Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mussa Bakari Mbarouk (7 total)

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUSSA BAKARI MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha na mimi leo kusimama hapa kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Vilevile nitakuwa ni mchoyo wa shukrani kama sikuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo langu la Tanga Mjini ambao kwa mara ya kwanza wamebadilisha historia ya Tanzania kwa kupatikana Mbunge wa Upinzani katika Jimbo la Tanga iliyokuwa ngome kuu ya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia viwanda, biashara na ubinafsishaji. Kwanza nisema bila umeme wa uhakika basi Tanzania ya viwanda itakuwa ni ndoto za alinacha. Nasema hivi kwa sababu nchi yetu imekuwa kama nchi ya kufikirika. Baada ya kugundulika gesi na makaa ya mawe tumekuwa tukiambiwa kwamba umeme kukatikakatika utakuwa kama historia ya vita ya Majimaji iliyopiganwa mwaka 1905 lakini leo umeme umekuwa hauna uhakika, humu humu ndani ya Bunge pia umeme unakatika, sasa sijui Tanzania ya viwanda itakuwa ni Tanzania ipi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba viwanda, biashara, reli na barabara ni vitu vinavyoambatana. Imefika mahali sisi Tanzania tumekuwa tunafanya vichekesho, kwa nini? Leo reli inayotoka Tanga kuja kuungana na reli ya kati imekufa, lakini vilevile pia viwanda vingi, hakuna asiyejua kwamba Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda. Tulikuwa na Kiwanda cha Chuma – Steel Rolling Mills, tulikuwa na kiwanda cha Sick Saw Mill, tulikuwa na Kiwanda cha Mbolea, tulikuwa na Kiwanda cha Kamba – Ngomeni, tulikuwa na NMC, tulikuwa na karakana kubwa ya reli, vyote hivyo vimeuliwa chini ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, kutokana na kufa viwanda hivi, leo Mji wa Tanga umekuwa hauna ajira. Tukumbuke Tanga ulikuwa siyo mji wa mazao ya vyakula, ilikuwa ni mashamba ya mkonge nayo pia yamekufa. Sasa imefika mahali Tanga umekuwa kama mji ambao ulikuwa na vita kama Baghdad vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kuuliwa viwanda vya Tanga matokeo yake sasa miaka 55 baada ya uhuru Tanzania leo tunaongoza kwa kilimo cha pamba lakini nepi za watoto wachanga made in China. Sindano ya kushonea kwa mkono made in China! Vijiti vya kuchokolea meno (tooth pick) made in China! Miti ya kuchomea mishikaki pia made in China! Basi hata handkerchief pia! Bado tukikaa humu ndani tunajisifu kwamba sisi tuna viwanda na tunataka kuifanya Tanzania ya viwanda, mimi sikubaliani na suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema kama tunataka kuifanya Tanzania ya viwanda kwanza tufufue vile viwanda vingi vilivyouliwa katika mji wa Tanga! Hakuna asiyejua, ukienda Tanga, Muheza ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya matunda hususan machungwa lakini leo tunanunua packet ya juice kutoka Saudi Arabia kwa shilingi 5,000. Hakuna asiyejua kwamba ukienda maeneo ya Hale na Korogwe kuna maembe ya kutosha lakini hakuna hata viwanda vya ku-process matunda hayo tukaweza kuuza sisi katika nchi nyingine. Leo matunda na juice zote zinatoka nje wanaoleta huku wanachukua pesa zetu za kigeni wakaenda kununulia. Unapokuwa una-import zaidi kuliko ku-export maana yake unajikaribishia umaskini lakini wenzetu hilo hawalioni! Anayezungumza hapa ataanza kupongeza, ataanza kusifu Ilani ya Chama cha Mapinduzi lakini yanapoharibika hasemi kwamba ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi ndiyo inayoharibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza mimi nashangazwa, mbona nchi nyingi duniani zinafanya maendeleo lakini hawataji ilani za chama! Kenya shule zinajengwa, maabara zinajengwa, ukienda Malawi barabara zinajengwa na maendeleo mengine yanafanyika lakini watu hawataji Ilani ya Chama! Mimi naona tatizo hapa ni Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, lazima tubadilike, Serikali yoyote inayokusanya kodi kazi yake ni kurudisha kodi hiyo kwa kuwapelekea wananchi maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala la biashara, Watanzania leo wamekuwa wakihangaika hususan akina mama, ukienda katika kila nyumba sasa hivi katika mikoa yetu na miji yetu mikuu, kila nyumba ina frame za maduka kwa sababu ajira hakuna na viwanda hakuna. Leo akina mama ndiyo wanaolea familia, wanahangaika wanafungua biashara lakini cha kushangaza sheria ya biashara ya Tanzania ni tofauti na sehemu nyingine. Kawaida ya biashara, mfanyabiashara anapoanza biashara upya lazima apewe tax holiday ili ajiweke vizuri aweze kupata faida alipe kodi. Hata hapa ndiyo sheria inavyosema kwamba usilipe kodi kabla ya kupata faida lakini Tanzania mtu anakwenda TRA akishapata TIN Number anafanyiwa assessment, analipa kodi kabla hajafanya biashara! Matokeo yake sasa akina mama wanaokopa mikopo katika taasisi za kifedha kama BRAC, Poverty Africa na wengine wamekuwa wakichukuliwa vyombo vyao, wamekuwa wengine wakijinyonga na wengine wamekuwa wakikimbia familia zao kwa kuogopa madeni wanayodaiwa na taasisi za fedha. Sasa kwa nini Serikali yetu haiwasaidii wananchi wake katika biashara? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda Rwanda na Burundi anayekuwa na nia ya kufanya biashara baada ya mtaji aliokuwa nao Serikali inamuongezea fedha na kuambiwa kwamba tunakuongezea fedha uajiri Waburundi wenzako au Warwanda wenzako wawili usaidie kukuza ajira katika nchi yetu lakini Tanzania ni kinyume. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, nakuomba ulizingatie hili, Tanga viwanda vingi vimeuliwa, hususan reli. Panazungumzwa hapa reli ya kati itajengwa katika kiwango cha standard gauge, lakini Waswahili wana usemi wao wanasema, mwiba uingiapo ndiyo unapotokea hapo hapo. Reli ya kati ilianza kujengwa na Wajerumani katika miaka ya 1905 na ilianzia Tanga, vipi leo twataja reli ya kati ijengwa kuanzia Dar es Salaam! Tumesahau kwamba mwiba uingiapo ndio utokeapo? Mimi naomba kama reli ya kati inataka kufanyiwa ukarabati basi ianzie Tanga, Bandarini pale ambapo ndio reli ilipoanzia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nalotaka kusema, tumeambiwa hapa na wazungumzaji wengi kwamba viwanda vilifanyiwa ubinafsishaji na vingine kuuzwa. Amesema Mheshimiwa Lijualikali kwamba kule kwake kuna mbuzi katika kiwanda cha sukari lakini hata Tanga kwenye kiwanda cha chuma! Cha kushangaza walikuja wawekezaji wa Bulgaria, wakaja Wajerumani wakataka kiwanda kile cha chuma lakini matokeo yake wakanyimwa, wakapewa wawekezaji waliotakiwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Matokeo yake sasa kiwanda kile imekuwa ndani kunafugwa mbuzi napo kama vile ilivyokuwa Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha chuma cha Tanga kilikuwa kinazalisha two products same time, kulikuwa pana misumari bora kabisa katika Afrika Mashariki na nondo zinazozalishwa Tanga zilikuwa ni bora. Sasa na mimi najiuliza, chuma bado kinahitajika siku hadi siku katika ujenzi wa maghorofa, katika ujenzi wa madaraja lakini hata katika body za magari, inakuwaje kiwanda cha chuma kipate hasara mpaka kife? Huu ni ushahidi kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kusimamia viwanda vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme Mheshimiwa Waziri, hoja yako siiungi mkono naunga mkono hoja iliyotolewa na Upinzani lakini kwanza iangalie Tanga! Katika viwanda vingine usisahau viwanda vya matunda, Tanga ni mji unaozalisha matunda kwa wingi, tunahitaji viwanda vya matunda navyo vijengwe Tanga ili Tanga iweze kurudia hadhi yake kama zamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nikumbushe historia kidogo, hata ukiangalia jina la nchi hii kabla ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar ilikuwa inaitwa Tanganyika. Sasa hebu angalia Tanga ilivyokuwa na umuhimu katika nchi hii, Tanga na nyika zake ndio tukapata hii Tanganyika lakini bado watu wamesahau historia kwamba Tanga imechangia mchango mkubwa katika kuleta uhuru wa nchi hii, leo Tanga imekuwa imeachwa kama mtoto yatima! Hata ukiangalia bajeti ya mwaka huu 2016/2017, Tanga tuna mambo mengi ambayo tumeachwa, tutakuja kuzungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata vilevile pia katika huo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar palikuwa pana mahusiano mazuri sana kati ya watu wa Zanzibar na watu wa Tanga na hususan katika masuala ya kibiashara. Mpaka leo watu wanaingiliana katika biashara, watu wanawekeza upande wa Bara na Visiwani, lakini Serikali imekuwa haitii nguvu kwa hawa wafanyabiashara ambao ni wazalendo.
Vilevile pia tumeacha sasa kuikumbuka na kuisaidia Tanga kwamba ndio yenye historia ya uhuru wa nchi yetu, lakini tunaomba Mheshimiwa Waziri asisahau kwamba hata yeye yawezekana akawa ana jamaa zake na ndugu zake Tanga, kwa nini? Kwa sababu Tanga ulikuwa ni mji wa viwanda, uliweza kukusanya makabila yote ya Tanzania 122 lakini hata nchi jirani kutoka Burundi, tunao Warundi wengi kule, kutoka Malawi tunao watu wanaitwa Wanyasa kule, kutoka Kenya, Uganda, Zambia watu walikuja kufuata ajira Tanga, sasa inakuwaje viwanda vya Tanga vife. Mimi naomba kama Waziri una nia ya kweli ya kuifanya Tanzania ya viwanda hakuna haja ya kujenga viwanda vipya, tukifufua viwanda vya Tanga peke yake na maeneo mengine ya Tanzania kweli tutakuwa Tanzania ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa kabisa tusisahau kwamba bila ya umeme wa uhakika viwanda vitakuwa ni kama vile mchezo wa alinacha. Lazima kwanza tuwe na umeme wa uhakika, iwe tuna dhamira ya kweli kwamba kweli tumegundua gesi, tumegundua makaa ya mawe lakini hata upo umeme pia wa upepo lazima tushirikishe umeme wote huo. Wenzetu wa baadhi ya nchi kama Ujerumani pamoja na ukubwa wake wanatumia solar power system na sisi kwa nini hatuna mpango wa muda mrefu wa Serikali wa kujenga mtambo mkubwa wa umeme wa kutumia solar power system? Kama tuki-fail katika hydro-electric power twende katika gesi, Kama kwenye gesi tumeshindwa, tungekwenda katika solar power. Sasa Waziri unapozungumzia viwanda bila ya kutuhakikishia kwanza kwamba tuna umeme wa uhakika, mimi hapo inakuwa sielewi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri, hakuna haja ya kujenga viwanda vipya, tufufue viwanda vingi zaidi ya 70 vilivyokuwa Tanga ambavyo vimekufa lakini tufufue na viwanda vingine ambavyo vya zamani kama alivyotaja Mheshimiwa mmoja kiwanda cha Nyuzi Tabora na vinginge ili tuweze kufikia maendeleo ambayo Watanzania wanayatarajia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, labda na mimi niungane na wenzangu katika kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa alivyotuwezesha kutupa afya njema tukaweza kuwemo katika Bunge letu leo hii siku ya tarehe 27 Mei, siku ya Ijumaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine nirudie kuwapongeza wapigakura wa Jimbo langu la Tanga Mjini. Kama nilivyosema kwa kubadilisha historia ya Tanzania na kuweza kumleta Bungeni Mbunge kutoka Kambi ya Upinzani kwa mara ya kwanza. Lakini vilevile niseme kwamba katika Wizara ya Elimu naunga mkono hoja iliyotolewa na Kambi ya Upinzani asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nianze kuchangia kama ifuatavyo; moyo na engine ya nchi ni elimu na ndio maana wanataaluma wakasema education is a life of nation. Lakini vilevile nimnukuu aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela, alisema kwamba education is the most powerful weapon which you can use to change the world yaani elimu ni silaha nzito ambayo inaweza ikaibadilisha dunia lakini sisi Tanzania imekuwa ni kunyume na ninasema hivyo kwa sababu leo ukienda katika Wizara ya Elimu kuanzia elimu ya nursery kuna matatizo, ukienda katika elimu ya msingi kuna matatizo, elimu ya sekondari kuna matatizo, ukienda kwenye vyuo vikuu ndio kabisa, sasa tujiulize hivi kweli miaka 55 baada ya Uhuru mpaka leo sisi Watanzania tunajadili madawati!
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wenzetu nchi ya India baada ya kupata Uhuru miaka 40 tayari Wahindi walikuwa wanaweza kutengeneza pikipiki aina ya Rajdoot, tayari walikuwa wanaweza kutengeneza magari aina ya Mahindra, tayari walikuwa wanaweza kutengeneza matreni, tayari wahindi baada ya miaka 40 waliweza kutengeneza vyombo vinavyokwenda aerospace katika anga za juu. Lakini leo Tanzania twajadili madawati, twajadili matundu ya vyoo, mashuleni vyakula hakuna it is a shame. Hii ni aibu, nchi kama Tanzania yenye rasilimali zote ambazo Mwenyenzi Mungu ametujalia lakini tumeshindwa kuisimamia vizuri elimu, tumeshindwa kuiweka misingi mizuri ya kielimu matokeo yake Tanzania tunakuwa na wa mwisho katika nchi tano za Jumuiya ya Afika Mashariki na kama sio ya mwisho basi labda tutakuwa tumeishinda Southern Sudan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunashindwa na Burundi, Rwanda,Uganda na Kenya. Leo Burundi waliokuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe wakauana watu milioni mbili lakini wana system ya one child onelaptop,sisi Tanzania ambao tunajisifi tuna eneo kubwa la nchi, tuna uchumi imara lakini tumeshindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi niseme na niishauri Serikali tusichanganye siasa na elimu. Tunaposema elimu bure basi iwe bure kweli, lakini kama tunawacheza shere Watanzania Mwenyenzi Mungu atakuja kutuhukumu kesho. Leo tumesema elimu bure, lakini hivi ni kweli elimu ni bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda shule za msingi leo hata maji ya kunywa watoto hakuna, kama pana nyumba ya jirani wakimbilie nyumba ya jirani kwenda kunywa maji. Leo watoto wa kike Ashakum si matusi anapokwenda kujisaidia lazima apate maji, shule zimekatwa maji, wanategemea kwenda katika nyumba za jirani, kama kuna muhuni, mvuta bangi huko mtoto wa kike ndio anaenda kubakwa huko huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wenzetu hamuoni kwamba haya ni matatizo. Sisi wapinzani tuna akili gani na ninyi wenzetu wa Chama Tawala mna akili gani. Miaka 55 baada ya Uhuru leo, tunajadili matundu ya vyoo, na ukiangalia hata katika matangazo ya Haki Elimu, mwalimu anakwenda kwenye choo na wanafunzi wamepanga mstari wanasukumana, choo hakina bati, hakijapauliwa, mwalimu anakanyaga mawe, lakini tunaambiana hapa ukitaka kuwa Rais lazima upitie kwa mwalimu, ukitaka kuwa Mbunge lazima upitie kwa kwa mwalimu, ukitaka kuwa Waziri Mkuu upitie kwa mwalimu. Tuna wacheza Watanzania shere, tuwaambieni ukweli kama tumeshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme kitu kimoja tu kwenye suala la elimu ya nursery, Mheshimiwa Waziri lazima ukasimamie vizuri kwa sababu elimu ya nursery tumeweka utaratibu kwamba mtoto haanzi standard one mpaka apite nursery school, lakini hivi Serikali imeangalia ufundishaji na mitaala ya kwenye nursery school? Hakuna kitu kila mwenye nursery school yake ana mitaala yake ana utaratibu wake wa kufundisha. Hii ni hatari kwa sababu mwingine anaweza akawa ana uwezo mzuri wa kufundisha, mwingine hana uwezo mzuri matokeo yake sasa wazazi wanapoteza fedha lakini watoto wakitoka huko kwa sababu msingi sio mzuri hakuna kitu wanapofika standard one.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi kwenye elimu ya msingi, hapa pana matatizo makubwa. Kwenye elimu ya msingi katika nchi yetu kumekuwa na utaratibu kwamba kwanza watoto wanakwenda shuleni wakati mwingine hata chakula mtoto hajapata nyumbani. Sasa matokeo yake mtoto anakwenda na njaa, na mtu mwenye njaa hafundishiki, matokeo yake mimi nilikuwa naishauri Serikali ikibidi lazima tupeleke bajeti ya chakula katika shule zetu za msingi, hata na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mtoto anapotoka nyumbani, anapokwenda shuleni na njaa hata mwalimu afundishe namna gani anakuwa haelewi. Amesema mwanafalsafa mmoja anaitwa Bob Marley, the hungry man is angry man, kwamba mtu mwenye njaa anakuwa na hasira, haelewi. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi niseme tupeleke bajeti kubwa ya chakula katika shule za msingi na sekondari na vyuo. Hata wale wanaotu-supply vyakula katika vyuo vyetu na shule zetu basi walipwe kama alivyotangulia kusema msemaji aliyetangulia, kwa sababu wengine wanapelekwa mahakamani, wametoa zabuni za vyakula Serikali haijawalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kwenye sekondari kuna matatizo makubwa, kuna suala zima la ukosefu wa walimu wa sayansi. Hakuna walimu wa mathematics, biology, physics na chemistry. Matokeo yake mtoto anamaliza form four hata ukimuuliza what is bunsen burner hajui, ukimuuliza what is test tube hajui, na matokeo yake wanakosa katika theory na practical zote wanakosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimtake Waziri ahakikishe maabara zinazojengwa zinaambatana pamoja na vifaa. Tusiseme tu kisiasa kwamba tunajenga maabara kumbe vifaa hakuna na matokeo yake hata wanaokuwa wanachukua masomo ya sayansi, kwa mfano wanaosoma PGM ndio hao tunaotegemea kwamba watakuja kuwa marubani. Lakini kwa ukosefu wa vifaa sasa tunakosa ma-pilot katika ndege zetu, matokeo yake tunaajiri wageni tunapeleka ajira katika nchi nyingine, mimi niseme lazima tujikite katika elimu iliyo bora kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye suala zima la vyuo vikuu. Vyuo vikuu kuna matatizo, na matatizo ni hayo ya mikopo, lakini hata na matatizo na uwezo wa wanafunzi wenyewe wengine wanaopelekwa. Lakini hata baadhi ya walimu pia nao uwezo wao sio mkubwa sana, matokeo yake sasa wanafunzi wetu wa vyuo vikuu wamekuwa nao elimu yao ikishindanishwa na nchi nyinine inakuwa sio bora.
Pia yupo Makamu Mkuu wa Chuo kimoja alisema, hata wanafunzi wa chuo kikuu hawawezi kuandika barua ya kuomba kazi, kwa kiingereza kwa sababu msingi ulikuwa ni mbovu, leo mtoto anakwenda shule ya msingi na njaa, leo mtoto anakuwa hana chakula, matokeo yake anateseka na njaa mpaka mchana, anatoka shule hana alichoelewa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba ya Bajeti ya Wizara yako kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la maliasili ni pamoja na Hifadhi za Taifa (TANAPA), bahari, mito, misitu na mbuga za wanyama au hifadhi. Tanga tunazo mbuga au hifadhi kama Mwalajembe, Kalalani, Mkomazi na Saadani, lakini bado hazijatangazwa katika medani za kitaifa, kiasi kikubwa cha kutosha. Naiomba Wizara yako ihakikishe inazitangaza mbuga za Mkomazi, Mwakijembe, Kalamani na Saadani katika viwango vya kimataifa ili ziweze kujulikana na kutembelewa na watalii wa ndani na nje na kuingiza mapato ya fedha za kigeni (foreign currency).
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapokuja watalii ajira zinaongezeka, kutajengwa hoteli, zitaajiri wahudumu pia wasafirishaji maliasili, pamoja na misitu. Napenda kuzungumzia utunzaji wa misitu ya nchi kavu na baharini pembezoni mwa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo ambayo kuna shughuli za utalii au maliasili na ikiwa kuna mapato yanaingia asilimia 20 zirudi katika eneo husika. Ikibidi isiwe fedha, ziwe samani au vifaa kama madawati, ujenzi wa zahanati na kadhalika. Naomba Tanga Mjini isikose madawati ya TANAPA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumezuka tabia ya kuibiwa wanyama pori wetu, ndege wetu na viumbe hai na kupelekwa nchi mbalimbali za Ulaya, Marekani na Asia, je, ni akina nani wanaofanya biashara hii haramu? Lazima nchi idai rasilimali zake na itunze viumbe hai hawa na anayehusika akipatikana hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia kwa maandishi bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kuboresha majengo ya ofisi zetu za Balozi za Tanzania nje ya nchi, zinatia aibu kwa majengo kuwa machakavu hata rangi hayabadilishwi. Naishauri Serikali, pale ambapo baadhi ya nchi zinatupatia viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kudumu ya Ubalozi mfano Oman, tuyajenge haraka iwezekanavyo ili kuepuka kunyang‟anywa viwanja hivyo na kupewa nchi nyingine kama ilivyotokea Oman; kiwanja chetu kupewa nchi ya India ambayo tayari wameshajenga jengo la kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafungu ya fedha yapelekwe mapema katika Balozi zetu za nje ili kuboresha utendaji bila kusahau kuboresha mishahara na elimu zao na kuwashughulikia Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi ambao wanapata matatizo katika ajira zao au shughuli mbalimbali za kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamekuwepo na tatizo la vyeti vya baadhi ya vyuo vyetu (certificates) kutotambulika katika nchi za nje, hali ambayo inasababisha usumbufu katika ajira kwa Watanzania waliopo nje. Mfano, Dar es Salaam Maritime Institute Certificates, hazitambuliwi Kimataifa kwa mujibu wa taarifa nilizopata toka kwa Watanzania, mabaharia wanaofanya kazi katika nchi za ng‟ambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ihakikishe inavitangaza vyuo vyetu Kimataifa kwa kufuata taratibu za Kimataifa ili vitambulike katika medani za Kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yetu kufanya taratibu ya kuondoa visa na kutumia entry katika nchi za Nordic United Arab Emirates, United Kingdom, German and Northern America. Hii itasaidia Watanzania wengi kupata fursa za kibiashara na kielimu, hali itakayowezesha Watanzania wengi pia kupata ajira na wale wenye vipaji vya michezo mbalimbali. Pia wataweza kuionesha dunia kuwa Watanzania wanaweza na wao pia watapata ajira. Mfano, wachezaji wa basketball, football, golf, tennis, athletics na kadhalika.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kukutana ili tuzungumze masuala ya nchi yetu. Vilevile nichukue fursa hii nikiungana na wenzangu waliotangulia kuchangia Kamati ya LAAC na PAC.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukumbusha tu kwamba Serikali za Mitaa zipo kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni. Hata hivyo, taarifa ya Kamati pamoja na kuandikwa vizuri kuna baadhi ya maeneo kuna upungufu. Labda nisema katika Halmashauri zetu kumekuwa matatizo ya matumizi mabaya, lakini Kamati imetupa taarifa ya baadhi ya maeneo yaliyochambuliwa kwa mfano katika uchambuzi wa taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014 na 2014/2015 na kuonesha hesabu zake zina matatizo katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano, katika matumizi yasiyozingatia Sheria za Manunuzi, hapa kuna upungufu mkubwa kwa sababu Sheria za Manunuzi hazifuatwi na matokeo yake baadhi ya bidhaa au huduma zinazotolewa katika Halmashauri zinakuwa chini ya kiwango au nyingine haziridhishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, mfumo uliopo sasa hivi katika Halmashauri zetu ambapo Madiwani wametolewa katika ile Tender Board na kuachwa watendaji peke yao ndiyo wanaofanya shughuli za manunuzi, naona huu ni upungufu, naishauri Serikali iliangalie upya suala hili kwa sababu watendaji wanapobaki peke yao huku tukiambiwa kwamba Madiwani ndiyo jicho la Serikali katika Halmashauri, wao wanafanya wanavyotaka, wanatoa zabuni kwa watu wanaowataka, matokeo yake sasa ama bidhaa au huduma zinazotolewa zinakuwa chini ya kiwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna upungufu katika kutekeleza mapendekezo ya Kamati kwa kipindi kilichopita na pia kutojibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Lingine kuna usimamizi mbovu katika kupeleka au kutokukamilika kwa miradi au miradi inakuwa chini ya kiwango. Vilevile katika Halmashauri kuna taratibu zilizofanyika za kuzinyang‟anya Halmashauri makusanyo ya property tax.
Kwa maoni yangu naona hili ni tatizo kubwa sana kwa sababu Halmashauri zilikuwa zikitegemea sana property tax kama chanzo chake kikubwa cha mapato. Leo Halmashauri zimenyang‟anywa kukusanya property tax imepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA). Kwa mfano, hata Halmashauri yetu ya Jiji la Tanga ilikuwa na nyumba za kupangisha (quarters) pia zimeingizwa katika ukusanyaji wa TRA. Mimi naliona hili ni tatizo au Serikali itueleze kama imeamua kuziua Halmashauri kwa kifo cha kimya kimya (silent killing). (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Leo Halmashauri zinahudimia wananchi ikiwa ni moja ya majukumu yake, kuna zahanati, shule, barabara, mifereji na usafi wa miji, unapozinyang‟anya vyanzo vya mapato shughuli hizo zitafanyikaje bila fedha?
Mimi nashauri ikibidi Halmashauri zirudishiwe kufanya mapato au kama Serikali imeona property tax ni chanzo ambacho inastahili kupata Serikali Kuu basi irudishe vyanzo vingine ambavyo ilizinyang‟anya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwenye suala la Serikali za Mitaa, Serikali nayo inahusika moja kwa moja kuziwezesha Halmashauri ili ziweze kutenda shughuli zake vizuri lakini Halmashauri zimenyang‟anywa uwezo wake. Hata katika kitabu chetu hiki kuna miradi ambayo imefanywa chini ya kiwango au haijatekelezwa. Kwa mfano, mradi wa maji katika Kijiji cha Kayanze, Jijini Mwanza wenye thamani ya shilingi 618,704,554 haujatekelezwa. Pia kuna mradi wa maji wenye thamani ya shilingi 5,049,000,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji nao pia haukutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia kwa kusema miradi ya maji itekelezwe.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naomba nichangie kwa maandishi katika Mpango wa 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mizigo kupungua Bandari ya Dar es Salaam; mizigo imepungua kutokana na urasimu au wizi wa mizigo ya wafanyabiashara na kodi kubwa kuliko thamani ya mizigo tofauti na bandari ya Mombasa - Kenya; Beira Port - Mozambique; Durban Cape town na Port Elizabeth za Afrika ya Kusini. Bandari nne za Tanzania ni sawa na mapato ya bandari ya Mombasa, Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri; Mamlaka ya Bandari (TPA) isifanye kazi kimazoea (business as usual) ifanye kazi kiushindani, iondoe urasimu katika utoaji mizigo; mizigo iweze kutolewa katika muda mfupi (min – 24 hours – max 72 hours).
Mheshimiwa Naibu Spika, ili bandari zote za Tanzania zifanye kazi kwa viwango vinavyokusudiwa, mizigo ifanyiwe classification. Aina ya mizigo ya Mikoa; Kanda ya Kaskazini- Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Mwanza na Kagera, mizigo ishushe katika bandari ya Tanga. Mizigo ya Mikoa ya Kanda ya Kati- Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Tabora, Singida, Shinyanga na Kigoma, mizigo ishushwe katika Bandari ya Dar es Salaam; meli nyingi zinatumia muda mrefu katika Bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, mizigo ya Mikoa ya Kanda ya Kusini (Southern Regions) Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Rukwa, na Katavi, mizigo ishushwe katika bandari ya Mtwara. Hii iangalie pia shehena ya mizigo ya Kimataifa na izingatie hali ya kijiografia (Geographical Conditions). Mfano, mizigo ya Burundi, Rwanda, Uganda na Sudan Kusini ishushwe bandari ya Tanga na mizigo ya Malawi, Zambia na Congo, ishushwe bandari ya Mtwara na Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, inatia huzuni kuona au kusikia kuwa katika Bank Economic and Investment Report kuwa, katika nchi 140, Tanzania inashika nafasi ya 120 huku tukiwa na rasilimali na malighafi nyingi tofauti na nchi nyingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, TRA na Mapato; pamoja na taarifa ya ukusanyaji mkubwa wa mapato unaofanywa na TRA, lakini wafanyabiashara wanakamuliwa sana, wanafanyiwa makisio (assessment) makubwa kuliko faida inayopatikana katika biashara zao. Matokeo yake, wafanyabiashara wengi wanafunga biashara zao au viwanda vyao. Wengine wanadiriki kuhamia nchi jirani za Burundi, Rwanda, Mozambique, Uganda, Kenya na Sudan Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati TRA inaongeza mapato ya Serikali, lakini inaua biashara na kuzorotesha uchumi wa nchi yetu. TRA inakamua ngo‟mbe maziwa hadi anatoa damu bado TRA inakamua tu! Nashauri TRA ifanye utafiti na uchambuzi ili ijue kwa nini wafanyabiashara wanailalamikia TRA na ikibidi itumie Demand Law System.
Mheshimiwa Naibu Spika, Third Law of Demand; in the high price low demand and in the low price high demands. Maana yake, kodi ikiwa kubwa walipaji watakuwa kidogo na kodi ikiwa ndogo walipaji watakuwa wengi. Wahindi wanasema, „dododogo bili shinda kubwa moja‟.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupeleka property tax kukusanywa na TRA ni kuzuia Halmashauri zetu nchini. Je, Mheshimiwa Waziri Mpango, Serikali imeamua kuziua Halmashauri kwa kuwa vyanzo vyake vikuu vyote vinatwaliwa na TRA? Tanga City Council imenyang‟anywa hadi nyumba za kupangisha! Naomba Serikali irudishe property tax itwaliwe na Halmashauri zetu. Tanga City Council irudishiwe nyumba zake na kupangisha. Zipo Serikali za aina mbili, Central Government and Local Government hivyo, tusizinyong‟onyeze Local Government.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ya Viwanda; viwanda vinahitaji umeme wa uhakika, vingi vimekufa au kuuzwa na Serikali. Ushauri; Serikali ifufue viwanda vilivyokufa kwa kuweka mitambo mipya. Mfano, Steel Rolling Mills, Sikh Saw Mill, Kamba Ngomeni na kadhalika katika Mkoa wa Tanga; General Tyres - Arusha; na Kiwanda cha Nyuzi, Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kilimo, Mifugo, Michezo na Uvuvi vyote vinahitaji kuboreshwa na kutekelezwa kwa vitendo.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami kwanza nichukue fursa hii kushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia na nitaanza na TAMISEMI. Kwa mujibu wa taratibu zilizopo Serikali zipo za aina mbili, kuna Central Government na Local Government, lakini sasa kuna kitu au utaratibu ambao umeanzishwa wa kuondoa makusanyo ya property tax ambacho kilikuwa ni chanzo cha mapato katika Halmashauri zetu tumekipeleka katika Serikali Kuu kwa kukusanywa na TRA. Naona hili ni kama kuzizika Serikali za Mitaa, kwa hiyo nakumbusha kwamba Serikali za Mitaa ndizo zinazoziba aibu ya Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na miradi mingi ambayo inatekelezwa na Serikali za Mitaa, kwa mfano uchongaji wa barabara za vijijini, miradi ya maji vijijini, pamoja na kwamba inapelekewa fedha na Serikali Kuu lakini bado wenye mamlaka ya kusimamia ni Serikali za Mitaa. Sasa kuzinyang‟anya Serikali za Mitaa chanzo hiki cha property tax ni kuziua Serikali hizo. Kwa hiyo, nashauri kwamba ikibidi property tax irudishwe katika Serikali za Mitaa kama kweli tunataka miradi ya wananchi inayofika moja kwa moja katika Halmashauri zetu iweze kusimamiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala zima la mapato, leo ukienda kwenye Halmashauri zote zipo hoi kimapato, baada ya kunyang‟anywa chanzo kile zimekuwa kama zimechanganyikiwa, zimekuwa zikitegemea tu kupata ruzuku kutoka Serikali Kuu ambayo nayo inacheleweshwa, inaletwa katika robo ya mwisho ya Mwaka wa Fedha wa Serikali, matokeo yake sasa inafanywa miradi kwa kukurupuka, miradi mingi inakuwa chini ya viwango na hapohapo pia ndipo watu wanapopiga „dili‟. Nashauri bado tuzitazame sana Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukumbuke pia Serikali za Mitaa kama alivyotangulia kusema mmoja imekuwa ni kama jalala, mizigo yote imesukumwa kwenye Serikali za Mitaa; elimu ya msingi na sekondari zinasimamiwa na Serikali za Mitaa, miradi ya maji vijijini inasimamiwa na Serikali za Mitaa na miradi mingine ya afya bado inasimamiwa na Serikali za Mitaa. Hata hivyo, tukija kwenye elimu kwa mfano, elimu kwa mujibu wa utaratibu siyo biashara ni huduma, lakini kuna utaratibu ambao umeanzishwa tena wa kukusanya mapato kutoka kwenye hizi English Medium Schools, matokeo yake sasa wamiliki wa shule nao kwa kuwa wanatozwa fedha nyingi, wanaongeza ada matokeo yake wananchi au wazazi wanashindwa kuwapeleka watoto katika hizi shule za English Medium. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, ikibidi tuondoe hii tozo ya kodi katika hizi shule za English Medium, vilevile pia hata kwenye sekondari. Tunasema hapa elimu bure lakini ukiangalia, kwa mfano katika sekondari kumesamehewa sh. 20,000 tu ya ada, vikorombwezo vyote bado mzazi anatakiwa kulipia, tena baya zaidi kunatakiwa counter books, counter book moja sh. 5,000 mtoto anatakiwa atumie zaidi ya counter books 12, hapohapo tena kuna nguo za michezo, kuna uniform, viatu pair mbili, majembe, tumewasaidia tu kuondoa hilo suala la madawati baada ya fedha iliyobaki katika Bunge kuingiza fedha hiyo kwenye madawati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Halmashauri napo labda nimpongeze tu Mheshimiwa Rais kwa hili suala la kumaliza tatizo la madawati lakini bado elimu bure siyo bure. Katika baadhi ya shule wanashindwa hata kulipa walinzi, wanashindwa hata kulipa maji, wanashindwa hata kulipa umeme! Hebu fikiria watoto wanashinda kutwa nzima lakini maji yamekatwa, yote hii inatokana na kutamka kwamba elimu itakuwa bure lakini siyo bure kwa asilimia mia moja. Nashauri Serikali kama tumeamua elimu iwe bure basi iwe bure kwelikweli kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kingine pia naishauri Serikali, TAMISEMI haina uwezo wa kulipia maji na umeme katika shule zetu za sekondari, sasa ikibidi shule za sekondari, shule za msingi, taasisi za kidini kama makanisa na misikiti, hili naona pia tungeondoa kabisa hilo suala la kuzichaji masuala ya bili ya umeme na maji tusiwe tumependelea, ili taasisi na shule hizi ziwe zinatumia maji pasipo malipo, tutasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida kwamba hata inapotokea kukiwa na majanga tunatumia viongozi wetu wa kidini kumwomba Mwenyezi Mungu aisalimishe nchi yetu na majanga na matatizo mengine sasa je, tunasaidiaje taasisi za kidini. Nashauri kupitia shule za msingi na sekondari pamoja na taasisi za kidini hizi tuondoe haya masuala ya malipo ya maji na umeme ili kama tunasema elimu bure iwe elimu bure kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika elimu natoa ushauri hata shule za private za sekondari tumekuwa tunawatoza kodi kubwa sana, matokeo yake na wao wanaongeza school fees ambayo imekuwa sasa ni kilio kwa wananchi. Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakuwa ni mashahidi, kila Mbunge hapa ana orodha ya watoto siyo chini ya 20, wote wamefaulu wazazi hawana uwezo unatakiwa Mbunge uchangie, utachangia watu wangapi? Naishauri Serikali elimu iwe bure kama katika baadhi ya nchi za wenzetu, wenzetu wanawezaje sisi tushindwe, upo usemi unaosema wao waweze wana nini, sisi tushindwe tuna nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala zima la Katiba na Sheria; mimi niliipitia taarifa hii lakini kuna baadhi ya maeneo naomba yafanyiwe marekebisho kidogo, kwa mfano, Waheshimiwa Wabunge wenzangu watakuwa mashahidi, sote katika Wilaya zetu kuna Magereza, ukiwa ni mwenyeji wa kutembelea Magereza utakuta kuna akinamama ambao wana watoto wachanga wananyonyesha. Mama ndiye amefanya kosa labda ameiba, labda amefanya kosa lingine huko ametiwa hatiani, lakini mtoto mchanga anayenyonyeshwa ambaye hawezi kuishi bila mama yake inabidi naye ageuke mfungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naishauri Serikali, kwa wale akinamama ambao wengine ni wajawazito wanajifungulia kule gerezani, lakini na kwa wale akinamama wote ambao watakuwa wana watoto wachanga, hawa watoto dini zote zinaamini kwamba mtoto mdogo kuanzia miaka 14 kuja chini ni malaika, kwa nini tumtese malaika huyu akae gerezani hali ya kuwa yeye hakufanya kosa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, kama mama ana mtoto mchanga basi ama asamehewe apewe kifungo kile cha kufanya kazi za kijamii kama kusafisha hospitali, ofisi ya Mkuu wa Mkoa au Mahakama, lakini kitendo cha kuwafanya watoto wachanga wawe wafungwa, hawapati haki za watoto za kucheza na watoto wenzao, hawapati muda wa kujinafasi, lakini pia mama zao wanakuwa wanyonge wanaona kwamba mimi nimekosa, mtoto wangu naye anafungwa amekosa nini. Naishauri Serikali tuangalie mtindo mwingine wa kuwafikiria hawa watoto ambao mama zao wamekuwa wafungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Sheria na Katiba kuna kipengele hiki tumekipitisha hapa cha kwamba wasaidiwe wale wasiokuwa na uwezo. Mimi naomba hili jambo kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria tuliangalie vizuri, kwa sababu ni watu wengi ambao wana kesi hawana uwezo wa kuweka Mawakili, vilevile pia kuna suala zima la ajali. Nchi nyingi zilizotuzunguka inapotokea ajali wahanga wa ajali wanaokufa ama wanaopata vilema vya maisha, utaratibu katika baadhi ya nchi Mawakili wa Kujitegemea wanakwenda hospitalini au wanakutana na familia za wale wahanga wanaweka makubaliano, kwamba kwa sababu mtu wenu amefariki, ameacha wajane na watoto yatima, sisi tutaisimamia kesi ya compensation, kwamba huyu mtu alipwe fidia ili aweze kusomesha watoto wake ambao wamebaki yatima au kama ana mjane au wagane waweze nao kupata haki yao ya malipo yanayotokana na insurance, lakini nchini kwetu…………
MWENYEKITI: Ahsante.