Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu (22 total)

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB - MWENYEKITI KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kwa kupata nafasi hii kumalizia hii hoja. Hoja hii imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 29. Waheshimiwa Wabunge 23 wamepata nafasi ya kuzungumza na sita wameweza kuleta kwa maandishi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge michango yao yote tutaichukua na kuboresha kwenye maazimio yetu. Nawashukuru pia Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Waziri kwa michango yao ambayo ni muhimu sana kwenye Kamati hii ambayo inajumuisha karibu Wizara tatu na nne. Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru pia wana Kamati wenzangu, wamefanyakazi nzuri sana na wengine kwa kweli wamekuwa na roho ngumu; hata tulipoingia kwenye Magereza na kuwaona wafungwa na mahabusu jinsi walivyo, wengine machozi yaliwatoka. Nawashukuru sana kwa kuwa wavumilivu. Mheshmiwa Mwenyekiti, amani na utulivu katika nchi yoyote ile ni jambo la msingi sana. Tukichezea amani na utulivu, naamini hatuwezi kukaa. Kuna mifano mingi sana ambayo ipo kwenye ulimwengu huu. Nchi ambazo zimechezea amani na matokeo yake wanayaona na wasingeweza kukaa hata kwenye ukumbi wa Bunge kama hivi. Sisi kama Kamati yetu tutajaribu kwa kadri tunavyoweza kushauri Serikali namna ya amani na utulivu umuhimu wake unavyotakiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya ambayo yote yapo kwenye Wizara hizi; za Mambo ya Ndani na Mambo ya Ulinzi na Usalama yanahitaji fedha; lakini kwenye Wizara zote hizi tatu ambazo tumezizungumza zote zimeonekana kuna upungufu wa fedha. Fedha ambazo zimepitishwa na Bunge lako Tukufu hili, zimeshindwa kuwafikia wahusika ili waweze kufanya shughuli za maendeleo. Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetembea kwenye baadhi ya Magereza na baadhi ya Magereza mengine tumekuta wafungwa wanadai vyombo, zana za kufanyia kazi ya kilimo. Wanasema tunaomba matrekta, tuna ardhi iko hapo imejaa na tuna hela zetu. Ni Gereza la Songwe wanasema tuna hela zetu shilingi milioni 40 ziko kule kwenye akaunti, tupeni tununue matrekta. Sijui kwa nini, nafikiri Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Ndani, atakuwa analisikia. Toeni hizo hela na kuacha huo urasimu, wapeni wafungwa walime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msongamano wa mahabusu kwa kweli ni tatizo kubwa sana. Kama nilivyosema kwenye taarifa yetu, kuna watu wamekaa Magerezani kwa miaka mine mpaka mitano kwa makosa ya mauaji na madawa ya kulevya; kitu ninachongojewa ni kitu kinaitwa High Court Session. Polisi na Mahakama zimefanya kazi nyingi sana za kesi ndogo ndogo, bado hizi kesi kubwa. Mahakama Kuu kuna nini? Kwa nini hambadilishi taratibu za kuangalia kubadilisha huu mfumo wa High Court Session ambao unawaweka mahabusu muda mrefu ndani ya Magereza? Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu, msongamano wa mahabusu ambao unaambatana na hiyo kwa kweli ni suala ambalo linatakiwa lishughulikiwe. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza na tumetoa mapendekezo na maoni ambayo tunaona ni muhimu yaweze kuchukuliwa, isipokuwa cha msingi ni fedha ziende kwenye Balozi nje ya nchi. Mabalozi kule hawana hela. Hela tumepitisha lakini haziendi. Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa mabalozi watatumika sana kwenye diplomasia ya uchumi. Wao wana uwezo mkubwa sana wa kuleta Wawekezaji hapa na watalii. Tuwapelekee fedha, tuwawezeshe waweze kufanya hayo mambo. Hii ni pamoja na Mabalozi ambao wako hapa nje; nyumba nyingi tu; mfano huo wa Sweden ni mmoja, lakini nyumba nyingi za Mabalozi ziko kwenye hali mbaya na zinahitaji kuboreshwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata mchango wa Mheshimiwa Bilago. Warundi wamejaa kwenye Gereza la Kibondo, kwa sababu pale ni mpakani, huwa kuna utaratibu wa mikutano ya ujirani mwema. Waburundi wanakuja na sisi tunakwenda, tunanunua vitu na wao wananunua vitu. Sasa wanapokuja wale, unawakamata kwamba wameingia nchini isivyo halali, unawajaza kwenye Magereza, kwa kweli siyo haki. Waziri wa Mambo ya Ndani na Serikali iliangalie hilo ikafanye mikutano ya ujirani mwema kuondoa hilo tatizo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wanafanya kazi nzuri sana na mpaka sasa hivi wamepunguza uhalifu kwa kiwango kikubwa sana, tukichukulia uhalifu in totality; lakini hawana nyenzo. Bajeti ambayo tumeipitisha hapa kuwapa fedha, hawajapata hizo hela, au kama wamepata, zote zimekwisha. Sasa tusiwafanye Polisi wawe ombaomba, isipokuwa naitaka Serikali iangalie hilo suala na kuhakikisha fedha ambazo tumepitisha hapa, basi Polisi wale wanapewa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Madawa ya kulevya ni tatizo kubwa, watoto wetu wameharibika, Watanzania wanakamatwa sana huko nje. Sisi tunaweza kuwafuatia Nigeria sasa hivi. Kwa hiyo, wamejaa kwenye Magereza ya nje, ni vita. Nami naomba tutakaporudi kwenye Majimbo yetu tuwasaidie kutoa taarifa ya wote wanaohusika na madawa ya kulevya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, Makamanda wa Mikoani wa Polisi na Makamanda wa Wilaya, wana jukumu kubwa sana la kuwasaidia Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Ni lazima wafuate taratibu za upelelezi. Taratibu za upelelezi zipo wazi. Upelelezi ni profession jamani. Kuna doctorate ya investigation inachukuliwa. Upelelezi hauendi hivi hivi. Huwezi ukatoa upelelezi kwa kutaja watu majina, hakuna! Mimi sijawahi kuona kitu kama hicho. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba Makamanda wa Polisi na wa Wilaya, waangalie. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo Police General Orders, Police Force Ordinance na Criminal Procedure Act ambazo zinaeleza kabisa namna ya Polisi kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo, kinachotakiwa ni kukaa pamoja na hao Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwasaidia. (Makofi) Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka wakati Mheshimiwa Lyatonga Mrema alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, mimi nilikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam na alifanya kazi kubwa sana, lakini kulikuwa na kazi nyingine anakwenda nje, kinyume. Nikasema tukimwacha Mheshimiwa Lyatonga aende hivi, ataharibu kesi Mahakamani. Ikabidi Wakuu wakae na Mheshimiwa Mrema, wakaelekezana taratibu za kufanya na Polisi walimpa support na mambo yakawa yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya wakae na Wakuu wa Mikoa wao na Wakuu wa Wilaya zao, waangalie na kuwashauri namna ya kugawanya hizi kazi. Hawa Makamanda wamesomea, wanaelewa. Wamekwenda kwenye vyuo mbalimbali, wanaelewa taratibu. Hatutaki waharibu hizi kesi nzuri au hii operation nzuri ambayo imeanza ili kesi hizi ziende kufa kule Mahakamani. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba yote ambayo mmeyaongea na kushauri tutayachukua na tutaweka kwenye maazimio yetu na ninawahakikishia kwamba tutaunda Kamati Maalum ya kufuatilia yote ambayo tumeyasema ili kuhakikisha kwamba kabla hatujatoa report nyingine mwaka kesho, basi tutatoa utekelezaji wa maazimio haya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kamati ya Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi na Usalama, napenda kuwasilisha taarifa yangu na naomba kutoa hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa leo kuniweka hapa.
Pili, ningependa kuwashukuru Wanamuheza ambao wakati wa kampeni niliwaomba wanilete kwenye jengo hili na wamenileta, nawashukuru sana tena sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono Hotuba ya Mheshimiwa Rais moja kwa moja kwa asilimia mia moja. Mheshimiwa Rais kwenye hotuba hiyo ameainisha mambo chungu nzima; nilikuwa nasoma mstari kwa mstari na nilikuwa na-underline, nilipofika mwisho wa kitabu
nikakuta nime-underline mistari yote kwenye kitabu hicho. Kwa sababu kila point, kila mstari ambao nilikuwa nauona, niliuona ni wa msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hotuba hiyo, lakini ningewaomba Waheshimiwa Wabunge waangalie namna Mheshimiwa Rais alivyokuwa anai-present hotuba hiyo, seriousness aliyokuwa nayo, commitment aliyokuwa nayo siku ambayo alikuwa anaiwasilisha hotuba hiyo na baada ya hapo matendo yake baada ya hiyo hotuba! Jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameainisha matatizo ambayo sijui ameacha tatizo gani kwenye hii hotuba. Ameanzia na huduma za jamii, matatizo yote yapo pale, matatizo ya maji, umeme, barabara, kila kitu kiko pale. Tatizo moja kubwa sana ambalo wote
humu Waheshimiwa Wabunge tunalo, isipokuwa wananchi wa Muheza wanalo zaidi ni la maji.
Wanamuheza wana shida ya maji! Yapo matatizo ya umeme, lakini umeme umefanyiwa kazi kubwa sana, REA imefanya kazi kubwa sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iangalie uwezekano, utaratibu ambao umetumika kwa REA, utaratibu huo utumike kwa maji vijijini. Wananchi wana taabu, sikupata nafasi ya kuchangia jana, lakini nina hakika Waziri wa Maji yuko hapa atahakikisha kwamba, kweli suala la maji linapewa kipaumbele kwenye bajeti inayokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila kuangalia matatizo hayo; sasa hivi tunakwenda kwenye sera ya Tanzania ya viwanda. Hatuwezi kujenga viwanda bila kuangalia kwanza haya matatizo ya umeme na maji tuyashughulikie, matatizo ya barabara, hivyo viwanda vitakavyopelekwa
huko, barabara zitapita wapi. Naamini Mheshimiwa Rais kutokana na ahadi zake alizozisema, kutokana na commitment ambayo anayo kwamba ahadi alizozitoa zitatekelezeka. Tumeona ahadi zinaahidiwa nyuma, kuna barabara yangu kule ya Amani mpaka Muheza kilomita 40,
awamu mbili zilizopita zimeahidi kwa kiwango cha lami barabara hiyo, lakini hakuna lami iliyowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Amani wanavuna, sasa hivi kuna viungo, kuna chai ambapo sasa ni wakati wa kuvuna viungo hivyo, wanashindwa kuteremsha mazao hayo, wanapata taabu kila saa magari yanakwama. Naamimi kabisa kwamba Waziri wa Ujenzi yupo hapa na ataliangalia suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia suala la viwanda, Tanzania ya viwanda, lakini naamini kwamba Waziri wa Viwanda ataangalia kiwanda kipi ambacho kinatakiwa kiwe wapi na mkoa gani ambao unatoa zao gani. Tuanze kufufua viwanda ambavyo vilikuwepo kabla ya kufikiria kuanza kujenga viwanda vingine, lakini Kiwanda cha Machungwa Muheza kianze kujengwa mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanga kulikuwa na viwanda chungu nzima, viwanda vimekufa pale; ningefurahi sana kuona kwamba viwanda vile vinaaza kufufuliwa na wananchi wa Mkoa wa Tanga basi wanaanza kufaidika na viwanda hiyo. Kuna mazao chungu nzima ambayo yako Tanga na ambayo naamini kabisa kwamba kama viwanda hivyo vitafufuliwa basi tutakuwa na uwezo wa kujenga uchumi wetu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kuna mambo mengi ambayo yamezunguka Tanga, hapa imezungumzwa reli ya kati tu, reli ya Tanga - Arusha mpaka Musoma hadi Nairobi imesahauliwa kabisa. Ningefurahi na ningeshukuru kama ningekiona kitu hicho kwenye Mpango huu wa Bajeti ambao unakuja. Vivyo hivyo pamoja na Bandari ya Tanga, tunazungumzia mambo ya Bandari nyingine tunaacha Bandari ya Tanga ambayo ni bandari kubwa kabisa pale, kwa nini hatuizungumzii? Naomba Waziri anayehusika aliangalie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu; Serikali imeanza vizuri kabisa. Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya elimu bure na imeanza kutekelezwa. Lazima tuwe na pa kuanzia, matatizo madogo madogo yanaweza kuwepo, lakini lazima tuweke sehemu ya kuanzia. Tumeanza vizuri na naamini wananchi wote nchi hii wamefurahi kwamba elimu imekuwa bure. Hayo matatizo ambayo yanatokea hapo yatarekebishwa. Tusiikatishe tamaa Serikali hii kwa jinsi walivyoanza, tuwaunge mkono Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna shule nyingi ambazo zinaishia darasa la kumi na mbili (form four), lakini tuna shule chache sana za Serikali za kidato cha tano na cha sita.
Umefika wakati sasa hivi Serikali iondoe ukiritimba ambao upo wa kusema kwamba lazima shule za Serikali za form five na six ziwe boarding. Tunahitaji sasa hivi iwe day, watoto wetu waweze kusoma kwa sababu sasa hivi shule zimekuwa nyingi, lakini za form five na six zimekuwa ni chache, naomba mliangalile.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Mheshimiwa Rais ameongelea suala la wawekezaji, lakini ni lazima tuangalie na tukubali kwamba maandalizi yetu ya wawekezaji not friendly, bado kuna matatizo mengi sana EPZA, TIC, bado kuna ukiritimba mkubwa sana ndiyo maana
wawekezaji wanatoka hapa wanarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Mabalozi tuna Sera ya Diplomasia ya Uchumi, tuliambiwa tulete wawekezaji, tunawaleta wawekezaji, wanarudi. Kuna leseni sijui karibu 18 mara ya mwisho nilipokwenda TIC pale au vibali ambavyo mwekezaji anatakiwa apewe. Unategemea
huyo mwekezaji atawekeza kweli, jamani tuangalie hilo suala na kama mnataka Mabalozi watekeleze kweli Economic Diplomacy, basi tuhakikishe kwamba huu ukiritimba na huu urasimu unaondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la utulivu na amani, Waheshimiwa Wabunge, lazima tukubali kwamba uchaguzi huu tumeufanya kwa utulivu na amani. Kama kulitokea uvunjivu wa amani, ni kidogo, lakini kazi ambayo wamefanya vyombo vya dola ni kubwa jamani. Ninyi hamuelewi namna ya kutuliza utulivu wa amani, ni kazi kubwa, vyombo vya dola vilikuwa havilali, ni lazima tuvipongeze na tuviunge mkono vyombo vyetu jamani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Balozi muda wako umekwisha.
MHE. BALOZI. ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kumalizia kwa
kusema kwamba….
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha naomba ukae tafadhali.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia bajeti ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda kumshukuru sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Napenda kumshukuru kwa jinsi alivyoanza kuendesha Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa nguvu, kwa kasi na kwa weledi mkubwa na kwa vitendo na sio blah blah. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia tukiwa na mipango mingi, miradi mingi, maneno mengi lakini sasa hivi tumepata mtu ambaye anaonesha vitendo. Rais ambaye anaonesha kitu gani ambacho kinatakiwa na sio kuzungumza blah blah. Kwa muda mrefu tumekuwa na sera nyingi lakini ndugu zangu mtakubaliana nami kwa kipindi kifupi mmeona vitendo ambavyo amefanya. Amechukua hela kutoka mafungu mbalimbali na kuyapeleka kwenye mambo muhimu ambayo yanawagusa wananchi wa kawaida kama mambo ya barabara, vitanda hospitalini, madeski ya shule na mambo kadha wa kadha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu nimefurahi sana na nashukuru kupata mtendaji wa aina hiyo. Nchi yetu sasa hivi inataka kiongozi wa aina hiyo anayeweza kutoa amri, kutekeleza na kufuatilia. Naamini kama Rais Magufuli angekuwa amechukua mafunzo ya komandoo basi miezi sita tu hii nchi ingeweza kuwa kwenye mstari ambao unatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kupongeza uongozi mzima kwa jitihada kubwa ambazo zimefanyika hivi karibu mpaka tumepata mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Kampala na kuyaleta kule kwenye bandari ya Tanga. Mradi huo ni mkubwa na lazima uende sambamba na sehemu ambazo bomba hilo litapita kwa kuonesha wananchi watafaidika namna gani. Bandari ya Tanga kama mlivyosikia ina kina kirefu kuliko bandari zote na ndiyo moja ya sababu iliyofanya tupate mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningefurahi sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kama wangechambua sasa hivi hiyo bajeti ambayo ipo, wahakikishe kwamba wanaimarisha vitu vyote ambavyo vinahitajika kwenye bandari ya Tanga, kuna vifaa ambavyo ni vichakavu sana kwenye bandari ile. Vifaa vyote hivyo na mambo yote hayo ambayo yanatakiwa ni lazima tuhakikishe kwamba bandari hiyo inaimarika ili tuweze kukabiliana na huo mradi ambao unakuja.
Ningeshukuru sana kama reli ya Tanga na yenyewe ingewezwa kuimarishwa. Najua imewekwa kwenye bajeti lakini nitashukuru kama na yenyewe inaweza kuwa kwenye standard gauge ili iweze kuungana na reli ya kati iweze manufaa makubwa kwenye mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru pia kama kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Tanga kitaimarishwa kwa sababu sasa hivi kutakuwa na watu wengi, wimbi litakuwa ni kubwa, kwa hiyo, tunaomba uwanja huo na wenyewe uweze kuwekwa kwenye mpango huu na kuweza kuimarishwa kwa kupanuliwa tayari kwa kupokea wageni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, sisi Muheza bomba hilo litapita, tunataka kutayarisha kituo cha matunda (center ya matunda) kuhakikisha kwamba kwa mradi huo panakuwa na additional value ili kuona tunafaidika vipi na mradi huo. Kwa hiyo, tumeshatayarisha sehemu za wawekezaji kuhakikisha kwamba tunatengeneza sehemu ya matunda, tunataka Mji wa Muheza uwe mji wa matunda. Matunda yote ya Mkoa wa Tanga yaweze kupatikana kutokea Muheza. Tumeshaanza kukaribisha wawekezaji na tungeomba Serikali ituunge mkono kwenye hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo lakini vitu hivyo vinakwenda na miundombinu, ni lazima tuhakikishe kwamba tunaziimarisha barabara, mkoa wa Tanga tuna barabara ya Muheza kwenye Jimbo langu, barabara ambayo Serikali imeahidi kuiweka lami, barabara ya Amani mpaka Muheza. Amani kutoa vitu chungu mzima, kuna viungo, karafuu, pilipili manga, kuna vitu vingi sana na wakulima wa kule wanapata taabu sana kuleta vitu hivyo mjini. Pamoja na kuweka kituo cha matunda tuna mpango tuweke viwanda vya kusafishia viungo ili kuhakikisha kwamba Muheza inakuwa ni Muheza kweli kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna tatizo la maji ambalo tumeanza kulishughulikia kwa kumuomba Waziri anayehusika lakini ningeomba liwekewe mkazo. Bila maji Muheza haiwezi kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nichangie suala la utalii. Vivutio ambavyo tunavyo nchi hii haviendani na watalii waliopo. Hatuwezi kusema tunakadiria watalii milioni 1.2 wakati tuna National Parks karibu 15, uwiano wake haupo. Kuna nchi ambazo zina kivutio kimoja tu, mimi nilikuwa Zimbabwe wana Victoria Falls tu lakini wanaingiza watalii milioni 2.5 kwa mwaka, sasa ni kwa nini sisi tushindwe kufanya vitu kama hivyo? Naomba suala hilo liangaliwe na tuone tunaweza kufanya nini kuweza kuongeza watalii. Kuna sehemu nyingi sana za utalii, Amani kule Muheza ni sehemu mojawapo ya watalii ila wanashindwa kwenda vizuri kule kwa sababu ya barabara. Naamini tutakapoiweka lami ile barabara kutakuwa na ongezeko la watalii sehemu za Amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo ni muhimu na linakwenda sambamba kabisa na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya viwanda. Bila kilimo, mazao na malighafi hatuwezi kufika. Tuchukue mifano ya nchi nyingine ambapo wanawawezesha wakulima, wanawakopesha pembejeo, wanawapa mbolea bure halafu baadaye wanakuja kuelewana na Serikali namna ya kuwakata. Kwa hiyo, naamini tukifanya hivyo tutaweza kuhakikisha kwamba wakulima wetu wanaweza kufaidika na kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda kuunga mkono bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ahsante sana.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Viwanda. Pia nawashukuru wapiga kura wangu, Wanamuheza kwa kuendelea kuniamini na kuweza kunifanya niendelee kuongea hapa leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda ni Wizara muhimu sana. Ni Wizara muhimu kwa sababu inaendana na malengo ya Awamu ya Tano; wananchi wa Tanzania wengi wana mategemeo makubwa sana na Wizara hii; wana mategemeo ya mabadiliko mengi sana kwenye Wizara hii; wana mategemeo ya kupata ajira nyingi kutokana na viwanda ambavyo Awamu ya Tano inategemea kuviweka. Kwahiyo, Wizara hii ni Wizara ambayo ni ya muhimu na Wizara ambayo tunaitegemea itakuza uchumi wetu, italeta ajira nyingi na itatuondolea umaskini kwa kiwango kikubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda ambavyo vilikuwepo tangu enzi za Mwalimu ni viwanda vingi, lakini vile viwanda vingi vimekufa. Sasa hivi kinachofanyika ni kutaka kuvifufua hivyo viwanda. Mkoa wa Tanga ulikuwa ni mmoja wa Mkoa ambao tulikuwa tunaongoza kwa viwanda hapa nchini.
Tuikuwa na viwanda karibu 180 na sasa hivi viwanda ambavyo viko ni 50 tu, ndiyo viwanda vikubwa na vidogo ambavyo tunaweza kusema kwamba ndio vinafanya kazi katika Mkoa wa Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama alivyosema Waziri kwenye hotuba yake kwamba malengo ya kwanza ni kuanza kuvifufua viwanda hivi, lakini hatuwezi kufufua viwanda hivi kama hatujajua vile vilivyokufa vilikufa kwa sababu gani. Kwa hiyo, tutakapovifufua viwanda hivi tutakuwa tunajua kwamba vile ambavyo vimekufa vimekufa kwa sababu gani, tusirudie hayo makosa tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muheza ni sehemu mojawapo tulikuwa na kiwanda. Tulikuwa na kiwanda cha matunda. Matunda ambayo yanazaliwa Muheza ni matunda ambayo yanajulikana hii Afrika na ulimwengu mzima. Sisi tunaweza kutoa matunda tani 100,000 kwa mwaka. Ni matunda ambayo yanaweza kuwa ya pili au ya tatu katika Bara la Africa baada ya South Africa na Egypt.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Muheza tunatoa machungwa mengi, lakini sasa hivi hatuna kiwanda cha machungwa. Wanakuja Wakenya, wanajaa pale, wanajaza hoteli za Muheza, miezi miwili iliyopita ilikuwa ukija Muheza huwezi kupata nafasi kwasababu wamejaa Wakenya pale kuchukua machungwa yetu ku-cross kupeleka Mombasa kwenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nategemea Mheshimiwa Waziri, atakapokuja ku-wind up kwenye hotuba hii, atatoa matumaini ya kiwanda cha matunda cha Muheza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuhitaji kiwanda cha matunda Muheza, lakini pia tunazalisha viungo vingi kuna pilipili manga, hiliki pale baada ya Zanzibar, kuna karafuu na mdalasini. Wanakuja watu kutoka nchi za nje wanajaa Wilayani pale kwa ajili ya kuchukua malighafi hizo na kuzipeleka nje. Kwa nini tusiweke hata kiwanda kidogo pale? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ame-present hotuba yake kwa nguvu sana na inaonekana inatoka moyoni kwake. Kwa hiyo, tunategemea utekelezaji wake utakuwa ni mkubwa ili wananchi wa Muheza na wenyewe waweze kufaidika na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kwamba viwanda hivi basi vitakapozalisha vitalindwa. Nimefurahishwa sana na Mheshimiwa Rais aliposema kwamba kuanzia leo basi furniture zote za maofisini ziwe zinatokana na malighafi yetu ya humu humu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna kiwanda chetu cha kamba, kama unavyojua katani, ni zao letu kubwa Mkoani Tanga, ni zao letu kubwa Wilayani Muheza. Kiwanda cha Ngomeni cha kamba ambacho ni kiwanda kikubwa Afrika Mashariki na Kati, ni kiwanda kimojawapo ambacho watu wanalipa hela kabla hata hawajapata hayo mazao yake ambayo wanayataka pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunategemea kwamba kiwanda kile kinatakiwa sasa kisaidiwe na Serikali. Nilikwenda pale na kuongea na uongozi, wakaniomba. Wao wanaomba kitu kimoja tu, wanaomba Serikali iwape tender ya wao kutengeneza mazulia ya maofisi zote za Serikali kwenye nchi hii na uwezo huo wanao, ni suala la kubadilisha zile mashine zao pale na kuwapa mashine nyingine. Mheshimiwa Mwenyekiti, namtegemea Waziri ataweza kuwapa upendeleo kiwanda hicho, kukuza kiwanda hicho kiweze kuzalisha mazulia yote ambayo yanatengenezwa kwenye ofisi zote za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee suala la EPZA. Kwanza nawashukuru sana EPZA kwa sababu wameweza kujaribu kuweka maeneo ambayo wawekezaji wakija wanaweza wakaoneshwa, ni hatua moja nzuri sana. EPZA imejikita zaidi kwenye Foreign Direct Investment (FDI). Vitu vyote wanaelekeza nje, vinapelekwa nje; vikitoka kule, vinatengenezwa, then vinarudishwa hapa hapa. Sasa nilitaka wapanue wigo wa kuweza kuwafanya Watanzania na wenyewe waweze kuelimika na kuwa wataalam na waweze kufanya vitu hivyo wao wenyewe na kuviuza hapa hapa nchini; kuleta mashine ambazo zinaweza kufanya kila kitu hapa hapa nchini na kuweza kutoa mali ambayo inaweza kuwa ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga tunataka tufaidike na bomba hili la mafuta la kwenda Kampala.
Kwanza tunaisifu sana Serikali kwa kuweza kupata hiyo zabuni ya kutengeneza hilo bomba la mafuta, lakini tunataka tuhakikishe kwamba tunaongeza value kwenye hilo bomba ili wananchi wa Tanga, wananchi ambao bomba hilo litapita sehemu zote, waweze kufaidika nalo. Wanaweza kufaidika nalo namna gani?
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja, na ningependa kuchangia kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika hoja hii. Elimu ndiyo msingi wa mambo yote hapa Duniani, yapo mambo ambayo yanatakiwa kuboreshwa ili tuzidi kuongeza ubora wa elimu yetu. Kwa mfano, mitaala yetu inabidi iangaliwe upya, tujaribu kuangalia mitaala ya nchi zingine zinazofanya vizuri ili tuiboreshe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitengo cha Ukaguzi cha Wizara inabidi kiimarishwe, sikumbuki au kusikia Wakaguzi wamekuja Muheza. Hawa ndiyo wanaweza kuboresha mambo mengi ni watu muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu mkubwa wa Walimu Muheza. Ingawa ni suala lililopo TAMISEMI shule za msingi na sekondari zote, ninaomba uliangalie kwa umuhimu wake, kuna shule zingne zina walimu wawili na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara sasa ni vizuri ifikirie kuanzisha mitihani mara mbili kama wenzetu wengi badala ya kungojea mwaka mzima kwa O- level na A- Level. Pia maslahi ya walimu yaangaliwe kwani inaonekana kama wamesahulika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msisitizo mkubwa naona Muheza High School ambayo ni hiyo tu Wilaya nzima ifanywe ya kutwa na bweni ili iweze kuhudumia ongezeko la wanafunzi wa „O‟ Level Wilaya nzima. Shule hiyo ilijengwa kwa nguvu za wananchi na ina uwezo mkubwa wa kuchukua wanafunzi wengi zaidi. Wizara isimamie TAMISEMI kuona vifaa vya maabara shule za sekondari vinapelekwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye bajeti hii ya mtoa hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ningependa kusema kwamba bajeti hii kwa kweli haikututendea haki Mkoa wa Tanga. Bajeti hii haiku-take into consideration kwamba sasa hivi tumepata tender, tumepata zabuni ya kutoa mafuta kutoka kule Ohima, Lake Albert - Uganda mpaka Tanga kwenye bandari ya Tanga. Lakini ukiangalia kitabu hichi hakizungumzi hata kidogo, hakuna hata mstari mmoja unaozungumzia kwamba Bandari ya Tanga itaboreshwa namna gani? Sasa hivi Bandari ya Tanga ina matatizo mengi, Bandari ya Tanga ina vitu ambavyo ni vichakavu, hata mashine za kubebea makontena ni taabu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hizi mashine za tag boats ambazo zinatakiwa kwenda kufunga meli baharini. Mashine ziko mbili, moja ni mbovu kabisa na nyingine tumekodisha kutoka Mombasa. Sasa sioni chochote ambacho kinaelezea mambo ya standard gauge kuhusiana na reli, sioni chochote ambacho kinaelezea kuhusiana na airport ya Tanga, mambo yote ambayo yanazungumzwa hapa ni standard gauge ya reli ya kati, au kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wako kwenye mstari wa reli ya kati basi Tanga tunasahaulika? Kwa nini Tanga tunasahaulika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana hapa Wabunge wa reli ya kati walikutana, sasa jamani Mheshimiwa Waziri nini sisi Tanga tumekukosea? Tumepata tender na hutaki kutupa chochote. Nimeona hapa maboresho ya Bandari ya Tanga ni shilingi milioni 7.6 kweli, are we serious? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahamia sasa Jimboni kwangu kuna barabara kule, nimeangalia kwenye Hansard tangu mwaka 2000 barabara ya Amani - Muheza kilometa 40 imeanza kuzungumziwa, kwamba ijengwe kwa kiwango cha lami. Awamu ya Nne Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aliahidi kuiweka barabara hiyo lami, Rais, Mheshimiwa Magufuli ameaihidi kuiweka lami barabara hiyo, Mheshimiwa Rais Mkapa ameiahidi kuiwekea lami barabara hiyo, na watu wote wa Amani wanategemea kwamba barabara hiyo itawekwa lami. Sasa hivi naangalia kwenye kitabu hapa naona shilingi milioni 250, nilitaka kuzirai Profesa, kwa sababu nitawaambia nini watu wa Amani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inategemewa kule, uchumi wa Muheza unategea Amani, mazao ambayo yako Amani ni kitukingine. Amani kuna kila kitu, kuna si mambo ya utalii tu, mbao, karafuu, chai, hiliki, pilipili manga na mdalasini zote zinatoka kule.
Sasa mimi nitawaambia nini watu wa Muheza jamani? Nategemea kwa kweli Mheshimiwa Waziri utakapo-wind up jioni basi ueleze chochote ambacho kitahusiana na barabara ya lami ya Amani, Bandari ya Tanga, reli standard gauge tunataka Tanga na kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Tanga utakifanya nini. Sioni chochote wala hata kugusiwa hakikugusiwa; na sasa hivi tunategemea kwamba mambo yatakuwa moto moto Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeahidiwa kilometa tatu, Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli alifurahi wakati wa kampeni jinsi uwanja ulivyojaa, akasema Muheza mmenifurahisha nawapa kilometa tatu za lami vumbi limezidi, na hizo kilometa tatu mtazipata kabla ya mwezi wa sita; mpaka sasa hivi sioni kitu. Nimeangalia kwenye kitabu kuanzia page ya kwanza mpaka ya mwisho sioni chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa kwa kweli utueleze na uwape matumaini watu wa Muheza hizo kilometa tatu za kuondoa vumbi Muheza utazifanya vipi, nitazipata namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala mengine niliwahi kuwasiliana Mheshimiwa Waziri, hakuna mawasiliano huko Amani ambako ndiko kwenye uchumi wetu Muheza. Hakuna mawasiliano Amani, Zirai, Kwezitu, Mbomole kote kule huwezi kuongea na simu, ukiongea na simu mpaka upande juu ya miti ama kwenye kichuguu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana nategemea kwamba Mheshimiwa Waziri labda atakuja na majibu, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kupata fursa hii kuweza kuchangia hoja hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili, jambo la kwanza ningependa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Profesa Muhongo. Nampongeza kwa kazi aliyoifanya yeye na Watalaam wake ambao waliwezesha kupata tender ya kutoa mafuta kutoka kule Lake Albert Uganda mpaka Tanga bandarini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kwa dhati kabisa, najua ilikuwa ni kazi kubwa, lakini mwishowe tumeipata! Pia nataka kusema tu kwamba Mheshimiwa Waziri tumepata hiyo kazi tunataka kujua kwamba tutafaidika vipi na hili bomba ambalo litapita kwenye Wilaya yangu na litaishia kwenye bandari yetu ya Tanga. Nafikiria kwamba ni vizuri wakajipanga na Waziri wa Uchukuzi kuona namna gani ambavyo wataweza kupanua bandari ya Tanga. Kuweka vitu vya kisasa kwenye bandari ya Tanga, kuhakikisha kwamba mafuta hayo basi, tunaweza kuyakidhi na kuyahudumia jinsi inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningefurahi sana kama Mheshimiwa Waziri angeitisha kikao ili tuone kwamba tutafaidika vipi, tu-sensitize na wananchi wetu tuweze kuona tunaweza kuongeza value gani kwenye hilo bomba na tunaweza kufaidika nini kwenye hilo bomba.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, pia napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kutokana na mradi wa REA. REA imetusaidia sana, REA imetusaidia kupata Majimbo haya na mpango huu ni mpango ambao unatakiwa uendelezwe hata kwenye Idara nyingine ambapo tutakuja kuchangia kwenye mada zinazofuata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Jimbo langu nafikiri linaweza kuwa ni Jimbo moja kubwa kuliko Majimbo yote hapa! Jimbo langu lina Kata 37, Vijiji 135, Vitongoji karibu 550, lakini mgao ambao umefanyika kwa REA awamu ya kwanza na awamu ya pili, vijiji ambavyo nimepata katika Jimbo la Muheza ni vichache sana! Namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie kwa dhati kabisa aone kwamba hii awamu ya tatu, Jimbo la Muheza linaweza kufaidika namna gani. Nafikiri hatujazidi hata asilimia 40 kwenye mgao ambao tumepata! Vijiji vingi kwenye kila Tarafa, Jimbo lina Tarafa nne na kila Tarafa ina matatizo, kuna vijiji ambavyo havijapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Waziri aangalie, akitilia maanani pia Hale power station tunatoa karibu megawatts inaweza kuwa 20, pia ukijumlisha na Pangani tunatoa karibu megawatts 60. Kuna vijiji ambavyo viko karibu na power stations hizo, lakini usiku wao wanaangalia umeme kwa mbali tu. Kuna Vijiji vya Makole, Mhamba, Kwafungo na Songa vyote hivyo vinaangalia umeme usiku kwa mbali. Ningeomba aangalie kabisa aone ataweza kutusaidiaje!
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu alipoteuliwa tu, ziara yake ya kwanza ilikuwa ni Hale na naamini aliweza kuwaona hao wanavijiji ingawaje Hale haiko kwenye Jimbo langu iko kwenye Jimbo la Korogwe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ningeshukuru na ningefurahi kama angeweza kuliangalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine sasa hivi Muheza tuna matatizo makubwa ya transformer, tunayo transformer ndogo na ambayo ni chakavu. Sasa Serikali inapata lawama kubwa sana ya umeme kuzimika zimika! Tungeomba Waziri atutafutie transformer kubwa, kwa sababu tunataka tufaidike na hilo bomba, tunataka tuifanye Muheza kiwe kituo cha matunda. Sasa kama hatutapata umeme wa uhakika ina maana kwamba hata hivyo viwanda ambavyo tunategemea kuvijenga Muheza vitakuwa ni matatizo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tungeomba sana ajaribu kuliangalia suala hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni Mkandarasi, nilishawahi kumwambia Waziri kwamba Mkandarasi Sengerema ana kazi nyingi sana! Speed anayokwenda nayo ni ndogo sana! Sasa nafikiri ni muhimu akampunguzia kazi ili tuweze kupata Mkandarasi mwingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Waziri kwa juhudi zake za kuhakikisha zabuni ya bomba la mafuta kutoka Ziwa Albert- Uganda hadi Bandari ya Tanga inafanikiwa. Namwomba aangalie uwezekano wa kusaidia vyombo mbalimbali bandari Tanga kwa sababu ni chakavu ili tupate vyombo vya kisasa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Waziri kwa mradi wa REA. Mradi huu ni moja ya sababu zilizotufanya tuingie Bungeni. Binafsi nina eneo la Jimbo kubwa kuliko Majimbo yote hapa Bungeni. Nina kata 37 na vijiji 135. Vijiji ambavyo nimefanikiwa kupata umeme ni asilimia ndogo sana ambayo haizidi asilimia 50. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri REA III nipate mgao mkubwa. Nimetuma orodha ya vijiji 100 kwa kuanzia. Aidha, naomba anitatulie tatizo la transformer Mjini Muheza, kila siku umeme unakatika sababu ni uchakavu na ni dogo, limeelemewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkandarasi Sengerema apunguziwe kazi. Kasi anayokwenda nayo kwenye mradi wa REA hairidhishi, anafanya taratibu sana. Aidha, utaratibu wa kuwekewa umeme usiruke kijiji kupunguza malalamiko ya vijiji vinavyorukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la madini, ni kwa nini Serikali isianze mipango maalum ya kujenga kiwanda kikubwa cha kuanza kusafisha madini yetu hapahapa nchini. Mipango hii imekwishaanza nchi nyingine kama Zimbabwe, Botswana na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ni lazima iangalie uwezekano wa kuweka maeneo maalum ya madini ambapo wawekezaji wakija wanaweza kuonyeshwa moja kwa moja badala ya wawekezaji kuzungushwa. Aidha, wale walioshika maeneo bila ya kuyaendeleza wanyang‟anywe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupata fursa hii ya kuweza kuchangia hoja hii ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kwanza, napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Lukuvi alikuja Muheza na alituletea ahueni kutokana na ziara yake hiyo. Wananchi wa Muheza wanamshukuru sana kwa sababu aliweza kurudisha mashamba karibu matano ambayo yanaonekana kwenye ukurasa wa 104 wa hotuba yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo ya katani yamekuwa ni ahueni sana kwa wana Muheza kwani yalikuwa yanawafanya wana Muheza wawe vibarua tu wa mashamba ya katani. Sasa hivi tunatengeneza mipango maalum ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na master plan ya Wilaya ya Muheza ili kuhakikisha kwamba mashamba hayo ambayo tumeyapata yanakuwa kwa manufaa ya wana Muheza. Wananchi watagawiwa maeneo yao ambayo yapo na tutatenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu muhimu sana ambacho tumekiweka na tunakisisitiza na tunahakikisha kwamba kwa kweli tunataka kuibadili Muheza. Nashukuru kwamba Waziri wa Viwanda yuko hapa, Waziri wa Kilimo yuko hapa, Waziri wa Miundombinu yupo hapa, Waziri anayeshughulika na TANESCO yuko hapa, Waziri wa Maji yuko hapa, tatizo sasa hivi linalotupata ni miundombinu, hatuna tatizo tena la ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua baadhi ya mashamba hayo yamevamiwa, lakini wana Muheza ni watu waungwana tutakaa chini, tutaongea na tutaona namna ya kutatua tatizo hilo. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na tunataka kuhakikisha kwamba ardhi hiyo tunaitumia ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ni kwamba, yapo mashamba mengine ambayo bado hayajafutiwa hati. Mashamba ambayo yameshafutiwa hati ni kama shamba la Lewa, Bwembwera, Luhuwi, Kilapula, Kwa Fungo, Kihuwi lakini shamba la Kibaranga na Azimio bado sijayaona kwenye hiyo list. Kwa hiyo, tutashukuru kama mashamba hayo pia na yenyewe yataweza kufutiwa hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo pia mashamba ambayo wanamiliki watu lakini hawalimi katani jinsi inavyotakiwa kulimwa. Wengine wanalima katani pembeni pembeni ili ukipita uone kwamba hili shamba linalimwa lakini ukienda katikati kuna pori kubwa sana. Nitampa Mheshimiwa Waziri list ya mashamba hayo na yenyewe pia tufanye mpango kwa wote ambao wanaweka mapori Muheza, mashamba hayo tuweze kuwanyang’anya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri alipokuja alijionea mwenyewe watu walikuwa wengi sana, migogoro ya ardhi ni mingi sana na hii ambayo imeoneshwa kwenye page 33 kwamba ni migogoro sita ipo mingine ambayo sijaiona hapa na ambayo nitaiorodhesha na kumkabidhi. Hata hivyo, napenda kumshukuru kwamba migogoro hiyo imeanza kushughulikiwa. Mwezi uliopita timu yake ilikuwa Muheza na imeanza kutatua migogoro hiyo, napenda kumpongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migororo hii ya ardhi najua iko mingi, lakini nina hakika kwamba yote tutaitatua kwa wema tu na tutaelewana vizuri na wananchi wataelewa vizuri tu. Kwa hiyo, hii mingine iliyobaki Waziri pamoja na timu yake ningefurahi sana kama ningeambiwa watarudi ili waweze kushughulikia matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba linafanya kazi nzuri ya kujenga nyumba, lakini kama walivyosema wenzangu tatizo kubwa ni bei zake, VAT iliyoko pale ni hela nyingi sana haina unafuu wowote kwa mwananchi. Sisi Muheza tumeshawapa eneo sehemu za Kibanda lakini tungeomba msukumo wa Waziri, tunataka wajenge nyumba za bei nafuu ili wananchi wa Muheza waweze kununua nyumba hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Rais ameshatoa maelekezo haya mashirika yetu sasa yawekeze kwenye viwanda na mashamba na sisi tunayo mashamba na sehemu za kuweka viwanda. Ningependa shirika hili liwe mfano waje Muheza tuwape eneo waweke viwanda, tunataka kutengeneza kitu kinaitwa economic corridor ya Muheza. Kwa hiyo, nafasi tunazo na ningeshukuru sana kama National Housing watakuwa wa kwanza kuja kuwekeza Muheza na tunawakaribisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo tunalo pamoja na kuwa na mashamba hayo ni la vifaa kwenye Ofisi ya Ardhi, kwani vifaa hakuna kabisa inabidi tukodi labda kutoka Korogwe au Mkoani Tanga. Ningeomba Waziri awasaidie wale vijana wa pale ili wapate vifaa vya kupimia, tuanze kazi ya kuangalia tunapima namna gani kufuatana na master plan ambayo tutaitengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumwomba Waziri kwamba awasaidie TIC (Tanzania Investment Center) wawe na land bank inayoeleweka. Wana shida sana pale ya land bank. Wafadhili wanakwenda pale wanataka kuwekeza, wanataka kuleta mambo chungu nzima lakini land bank ambayo wanayo TIC ni ya watu binafsi. Kwa hiyo, ningeshukuru sana kama Waziri atashughulika na kuwasaidia TIC waweze kuwa na ardhi, mwekezaji anapofika anapelekwa moja kwa moja kwenye site na kuoneshwa kwamba ardhi hiyo hapo badala ya mwekezaji kuanza ku-negotiate na mtu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, namtakia Mheshimiwa Waziri kila la kheri na tunamkaribisha Muheza. Wana Muheza wanamkumbuka kwa jinsi alivyowaletea ufumbuzi na tunamhakikishia ardhi hiyo tutawagawia wana Muheza na tutaweka sehemu maalum za uwekezaji na tunawakaribisha sana. Nawashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii kuweza kuchangia hoja hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja hii ni muhimu sana kwa sababu suala la Maliasili na Utalii ni kitu kimoja ambacho ni muhimu na kinachangia pato kubwa kwenye uchumi wa Taifa asilimia 17.3 siyo mchezo. Sasa kuna mambo mengi ambayo yapo ndani ya Wizara hii lakini mimi ningependa kujikita kwenye mambo ya hifadhi na pili kwenye suala la utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo hifadhi nyingi sana lakini kuna hifadhi nyingine ambazo zimesahauliwa, kuna hifadhi ya misitu ya Amani kwa mfano, ni hifadhi kubwa ambayo ina hekta karibu 47,000 na ina mambo chungu nzima ndani yake. Kuna vitu ambavyo viko ndani ya msitu huo ambavyo havipatikani ulimwengu huu. Kuna vipepeo ndani ya msitu huo ambavyo huwezi kuvipata dunia yote hii, kuna kima weupe ambao wako mle, kuna nyoka wa ajabu ambayo mimi nilipata nafasi ya kuyaona pia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yapo ndani ya msitu huo na ambayo naona kama Wizara hii haikuyaona kama ni muhimu na ndiyo maana msitu wa Amani imechangiwa kidogo sana kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukiangalia kwenye page 54, page 61, 62 na 63 ni kama imeguswa tu by the way. Lakini kuna mambo muhimu ambayo yapo huko kwenye msitu wa Amani ni msitu mkubwa na msitu ambao una mambo mengi sana kuna ua ambalo liko pale huwezi kulipata dunia nzima, kule Amani wanaliita Dungulushi. Hili ni ua ambalo lina harufu ambalo likichanganya na mambo ambayo yako kule Amani mambo ya hiliki, mambo ya karufuu sasa ile mandhari yake ambayo unaipata kule ni kitu tofauti sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maofisa wa Mheshimiwa Waziri wamesahau kitu kama hicho kwamba Amani kuna vitu ambavyo ni muhimu, Amani kuna vitu ambavyo ni vya msingi na ingetakiwa waweke umuhimu sana kwenye hifadhi hiyo ya misitu. Pamoja na msitu huu kuwa na hekta 47,000, lakini pia umezungukwa na misitu mingine midogo midogo karibu sita ambayo ipo pembeni yake. Kuna misitu midogo kwa mfano msitu wa Derema, Lunguza, Tongwe Kwani, Nilo, Kambai, Manga, Mlinga yote ni misitu ambayo inazunguka pale Amani na kuufanya ule msitu uwe mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mtafiti mmoja na mtalii mmoja ambaye alitembea hifadhi nyingi hapa duniani na alipofika pale Amani alishangaa sana namna ambavyo hatuupi ule msitu wa Amani. Aliulinganisha msitu wa Amani na Kisiwa kimoja kiko kule Amerika ya Kusini Ecuador, hicho kisiwa kinaitwa Galapagos muangalie kwenye ramani mtakiona. Kuna vitu ambavyo vina vutia zaidi sasa alipoangalia msitu wa Amani akaona msitu ulivyo jaa, ulivyo nona, akasema huu ni msitu kwa ulimwengu na hifadhi ambayo nimewahi kutembea huu unaweza kuwa wa pili duniani. Sasa hii ni kitu muhimu sana ambacho Mheshimiwa Waziri inabidi uangalie na uone umuhimu wa msitu huu ambao una kila aina ya vitu, viumbe mbalimbali ambavyo viko pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msitu huu pamoja na kuwa ni wa asili kuna malalamiko ambayo wananchi wa Derema wako 1,128, ambao wamehamishwa kutoka kwenye ule msitu na kwamba tunaenda kuwapa maeneo mengine na wale wananchi fedha ambazo wamelipwa ni ndogo sana. Wananchi hawa wamezunguka wamekwenda Ikulu karibu sijui mara ngapi? Wamekwenda hapo Wizarani kwako Mheshimiwa Waziri sijui mara ngapi? Na mimi tu nilipokuwa Mbunge hii ni barua yangu ya tatu kukuandikia kwamba hawa wananchi 1,128 kwa nini wamepunjwa wamepewa hela kidogo mimea yao ambayo ilikuwa ndani ya hifadhi kama hiliki, karafuu ilikuwa ni mingi, lakini hela ambayo wamepewa wamekadiriwa ni kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, last week nimepokea barua kutoka Wizarani kwako inasema kwamba kufuatana na sheria hao walitakiwa walipwe sijui kila mche shilingi hizi, jamani, kila sheria general rules ina exception zake, kwa hiyo exception ambayo unaweza kuipa kutokana na umuhimu wa huo msitu mmeamua kuwahamisha hao watu jamani wapeni haki zao. Nitakuja kukuona Mheshimiwa Waziri, lakini ni muhimu sana uangalie namna gani mtaweza kuwapa hawa wananchi ambao wamelalamika, wamehangaika, wamekwenda kila ofisi wamekuja Dar es Salaam sijui mara ngapi kudai hizo haki zao lakini hawasikilizwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hiyo tulisema kwamba hawa tunawahamishia kwenye shamba moja la Kibaranga pale ambalo shamba hilo ni haya ambayo yamerudishwa hati, lakini shamba la Kibaranga bado halijarudishwa hati na Mheshimiwa Lukuvi, Waziri wa Ardhi simuoni hapa lakini nilishamlalamikia kwamba tunasubiri hati inyang‟anywe ya shamba hilo tuweze kuwakabidhi hao wananchi wa Derema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema kwamba kuna mambo mengine ambayo amesahau, kuna Pango la Amboni kule karibu na Muheza, Tanga pale. Sasa lile pango badala ya kuwa utalii limekuwa ni maficho ya magaidi, magaidi wako mle kila siku askari wanakwenda mle, kila siku wanawatoa, sasa sijui limesahauliwa kwamba siyo eneo moja la utalii au ni namna gani? Ninaomba Mheshimiwa Waziri suala hilo pia liangaliwe na hilo pango pia lipewe kipaumbele kwa sababu ni kitu kimoja muhimu sana. Kuna vitu ambavyo viko vya kihistoria kwenye vitu kama hivyo ambavyo tunatakiwa kuviangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Amani pamoja na kuwa na kutengeneza mbao za mitiki ni sehemu moja ambayo tunatengeneza mbao za mitiki, tuna mashamba makubwa sana ya mitiki pale. Mjerumani alitengeneza reli mpaka inafika Amani kwa ajili ya kuichukua mitiki, lakini hiyo reli imekufa na ndiyo maana nilikuwa napiga kelele kwamba ni muhimu tupate barabara ya lami ya kutoka Amani kilometa 40 mpaka Muheza. Kuna mambo chungu nzima ambayo yako pale ambayo yangeweza kuwa facilitated na huo mlima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie suala la utalii kwa haraka haraka, utalii kama unavyoonekana kwa kweli haulingani, watalii ambao wanakuja hapa nchini hawalingani na vivutio ambavyo tunavyo. Tuna mbuga karibu zaidi ya 15 acha hizo hifadhi ambazo tunazo kubwa kabisa hapa ulimwenguni, nasikitika sana kusema kwamba utalii tunaingiza watalii milioni 1.1.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Victoria falls pale Zimbabwe wao Victoria Fall alone na wanaingiza watalii milioni mbili na nusu wanaingia pale kwa mwaka, tuna kila aina, jamani nafikiri Mheshimiwa Waziri inabidi uangalie namna gani ambavyo tunaweza kufanya au kuwafanya watalii waingie nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua njia moja ni hiyo kwamba hatuna ndege na ninashukuru sana kwa bajeti hii kuweka ndege. Watalii wengi wanapenda direct flight akitoka Ulaya moja kwa moja anatua hapa, kwa hiyo naamini kwamba hizo ndege ambazo zimepatikana mtazitumia vizuri na mtazipanga vizuri ili ziweze kutuletea watalii wengi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Mlima Kilimanjaro, ni muhimu sana mimi nilipata bahati ya kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka juzi, mwezi Disemba. Ningefurahi sana mngetengeneza programu ya Waheshimiwa Wabunge wapande mlima huu ili waone huko njiani kukoje, lakini njiani hakulingani na hali halisi iliyopo huko Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vibanda ambavyo viko hapo Horombo, vingine vipo pale Kibo, watu wanalala kwa shida. Mheshimiwa Mbunge mmoja alizungumzia mambo ya vyoo, mimi nilipandia njia ya Marangu naomba viangaliwe. Vile vi-hut vimejengwa miaka sijui mingapi iliyopita, ukienda pale Kibo hut kuna vibanda ambavyo vimejengwa sijui lini? Sasa hii sijui kwa sababu labda viongozi hawapandi ule mlima na kuona matatizo ambayo yako mle, lakini ni vizuri wakayatatua....
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kupata nafasi hii kuweza kuchangia bajeti ya mwaka huu. Kwanza napenda kukupongeza sana wewe kwa ujasiri ambao unao na katika hali ya sasa hivi jinsi ambavyo unaliendesha Bunge hili. Nakupongeza na haya matatizo ya wenzetu yasikupe tabu sisi tunaku-support moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Waziri, Naibu wake na wataalam wake ambao wameweza kutuletea bajeti nzuri ambayo haijawahi kutokea tangu tumepata uhuru. Ni bajeti yenye mwelekeo ambayo inajieleza yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kifupi tu tangu Awamu ya Tano imeingia madarakani imeweza kukusanya mapato mengi sana ambapo nchi yoyote bila kuwa na mapato haiwezi kwenda vizuri. Mapato ni kitu cha msingi kwenye nchi yoyote. Hata ukiangalia wakati wa ukoloni ukusanyaji wa kodi ni kitu muhimu, kulikuwa na kodi za vichwa, kulikuwa na kodi za vipande na kodi za matiti. Zote hizo zilikuwa ni kodi ambazo zinakusanywa kwa lengo la kuweza kupata mapato ya Serikali na kuweza kufanya nchi iweze kuendelea, nchi iweze kutengeneza miundombinu mbalimbali. Ndiyo maana mpaka leo hata wenzetu wa Ulaya watu ambao wanakwepa kulipa kodi wanakwenda jela. Hapa tuna kesi ya mcheza soka bora duniani Lionel Messi ambaye yuko Mahakamani kwa kosa la kukwepa kodi. Sasa huo ni mfano tu wa kuonesha namna gani kodi ni muhimu katika kuendeleza maendeleo ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii kama ambavyo ilivyo asilimia 40 imekwenda kwenye maendeleo, ni kitu ambacho hakijawahi kutokea hapa nchini na imelenga kuleta maendeleo kwenye maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Waziri pia kwenye bajeti hii ameweza kuangalia ni vitu gani ambavyo vinaweza kuboreshwa kwenye huduma za jamii, mambo ya maji, umeme, barabara na mambo mengine kwa lengo la kuweza kupata maendeleo ya haraka hapa nchini. Hii ni pamoja na bajeti ambayo imejikita zaidi kuondoa tozo mbalimbali kwa manufaa ya wakulima. Kuna tozo zimeondolewa, tozo za mazao ya korosho, chai, pamba na kadhalika. Sasa yote haya ni muono wa bajeti hii ambao kwa kweli naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na yote hayo ningependa Mheshimiwa Waziri na wataalam wake wajielekeze kwenye baadhi ya maeneo ambayo ningependa kuyataja. Wakati tunachangia Wizara ya Maji, Wabunge wengi sana walisisitiza suala la Wakala wa Maji Vijijini. Suala hili lingepewa umuhimu wa kipekee kwa sababu tatizo la maji ni kubwa hapa nchini, hata Jimboni kwangu ndilo tatizo linaloongoza. Kwa hiyo, uanzishwaji wa Taasisi ya Maji Vijijini ni muhimu na naomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuliangalia aone kama anaweza kulipenyeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni road toll. Road toll kwenye nchi hii naona halipewi umuhimu, nikiambiwa kwamba kodi yake imeongezwa kwenye mafuta lakini huwezi kuona impact hiyo. Nchi nyingi duniani kubwa na ndogo ukiangalia zimewekwa road toll barabarani. Nashangaa ni kwa nini sisi hatuwezi kuiga na kuona kwamba tunaweza tukapata mapato mengi kutokana na road toll. Naamini kabisa kwenye highway zetu pamoja na matatizo ya barabara zetu kuwa ndogo lakini tukianzisha road toll tunaweza kupata mapato ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la transit good, sasa hivi naambiwa kwamba meli nyingi zinakwepa kuja Dar es Salaam na meli nyingi sasa hivi zinakwenda Beira na Maputo kwa sababu ya VAT ambayo imewekwa kwenye transit goods. Ni vizuri Waziri akaliangalia eneo hilo kama ni kweli akaangalia namna gani anaweza kutoa hiyo VAT ya asilimia 18 ambayo inatukosesha malipo ya transit kwa mizigo ambayo inapita hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni reli ya kati. Naipongeza kabisa kwamba bajeti hii imegusa reli ya kati kwa standard gauge, lakini nasikitika kwamba sijaona reli ya kwetu, reli ya Tanga sijaiona kwenye bajeti hii ambayo nilitegemea hata itaguswa pia. Pia nasikitika sijaona maboresho ya bandari ya Tanga ukitilia maanani bomba tumelipata kutoka Uganda. Kwa hiyo, labda Mheshimiwa Waziri aangalie namna atakavyoweza kupenyeza suala hilo ambalo ni muhimu ili vitu hivyo viende simultaneously, reli ya Tanga pamoja na reli ya kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefarijika sana kuona kwamba tutanunua ndege tatu, ndege ambazo naamini kabisa zitatuletea wawekezaji na watalii wengi. Nasikitika kuona kwamba kwenye suala la watalii Kodi ya Ongezeko ya Thamani imewekwa pale kinyume na wenzetu wa Rwanda na Kenya ambao wameondoa kodi hiyo. Kwa hiyo, hii ina maana kwamba watalii ambao watakuja wote wataishia Kenya ukitilia maanani kwamba wao usafiri wa ndege ni wa uhakika na wanao. Kwa hiyo, ni vizuri eneo hilo pia akaliangalia kama ambavyo ameweka kwenye page yake ya 49. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi ni muhimu na ambalo Mheshimiwa Rais ameliongelea tangu wakati wa kampeni. Mahakama hii inategemea sana ripoti au taarifa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Katika kesi ambazo naamini zitapelekwa kwenye Mahakama hiyo robo au nusu ya kesi hizo zitatokana na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Ni kilio cha Wabunge wengi ambao wameongelea, hivyo ni vizuri wakaangalia eneo hilo, namna ambavyo wataweza kuwaongezea fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la kodi ambayo imeondolewa hasa kwenye maduka ya vyombo vya ulinzi na usalama. Hivi vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa vimezoea maduka hayo na tozo hiyo imeondolewa hasa baada ya kuonekana kuna misuse kwa hao ambao wamepewa hizo zabuni za kupeleka vyombo hivyo. Nimesoma hotuba lakini haielezi mbadala kwamba ni shilingi ngapi watapewa hawa maaskari au walinzi wetu ambao wapo kwenye vyombo hivyo badala ya kununua hivyo vitu kwenye maduka. Kwa hiyo, ningeomba suala hilo pia liangaliwe litakuwaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia suala la makato ya kodi za Wabunge lakini nimeliona kwamba halina mashiko kwa sababu halina basis. Kama suala hili la viinua mgongo vya Wabunge ambalo inatakiwa likatwe kodi mwaka 2020 sielewi kwa nini limeletwa wakati huu wa 2016. Ni vizuri suala hili likaletwa kwenye bajeti ya 2019/2020. Hapo ndiyo tunaweza tukalijadili kwa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumalizia kwa ushauri. Ukiangalia taarifa ya Kamati ya Bajeti inaonekana kuna msuguano au hakuna maelewano yaliyokuwepo kati ya Wizara na Kamati ya Bajeti. Ni vizuri wakikaa na kuona wanaweza kulitatua namna gani na kuangalia mawazo ya Kamati ya Bajeti ambayo wameyatoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimefarijika kuona kwamba bajeti hii isiwe tegemezi kwa wafadhili. Nimeona kwamba hela za nje ambazo zimetengwa ni shilingi trilioni 3.12 lakini ni vizuri kabisa kwenye bajeti ambazo zinakuja tujaribu kujifunza, tujaribu kuelewa kwamba tusitegemee fedha za wafadhili ambazo zinakuja na masharti kemkem. Kwa hiyo, ni vizuri kabisa katika bajeti hii hela za wafadhili ni kidogo, lakini katika bajeti zinazokuja suala hili linatakiwa tuliondoe moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kushauri ni hizi fedha ambazo zimetengwa. Tunategemea kwamba fedha hizi zitakapopitishwa na Bunge hili fedha hizo zote ziwe zinafika kwenye Wizara kama zilivyopitishwa. Vinginevyo kama zitakuwa zinakwenda nusu nusu au mwishowe unakuta kwamba fedha hizo hazifiki itakuwa ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia napenda waangalie hili suala ni kwa nini nchi yetu hatuwezi kutumia currency ya kwetu. Currency zinatumika hovyo hovyo tu, unaweza ukawa na dola au pound unakwenda hapo nje unabadilisha tu, wenzetu hawatumii hivyo. Naamini restrictions ambazo wenzetu wameziweka zinakuza uchumi kwa sababu tutatumia currency yetu. Kwa hiyo, naamini kabisa tutakapotumia fedha zetu tutakuwa na uwezo wa kukuza uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ningependa kuunga mkono hoja na nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda kuwa mdogo, ningependa kuongeza mchango wangu niliozungumza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwaombea wananchi 1,128 wa Derema wafikiriwe kuongezwa fidia, lakini bado hati ya shamba la Kibaranga tunapotegemea kuwahamishia haijapatikana, Waziri wa Ardhi anafahamu suala hili. Wizara ifikirie zaidi kuwaongezea vibali wanavijiji ambao wako karibu na shamba la Tiki. Wananchi hawa ambao ni vibarua wa shamba hilo la Derema wanalalamika kwa kupewa vibali vichache mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ifikirie kuanzisha Chuo cha Hifadhi ya Asili ambacho hakuna hapa Afrika Mashariki na Kati. Muheza tutakuwa tayari kutoa eneo la chuo hicho. Ili kuongeza watalii nchini, pamoja na kununua ndege tatu ambazo hakikisha kati ya hizo zilenge nchi zenye watalii wengi, ni vizuri kuongeza au kuwatafuta tour operators, ambao wanaweza kufungua ofisi hizo kwa wingi nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ifikirie kuboresha sehemu ya kituo cha Horombo ambacho ni njia ya kupanda Mlima Kilimanjaro. Iboreshe kukuza utalii wa ndani ili kuwawezesha wananchi kufika hapo kwa kuwa magari yanafika na wengi wanaweza kufika na kuona milima yote vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari wanyamapori waendelee kupata mafunzo zaidi na waajiriwe wengi kukidhi mbuga zote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii adimu ya kuweza kuchangia hoja hii. Suala la maji ni suala ambalo linamgusa kila mtu katika ukumbi huu. Kila mtu katika eneo lake, katika Jimbo lake ana tatizo la maji na tatizo ni kubwa sana. Ningependa kuchukua ushauri ambao umetolewa hapa wa kuanzisha wakala wa maji vijijini. Ni ushauri muhimu na ni ushauri ambao ni lazima tujifunze na mafanikio ambayo yametokea au yamepatikana kwa REA. REA imetusaidia sana, imesaidia sana kwenye mambo ya Kampeni, sasa ni kwa nini tunashindwa kuanzisha huo Wakala wa Maji Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tabu ambazo Jimbo la Muheza linapata katika suala la maji sijui naweza kufananisha na nini, sijui ni sugu au sijui ni nini, lakini wananchi wa Muheza wana matatizo makubwa sana ya maji. Kuanzia pale mjini mpaka vijijini akina mama wanapata tabu sana ya maji wanashinda kwenye visima, na ukiangalia hayo maji ambayo wanayashindia huku visimani huwezi ukaamini. Wakati wa kampeni nilikuwa nakaribishwa na ndoo na nikaoneshwa maji ni udongo mtupu, maji sio salama kabisa. Kwa hiyo, kuna mambo mengi ambayo yanafanyika ambayo unaona wewe mwenyewe kama binadamu kwa kweli unashindwa. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, tunayo Hospitali teule pale, Hospitali teule ya Wilaya inashindwa kufanya operation kwa sababu hakuna maji, kwa hiyo maji ni tatizo kubwa sana Wilayani Muheza. Nimefarijika kuona kwamba kuna mpango ambao upo ndani ya kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwamba mpango wa kutoa maji kutoka Mto Zigi ambao ni kilomita ishirini na mbili na nusu kutoka Muheza mjini mpaka mto Zigi Amani kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanga wanatumia maji kutoka Mto Zigi na sisi wenyewe hatuna maji tulishakubaliana na watu wa Tanga kwamba na walishayapima kwamba maji hayo yana uwezo wa kutosheleza Muheza na Tanga yote na maji hayo kuna uwezo wa kuweza kukaa kwa miaka 30 ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo umefanyika utafiti wa mwanzoni, sijui imekuja Kampuni moja ya Hispania pale, EUROFINSA, Wizara ya Maji hii, Waziri kwenye bajeti iliyopita hapa Hansard nimeangalia ameahidi kabisa kwamba hao EUROFINSA watakuja na wataweka maji. Upembuzi yakinifu ulishafanyika na nimeona hapa kwenye miradi mikubwa 17 ya maji ambayo tunategemea labda, tunamwombea Mheshimiwa Waziri afanikiwe kupata hizo fedha ili huo mradi uweze kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri kwamba, anafahamu matatizo ya Muheza, amefika Muheza na ndiyo maana kwenye mradi huo ameuweka wa kwanza Muheza. Kwa hiyo, nataka wakati atakapokuja ku-wind up awahakikishie wananchi wa Muheza kwamba maji kutoka mto Zigi safari hii yatateremshwa. Awamu ya Tano imedhamiria na itateremsha maji hayo kutoka Mto Zigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimefarijika kuona kwamba Mheshimiwa Waziri vijijini ametoa fedha ambazo ni karibu bilioni moja point moja na ushehe.
Kwa hiyo, fedha hizo namwomba zije zote, tutahakikisha kwamba maji vijijini Muheza kote wanaweza kupata na tutawachimbia visima na kuhakikisha kwamba maji hayo ni salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuona fungu lolote la kusaidia maji Mjini Muheza. Ningeomba aangalie ataweza kunisaidia namna gani kuweza kuweka at least fedha kidogo katika maji Mjini Muheza, tuangalie uwezekano wa kuvuta maji kwenye visima ambavyo ni vingi na vinatoa maji kwa wingi, kuweza kuyasambaza kwa sababu ardhi ya Muheza ni chumvi kubwa sana ambayo iko pale kiasi kwamba hata ukichimba visima basi yatatoka magadi matupu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitu ambacho Mheshimiwa Waziri anataka kufanya ni kuangalia vile visima vyenye maji mengi na kuangalia jinsi ya kuweza kuyatoa yale maji na kuyasambaza kwenye visima ambavyo viko karibu karibu. Nashukuru sana isipokuwa nilikuwa nashauri kwamba suala hili la maji hasa katika Jimbo la Muheza Mheshimiwa Waziri alipe kipaumbele kwa sababu 2020..
Mheshimiwa Menyekiti, naomba kuunga mkono hoja .
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi hii, kuchangia hoja hii ya Mambo ya Nchi za Nje. Nashukuru sana kwa sababu Wizara hii ni Wizara ambayo ni muhimu sana, Wizara ambayo inatuunganisha na mambo yetu huko nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa tu kukuhakikishia kwamba Mabalozi ambao wako nje, Mabalozi ambao wameteuliwa na Mheshimiwa Rais huko nje wanafanyakazi nzuri sana. Wanafanya kazi nzuri na wanajenga, wanatoa sifa kubwa kwa nchi yetu ya Tanzania. Sisi ambao tumekuwa Mabalozi huko nje tunaelewa uthamini ambao tulikuwa tunapewa, heshima ambayo tulikuwa tunaipata huko nje na consultation nyingi nchi ya Tanzania, Mabalozi ambao wako nje walikuwa wanakuwa consulted kwa ushauri na kwa kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemshangaa sana Mheshimiwa Waziri Kivuli, anapotupiga critic na kutulinganisha na Wajumbe wa Nyumba Kumi Kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli unaweza ukanilinganisha mimi na Mjumbe wa Nyuma Kumi Kumi? Unaweza kumlinganisha Balozi Mahiga na Mjumbe wa Nyumba Kumi Kumi, amekuwa Balozi wetu kwenye Umoja wa Mataifa kwa miaka kemkem mpaka Katibu Mkuu mwenyewe Ban Ki –Moon, akasema kwamba, hapana wewe umefanya kazi nzuri akampa kazi Somalia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa Balozi na kiongozi wa Mabalozi Zimbambwe kwa miaka chungu nzima, Mheshimiwa Msigwa unaweza kusema hivyo kweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi Mheshimiwa Msigwa nilikuonya nikakwambia kwamba, ushauri ambao tunakupa kwenye Kamati, usiuchukuwe ushauri huo ukaugeuza kwamba ndiyo critic na ndiyo ulichokifanya hicho. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingi ambao umeuzungumza hapa ni ushauri ambao tumeupa Wizara kwamba vitu gani muhimu ambavyo wanatakiwa kuvifanya. Sasa yeye kazigeuza kwamba ndiyo critic, ndiyo madongo ya Wizara, hapana hivyo, hatuendi hivyo Mheshimiwa Msigwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema ni kwamba, kazi ambayo wanafanyika huko ni kubwa na heshima ambayo tunaipata huko nje ni kubwa na Mabalozi hawa msiwakatishe tamaa, wanafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia diplomasia ya uchumi, wameleta wawekezaji chungu nzima hapa. Mimi mwenyewe nimeshaleta wawekezaji chungu nzima hapa, wamekuza biashara chungu nzima na nchi yetu na nchi za nje. Jamani tusiwakatishe tamaa, tuzidi kuwaunga mkono, Mabalozi hawa kazi wanayofanya ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokisema sasa hivi, Foreign Policy ya kwetu inabidi ibadilike kwamba zamani foreign policy ilikuwa politically, inakwenda politically, lakini sasa hivi ni lazima twende na hali halisi inavyokwenda duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tumeishauri Wizara kwamba, ni lazima waangalie wanapoanzisha Balozi sasa hivi waanzishe balozi sio politically, waangalie kwamba tunaweza kufaidika vipi kiuchumi na ndiyo maana sasa hivi unakuta kwamba Balozi wana mipango, ambayo tumeshauri, sisi tumeishauri Kamati kwamba ni lazima wahakikishe kwamba wanaanzisha Balozi kwenye zile nchi, ambazo wanaona kwamba tunaweza kupata wawekezaji, kukuza biashara zetu na tunaweza pia kuleta watalii wengi hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na ndiyo maana sasa hivi Wizara ina malengo makubwa sana ya kuanzisha ubalozi kule Uturuki, Qatar, South Korea na sehemu nyingine nyingi. Kwa hiyo, ni suala ambalo tunatakiwa tuwaunge mkono na tuhakikishe kwamba, wanapata fedha za kutosha kwa sababu diplomasia…. aaha!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BALOZI ADADI. M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupata nafasi hii ya kuchangia taarifa za Kamati hii. Kwanza nawapongeza Wenyeviti wote wa Kamati kwa mchanganuo mzuri na mambo mazuri, mapendekezo na maoni ambayo wameyatoa kwenye Kamati zao. Nitajikita kwenye Kamati zote mbili kwa kifupi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kamati ya Katiba nilitegemea sana wangeweka msisitizo pia pamoja na mambo mengine suala la msongamano na ucheleweshaji wa kesi Mahakamani. Kamati hii ya Katiba ina mwingiliano sana na Kamati yangu ya Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi na Usalama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu imetembelea sana Magereza na imeona namna ambavyo mahabusu pamoja na wafungwa walivyosongamana ndani ya Magereza, ni tatizo kubwa sana. Tatizo hili linatokana hasa na makosa mawili tu au matatu. Utaona makosa ya mauaji na makosa ya madawa ya kulevya ndiyo ambayo yanachukua muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahabusu wako wengi sana wa makosa ya mauaji, madawa ya kulevya na Wahamiaji haramu. Sasa hawa watu wamekaa gerezani muda mrefu, mtu anakaa miaka miwili, mitatu, minne anasubiri apangiwe kesi Mahakama Kuu. Kwa hiyo unaona kwamba Kamati hii ilikuwa na uwezo wa ku-force Serikali hasa Mahakama Kuu kuangalia uwezekano wa kubadilisha taratibu zao, kanuni zao kuendana na wakati kwa sababu mahabusu wanakaa sana wakisubiri kesi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa hiyo High Court Session. High Court Session inapangwa, inaweza kukaa miaka mitatu mahabusu wanasubiri High Court Session iweze kuitwa. Ni muhimu sasa hivi Kamati ipendekeze kwa Jaji Mkuu waangalie uwezekano wa kubadilisha kitu kinaitwa High Court session.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wafungwa kule ambao wamehukumiwa kunyongwa. Wamejaza Magereza na kama unavyojua ukihukumiwa kunyongwa hufanyi kazi yoyote, wanakula tu, wanasubiri kunyongwa. Kunyongwa kwenyewe hakujulikani watanyongwa lini. Sasa sijui mamlaka zinazohusika zinafikiria namna gani kwa sababu wanaendelea. Sasa hivi karibu miaka ishirini, thelathini kuna watu wamehukumiwa kunyongwa wako kule hawanyongwi, vifaa vya kunyongea vimekaa mpaka vimeota kutu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kama sheria hiyo mamlaka inaona kwamba haitekelezeki basi iletwe Bungeni tuifute, maana hata kwenye kupunguziwa adhabu wafungwa ambao wanataka kupunguziwa adhabu wale waliohukumiwa kunyongwa hawapunguziwi adhabu hata siku moja sasa sijui ni kwa nini. Ni vizuri suala hilo Kamati pia ingeshauri ili tuibane Serikali ili mamlaka zinazohusika zifikie maamuzi ya hawa watu ambao wamehukumiwa kunyongwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mamlaka zinazohusika zinashindwa basi zirekebishe ziteremshe kwa Mwakyembe huenda atasaini watu wanyongwe, lakini vinginevyo kwa kweli wanajaa na wahamiaji haramu ambao wako mle wanajaa. Maafisa uhamiaji, mhamiaji haramu anakosa anamtupa jela hata bila kupelekwa Mahakamani. Ni vizuri Sheria hiyo pia iangaliwe na kuletwa hapa Bungeni tuweze kuiangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ajali. Suala la ajali ni kubwa sana na zinaleta athari kubwa sana. Watu wanakufa sana kwa ajali, watu wanapata vilema kwa ajali. Nilitegemea pia tuungane na Kamati hii ya Katiba na Sheria tuweze kulazimisha Serikali ilete mapendekezo ya kubadilisha suala hilo, kwa sababu mambo mengi ambayo yanatokana na ajali ni mambo personal (mtu binafsi). Ajali ambazo zinatokea karibu asilimia 70 na ushee zinatokana na matatizo ya mtu binafsi. Ni vizuri Sheria hiyo tukaiangalia upya na iletwe Bungeni tuweze kuifanyia marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye Kamati ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa, hii kitu inaitwa TAMISEMI. TAMISEMI ni jalala, limechukua kila kitu. Kwenye Majimbo yetu huwezi ukazungumza chochote bila kuangalia TAMISEMI. Ukiangalia afya TAMISEMI, sijui shule TAMISEMI, barabara TAMISEMI, matatizo ya maji TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ina mambo mengi sana na kwenye Halmashauri inakuwa ni tatizo, kwa sababu tuna mipango mizuri ya kutekeleza bajeti hii ya TAMISEMI lakini hela hakuna, hela zimeanza kuja juzi. Nashauri tu kwamba, tuilazimishe Serikali hizi fedha zilizopangwa kwenye Halmashauri zetu ziletwe kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Muheza tuna mipango mingi sana ambayo tumepanga kwenye bajeti, lakini mpaka sasa hivi sijui hata kama robo zimefika ambazo tumepokea kwenye mpango wa maendeleo. Kwa hiyo, naomba hela hizi ziletwe ili tuweze kukamilisha mambo ambayo yamepitishwa hapa Bungeni na mambo mengi ya maendeleo ambayo tumeamua kuyafanya katika kipindi hiki cha fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Madaraka ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa; suala hili sasa hivi linakwenda kubaya na nashauri Serikali iliangalie kwa kina. Hawa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wanaonekana hawajapata semina yoyote ya kuelewa madaraka ya ukamataji. Wao wanaelewa tu mtu mpeleke ndani. Mtu amekubishia kwenye mkutano unaamua akamatwe apelekwe ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, askari Polisi anachukua miezi sita kusomea namna ya kumkamata mtu, namna ya kuondoa haki ya mtu, sasa huwezi ukajibishana na mtu tu kwenye mkutano wewe Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa unaamua huyu mtu umweke ndani. Ni suala ambalo ni sensitive na ningeshauri Kamati suala hili tuwabane Serikali hawa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wapate semina, waelewe maana ya ukamataji, waelewe maana ya kuweka watu ndani vinginevyo itakuwa chaos hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kupongeza suala la mradi wa mabasi wa DART, ni mradi ambao unatakiwa upongezwe. Kwa kweli huu mradi sijui kwa nini umechelewa, lakini haya mabasi yangeweza kuwa kwenye Jiji la Dar es Salaam sasa hivi naamini Dar es Salaam upungufu huu wa usafiri ungeweza kupungua kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala ambalo ndugu yangu aliyesema la kutoa matairi alilosema Mheshimiwa Rais, zile ni mbinu za Askari, Rais amewashauri tu Askari namna ya kufanya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa hiyo, si kutoa matairi ni vielelezo mojawapo ambavyo vitatolewa Mahakamani kuthibitisha huyu mtu alikuwa anaingia kwenye barabara ya mwendokasi. Ile ni barabara ya mabasi ya mwendokasi na yanapokukuta wewe ni maiti. Sasa ni lazima askari wawe wakali na wahakikishe kwamba kweli wanatekeleza hizo sheria inavyopaswa. Kwa hiyo, Rais alifanya kuwashauri tu askari, hiyo ni mbinu mojawapo ya kuwakamata hao watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge ni suala ambalo tunatakiwa tulipongeze kwamba hawa wapanda bodaboda wanapoingilia haya mabasi kwa kweli waelewe kwamba ni kifo. Kwa hiyo, ni lazima kwamba Sheria iwe kali kwenye suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza sana suala la TASAF, suala ambalo linatujengea imani sana kwa wananchi. Kuna matatizo madogo madogo ambayo wanatakiwa wayarekebishe lakini huu mpango wa TASAF uongezwe na tunaunga mkono sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono mapendekezo yote na ningeshukuru mapendekezo haya ambayo tumeyashauri, basi yachukuliwe ili tuwabane Serikali vizuri, nakushukuru sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii
kuweza kuchangia hoja hii ya Kamati. Kwanza kabisa ningependa kupongeza sana Wizara hii
ya miundombinu, kwa kiwango kikubwa katika miezi sita hii ambayo tumekuwa nayo
imeonyesha dalala kweli kwamba kuna mambo ambayo yanaonekana kabisa na ni dhahiri
kabisa kwamba wamejitahidi kwa kadri ya uwezo wao. Waziri mwenyewe, Mheshimiwa Profesa
ametembea nafikiri nchi nzima hii nilikuwa kila nikiangalia television naangalia anapumzika
wakati gani lakini naamini kabisa amefika mikoa yote kwenye nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaona tu ni dhahiri kabisa ametuletea ndege zimeletwa hapa
bombardier mbili na nyingine zinakuja, mkataba wa reli umetiwa saini juzijuzi hapa, barabara
wametengeneza karibu kilometa 400 za lami, kuna flyovers ambazo zimeanza kuonekana pale
TAZARA, madaraja ya Coco Beach yameanza kushughulikiwa na magati mengi kule bandarini.
Kwa hiyo, ninachosema ni kwamba Wizara hii ya Miundombinu kwa kiasi fulani imejitahidi na
imetoa nuru ya Awamu ya Tano ni kitu gani ambayo inataka katika hiki kipindi cha miezi sita.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengi ambayo imeyafanya especially
mambo ya reli, lakini utaona kwamba reli yetu ya Tanga kidogo imesahaulika na sijui ni kwa nini,
katika taarifa ya Kamati kwa kweli ingebidi na reli hii ya Tanga iangaliwe, hatuwezi kusubiri
mpaka reli ya kati imalizike ndiyo mipango wa kuanza kushughulikia reli ya Tanga ianzishwe.
Kwa hiyo, ningeomba vitu hivi viende kwa pamoja, simultaneously, huku inafanyika na huku
inafanyika kidogo.
Kuna suala la bandari pia, bandari Tanga sijaona kitu chochote ambacho kimefanyika
ukitilia maanani kwamba kuna bomba la mafuta ambalo linafanyika lakini mipango ya
kupanua ile bandari ya Tanga ili kuweza kukidhi mahitaji ya hili bomba ambalo linakuja bado
sijaiona. Kwa hiyo, ningeshauri Kamati iitake Serikali maandalizi hayo yaanze mapema ili n watu
wa Tanga waanze kufaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la barabara ambazo Wizara hii imejitahidi sana kwenye
kilometa 400 lakini barabara hasa jimboni kwangu, sijaiona na ninaomba Mheshimiwa Waziri
usisahau kuiingiza kwenye bajeti inayokuja barabara kilometa 40 ya Amani mpaka Muheza, ni
barabara muhimu sana na ambayo sasa hivi ina matatizo sana ya kuipitika. Kwa hiyo,
wananchi wa Muheza wanaamini kwamba safari hii barabara hiyo basi itawekwa kwenye
bajeti hii.
Vilevile kutokana na ukame ambao upo sasa hivi tunategemea kwamba ahadi zile za
Mheshimiwa Rais za kilometa tatu ambazo alituahidi pale Muheza basi zitatekelezwa kwa
sababu vumbi limekuwa kbwa na ukame umeongeza vumbi, basi tunategemea hizo kilometa
tatu tukipata lami kidogo tutapata ahueni ya lami. (Makofi)
Kuhusu mawasiliano, kuna tatizo kubwa, hasa kwenye Mlima wa Amani kule, ambapo
redio hazisikiki, simu hazisikiki na nilikwishamuomba Mheshimiwa Waziri ili aweze kuliangalia
tupate minara maana yake hatupati mawasiliano kabisa maeneo ya Amani, tarafa yote nzima,
vijiji vya Ngomole, vijiji vya Zirai, Vijiji vya Kwezitu, inakuwa mawasiliano ni matatizo makubwa
sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nije kwenye Wizara ya Nishati na Madini; ishu ya bomba
la mafuta kutoka kule Hoima, Uganda mpaka Bandari yetu ya Tanga linasisimua sana pale
Mkoani Tanga na linasisimua sana hata Muheza. Lakini sijaona fukutofukuto lolote ambalo
wananchi wanaweza kusema kwamba sasa hivi hii kitu inafanyika, tunaona mkataba umetiwa
saini, lakini hatuoni…
Mheshimiwa Naibu Spika, REA Awamu ya Tatu…
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa.
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante
sana.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) Bill, 2016
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuchangia kwenye marekebisho ya sheria hizi ambazo zimewasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwanza nampongeza sana kwa sababu mabadiliko hayo ambayo ameyaleta, ni muhimu sana kwa wakati huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye hii Mahakama ya Division ya Mafisadi, Mahakama hii sasa hivi ni muhimu sana jinsi ambavyo imeanzishwa na ni dhamira ya Awamu ya Tano kuanzisha Mahakama hii. Mahakama ya Division ya Mafisadi ambayo inategemewa kuanzishwa, ukiangalia mabadiliko ambayo yamefanyika, yametoa Mahakama ya uhujumu uchumi na kuweka Mahakama hii ya Division ya Mafisadi. Sasa provisions kifungu cha tatu ambacho kimerekebisha kifungu cha pili na kifungu cha tatu ambacho kimeweka makosa ambayo Mahakama hii ya Mafisadi itashughulikia, utaona pamekuwa na msururu wa makosa mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kuanzishwa kwa Mahakama hii ni kuangalia zile kesi nzito, kesi kubwa kubwa ambazo zinatakiwa ziende kwenye hii Mahakama na siyo lengo la kuweka msururu wa kesi nyingi nyingi. Kwa hiyo, utaona kwamba, makosa ambayo yalikuwepo kwenye Sheria ya Uhujumu Uchumi (Economic and Organized Crime Act), mengi ni kama yamehamishwa sasa kwenye Mhakama hii ya Division ya Ufisadi. Ndiyo maana nasema pamekuwa na msururu mkubwa pamoja na kuwekewa kiwango cha bilioni moja kwamba kesi zote ambazo zitakuwa zinakwenda kule ziwe zimefikia bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta makosa mengine ambayo yanakwenda kwenye Mahakama hiyo, gharama ambazo zinapatikana ni gharama za mitaani (street value), kwa mfano makosa ya madawa ya kulevya, thamani yake inachukuliwa kama street value ya mitaani ndiyo ambayo inawekwa pale. Kwa hiyo, hakuna gharama halisi ambayo unaiweka pale ya kusema kwamba, kweli madawa haya au meno haya ya tembo, basi gharama yake ni bilioni moja. Wenzetu nchi za nje sasa hivi wameondoka kwenye suala la kufikiria gharama bali wanafikiria uzito, kwamba madawa haya ya kulevya uzito wake ni kilogram ngapi? Ni kontena ngapi au pembe hizi za ndovu ni kontena ngapi? Uzito wake ni kiasi gani na siyo kufuata gharama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hii gharama ambayo imewekwa hapa, ningemwomba Mwanasheria Mkuu ajaribu kuangalia kwamba tuzingatie sasa hivi uzito badala ya kuangalia gharama. Nasema hivyo kwa sababu, Kamati yangu tumekwenda katika Magereza mbalimbali na imegundua kwamba makosa ya madawa ya kulevya, watu ambao wako magerezani kule utakuta uzito wa kesi ambazo wanazo ni mdogo, kwa mfano, ambao wanaambiwa wamesafirisha madawa ya kulevya. Kusafirisha madawa ya kulevya mtu ambaye amemeza yale madawa, anashtakiwa kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya whatever grams ambazo wanazo, lakini zimeshaingia tumboni, sasa anaambiwa kwamba, basi hili tumbo ni kontena wewe umesafirisha haya madawa, kwa hiyo, ni lazima ushtakiwe chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia pia kwenye mabadiliko haya ambayo yameletwa hawa watu ambao wamekamatwa kamatwa wamemeza madawa au wamekutwa na gram ambazo zimekutwa kwenye viatu au kwenye mabegi, wote hawa pamoja na gram zao kuwa ndogo utakuta kwamba wanashtakiwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi. Sasa kitu ambacho kitatokea sasa, kwa sababu hawa ni wasafirishaji wameweka kwenye makontena, wameweka kwenye viatu, wameweka kwenye matumbo yao, wamekamatwa wanaambiwa wao ni wasafirishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Mahakama hii ni kupeleka wale watu ambao wana makontena. Sasa tukiipeleka jinsi ilivyo, patakuwa na msururu mkubwa kweli kwenye hiyo Mahakama na lengo lake ambalo liko pale utakuta kwamba halitafikiwa. Kwa hiyo utaangalia hapa kwenye presentation ambayo ametoa Attorney General, msururu wa makosa nauona ni mkubwa sana, ni makosa mengi sana, kiasi kwamba hii Mahakama sasa tutaichosha, badala yake itakuwa kazi ambazo inazifanya zitakuwa sio tulizokusudia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, hebu angalia kuna kosa hapa za kupatikana na silaha, yaani gobore ni silaha, sasa gobore mtu amekamatwa na gobore itabidi aende kwenye hiyo Mahakama ya Ufisadi. Sasa hiyo Mahakama itakuwa na maana gani kwa sababu hizi kesi zote ndogo ndogo zitakwenda. Kwa hiyo, nafikiri kwamba Serikali iangalie tena kwamba ni kesi gani na hasa zile nzito ndiyo zinatakiwa ziende kule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ninaloliona ni suala la zile kesi ambazo zimetoka kwenye Economic and Organized Crime Act ambazo zimeonekana ni ndogo ndogo, maana siyo zote ambazo zimehamishiwa hapa, haiku-specify hapa kwamba zile kesi zitapelekwa wapi au zitasikilizwa kwa utaratibu gani na Mahakama hii inatakiwa ianze kazi kwa kesi gani? Ni fresh cases ambazo zinakuja au nyinginezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuanzishwa kwa Mahakama hii, ingekuwa ni vizuri kwamba, baada ya sheria hii kupita, wale wadau stakeholders wote wapate semina, wapate mafunzo maalum kuanzia Wapelelezi mpaka Majaji na Waendesha Mashtaka ili kuweza kuwa na uwiano mzuri wa usikilizaji wa kesi hii katika Mahakama hii ambayo tunategemea kwamba, iende kwa uharaka jinsi inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nategemea kwamba uanzishwaji wa Division hii basi utakuwa ni mzuri, utaratibu mzuri kama vile ilivyokuwa Division ya Biashara, Commercial Court au Division ya Kesi za Ardhi. Utaratibu ambao utakuwepo pawe na jengo lake kwa sababu utaratibu ambao ulikuwa unafanywa katika kesi za uhujumu uchumi kama alivyosema Mwanasheria Mkuu kwa kweli haukuwa utaratibu, ni Majaji wale wale tu kama kuna kesi ya wahujumu uchumi, basi jaji huyo huyo anahamia hapo hapo anaanza kusikiliza hizo kesi. Kwa hiyo, unakuta kwamba msongamano wa kesi unakuwa mkubwa. Kwa hiyo, hapa tunategemea kwamba Divisheni hii itakuwa na jengo lake maalum, Majaji wake maalum, wafanyakazi maalum kama ilivyo kwenye Commercial Court, pamoja na Ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ningependa kuunga mkono hoja kwa marekebisho ambayo nimeyaeleza. Nakushukuru sana.
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia hoja hii ambayo imeletwa na Waziri wa Fedha. Kwanza, nampongeza kwa kuleta mabadiliko ya hoja hii ambayo ni muhimu sana. Suala la manunuzi ya umma Serikalini ni kitu cha msingi na muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ununuzi wa umma ni kipimo cha namna Serikali inavyoendesha shughuli zake, inavyofuata sharia, uwazi na namna ambavyo inadhibiti vitendo vyovyote vya rushwa kwenye zabuni. Zabuni ni eneo ambalo linaleta rushwa sana. Zile rushwa kubwa kubwa zinazozungumzwa zinatoka kwenye zabuni kubwa, mikataba mikubwa, yote inatokea hapa kwenye hii kitu inaitwa zabuni na ndiyo maana asilimia 70 ya bajeti inakwenda huko kwenye suala la mchakato wa zabuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria yetu ya Public Procurement, Cap 410 ina historia ambayo imeanzia tangu 1990, tukaja kwenye ya 2011 pamoja na regulations zake lakini pamoja na sheria zote hizo utaona kwamba bado haijakidhi matakwa yale ambayo yanatakiwa ili sheria hii iweze kuwa nzuri na itekelezeke vizuri. Kwa hiyo, mabadiliko yanatokea na ndiyo maana sheria hii sasa hivi imeletwa hapa kufanyiwa mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sheria hii ambayo bado haijafanyiwa marekebisho imesaidia kwa kiwango kikubwa hasa kwenye udhibiti wa corruption. Imedhibiti rushwa kwa sababu imekuwa na Kamati nyingi sana pamoja na changamoto ya urasimu na muda lakini kwa njia moja au nyingine imesaidia kuweka transparency kwenye suala zima la mchakato wa hizo zabuni. Pia sheria hii ambayo tunataka kuibadilisha imesaidia sana kutoa opportunities za kutoa zabuni za kimataifa ambazo sasa hivi tunazifanyia mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii sheria ambayo sasa hivi imeletwa hapa ina umuhimu sana kwa sababu imeingiza kitu ambacho kinaitwa value for money ambacho ni muhimu sana na kimewekwa mpaka kwenye hii preamble ambayo ipo kwenye haya mabadiliko. Ukiangalia kifungu cha 3 au cha 2 kimeweka hiyo preamble ambayo inaonyesha kwamba sasa sheria hii itaangalia value for money na sasa hivi ndiyo sheria nyingi za zabuni zinakwenda kwenye mwelekeo huo. Nilikuwa naangalia Sheria ya Manunuzi ya World Bank pamoja na EU zote hizo zimeingiza kitu kinaitwa value for money. Pia imejaribu kuondoa mlolongo mzima wa michakato hii na kupunguza hizi Kamati ambapo kila Kamati ikikaa inapewa hela, sasa mlolongo wote huo umeondoka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kimoja kimewekwa ambacho wenzetu pia wamekiweka badala ya kulenga tu bidder yule ambaye ana bei ya chini inaangalia huyu mzabuni pamoja na kuwa na bei ya chini, je, vitu vyake vina ubora kiasi gani? Sasa hicho ni kitu muhimu, kuangalia ubora na siyo kuangalia tu thamani kwamba hii ni thamani ndogo basi huyu mpe kwa sababu thamani ndogo ameshinda hiyo tenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha msingi ambacho nimekitafuta kwenye marekebisho haya sikukiona ni suala la negotiations kwamba huyu ameshinda, je, kuna utaratibu gani umewekwa ambapo wanaacha mambo ya kwenda kwenye bei ndogo wanaingia kwenye majadiliano na wazabuni kuweza kuangalia ubora irrespective ya bei ambayo ameitenda? Kwa hiyo, ni kitu cha msingi naomba Mheshimiwa Waziri aeleze amekiweka wapi kwenye hizi provisions ambazo zipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na-support kabisa suala ambalo limewekwa kuanzia kifungu cha 55A, 55B, 55C na 55D ambapo inawakata makali wageni na kuwaruhusu wazawa kushiriki kwenye zabuni hizi. Suala hili limekuwa likiathiri sana zabuni nyingi kwa sababu utakuta wanapewa watu wa nje na wanaleta wataalamu wao na wengine hata hawana utaalam wanajaa kwenye hizo zabuni wanafanya kazi na watu wetu wanakosa kazi za kufanya. Hii itasaidia sana kwa sababu watu wetu watapata nafasi ya kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la ushindani wa zabuni, kwenye zabuni lazima pawepo na ushindani lakini pawepo pia na zabuni ambazo hazina ushindani (single source) lakini hizi single source pia ni lazima zirekebishwe ziendane na wakati. Nimeangalia kwenye kifungu cha 65A na 65C na nimeona ushindani huu wa single source ameachiwa Waziri kutengeneza hizo regulations. Hapa ni lazima tuwe waangalifu sana vinginevyo tunaweza tukarudi kwenye suala lile lile ambalo liko chini. Single source ni muhimu na lazima tui-encourage kwa sababu kuna mifano mingi ambapo zabuni unaweza ukanunua moja kwa moja kutoka kiwandani na ikaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, ningeshukuru kama suala hili litapewa umuhimu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la zabuni maalum wakati wa athari au panapotokea chochote kile ambacho ni cha dharura hapo tena huwezi ukasema kwamba unaanza mambo ya tenda itachukua mlolongo mrefu. Ni lazima sheria iruhusu vitu vya wakati huo kwamba sasa hivi vitu vya dharura viruhusiwe mtu aweze kwenda moja kwa moja kwenye single source na kuanza kufanya manunuzi. Hiyo special provision lazima iwepo na ionekane.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa ambalo linatakiwa kwenye zabuni ni uaminifu na uadilifu na namna watumishi wa Serikali watakavyofanya kazi hiyo. Naunga mkono hoja hii kwa sababu imejaribu kutaja mambo mengi ambayo ni muhimu. Cha msingi hasa ambacho sijakiona na napenda Waziri atuthibitishie, wakati wazabuni wanaingia kwenye majadiliano, suala la kui-inflate rate ni kitu cha muhimu sana. Watumishi wengi wa Serikali wanaongeza bei pale kwenye zabuni na ile kuongeza bei inawapa tabu sana hata wapelelezi namna ya kuchunguza na kujua hii kitu bei yake ni shilingi ngapi. Kwa hiyo, ni vizuri wakati wa zabuni tuwe na assessment ya kujua kwamba chombo hiki ambacho tunataka kiingie kwenye zabuni au gharama ya kutengeneza hii barabara inaweza kuwa shilingi ngapi? Atleast tukiwa na maximum evaluation itasaidia kuondoa hii thinking ya kuongeza bei jinsi anavyotaka mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja hii na nashukuru kwa kupata nafasi hii.
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Wanataaluma wa Kemia wa Mwaka 2016
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kupata nafasi hii kuweza kuchangia Miswada hii miwili ambayo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Miswada hii muhimu kwa sababu ni Miswada ya kitaalam na watendaji wake wengi ni wataalam wa fani mbalimbali. Mkemia Mkuu wa Serikali amekuwa akifanya kazi nyingi sana za kitaalam. Nimebahatika kufanya kazi na Mkemia Mkuu wa Serikali kwa miaka mingi, kwa kweli wanafanya kazi nyingi sana za upelelezi na Idara ya Upelelezi inamtegemea sana Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali za kitaalam za matukio mbalimbali ya makosa ya jinai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Idara ya Upelelezi kwa muda mrefu imekuwa ikishirikiana na Mkemia Mkuu na inaendelea kushirikiana nayo kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali ili kukamilisha upelelezi wa makosa mbalimbali ya kemikali. Idara ya Upelelezi inayo Forensic Unit ambayo ina-cover mambo ya kitaalam kwa mfano utaalam wa maandishi, ballistic, finger prints, cyber crime na utaalam mbalimbali lakini hivi karibuni idara hiyo pia imeanzisha utaalam mwingine zaidi wa mambo ya kemikali, toxicology na mambo mengine mengi ya bombing na drugs. Ili kupunguza workload ya Mkemia Mkuu wa Serikali anapaswa kusaidia kwa kiwango kikubwa kabisa maabara nyingine ambazo zitakuwa zinafanya kazi za kimaabara hapa nchini ikiwepo na maabara iliyo chini ya Idara ya Upelelezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata mafunzo kwa matukio makubwa ambayo yamewahi kutokea hapo nyuma na hata ukichukulia tukio hili la sasa hivi lilitokea huko Kagera la tetemeko la ardhi. Mwaka 1998 Ubalozi wa Marekani ulilipuliwa hapa nchini na ulipolipuliwa Watanzania walikufa pale na viungo vyao vilitawanyika kwa sababu lile bomu liliwatawanya kwa hiyo utaalam wa DNA ulihitajika lakini tulikuwa hatuna huo utaalam. Tulikuwa hatuna utaalam wa bombing kujua kwamba bomu ambalo lilipiga Ubalozi wa Marekani lilikuwa kubwa kiasi gani, lilikuwa na uzito kiasi gani hivyo hivyo tukio hili la tetemeko la ardhi ambalo limetokea huko Kagera hatujui ukubwa wake ni kiasi gani. Labda kwa mfano tetemeko hili la ardhi lingekuwa limetawanyisha viungo ingebidi sasa hivi navyozungumza wataalam wa DNA wanatakiwa wawe kule Bukoba.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata lile tukio kwa mfano la 1998 ilikuwa ni fundisho kubwa sana kwa Idara ya Upelelezi hapa nchini ambapo tulikuwa ni weupe kabisa kwenye mambo ya kitaalam ya DNA na hata ilikuwa ni fundisho kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Nashukuru sana baada ya pale Idara ya Upelelezi ya FBI ilitushauri na ikasisitiza kwamba Forensic Units za Polisi ambazo ziko duniani ni lazima ziwe zina-cover maeneo yote haya ambayo ni muhimu ya toxicology, DNA na kadhalika ndiyo inakuwa imekamilika kwa sababu itasaidia wataalam kwenda kwenye matukio haraka na wataweza kusaidia kurahisisha kazi za Mkemia Mkuu. Namna ya kuchukua vielelezo pale, namna ya kuchukua sampuli mbalimbali yote hiyo ni utaalam ambao unatakiwa na ni utaalam ambao unatakiwa usaidiwe sana na Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sheria hii imekuja wakati muafaka na nashauri kabisa Waziri atakapokuja ku-wind up aonyeshe nia kweli kwamba Mkemia Mkuu wa Serikali yuko tayari kusaidia maabara nyingine ambazo ni muhimu kabisa ili kuweza kurahisishia kazi. Sasa hivi kuna kesi nyingi sana za mauaji, za drugs, kama Kamati tumetembelea kwenye magereza mbalimbali na kule ambapo zimekwama unakuta labda wanasubiri taarifa ya Mkemia kuhusu mauaji au drugs hizo. Kwa hiyo, sheria hii inatakiwa itoe nguvu kwa maabara hizi nyingine ili ziweze kusaidia kazi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia kwenye vifungu mbalimbali ambavyo viko katika Sheria hii ya Mkemia Mkuu wa Serikali na nimeona kwamba mambo mengi yameguswa lakini kuna mambo mengine ambayo yanatakiwa kuguswa kwa mfano hilo la kuhakikisha kwamba Mkemia Mkuu ana-support maabara nyingine, ni muhimu liwe wazi na liwe na kifungu chake maalum cha kuhakikisha kwamba Mkemia Mkuu anasaidia maabara nyingine hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napata pia wasiwasi kwenye kifungu cha 4 ambacho kinatoa supremacy na referral. Sijapata lugha sahihi ya kuweka katika kifungu hiki, lakini labda Mheshimiwa Waziri angetusaidia, Mkemia Mkuu yeye ni operational, regulator sasa itakuwaje tena awe supremacy na at the same time yeye ndiyo apelekewe rufaa? Ningeshauri labda kifungu hiki kingehamishwa aidha kipelekwe kwenye Bodi ile iweze ku-oversee maabara zote nchini ikiwepo na hii ya Mkemia Mkuu kama kuna tatizo lolote ambalo linatokea. Kwa hiyo, natashukuru kama suala hilo lingeangaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 5 pia nina wasiwasi nacho ambacho kinakwenda sambamba na kifungu cha 4 pale kinaposema kwamba results shall be final and conclusive. Hii final na conclusive inanipa wasiwasi kidogo kwa sababu ripoti ambazo zinatolewa na Mkemia Mkuu ni za utaalam chini ya Sheria ya Ushahidi pia ambapo ripoti hiyo inaweza kutolewa na utaalam mwingine.
Kwa hiyo, ni lazima kuangalia badala ya kuweka final and conclusive inaweza ikasema labda taarifa ambazo zinatolewa ni unreliable. Kwa hiyo, labda Waziri angekiangalia kifungu hicho na kukirekebisha ili ku-come up na good provision.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu kingine…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi napenda kuungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Nape na Mheshimiwa Naibu Waziri pamoja na Mwenyekiti wa Kamati kwa kazi nzuri ambayo wameifanya kuweza kuchambua muswada huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu ni muhimu sana. Taswira ya habari hapa nchini ni kitu ambacho humu ndani hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kusema kwamba waandishi wa habari au taswira ya habari ni mbovu. Waandishi wa habari kwenye nchi hii wamefanya kazi nyingi sana; wanafanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ndiyo maana kila siku asubuhi unaangalia kwenye television kutaka kujua kuna habari gani? Kuna kitu gani leo? Kila mtu kila saa ana-google au ana-whatsapp kila leo, lakini yote hayo ni mahusiano ya habari. Hizi habari zinatafutwa. Hawa waandishi wa habari hawaokoti hizi habari, wanazitafuta kwa bidii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa kabisa, nimesoma huu muswada, ni mzuri sana. Kama ni marekebisho yanahitajika kufanyika, ni kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 58 kinawatambua na kuwathamini waandishi wa habari. Kimewapa bima, kimewafanya wawe na mifuko. Hawa waandishi wa habari imefika hatua wanaitwa mapaparazi, wengine hawana mishahara, wengi tu. Wanafanywa kama vibarua, wanalipwa kwa story, kwa mistari. Ukiangalia kwenye vyombo vyote vya habari, karibu nusu ya hao waandishi wa habari hawalipwi na hawana barua za ajira; lakini wanavumilia na hawataki kutoa hizo taarifa kwa sababu wanajua wakitoa tu watafukuzwa kazi na watakuwa hawana cha kusema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka kusema kwamba wamiliki wa vyombo vya habari na watu wengine wawe waangalifu, wasikazanie kusema kwamba muswada ni mbaya ili hawa waandishi wa habari wanaopata taabu kila siku wasipate haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhuru wa habari hapa nchini, mimi nimeangalia kwenye google, Tanzania ni nchi mojawapo ambayo ina uhuru mkubwa sana wa vyombo vya habari. Nimetembea, nimeona nchi mbalimbali, sijawahi kuona nchi ina magazeti kama hapa nchini, lundo la magazeti. Hapa huwezi ukasema unaweza ukanunua magazeti yote ambayo yanatoka kwa siku, ndiyo maana magazeti yote yanafanya kubandikwa, mtu unaangalia hii heading ngoja ninunue hili na hili. Uhuru ni mkubwa, vyombo vya televisheni viko vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba uhuru wa vyombo vya habari ni mkubwa hapa nchini na ambao inabidi uangaliwe na hawa watu wanaotupa habari tuwaangalie maslahi yao jamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ngoja niende kwenye sheria, kwenye muswada wenyewe unavyosema. Mwandishi wa habari ni nani? Pale imesema, a journalist is the one who has been accredited, lakini inategemea kwamba Mheshimiwa Waziri atakwenda further na kufafanua kwamba huu ni muswada wa waandishi wa habari, kwa hiyo, ni lazima afafanuliwe nani ni mwandishi wa habari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye media inasema ina-include na social media. Kulikuwa na utata hapa kwamba labda blogs au social media basi siyo media. Nilikwenda nikaangalia baadhi ya kesi kwenye commonwealth; Mahakama Kuu ya Australia, New Zealand kulikuwa na huo utata kwamba social media labda siyo media na imetolewa uamuzi kwamba blogs zote ni social media. Ipo na nenda mwangalie kwenye Mahakama Kuu za Australia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, kwenye accreditation ni lazima Waziri aseme vigezo gani ambavyo atavitumia kuweza kumfanya huyu mtu aweze kuitwa Mwandishi wa Habari. Hatuna maana kusema basi wale ambao hawatakuwa accredited, basi hawatafanya kazi za uandishi wa habari. Ni lazima Waziri atambue kwenye kanuni atakapozitengeneza, ahakikishe kwamba anawatambua mpaka ma-repoter, ma-photographer, waandishi, ma-digital waandishi, waandishi wanaoandika makala mbalimbali ni lazima wote wa-appear kwenye kanuni. Hii tunataka kuifanya profession ya uandishi wa habari iwe kama profession nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo wanasheria wote ni mawakili. Tunao wanasheria wengi lakini pia tunao mawakili. Kwa hiyo, tunataka waandishi ambao wako accredited ili waweze kutambua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitakwenda kifungu cha 20(3) kimeshakuwa amended ambacho kinasema kwamba journalist yeyote ambaye amekuwa suspended basi asifanye hizo kazi. Kilikuwa ni kifungu kibaya sana, lakini nakushukuru kwa kufanya hiyo amendment na kuhakikisha kwamba basi atasimamishwa kwa miezi mitatu na aendelee na kazi zake. Kilikuwa ni kifungu kibaya ambacho kingeendelea kuleta taswira mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 18 ambacho kinatambua waandishi wageni, hiki ni muhimu sana. Nimekiona na kimeleta madhara makubwa sana. Waandishi wa habari wageni ni lazima wadhibitiwe. Kama wanapewa vibali ni lazima wahakikishe kwamba wanakwenda kwenye hiyo specific area ambayo wameambiwa waka-cover hiyo habari. Hatuwezi kukubali nchi hii waruhusiwe tu waandishi ambao ni foreigners waingie nchini kiholela holela, hatuwezi kukubali. Kwa hiyo, nakipongeza sana kifungu hicho na kuhakikisha kwamba ni lazima tukidhibiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imetambua mambo mengi. Sheria hii imetambua pamoja na kujua mwandishi wa habari ni nani, lakini imekwenda further na kutengeneza hiyo Bodi ya Ithibati, Mfuko wa Waandishi wa Habari, imetengeneza Baraza la kudhibiti ethics za waandishi wa habari na pia imempa Waziri madaraka ya kuthibiti mambo mbalimbali. Jamani hatuwezi kutengeneza sheria bila kumpa madaraka Waziri ya kuangalia mambo muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi sana kwenye mambo ya uhandishi wa habari, ni lazima pawepo na msimamiaji. Yuko pale kwa nia njema tu. Waziri atatengeneza kanuni ambazo zitakwenda sambamba na uandishi wa habari. Yeye ni binadamu, hataki kuua hii kitu ya uandishi wa habari, anataka kuendeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia makosa katika sheria hii, hasa makosa ya uchochezi. Makosa mengi yametolewa kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976; seditious offences. Makosa ambayo yameorodheshwa kwenye sheria hiyo ambayo Sheria ya Magazeti, imeifuta, yale makosa ya kwenye Kifungu kuanzia cha 50, kwenye sheria ile yalikuwa ni lazima yapate kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii imeondoa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka na kuwapa madaraka polisi wote wakamate hayo makosa na kuyafikisha mahakamani. Mheshimiwa Waziri ni muhimu madaraka ya Mkurugenzi wa Mashtaka dhidi ya seditious offences madaraka hayo yarudishwe. Itasaidia sana kuweza kudhibiti makosa hayo ambayo yataonekana yanatokana na uchochezi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kumpongeza tena Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, lakini nitashukuru wakifanya marekebisho hayo ambayo nimeyasema ili tuweze kwenda sambamba na sheria hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haki za waandishi wa habari lazima zitambuliwe, waajiri lazima wawekewe vifungu pale tuwathibiti waweze kuwalipa vizuri waandishi wa habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono.
Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016
MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia Muswada huu ambao ni muhimu sana. Kwanza natoa pongezi kwa Chama changu kwa kuweza kupiga magoli mengi kule magoli 19 kwa 1 na pia nawapongeza Wabunge wote hasa ndugu yangu Juma ambae ameweza kushinda kwa kishindo kule Unguja-Dimani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu kwa kweli ni muhimu sana na Muswada huu kama walivyosema wenzangu kwa kweli umechelewa sana. Ni Muswada ambao unalenga watu ambao hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria. Ni Muswada ambao utaweza kusaidia watu wengi sana masikini, walemavu na kila watu na wafungwa ambao hata wako kule Magerezani ambao wanashindwa hata kuandika nanihii za kukata rufaa ambao wamejaa na ambao huwezi kusema kwamba kweli wote wamefungwa kwa makosa hayo lakini wana-right ya kukata rufaa lakini wanashindwa kutumia rufaa hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwamba Muswada huu umepanua wigo na umepanua wigo wa kuleta watu wengi kuweza kudai madai yao kwa kufuata sheria hii na nasema umepanua wigo kwa sababu ukifuata sura, Muswada ambao ulikuwa unatoa mamlaka kama haya kwenye sura ya 21 ambayo ni sheria ambayo ni The Legal Aid ambayo ilikuwa inatoa kwa ajili ya sheria ya makosa ya jinai pekee sasa hivi Muswada huu umepanua wigo na unatoa siyo makosa ya jinai ya mauaji tu au wale ambao wamehukumiwa kifungo bali unakwenda mpaka kutoa kwenye kesi za madai. Pia Muswada huu siyo kwamba utatoa huduma Mahakama Kuu tu, lakini Muswada huu unakwenda mpaka kwenye Mahakama za Wilaya, kwa hiyo ni Muswada ambao unatakiwa kupongezwa na ambao ni lazima tuangalie namna ya kuupitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo yote hayo, lakini nimepata wasiwasi wa mambo kama matatu hivi ndani ya Muswada huu. Ukiuangalia Muswada huu utaona kwamba mara utakapoanza kutumika wananchi wengi sana watakuja kudai huduma hiyo. Wananchi wengi watataka huduma za Mawakili, watataka huduma za hizo Taasisi ambazo zimeandikishwa kwa ajili ya kutetea haki zao. Sasa najaribu kuangalia wigo wa kesi ambazo ziko katika Mahakama zetu, wigo wa kesi chukulia kesi ambazo ziko Mahakama ya Wilaya tu au chukulia kesi ambazo ziko Mahakama kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa watu wengi ambao wako pale watataka hiyo huduma ya Wakili ambao atakuja kunanii sasa utaona kwamba kuanzia kifungu cha 21 mpaka 36 nimejaribu kukiangalia lakini sijaona sehemu ambayo Muswada huu umeelekeza ni makosa ya aina gani ambayo yatataka kupata msaada huu. Sasa ukiacha hiyo vinginevyo itakuwa ni chaos kwa sababu kila mtu atataka kupata msaada huo na makosa ambayo yanatakiwa yapatikane msaada huo hayakuainishwa kwenye sehemu yoyote ile. Kama ni lengo la Serikali kwamba makosa ambayo yataainishwa yawe yanatakiwa kupata msaada yatatengenezwa kwenye kanuni, sijaona pia Mamlaka (provision) yoyote ambayo imeipa bodi, kuishauri kutengeneza hizo kanuni ili kuainisha ni makosa gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningependa kuishauri kwamba ni lazima basi pawepo na provision ambayo itaipa Mamlaka Bodi ya kuhakikisha kwamba inachambua ni makosa gani ambayo yanahitajika kutolewa msaada huu vinginevyo itakuwa ni chaos na itakuwa ni watu wengi ambao watahitaji huo msaada.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa sababu niliangalia sheria mbalimbali na nikakuta sheria ya Afrika Kusini ambayo imetoa uwezo kama huo kwamba imetoa uwezo kwa bodi na bodi ile wametengeneza regulations, wame-identify makosa gani ambayo yanatakiwa yapewe msaada na ndiyo ambayo yanafuatwa, kwa hiyo na hapa ningeshauri pia na sisi tungeiga hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika la tatu, ambalo naliona, ukiangalia sheria ya 21 ambayo imefutwa, sheria ile imetoa madaraka kwa Mawakili ili Msajili wa Mahakama Kuu ndiyo ambaye anaweza kuchagua ofisi yoyote ya Uwakili kumwakilisha yule ambaye ameomba kuomba huduma hiyo ya msaada ambao anautaka. Kwa hiyo, ofisi yoyote ya Wakili ambayo imeandikishwa basi ilikuwa ina utaratibu kwamba hata kama ni Wakili wako mikoani walikuwa wanaamriwa kwenda kutetea hizo kesi za mauaji au zile ambazo zina adhabu ya vifo sasa ilikuwa centralized, registrar alikuwa na madaraka hayo, lakini ukiangalia kwenye hii sheria inasema kwamba mtu ambaye anahitaji kutoa huduma za kusaidia basi inabidi aombe kwenye bodi. Kwa hiyo, ina maana kwamba Taasisi zote ambazo zinataka kutoa huduma, ofisi za Mawakili ambazo zinataka kutoa huduma hii inabidi ziombe kule kwenye bodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tatizo ambalo naliona ni kama ofisi hizi zisipotaka kuomba itakuwaje kwa sababu sasa hivi sheria ambayo ipo ya sura ya 21 Mawakili hawaombi, wanaamriwa kwa sababu ni Maafisa wa Mahakama wanaamriwa kwenda na bado hapo hapo wanakwenda kwa kinyongo kwa sababu fedha ambazo wanalipwa ni kidogo sana kwa kila kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia sura hii utakuta kwamba Wakili sasa hivi analipwa kwa kesi elfu 40, elfu 60 sasa utakuta kwamba ni hela ndogo sana na hakuna motivation ya kuwafanya Mawakili au ofisi hizo ziombe. Sasa kitu gani ambacho sheria hii imekifanya ambacho kitawafanya Mawakili waweze kuomba au Taasisi zinaweza kuwafanya kwamba wakimbilie kuomba ili kutoa huduma kwa hawa ambao watatakiwa kupewa hiyo huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni suala ambalo linatakiwa liangaliwe kwa sababu hawezi wakili akapoteza muda wake wote pale hajui atalipwa nini ndiyo anayekwenda kutoa msaada lakini analipwa nini? Kwa hiyo sheria hii haikugusa chochote. Naomba kwamba Waziri aliangalie hilo na atakapokuja ku-sum up aweke kipengele hicho vinginevyo nitaleta mapendekezo ya marekebisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, ni suala ambalo sasa hivi hii itakuwa ni ofisi kubwa sana, itakuwa ni institution kubwa sana. Haitakuwa kwenye kiwango cha bodi kama hivi ambavyo sheria inasema, haitakuwa kwamba ni mwakilishi mmoja tu kama ni Paralegal ambao wako kule wilayani basi hao hao ambao watafanya kazi. Sasa hiki ni kitu ambacho kinatakiwa pawe na independent board, institutions ambayo itashughulika kabisa na suala hili la kutoa hizi huduma. Hapa amezungumza Msemaji wa Kambi ya Upinzani ambayo ni mifano ambayo iko kwenye nchi nyingine. Nchi nyingine South Africa wana-independent board, institutions kabisa ambayo inatoa hii misaada kwa watu wote ambao wanahitaji huduma za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kusema kwamba tunaweka ki-board tu au Wakala tu, ni lazima pawe na ofisi special office ambayo itatoa hizi huduma vinginevyo tutakuwa tunafanya masihara masihara tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru na naunga mkono mapendekezo ambayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati kwamba ufafanuzi wa baadhi ya mambo ya Mwanasheria ni nani? Paralegal ni nani? Sheria hii ita-cover Mahakama zipi? Lazima ufafanuzi huo utolewe kwa sababu imeacha wazi, mtu anaweza kusema nataka kwenda hata Primary Court, jinsi mapendekezo haya yalivyo ina maana ana-cover mpaka Primary Court, kwa hiyo ni lazima ufafanuzi huu utolewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja baada ya marekebisho hayo. Nakushukuru sana.