Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Salum Mwinyi Rehani (11 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE: SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii adhimu kwangu ya kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais na nitaomba tuchangie na sisi wengine tutachangia kitaalam zaidi kuliko kisiasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo langu la Uzini, walioniwezesha leo hii kuweko hapa ili kutoa mchango wangu huu katika Ofisi ya Makamu wa Rais na hasa kwenye upande wa Mazingira. Hali ya Tanzania ni tete, bado hakujawa na mikakati ya utekelezaji wa Sera na miongozo mbalimbali, kwa ajili ya kuhami mazingira yaliyopo. Nchi hii miaka 20 na miaka 10 iliyopita sivyo ilivyo leo, kila siku zikienda nchi inakwenda na maji na kama hakutakuwa na uthubutu wa udhibiti wa mazingira tuliyonayo baada ya miaka 10 hapa tutakuwa hatuna tofauti na wale wenzetu wa Ethiopia na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala zima la uharibifu wa mazingira lakini vilevile na kuondoka kwa uoto wa asili kwa maeneo mbalimbali tuliyonayo katika nchi yetu, miaka 20 iliyopita katika mabonde ya Usangu, ukija mpaka Mlimba na Iringa, yalikuwa ni mabonde ambayo yanaitwa ni mabonde chepe, leo hii maeneo yale yameharibika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali ni mbaya zaidi katika Kanda ya Ziwa, hali ya hewa imebadilika, joto limepanda, miti hamna, hali imekuwa ni ngumu zaidi. Ushauri wangu kwa Wizara hii ni kwamba kuwepo na mkakati maalum wa kurudisha uoto wa asili na hasa kwa maeneo yale ya Kanda ya Ziwa na Mikoa ya Kati hapa. Nakuomba Waziri na Waziri Mkuu, uwepo mkakati wa kupanda miti, kwa Watanzania wote, angalau miti minne kwa kila Mtanzania kwa kila mwaka. Mkakati huu ukiwekwa sahihi, tutaweza kuwa na uhakika wa kurudisha hali ya mazingira tuliyonayo. Pia kuweko na aina maalum ya miti ambayo inaweza kuongeza kiwango kikubwa cha uzalishaji wa carbon katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa katika taarifa iliyoletwa hapa na Waziri kwamba uharibifu uliopo uko wa asilimia mbili, latest information na hasa ile taarifa iliyotoka Durban iko zaidi ya hapo. Kila siku tunapokwenda Ozone Layer inazidi kumomonyoka na ndiyo maana joto linapanda na linashuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka mitano iliyokwisha Dodoma kipindi hiki tulikuwa na baridi leo hii tuna joto na hatuna uhakika kwamba itafika mwezi wa saba baridi itarudi kama vile ilivyokuwa, nchi inakwenda na maji!
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu nataka kuunganisha na ule Mfuko aliousema Waziri wa Mazingira, ule ndiyo ukombozi wa nchi hii. Mheshimiwa Waziri nikushauri kitu kimoja, tuanzishe kwa maksudi Mfuko huu na upitie kwenye simu zetu. Kila Mtanzania mwenye simu angalau achangie nusu shilingi katika Mfuko wa Mazingira. Kwa kila sh. 1,000 itaweza kutusaidia utekelezaji wa mbinu mbalimbali za kuweza kuokoa maeneo yale ambayo yameathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ni kwamba, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana urudi kwenye mkakati ule uliotengenezwa na NEAP ambao ulikuwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais. Ule Mpango Mkakati na action plan ya NEAP itaweza kututoa kuhakikisha kwamba tunakuwa na mfumo mzuri wa ufugaji, mfumo mzuri wa kilimo, mfumo mzuri wa viwanda na mfumo mzuri wa kuhakikisha kwamba, kila idara inaweza kushiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira, Wizara zote ni wadau, suala la mazingira ni mtambuka, hivyo kila Wizara inastahili kuweka fungu maalum kuchangia katika Mfuko wa Mazingira. Wizara ya Madini maeneo mengi yanayochimbwa mashimo ya madini hakuna mpango mkakati wa kuyarudisha kama yalivyokuwa, basi isiwe kurudisha lakini kuweza kuyafanya yale maeneo kutumika kwa shughuli nyingine. Mfumo wa Kilimo tunaolima unasababisha ardhi iondoke rutuba, uoto wa asili unapotea na hali ya hewa inazidi kuwa disturbed, uzalishaji kila siku unaendelea kuwa chini. Hofu yangu kama hakutakuwa na nia thabiti ya kudhibiti mazingira haya, Tanzania itafika mahali itaomba chakula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika kuangalia suala zima la uharibifu wa mazingira katika bahari, Tanzania imezungukwa upande mmoja na bahari, lakini kule Zanzibar tumezungukwa na bahari kila pembe. Bado sijaona udhibiti au mkakati maalum wa kuvinusuru visiwa vile na kuinusuru hii nchi upande wa bahari na hali ya mmomonyoko unaokwenda siku hadi siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo za utafiti, kila mwaka bahari inasogeza nusu mita mpaka mita moja juu ya ardhi, kwa hiyo eneo tulilonalo linazidi kupungua, ukiangalia miaka 20 ijayo maeneo mengi ambayo sasa hivi yanakaliwa na watu yatakuwa yamehamwa na maji yatakuwa yamechukua nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi zetu za NEMC na zile zinazofanya impact assessment za kutoa vibali vya ujenzi wa mahoteli na vitu mbalimbali katika maeneo yetu ya bahari, zimekuwa nazo zinatumika kuchangia uharibifu wa mazingira badala ya kunusuru. Nitoe mfano mmoja, tumekuwa na kawaida mahoteli mengi ya Waitaliano yanajengwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nilitaka nitoe shukrani kwa uwasilishaji wa hotuba hii ya Waziri kuhusu bajeti ya elimu. Nilikuwa na mambo ambayo yananisikitisha na hasa kuhusiana na mfumo mzima wa elimu unavyokwenda hapa Tanzania. Kwa kiufupi kusema ukweli, hakuna consistency ambayo tunaiona inatolewa kwa elimu yetu katika level zote. Tuchukulie mfano kule Zanzibar, safari hii wamesema wameanza kufanya mitihani ya Darasa la Sita. Ukitoka Darasa la Sita unaaza Form One.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa wanaoanza shule miaka minne, miaka mitano anaanza Darasa la Kwanza, akifika Darasa la Sita, ana umri gani? Halafu arukishwe aende Form One. Mtu huyo huyo anatakiwa afanye Common Exam Form Four, ambayo inasimamiwa na NECTA. Huku Tanzania Bara Darasa la Saba, lakini Form Four wanafanya Common Exam. Sasa hizi elimu tunaiga mifumo ya nje ambayo kwa kweli haijafanyiwa uchunguzi na utafiti wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya utafiti katika Jimbo langu la Uzini na nilikuwa naandaa strategic plan. Preliminary survey niliyokuwa nimeifanya matatizo niliyoyakuta ndani ya lile Jimbo, kuna tofauti kubwa baina ya shule na shule ndani ya Jimbo, achilia mbali ndani ya Wilaya. Tofauti nyingine iliyokuwepo, ni baina ya shule za private na shule za Serikali, there is no common syllabus. Kila mmoja anaangalia mazingira ya uboreshaji wa elimu kwa eneo lake.
Sasa kwenye Serikali unajiuliza, tofauti ya syllabus hii ya Serikali inatofautiana baina ya shule moja na shule nyingine, lakini kubwa linatokana na kwamba hakuna monitoring, ufuatiliaji haupo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakaguzi ndio wanaoweza kupita katika zile shule wakaweza kuhakikisha kwamba syllabus inayofundishwa pale ni sahihi. Shule zetu nyingi nyingine zinatumia mitaala inayotoka Cambridge, nyingine zinatumia mitaala ya Kenya nyingine zinatumia mitaala waliyotengeneza wenyewe kulingana na mazingira yao; ndiyo maana unakuta level ya upasishaji inakuwa tofauti baina ya eneo moja na lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kama tuna Common Exam, lazima tuwe na mtaala mmoja na flow iwe inaeleweka kutoka chini kuja juu. Flow yetu iliyokuwepo ndiyo kitu kinachotutesa. Kila mmoja anakwenda njia yake. Nchi hii hatutafika kwa kila mmoja kwenda vile anavyoona yeye. Leo ukienda St. Mary‟s na shule nyingine za mission zina miongozo na mitaala yao na kiwango chao cha elimu kinachotolewa ni tofauti kabisa na shule nyingine za private, lakini halikadhalika shule nyingine hizi za vipaji maalum zina miongozo yake na mitaala yake mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tukae pamoja, kama ni NECTA na wadau wake wengine ili kuweza kutoa common syllabus itakayoweza kufuatwa, lakini vilevile ile consistency ya madarasa tukubaliane, kwa sababu wale Wazanzibari wanasema wao wakiona flow imekwenda vizuri mwakani nao Tanzania Bara inataka kuanza mwisho Darasa la Sita, haieleweki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoamua jambo, tujiandae kwanza, tufikiri hawa wanafunzi kweli tunataka kuwapa kitu gani na kwa level gani? Mtoto akimaliza Shule ya Msingi, Darasa la Sita, huyo anamaliza Form Four bado mdogo sana na uwezo wa kukabili mtihani wa Form Four unakuwa haupo. Sasa nashauri kwamba mkutane viongozi wa elimu wa sehemu hizi mbili ili kuwe na mustakabali mzuri wa kuweza kuendesha hizi shughuli na mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linakwaza kwenye elimu ni suala zima la ukosefu wa Walimu husika kwa masomo husika. Shule zetu nyingi Walimu wamekuwa wanabambikiziwa masomo ambayo hawana ujuzi nayo. Mwalimu amesomea arts kwa vile hakuna Mwalimu wa science, anapewa science anaambiwa bwana utaziba kiraka.
Vilevile Mwalimu amesoma science sekondari, pengine Form Two au Form Three, lakini leo ndiyo unamweka Mwalimu huyo aweze kufanya practicals za chemistry na physics kwa wananfunzi wa Form Four. Sasa kwa kufanya hivi, tunaziba viraka. Hii siyo elimu ambayo tunategemea kwamba itaweza kuwasaidia Watanzania. Kuwepo na utaratibu maalumu wa kuajiriwa Walimu wapelekwe katika maeneo maalum ili kuwe na uwiano wa utoaji wa elimu. Vinginevyo bado tutaendelea hapa kuhangaika na kutengeneza bajeti na kushauri lakini hakuna kinachoendelea. Elimu inaporomoka kwa mfumo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kinachotofautiana, shule nyingi zimejenga maabara, lakini tatizo la vifaa vya maabara limekuwa sugu na haviko katika shule chungu nzima. Na leo tuna lengo la kuhakikisha kwamba tunainua elimu ya sayansi katika nchi hii. Watu wale waliokuwa wamejenga maabara pengine inawezekana kwa shinikizo, kwamba lazima iwepo maabara pale, hapana walimu, vifaa vile hata kama wanavipeleka walimu waliokuwepo hawana uwezo wa kufanya zile practical. Kwa hiyo, mtu anakuwa na majengo na vifaa ambavyo havitumiki. Nakuomba Mheshimiwa Waziri hili nalo ukae na timu yako …
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kupata fursa ya kuchangia katika hoja iliyokuwepo sasa hivi Mezani ya Bajeti ya Fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuishukuru Serikali, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha hapa taarifa yake nzuri. Vile vile naishukuru sana taarifa ya Kamati ya Bajeti, imeshauri mambo mengi ya msingi, Namwomba Mheshimiwa Waziri aiangalie kwa jicho la aina yake. Nina mambo kadhaa ambayo napenda niishauri Serikali kuweza kuyaangalia na ikiwezekana kuyafanyia marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza nataka kuzungumza juu ya suala zima la tozo ya bidhaa za mbogamboga za kilimo na hasa kwa wafanyabiashara wale ambao wanatoka Bara kwenda Zanzibar na wale ambao wanatoka Zanzibar kuja Tanzania Bara. Mheshimiwa Waziri hili linarudisha tena kidonda cha kero za Muungano; isitoshe, suala hili halijaangaliwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar hivi sasa ina zaidi ya mahoteli 450 ya utalii. Asilimia 70 ya vyakula ambavyo ni mboga mboga na matunda vinatoka Tanzania Bara. Mazao haya ni very perishable, yaani hayana uwezo wa kustahimili kwa muda mrefu. Leo ukichukua nyanya Ilula, ukifika Dar es Salaam, umemaliza siku moja au siku moja na nusu; robo ya ile bidhaa tayari imeshaharibika. Unangoja meli uyasafirishe kufika Zanzibar, nusu yake nyingine tayari imeshaharibika; lakini bado unatoa pale uyapeleke Kiwengwa au Nungwi ambako ndiko kwenye ulaji wa yale matunda. Mfanyabiashara yule atakwenda mara mbili mara tatu, biashara ile imemshinda. Hapa hatujengi. Tunawavuruga hawa wafanyabiashara na mwisho wake badala ya kwenda mara tatu, mara nne, biashara hii imemalizika. Hakuna biashara itakayokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utafiti tulioufanya mwaka 2014 kwa mwezi mmoja, biashara ya mboga mboga na matunda ni zaidi ya tani 160,000 kwa mwezi mmoja zinasafirishwa kutoka Bara kwenda Zanzibar. Biashara hizo zinaingiza zaidi ya shilingi bilioni 2.6, fedha zinazunguka kila siku kutoka Bara kuja Unguja; yaani eneo hili tunalivuruga. Lazima tuwe makini na tupate maelezo yaliyo sahihi kuhusiana na mazao haya kutozwa tozo hizo ambazo zimependekezwa na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kuzungumza suala zima la makato au tozo za Waheshimiwa Wabunge. Ni eneo ambalo kwa kweli limemgusa kila Mbunge aliyekuwemo ndani ya Bunge hili. Siyo hivyo tu, hasa wale Wabunge ambao wanatoka katika Majimbo waliyogombea; hali ni ngumu Mheshimiwa. Sms zaidi ya 300 kwa siku, kati ya hizo sms 200 zote zinaomba hela. Leo Mbunge huyu unakwenda kusema unamkata kile kiinua mgongo chake unategemea nini? Atarudi vipi hapa? Ni wazi kabisa huo ni mkakati wa kuwadhibiti kwamba hapa wasirudi mwaka 2020 au 2021. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo tu athari yake haitokani na hapo, athari hiyo itatokana vilevile na ile miradi ambayo ilionekana kwamba Mbunge huyu angeweza kusaidia kuleta maendeleo katika maeneo yake. Kwa mtazamo ninaouona, katika watu wenye hali ngumu hivi sasa ni Waheshimiwa Wabunge. Waonewe huruma! Waangaliwe kwa jicho ambalo litaweza kuwafanya Wabunge hawa, hasa wengi wa CCM, warudi katika miaka mitano ijayo. Vinginevyo, wanakwenda na maji kama eneo hili halikufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumza vile vile suala zima la zile shilingi milioni 50. Naomba nishauri kwamba fedha hizi tusiangalie kuzipeleka kwenye SACCOS, ziangaliwe kuboresha mazingira ya vijiji ambavyo vinapelekewa hii fedha, kwa sababu, kuna mahitaji mengi ya msingi; hospitali hazijamalizika, zahanati, shule zimekaa magofu na zilizomalizika hazina vitendea kazi, hazina madawati, hazina vitu mbalimbali; maji hamna na barabara ni mbovu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi fedha ni muhimu sana, lakini ziangalie kujenga maendeleo ya vile vijiji, viwe bora zaidi na watu wanahitaji kuishi maisha bora zaidi kuliko hali ilivyo sasa hivi. Kila mmoja anatamani fedha ile iende katika eneo lake kwa ajili ya kuboresha vijiji vilivyokuwa na hali mbaya katika maeneo husika. Naomba kasma ikatwe kwa ajili ya kuangalia vikundi vya akinamama na hizo SACCOS, lakini zaidi fedha hizi zielekezwe kuangalia miradi ya maendeleo katika kila kijiji ili kuboresha mazingira yaliyokuweko kule na kuwafanya watu wawe na maisha bora zaidi kwa kila Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania bado tuna fursa nyingi ambazo Serikali kama itaweza kusimamia vizuri, tunaweza kutengeneza maeneo mengine ya mapato kuliko vyanzo ambavyo sasa hivi vimeainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Fursa iliyokuweko katika corridor ya Mtwara na hasa kwenye yale maeneo ya uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kujikita zaidi kwenye suala zima la kilimo. Bajeti haikumtazama mkulima, haikutazama kilimo kwa ujumla wake. Mimi kilichonisikitisha zaidi, bajeti ya mwaka uliopita pembejeo zilitengewa karibu zaidi ya shilingi bilioni 50, lakini mwaka huu ambao tunajiandaa kuwa Tanzania ya viwanda pembejeo haikuzidi shilingi bilioni 20. Sasa tunaposema kwamba tuna lengo la kuongeza uzalishaji au kupata mazao kwa ajili ya viwanda, mazao haya yatapatikana vipi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia tathmini ya pembejeo zilizotoka miaka iliyopita siyo zaidi ya asilimia 10 kwa wale wasambazaji wa pembejeo, wakulima walikuwa wanapata pembejeo hizo katika maeneo yao. Hali hii mwaka huu tunaitazama kwa jicho gani? Obvious, uzalishaji utashuka. Hakuna njia ya mkato, uzalishaji utashuka kwa sababu hakuna pembejeo ambazo zitatosha kwa ajili ya kuwafanya wakulima hao waweze kuzalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili litaathiri maeneo mengi, litaathiri kwanza wazalishaji wenyewe, litaathiri zile Taasisi na Mamlaka tulizoweka kwa ajili ya kununua mazao katika maeneo yao mbalimbali na hasa kwa zile taasisi ambazo tumeziweka zinunue chakula kwa ajili ya chakula cha akiba na kile cha ruzuku, hakutakuwa na chakula cha kutosha kwa hali inavyokwenda. Vilevile athari nyingine iliyojitokeza hapa ni kufungua milango kwa private sector au waleta pembejeo binafsi kuweza kuleta hizi pembejeo na kuziuza kwa bei ya juu sana kwa sababu ndiyo mahali pekee panapopatikana hizi pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, niliona kwenye ripoti au taarifa ya Kamati ya Bajeti na tulilipeleka kama Wajumbe wa Kamati ya Kilimo suala hili liongezewe fedha na lipewe msukumo maalum ili kuwafanya wananchi wa nchi hii waweze kuzalisha kwa uhakika na ile surplus itakayopatikana iweze kupelekwa kwenye hivyo viwanda ambavyo tunataka tuvianzishe. Wasiwasi wangu, mpango mzima wa kuanzisha viwanda katika maeneo haya hasa kwa kutumia raw materials za kilimo utaweza kuathirika na vinginevyo usiweze kufanyika kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuzungumza kwenye suala zima la kilimo cha umwagiliaji maji. Bado Serikali hapa haijawa na kipaumbele. Tanzania hii ya leo iliyokuwa imeathirika na mazingira na hali ya hewa katika maeneo mbalimbali vyazo vingi vya maji vimepotea, hata yale unayochimba sasa hivi unayochimba katika urefu mkubwa sana kwenda chini, water table imeshuka. Njia pekee ya kulima ni kutumia umwagiliaji. Scheme zetu zilizokuweko nyingi zimechoka zimetengenezwa zamani na zile zinazotengenezwa sasa hivi speed ya utengenezaji wa hizo scheme mpaka kuwafanya wakulima waweze kulima kwa kutegemea maji ni ndogo, lakini fedha vilevile zilizotengwa kwa ajili ya masuala mazima ya umwagiliaji maji ni kidogo sana. Sasa nina wasiwasi nia ya kweli ya dhati ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wakulima hawa wana uhakika wa kulima iko wapi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Waziri wa Fedha aangalie sana, tuwe na mpango maalum wa kuhakikisha kwamba tunaongeza maeneo ya umwagiliaji angalau asilimia kumi kila mwaka ili tuwe na uhakika wa uzalishaji wa mazao mbalimbali na kuweza kuwafanya wakulima wetu wawe na uhakika wa uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine katika hilo ni suala zima la utafiti. Nchi yoyote katika eneo ambalo linatakiwa liwe na kipaumbele utafiti ni eneo mojawapo kwa sababu ndipo mahali ambapo unapata hizo facts. Nina-declare interest kwamba na mimi niluwa mtafiti kwa zaidi ya miaka nane, ninajua machungu, adha na taabu za utafiti kama hakuna fedha zinazotikawa. Leo hakuna msukumo wa fedha ambazo zinakwenda kwa watafiti moja kwa moja wakati watafiti wale tayari wameshaanza kazi kubwa ya miaka mitatu, miaka minne kutafiti aina mbalimbali, aidha, mbegu, au maradhi mbalimbali au dawa au ufumbuzi wa tatizo ambalo limekabili katika eneo fulani. Leo hii kama hakuna fedha ambazo zinapelekwa katika maeneo haya ya utafiti kwa kweli tunaanzisha kitu ambacho kitawavunja moyo watafiti na hatutakuwa na maendeleo thabiti kwa sababu hatutakuwa na uhakika wa kile ambacho tunakifanya, tutakuwa tunakwenda kwa kubahatisha. Niombe sana kuwepo na msukumo maalum katika eneo hili la utafiti na zipelekwe fedha ili hawa watafiti wengine wamalize research zao na wengine waweze kuanzisha zile research ambazo zitaleta manufaa na mwelekeo mpya wa Tanzania hii ya viwanda tunayokwenda nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti uko katika kila eneo, hata hivyo viwanda ambavyo tunataka kuvifanyia kazi au kuvianzisha lazima kuwe na tafiti za kutosha kuona kwamba zinaweza zikafanya kazi vipi. Kuna material au kuna malighafi za kutosha za aina gani na ubora wa hizo malighafi ambazo zitatumika katika hivyo viwanda tulivyokuwa navyo. Niombe sana tuziangalie taasisi zetu za elimu ya juu, lakini tuangalie Taasisi za Utafiti ili ziwe na kazi na kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini. (Makofi)
Nizungumzie eneo lingine ambalo nimeona bado mkazo wake siyo mkubwa. Tuna mifugo mingi Tanzania, lakini bado eneo hili halijawa productive kwa nchi yaani zile revenue hazijaonesha kwamba kweli inaisaidia hii nchi kupunguza umaskini na kuwaongezea kipato, siyo kwa wananchi wenyewe lakini siyo kwa Serikali vilevile. Eneo hili linahitaji tafiti, lakini inahitaji kutiliwa mkazo ili tuweze kuwa na mifugo iliyo bora na kuwa na ufugaji wa kisasa zaidi. Bado mifugo yetu tunaendelea kuendeleza ufugaji ule tunauita indigenous ufugaji wa kizamani sana, kiasi kwamba mifugo yetu inakosa bei lakini inakosa vilevile kustahimili mazingira yaliyokuwepo hivi sasa matokeo yake ng’ombe, mbuzi na wanyama wengine wanakufa kwa wingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitishwa na kitu kimoja ambacho Serikali inapoteza pesa nyingi sana. Utafiti tulioufanya kuna ng’ombe wengi wanavushwa kimagendo hasa katika mpaka wa Arusha kwenda Kenya. Wakenya wanatarajia kupokea ng’ombe 2,000 karibu kila wiki kutoka Tanzania, lakini ng’ombe wale wakishachinjwa na kufanyiwa process nyinginezo miguu na zile kwato tunaletewa Tanzania kwa ajili ya viwanda au kwa ajili ya ku-pack na kupeleka katika maeneo ambayo watu wanaweza kuifanyia bidhaa. Sasa tunajiuliza…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuunga hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango ambayo yamewasilishwa leo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Nishukuru Mpango umeeleza mambo mengi na umejikita kwenye mambo mengi makubwa zaidi. Inawezekana yakawa size ya uwezo wetu kama nchi au yakawa zaidi ya uwezo wetu kama nchi kwa sababu projections zilizopo kwenye Mpango huu ni kubwa kiasi fulani.
Mimi nataka kujikita zaidi katika kutoa ushauri ushauri kuhusiana na mwelekeo mzima wa huu Mpango ulivyo na mbele tunakokwenda. Mchango wangu zaidi utajielekeza kwanza kwenye sekta ya kilimo, lakini na uanzishaji wa viwanda kwa bidhaa zinazotokana na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ulitakiwa zaidi uoneshe mwelekeo sahihi kwenye kilimo na hasa kwenye uzalishaji ili tuweze kupata dira na mwelekeo wa kuelekea kwenye viwanda. Tunajua kwamba kutakujakuwa na udadavuaji wa baadhi ya mambo lakini kwa hivi ilivyoelezwa ndani ya huu Mpango iko too brief na hapa ndipo penye roho ya uchumi na maisha ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza katika hili, mpango haujaeleza mkakati mzima wa udhibiti na uendelezaji wa maeneo yale ambayo mazingira yake yameathirika. Miaka kumi iliyopita Tanzania ilikuwa zaidi inategemea mikoa minne kwa upatikanaji wa mvua ya uhakika, lakini sasa hivi hiyo mikoa minne tuliyokuwa tunasema ina mvua ya uhakika imeshapoteza mwelekeo. Tulikuwa tunaiangalia zaidi Kigoma, Kagera, Katavi, Njombe pamoja na Iringa. Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa maeneo haya yamekumbwa na uharibifu wa mazingira na unapoweka mpango kama huu ambao unataka kutengeneza mazingira ya uzalishaji, vitu hivi lazima viwe na mtazamo maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yetu tumeyaharibu, tukiangalia eneo kubwa tulilokuwa tunalitegemea, tunaliita eneo chepe la mabonde ya Usangu mpaka Ruaha leo hii imekuwa ni mbuga ya kufugia ng‟ombe tu. Hata tukienda maeneo yale ya Kagera, Karagwe, Misenyi na Biharamulo nayo vilevile tumeyaachia huru as if nchi yetu haina mpango mkakati wa udhibiti wa uharibifu wa mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo langu, turudi kwenye kuweka mkakati maalum wa udhibiti wa uharibifu wa mazingira katika maeneo hayo ili kurudisha uoto wa asili na hali nzuri ya unyeshaji wa mvua katika maeneo yale. Sambamba na hilo, ule mkakati uliokuwa umeanzishwa Dar es Salaam wa upandaji miti, tunarudia tena, uweze kusambaa nchi nzima kuwe na mkakati kama ule vinginevyo hatma ya nchi hii ndani ya miaka kumi tutakuwa kwenye mtihani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ni lazima nchi iwe na mkakati wa kuhakikisha kwamba kunakuwa na uzalishaji. Kwa kipindi hiki sasa mkakati mkubwa uelekezwe kwenye umwagiliaji maji. Bado mpango haujaonesha kiwaziwazi mkakati wetu wa ujengaji ama mabwawa au miundombinu yoyote ya umwagiliaji maji kwa kutumia rasilimali ya mito na maziwa tuliyonayo hapa nchini. Tanzania tumejaliwa, lakini mpaka tunajiuliza sijui tumerogwa wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tuliokuwa nao sisi wengine tuliopata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi za wenzetu, mwezi uliokwisha kulikuwa na kikao cha wataalam wa kilimo cha SADC pale Angola, Wamisri walikuja kutoa taarifa na uzoefu wao tu, kwa kutumia maji ya Mto Nile, ile Suez Canal, wenyewe wanaita Suez Belt, wana uwezo wa kuzalisha pamba tani milioni tano kwa miaka miwili. Sisi tuna Ziwa Victoria lakini uzalishaji wetu kwa Kanda ya Ziwa ambayo ndiyo maarufu kwa ajili ya uzalishaji wa pamba tunasuasua kwenye tani 300,000, wenzetu wanazungumzia kuongeza kutoka milioni tano kwenda kwenye milioni nane sisi tunaangalia 300,000 tutai-maintain vipi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ili uwe smart uangalie raw material zinazotokana na uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo. Hata hivyo, mwelekeo wetu uwe kwenye irrigation ili na sisi kama wananchi tupate fursa ya kutumia maji na mito ambayo ipo ndani ya maeneo yetu, kitu ambacho bado hakijatendeka vilivyo. Maji tunayo yanaishia baharini kama wengi walivyosema. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tukafanye restructuring kwa baadhi ya mambo tuelekeze nguvu kwenye umwagiliaji maji ndipo tutakapokomboka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ni usalama wa chakula, tuwe na mipango ambayo itatuwezesha kuwa na uhakika wa usalama wa chakula hapa nchini. Kwa kweli bado na mimi nasema ni aibu nchi hii kulalamika njaa wakati fursa za vyanzo vya maji tulivyonavyo ni nyingi sana lakini bado hatujajiweka sawa, mipango yetu haijajielekeza kuhakikisha kwamba watu hawa wanalima kwa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano mmoja, kama tutaweza kujenga mabwawa yakawa yanatumika kwa kilimo na mifugo, tukaweza kuendeleza hekta 50 tu kila Mkoa kwa yale maeneo yenye uwezekano wa kutengeneza yale mabwawa tuna uhakika wa reserve ya tani 500,000 kila mkoa kwa kila mwaka. Hii ni akiba nzuri lakini hiki ni chanzo cha raw material ya viwanda ambavyo tunategemea tuvianzishe na maeneo mengine yatumike kwa ajili ya chakula na mambo mengine. Tuwe na mkakati na muono wa mbele wa kuona kwamba nchi inakuwa na uhakika wa ile reserve iliyokuwa tunaisema tu lakini kuweka reserve ya chakula kwa kutegemea mvua ambazo hazina uhakika bado hatujaenda vizuri na hatujawa stable. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tuzingatie kuyafanyia marekebisho baadhi ya mambo, mtuite tuwape mawazo ambayo yataweza kutujenga. Kinachotia uchungu ni kwamba tunatumika katika nchi za wenzetu kutoa mawazo ambayo wao wanayafanyia kazi na wanaweza kupiga hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea mwezi uliokwisha, wenzetu wa Malawi baada ya kupata tatizo kubwa la ukame mtazamo wao sasa hivi ni huo. Haya maelezo ambayo mmeyatoa hapa katika page number 16 ya mpango tuliokuwa nayo ni mkakati ambao EU kwenye agricultural sector ndiyo waliokuwa nao, AU ndiyo waliokuwa nao na SADC wame-copy and paste huohuo.
Kwa hiyo na sisi tusiwe tunauweka kimaandishi, tuuweke kivitendo uwe practical na siyo tunachukua mipango kama hii na maelekezo ambayo wenzetu wameyaweka sisi kwetu baadaye yanaishia kwenye shelf. Nimuombe sana, tusipozingatia na tukaelekeza nguvu zetu kwenye kilimo tumewamaliza Watanzania na tutakuwa na ndoto tu ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mpango bado haujatuambia kwenye uvuvi tunafanya nini. Tumepata maelezo na baadhi ya watu wameeleza lakini katika eneo kubwa ambalo tutaweza kuajiri watu wengi kabisa ni sekta ya uvuvi. Tukijipanga vizuri katika eneo hili, wenzetu wametoa mawazo pale kwamba tutafute angalau meli moja tu ya uvuvi ina uwezo wa kutuanzishia viwanda viwili lakini ina uwezo wa kutoa ajira kwa watu mpaka 3,000. Kwa sababu kazi zilizopo kupitia sekta ya uvuvi ni nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tutengeneze mazingira ya pale bandarini kuwepo na port dock ambayo itawalazimisha wale wanaovua katika maeneo mengine yote ile kuchakata wale samaki na process nyingine zifanyike katika maeneo yetu, tutatengeneza pesa ya kutosha. Taarifa zilizopo sasa hivi duniani, Tanzania baada ya kuzuia leseni za uvuvi katika uvuvi wa bahari kuu, demand ya samaki katika soko la dunia imepanda mpaka tani 230,000, soko lipo wazi, nafasi hii ndiyo pekee ya kuitumia. Nimuombe Waziri wetu wa Kilimo azuie kutoa vibali vya uvuvi wa bahari kuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaofuatilia haya mambo na tunayajua, ukiikodi meli moja ya uvuvi Philippines au Thailand wanakodi kati ya dola milioni tano mpaka milioni saba, catchment yake kwa wiki tatu mpaka miezi miwili ina thamani ya dola milioni 40.
Kwa hiyo, kwa wale wanaokodi, kwa wenzetu wanafanya deal kwamba akikodi meli mara moja harudi tena baharini kapata utajiri wa maisha anafanya mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utafiti unavyoonesha samaki wale wengi wanawatoa katika maeneo yetu na wakija katika maeneo yetu haya hawavui jodari tu peke yake, wanavua kamba, pweza, ngisi na samaki mbalimbali na baadaye wanakwenda kufanya uchambuzi katika maeneo yao sisi tunabaki kama tulivyo. Ile ni bahati, ni riziki Mungu katupa tujipange vizuri tuitumie vizuri ilete manufaa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linajieleza hapo, tutakapoweza kuwa na eneo la kuweza kushusha samaki, tukaweza kuanzisha maeneo ya majenereta ya kuhifadhia vizuri samaki, tutaweza kuongeza ajira kubwa kwa sababu wenzetu Ulaya wanachotaka ni minofu. Hivi sasa biashara kubwa iliyojitokeza maeneo ya Kongo ambao wanakuja kuchukua dagaa kwa wingi sana Zanzibar, Mwanza na Kigoma wanakwenda kutengeneza raw material ambayo wanapeleka Ulaya kama ni fish meal, demand yake sasa hivi ndani ya soko la dunia kubwa. Sisi tukiwa na meli hiyo pale zile by products zilizotokana na kutoa zile nyama za samaki tunatengeneza fish meal kwa kiwango kikubwa sana ambapo soko ndani ya eneo la soko la dunia ni kubwa sana. Fursa nyingine ni hizo, pale hutupi kitu, hata ule mwiba wa katikati wa samaki bado ni bidhaa adimu kabisa kwa sababu ile calcium iliyomo mle ni bora zaidi na inahitajika katika maeneo mengi sana kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali na dawa.
Kwa hiyo, mimi wito wangu na wazo langu ni kuiambia Serikali hili eneo la uvuvi lina fursa kubwa sana, kuliko kuwaita Wachina kuja kuweka soko pale la bidhaa zao mbalimbali, hapa pana pesa za waziwazi, tujikite jamani katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninalotaka kuzungumza ni kwenye mazao ya biashara bado kama nchi tunaendekeza ukiritimba fulani hivi ambao hauleti maana. Leo hii kutengeneza rustan coffee mpaka twende Moshi, Arusha? Gharama za kuchukua kahawa iliyoko Mbinga ambapo kule tunafanya process ya mwanzo tu ya catchment uisafirishe uipeleke Moshi ni kubwa. Wakati mwingine unachukua kahawa kutoka Manyovu au Kigoma iende Moshi, very unfair! Tutengeneze viwanda ambavyo tutaweza kutengeneza kahawa ambayo itaweza kwenda kuuzwa katika soko la nje moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kahawa yetu ni ya nne duniani, bado tuna nafasi kubwa. Kwa ubora hatujawapita Ethiopia, Rwanda lakini tumewapita Uganda, Burundi na Kenya. Kahawa yetu ni bora kuliko ya Brazil, bado tuna nafasi katika soko la dunia. Hata hivyo, utaratibu wa makampuni yanayoshughulika na zao la kahawa ni wa kujitengenezea faida wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kesi hiyohiyo ipo kwenye tumbaku. Tumbaku kilichotokea pale ni ukiritimba tu wa yale makampuni ya kujifanya wao ndiyo wao wakati bado kuna fursa kubwa ya ile tumbaku katika soko la dunia. Mnunuzi mkubwa wa tumbaku ni China. Sasa hivi China baada ya kuona bureaucracy ya Afrika anatenga hekta karibu milioni mbili azalishe tumbaku nchini mwake, lakini mbegu ya tumbaku kutoka China sisi tunayo hapa. Sasa lile tishio la yale makampuni la kusema kwamba sisi hatununui wanasema wanatisha bwege ni ili sisi tuweze kujiachia hawanunui tupunguze uzalishaji ili wao …
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii kwa uchache nizungumze yale ambayo nilikuwa nimepanga niweze kutoa kama ushauri kwa Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mbali saa nyingine kwa baadhi ya maelezo ambayo wenzangu wameyatoa, moja hasa likugusa kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu. Ni lazima tukubali ukweli kwamba tumepitisha bajeti ambayo siyo practicable, haifanyi kazi ile bajeti ni ndogo na hasa tukizingatia kwamba kwa kiwango kikubwa tumepunguza pembejeo kutoka kuwahudumia wakulima 999 mpaka kuwahudumia wakulima 300, hapa hatujawatendea haki wakulima wa nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zimeelekezwa katika maeneo mengine lakini pembejeo zimeshuka sana, sasa tuna ukame ambao umekabili nchi yetu, tulichokuwa tunatakiwa ni kuongeza nguvu kwa yale maeneo ambayo yamepata mvua ili wananchi wale waweze kuzalisha kwa wingi kuweza kufidia maeneo ambayo yalikuwa yamekosa mvua kwa kipindi hiki, ingeweza kuiweka nchi yetu kuwa salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii ya ukosefu wa mvua bado katika Ukanda wetu wote wa SADC unazikabili nchi zote hizi na ukosefu wa mvua.
Kwa hiyo, ukame utaendelea na ukosefu wa chakula utaendelea. Nchi pekee wanayoitegemea ni Tanzania, Tanzania yenyewe uzalishaji wake umekuwa wa kusuasua, tunakimbilia wapi, hapo ndipo pa kujiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba bajeti ijayo tukubaliane Waheshimiwa Wabunge tuhakikishe kuna maeneo lazima yawe ya kipaumbele na tuhakikishe Serikali inasikiliza kilio chetu. Tulipendekeza kwa nguvu zote kwamba bajeti ya pembejeo ipande tukapendekeza fedha wapewe NFRA waweze kununua chakula kwa msimu uliokuwepo, NFRA hawanunui chakula wanangoja bajeti ya Serikali, chakula wananunua walanguzi na watu wengine wakianza kununua wao bei zimeshapanda.
Kwa hiyo, tuwatake NFRA wanunue chakula mwezi wa tano kwa yale maeneo yenye uzalishaji ili kuwepo na chakula cha akiba kujihami kwa hali ambayo inaweza kujitokeza huko mbele tunapokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nataka kusisitiza ni kwamba nchi hii hakuna kitu ambacho kimeonesha mwelekeo mzuri kama Mfuko wa Maji na tozo ya shilingi 50, tuliishauri Serikali msimu uliopita kwenye bajeti ipandishwe iwe shilingi 100, leo hii miradi yote iliyofanyika inaonekana katika Majimbo yetu ni kwa shilingi 50 ambayo imeweza kutengeneza zaidi ya bilioni 75 ambazo zimekwenda katika maeneo yetu mbalimbali. Kwa hiyo, nitoe wito wa Waheshimiwa Wabunge, bajeti ijayo tuiombe Serikali hiki kilio itusikie, ipandishe hadi shilingi 100 ambapo tutakuwa na uhakika kwa mwaka zaidi ya shilingi bilioni 300 na miradi yote ya maji itaweza kufanya kazi au itaweza kumalizika kwa wakati pasi na kutegemea tu pesa kutoka Serikalini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba fedha zaidi ziangaliwe maeneo ya utafiti, Tanzania tuna matatizo ya kupata mbegu ambazo zinatumika katika maeneo yetu, asilimia 70 sasa hivi ya mbegu tunaagiza nchi za nje. Tatizo kubwa ni zile tozo za wale watafiti au wale wazalishaji mbegu wa hapa nchini, lakini ukizalisha mbegu nchi za nje au nje ya Tanzania unakuwa na duty free. Hivyo, makampuni ya uzalishaji mbegu yamekimbilia Zambia, Malawi, Zimbabwe, yanazalisha halafu yanaleta Tanzania kwa sababu kuingiza Tanzania ni bure. Kwa hiyo, kitendo hiki kinawavunja moyo watafiti, kinavunja moyo makampuni ya uzalishaji mbegu, hivyo basi kila mmoja anaona bora akazalishe nje au aende akanunue mbegu Belgium na afunge Tanzania halafu auze ndani ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine kinacholeta athari zaidi ni baadhi ya mbegu zinazotoka katika nchi hizo hazifanyiwi uchunguzi, matokeo yake zinaleta athari za maradhi kwa watu mbalimbali na hasa kwenye ugonjwa wa kansa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linaloleta athari hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Rehani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nakushukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa taarifa yake na hotuba yake ya bajeti hii ambapo angalau tunaona mwelekeo kidogo ukisimamiwa mambo yataweza kwenda vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile niwashukuru Mawaziri ambao wamo ndani ya Wizara hii Ofisi ya Waziri Mkuu, swahiba yangu pale dada Mheshimiwa Jenista, lakini vilevile na kaka Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kujielekeza kwenye mambo matatu makubwa ambayo nahisi kama nchi tunaweza tukaleta mabadiliko. La mwanzo niombe ofisi yako na tuiombe Wizara ya Kilimo na Serikali kwa ujumla ili nchi hii kuinusuru na janga kubwa la njaa ambalo linatokea katika maeneo mbalimbali ambalo hasa linasababishwa na tatizo la hali ya hewa lazima tuwe na kilimo cha umwagiliaji maji, hatuna njia ya mkato. Mataifa yote ya wenzetu wengine mkakati uliokuwepo ni kuwa na kilimo cha umwagiliaji maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Novemba mwaka jana tulishiriki kwenye Agriculture Council ya SADC nchi zote zinazotuzunguka tamko lao limejielekeza kwenye umwagiliaji maji. Napenda kutoa rai tufanyaje katika hili ili tuweze kupata mlango wa kutokea. Niombe Serikali kwa ujumla iridhie kuufufua Mfuko wa Umwagiliaji Maji uwe unachangiwa kama inavyochangiwa mifuko mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfuko huu ni muhimu na ndiyo dawa ya kuweza kukomboka na kuwa na miundombinu ya umwagiliaji maji. Hesabu ya haraka haraka kama tutakuwa na wachangiaji wa shilingi 50 tu, tukiwa na wapiga simu au wamiliki wa simu milioni 20 ambao kwa Tanzania tunafika idadi hiyo, pesa ile kwa mitandao mitano iliyokuweko ndani ya nchi tunaweza kuwa na zaidi ya shilingi bilioni 144. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha hizi tunaweza kuwa na maeneo maalum ya kimkakati na mazao ya kimkakati, kila eneo tukaweza kuchimba visima vinane, tukaweza kuwa na zaidi ya hekta 1200, tayari tuna uhakika wa reserve ya tani 300,000 za chakula kwa mwaka. Hivyo, tishio la NFRA na mazao yale mchanganyiko ya kusema tutanunua wapi chakula, wale watanunua kwa hawa ambao wamewekeza kwenye umwagiliaji maji hivyo Taifa litakuwa na uhakika wa akiba ya chakula na tatizo kubwa la njaa litakuwa halipo katika maeneo yetu, hiyo ni rai yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka kumuomba Waziri Mkuu, kazi nzuri aliyoifanya kwenye Bodi ya Korosho ahamishie kazi ile kwenye bodi nyingine za Wizara ya Kilimo. Kuna matatizo na hakuendi vizuri kwenye Bodi ya Pamba, kuna matatizo na hakuendi vizuri kwenye Bodi ya Kahawa, kuna matatizo kwenye Bodi ya Chai, chai kama kaachiwa limekuwa shamba la bibi tu hamna anayemuuliza mtu. Tulikuwa na Bodi ya Pareto, leo hii tumeanzisha vilevile Bodi
ya Maziwa, bodi hizi zinatakiwa zipitiwe, zifuatiliwe, utendaji wao wa kazi ujulikane lakini vilevile yale makato wanayowakata lazima yajulikane yanatumika vipi. Hali ilivyo sasa hivi kama hakuna anayesimamia bodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Waziri Mkuu mkakati zaidi ulioufanya kwenye Bodi ya Korosho ambapo umewakomboa wakulima na wamerudisha imani wakulima wa korosho tuhamishie kwenye bodi nyingine hizi ili kurejesha imani ya wakulima wa kahawa ambao wengi
wao wameacha kulima kahawa kutokana na makato na mazingira mabaya yaliyokuweko kwenye kahawa. Hali kadhalika, tuangalie pamba inakuwaje, chai inakuwaje lakini tusisahau na pareto vilevile. Tulikuwa ba Bodi ya Pareto ambayo sasa hivi hata haizungumzwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa linalotukabili kwenye kilimo ni kutokutilia maanani suala zima la upatikanaji wa pembejeo. Kilimo bila pembejeo hatuna kilimo, ardhi yetu tumeshaitumia imechoka. Serikali kadri tunavyoishauri kuhusiana na pembejeo linaonekana suala lile kwamba ni jepesi na halina uzito wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka juzi nchi ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 250 kwa ajili ya pembejeo, zikapatikana zaidi ya shilingi bilioni 120, mwaka jana tumekwenda na shilingi bilioni 20, hali imekuwa tete. Tumetoka kwenye wakulima waliopewa ruzuku ya pembejeo 99,000 sasa hivi tumekuja kwenye wakulima karibu 350, hali ni ngumu. Niiombe Serikali hili suala iliangalie kwa jicho la maana, bila pembejeo utazalishaje? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito wangu kwamba, Kamati ya Bajeti na Wizara ya Fedha hili jambo iliangalie kwa jicho la huruma. Wakulima hawa wana nia ya kuzalisha, pamoja na ukata na hali ngumu ya hali ya hewa lakini ukosefu wa pembejeo nao vilevile unachangia kudumaza
maendeleo yao. Hili tulitilie maanani na tuweze kuwasaidia wakulima katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kuzungumza ni la mifugo. Nikushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu umeshughulikia vizuri suala zima la mifugo hasa maeneo ya Loliondo. Wafugaji wale wa Loliondo bila Kamati ile wangefikia pabaya, sasa hivi wangekuwa wameshafukuzwa na hawaelewi pa kwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wale wafugaji kule wako zaidi ya 64,000 ukiwaondoa pale wana ng’ombe zaidi ya 500,000 wale wanakwenda maeneo ya Morogoro na wanakwenda maeneo ya Kusini kitu ambacho kinakwenda kuchochea machafuko baina ya wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu, suala hili tuweze kuli-handle vizuri kwa sababu bado Wamasai wale wana uwezo wa kufuga ng’ombe na wakatunza zile rasilimali zilizokuwapo pale za hifadhi bila kuathiri na maisha yakaweza kuendelea baina ya wanyama wa porini na wanyama wa kufugwa. Wito wangu, Kamati iendelee na uchunguzi na mkakati wake, lakini ifike mahali uwekwe utaratibu mzuri wa kufuga pasiwe na wazo la kuwafukuza watu wale. Kwa sababu kuondoka kwao sio kama watachinja wale ng’ombe wao, watahama maeneo na
hivyo tutaongeza tatizo la ugomvi baina ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia Bodi ya Maziwa. Bodi hii ina malengo mazuri, imesema mwaka huu inataka kuimarisha ng’ombe wa maziwa angalau wafike milioni moja na laki tano. Ushauri wangu tuanzishe cowshed au vijiji vya ufugaji ili kuweza kuwapelekea huduma hawa wafugaji ambao watapewa hawa ng’ombe wa maziwa. Tutakapoanzisha cowshed hizi itakuwa rahisi kuweza kuwapelekea elimu ya ugani kwa wale wafugaji ambao
wataanzisha mabanda haya kwa pamoja lakini vilevile tutaweza kuweka zile collection centre. Bado Tanzania inaathirika na maziwa ambayo yanatoka nje, ni aibu jamani! Tanzania hatuna kiwanda cha maziwa ya unga tunashindwa na Zimbabwe walau wana kiwanda cha maziwa ya unga. Tatizo letu ni kwamba maziwa yetu hayana viwango na ng’ombe tulionao hawana uwezo wa kutoa maziwa ya kutosha tukaweza kuanzisha hivyo viwanda tulivyokusudia. Kwa hiyo, kama hatukujipanga kuweza kusambaza ng’ombe wa kutosha katika nchi hii… (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kupata nafasi hii adhimu ili niweze kuchangia katika taarifa hii ya bajeti ya Wizara ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kasi aliyoanza nayo katika Wizara hii na kuonesha nia kweli kuleta mabadiliko yaliyoachwa na mtangulia wake kwa Wizara hii ya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo nataka nitoe shukrani ya dhati kabisa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha Zanzibar kuweza kupata nafasi ya kuwa mwanachama wa CUF au Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CUF), nafasi ambayo ilikuwa imetafutwa kwa miaka mingi na kilio kikubwa kwa Wazanzibari kuweza kupata nafasi hiyo, nao kushiriki kama nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupata nafasi hiyo, bado naomba Wizara hii kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania TFF na kile cha Zanzibar ZFA kuendelea na jitihada hizo katika kutafuta nafasi ya FIFA ili nayo iwe mwanachama kama ilivyo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilichokuwa nakiomba, ushirikiano uliokuwepo baina ya ZFA, TFF na Wizara zetu mbili hizi za Michezo za Tanzania Bara na ile ya Zanzibar uweze kuendelezwa katika mtazamo wa kuisaidia Zanzibar au ZFA ili nayo timu zake zinazoshiriki katika mashindano hayo ya Afrika ziweze kuwa na nguvu, kwani kwa hivi sasa timu nyingi zilizokuweko kule Zanzibar, kwa mfano, ndani ya Jimbo langu nina zaidi ya timu 60, lakini nina wachezaji ambao tumechukua Tanzania Bara wanaweza kufika hata 300. Kwa hiyo hii fursa ya ushirikiano huu iliyokuwa imepatikana isikatikatishwe kwa vile Zanzibar sasa hivi imepata kuwa mwanachama wa CUF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ninachotaka nikione kwamba kinaendelezwa ni suala zima la michezo hasa kwa vijana wadogo. Tuna mashindano ya Coca Cola na kuna mashindano mengine mbalimbali ya NSSF ambayo yanashirikisha timu kutoka Zanzibar na hizi Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli timu hizi au mashindano haya yanaleta chachu ya ushindani na kuibua vipaji vingi vya wachezaji mbalimbali kuonekana wale wa Zanzibar wanapata nafasi ya kuja kucheza timu za Tanzania Bara, lakini na wale wa Bara wanapata nafasi ya kuja kucheza kule Zanzibar. Naomba fursa hii iweze kusimamiwa na Wizara na kuwe na mashindano ya ushindani kweli ambayo yataweza kuwanufaisha pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumza ni programu zima ya kuendeleza vijana wetu. Zanzibar miaka ijayo tunategemea nasi kuanza maandalizi ya vijana kwa ajili ya AFCON kama ilivyo Serengeti Boys, mkakati ambao unatakiwa uungwe mkono pande zote mbili na kuwe na programu za kushirikiana ambazo zitaziwezesha kuwa na timu ambayo itaweza kufanya vizuri na kupata nafasi kama ilivyopata nafasi Serengeti Boys.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi hizi zinataka ziungwe mkono na wanachama wote, Wabunge, wadau mbalimbali wa ndani na nje ili leo hii tuione kwamba Serengeti Boys inavuka hapa tulipo na inatimiza lengo ambalo ilikuwa imetuahidi na iliyomwahidi Makamu wa Rais kwamba safari hii italeta kombe la Afrika la Vijana Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri akae na mwenzie, Mheshimiwa Waziri yule wa Zanzibar waangalie mkakati ukoje, kwa miaka mingine mitatu ijayo timu zetu hizi tutaweza kuziinua na kutengeneza timu ambazo zitaweza kuonesha ushindani na kupandisha kiwango cha mpira hapa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa tarehe mosi kulikuwa na maadhimisho ya siku ya habari ambayo yalifanyika kule Mwanza. Waziri alitoa kauli kali kidogo, nami kama mdau wa habari vilevile niliguswa na ile kauli. Sasa sijui iko vipi? Kauli ambayo ilipiga marufuku uchambuzi wa magazeti katika vyombo vyetu vya habari. Sasa tunauliza; Mheshimiwa Waziri, siyo Watanzania wote ambao wanaweza kuwa na uwezo wa kununua gazeti, lakini siyo Mtanzania yeyote anaweza kufikishiwa magazeti haya. Leo tutakapopiga marufuku uchambuzi ule wa habari, wengi wao tumewanyima haki ya kupata habari Watanzania. Kwa sababu Magazeti yale au uchambuzi ule wengi wetu tulikuwa tunasikiliza kupitia redio, kwa hiyo, hata vile wengine kununua…

T A A R I F A...

MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimeipokea hiyo taarifa. Naomba kuisherehesha. Fursa hii ya uchambuzi wa magazeti ndiyo sauti ya Watanzania wengi, inaweza kuwaambia kwamba ndani ya dunia hii au ndani ya Tanzania hii kuna taarifa hizi, hizi na hizi kwa leo; na kesho kuna taarifa hizi na hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kulitathimini agizo lake hili, kwa kweli linawakosesha fursa kubwa Watanzania kupata habari ambazo zinapita katika vyombo vyetu vya habari hivi hasa asubuhi kwa uchambuzi wa magazeti mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwenzetu alivyosema, kundi hilo la wasioona na kuna makundi mengine mengi tu ambao uwezo wa kununua gazeti hawana, lakini wanazihitaji taarifa. Hili lipitiwe tena upya na Mheshimiwa Waziri atoe kauli ili kuweza kuwapa fursa Watanzania kupata habari kama walivyokuwa wanapata habari hivi sasa. Nitamsikiliza kwenye majibu yake ili tuone kitu gani ambacho ataweza kutuambia Watanzania katika hili eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kuzungumza suala zima la Wasanii. Tanzania hii wanapozungumzwa Wasanii wanadhaniwa kwamba ni Wanamuziki na wale watu wa Filamu; lakini kuna kundi kubwa la wafinyanzi, wachongaji, waandishi wa vitabu mbalimbali, sijaona jicho la Mheshimiwa Waziri au Wizara yake kuweza kuangalia kundi hili na vipi wanavyoweza kuwasaidia kuinua vipaji vyao, lakini watu hawa wanaitangaza Tanzania katika Sanaa hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Kisiwa cha Brunei ni mteja mkubwa wa bidhaa za vinyago ambazo zinachongwa Tanzania. Taarifa nilizonazo, kwa miaka mitano iliyopita wamenunua bidhaa hizi zaidi ya Dola milioni 600, zinanunuliwa katika maeneo mbalimbali na yeye kule wameweka ma-shop mall ya vinyago hivi ambavyo vinachongwa katika maeneo yetu mbalimbali.

Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, eneo hili nalo jicho lake liweze kuelekea. Wakurugenzi au Wizara iwe na mpango maalum wa kuwatambua kwanza, lakini siyo kuwatambua tu kama ilivyokuwa wanatambuliwa wanamuziki ambao mpaka leo hawana walichokipa kutokana na mirahaba inayopatikana waweze kupewa support na Serikali na zile bidhaa zao zitangaze utalii wa nchi yetu na sanaa iliyokuwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba BASATA, bado haijafanya kazi ya kuwasaidia wanamuziki na wacheza filamu wa Tanzania.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilikuwa na mambo mawili matatu lakini nitachangia japo moja atleast nami niweze kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ulikuwa kwenye suala zima la Madaktari, katika hiki kifungu cha 219 cha Veterinary Act Cap No. 319 Ibara 59 ambayo inatoa usajili wa Madaktari kwa mtu ambaye aliweza ku-attend course pengine au mafunzo ya mwaka mmoja. Neno Udaktari ni professional, sasa mtu ambaye ame-attend course ya mwaka mmoja leo tunampa usajili wa cheti cha Daktari it is not realistic. Tuwe realistic!
Mheshimiwa Naibu Spika, huu Udaktari wa Mifugo uliokusudiwa hapa, una nyanja nyingi. Mtu huyu inawezekana amekwenda kule ameshiriki course inayoitwa An Animal Production; leo unampa cheti cha Udaktari, ataua mifugo! Kesho mwingine anashiriki course ambayo inaitwa Animal Breeding, siyo Daktari. Angalau yule mtu ambaye ameshiriki Animal Health au Veterinary. Ukizungumza veterinary ni wale waliopata course ya miaka mitano ya Udaktari.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii nafikiri iangaliwe kwa jicho lingine, hawa watu bado hawajawa na capacity ya kula Daktari.huyu ni livestock attendance, ambaye yeye anaweza kwenda kule akatoa ushauri wa mifugo kwenye kada hii ya matibabu, lakini hawezi kuwa anatibu wala kupewa hii certificate au cheti ya kwamba yeye anaweza kutibu mifugo. Kwa sababu hapa unamwingiza kwenye kada ambayo anaweza kufanya mambo mengine makubwa zaidi. Anaweza kukuta kesi ya kutakiwa kuzalisha ng‟ombe katika maeneo mbalimbali au mbuzi; amekwama mtoto wa ng‟ombe au mbuzi, anaweza ku-attend course kama hiyo na kama ana cheti, basi hata kama akiua yule kiumbe pale, atajitetea kwamba yeye ana cheti cha kufanya vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hili tuliangalie kwa jicho la ukubwa zaidi. Professional izingatiwe zaidi katika kipengele hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka kueleza kuhusiana na suala zima la adhabu hizi za viboko kwa hawa wanafunzi. Adhabu ya viboko bado naona kama ni nyepesi, haitoshi. Kwa wengine waliozoea, ni suala tu la kumlea. Kuna watu hata viboko haviwaingii ndani ya mwili wao; anaweza akapigwa hata kama ni viboko 30, akiingia, 30 akitoka, kesho yake unamkuta mtaani na anafanya jambo lile lile. Bado itafutwe adhabu ambayo itaweza kuwasaidia hapa, apate funzo huyu ambaye amepewa adhabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sawa ni watoto, tunasema kwamba tunachukua tahadhari kwa utoto wao, lakini kwa age zetu na mazingira yetu hapa, kijana wa miaka 18 anaweza akafanya uhalifu wa kuua, anaweza kufanya uhalifu mwingine wowote ule au akashirikiana na wahalifu kufanya jambo ambalo linakuwa kubwa zaidi.
Kwa hiyo, adhabu ya kiboko bado haijawa ni adhabu ambayo inaweza kumfanya yule mtoto aweze kujifunza kwa kosa alilolifanya au wengine kuweza kuwafanya waweze kujifunza kwa kosa walilolifanya. Hapa panataka pakaziwe, kidogo, kuwepo na adhabu ambayo kweli itaonekana hii amejifunza na imeonekana kwamba ni adabu kwa wengine waweze kujifunza kwa kosa ambalo anaweza kulifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliangalie kwa undani zaidi, tusichukulie kwamba labda huyu ni mtoto pengine labda ni miaka 12, 13 basi ukimtia bakora anaweza kujifunza, lakini wengine hawa bado unaweza kumpa njia akaweza kuendelea kufanya mengine zaidi. Hata hivyo, kwa wale ambao wanaweza kuweza kufungwa jela nao vile vile bado mimi nilikuwa na wazo lile kwamba kuna maeneo yale yalikuwepo kipindi cha nyuma, yanaitwa maeneo ya kuwafunza vijana, maalum kwa ajili ya vijana watukutu kama hawa, yangeweza kuimarisha maeneo hayo na ikawa adhabu mbadala kuliko kusema kwamba unampiga viboko, baadaye anaendelea kuweko mtaani, bado hajaweza kujifunza.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE: SALUM M. REHANI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana na mimi niipongeze Serikali kwa kuleta muswada huu ambao kusema ukweli umechelewa kwa sababu ni muda mrefu nchi ilikuwa inakwenda katika muelekeo ambao kwa kweli hakuna mdhibiti, yaani hakuna eneo lile ambalo lina mwenyewe hasa katika eneo hili la maabara. Naomba nizungumzie katika baadhi ya maeneo ambayo nahisi yanaleta ukakasi, yanaji-contradict.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na mwenzangu aliyemaliza tunapozungumzia jina kamili la hii maabara yenyewe, ni Government Chemical Laboratory Authority. Tukitia authority hapa tunakusanya na maabara nyingine zilizokuwa nje ya hii ya chemistry kwa sababu moja. Kemikali zinazotumika ndani ya nchi ziko za aina nyingi, na kila maabara inatumia kemikali. Sheria hii inahusiana na maabara za kikemikali tu peke yake, lakini tukija kwenye laboratory za mifugo tunatumia kemikali za aina nyingi na humu hazijaguswa wala hazijazungumzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye maabara za kilimo, zinatumia kemikali za aina tofauti. Ni-declare interest sisi watafiti kazi zetu hazimaliziki shambani, zinakwenda kwenye maabara. Utakapokwenda kwenye maabara unatumia aina mbalimbali za kemikali. Sasa sijui sheria hii inaweza ikasema nini ili kuwadhibiti wale wote wanaotumia kemikali ndani ya nchi kuwa katika mfumo unaoeleweka. Kinachohitajika hapa ni consistence ya matumizi ya kemikali ambazo zinakuja ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nililoliona ni suala zima la uingizaji wa kemikali na watumiaji hapa nchini. Tuna maabara binafsi nyingi. Zipo zinazofanya shughuli ambazo nyingine hata huelewi, ili mradi tu mtu anasema kwamba mkono unaenda kinywani. Sasa hapa kwenye sheria hii sijaona pahala ambapo tunaweza kuwakamata hawa ambao kwanza waagizaji, wanaagiza bidhaa au kemikali hizi kwa sheria ipi na nani atakuwa anawasimamia. Je, ni huyu Chief Government Chemical Laboratory au kuna mamlaka nyingine ambayo itaweza kuwakamata hawa? Naomba Mheshimiwa Waziri pale tupate clarification hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile mwongozo wa matumizi ya hizi kemikali kwa watu mbalimbali, kwa matumizi mbalimbali bado kumeonekana kuna uhuru mkubwa ambao hauna udhibiti wa matumzi ya hizi kemikali; na ndiyo maana hapo nyuma kukajitokeza wimbi kubwa la watu kutengeneza mabomu, kutengeneza vitu mbalimbali vya kemikali na acid nyingine zikawa zinatumika bila ya kuwa na mdhibiti maalum. Sasa kama sheria hii inakwenda kujibu hoja hii niliyokuwa nimeitoa hapa naomba ijielekeze au kuwepo na vipengele ambavyo vitaweza kueleza straight, kwamba hawa wanatakiwa ili kuweza kufanya matumizi yao wapite njia hii na kibali chao kitapatikana katika ofisi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nilitaka kuzungumzia suala zima la research on toxicity and food toxic. Hapa napo pana shida kwa sababu kuna sheria tofauti na mamlaka tofauti zinafanyakazi katika eneo hili. Mamlaka ya udhibiti wa chakula, TBS wote wanafanyakazi katika eneo hili. Lakini hapo hapo tunapokwenda kuangalia insurance of quality and service nao vilevile sheria inaji-contradict, kwa sababu kuna mamlaka chungu nzima ambazo zinafanyakazi katika eneo hilo. Sheria hii inabidi iwe specific au iwe na mamlaka ya kugusa hawa wote na wawekwe katika kapu moja na tuwe tunazungumza sauti moja kama Serikali ili kuweza kuonekana kwamba msimamo wa Serikali kwa wote ambao wanakuwa wananasibishwa na matumizi ya kemikali basi wanaeleweka na kunakuwa na mfumo unaotambulika.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nililotaka kuzungumzia ni kwenye suala la directory, zone unit and section; hapa panahitaji clarification. Kwa sababu tunaposema kwamba tuna-establish set number of directory zone, unit, section with pre-describe function as the board determine, bado hapajakaa sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtazamo uliokuweko kwamba, je, hizi zone, unit zitakuwa kwa kanda zetu kimikoa au kulingana na institutional entity ya pahala fulani? Inabidi tuweze kujua kwa undani zaidi zone hizi na unit hizi ni za aina gani na set yake inakuwaje, tupate clarification na function zake zitaweza kufanyakazi vipi na wata-flow kwa nani? Kwenye act hii au watakuwa na watu wengine? Kwa sababu hao watu wanaosimamia vitu hivyo kwa hivi sasa kila mmoja ana-play, wanasema kwa yule ambaye anaweza kumpa tonge, yule anayeweza kukufadhili ndiyo mtu anaweza ku-play katika maeneo hayo. Tumezikuta baadhi ya laboratory zinafanya shughuli tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine tunaloweza kulisema hapa, kuna kundi moja kati ya hizi directory units kuna watu wa pathology wanahitajika wawemo katika eneo hili na wanafanya shughuli hizi, ambao ni biologist hao, hawamo na hawakuonyeshwa, lakini wanatumia kemikali, wanafanya shughuli za maabara ambazo zinafanana na maeneo haya, lakini hakuna mwongozo ambao unaosema kwamba hawa wako wapi. Tuwaweke kwamba hawa ma-pathologist wako kwenye health tu pake yake au wako wenye agriculture au mifugo peke yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano; kuna maeneo ambayo linatokezea tatizo ambalo linawakutanisha hawa watu wote. Kuna kichaa cha mbwa katika maeneo yetu mbalimbali ya nchi yetu hii. Kichaa cha mbwa kinapotokea nani mwenye ku-play ile role? Je, maabara za mifugo au ni Maabara hii ya Mkemia Mkuu ndiyo inayoweza ku-sound na kusema kwamba mwongozo uliokuweko sasa hivi utumike labda drugs aina hii au uthibiti uweko hivi? Kwahiyo tunahitaji tupate clarification katika hayo maeneo, na hao watu ambao tunahisi kwamba wako nje ya hii taasisi waweze kuingizwa na tuweze kuwajua wanafanyaje.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalotaka nilizungumze ni suala zima la uchunguzi. Kwanza nilitaka kuzungumza kwenye suala zima la Bodi. Bodi imeelezwa hapa vizuri kwenye hii Part Three, Administration and Institutional Arrangement, lakini haya mamlaka ya huyu Mtendaji Mkuu ambaye ndiye Katibu wa Bodi. Nahisi upande mmoja yako makubwa zaidi kuliko uwezo wake, lakini upande mwingine namhisi kwamba hana mamlaka ya kuingilia baadhi ya maeneo. Kwa mfano, dhana yangu mimi ningefikiri, Bodi hii ingekutanisha na wale ma-director ambao wanatumia laboratory nyingine; kwa mfano wale wanaotumia maabara za mifugo, wale wa pale Mikocheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna maabara nyinginezo kama za Muhimbili. Maabara nyingine zilizo kubwa ni za SUA; lakini kuna maabara nyingine za chemistry ambazo watu wako nje ya institutions za Serikali, nao ni sehemu ya Bodi ambayo wangeweza kuchangia sana kutoa muelekeo sasa wa laboratory hii ili kuwa na maamuzi ya kikemia zaidi kuliko kuchukua watu ambao wako ndani ya taasisi moja au Wizara tu peke yake ukatengeneza bodi na wengine ukawaacha; kwa hiyo, wale wengine wanakuwa hawana role ya ku-play. Tukifanya hivyo angalau tutaweza kuwakutanisha na wao wataweza kupangiwa majukumu yao kulingana na mwongozo wa act hii. Sasa suala la uchunguzi linatakiwa kuweko na ile wanaita advisory committee, hii iwe ina-prove kwa zile kesi zilizo kubwa zinazojitokeza, zinazofanyiwa uchunguzi na si ni kazi ya huyu chief peke yake kuweza yeye ku-authorise kila kitu. Ushauri wangu ulikuwa hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna pahala ambapo nimehisi kwenye hii function and power of the board; kuna eneo naona kwamba linaji-contradict linahitaji kuwa na clarification; ya mwanzo, kwenye ile namba 8(b); “ approval registration, suspension or councilation of Industry chemical, consumer chemical or chemical dealers.”
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa panahitaji paongezwe na non-industrial chemical kwa sabaabu hawa kwa muktadha huu wametolewa na wanahitaji wawepo, na ndio hao wanaotengeneza aina mbalimbali za kemikali katika maeneo yao; kama alivyokwishakuwataja hapa ndugu yangu Waitara wengine wanatengeneza mpaka gongo zinazotumika kwa vitu vinginevyo na spirit kwa hiyo hao nao waweze kuwemo ili tuweze kuwatambua. (Makofi)
Lakini vilevile nilitaka kuangalia suala zima la disposal of articles, chemicals and chemical products. Hii hapa inakuwa na shida. Shida iliyokuweko kwenye maabara hii kuu ya Mkemia panatawaliwa zaidi na rushwa. Na rushwa inatokezea kwasababu kila mmoja anayepeleka sampuli zake pale anahitaji kuwa na positive results. Na ili aweze kupata positive results anatengeneza mazingira ya kupata positive results. Nafikiri ni pahala ambapo pa kuweza kuangalia vizuri. Wale ambao wanaambiwa kwamba hii bidhaa iende ikawe disposed nyingine nyingi zinafika njiani zinageuzwa na zinaingizwa mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja ya kwamba kunakuwa na Askari wanao-escort lakini tushashuhudia bidhaa nyingi nyingi ambazo tunaambiwa hizi aidha zime-expire au zimekuwa condemned zikawe disposable lakini baada ya wiki moja, mbili unazikuta ziko mtaani pengine zimehamishwa Mkoa mmoja na kupelekwa Mkoa mwingine. Nafikiri hapa kungekuwa na sheria yenye adhabu kali inayoweza kuoneka ya kuweza kuwadhibiti hawa watu ambao bidhaa zao zimeshakuwa condemned au zimeshaambiwa hizi zikawe disposable na ziweze kuwa disposable; lakini wasimamizi wa hapa waweze kueleweka. Hii technical committee (advisory board) ndiyo inayotakiwa ifanye usimamizi wa zile bidhaa ambazo zinakuwa disposable.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nimeliona kwamba lina mkanganyiko, tuna maeneo ambayo tumeyaona kwamba ni kazi za bodi lakini siyo kazi za bodi. Ni kazi za Chief huyu wa Government Chemical Laboratory, yeye ndiyo anaweza kuzifanya na zisiingizwe kwenye bodi, ni shughuli ambazo ni nyepesi za kuingizwa huko. Kwa mfano; take the sample of laboratory test imo kwenye moja ya function ya power of the board, haihusiki hapa. Tuitoe na tumuachie Mtendaji Mkuu hiyo kazi anaweza kuifanya na ikamalizika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nyingine hata hii tuliyosema conducting inspection of premises of service regularly by the authority, hii hapa nayo vilevile haina haja ya kuweko kwenye bodi, ni kazi ambayo inaweza kufanywa na chief na hiyo kazi ikaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nililiona ambalo linahitaji kufanyiwa marekebisho ni power of inspection. Kwenye power of inspection article ya 15 hii hapa…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kupata fursa hii ya kuchangia hii miswada miwili iliyo mbele yetu. Kwanza nishukuru Mungu kwamba Serikali imeshtuka na kuweza kujitambua katika eneo hili. Na mimi ni-declare interest kwamba na mimi ni mtafiti na nimefanya hii kazi kwa muda wa miaka tisa, najua machungu na najua kazi inayotakiwa kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaloweza kusema la mwanzo, sheria hii ndiyo roho ya nchi ya uhai wa chakula cha nchi hii ya Tanzania. Dunia yoyote bila ya kuwa na utafiti/watafiti haiwezi kupata maendeleo. Tanzania tumekuwa siku zote watafiti kama watoto waliokuwa yatima; kila mmoja anafanya shughuli zake kwa mujibu wa anavyoona yeye na kwa mujibu wa fedha alikozipata. Lakini kuweko na sheria hii utaweza kuifanya nchi kuwa na mwelekeo na kuratibu hizi tafiti mbalimbali ambazo zimeshafanywa, na nyingine ambazo zinahitajika kufanywa katika utaratibu ambao wa kuleta maendeleo au tunaita research impact. Act hii imeweza kutuonesha mwelekeo sasa vipi tuweze kuelekea na vipi tuweze kujipanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilokuwa nalo ndani ya nchi hii watafiti wamekuwa hawana coordination ya kuweza kujua kwamba huyu mtafiti anatakiwa afanye utafiti huu kwa ajili gani. Matokeo yake siku zote tunapata tatizo kubwa la asilimia 80 ya mbegu ambazo tunatumia katika mazao yetu tunaagiza nje au mbegu hizo zinatumika zile ambazo zilikuwa zimeshatumika miaka mitatu ama minne nyuma, yaani wakulima wetu bado wana ule utamaduni wa kutumia mbegu wanazoweka katika moshi; zikapigwa na moshi kwa muda wa mwaka mzima baada ya mwaka unaofuata zikaenda shambani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa utafiti huu kutaweza sasa kuratibu utaratibu mzuri wa upatikanaji wa mbegu katika vituo vyetu mbalimbali vya uzalishaji mbegu lakini vile vile itawasaidia watafiti na Sheria ile ya Breeding Act kuweza kkujitambua na kutoa mbegu hizi kwa mujibu wa mahitaji ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi itawasaidia wajasiriamali mbalimbali waliohusiana na utafiti kuweza kupata soko la uzalishaji wa mbegu ambazo zitaweza kutumika nchini na kupunguza tatizo la upatikanaji wa mbegu mbovu, zisizo na viwango na zisizotoa mazao ambayo yanalingana na uzalishaji kwa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo linajitokeza, sheria hii itaweza kuisaidia nchi kuanza sasa kupata fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vya taasisi vya utafiti duniani. Kuna mashirika manne makubwa duniani ambayo wao kazi yao kubwa kusaidia taasisi za utafiti. Kwa hiyo, kuanzishwa kwa mfuko wa utafiti utasaidia mashirika yale kuitambua nchi hii kwamba ina sheria ya utafiti na kuweza kuleta fedha zao ambazo zitawasaidia watafiti kwa kiasi kikubwa kufanya shughuli zao na kuleta mabadiliko chanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, si hilo tu, hata kwenye vyuo vyetu vikuu ambavyo kwa kiasi kikubwa ndizo zinazoratibu na kufanya tafiti nyingi ambazo hazichukuliwi zikafanyiwa kazi. Sheria hii itaweza kuvifanya vile vyuo zile tafiti zao zitambulike na ziweze kufanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa lililokuwepo ni database ya utafiti haipo, kila mmoja amekusanya data zake kwa mujibu wa vile alivyokuwa nazo yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kubwa linalotakiwa hapa ni kuwepo na uratibu mzuri wa Mkurugenzi huyu wa TARI kuweza kukusanya taarifa za tafiti mbalimbali katika vituo mbalimbali na kuweza kuzi-publish lakini nyingine kuanza kuzifanyia kazi kama zilivyopendekezwa katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sasa hivi ni msimu wa kilimo katika maeneo yetu mbalimbali, Tanzania hii mikoa minne tu ndio yenye uhakika wa kupata mvua ya milimita 800 kwa mwaka, mikao iliyobaki mvua zake ni za kubahatisha; zipo chini ya milimita hizo 700 na wakati mwingine zinanyesha katika mazingira tofauti kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa utafiti kila Mkoa utaweza kusaidia sasa watu hawa wanatakiwa wapande zao gani, kwa wakati gani na kiwango gani ambacho cha mazao kinachoweza kutoka katika yale mashamba kulingana na uwezo wa uzalishaji na nyenzo zile alizozipata za kuzalishia. Lakini vilevile itaisaidia Serikali kuweza kuweka nguvu katika ile Mikoa ambayo ina uhakika wa uzalishaji, ili kupeleka mbolea na pembejeo nyingine kwa wakati unaofaa na kuwa na uhakika wa uzalishaji kuliko hali ilivyo sasa hivi, kila mmoja anakwenda kulingana na mazingira yanayomkabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimeliona na nililotaka kuchangia ni suala zima la kazi za hizi taasisi. Taasisi ina kazi nyingi na ni za msingi. Kwa bahati na mimi ni mjumbe wa Kamati hii, nilichangia mengi katika Kamati lakini yapo yale ambayo nilikuwa nataka kukazia tu. Moja kati ya kazi ambayo nlitakiwa kuhakikisha ina-coordinate ni kukusanya database ya utafiti iweze kuwa alive, iweze kuwa strong na kuwe na mfumo mzima wa upashanaji habari; hiki ndicho kitu kitakachoweza kutusaidia. Kwa sababu wavumbuzi ni wengi, wanavumbua vitu vingi lakini hakuna taarifa zinazotangzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, juzi kulikuwa na kikao cha wavumbuzi waliokuwa wamefanya tafiti za kuzalisha miche bora ya kahawa ambayo inakubali katika mazingira ya baridi kama maeneo ya Arusha, Moshi, Mbeya na maeneo mengine ambayo yana baridi ambayo inafikia mpaka degree 18 na miche ile inafanya uzalishaji ulio mzuri. Taarifa zile ni nzuri, miche ile inakomaa au inazaa kwa muda mfupi lakini vile vile inastahamili yale magonjwa ambayo yanasababisha miche ile ieweze kufa. Kwa mfano leaf mina ni tatizo kubwa, coffee stem borer, wale ambao wana athiri katika maeneo yale, wamefanyia utafiti mzuri, wamepata tiba ya kuweza kuhakikisha kwamba miche ile imekuwa resistance na mazingira yetu. Kinachotakiwa sasa hivi ni kuwepo uhakika sasa wa kuisambaza kwa wakulima. Lakini vilevile kuwepo na taaluma ambayo itatolewa na mabwana shamba na mabibi shamba katika maeneo mbalimbali ili uzalishaji uweze kubadilika baada ya miaka mitatu. Miche mingi tuliyokuwanayo sasa hivi inazaa hasa kuanzia miaka mitano, lakini hii ya sasa hivi iliyokuwa imegunduliwa na vituo vyetu vya utafiti vya Arusha na KCU wameweza kutoa miche ya miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu kuna tafiti ambazo zinafanywa siku nyingi na bodi ya korosho, kule Naliendele, mpaka tafiti zile hazitangazwi, mpaka leo tafiti zile hazijaleta matunda. Kunachohitajika ni kupata mikorosho ambayo itazaa kwa muda mfupi, njia za kufanya hivyo zipo. Kumepatikana njia za kuweza kufanya grafting ya mikorosho ambayo itaweza kuzaa kwa muda wa miaka mitatu na ikifika miaka mitano tumeshafikia pick ya production na kuweza kupata matunda kwa muda mfupi, lakini yaliyo bora na yanayoweza kustahamili ukungu kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya utafiti watu wengi lakini tafiti zile bado zipo kwenye makabati; tunahitaji zitoke, tunahitaji ziwasaidie wakulima waweze kuzalisha mazao kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine linalokuwa linaleta ukakasi ni suala zima la tafiti zinazofanyika hasa kwa nzi wa maembe au wadudu ambao wanaathiri matunda mbalimbali. Tanzania ilikuwa ni moja kati ya nchi ambayo inasafirisha matunda nje kwa kiasi kikubwa sana. Lakini kutokana na tatizo la kupatikana na hawa nzi wa maembe ambalo limekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini tumeshindwa kabisa kuweza kuingia katika hayo masoko ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zipo za kugundua tiba ya hawa nzi wa maembe lakini vilevile tiba ya nzi ambao wanasababisha matunda mbalimbali kuweza kuharibika, lakini bado zimefungiwa kwenye makabati. Lakini watu tayari wameshachukua Ph.D kwa tafiti hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii timu ya watafiti au huyo director aweze kukusanya hizi taarifa mbalimbali za tafiti na kuzitangaza ili watu ambao wanaweza kusaidia kutoa ufadhili wa kutengeneza hizo dawa au kununua hizo dawa nje ya nchi ziweze kuja, ziweze kutusaidia ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.