawiwa kwa wananchi kwa sababu hayaendelezwi?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuyatoa kwa wananchi mashamba ambayo hayaendelezwi ili kuwapa fursa ya kuyatumia kwa shughuli za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali namba 67 la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani, naomba kutoa maelezo ya utangulizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kukagua mashamba na kuwasilisha taarifa za ukaguzi na hatua stahiki. Mashamba yatakayobainika kwamba hayajaendelezwa ilani ya ubatilisho zitatumwa na Wakurugenzi husika kwa umilikishaji. Baada ya kipindi cha siku 90 kumalizika Halmshauri zitatakiwa kuleta mapendekezo ya ubatilisho Wizarani.
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukaguzi uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, umebaini kuwepo kwa shamba lisiloendelezwa la Mwakijubi Farm linalomilikiwa na Ndugu Chavda. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ameanza kufanya taratibu za ubatilisho wa milki kabla ya kuwasilisha mapendekezo Wizarani.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ugawaji wa mashamba kwa wananchi hufanyika baada ya taratibu za ubatilisho kukamilika na kupata kibali cha Mheshimiwa Rais. Taratibu za ubatilisho zinapokamilika mashamba haya hurejeshwa katika Halmashauri husika ili yapangiwe matumizi mengine ikiwemo kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yetu sasa baada ya taratibu za ubatilisho kukamilika na maeneo haya kukabidhiwa kwenye Halmashauri, Halmashauri watapanga matumizi kulingana na uhitaji wa eneo husika ikiwa ni pamoja na matumizi ya kilimo. Kwa sasa, wakati zoezi la ubatilisho linafanyiwa kazi, tunaomba wananchi waendelee kuvuta subira mpaka hapo mchakato wa ubatilisho utakapokamilika.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Mji wa Mombo ni mji unaokua kwa kasi kubwa na kuna mradi mkubwa wa maji unaotoka Vuga – Bumbuli kwenda Mombo katika Kitongoji cha Mlembule na mradi huo utagharimu shilingi 900,000,000.
(a) Je, ni lini mradi huo utakamilika?
(b) Kwa kuwa mradi huo unapita katikati ya Mji wa Mombo, je, Mji wa Mombo utafaidikaje na mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Kijiji cha Mlembule ambacho kwa sasa ni mtaa ndani ya Mji Mdogo wa Mombo ni Mradi wa Maji ya Mtiririko ambao ulianza kujengwa mwezi Desemba mwaka 2013 chini ya mpango wa vijiji 10 kwa kila halmashauri. Mradi huu ulikusudiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 913.5. Mradi huu ulishindwa kukamilika kwa wakati kutokana na wananchi wa vijiji vya Kishewa, Kihitu na Kidundai kumzuia mkandarasi asijenge chanzo cha maji hadi wao pia wapatiwe huduma yao kwani chanzo cha maji kipo kwenye kijiji chao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa utekelezaji unahusisha jamii, Serikali imeridhia mradi huo uendelee kwa kujenga chanzo kipya kitakachokuwa na maji ya kutosha ili kuwahudumia pia wakazi wa vijiji vya Kishewa, Kihitu, Kidundai pamoja na Mji wa Mombo. Kwa sasa Mhandisi Mshauri yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha usanifu ikihusisha chanzo kipya cha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Halmashauri ya Korogwe imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya kukamilisha miradi inayoendelea ukiwemo mradi huo.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Kata ya Kizara tangu uhuru haijawahi kuwa na mawasiliano ya simu:-
Je, ni lini Kata hiyo itapatiwa mawasiliano ya simu?
NAIBU WIZARA WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kuwa Kata ya Kizara haina mawasailiano ya uhakika ya simu. Kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ilikiingiza Kijiji cha Bombo-Majimoto kutoka katika Kata ya Kizara katika utekelezaji wa Mradi wa Mawasiliano Vijijini wa Awamu ya Pili ‘B’.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unaotekelezwa na Kampuni ya Simu ya TIGO kwa ruzuku ya Dola za Kimarekani 105,920, ulianza kutekelezwa tarehe 23 Mei, 2015. Hadi sasa TIGO wameshafanya technical surveys ya eneo la kujenga mnara na manunuzi ya eneo hilo ambapo mradi unategemewa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Vijiji vya Kilangangua, Kizara Kwemkole na Kwenkeyu vimo katika utekelezaji wa Awamu ya Pili na Awamu ya Tatu ya miradi ya Viettel kwa maana ya Hallotel ambapo vijiji vinavyobaki vya Foroforo, Kiuzani na Mangunga-Mziya vitaingizwa katika miradi ya mawasiliano itakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 kutegemeana na upatikanaji wa fedha za mradi.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Shamba la Mkonge la Hale Mwakinyumbi lilimilikiwa na Chavda Ltd. lakini Serikali ililitoa shamba hilo kwa wananchi wa Hale kwa matumizi yao lakini hulimwa huku wakiwa na wasiwasi kila wakati.
Je, kwa nini Serikali isiwakabidhi rasmi wananchi wa Hale shamba hilo ili wawe na utulivu wanapoendelea na shughuli zao za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 95 la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shamba la Mwakinyumbi ni shamba linalomilikiwa na Kampuni ya Mwakinyumbi Sisal Estates Ltd. ya M/s Chavda. Bwana Chavda alinunua shamba hili kwa Mamlaka ya Mkonge Tanzania wakati wa awamu ya kwanza ya ubinafsishaji wa mashamba ya mkonge mwaka 1985 na 1988.
Mheshimiwa Spika, wakati wa ubinafsishaji sehemu ya shamba hili lilitolewa kwa wananchi wa vijiji vya Mwakinyumbi Stesheni na Hale kwa ajili ya makazi na kilimo cha mazao ya chakula. Shamba hili limeacha kuzalisha tangu mwaka 1994 baada ya kutelekezwa na mmiliki.
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 20 Julai, 2016 nilifanya ziara Mkoani Tanga na katika ziara hiyo nilitembelea mashamba ya Mwakinyumbi, Magunga, Magoma na Kwashemshi yaliyopo katika Wilaya ya Korogwe. Katika kulikagua shamba la Mwakinyumbi, tulibaini kuwa shamba hili limevamiwa na wananchi na taasisi mbalimbali kwa shughuli za kilimo na uchimbaji kokoto.
Mheshimiwa Spika, tayari Wizara yangu ilishatoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kuanza utaratibu wa ubatilisho wa miliki hiyo. Hata hivyo, katika kutekeleza maelekezo haya mnamo tarehe 5 Agosti Halmashauri ilituma ilani ya siku 90 ya kusudio la kufuta miliki ya shamba hilo.
Mheshimiwa Spika, ili wananchi wa Korogwe waweze kukabidhiwa sehemu ya shamba hilo rasmi kupitia Halmashauri yao, taratibu za ubatilisho lazima zikamilishwe. Ninatoa rai kwa wananchi wa Korogwe kuwa na subira wakati Serikali inashughulikia suala hili.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu, nitoe rai pia kwa Halmashauri zote nchini kuendelea kuainisha mashamba pori na viwanja vilivyotelekezwa ili mchakato wa kisheria wa kufuta milki zake ufanyike kwa wakati na kuondoa migogoro inayozidi kushamiri siku hadi siku.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Wakulima wadogo wadogo wa mkonge wamekuwa wakiuza mkonge kwa Kampuni ya Katani lakini kampuni hiyo imekuwa haiwalipi wakulima fedha zao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wote kumkaribisha Mheshimiwa Ngonyani tena Bungeni, lakini zaidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumrejesha salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme vilevile kwamba kuna kitu ambacho mimi kimenigusa sana. Muda wote ambao Mheshimiwa Ngonyani amekuwa mgonjwa hakusita kuendelea na majukumu yake ya Kibunge kwani aliendelea kuwasiliana na Wizara yangu kuwatetea wananchi wake na hata hili swali ambalo ameuliza, amepiga simu mara nyingi sana kuulizia madeni ya wananchi wake wanaodai madai ya Katani, kwa hiyo, ameonyesha uwakilishi uliotukuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Steven Hilary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko ya wakulima wadogo wa mkonge walio chini ya scheme ya Sisal Smallholders and Outgrowers Scheme (SISO) ya kutoridhika na ucheleweshwaji wa malipo yao kwa mkonge unaosindikwa na Kampuni ya Katani Limited. Scheme hii inaendesha kilimo cha mkataba ambapo chini ya mfumo huu Katani Limited ni mnunuzi na msindikaji wa mkonge wa mkulima wakati mkulima ana wajibu wa kupanda, kutunza, kuvuna na kusafirisha mkonge wake hadi kwenye kiwanda (Korona) inayomilikiwa na Katani Limited katika shamba husika kwa ajili ya kusindikwa.
Kwa mujibu wa mkataba kati ya mkulima na Katani Limited, Katani inapaswa kumlipa mkulima fedha zake ndani ya siku 60 baada ya kusindika mkonge wa mkulima, na inapotokea kampuni ya Katani kuchelewesha malipo zaidi ya siku 60, inalazimika kumlipa mkulima malipo hayo pamoja na riba ya asilimia 1.5 ya malipo hayo kwa kila mwezi uliocheleweshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumetokea ucheleweshwaji wa malipo haya kwa mwaka 2016 kutokana na kuyumba kwa masoko ya mkonge duniani na kushuka kwa bei za mkonge. Kampuni imelazimika kuuza shehena iliyokuwepo japo kwa hasara na hivyo hadi sasa wakulima wanadai malipo ya mkonge waliovuniwa ya miezi mitatu yaani Septemba hadi Novemba, 2016 ambayo hayajalipwa. Malipo ya miezi hiyo mitatu yanatarajiwa kufanyika mwezi Februari, 2017 yaani mwezi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Mkonge Tanzania imekuwa ikichukua hatua za kuhakikisha kwamba wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Serikali inapeleka umeme vijijini kupitia mpango wa REA lakini kuna maeneo mengi ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme kwenye kijiji cha Mlalo, Bagamoyo, Mngaza na Kieti kwenye kata ya Vugiri?
(b) Je, ni lini Serikali itafikisha umeme kwenye kata mpya ya Mpale?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Ngonyani, almaarufu Maji Marefu, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Mradi Kabambe wa REA katika nchi nzima kama nilivyosema umeanza tangu mwezi Machi, 2017. Mradi huu utajumuisha vipengele vya mradi vitatu katika mikoa yote, Grid Densification, Grid Extension na Off-Grid Renewable. Katika eneo la Mheshimiwa vijiji vya Bagamoyo, Kieti, Mlalo na Mganza katika Kata ya Buhuli vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu utakaokamilika mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme maeneo hayo itajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa umeme wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 6.6; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 19; ufungaji wa transfoma saba pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 350. Gharama ya kazi hiyo ni shilingi bilioni 940.9
MHE. MARY P. CHATANDA (K.n. y. MHE. STEPHEN H. NGONYANI) aliuliza:-
Serikali ilitenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi lakini baadaye Serikali ilihamishia fedha hizo Mkoa mwingine.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha pesa hiyo ili Bwawa lililokusudiwa lijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2003 na 2004 wananchi wa kijiji cha Manga Mkocheni, kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe walionesha hitaji la mradi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga katika Bonde la Mkomazi. Aidha, mwaka wa fedha 2006/2007 Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa wakati huo kupitia Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanyika upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ambapo walibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni kumi na tatu zingehitajika kuendeleza Bonde la Mkomazi ikiwemo ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo, usanifu huo ulibaini kuwa bwawa hilo lingezamisha Ziwa Manga lililopo katika Kijiji cha Manga, ambalo lina maji ya chumvi ambayo yangeathiri kilimo cha zao la mpunga. Kutokana na changamoto hii mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilianza kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu kwa kuepuka kuzamisha Ziwa Manga na kubaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufikia azma hii Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016 ilitenga jumla ya shilingi milioni mia nane kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi. Hata hivyo bajeti ya maendeleo kwa fedha za ndani iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji ikiwemo Bwawa la Mkomazi haikutolewa na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezwa. Sambamba na fedha hizo kutotolewa bado kuna baadhi ya wananchi ambao walikuwa wanaukataa mradi kwa sababu ya maeneo yao kuzamishwa ndani ya maji na hivyo kufanya mazingira ya kutekeleza mradi huo kutokuwa rafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi walio wengi wa Kata ya Mkomazi kupitia Mheshimiwa Mbunge bado wanaona umuhimu wa mradi huo na hasa katika hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji italiingiza bwawa hili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza utekelezaji ili hatimaye lengo la Serikali na wananchi wa Mkomazi waweze kuwa na kilimo cha uhakika na hivyo kuwa na usalama wa chakula na kujiongezea kipato kupitia zao la mpunga.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Serikali iliahidi kutoa shilingi milioni 60 kwa ajili ya mradi wa maji wa Sakare ulioko Tarafa ya Bungu na mpaka sasa imetoa shilingi milioni 20 tu; Je, ni lini fedha iliyobaki itatolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Sakare unahudumia jumla ya vijiji saba kutoka kwenye Tarafa ya Bungu vyenye wakazi wapatao 18,460. Ili kutekeleza ahadi iliyotolewa katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeidhinisha shilingi milioni 81.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Sakare. Azma ya Serikali ni kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi wa vijiji saba katika Tarafa ya Bungu waweze kupata maji safi na salama.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Miongoni mwa Mahakama za Mwanzo ambazo Serikali iliahidi na kuamua kuzijenga ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Mkomazi. Je, ni lini Mahakama ya Mwanzo Mkomazi itajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niba ya Waziri wa Katibu na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Mwanzo ya Mkomazi ni moja ya Mahakama zilizo kwenye mpango wa ukarabati na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo nchini. Hivyo, kwa mujibu wa mpango huo Mahakama ya Mwanzo Mkomazi imepangwa kujengwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. MARY P. CHATANDA (K.n. y. MHE. STEPHEN H. NGONYANI) aliuliza:-
Serikali ilitenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi lakini baadaye Serikali ilihamishia fedha hizo Mkoa mwingine.
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha pesa hiyo ili Bwawa lililokusudiwa lijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2003 na 2004 wananchi wa kijiji cha Manga Mkocheni, kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe walionesha hitaji la mradi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga katika Bonde la Mkomazi. Aidha, mwaka wa fedha 2006/2007 Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa wakati huo kupitia Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanyika upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ambapo walibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni kumi na tatu zingehitajika kuendeleza Bonde la Mkomazi ikiwemo ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Hata hivyo, usanifu huo ulibaini kuwa bwawa hilo lingezamisha Ziwa Manga lililopo katika Kijiji cha Manga, ambalo lina maji ya chumvi ambayo yangeathiri kilimo cha zao la mpunga. Kutokana na changamoto hii mwaka wa fedha 2014/2015 Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilianza kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu kwa kuepuka kuzamisha Ziwa Manga na kubaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufikia azma hii Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016 ilitenga jumla ya shilingi milioni mia nane kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi. Hata hivyo bajeti ya maendeleo kwa fedha za ndani iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji ikiwemo Bwawa la Mkomazi haikutolewa na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezwa. Sambamba na fedha hizo kutotolewa bado kuna baadhi ya wananchi ambao walikuwa wanaukataa mradi kwa sababu ya maeneo yao kuzamishwa ndani ya maji na hivyo kufanya mazingira ya kutekeleza mradi huo kutokuwa rafiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi walio wengi wa Kata ya Mkomazi kupitia Mheshimiwa Mbunge bado wanaona umuhimu wa mradi huo na hasa katika hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Wizara yangu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji italiingiza bwawa hili katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza utekelezaji ili hatimaye lengo la Serikali na wananchi wa Mkomazi waweze kuwa na kilimo cha uhakika na hivyo kuwa na usalama wa chakula na kujiongezea kipato kupitia zao la mpunga.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Katika Kata ya Magoma, Korogwe Vijijini kumejengwa Mahakama ya Mwanzo ya Kisasa, lakini toka ijengwe imefika miaka saba sasa haijafunguliwa:-
Je, ni lini Serikali itafungua Mahakama hiyo ili wananchi waachane na usumbufu wa kufuata huduma za Mahakama Korogwe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ya Mwanzo ya Magoma ilijengwa muda mrefu kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge wa Korogwe, lakini jengo lile halikukamilika. Mahakama iliyojengwa ni ya kisasa, iliyohusisha ujenzi wa jengo la Mahakama, nyumba ya Hakimu na kantini.
Mheshimiwa Naibu Spika, majengo haya yalisimama kwa muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa fedha. Mradi huu sasa umefufuliwa na unatekelezwa na SUMA JKT, chini ya usimamizi wa TBA Mkoa wa Tanga na unatarajiwa kukamilika na kuanza kutumika kabla ya Julai mwaka huu 2018.
MHE. MARY P. CHATANDA - (K.n.y MHE. STEPHEN H. NGONYANI) aliuliza:-
Serikali ilitenga shilingi bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi lakini baadaye Serikali ilihamishia fedha hizo mkoa mwingine:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha fedha hizo ili bwawa lililokusudiwa lijengwe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nimpe pole Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake wa Korogwe Vijijini kwa msiba wa kufiwa na mke wake kipenzi. Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2003 na 2004 wananchi wa Kijiji cha Manga Mikocheni, Kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe walionesha hitaji la mradi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji kwa zao la mpunga katika Bonde la Mkomazi. Aidha, kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa wakati huo kupitia Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ambapo walibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 13 zingehitajika kuendeleza bonde la Mkomazi ikiwemo ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Spika, aidha, upembuzi huo, ulibainisha kuwa ujenzi wa bwawa hili ungesababisha Ziwa Manga lilipopo katika Kijiji cha Manga ambalo lina maji ya chumvi kuchanganya maji yake ya Bwawa la Mkomazi hivyo maji yote kuwa ya chumvi ambayo yangeathiri kilimo cha zao la mpunga.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hii mwaka 2014/2015, Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro ilifanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kuepuka kuzamisha Ziwa Manga na kubaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zingehitajika kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
Mheshimiwa Spika, katika kufikia azma hiyo, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2015/2016, ilitenga jumla ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Mkomazi. Hata hivyo, fedha za ndani zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo hazikupatikana na hivyo kusababisha mradi huo kutotekelezwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa mradi huo na hasa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Wizara kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inatarajia kuliingiza bwawa hilo katika vipaumbele vya kutekeleza Mpango Kabambe wa Umwagiliaji wa Taifa ambao kwa sasa unafanyiwa mapitio kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA). Mapitio hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018. (Makofi)