Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Ally Yusuf Suleiman (7 total)

MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazo Mahakama Kuu mbili, ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar.
(a) Je, ni Mahakama ipi ipo juu ya nyingine?
(b) Je, kuna utaratibu gani wa ushirikiano katika kusimamia kesi au mashauri ambayo yanaanzia upande mmojawapo wa Muungano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 108 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, kwa mujibu wa Muundo wa Mahakama katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna Mahakama ya Zanzibar iliyotamkwa katika Ibara 114 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 93 ya Katiba ya Zanzibar. Mahakama zote tajwa zina hadhi sawa katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, upo ushirikiano katika masuala ya utekelezaji wa amri za Mahakama katika suala linaloanzia upande mmoja wa Muungano ambalo limeshughulikiwa na kufikia mwisho. Ingawa kama ilivyoelezwa hapo juu, kila Mahakama ina hadhi sawa na nyingine na hivyo shauri lililoanza kusikilizwa upande mmoja, haliwezi kuhamishiwa upande wa pili ili kukamilisha usikilizwaji wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, shauri likianza kusikilizwa, linapaswa kusikilizwa na kuhitimishwa na Mahakama Kuu ya upande husika wa Muungano.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-
Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kuna watu kadhaa ambao wamekuwa wakikamatwa na Jeshi la Polisi Unguja na Pemba huku baadhi yao wakifunguliwa mashtaka na wengine kuachiwa:-
(a) Je, ni kwa nini Jeshi la Polisi linashindwa kufanya kazi kwa weledi na kukamata watu pasipo ushahidi kwa lengo la kukomoa tu?
(b) Ili kulisafisha Jeshi la Polisi, je, Serikali haioni haja ya kuwawajibisha watendaji ambao wenye tabia ya kuwakomoa wananchi kwa kuwakamata pasipo ushahidi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Polisi ni chombo kilichoundwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria na linatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kanuni na taratibu zilizopo, jukumu lake kuu likiwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Jeshi la Polisi limepewa mamlaka ya kisheria ya kukamata, kuhoji na kuweka watuhumiwa mahabusu kwa muda ulioruhusiwa kisheria endapo itabainika kuwa kuna viashiria au taarifa ya kuhusika katika kutenda kosa la jinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria na kanuni na taratibu za utendaji zinazoongoza Jeshi la Polisi linapobainika askari amebambika kesi kwa sababu zozote zile huchukuliwa hatua mbalimbali za kinidhamu ikiwamo kufukuzwa kazi.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-
Serikali iliunda Akaunti ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa Ibara 133 ya Katiba kupitia Sheria Na.15 ya Mwaka 1984 ili kila upande usimamie uchumi wake na uchumi wa Muungano usimamiwe na chombo cha Muungano:-
• Je, ni kwa nini miaka 33 sasa Akaunti hiyo haijafanya kazi yake?
• Je, gharama kiasi gani imetumika kuanzisha taasisi ambayo haina faida yoyote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Magogoni, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua uwepo wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha pamoja na Tume ya Pamoja ya Fedha. Ibara ya 133 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imebainisha sharti la kutungwa kwa sheria itakayoweka utaratibu wa uendeshaji wa Tume ya Pamoja ya Fedha pamoja na Akaunti ya Pamoja ya Fedha. Ili kutekeleza sharti hilo la kikatiba, Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha ya Mwaka 1996 (The Joint Finance Commission Act, 1996) na hivyo kuwezesha kuanza kazi kwa Tume ya Pamoja ya Fedha mwaka 2003.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa uendeshaji wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha umependekezwa kwenye ripoti ya mapendekezo ya vigezo vya kugawana mapato na kuchangia gharama za muungano iliyoandaliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha mwaka 2006. Hata hivyo, akaunti ya pamoja ya fedha haijaanza kufanya kazi kwa kuwa majadiliano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mapendekezo ya Tume hayajakamilika.
(b) Mheshimiwa Spika, tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2003 Tume ya Pamoja ya Fedha imekuwa ikiidhinishiwa bajeti yake na Bunge lako Tukufu kupitia bajeti ya Fungu 10, chini ya Wizara ya Fedha na Mipango. Katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2003/2004 hadi 2017/ 2018, Tume imeidhinishiwa bajeti ya Sh.31,971,490,663 kwa ajili ya uendeshaji na utekelezaji wa majukumu yake.
Mheshimiwa Spika, aidha, si kweli kwamba Tume ya Pamoja ya Fedha haina faida yoyote. Katika kutekeleza majukumu yake ya msingi, Tume imefanya stadi sita tangu kuanzishwa kwake kwa lengo la kutoa mapendekezo na ushauri katika eneo la uhusiano wa kifedha kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia, Tume ya Pamoja ya Fedha imeandaa rasimu ya Mwongozo wa Uendeshaji wa Akaunti ya Fedha ya Pamoja ambao unatarajiwa kutekelezwa mara majadiliano ya pande mbili za Muungano yatakapokamilika.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF) aliuliza:-

Zanzibar kwa namna ilivyo inahitaji uchumi wa Visiwa ambapo Bandari ni kitu cha lazima:-

Je, Serikali ya Muungano inaungaje mkono nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga Bandari kubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Bandari Na. 17 ya mwaka 2004 (The Ports Act No. 17), majukumu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ni kuendeleza bandari, kuendesha shughuli za bandari, kutangaza huduma za bandari na kushirikisha na kusimamia sekta binafsi katika uendelezaji na uendeshaji wa bandari.

Aidha, Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) lilianzishwa kwa Sheria ya Bandari ya mwaka 1997, Sheria hii ilifanyiwa marekebisho mwaka 2013. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, ZPC ina majukumu ya kuendeleza bandari, kuendesha shughuli za bandari na kutangaza huduma za bandari ndani na nje ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Nyongeza ya Kwanza imeorodhesha Mambo ya Muungano ambapo kipengele cha 11 katika orodha ya Mambo ya Muungano kinahusu Bandari, mambo yanayohusika na usafirishaji wa anga na posta na simu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo hayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya uendelezaji wa bandari nchini. Ushirikiano huo umedhihirika zaidi katika kupanga miradi ya kipaumbele na kutafuta fedha za uendeshaji wa miradi hiyo kutoka vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Washirika wa Maendeleo. TPA na ZPC zimeendelea kushirikiana kwa utaalam na kushirikiana katika kutoa huduma za bandari nchini hususan katika uongozi wa meli kutoka nje ya nchi. Aidha, tunaendelea kuboresha ushirikiano kupitia vikao vya mara kwa mara vya Sekta za Uchukuzi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo hayo, Serikali ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiunga mkono nia ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga bandari kubwa ili kuimarisha miundombinu na huduma ya bandari nchini.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-

Ibara ya 130 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inataja kazi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, moja ya kazi zake ni kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa Haki za za Binadamu na ukiukwaji wa msingi ya utwala bora.

(a) Je, kwa nini ripoti za tume hiyo haziwekwi wazi kwa Umma?

(b) Je, Serikali haioni kuwa umefika wakati wa kujenga utamaduni wa ripoti hizo kujadiliwa Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf Mbunge wa Mgogoni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijalijibu Mheshimiwa Ally Yussuf, amesema wadhurumiwa wote kwa hiyo inawezekana hata yeye kuna ambao amewadhurumu lakini naomba nijibu swali kama alivyouliza maana hakuuliza hivyo huko nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli kwamba Ibara ya 130 ya katiba ya Jamhuri ya Muugano ikiosomwa kwa pamoja na sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya 2001) inaipa Tume mamlaka ya kufanya uchunguzi wa mambo yote yanayohusu uvunjwaji wa haki za binadamu, kifungu cha 28(1)(a) mpaka (f) cha sheria hiyo (Na. 7 ya 2001) kinafafanua kuwa, tume baada ya kufanya uchunguzi na kuthibitisha kuwepo kwa uvunjifu wa haki za binadamu itawaslisha taarifa na mapendekezo yake kwenye mamlaka kusika kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 33 (1) (a) –(c) cha Sheria Na. 7 ya 2001 kinaitaka Tume kuwasilisha taarifa yake ya mwaka katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Mawaziri kupitia wanaoshughulikia masuala ya haki za binadamu kwa Tanzania Bara na Zanzabar, hata hivyo, Tume imekuwa ikitimiza jukuu hilo kwa mujibu wa sheria. Aidha, hakuna sheria yoyote inayokataza taarifa za Tume kujadiliwa Bungeni endapo Mbunge ataona kama kuna jambo la kuibua kutoka kwenye taarifa iliyowasilishwa.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. DKT. SULEIMANI ALLY YUSSUF) aliuliza:-

Kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kumekuwa na ongezeko kubwa la makosa katika jamii jambo ambalo linasababisha mfumo wa utoaji haki pamoja na Mahakama kuelemewa.

(a) Je, kila Jaji au Hakimu anapangiwa kesi ngapi kwa mwaka ili kupunguza mlundikano wa kesi?

(b) Je, ni mambo gani kimsingi yanayosababisha mashauri kuchukua muda mrefu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleimani Ally Yussuf, Mbunge wa Mgogoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu ili kuhakikisha mashauri yote yanayofunguliwa Mahakamani yanamalizika kwa wakati. Utaratibu huu ni pamoja na kujiwekea malengo ya idadi ya mashauri yatakayoamuliwa na Jaji na Hakimu kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, malengo ni kuhakikisha tunapunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani ambapo kwa mwaka kila Jaji anatakiwa kumaliza mashauri 220; Mahakimu katika Mahakama za Hakimu Mkazi wa Wilaya kumaliza mashauri 250 na katika Mahakama za Mwanzo 260.

Mheshimiwa Spika, pia Mahakama imejiwekea ukomo wa muda wa mashauri kukaa Mahakamani. Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu ni miaka mwili; Mahakama za Hakimu Mkazi na Wilaya mwaka mmoja na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita. Mikakati hii imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri kwa kiasi kikubwa hususan kwa Mahakama za Mwanzo ambapo kwa sasa mlundikano wa mashauri ni asilimia sifuri.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo bado Mahakama zetu zimekuwa zinakabiliwa na changamoto za mlundikano wa mashauri na baadhi ya mashauri kuchukua muda mrefu zaidi. Changamoto hizi zimetokana na idadi ndogo ya Majaji na Mahakimu ikilinganishwa na idadi ya mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama zote nchini. Vilevile upelelezi katika Mahakama na mashauri kuchukua muda mrefu na mashahidi kutotoa ushahidi wao kwa wakati katika baadhi ya mashauri yanayofunguliwa katika Mahakama zetu nchini ni miongonzi mwa sababu na baadhi ya mashauri kuchukua muda mrefu Mahakamani. Hata hivyo ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa kuteuwa Majaji 11 wa Mahakama ya Rufaa na Majaji 39 wa Mahakama Kuu katika Awamu ya Tano, ahsante.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF aliuliza:-

Mfumo wa Mahakama umejiwekea utaratibu wa kuanza na kuamaliza mashauri ambapo kwa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu ni miaka miwili, Mahakama za Mahakimu Wakazi ni mwaka mmoja na Mahakama za Mwanzo ni mie zi sita. Utaratibu huu ni mzuri ambao unaendana na msemo usemao: “Haki iliyocheleweshwa ni sawa haki iliyonyimwa.”

Je, ni kwa nini utaratibu huu haufuatwi na badala yake kesi nyingi zinachukua muda mrefu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshi miwa Spika, n apenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ally Yussuf, Mbunge wa Magogoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mahakama ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha mashauri yote ambayo yanafunguliwa Mahakamani yanakuwa na muda maalum wa kukamilika katika ngazi husika za Mahakama kama yalivyo maelezo kwenye Swali la Msingi la Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huu kwa kiasi kikubwa umesaidia kupunguza changamoto ya mlundikano na mashauri kuchukua muda mrefu kusikilizwa. Pamoja na mfumo huu mzuri, bado kwa baadhi ya Mahakama utaratibu huu umekuwa haufuatwi kutokana na sababu mbalimbali kama idadi ndogo ya Majaji na Mahakimu ikilinganishwa na mashauri yanayofunguliwa Mahakamani, upepelezi kwa baadhi ya mashauri y a jinai kuchukua mud a mrefu, maahirisho ya mara kwa mara kutoka kwa Wadaawa wenyewe na sababu nyingine nyingi ambazo zinawagusa wadau wakubwa wa Mahakama katika uendeshaji wa mashauri.

Mheshi miwa Spika, itakumbukwa, w akati w a maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Sheria nchini Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ali ke mea ucheleweshwaji wa upelelezi katika mashauri mbalimbali na kutaka taasisi zinazohusika kufanya kazi hiyo kwa haraka ili haki za watuhumiwa zipatikane kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Jaji Kiongozi aliwataka Mahakimu wa Mahakama za Wilaya na Mahakama za Hakimu Mkazi nchini kutopokea kesi za jinai ambazo upelelezi au ushahidi wake haujakamilika (Tangazo la Serikali Na. 296 la mwaka 2012). Utekelezwaji wa mwongozo huu utasaidia sana usikilizwaji wa mashauri haraka na hivyo haki kupatikana kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, vilevile ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli katika Awamu ya Tano kwa kuteua idadi kubwa ya Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.

Mheshimiwa Spika, napenda kulithibitishia Bunge lako kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama, tutaendelea kuhakikisha changamoto hizi zinapungua kwa kiasi kikubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu katika Mahakama zetu.