Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Juma Kombo Hamad (8 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema mchana huu na kupata fursa hii ya kuchangia kwenye bajeti hii ya Wizara muhimu, Wizara ya ELimu.
Pili kwa sababu ni mara ya mwanzo kabisa nichukue fursa hii pia kuwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Wingwi kwa kunipatia ushindi mkubwa wa asilimia 90 dhidi ya mgombea mwenzangu. Pia nikishukuru chama changu, Chama cha Wananchi (CUF) kwa kuniamini kabisa na kunipa fursa hii, nakiahidi kwamba sitakiangusha, nitakitumikia kwa nguvu zangu zote kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze kwa kusema kwamba ili tufanikiwe na ili tuendelee tunahitaji tuwekeze kwenye suala zima la elimu. Kinachoonekana hapa bado kama vile hatujakuwa tayari kuwekeza katika suala zima la elimu. Kinachoonekana hapa ni kama vile tunakuja kutaniana, kwa sababu kile ambacho kimezungumzwa mwaka wa jana, kile ambacho kimezungumzwa mwaka wa juzi ndicho kile kile kinachopigiwa kelele, hakiongezeki wala hakipungui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ambayo ili zungumzwa mwaka wa jana tulipaswa leo tuje tuione angalau imetatuliwa kiasi fulani ili tuondoke pale tulipokuwa mwaka wa jana na sasa tuzungumzie kitu kingine. Lakini hadi sasa wenzangu wengi wamezungumza hapa, tunapiga kelele kwa matundu ya vyoo, tunapiga kelele ukosefu wa madawati na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kwa nia njema kabisa, hebu fuatilia zile hotuba mbili, hotuba ya Kambi ya Upinzani pamoja na hotuba ya Kamati. Kama utazifuata vizuri basi zimetoa mwanga mzuri wa kukuongoza kufikia kule Watanzania tunakokuhitaji. Na wala sioni sababu ya kwamba usifuate mawazo yale ya vitabu vile viwili, ni vitabu ambavyo vimezungumza vizuri, vimetoa mapendekezo mazuri, vimetoa maelekezo mazuri ambayo yatatutoa hapa tulipo na kuelekea pale tunapopahitaji.
Ninakuomba sana mama yangu, kwamba kwa hili bora tu ulifuate ili maelekezo yale ukichanganya na uliyo nayo wewe mwenyewe basi utapata kitu cha kushika na mwakani utatueleza kitu kipya kabisa hapa kwenye Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uwekezaji huu yamezungumzwa mengi, lakini lazima tukubali kugharamia, lazima tukubali kuchagua vijana tuwapeleke wakasomee taaluma mbalimbali ili waje waisaidie Tanzania; nchi nyingi zimefanya hivyo. Hata China pale ilipo leo kwanza ilianza zaidi miaka kumi kula hasara kwenda kuwasomesha vijana nje ya nchi kusoma kwa ajili ya taaluma fulani ili kwenda kuisaidia nchi yao. Sasa na sisi si aibu wala si fedheha.
Leo kuna mtu alitoa mfano hapa, mpaka leo tunategemea marubani, tunagemea ma-captain wa meli zile ambazo ziko hapa ndani ya nchi yetu ukienda pale unawakuta wote ni wageni. Kwa nini tusiende tukasomeshe wakwetu? Hivi kuna ugumu gani kuwa rubani? Hivi kuna ugumu gani kuwa captain wa meli? Hivi kuna ugumu gani kuwa meneja wa kiwanda fulani au mtandao fulani ambaye huyu atakuwa ni mzalendo wa nchi yetu? Naomba kumshauri Mheshimiwa Waziri afuate yale mawazo, naamini atatukwamua katika hatua hii na tutakwenda katika hatua nyingine nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo ninaomba kulizungumzia hapa ni suala la mikopo. Suala la mikopo limekuwa na malalamiko makubwa na ya muda mrefu hasa kwa upande wa Zanzibar. Mimi nikuombe kitu kimoja katika hili, nikuombe wakati utakapokuja, au ujiandae kuanzia sasa, kama utakuwa hujajiandaa basi ujiandae vizuri ili kuwe na utaratibu maalum wa utoaji wa mikopo. Suala la elimu ya juu, suala la Bodi ya Mikopo ni suala la Muungano, Wazanzibari wanahusika katika suala hili, hawapaswi kama vile kuchotewa, kama vile ni waalikwa. Zanzibar si mualikwa katika ile Bodi ya Mikopo, Zanzibar ni mshirika kwa sababu suala la elimu ya juu Kikatiba, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni suala la Muungano.
Sasa mimi nikuombe tu kwamba uandae utaratibu mzuri, wakati unakwenda kufanya udahili unatuletea hapa bajeti, unaisoma bajeti. Ukionesha kwamba fungu hili ndilo la mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu utuambie basi katika fungu hili kiasi hiki ndicho kinachokwenda kwa wanafunzi watakaodahiliwa watokao Zanzibar. Sioni kama kuna dhambi, sioni kama kuna tatizo hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri sana kwamba hili ulifanye ili kuondoa haya malalamiko ya muda mrefu. Utakapotuambia, pengine fungu la mikopo lina milioni 40, lakini hizi Shilingi 200,000 zitakwenda kwa wanafunzi wa Zanzibar, wewe utakuwa umejiondoa kwenye malalamiko, na umeitoa wizara kwenye malalamiko. Tutajua tuna wanafunzi wangapi kutoka Zanzibar ambao watapata mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Tanzania.Nitakuomba sana hili ulichukue, ulifikirie na ulipatie maamuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo ninaomba kulizungumzia hapa ni suala la uwekezaji hasa katika vyuo vikuu. Kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu, na Serikali hapa ilifanya jambo kubwa na lenye nia njema kabisa. Suala la uanzishwaji wa sekondari katika kila kata lilikuwa ni suala muhimu, limetekelezwa na Serikali kwa kiasi fulani, hivyo hivyo, lakini lipo na limetekelezwa. Sasa, kuna ukanda huu wa Kusini, baada ya kuanzishwa sekondari hizi za kata imepelekea wanafunzi wengi kujiunga na sekondari za O-Level na A-Level. Udahili wa wanafunzi kwenda vyuo vikuu umeongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini miaka mingi mmekuwa mkisema Chuo cha Ualimu kilichoko Mtwara mtakigeuza kiwe Chuo Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mpaka leo suala hili halijachukuliwa hatua yoyote. Tunakuomba Mheshimiwa Waziri, kwa heshima zote mama yangu Ndalichako ukija hapa utueleze, kile chuo ni lini kitachukuliwa hatua ya kugeuzwa sasa kuwa Chuo cha Ualimu na sasa kiende kwenye kuwa chuo kishiriki kisaidie ule ukanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mikoa mitatu, Lindi, Mtwara na Ruvuma, huu ni ukanda mmoja, mikoa hii imefuatana kabisa, lakini hakuna hata chuo kikuu kimoja cha Serikali. Tunakuomba sana suala hili lichukuliwe hatua na ni vyema utakapokuja hapa sasa utuambie ni lini suala hili litachukuliwa hatua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba hakuna elimu bora bila huduma bora za walimu. Muda umefika sasa kuwaonea huruma walimu, wamehangaika muda mrefu sana. Imefika muda sasa kuboresha maslahi ya walimu katika nyanja zote, ukae pamoja na TAMISEMI uboreshe, uone kwa namna gani mtashirikiana kuikwamua kada hii ya walimu katika sekta au katika maslahi ya walimu. Walimu hawa ni wetu, ni Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamekuwa wakisema, hata wewe leo usingekuwa Waziri wa Elimu kama hujapitia kwa walimu. Ulianza darasa la kwanza mpaka ulipofika, waliokuwezesha hapo ni walimu. Hebu wahurumie walimu, waonee huruma walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba mchango wangu kwa leo uwe huo, ninaamini kwamba mawazo yangu haya yatasaidia kwa namna moja ama nyingine kufikia pale tunapopahitaji, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie mawili, matatu kuhusiana na hotuba ya Waziri Mkuu. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa kuanza kuchangia katika sehemu
ambayo mara nyingi tumekuwa tukiisemea au imekuwa ikizungumzwa humu kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wazanzibari mara nyingi wamekuwa wakijiuliza hatma ya Mashekhe hususan kupitia Wizara ya Katiba na Sheria, lakini leo nimeamua kulizungumza hili kwenye hotuba hii ya Waziri Mkuu tukiwa na matumaini kwamba kilio hiki sasa kinaweza kikasikika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni juzi tu kupitia Mahakama Kuu ya Zanzibar, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar alinukuliwa kupitia vyombo vya habari akisema kwamba Mashekhe wale wameletwa huku kwa makosa na sasa wanatakiwa warejeshwe Zanzibar kwa namna yoyote itakavyokuwa. Kwa bahati mbaya sana hatukuona hata dalili ya namna ambavyo kuna ushughulikiwaji wa suala lile kuona kwamba Mashekhe wale sasa watarejeshwa Zanzibar na kama ni kuhukumiwa basi watahukumiwa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka minne sasa Mashekhe wale wako ndani, haijulikani tatizo ni nini isipokuwa kinachoonekana pale ni mihemko au hisia tu za kisiasa ambazo zimewafanya Mashekhe wale wanaendelea kusota ndani. Miaka minne imetosha, kama masuala ya upelelezi hayajakamilika kwa nini basi wasipewe dhamana wakaendelea kufuatiliwa wakiwa pamoja na familia zao na huku kesi ile inaendelea? Miaka minne ni mingi sana, naamini kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa, Waziri Mkuu ni mtu mkubwa katika Serikali hii, ndiyo msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali anaweza akasikia vilio hivi vya Wazanzibari kuona kwamba Mashekhe wale ni sehemu ya Watanzania wanasikilizwa na wanaachiwa na wanaendelea kuwa huru pamoja na familia zao, hilo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, katika mambo ambayo tutayapitisha kupitia Bajeti ya Waziri Mkuu hii ambayo tunaijadili sasa ni pamoja na kujadili Fungu Namba 27 ambalo linagusa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Ni jambo ambalo halikujificha, liko wazi kwamba Msajili wa
Vyama vya Siasa sasa ameamua kwa makusudi kabisa kuingilia na kupandikiza migogoro ndani ya vyama vya siasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu ofisi hii majukumu yake yamezungumzwa ndani ya sheria inayoongoza vyama vya siasa ya mwaka 1992. Moja, kusimamia kumbukumbu za vyama vya siasa; pili, kusajili vyama vya siasa ambavyo vimekidhi matakwa ya sheria hiyo;
tatu, ni kufuta chama cha siasa ambacho kimekwenda kinyume na taratibu hizo ambazo zimezungumzwa ndani ya sheria pamoja na majukumu mengine lakini haya matatu ndiyo majukumu makuu ya Ofisi hii ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Kwa bahati mbaya sana Msajili wa Vyama vya Siasa leo amejipa majukumu mengine, sijui kayatoa wapi, madaraka haya sijui ameyatoa wapi ya kuona kwamba sasa ana mamlaka ya kuchagua chama cha siasa kiongozwe na nani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wote wanafahamu, Watanzania wote wana akili timamu na wanafahamu kwamba Profesa Lipumba alijiuzulu Agosti, 2015 kwa kuandika barua ya kujiuzulu kabisa. Baada ya miezi kumi Profesa Lipumba anasema anarudi katika nafasi yake ya
Uenyekiti. Katika Katiba hii ya Chama cha CUF hakuna sehemu yoyote ambayo inatoa mamlaka kwamba mtu anapojiuzulu baada ya muda anaandika barua kwamba narudi kwenye nafasi yangu, hakuna. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilipokea barua na minutes zote za vikao
kwamba sasa wanaokaimu nafasi ya Mwenyekiti ni hawa. Chama cha CUF kupitia Baraza Kuu la Uongozi kikaunda Kamati ya Uongozi ya Chama na kupeleka kila kilichotakiwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kutambulisha kwamba sasa wanaoongoza majukumu ya Mwenyekiti ni hawa kwa muda wa miezi kumi. Baada ya miezi kumi Profesa Lipumba anaandika barua ya kurudi kwenye nafasi yake ya Uenyekiti, very shameful. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jaji akaamua kwa makusudi kabisa kwa sababu eti anataka kuivuruga CUF kutambua kurudi kwa Profesa Lipumba bila kufuata sheria, kanuni, Katiba ya nchi, kwa matakwa yake akaamua sasa kupandikiza mgogoro ndani ya Chama cha CUF. Chama cha CUF hakina mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke sawa, mama yangu mmoja pale alifananisha mgogoro wa Chama cha CUF na ndoa ya mtu na mke wake, akasema kwamba mambo ya mtu na mkewe yanamalizwa chumbani. CUF haikuwa na mgogoro, mgogoro huo ulimalizika mapema Profesa kajiuzulu, Mkutano Mkuu wa Chama ukaitishwa, quorum ikaridhika kwamba Profesa kajiuzulu kama Katiba inavyozungumza, ya nini leo Msajili kufanya haya? Tena angalia sasa cha kushangaza, Msajili wa Vyama vya Siasa anatambua vikao vile na mkutano ule ulikuwa halali lakini anasema maamuzi yake ni haramu. Maana yake ni sawa na kusema nguruwe haramu, lakini mchuzi wake halali, hii haiingii akilini, kwa makusudi akaamua kufanya alivyofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi cha ajabu zaidi Msajili huyo wa Vyama vya Siasa alikuja kwenye Kamati, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria, kama Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria tulimuuliza sheria hizi umezitoa wapi? Nashukuru Kamati yangu imeandika kama miongoni mwa maazimio, ukurasa wa 30, Kamati pia inaagiza Ofisi ya vya siasa, si jukumu lake. Migogoro ya vyama vya siasa viachiwe vyama vya siasa, Msajili asiwe ni sehemu ya mgogoro wa chama cha siasa. Chama kina taratibu, sheria, Katiba na kanuni zake, leo iweje yeye apange? Ni ajabu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi anatushangaza hapa sasa, anakuja kwenye Kamati anajitetea siku ya pili anasema anamtangaza kwamba sasa Sakaya ni Kaimu Katibu Mkuu. Sakaya alishasimamishwa uanachama, Sakaya alishasimamishwa uongozi, leo kwa sababu tu una mambo
yako unayatafuta unakuja …
Mheshimiwa Sakaya, Mbunge wa Kaliua, anamtambua kwamba eti ni Kaimu Katibu Mkuu wa Chama, aibu! Katibu Mkuu wa Chama yupo anafanya shughuli zake za kisiasa kama kawaida unashawishiwa, wewe umepanda shetani gani? Aliyekushawishi ni nani? Kakupandikiza nini? Kama kuna mtu anakusukuma au anakushawishi, wewe ni Jaji unapaswa uwe na heshima. Tunasema kama ana ndoto ya kufikiria kwamba Chama cha CUF kinakwenda kufa mikononi mwake, Chama cha CUF hakifi, kitaendelea kuweko imara na kitaimarika zaidi. Kama anahisi kwamba Chama cha CUF kinakwenda kufa basi hilo alisahau kabisa (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kidogo suala la utekaji. Nchi hii haiko salama tuseme kweli. Asubuhi watu wameomba miongozo umewakatalia ni suala la hatari. Kama unakumbuka kila siku zikienda mbele hali hii inazidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulinisimamisha kidogo naomba dakika yangu moja ambayo ulinisimamisha…
NAIBU SPIKA: Zilikuwa ni sekunde 10 ambazo zimeshaisha.
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, tulishuhudia Salma Said, Mwandishi wa DW alitekwa uwanja wa ndege...
NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mawili, matatu katika Wizara hii muhimu, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana wakati tuko katika Bunge la Bajeti, Mheshimiwa Waziri aliyekuwa na dhamana muda huo au mwaka jana aliwaambia Wabunge wa Bunge hili Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba jembe la mkono litakuwa historia, lakini jembe la mkono litaonekana au litatumika katika maeneo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo jembe la mkono litatumika kwa mujibu wa Mheshimiwa Waziri wa kipindi hicho alisema jembe la mkono litaonekana kwenye majumba ya kumbukumbu (makumbusho), alisema jembe la mkono litatumika kwa ajili ya kuchimbia makaburi lakini alisema jembe la mkono litaonekana kwenye Nembo ya Chama cha Mapinduzi na kwamba jembe la mkono halitatumika tena kwa shughuli za kilimo na alisema haya kwa sababu sasa Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa kati na uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, kama tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda lazima tuboreshe kilimo na lazima tuwe na zana bora kwa ajili ya kuendeleza kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya winding-up ya hotuba yake atueleze hadi sasa shughuli hii au azma/dhamira hii tumefika katika eneo gani. Tumevuka pale ambapo tulikuwa tunahitaji kuvuka au bado Watanzania wanaendelea kuhenyeka na kuumia kwa kutumia jembe la mkono. Nadhani ni wakati sasa wa kupata angalau maelezo ya Serikali kupitia Wizara hii kuwaeleza Watanzania tumefikia katika hatua gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka kuchangia ni la uvuvi. Tanzania tumebarikiwa kuwa na eneo kubwa la bahari lakini Tanzania ni pamoja na Zanzibar. Zanzibar ni visiwa ambavyo vimezungukwa na eneo lote la bahari, bahari kubwa ni bahari ya Hindi. Kiuhalisia ni kwamba hatujaitumia bahari ipasavyo katika masuala ya uvuvi wa samaki lakini katika kutumia resource zilizomo ndani ya bahari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimtaarifu Waziri kama atakuwa hajui, lakini nina imani anajua kwa sababu naamini ni mlaji wa samaki. Hivi Waziri anajua kwamba hapa Dodoma tunakula vibua kutoka China?
Hivi Waziri anatambua kwamba tunakula vibua kutoka South Africa? Namwomba Mheshimiwa Waziri atambue hili, hivi sisi Watanzania tuna sababu gani kwa eneo kubwa la bahari ambalo limejaa resource ya samaki kwa nini hadi leo tunakula vibua vya South Africa. Mheshimiwa Waziri tunaomba na eneo hili atufafanulie kidogo tuone uhalisia na ukweli hasa wa matumizi ya bahari yetu ambayo tunayo katika Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la korosho. Wachangiaji wengi wamezungumza hapa kwamba zao la korosho linastawi zaidi na sana pembezoni mwa Ukanda wa Bahari au Ukanda wa Pwani. Natambua kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi si miongoni mwa Wizara za Muungano lakini kila siku hapa tunajivunia kwamba Wizara zilizoko katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Wizara ambazo zinafanya kazi kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinafanya kazi kwa pamoja. Hebu tueleze hivi mmekaa lini kusaidiana na Wizara ambayo iko kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala ya utafiti na kuangalia labda kwa kiasi gani zao la Korosho tunaweza kuliimarisha kwa upande wa Zanzibar na likawa ni sehemu na mbadala wa zao la karafuu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikupe pole na nimwombe Mwenyezi Mungu akujalie uendelee kuwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la demokrasia na utawala bora na haki za binadamu nchini mwetu linapotea kila siku. Leo Tanzania, wananchi wanatekwa na kuuawa, wanasiasa na wanaharakati pia wanahujumiwa na Tanzania hata waandishi wa habari na vyombo vya habari hawako salama. Hali hii haileti afya kwa Taifa. Tunaiomba sana Serikali na Wizara ya Mambo ya Ndani, usalama kwa wananchi ni jambo muhimu kwa mustakabali wa amani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza kuna vijana sita Pemba wametekwa na wa watatu kati yao hadi sasa hawajulikani walipo. Vijana hawa wametekwa Pemba Jimbo la Mtambwe na hadi sasa vijana watatu hawajaonekana nao ni Thuwein Nasor Hemed (30), Khamis Abdallah Mattar (25), Khadid Khamis Hassan (30). Tunaomba Serikali itupe jibu, je vijana hawa wapo wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la sukari ya Zanzibar kuzuiwa kuuzwa Tanzania Bara sio haki na ni uonevu mkubwa Zanzibar na maendeleo ya Wanzanzibari, jambo hili halileti afya kwa Muungano wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kodi hasa katika Bandari ya Dar es Salaam ni tatizo na ni kero kubwa, mustakabali wa biashara kwa wafanyabiashara wa Zanzibar. Tunaiomba sana Serikali kulifanyia kazi suala hili ili kuleta nafuu kwa wafanyabiashara wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msamiati wa kero za Muungano sasa imekuwa hadithi zisizo na tija kwani kila siku kero hizi zinaongezeka na kuzidi kudumaza maendeleo ya Zanzibar. Kama suala hili halikupatiwa ufumbuzi linaweza kutikisa Muungano hatimaye kuvunjika kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwaweka watu mahabusu kwa muda mrefu bila kuwafikisha Mahakamani sio jambo jema. Suala la Mashekhe wa Uamsho na dhuluma wanayofanyiwa sasa imekuwa haivumiliki tena. Ni lazima Serikali kutoa jibu juu ya Mashekhe hawa. Sasa ni miaka mitano wapo ndani bila kufikishwa Mahakamani, hii sio haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni uonevu uliovuka mipaka na uvumilivu unafika mwisho. Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia angalau kwa uchache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza niwashukuru viongozi wangu wa Kambi ya Upinzani kwa kutupa maelekezo mazuri na kutuongoza na kufikia kwenye ufanisi hadi leo tumo na tunaendelea kujadili katika Bunge hili la bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote humu tunakumbuka kwamba katika dunia hii nchi yoyote hata zile ambazo zimeendelea, tukielekea kwenye uchaguzi kitu cha mwanzo wagombea Urais wanachokijadili ni suala la kuongeza ajira kwa wananchi wao hususani kwa vijana. Pili wanajadili mkakati imara na madhubuti wa kuondoa umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na msemaji aliyepita hivi punde, Mheshimiwa Silinde kwamba bado Mheshimiwa Mpango katika hotuba hii hajatuonyesha mkakati imara wa Serikali namna gani na kwa njia zipi ataondoa tatizo la ajira kwamba ni kwa namna gani atawaajiri vijana wa Kitanzania. Pia ni mkakati gani atakaoutumia katika kuhakikisha umaskini uliokithiri wa Watanzania unapungua kwa kiwango fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nina imani, suala hili mara nyingi linajitokeza hapa Bungeni, dada yangu pale Mheshimiwa Angellah Kairuki ana jawabu lake moja mara zote huwa analizungumza kwamba tunafanya uhakiki na baada ya kumaliza uhakiki tutaajiri vijana wa Kitanzania kwa kiasi fulani. Hebu wakati wa kufanya majumuisho, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Kairuki mje basi mtueleze ni lini sasa mtawaajiri vijana wa Kitanzania. Tunaenda kwenye mwaka wa pili sasa wa Rais John Pombe Magufuli bila vijana wa Kitanzania kupewa ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo napenda kulizungumza ni mfumo wa kodi ambao tunauendeleza Tanzania. Miongoni mwa mambo ya Muungano suala la Wizara ya Fedha siyo suala la Muungano lakini kodi ni suala la Muungano, kwa maana ya TRA. TRA ipo na inakusanya kodi kwa maslahi ya nchi nzima ya Tanzania kwa maana ya Zanzibar na Tanzania Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa ni sahihi kabisa kwamba Zanzibar haifuati mfumo wa kodi wa kilimwengu kwa maana ya mfumo wa kuthaminisha bidhaa kwa ajili ya kodi, ni sahihi kwamba Zanzibar mfumo huu imeukataa na haiufuati. Haiufuati kwa sababu ya uchumi wake mdogo na population ya Wazanzibar ni ndogo, uchumi wa Zanzibar hauwezi kuulinganisha na uchumi wa Tanzania Bara. Tanzania Bara ina mchango mkubwa katika kufanya uchumi wa Zanzibar hauendi mbele kwa sababu ya mfumo mbovu wa kodi tunaouendeleza Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba suala la Mtanzania yeyote kutoka Zanzibar na kitu pengine cha shilingi milioni moja, kwa mfano tv akalipishwa kodi pengine laki moja na nusu Zanzibar, anakuja kutumia katika matumizi yake ya kawaida lakini anafika Tanzania Bara bandarini anaambiwa alipe difference, hii sio sahihi. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ipo haja sasa ya kutafuta namna bora ya mfumo wa kodi ili kuhakikisha kwamba wajasiriamali wadogo wadogo wa Zanzibar wana-enjoy soko la Tanzania Bara. Leo anatoka mjasiriamali na mzigo wake mdogo wa shilingi pengine milioni moja au moja na nusu anakuja kutafuta riziki Tanzania Bara, lakini mzigo ule Zanzibar kalipia kodi pengine shilingi laki mbili, lakini akifika Tanzania Bara anaambiwa lipia tena laki mbili tukiwa na dhana eti ni difference, hii siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tena mdogo wangu mmoja alizungumza kule kwamba hata zile bidhaa zinazotoka ndani ya nchi, zinazozalishwa Tanzania Bara au Zanzibar lakini zikivuka kutoka Tanzania Bara kuja Zanzibar au kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara pia zinalipishwa kodi. Hata Afrika Mashariki tumeandaa utaratibu wa kusameheana kodi kwa bidhaa ambazo zinazalishwa ndani ya Afrika Mashariki, leo iweje ndani ya Tanzania moja tuna mifumo ya ajabu ya kulipishana kodi? Mheshimiwa Waziri wa Fedha hii siyo sahihi.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitoe ushauri tungekuwa na mfumo kwamba basi kama tuna difference tungekuwa na baadhi tu ya bidhaa au aina fulani ya bidhaa au thamani fulani ikifikia ndiyo suala la difference hapa mnalizingatia. Siyo sahihi kwamba mjasiriamali ana mzigo wake mdogo anakuja kutafuta riziki Tanzania Bara au mjasiriamali anaondoka hapa na mzigo wake mdogo kwenda Zanzibar tuwe na mfumo wa ajabu wa kodi ambao unadumaza upande mmoja wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Tume ya Pamoja ya Fedha, ni sahihi kwamba Zanzibar stahiki yake kwa mujibu wa sheria ni asilimia 4.5. La ajabu la kwanza, Mheshimiwa Mpango, ipo haja sasa kuufanyia review ya mfumo huu wa asilimia 4.5 na kuuangalia upya kwa sababu ulipitishwa miaka 40 nyuma. Uchumi wa nchi hizi unabadilika, lakini uchumi wa Tanzania Bara siyo uchumi wa Zanzibar, uchumi wa Zanzibar ni uchumi wa bidhaa, uchumi wa Tanzania Bara umejitawanya katika mambo tofauti tofauti. Sisi kule Zanzibar hatulimi korosho, ufuta wala pamba, uchumi wetu unategemea bandari na bidhaa kutoka nje. Inapofika mahali kwamba suala la mfumo wa Tume ya Pamoja ya Fedha kutokuwepo…

TAARIFA

Mheshimiwa Mwenyekiti, jawabu limetoka, tena limetoka kwa watu wa CCM kule nyuma kwamba Makunduchi wanalima korosho, lakini mbili/ tatu za kula wenyewe, sisi tunazungumzia zao la biashara.(Makofi)

Mheshimiwa Mattar ni rafiki yangu, umerogwa na nani? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la Tume ya Pamoja ya Fedha, nikuombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha utakapokuja kuhitimisha ulitolee majibu suala hili kwa sababu limechukua muda mrefu na hili ndiyo mwarobaini wa kukuweka wewe salama. Mheshimiwa Mpango nataka nikuhakikishie kwamba Wazanzibari hawatokuelewa bila suala hili kupata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mpango na tuna ushahidi kwamba hata hiyo asilimia 4.5 kwanza haifiki kikamilifu, ikifika ni asilimia 2.5 au 3.5 lakini pia hata huo mrejesho wenyewe hauendi. Mheshimiwa Mpango hadi sasa hivi Zanzibar inakudai mrejesho tena karibuni wa shilingi bilioni 30, Mheshimiwa Mpango umerogwa na nani? Yaani wewe huna haya wala aibu? Yaani Zanzibar leo inaikopa huna aibu? Kwa uchumi ule mdogo unakuja kuikopa Zanzibar? Hili Mheshimiwa Mpango inabidi uje utujibu ni lini fedha hii utairejesha Zanzibar? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naomba nizungumzie suala la madini. Hili suala limezungumzwa kwa mapana yake. Mimi nataka kuzungumza kitu kimoja kwamba ili Watanzania wawaelewe CCM na wafute ile dhana inayosambaa kwenye mitandao kwamba CCM ni ukoo wa panya, baba mwizi, mama mwizi na mtoto mwizi ni kwa waliohusika kupelekwa mahakamani. Hii ni kwa sababu viongozi walioshutumiwa wote walikuwa viongozi waandamizi wa CCM, majanga haya yanafanywa viongozi hao ni viongozi wakuu wa CCM, ni Mawaziri, Makatibu Wakuu na kadhalika, tuone sasa viongozi wale wanapelekwa mahakamani, wamechunguzwa na wamechukuliwa hatua stahiki kwa sababu tayari ripoti mnayoita ya kisayansi imethibitisha kwamba viongozi hawa wamehusika kwa namna moja au nyingine. Hapo ndiyo msemo huo tutau- delete sasa kwenye mitandao kama CCM ni ukoo wa panya kwamba baba mwizi, mama mwizi na viongozi wengine wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia hizi dakika tano niseme machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muda mrefu tulikuwa tunazungumzia juu ya suala la Muungano na hizi zinazoitwa kero za Muungano, lakini sasa ni dhahiri kwamba imenoga. Imenoga kwa sababu pande zote hususan za Wabunge kutoka Zanzibar sasa wameungana na wamekutana kwenye angle moja ya kusemea namna kero hizi za Muungano zinavyoathiri maendeleo na uchumi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Zanzibar ni uchumi wa visiwa, uchumi wa visiwa siku zote unategemea zaidi biashara, biashara za fedha, benki na biashara nyingine. Leo biashara hizi zote kwa kutumia kivuli cha Muungano zimekufa na uchumi wa Zanzibar tayari ni kusema kwamba tayari ni sawa na kusema umekufa kwa sababu umesimama na biashara Zanzibar haziendi kwa sababu ya mfumo mbovu wa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisikitike sana, leo wafanyabiashara kutoka Tanzania Bara wameona bora kwenda kuchukua bidhaa Mombasa, Uganda na Kongo kuliko kusafiri kwenda Zanzibar kuchukua bidhaa kama ilivyokuwa zamani kwa sababu tu ya mifumo mibovu ya kodi, kuna nini hapa? Ni kutokana na ukiritimba na mfumo mbovu wa kodi na mfumo mzima wa mzunguko wa biashara hasa katika Tanzania yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala la pili, Zanzibar ilikuwa na system ya kusajili meli, miezi miwili mitatu nyuma mfumo huu wa usajili meli umezuiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nikwambie Zanzibar kwa mwezi ilikuwa inakusanya jumla ya dola 79, jumla ya shilingi milioni 333 kwa mwezi. Nikwambie sasa ninavyozungumza Zanzibar mpaka inazuiwa ilikuwa imesajili meli 457. Leo kwa sababu Zanzibar imezuiwa na vikwazo vile vimewekwa leo zimebakia meli 350 tu, watu mmoja mmoja waliosajili meli zao wanaondoka kwa sababu ya vikwazo ambavyo vimewekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme usajili wa meli, Zanzibar toka miaka kumi iliyopita, Zanzibar zimekamatwa meli mbili kwa hizo sababu zilizotajwa kwamba ni sababu ya unga, lakini kuna nchi mwezi mmoja zinakamatwa meli zisizopungua 27, Zanzibar miaka 10 zimekamatwa meli mbili? hivi kuna sababu ipi kwamba Zanzibar zimekamatwa meli ipi na iwekewe vikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa zilizopo sasa ni wazi na ni dhahiri kwamba Zanzibar inanyang’anywa usajili wa meli na usajili wa meli sasa unawekwa kwa jina la Tanzania. Huu ni uonevu na ni uonevu ambao haukubaliki, Muungano huu ambao tunauhubiri kila dakika na kila wakati kwa kweli umekuwa ni tatizo kwa uchumi wa Zanzibar na kwa kweli umekuwa ni kilio kikubwa kwa uchumi wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikitikia mifumo hii ya kodi ambayo tumekuwa tukizungumza, kila Mzanzibar anaenyanyuka analilia mfumo wa kodi. Mimi binafsi nimewahi kumfuata Waziri wa Fedha tukazungumza kirafiki kabisa, nimemfuata Naibu Waziri wa Fedha nikamfuata nikazungumza naye, lakini kwa masikitiko majibu ninayoyapata ni ya aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafika Waziri wa Fedha au Naibu wake anakujibu na anakwambia hasa kwamba wewe nia yako Bandari ya Tanzania Bara ife, sasa ndio maana nikamuuliza tu ina maana wewe umeridhika baada ya kuua Bandari ya Zanzibar, kwa sababu Bandari ya Zanzibar ni kama vile imekufa, biashara hakuna lakini yeye ameridhika kwamba Bandari ya Zanzibar ife, lakini amefurahi kuinyanyua Bandari ya Tanganyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii haikubaliki, lazima tuwe na mkakati na msimamo imara wa kuhakikisha kwamba bandari zote mbili zinatumika na tunaziimarisha kwa maslahi ya uchumi wa pande zote mbili, Tanzania Bara na Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na Waziri wa Fedha au Waziri wa aina yoyote ambaye ana-favor upande mmoja na kuukandamiza upande mwingine, hii haikubaliki na haitokubalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme wazi kama kuna watu ambao watavunja Muungano ni watu wanaowadanganya wananchi kwamba tunatatua kero za Muungano, lakini tukitizama kero za Muungano kila uchwao zinazidi, uchumi wa upande mmoja kila uchwao unanyanyuka na uchumi wa upande mwingine kila uchwao unakufa. Sababu hii kizazi kinachokuja hakitokubali na nina kuhakikishia Muungano huu utaenda kuvunjika bila ridhaa na mitazamo ya watu. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia dakika tano hizi na naomba niseme machache. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kupata muda huu wa dakika chache na nianze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Katiba na Sheria kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 133 na Ibara ya 134, inazungumzia uwepo wa Tume ya Fedha ya Pamoja na Akaunti ya Pamoja ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume hii ilianzishwa mwaka 1996 na ilizinduliwa rasmi mwaka 2003.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie je, Tume hii ipo na kama ipo inafanya kazi gani? Naomba hili suala liwekwe sawa, kwa sababu uwepo wa Kamati ya Pamoja ya Fedha na Tume ya Pamoja ya Fedha au Akaunti ya Pamoja ya Fedha bila shaka ingetufanya sisi Watanzania tukawa na mgawanyo sahihi wa mapato ya Muungano na Tume hii ingetusaidia sisi kuondoa na ikawa ndiyo kimbilio la kuondoa changamoto zote zinazogusa maslahi ya pande mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa sababu Tume hii haipo ingawa imezungumzwa kwenye Katiba, ni suala la Kikatiba, lakini kwa sababu haipo na haijaundwa tunaamini kwamba kero za Muungano ambazo tokea juzi zimekuwa zikitawala kwenye Wizara hizi mbili za Katiba na Sheria na Wizara inayoshughulikia mambo ya Muungano zitaendelea kuwepo na haziwezi kutatuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatujui ni sababu zipi ambazo au kuna changamoto zipi ambazo zimepelekea Tume hii ya Pamoja ya Fedha mpaka leo iwe haipo na haijaanzishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo naomba nilizungumze ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya nne (4) ambayo imezungumzia mamlaka mbili za Serikali ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Katiba imezungumzia Mamlaka mbili za Mahakama; Mahakama ya Tanzania Bara au Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini imezungumzia Mahakama ya Zanzibar ambazo Taasisi hizi mbili zote zina mamlaka sawa ya kiutendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano inatekeleza matakwa na masuala yanayohusu Muungano na Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatakiwa isimamie masuala yanayohusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kumekua na mwingiliano mkubwa wa utekelezaji wa majukumu haya.

Mhesimiwa Mwenyekiti, ambacho nataka kukisema hapa kwamba tumekuwa tukizungumzia malalamiko mengi na masuala mengi yanayohusu utekelezwaji wa Mamlaka hizi mbili kwamba kumekuwa na mwingiliano na kumekuwa na kutokuaminiana katika utekelezaji wa majukumu. Tunachokizungumza hapa ni kwamba, Wizara ituweke wazi na akija Mheshimiwa Waziri atuweke wazi juu ya Mamlaka hizi mbili zinatendaje majukumu yake.

Mheshimiwa Mwneyekiti, kubwa, Zanzibar imekuwa ikipigania mara nyingi kujiunga na Taasisi ambazo ingeruhusiwa kujiunga, lakini Mamlaka moja imekuwa ikichukua fursa ya kuiamuru Mamlaka nyingine kwamba hamna haki ya kujiunga na Taasisi hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukishirikiana katika masuala pengine ya Zanzibar kujiunga na FIFA, Zanzibar kujiunga na CAF, lakini tumeambiwa au tunaelezwa kwamba tunashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili Zanzibar ijiunge na vyombo .

Mheshimiwa Mwenyekiti, masikitiko makubwa ni pale Zanzibar ilipokuja kuruhusiwa kujiunga na OIC kwa nini iliambiwa ijitoe? Halafu leo tunajikomba tunakuja kusema kwamba tunaisaidia Zanzibar ili ijiunge na FIFA, ili ijiunge na CAF huu si uongo kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunapigania kujiunga na vyombo hivi kwa nini leo tusiiruhusu Zanzibar kwa sababu ina uwezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo naomba nizungumze, nalielekeza kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Kila siku tumekuwa tukilalamika kuna kesi zimechukua muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wale Masheikh wa Uamsho na wale Masheikh waliokamatwa katika Mji wa Arusha, tunaomba kama Ofisi hii ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeshindwa kupeleka ushahidi wale ni Watanzania, wale ni Wazanzibari tunaumia na lazima tuwasemee kwa sababu hawana mtu wa kuwasemea, lazima tutasimama Bungeni, tutaendelea kusema, tutaendelea kupiga kelele. Kama Serikali kupitia Ofisi hii imeshindwa kuthibitisha kwamba wale watu wana hatia basi waachiwe huru waende kwenye familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie na Tume ya Haki za Binadamu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2016
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii nikiwa mtu wa mwanzo kuchangia muswada huu, nikushukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia kile ambacho nilitaka kukisema hapa, nimpongeze Mnadhimu na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa kile ambacho amekiwasilisha kwa ufasaha mkubwa sana. Lakini pia niunge mkono hotuba ya Kamati ya Katiba na Sheria na mimi nikiwa miongoni mwa Wajumbe wa Kamti hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie muswada huu nijielekeze kwenye Ibara ya 13 ya muswada huu inayohusiana na masuala ya mikopo ya Serikali pamoja na misaada na dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la aibu kubwa kuona kwamba miaka 50 ya uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini hadi leo tunakuja kupitisha sheria ambayo inaifanya sasa Zanzibar, maana tunaweka masharti ya kukopa Zanzibar kama vile Serikali ya Mtaa, tunaipa mamlaka kama Serikali ya Mtaa, masharti ambayo inawekewa kukopa Serikali ya Mtaa ndiyo masharti ambayo leo tunaiwekea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hili ni jambo la aibu na ni jambo la masikitiko makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tupo katika mjadala, si mara moja wala mbili, kwenye Kamati ya Katiba na Sheria, tumelizungumza suala hili lakini bado Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia Mwanasheria Mkuu kaendelea kubakia na msimamo wake, kaendelea kifungu kile kile kukibakisha na masharti yale yale, alichokibadilisha ni matumizi ya lugha tu. Lakini masharti yako palepale kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili ipate mkopo wa aina yoyote, kwa matumizi yoyote ni lazima ikakopewe au Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikakope halafu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ianze sasa procedure ya kuomba mkopo ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni aibu na ni aibu ya mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo ambalo limezungumzwa hapa kwa kina na Mnadhimu na Msemaji wa Kambi ya Upinzani limezungumzwa kwa ufasaha. Ni miaka mingi suala hili limekuwa ni kero kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni kero kwa Wazanzibari, kwamba leo, miaka 50 mtoto kakua tayari, kwa nini Serikali ya Jamhuri ya Muungano isianze kufikiria sasa kuipa angalau mamlaka Zanzibar ya kuanza kutembea kwa miguu yake? Kuna tatizo gani? Kuna ubaya gani sasa Zanzibar kuanza kuiachia kidogo kidogo ikatembea kwa miguu yake? Mpaka leo tunaendelea, maana mnaandaa sheria ya kuendelea tu, maana kile kinachozungumzwa kwamba kilichopo hapa ni…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiifafanua kwa kina Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya sasa inatambua mamlaka tatu. Tujiulize, hivi mamlaka ya Tanganyika ambayo imo ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi inakopewa na nani? Inaenda kumsujudia nani ikakopewe, maana yake ni mamlaka ambayo imejivisha koti la Muungano, huoni sehemu yoyote, huoni sheria yoyote kwamba sasa yale mambo ambayo yanagusa Tanganyika, si mambo ya Muungano, ni ya Tanganyika, yanaomba ruhusa kwa nani kwenda kujitafutia mkopo, msaada na kitu kingine chochote nje ya Tanzania au ndani ya Tanzania. Mamlaka hii ya Tanganyika inaomba ruhusa kwa nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini mamlaka ya Zanzibar ambayo kuna Serikali kamili, kuna Rais, kuna Baraza la Wawakilishi, kuna kila kitu. Kwa nini kila siku iombe ruhusa? Kwa nini kila siku ije ipige magoti kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba ruhusa eti ikakopewe? Huo msingi wa kukopa, kwamba sio ikakopewe tu lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano ikakope halafu waje waanze sasa kuiwekea masharti Zanzibar kwamba baada ya Serikali ya Muungano kukopa ikapewa masharti haya, huko ambako imeenda kukopa, na hiyo ikija sasa inapanga masharti mapya kuipangia Zanzibar kama vile ambavyo Serikali ya mtaa fulani imewekewa masharti, hivi mnatuelekeza wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani muda umefika sasa, miaka 50 si kidogo, muda umefika sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba Pendekezwa ukisoma Ibara ya 254(1), (2) na ya (3) imezungumzia vizuri suala hili na tayari ilikuwa imeshaipa Zanzibar kutaka kutembea kwa miguu yake, na wanazungumza kwamba kuna matatizo ya Kikatiba. Matatizo ya Kikatiba ya nchi hii hayakuanza leo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mpaka leo inatambua uwepo wa Waziri Kiongozi kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hivi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijavunja Katiba ya Muungano? Kimsingi tayari imevunja Katiba ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuna mambo yameorodheshwa kama mambo ya Muungano, utekelezaji wake hautekelezwi kama mambo ya Muungano, Zanzibar inatekeleza kivyake na Tanzania Bara inatekeleza kivyake. Kwa nini leo tuambiwe kwamba kurekebisha kifungu hiki, kutoa mamlaka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenda kukopa, kwenda kuomba misaada nje ya nchi, nje ya Tanzania inavunja Katiba ya Muungano, kwa hili tu? Kwa nini tusiseme kukusanya kodi sasa, kwa sababu ni suala la Muungano ile ZRB kule Zanzibar ifutwe, kwa nini tusiseme?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tusiseme masuala ya hali ya hewa sasa Zanzibar isiwe na kitengo kinachotabiri masuala ya hali ya hewa? Kwa nini tusiseme kwamba hapa tunavunja Katiba tuje tuseme tunavunja Katiba eti kwa sababu tunaomba sasa Zanzibar ipewe mamlaka ikakope nje ya nchi. Kwa nini tunasema tunavunja Katiba eti kwa sababu tumesema Zanzibar sasa iende ikaombe misaada nje ya nchi, hapo tunavunja Katiba. Tulijiunga na OIC kwenda kuomba misaada tukaambiwa tunavunja Katiba tujitoe, kwa nini kila sehemu ambapo kuna maslahi ya Zanzibar tunaambiwa tunavunja Katiba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wawazi na tuwe wakweli, muda umefika sasa kuiachia Zanzibar ianze angalau kutambaa kama si kutembea. Zanzibar nayo ina mahitaji, leo inafika mahali Serikali ya Jamhuri ya Muungano inataka kwenda kukopa eti halafu waje waikopeshe Serikali ya Zanzibar, pia tunawekewa masharti kwamba tunakwenda kuwakopea lakini mtumie kwa matumizi haya na haya, hee! jamani, hata huyo mke time nyingine unampa nafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo mke uliyemuoa ukamtolea mahari wakati mwingine akikwambia nipe laki moja wala humhoji unaenda kutumia nini. Mambo mengine ni yake yeye, wewe si utakuja kuyaona tu? Huwezi kumwambia kwamba nakupa laki moja lakini katumie kwa hiki na hiki na hiki. Hii ndoa au ujeshi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nimalizie kwa nia njema kabisa. AG akubali kwamba kile kifungu ambacho kiliwekwa ndani ya Katiba Pendekezwa ambalo bado halijamaliza mchakato wake basi kinyofolewe kiwekwe katika maeneo haya, na kilizungumza wazi kwamba Zanzibar sasa ina mamlaka ya kwenda kukopa nje na ndani ya nchi, halafu haya masharti mengine yatafuata baadaye. Si lazima na wala si wajibu na kama Katiba hii, hii Katiba ni yetu sisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba hii haijatufunga kwamba sasa Zanzibar lazima tuikabe koo hata pa kusema, hata pa kufurukuta haina. Lazima tujipangie mikakati kama ni kweli tuna nia njema ambayo haipo ya kuendeleza na kuudumisha Muungano huu. Hiyo nia haipo na ndiyo maana vifungu hivi vya Katiba ndiyo kwanza vinaandaliwa ili kuendelea kuibana Zanzibar ili Zanzibar iendelee kuja kusujudia Bara kwa maslahi ya watu fulani. Ahsante sana, nashukuru sana kwa nafasi hii.