Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Muhammed Amour Muhammed (7 total)

MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini pia sikuridhika sana na majibu yake ambayo ameyatoa ya kubahatisha zaidi. Tunao ushahidi wa kutosha kabisa mpaka wahanga waliopigwa na kunyang‟anywa samaki wao wavuvi na JW (Jeshi la Wananchi) sasa sijui Mheshimiwa Waziri na kisingizio hapa ni license zinazotumika wanadai kwamba sizo.
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu la kwanza katika swali la nyongeza ni aina gani ya license zinazotakiwa kutumika na wavuvi hawa?
Swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana na mimi tukamuonesha wale wahanga ambao walipigwa na wakati mwingine walinyang‟anywa samaki wao, matendo haya yanafanyika zaidi katika bahari ya Kigamboni na Kunduchi? Ahsante sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kwamba niko tayari kufuatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kuwaona hao ambao inasemekana ni wahanga wa kipigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini napenda nirudie yale niliyoyasema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa kuwa nchi hii inafata utawala wa sheria ni vema basi Mheshimiwa Mbunge anapopata tuhuma kama hizo akazifikisha sehemu husika.
Mheshimiwa Spika, siyo vema suala kama hili tulisikie mara ya kwanza ndani ya Bunge, sisi tupo, ofisi zetu zipo, Mheshimiwa Mbunge alipaswa kutufikishia ili tufanye uchunguzi na pale inapothibitika tuchukue hatua stahili, ningependa tuende kwa mwendo huo zaidi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu ni aina gani za leseni niseme tu kwamba hili ni suala ambalo liko chini ya Wizara inayohusika na masuala ya uvuvi. Wanajeshi wanajukumu moja la kuhakikisha kwamba wavuvi hawatumii njia za uvuvi wa haramu basi, siyo suala la kuangalia leseni, leseni ina mamlaka zake.
Mheshimiwa Spika, hivyo, tunachoweza kusema hapa ni kwamba yanapotokea matukio kama haya toa taarifa ili tufanye uchunguzi na kuchukua hatua zinazostahili.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ambayo hayako makini, majibu ambayo hayaendi sambamba na swali langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mantiki ya swali langu lililenga usalama wa wasafiri pale na mali zao. Kwa kipindi kirefu sasa wananchi wanaotumia bandari mbili hizi, kila bahari inapopata michafuko kidogo wamekuwa wakifa kwa wingi sana pale.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inathibiti vifo vya watanzania katika bandari mbili hizi ambao mara kwa mara wanapotea wao na mali zao?
Swali langu la pili la nyongeza, inaoneka Serikali haikufanya utafiti wa kutosha. Swali langu halilengi ubora wa bandari, linalenga usalama wa raia wetu pale kati ya bandari mbili hizi.
Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kufuatana na mimi kuona mazingira halisi ya usafiri pale katika bandari ya Mkokotoni kwa sababu TRA wako pale wanakusanya kodi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama amenisikiliza vizuri katika jibu langu la msingi hatua ambazo tunazichukua ya kwanza ilikuwa inajibu swali lake kikamilifu. Hatua zilizofuata tumeongeza mipango mingine tunayoifanya, kwamba SUMATRA hufanya ukaguzi kila mwaka, vilevile hufanya kaguzi za kushtukiza kuhakikisha kwamba vyombo hivi vinavyoelea majini vinakuwa na usalama wa abiria na mizigo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili niko tayari, tutapanga tukubaliane siku ya kwenda na tukaelee majini kati ya Bandari ya Tanga na Mkokotoni ili tukubaliane haya ambayo Serikali inayasema na Mheshimiwa Mbunge anadhani kwamba hatuyajibu kikamilifu. (Makofi)
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa nami kuuliza swali la nyongeza.
Pamoja na majibu ambayo ni ya kawaida, hayana details za kutosha kutoka kwa Serikali na kwamba yako zaidi kimaelezo, kwenye implementation stage hayaonekani kwamba yako hivyo; je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba wanashirikisha ipasavyo; yaani wanaitumiaje PPP ili kuona kwamba tunafika kwenye huo uchumi wa viwanda ifikapo 2025?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili ni kwamba kumekuwa na kero na manyanyaso makubwa sana yanayofanywa na TRA kwa wafanyabiashara hususan hawa wenye maduka kwa kuwapa kodi ambazo hazistahiki. Je, Serikali haioni kwa manyanyaso haya itasababisha hayo malengo ya kufika uchumi wa kati na kwenda kwenye viwanda ifikapo 2025 ni ndoto tu kwa Watanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli kwamba hakuna mipango inayoshikika ya kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Ni dhahiri kuwa Serikali inachokifanya ni kuandaa mazingira wezeshi ya kuwafanya wawekezaji ambao kwa kiwango kikubwa sana tunategemea sekta binafsi kuja kuwekeza na kuifanya nchi yetu ifikie katika uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ambayo yanaweza yakaifanya nchi ikafikia katika uchumi wa viwanda, mojawapo ikiwa ni masuala ya miundombinu ambayo ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Mbunge naye ni shahidi, anaona kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali katika eneo hili, lakini pia katika usafirishaji na maeneo mengine ya utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tulichokisema hapa kama Serikali, siyo maneno tu, lakini mipango na mikakati ya kuifanya Tanzania kufikia katika nchi ya viwanda, imeelezwa katika majibu yangu ya msingi na ninaomba nisirudie, lakini tu niseme tu kwamba ni dhamira ya Serikali kuifanya nchi yetu iwe nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili, ameuliza kuhusu manyanyaso wanayopata wafanyabiashara kutokana na kodi inayotozwa na TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya mambo ambayo Wizara tumekuwa tukifanya muda wote ni kuhakikisha tunaweza mazingira rahisi ya kufanya biashara katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweka utaratibu wa kukutana na wafanyabiashara kila baada ya muda mchache kusikiliza kero zao na yale ambayo wamekuwa wakituwasilishia tumekuwa tuliyafanyia kazi. Hivi sasa tuna blue print document ambayo imeelezea namna gani Serikali itasaidia kutatua vikwazo ambavyo vinawakabili wafanyabiashara ili kuifanya nchi hii iende katika nchi ya uchumi wa viwanda. (Makofi)
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Majibu ya Serikali hayatoshelezi, ni afadhali tu kidogo. Pamoja na majibu hayo, nina maswali mengine mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kuna kauli mitaani zinasemwa na Watanzania kwamba Tanzania inashiriki hasa hasa kwa maslahi binafsi ya kukomba mali za DRC kwa mfano. Je, Serikali ina matamshi gani kwa lengo la kuwaosha Watanzania kutokana na tuhuma hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Jeshi letu linapopigwa kwenye vita hasa pale DRC kuna kauli pia kwa Watanzania wanaamini kwamba Jeshi la Uganda linashiriki katika kulipiga Jeshi la Tanzania kwa kuwa wakati fulani kihistoria Waganda na Watanzania walipapurana kivita. Je, ni ipi kauli ya Serikali kuhusiana na kadhia hii? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa bahati mbaya sana maneno kama haya yanatolewa na Watanzania ambao kwa kweli wanatakiwa wao wawe wazalendo na kuweza kupongeza juhudi za Serikali za kuwasaidia wenzetu ambao wako katika hali ambayo haina amani katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna suala la kukomba mali za DRC kwa maslahi binafsi, halipo. Tanzania haishughuliki na kuchukua chochote sehemu yoyote wanayolinda amani. Majeshi yetu yako kule kusaidia kurudisha hali ya amani, kuwalinda wananchi dhidi ya waasi ambao wanapigana katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kwamba Jeshi la Uganda linashiriki katika kuwapiga Watanzania pia halina ukweli wa aina yoyote. Matukio yote yaliyotokea tuna ushahidi wa kutosha kwamba ni vikundi vya waasi. Mwanzoni walikuwa M.23 na sasa hivi kuna vikundi vingine ambavyo vinatokea katika nchi mbalimbali za jirani pale lakini hakuna ukweli kwamba Majeshi ya Uganda yanashiriki katika kuwapiga askari wa Tanzania. (Makofi)
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Serikali ambayo yanaonekana kuchupachupa kwa baadhi ya mambo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ni community based, kwa kuwa research ni suala la Muungano na 2018 ilifanywa research kule Zanzibar nzima, ndani ya harakati za wale vijana kufanya research waliwaharibia wananchi wetu mazao yao. Je, ukizingatia research ni suala la Muungano Serikali ya Jamhuri ya Muungano ina namna gani ya kurejea nyuma angalau kuwapa mkono wa pole wale waliowaharibia mazao yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali imesema kwamba wamekubaliana mafuta na gesi kila upande ufanye kwa kutumia taasisi zake. Pamoja na Azimio ambalo limepitishwa na Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar lakini bado suala la mafuta linabaki ni la Muungano. Je, hatuoni sasa ni wakati mwafaka sheria hii ambayo imo ndani ya Katiba ya Muungano kwamba mafuta ni suala la Muungano tukalitoa sasa ili kurahisisha uwekezaji kule Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri. Swali lake la kwanza ameulizia namna gani Serikali ya Muungano inaweza ikawalipa fidia wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa wakati wa utafiti. Kama lilivyosema jibu langu la msingi, utafiti huu ulifanyika kwa ajili ya masuala ya mafuta au gesi; na kwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar kwa nia njema ilipofika mwaka 2015 Bunge hili lilipitisha Sheria ya Mafuta na kifungu cha 2 kilianisha kabisa mamlaka ambazo zitatumika katika suala zima la utafutaji mafuta ni kwa pande zote mbali na ni kwa nia njema ya kupunguza urasimu. Kwa kuwa shughuli hizi za utafiti za mafuta na gesi zilifanyika upande wa Zanzibar ambao wana mamlaka na walipitisha Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 labda nilichukue na kwa sababu tuna ushirikiano mzuri tutawasiliano na Wizara ya upande wa pili wa Muungano Zanzibar kuona hili jambo wanalifanyia kazi vipi lakini nia ilikuwa njema.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ameuliza kwa kuwa suala hili lilifanyika kwa nia njema kwa nini lisifanyiwe marekebisho. Jambo la kufanya marekebisho katika Katiba limeundiwa utaratibu wake ndani ya Katiba hiyo hiyo lakini kwa sasa kwa nia njema Bunge hili hili liliridhia kupitisha Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 na Baraza la Wawakilishi wakapitisha Sheria yao ya Mafuta ya mwaka 2016 kwa sasa shughuli zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako walikuwa mashahidi tarehe 23 Oktaba, 2018, Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ilitiliana saini mkataba wa kugawana faida itakayopatikana wakati wa kuchimba mafuta au gesi na Kampuni ya RAK Gas kutoka nchi ya Ras Al Khaimah. Kwa hiyo, ni wazi kwamba tangu waingie mkataba huo kazi inaendelea na hakujatokea mgongano. Hata hivyo, hili naomba niliachie mamlaka zingine na Bunge hili kama itaona inafaa. Ahsante sana.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali ambayo kwa kiasi fulani yanatoa mwangaza kidogo na yanaonesha matumaini katika maelezo sijui kwenye utendaji itakuwaje. Pia nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kulitamka jina langu kama vile ambavyo linatakiwa litamkwe, hakulikosea hiyo ndio asili ya jina Muhammed Amour Muhammed.

Mheshimiwa Spika, pamoja na yote hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tunategemea idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka nchi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka ratio ya uwazi kabisa katika kutoa ajira Serikalini kwa watu wenye ulemavu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, watu wenye ulemavu nao ni watu kama wengine, wanasafiri wanaenda kwenye viwanja vya michezo kama football na kadhalika tunawaona mara nyingine wanapata tabu bandarini pale, saa nyingine airport na mara nyingine kwenye vituo cha mabasi. Je, Serikali imejipangaje katika kuweka miundombinu wezeshi kwa watu wenye uleamavu katika maeneo kama yale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge vile ambavyo anafuatilia masuala haya ya watu wenye ulemavu. Ameulizia kuhusiana na ratio ni kwa jinsi gani Serikali ina weka ratio ya ajira kwa watu wenye ulemavu. Bunge letu Tukufu lilitunga Sheria Na.9 ya mwaka 2010, ndani sheria imeelezwa wazi kwamba watu wenye ulemavu ni kwa jinsi gani wanatakiwa kuajiariwa. Mwajiri yoyote mwenye watu kuanzia 20 na kuendelea, basi 3% inatakiwa kuwa ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, kwa hili lipo wazi na niendelee kuwasihi na kuhawamasisha waajiri kwamba waweze kuitekeleza sheria hii kwa sababu sheria hii ya watu wenye ulemavu ni sawa na sheria zingine na pia inapobidi sheria itachukua mkondo wake wa yule ambaye atakuwa hatekelezi.

Mheshimiwa Spika, vile vile ameuliza ni kwa jinsi gani Serikali inahakikisha kwamba usafiri kwa watu wenye ulemavu unakuwa ni rafiki. Mimi mwenye nimefanya ziara katika maeneo kadhaa ikiwemo airport, lakini pia tumeendelea kusisitiza na kuweka mkazo kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwa rafiki. Katika airport kwa hapa nchini tunahakikisha kwamba kunakuwa na wheelchair lakini kunakuwa na zile ambulift kwa ajili ya kubeba watu wenye ulemavu pamoja na wazee.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia kwenye maeneo ya usafiri wa umma ikiwemo huu usafiri wa kawaida hiyo ni changamoto ambayo nikiri wazi tunaendelea kuifanyia kazi kwa kuendelea kuelekeza wamiliki wa vyombo hivi kuhakikisha kwamba miundombinu inakuwa ni rafiki kwa watu wenye ulemavu.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu ambayo Serikali imetoa ambayo ni ya kawaida sana hayako katika uhalisia yako much shallow kwa kweli katika swali langu la msingi lililenga zaidi ufaulu wa wanafunzi kutoka kidato cha IV kwenda kidato cha V, sio labda majengo zaidi aaah! Ni kiasi gani asilimia ngapi inafaulu kutoka IV kwenda V na pia lilenga zaidi kwenye subject matter.

Sasa je, Serikali inajiridhishaje hata hizi takwimu ulizonipa nina mushkeli nazo nitaomba zaidi kama ziko takwimu za ufaulu kutoka IV kwenda V nipatiwe kwa Tanzania nzima. Sasa swali langu la nyongeza ni hili. Je, Serikali kupitia Wizara inayohusika inajiridhishaje kwamba zile competences zilizoainishwa kwenye syllabus zinafikiwa? Hapo ndiyo ulipo mushkeli wangu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema majibu yetu yamekuwa ya kawaida na ni shallow. Ukweli wa mambo tumejibu kutokana na swali alilouliza yeye kauliza matokeo ya mtihani wa kidato cha IV yamekuwa mabaya kwa kipindi kirefu sana na hali hii haijapatiwa ufumbuzi wowote na maswali ikawa ni nini tamko la Serikali kuhusiana na hali hiyo, lakini vile vile akauliza kuhusu juhudi.

Mheshimiwa Spika, sasa tamko la Serikali nililokupa ni kwamba tumekupa takwimu kuonyesha kwamba ukiangalia kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa kumekuwa na ongezeko la ufaulu katika mitihani ya Kidato cha IV kutoka mwaka hadi mwaka. Mwaka huu tumefikia asilimia 78, wakati mwaka 2015 tulikuwa asilimia 67. Sasa kama unataka kujua ni kiasi gani cha hao wanaoenda kidato cha V hapo sasa ungeleta swali lingine au ungeuliza kwenye swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, na kuhusiana na hilo suala alilouliza la competences naomba nimuhakikishie Mbunge kwamba tunajaribu kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kwamba elimu yetu inakuwa bora na ndiyo maana nimeorodhesha hatua au mambo mbalimbali ambayo tunayafanya ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu, ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu, tunapitia mitaala, tumehuisha mfumo wa udhibiti ubora. Kimsingi tulipo sasa ni bora kuliko tulikotoka na nimuhakikishie tu pamoja na Mheshimiwa Wabunge wengine kwamba Serikali itaendelea kuweka mkazo ili kuendelea kuboresha elimu yetu.