Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Ally Yusuf Suleiman (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. DKT. SULEIMAN A. YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanah Wataala na kumsalia Mtume wake Muhammad Swallalahu Alayhi Wassalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu naanza kwa masikitiko makubwa kwamba alipokuja Waziri nilidhani anakuja kutuambia kwamba elimu yetu imekwama na kutufahamisha njia ambazo tutakwamuka, lakini badala yake Waziri amekuja hapa, akaja na majibu ya maswali ya kawaida, ukweli hicho si sahihi. Hata hivyo, kwa upande mwingine namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati, ukweli namfahamisha Waziri kwamba atupe zile karatasi zake achukue ushauri wa Kamati, ni mzuri na utamwelekeza pazuri pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, naanza mchango wangu kwa kutoa ushauri, nasema kwamba, elimu hapa kwetu imekwama na nadhani Wizara ya Elimu inajua vizuri sana kwamba elimu kwetu imekwama, lakini hatujui ni namna gani tujikwamue kutoka hapo tulipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa tunalolifanya hapa kwetu la kusababisha elimu ikawa duni na haina thamani ni kwambakatika udahili tunachukua wanafunzi ambao wame-fail fani nyingine, wameshindwa, tunawachukua wale ndiyo tunawapeleka kwenye ualimu. Tunapanda mbegu mbovu, tunategemea tupate matunda gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ili tufanikiwe tuwe na elimu yenye thamani, tuchukue wanafunzi ambao wame-pass vizuri sana kuanzia O-level mpaka kufikia A-level na tuwashawishi namna gani ya kuwashawishi hawa, tunaweza kuwashawishi kwa kuwapa mishahara minono kama mishahara ambayo tunawapa Madaktari na fani nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukwambia kwamba hakuna mtu ambaye ni muhimu baada ya mzazi kuliko Mwalimu. Ndiyo sababu tunapokuja katika ulinganisho, tunasema nani ambaye ni bora Mwalimu ama mzazi. Husemi Mwalimu au Dokta, husemi mzazi au Daktari, husemi mzazi au Mwanasheria bali ni Mwalimu pamoja na mzazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fani zote ni muhimu, lakini fani ya ualimu ni muhimu zaidi. Ukitaka kuwa Rais ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka kuwa Waziri Mkuu ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka kuwa Spika, ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka uwe Mwenyekiti wa Bunge, ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitana uwe Mbunge ni lazima uende kwa Mwalimu, ukitaka Ukurugenzi, ni lazima uende kwa Mwalimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mwalimu ni mtu muhimu kupita kiasi na ndio sababu mshairi mmoja wa Kiarabu anakwambia kumli lmuallimi wafii ttamijina kaadha lmuallimu an-yakuna rasula, alimta akrama au ajalla mina lladhi yubni, wayunshiu jabni, wayunshiu anfusan waankula. Anakwambia msimamie mwalimu na mtukuze kwa hali yoyote ya utukufu, kwa sababu Mwalimu anakaribia kuwa Mtume. Je, unamjua mkaribu zaidi na mtukufu zaidi kuliko yule ambaye anajenga nafsi za watoto na akili zao, kuna mtukufu kuliko huyo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo la kwanza hilo kama tunataka tufanikiwe katika elimu tuchukue wanafunzi waliokuwa bora kwa kuwapa mishahara minono Walimu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili hapo hapo kwa Walimu kila siku tunazungumzia upungufu wa Walimu katika vijiiji, kuna shule zina Walimu wawili, kuna shule zina Walimu watatu, jamani sababu yake mnajua. Sababu yake ni kwamba kule vijijini mazingira ni mabovu, kwa hivyo, Mwalimu anapopelekwa kijijini, huyu ni kama anaadhibiwa. Ili kuwafanya Walimu wakae vijijini, ni muhimu sana hawa tukawazidishia mishahara kwanza, halafu kuna posho ya mazingira magumu, ni lazima tuwape. Mahali hakuna barabara, hakuna umeme, hakuna kilichopo, hata kuja mjini ni matatizo, ni lazima tuwanyanyue, tuwape hadhi nzuri hawa ili waishi maisha yaliyokuwa bora kule shamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo lakini nataka nisizungumze upungufu wa Walimu vijijini tu, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, atueleze ni Walimu wangapi ambao hivi sasa tunao, hitajio letu ni Walimu wangapi kwa jumla na upungufu wa Walimu tulionao. Pia atueleze ni jitihada gani ambazo Wizara inachukua ili kuhakikisha kwamba tunaziba lile gape lililopo, nataka akija hapa atujibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo naelekea katika masuala ya elimu kwa upande wa Zanzibar. Nataka Mheshimiwa Waziri pia atakapokuja hapa anifahamishe ni nini maana ya elimu ya juu, maana yake nashindwa kuelewa elimu ya juu ni ipi, kwa sababu gani? Kwa sababu leo tunakuta mitihani ya form four, mitihani ya form six, Zanzibar inafanywa mitihani kutoka bara na nijuavyo mimi A-level na O-level sio elimu ya juu, siyo mambo ya Muungano, ni kwa nini vijana wale wanafanya mitihani kutoka hapa, wakati hata mitaala inatungwa hapa na mara nyingine inachelewa kufikishwa kule, kadhalika inaweza ikapita miezi sita kabla ya kupewa elimu ya mitaala ambapo hapa Bara tayari wanakuwa watu wameshapatiwa elimu hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unategemea wale vijana mitihani waifanye vipi kama ni kusema kwamba, wanataka tuwasaidie, ikiwa wanataka kusaidiwa kule Zanzibar hata mtihani wa form four na form six naiambia Serikali ya Zanzibar haifai ikae chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu masuala madogo madogo kama hayo ni masuala ya mtu kufanya mwenyewe, kwa hiyo, kama hawayawezi basi wakae pembeni wampe mtu ambaye wanamjua ambaye ni Maalim Seif. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika nataka kujua haki ya Wazanzibar katika mikopo ya elimu ya juu. Kwa sababu elimu ya juu ni suala la Muungano, lakini mpaka dakika hii Wazanzibar hawajui haki yao ni ipi katika mkopo ule bali wanachotewa kama watu waliokuwa wanafadhiliwa tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunafanyiwa vitendo kama hivyo! Nataka atakapaokuja hilo pia anijibu. Nimetoa baadhi ya ushauri na kwa sababu muda umekwenda sana lakini sidhani kama ushauri huu utafanya kazi na sababu kubwa nahisi kwamba Mheshimiwa Waziri kavishwa koti ambalo limemzidi kimo, koti alilovalishwa ni kubwa sana.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa Waziri alikuwa Katibu Mtendaji wa NECTA. Lakini akafukuzwa kwa kushindwa kazi leo, ghafla anaibuka eti ni Waziri, ni mkombozi huyo, atatukomboa kitu gani! Wanasema waarabu faqidu shei la yuutwi (aliyekuwa hana hawezi kutoa) na yeye ikiwa kashinda pale padogo hapa pakubwa hapawezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naam halafu kaja tu anafanya mambo Mheshimiwa Waziri kwa kukurupuka anatusifu...
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Suleiman, umemaliza muda wako.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu-Wataala kwa kunipa afya njema na kuwepo hapa leo, na namswalia Mtume Mohamad Swalallahu Alayhi Wassallam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, mimi nina mambo machache sana tu ya kuzungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, kila matokeo ya form four na form six yanapokuja kwa upande wa Zanzibar inakuwa ni vilio tu, hakuna vicheko kabisa kabisa. Tukiziangalia katika shule ambazo zinashika mkia zile shule 10 bora zinazoshika mkia basi kati ya sita mpaka saba zinatoka Zanzibar.

Mheshimia Mwenyekiti, tunataka kujiuliza Wazanzibar kwa nini kila siku tunafanywa kuwa watu wa daraja la pili? Ni kwa nini inakuwa hivyo? Na ikiwa masuala ya elimu ya juu ni masuala ya Muungano, naiuliza Wizara ni jitihada gani ambayo inachukua kuweza kuisaidia Zanzibar kuepukana na udhaifu ulio mkubwa kiasi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nijue hivi katika Bodi ya Mitihani, katika Bodi ya Wakurugenzi ile Bodi ya Mitihani kweli tuna wawakilishi kutoka Zanzibar pale? Mara nyingine inawezekana sababu ya udhaifu huu ni kwamba hakuna watu ambao wanaweza wakaishauri bodi vizuri katika masuala ya Zanzibar. Nataka Waziri aje anieleze kweli tunao watu pale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ninataka nilijue kwa kifupi tu ni suala la mikopo. Bodi ya Mikopo imekuwa siku zote ikitoa mikopo kwa upande wa wanafunzi wa Zanzibar. Lakini mpaka hivi sasa hatujui haki ya Zanzibar katika mikopo ile ni kiasi gani. Wazanzibari ni asilimia ngapi tunapata? Kwa sababu tukijua hili itasaidia kuondoa yale malalamiko ambayo yako kwa wanavyuo wa Zanzibar kwamba Wazanzibari hatupendwi, Wazanzibari tunadhulumiwa. Hebu tuambieni Mheshimiwa Waziri, ni asilimia ngapi, tunataka kujua asilimia yetu katika Bodi ya Mikopo ni kiasi gani ili kuondosha haya malalamiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia Mheshimiwa Waziri atakapokuja atufahamishe kati ya wanafunzi 122,623, Wazanzibari wangapi ambao wanapata mikopo miongoni mwao? Kati ya hao Wazanzibar ni wangapi? Kadhalika kuna wanafunzi 350 ambao wanasomeshwa nje kwa kupewa mikopo, nataka nijue kati ya hawa 351 Wazanzibar ni wangapi ili tujue haki yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala dogo pia nataka nilijue, ni kwa nini Wazanzibari hawapati grade A katika hii mikopo, wote ni B, C na kwenda chini. Ni kwa nini Wazanzibar hawapati nafasi hiyo ya kuwa full sponsored badala yake ni wa upande mmoja tu ndio ambao wanapata? Nataka uje unijibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda haraka haraka tukija upande wa TCU. Upande wa TCU umeandika kwamba katika kazi zake ni kuhakiki ubora wa elimu na kuidhinisha programu zifundishwazo. Nataka kujua ni kwa nini TCU au TCU imeona nini katika elimu za dini? Elimu za dini hapa nijuavyo zinasomeshwa katika Chuo cha Muslimu University (MUM) na pia kinasomeshwa katika Chuo cha Abdulrahman Sumait kule Zanzibar. Lakini hawajaidhinisha chochote ni udhaifu gani waliouona au ni kitu gani kibaya… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu Subhannahu Wataalah aliyeniweka hai mpaka leo nimefunga Ramadhani, nimemaliza sita, kwa hivyo leo ni sikukuu kwangu Alhamdulillah. Pili namswalia Mtume Muhammad (Swalallah alayh wasalaam).

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sana nitakuwa ni mtu mwenye kushangaa shangaa lakini wewe usishangae. Jambo la kwanza ambalo linanishangaza sana ni kuangalia pande mbili za Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika kwa upande mmoja, lakini upande wa pili tuangalie Zanzibar na nchi zote za Afrika Mashariki huo ni upande wa pili. Kipi cha kuangalia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tumeshuhudia kwamba bajeti za nchi za Afrika Mashariki zimesomwa siku ya Alhamis tarehe 14 Juni, 2018, lakini Bajeti ya Zanzibar imesomwa juzi tarehe 20/6/2018 hii ni kwa sababu gani? Je, Zanzibar haimo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki au vipi? Kwa nini Zanzibar inabaguliwa kiasi chote hiki. Sababu tunaijua, sababu ni kwamba kwanza ni lazima Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa upande wake awasilishe Wizara yake ijulikane marekebisho ya kikodi ndiyo baada ya hapo Zanzibar nayo waige, wafuate mfumo ule. Kwa hivyo, haiwezekani kabisa kabisa kwa Zanzibar kusoma bajeti siku moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baya zaidi ni kwamba kwa kawaida Bara huwa wanaunda vikosi kazi vya kushughulikia mambo ya kikodi na mambo ya kibajeti. Wakishamaliza wenyewe kwa wenyewe ndiyo wanaalika wadau kwa jumla waje na wao watoe maoni yao ikiwemo Zanzibar inaalikwa kama mwalikwa wa kawaida tu na siyo kama mshiriki wa Muungano. Ni kwa nini Zanzibar inafanyiwa hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka atakapokuja Mheshimiwa Waziri atueleze ni kwa nini Zanzibar isishirikishwe katika vikosi kazi badala yake ibaguliwe kiasi kikubwa namna hiyo. Kwa sababu kama tunakumbuka mwaka 1985, Zanzibar na Bara walipitisha bajeti siku moja. Bara wakashusha kodi, Zanzibar wakapandisha ikalazimu Zanzibar iitake Bara ilipe tofauti na ikalipa tofauti. Je, wanataka tuendelee na hali hiyo? Hakuna haja, tushirikiane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili Serikali iliunda Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa Ibara ya 133 ya Katiba kupitia Sheria Na. 15 ya mwaka 1984 ili kila upande usimamie uchumi wake na masuala ya Muungano pia yasimamiwe na shughuli za Muungano. Ni miaka 34 tokea Tume hii ilipoundwa mpaka leo hii nilijibiwa wiki mbili zilizopita na Waziri wa Fedha kwamba akaunti hii haijafunguliwa miaka 34. Waziri atakapokuja jambo la kwanza atuambie hii akaunti itafunguliwa lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linatuonesha ni vipi Serikali ya Muungano ilivyokuwa haina nia njema kwa Zanzibar, kabisa. Serikali ya Muungano haina nia njema kwa Zanzibar kwa sababu kwa kuunda Tume hii au kwa kuunda akaunti hii matatizo mengi sana ya kifedha, ya kikodi yangelikuwa yametatuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uwoga huo wa Serikali tumeshindwa kuelewa mambo mengi sana kwa mfano, hivi sasa hatujui mahitaji halisi ya Muungano ni kiasi gani, matumizi ya Muungano hatujui ni kiasi gani, hatujui mchango wa kila upande katika Muungano ni kiasi gani, pia hatujui hata kodi zipi ni za Muungano, kodi zipi siyo za Muungano, nia njema haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, study iliyofanywa na PriceWaterHouseCoopers imeonesha kuwa vyanzo vya mapato vyenye vinasaba vya Muungano kwamba vyanzo hivyo vinatosha kabisa kuendesha Muungano kwa mambo ambayo ni ya Muungano. Pia pande mbili za muungano zikabakiwa na vyanzo vya kutosha kwa ajili ya kujiendesha kila upande.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya mfuko huo mpaka leo hii haujaanzishwa na wala nia haipo, tunaambiwa tu kwamba majadiliano yanaendelea. Miaka 34 majadiliano hayajakamilika, hebu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie tumpe miaka hamsini na ngapi tena ili akaunti hii ya pamoja ianzishwe. Nataka kusema kwamba kama wanataka kujua kero za Muungano, basi hii ni kero mama katika kero za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa kweli nashangaa tena na napata mashaka makubwa sana juu ya nia ya Tanganyika kwa Zanzibar. Najiuliza ni faida zipi hasa za kiuchumi ambazo Zanzibar zinapata kutokana na Muungano huu kwa sababu jambo lolote ambalo ni la Zanzibar, Bara halitakiwi. Sukari ya Zanzibar imekataliwa, ukileta bidhaa kutoka Zanzibar tunaambiwa kwamba tulipie kama vile bidhaa inatoka Dubai. Jamani huu Muungano uko wapi? Muungano uko wapi ndugu zangu nataka kulijua hilo mnieleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha sana hata lile ambalo ni haki ya Zanzibar, hatupewi, kwa mfano katika suala la uajiri ni asilimia 79 Bara, asilimia 21 Zanzibar, hata hili halijatekelezwa mpaka leo hii, lini tuambie litatekelezwa suala hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yote yenye maslahi na Zanzibar basi tunanyang’anywa. Leo hii tumeambiwa kwamba usajili wa meli tunataka kunyang’anywa, jamani! Mnatutakia nini Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nizungumze kidogo tu Kisiwa cha Fungu Mbaraka au kinaitwa Latham Island. Latham Island imepandishwa bendera ya Zanzibar pale tarehe 19 Oktoba, 1898, tokea wakati huo kisiwa hiki ni milki ya Zanzibar na hata siku moja bara haijawahi kusema kwamba ni chao, lakini waliposikia pale kwamba kuna block ya mafuta wamekuja mbio kwamba hiki kisiwa ni chetu. Nawa-challenge Mawaziri wote waliopo hapa waje hapa watuambie ni lini Bara imemiliki Kisiwa cha Latham Island, wote nawa-challenge waje hapa waniambie, lini wamekimiliki kisiwa hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bara zipo fursa nyingi sana. Tanzania Bara kuna madini, mbuga za wanyama, kilimo, mifugo na gesi, Zanzibar hakuna chochote lakini inapotokea tundu moja tu kidogo kwamba kuna heri inataka kuja haraka wanakwenda kuiziba, tukiuliza jamani kulikoni, wanatuambia atakayeuchezea Muungano tutapambana naye kwa thamani yoyote. (Makofi)

Ahsante.