Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kasuku Samson Bilago (35 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Awali ya yote, niwashukuru wananchi wa Jimbo la Buyungu kwa imani kubwa waliyonipa ya kuniamini, kuwawakilisha katika Jimbo la Buyungu na nina uhakika wamepata mwakilishi makini
na sahihi. Kabla sijaanza kuzungumzia vipengele kadhaa nitakavyovizungumzia, nataka niseme kwa ujumla wake, Hotuba ya Rais imesheheni matatizo ya Watanzania. Matatizo makubwa sana waliyonayo Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nilidhani tungekuwa pamoja kama itawezekana, tuone namna ya kuondoa haya matatizo na matatizo yenyewe, hata Watanzania nawashangaa, kwa matatizo yote haya yaliyosababishwa na Chama cha Mapinduzi, wameendelea kukiamini na kukirudisha madarakani. Hapa ndipo ninapopata mashaka makubwa sana. Kwa matatizo lukuki yaliyoko ndani ya Hotuba ya Rais, Watanzania
hawakutakiwa kukiamini Chama cha Mapinduzi na kukirudisha madarakani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza maelezo yote hayo, nataka niulize style ya nchi hii sasa hivi tunayokwenda nayo ni ipi? Kuna style imeanza sasa hivi ya kuvamia. Mawaziri wetu wanavamia, wanaweza wakaja Mkoani hata Mkuu wa Mkoa hajui, sasa ni style ipi tunayokwenda nayo. Maana sekta zote tukubaliane zianze kuvamia, walimu nao wawe wanavamia, ukiingia darasani ilikuwa Kiswahili uvamie na wewe ukafundishe somo lolote tu.
Madaktari nao wavamie, yaani sijui ni style ipi ambayo haina work plan. Niwashauri Mawaziri, mtumie work plan, acheni kuvamia vamia. Aliyevamia mmoja tu yule alifanya tu vile msi-copy na ku-paste. (Kicheko)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba dakika zangu zitunzwe, lakini naomba kutoa tahadhari nisifundishwe namna ya kuchangia. Mimi ni Mwalimu, nina uzoefu mkubwa sana na hizi shughuli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nitoe tu angalizo hili, nadhani wamelichukua na watalifanyia kazi. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, suala la elimu bure limetajwa, lakini limeleta mkanganyiko kwa wananchi. Sasa hivi hali ya neno elimu bure, nafikiri tungetafuta utaratibu wa ku-define neno bure, kama linaonekana linaleta utata. Kwa mujibu wa maelezo yanavyotolewa na inavyotekelezeka kule, hata Jimboni kwangu kule Buyungu hali ni ngumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, walioko shule za kutwa, wanaona hawajapata ule ubure unaotajwa kama bure. Walikuwa wanalipia chakula shule za kutwa, walikuwa wanachangia michango mbalimbali, chakula kimeendelea kubaki gharama kubwa, kuliko 20,000/= iliyoondolewa, sasa wanatusumbua na sisi Wabunge, hivi kweli hii ni elimu bure? Kama tunasema neno elimu bure, tusiwe na double standard, shule zote ziwekwe elimu bure na kama ni chakula kitolewe kwa wote, hata shule za kutwa wapewe chakula na Serikali na wao ni Watanzania wanahitaji kula ili waweze kupata masomo vizuri darasani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwenye elimu kuna matatizo lukuki, bado kuna wazabuni wanadai hawajalipwa, bado kuna walimu wanadai madai mbalimbali ambayo yameshaelezwa na baadhi ya Wabunge waliopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nizungumzie habari za kilimo. Katika kilimo nitajikita kwenye pembejeo. Pembejeo ni tatizo kubwa tunaweza tukasema ni la Kitaifa. Pembejeo zinakuja wakati ambao huwezi kujua huu ni wakati wa kulima, ni wakati wa palizi,
itafika wakati tutaleta mbolea ya kuvunia, kama itapatikana baadaye, lakini naona wakati wa kupanda DAP haipatikani. Unapofika wakati wa palizi ndio DAP inapatikana, yaani mbolea ya kupandia, inapatikana wakati wa palizi. Muda wa palizi unakwenda wakati mwingine, sijui
mbolea ya kukuzia inakuja wakati gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ilikuwa ni hivi, wakati wenyewe wa kuleta mbolea ile siyo wakati muafaka. Wananchi hawana fedha kabisa, ni miezi ambayo siyo ya mavuno, mbolea ikifika wakati wananchi wamevuna, watakuwa na uwezo wa kununua hiyo mbolea na
itatumika muda muafaka majira ya kutumia mbolea yanapofika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nataka nizungumzie, mtaniwia radhi natumia miwani wakati fulani, kodi kubwa kwenye mishahara ya wafanyakazi. Ifikie hatua, Watanzania, wananchi, wafanyakazi wanalalamika kuhusu kodi kubwa. Hili bila kuliangalia,
wafanyakazi tunawapa mkono wa kulia, tunachukua mkono wa kushoto. Lazima tufike mahali tuangalie nchi zinazotuzunguka, tusiwe kisiwa, nchi za wenzetu katika Afrika Mashariki hii wameshafikia single digit. Sisi hapa Tanzania kwenye Vyama vya Wafanyakazi walipoulizia
habari ya single digit kwenye Kodi ya Mapato ya wafanyakazi wanaambiwa itafikiwa mwaka 2018, kuna tatizo lipi? Wafanyakazi hawana amani nalo wanalipwa mshahara, halafu unarudi Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni ya suala la kuimarisha Muungano. Nilitegemea Waheshimiwa Wabunge, suala la Zanzibar tungeliangalia wote kwa pa moja. Zanzibar siyo kwamba siyo sehemu yetu, lakini kunakotokea matatizo Zanzibar, tuyabebe wote kwa pamoja, tuyajadili kwa pamoja. Hapa imefikia hatua ukizungumzia habari ya Zanzibar, unaonekana wewe una matatizo. Hivi kati yetu hapa nani hakuwa kwenye uchaguzi? Baada ya uchaguzi matokeo yako yangefutwa, ungejisikiaje? Wenzetu wamefanya chaguzi tano, zikafutwa nne, ikabaki moja ndiyo salama.
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, niliibiwa muda mtakumbuka hilo. Kama uchaguzi mmoja ulikuwa salama, hizi nne zinakosaje usalama? Tuwe na huruma kwa wenzetu!
Mheshimiwa Naibu Spika, tufike mahali tukubaliane uchaguzi ulio huru na haki, siyo lazima ishinde CCM, muwe tayari kumeza pini, ifike hatua mseme hapa, ngoma ime-tight, tunakubaliana nayo, tunasonga mbele. Mataifa yanatucheka, tunachekwa na Mataifa kufuta
uchaguzi wa nchi nzima mwanzo mwisho, halafu mnabakiza Wabunge wa Jamhuri wenyewe hawa ni halali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda haraka haraka, fedha za Jimbo zimezungumzwa kwenye hotuba hii, nashauri na niungane na Wabunge wengine, fedha hizi ziangalie ukubwa wa Jimbo. Kama hazitaangalia ukubwa wa Jimbo, zitakuwa haziwezi kukidhi mahitaji yaliyokusudiwa katika Jimbo. Kazi yangu siyo kulinganisha ukubwa wa Majimbo, lakini uhalisia wa Jimbo. Fedha zifanane na uhalisia wa ukubwa wa Jimbo.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa afya, hali ni ngumu sana upande huo, bado wananchi hawana dawa kabisa, hali ni ngumu dawa hazipatikani. Niwaombe Mawaziri waliopo washughulikie hili wananchi waanze kupata dawa. Nakaa karibu na Burundi, kule Burundi
hospitali zake ni nzuri kuliko pale kwetu Kakonko na Watanzania wanaougua wanakwenda kutibiwa Burundi badala ya kutibwa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Burundi, yaani nchi ndogo kama ile ambayo ina vita ya asubuhi, mchana na jioni, ina dawa nzuri, kwetu tuna amani na utulivu, lakini dawa hatuna!
Naomba hili tuliangalie kabisa, Watanzania waanze kupata huduma za afya ndani ya nchi yao, inaweza ikatusaidia vilevile kurudisha imani kwa Serikali yao, pale ambapo inaanza kupotea.
(Makofi)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia na suala la maji.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Bilago tafadhali, naomba ukae muda wako umekwisha.
Nilikuwa pia nimemtaja Mheshimiwa Selasini ameshafika? Tafadhali endelea!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii. Naomba nianze na Utumishi na hasa nikiendeleza lile suala langu la asubuhi linalohusiana na ajira.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa kauli yake mwezi wa Sita mwaka 2016 kwamba inasitisha ajira huku ikifuatilia suala la watumishi hewa na kwamba zoezi hilo likiisha, ajira mpya zingetoka. Mpaka leo suala la ajira mpya halizungumzwi.
Mheshimiwa Spika, juzi wamezungumzwa wachache, walimu wa sayansi kama 4,000 na kidogo lakini kwenye orodha iliyotoka juzi, kuna walimu wawili wa masomo ya book-keeping na commerce, history na kiswahili na wao wameajiriwa kwenye hiyo orodha ya walimu wa sayansi.
Siwaonei wivu, lakini nataka kujua tu kwamba na hii history na kiswahili siku hizi ni sayansi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ifike mahali ituambie, uhakiki wa wafanyakazi unaisha lini na ajira mpya zinatoka lini? Watu wasikae na matumaini tu bila kujua wanaajiriwa au hawaajiriwi katika Awamu ya Tano. Nilitaka nizungumzie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba sekta ya elimu haina wafanyakazi/walimu wa kutosha. Afya haina wafanyakazi wa kutosha, kwa hiyo, Serikali itoe ajira na wale watoto walioko mitaani wanaendelea kuichukia tu Serikali bure bila sababu, wakati ajira zingeweza kutoka.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, wale hewa walioondolewa 18,000 kazi zao wanafanya nani leo? Hakuna replacement, pamebaki wazi au inakuaje? Hao wangeweza kuajiriwa wengine ingetusaidia kupunguza idadi ya ambao hawana ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la vyeti fake. Hili nalo limekuwa kizungumkuti katika nchi hii. Kuzungumzia vyeti fake nchi hii mpaka uwe na roho ngumu kwa sababu kuna cheti kimoja hapa sasa kimekuwa ni tatizo kabisa. Hiki cheti cha Bashite kina shida gani? Kina tatizo gani imekuwa sasa kinachafua mpaka jina la watu wakubwa kabisa. Hata mtu akifungwa magoli manne bila kitu chochote, wanasema ni
nne kwa Bashite; yaani tunaongeza misamiati isiyo na sababu. Hiki cheti cha Bashite kinalindwa kwa sababu zipi?
(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Waziri wa Utumishi utakapoanza kushughulikia vyeti kwa watu wasio na vyeti na kuchukua hatua, hiki cha Bashite sijui kitabaki wapi. Ingawa siyo mamlaka yako, lakini najua utashauri kwa utaratibu fulani ili na Bashite naye awajibike pamoja na wale walio na vyeti
fake na ionekane, isije ikatokea double standard katika hili.
Huyu achukuliwe hatua zake na huyu apate haki zake, tumalize suala la Bashite nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuzungumzia kidogo suala la utawala bora. Ukiona haki inapotea…
SPIKA: Mheshimiwa Bilago, hiyo Bashite ndiyo kitu gani? Mheshimiwa endelea kuchangia tu, endelea. (Kicheko)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Ni cheti cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambacho siyo cha kwake, alisomea cheti cha mtu mwingine. Kwa hiyo, nilitaka nacho kiangaliwe na Waziri anayehusika.
Mheshimiwa Spika, suala la utawala bora; ukiona haki inapotea; haki inakwenda sambamba na amani. Hawa maaskari wetu waliofariki Mungu awaweke mahali pema Peponi; mkiangalia kwenye mitandao, kwa nini baadhi ya wananchi wamefurahia? Yaani binadamu wenzetu
wanapoteza maisha, lakini baadhi ya watu wanafurahia kwenye mitandao? Ni kwa sababu kuna baadhi ya haki zinapotezwa na hao watu wanaokufa. Sasa wakifa, watu wanapumua kidogo. Kwa hiyo, tuangalie mahusiano, tulete mahusiano mazuri kati ya wananchi na vyombo vya dola vyote, Usalama wa Taifa, Polisi, Jeshi tuwe na mahusiano mazuri.
Shirikishi, watu walikuwa wanakwenda vizuri. Leo hii ukipita kwenye mitandao unaona watu wanakufa, wengine wanashangilia. Siyo kitu kizuri, hata mimi sikipendi. Siyo kitu kizuri, lakini chanzo chake ni pale ambapo haki ya watu inapotezwa, watu wengine wanaona sasa likitokea la
kutokea wapate mahali pa kupumua. Maandamano ya moyoni hayo, yanaendelea moyoni, watu wanaandamana.
Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumzie upande wa afya kidogo sana, kwamba Waziri wa TAMISEMI atusaidie namna bora ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kule kwenye Halmashauri zetu. Sasa hivi takwimu zinafikia kama 550.
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, tunapolizungumza kwenye Kamati yetu, tunaona kama lilihitaji Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI awepo na sijui kuna siku utatupa hiyo offer tumpate Waziri wa TAMISEMI kwenye Kamati yetu, wawepo pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Afya. Tukizungumzia la afya na elimu wote wakiwepo pamoja, nadhani inaweza ikawa na mantiki nzuri kwenye Kamati yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumzie suala la Wakala wa Barabara Vijijini, nimeliona. Suala hili linaweza kutufikisha mahali pazuri kama litasimamiwa vizuri, kwa sababu kuna baadhi ya barabara zinashindikana kutengenezwa kule kwenye Halmashauri zetu na hasa zile
zinazotokana na Madiwani wa Upinzani. Kwa mfano, Jimboni kwangu, ninazo barabara za kufungua Jimbo na nchi jirani ya Burundi; Rumashi - Burundi, Malenga - Burundi, Kiga - Burundi, Kimiha - Burundi, Katanga – Burundi; zile ambazo zina Madiwani wa CHADEMA hazitengenezeki kwamba zitaendelea kuwapa umaarufu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wakala huyu hawezi kuwa na tabia kama hiyo, nadhani atakuwa na tabia nzuri kuliko hii. Kwa hiyo, ni vyema hili jambo likaenda vizuri tukapata huyu Wakala wa Barabara Vijijini, anaweza akatusaidia kuliweka vizuri ili wananchi wapate barabara bila
kujali itikadi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ushuru wa mazao. Mheshimiwa Rais aliwahi kutoa maelekezo ya ushuru utozwe namna gani katika hotuba yake, akihutubia wananchi kwenye Mkutano wa Hadhara, likaanza kutekelezeka, lakini bado lina mkanganyiko. Ni ujazo gani unatakiwa kutozwa ushuru katika mazao haya ya nafaka na kadhalika? Maana debe moja halitozwi ushuru. Kule kwangu Kakonko, ukienda baadhi ya vijiji wanatoza ushuru debe moja, baadhi ya vijiji hawatozi debe moja. Kwa hiyo, kunakuwa na mkanganyiko.
Mheshimiwa Spika, hebu tupate uniformity nchi nzima; mazao yatatozwa ushuru wa ujazo wa kiasi fulani ili kuondoa huu mkanganyiko katika nchi.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni elimu. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, tuepuke madeni ya walimu yasiyo na sababu. Mkurugenzi anaamua anahamisha walimu 50, 60 hana hata senti tano, anawaambia nendeni tu mtalipwa.
Watalipwa na nani? Kama huna hela ya kuwalipa watu, usiwahamishe. Kuna walimu 85,000 mwaka jana walipanda madaraja; tena madaraja ya kufungua vidato (E to F; F to G; G to H; H to I). Wale watu wage bill yao ya mwezi ni shilingi bilioni 21; inaendelea ku-pile up tangu mwaka 2016.
Mheshimiwa Spika, ni vyema Serikali ingelipa hili deni likasimama kwanza wakabaki wanadai hizi nyingine. Yaani likasimama kwa sababu kila mwezi kuna shilingi bilioni 21 na ndiyo inakwenda kufika kwenye shilingi trilioni 1.06 wanayodai Walimu nchi hii.
Mheshimiwa Spika, sasa na Walimu wenyewe wamesema wanadai, imeanza kufanyika uhakiki; uhakiki huu ni kama una dalili za delaying tactics, yaani unafanya uhakiki polepole ili usifikie wakati wa kulipa, lakini mwisho wa siku deni lile lipo na walimu wanaendelea kuhangaika nchi hii, wanafanya maandamano moyoni, wanafanya mgomo wa kutofundisha moyoni. Hawa watu kama hawajatekelezewa mambo yao, hawawezi kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, mimi ni mwalimu, nimefundisha darasani, nafahamu namna ya kugoma polepole. Kwa hiyo, tuwatekelezee mambo yao. Mwalimu huyo huyo, kimshahara hicho kidogo, halafu hata madai yao, zaidi ya Walimu asilimia 70 wote wana madai.
Taarifa....
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, ni ukweli usiopingika kwamba mimi ni mtu mzima, nina zaidi ya nusu karne. Kata hizo ninazozizungumza barabara zake, inaanzia ndani ya Kata inaenda mpakani mwa Burundi; haiwezi kupita kwenye Kata nyingine. Lazima ianzie ndani ya Kata kwenda mpakani. Sijazungumza barabara za ndani, niko makini na hilo. Kwa hiyo, nilikuwa nalizungumza hili kwamba huyu Wakala wa Barabara Vijijini anaweza akatufikisha mahali pazuri kama kweli utaratibu utakwenda kama ulivyopangwa.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa bado naendelea na hoja ya walimu nikitaka kuzungumzia juu ya motisha kwa walimu. Tuliwahi kutoa wazo wakati niko Chama cha Walimu na walimu wa nchi hii niwaambie wana matumaini makubwa sana na Serikali hii.
Kwanza, wakijua Rais ni mwalimu, Waziri Mkuu ni mwalimu, tena kiongozi aliyekuwa wa Chama cha Walimu kama mimi, huenda hata mimi tutakaposhika Serikali nitakuwa Waziri Mkuu, kwa sababu ndiyo Makatibu wa Chama cha Walimu wameanza kuwa Mawaziri Wakuu.
Kwa hiyo, walimu wana matumaini makubwa sana juu ya hili, tunaomba Serikali iwasikilize. Najua na sekta nyingine, sawa wana madai lakini tuangalie hii population kubwa ambayo inagusa karibu kila kijiji, kuna mwalimu anayekuwa na madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, motisha ambayo tulikuwa tunazungumzia ilikuwa ni teaching allowance. Teaching allowance mpaka leo haizungumzwi kabisa. Naomba Waziri anayehusika anaposimama atueleze, teaching allowance lengo lake ilikuwa; muda wanaofanya kazi walimu ni tofauti na sekta nyingine. Walimu walioko shule za bweni (boarding) wanatakiwa kuangalia watoto usiku mpaka asubuhi. Mtoto
akiugua, mwalimu anampeleka hospitali. Muda wa kusahihisha, mwalimu hawezi kusahihisha shuleni akamaliza kazi, lazima kazi ile aende nayo mpaka nyumbani, itamfuata mpaka nyumbani.
Kwa hiyo, ndiyo maana tukasema teaching allowance iwepo ku-offset hizi gharama za overtime na kadhalika. Nayo ilifanywa vizuri tu wakati ule wa Tume ya Makweta, ikaja ikatuletea taarifa nzuri kama hiyo na Walimu wakawa wanapata teaching allowance. Wale tuliofundisha zamani
kama mimi, nilikuwa napata 55 percent ya mshahara wangu, kwa sababu mimi ni mwalimu wa sayansi.
Kwa hiyo, Serikali ikifanya hilo, ita-motivate walimu, itawafanya waipende kazi yao na wafundishe watoto wa nchi hii ili tuweze kupata wataalam wazuri katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kuzungumzia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Buyungu, Wilaya ya Kakonko linazalisha mazao ya chakula na biashara. Mazao ya chakula huzalishwa kwa wingi kama mahindi, maharage, mihigo, ufuta, mpunga na kadhalika. Mazao haya huuzwa pia kama ya biashara ili kupata kipato. Wakulima wanaouza mazao nje ya nchi yaani Burudi wengine hupata misukosuko bila sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nashauri wakulima hawa waruhusiwe kuuza mazao yao Burundi kwani bei ni nzuri. Aidha, zao kubwa la biashara ni tumbaku ambayo nayo inauzwa kwa deni/mkopo ambao unalipwa kwa tabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao kukatwa/kuharibiwa na wakimbizi. Kambi ya Wakimbizi Mtendeli-Kakonko imeharibu mazao/mashamba kwa kiasi kikubwa bila fidia yoyote. Serikali itoe fidia kwa wakulima waliopata madhara haya kwani wameharibiwa mazao ambayo yangewasaidia kwa chakula na kwenye pato la familia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vocha za pembejeo Wilaya ya Kakonko kuna chembechembe za rushwa na udanganyifu wa kutosha. Mfano, mbolea na mbegu haziwafikii wananchi kwa wakati na wakati fulani wakulima wanasainishwa vocha bila kupewa pembejeo na hivyo kulipwa fedha kati ya shilingi 10,000 hadi 20,000 au 5,000 tu, hii ni hatari. Nashauri pembejeo zifike Wilaya ya Kakonko mwezi Agosti kila mwaka na ziletwe za kutosha kwa kila kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha umwagiliaji Jimboni kimesusua kwani miundombinu imeharibika maji hayafiki mashambani. Nashauri suala hili nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya ufugaji katika Wilaya ya Kakonko si nzuri sana kwani hata wale wanaofuga ng‟ombe wanakabiliwa na wizi wa mara kwa mara na kwenda kuuzwa Burundi, hali hii inakatisha tamaa. Aidha, wafugaji wanaohitaji kuuza mifugo nchi jirani ya Burundi hupata misukosuko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hali ya majosho siyo nzuri kwani hakuna josho hata moja wilaya nzima kwa hiyo mifugo inashambuliwa na wadudu ambao mwisho wake huleta magonjwa. Kuna uhaba pia wa dawa za mifugo na chanjo hali ambayo huongeza vifo vya mifugo kama ng‟ombe, mbuzi, kuku, kondoo na kadhalika. Vile vile kuna uhaba wa Maafisa Ugani Wilaya ya Kakonko wakati waliohitimu wakiwepo mitaani bila kupewa ajira. Hali hii husababisha wafugaji kufuga kienyeji mno na hivyo kutokuwepo na tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya uvuvi Wilayani Kakonko haijapewa kipaumbele. Sababu kubwa ni wananchi kukosa mwamko wa shughuli za uvuvi; wananchi kukosa utaalam wa uvuvi; wachache wanaojitokeza kutaka kufanya ufugaji wa samaki hukosa vifaranga vya kupanda kwenye mabawa na uchimbaji wa mabwawa ni mgumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya jumla (general comment) ni kama ifuatavyo:-
(i) Bajeti ya Wizara ni ndogo sana, majukumu mengi;
(ii) Serikali itafute ufumbuzi/utatuzi wa migogoro ya wafugaji na wakulima. Yatengwe maeneo ya kila mhusika. Aidha, elimu itolewe kwa wafugaji kupunguza mifugo yao ili iweze kupata maeneo ya kufugia;
(iii) Wafugaji washauriwe ili wasihamehame ili watoto wao wasome shule;
(iv) Bajeti ya mbolea mwaka huu iongezwe toka shilingi bilioni 78;
(v) Tafiti za kilimo zisaidie kuinua ubora wa kilimo, mifugo na uvuvi; na
vi) Ziwa Tanganyika kuna samaki wengi ambao hawajavuliwa kutokana na zana duni za uvuvi (Low quality fishing gears). Serikali inunue meli za uvuvi zinazovuna na kusindika samaki (fishprocessing).
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio cha wananchi wa Kakonko kutosikia chombo cha Taifa yaani TBC Redio. Hali hii hupelekea wananchi hao kusikiliza redio za nchi jirani kama Burundi na Rwanda, hivyo kukosa haki ya kujua nini kinaendelea nchini mwao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri ujengwe mtambo wa kuwawezesha kusikiliza redio yao ya Taifa (TBC), mtambo wa Kigoma Mjini uboreshwe ili usikike mkoa mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kakonko haina Afisa Habari, Utamaduni na Michezo. Hali hii inawanyima vijana haki ya kupata fursa ya elimu juu ya utamaduni, sanaa na michezo kwa kukosa mtalaam huyo. Nashauri aajiriwe mtalaam huyo mapema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanja vya michezo vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi, baadaye vikachukuliwa na CCM. Viwanja vingi vina hali mbaya, havina hadhi ya kuendeshea michezo. Nashauri kwa nini visibinafsishwe kwa wadau wapenda michezo, vichukuliwe na Jeshi kama vile SUMA ili waviendeleze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ijipange kuandaa timu ya Taifa ambayo ina mrengo wa kucheza Kombe la Dunia, maandalizi haya yaanzie ngazi ya chini kwa vijana wadogo na ichukue muda hata miaka kumi kwa kuweka kwenye shule maalum (sport academy).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu motisha kwa wachezaji na wasanii hodari; Serikali iwe na utaratibu wa kutoa motisha kwa wachezaji hodari na wale wanaoileta sifa kwa nchi hii kama vile Ndugu Mbwana Samatta, Ndugu Francis Cheka na wengine. Mfano mzuri wa kuigwa ni wachezaji wa timu ya TP Mazembe ya Congo ilivyotwaa Kombe la Afrika, wachezaji wake walizawadiwa magari aina ya Prado tena mapya kila mchezaji. Hii pia ifanyike kwa wasanii wanaofanya vizuri nchi za nje kama vile Diamond, Mpoto na wengine.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii adhimu. Awali ya yote, nawapa pole wanawake wote waliodhalilishwa jana, maana pande zote walidhalilika; wanawake hawana chama; kudhalilishwa hakuangalii chama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kwanza nijue suala la viwanda kama ni vision ya nchi au ni vision ya Mheshimiwa Rais? Mheshimiwa Waziri baadaye akija atusaidie, atuambie kama ni ya Mheshimiwa Rais atusaidie. Atakapovianzisha, hawataviuza wengine? Maana vilikuwepo, wakauza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri, kama inawezekana, kwa baadhi ya vitu tunavyoanzisha tuwe tunatunga sheria ya kuvilinda hivyo tulivyovianzisha. Yaani siyo tunaanzisha, anakuja mtu mwingine baada ya miaka mitano, naye anabadilisha anakuja na mambo mapya mengine kabisa, kama vile hatukuwahi kuwa na kitu chochote hapa nchini. Kwa hiyo, hata hiki kitu kama kingefanikiwa, kitungiwe sheria ya kudhibiti, atakayekuja asikiharibu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa nchi zilizoendelea, waliouza viwanda vyetu wangekuwa ndani, jela! Walitakiwa wawe jela, maana mlijua kabisa ili twende kwenye uchumi imara wa nchi hii ni kuwa na viwanda na lilijulikana mapema, lakini sasa hivi ndiyo linatokea, linashamiri baada ya kuwa tumeviuza vile tulivyokuwanavyo. Maana yake nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba wale walioviuza ndio wametufikisha kwenye uchumi mbovu tulionao! Kwa hiyo, nchi za wenzetu zilizoendelea, hawa walitakiwa watangulie Segerea ili watusaidie kujibu kwa nini wameifanya nchi kuwa maskini kwa kuuza viwanda ambavyo vingetupeleka mahali pazuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze mambo madogo kabisa yanayohusiana na viwanda. Wala tusiende kwenye viwanda vikubwa sana vya mtani wangu Mheshimiwa Mwijage, akiyaeleza unaweza ukadhani kesho asubuhi hii nchi inakuwa mbinguni. Hii nchi ni Tanzania ile ile, hii hii! Haiwezi kubadilika katika wiki moja, mbili, miaka mitano au kumi, haiwezekani! Atusaidie! Tena nimshauri, ni mtani wangu, aongee machache, atende mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni hii hii ambayo machungwa yanaoza, hakuna anayeshituka; maembe ya wakulima yanaoza, hakuna anayeshituka; nyanya za Watanzania zinaoza, mnaagiza tomato sauce Ulaya na mko hapa hapa! Nanasi zinazooza ni nyingi! Nani kiongozi wa Serikali anaona uchungu kwa mazao yanayoweza kufanyiwa process ya viwanda na akashituka akasema hapa tuweke kiwanda? Tunaangalia tu! Wala havihitajiki viwanda vikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kawaida sana vingeweza kututoa hapa tulipo kwenda mbele zaidi. Tunafikiria makubwa wakati uwezo wa makubwa hatuna. Hii bajeti ya Mheshimiwa Waziri haiwezi kutengeneza hayo yote tuliyoyasema na wafadhili tunaowategemea, Mheshimiwa Waziri atuambie, walikaa mkutano wapi, kwamba watakuja waweke viwanda Tanzania? Watakuja wawekeze viwanda vyetu Tanzania; uwekezaji Tanzania sasa hivi nao unaanza kuwa shida na unaanza kuwa taabu! Masharti lundo! Kwa hiyo, tungeanza na vitu vya kawaida, vya chini mno! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za wenzetu; nimeona Uingereza, mwananchi mkulima wa kawaida mazao yakiharibika, Serikali ina-compensate.
Sisi hapa halipo! Tunaliona la kawaida tu! Tena mazao yakiharibika ndiyo mnakwenda, jamani poleni, zile nyanya vipi, zimeharibika? Yaani ni jambo la kawaida tu, lakini hatujui nguvu aliyotumia, familia yake itaishije kwa taabu kabisa katika mazingira kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumzia viwanda Kigoma kwenye swali asubuhi. Mpango ule wa Kiwanda cha miwa na sukari Kigoma kilianza Bunge la Kumi. Mpaka leo hakuna muwa hata mmoja pale Kigoma! Kwenye kitabu chako hiki, hakuna hata ukurasa uliotaja ile miwa ya Kigoma, hakuna! Sasa watakujaje humu hawamo? Hata hao wawekezaji wenyewe ambao wangekuja! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli tunahitaji kukaa vizuri na hili suala la viwanda. Tusiwaaminishe sana Watanzania, baadaye watatuuliza maswali haya haya, humu humu kwamba hivi mlisema viwanda yaani kwa mbwembwe kwa mkwara kweli kweli, mmefika wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo naona linaleta shida, ni biashara ambayo iko chini ya Waziri mwenyewe. Nchi hii kufanya biashara ni risk yaani owners risk. Hakuna mazingira rafiki ya kufanya biashara katika nchi hii. Wakati wa uchaguzi mimi huwa naupenda sana, ni kwa sababu tu unakuwa ni muda mfupi. Watu wanafaidika na mambo yote mabaya yanasimama ili watu wapate kura, baada ya hapo yanarudi yale yale mabaya waliotendewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna watu wanateseka nchi hii kama bodaboda! Wanakimbizwa na polisi kila asubuhi! Tujiulize, wale watu wa bodaboda wangekuwa hawana hizo bodaboda, nani angekuta side mirror kwenye gari lake? Ujambazi ungekuwa mkubwa kiasi gani? Watu wametafuta ajira binafisi, lakini wanakimbizana na polisi kila asubuhi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu, Wilayani kwangu Kakonko ili uweze kupata TIN Number unakwenda kilometa 300 za barabara zisizo na lami, kuifuata Kigoma Mjini. Unamwambia mtoto wa watu afuate hiyo TIN Number, halafu afuate na leseni, sijui na vidude gani, kilometa 300, anakimbizana na oolisi tu! Bodaboda wangapi wamekufa wakiwa wanakimbizwa na polisi ili wawakamate tu wachukue fedha? Matokeo yake sasa umekuwa ni mradi wa polisi na mwenye bodaboda. Bwana eeh, una leseni? Wewe unaniulizaje leseni na jana sikuwanayo, unaniuliza leo tena? Anachukua fedha zake, anaweka mfukoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawakatisha tamaa wafanyabiashara wa nchi hii. Biashara ya maduka, VAT inasema hivi ili uweze kulipa VAT TRA, mwenye biashara awe na bidhaa inayozalisha shilingi milioni nne kwa mwaka. Wanakimbizana na wauza soda vikreti viwili, anakuja anampigia hesabu mtu wa TRA, wewe unauza soda, eeh, kreti tano kwa siku mara siku 30 mara mwaka mzima, anamtoza kodi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Naomba nianze na hoja ambayo iliwahi kuletwa hapa kwenye Bunge la Kumi na Mheshimiwa Margaret Sitta, baadaye ikapigwa danadana, sijui alikosa nguvu huyu, sasa nimekuja nimsaidie, tuongeze nguvu katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja Mheshimiwa Waziri wa Afya anaitangaza kwa nguvu zake zote; hoja ya fifty by fifty. Mheshimiwa Waziri, huwezi kufanikiwa hii hoja kama watoto wa kike wanaobeba mimba mashuleni waharuhusiwi kurudi kusoma. Utakwama tu! Utakwama mapema kwa sababu tunapofanya enrolment shuleni wanafunzi wa kike 50, wa kiume 50 au 40 kwa 40. Mwisho wa siku wale wasichana wako wanabeba mimba, wanaume wanabaki. Hiyo hamsini utapata wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekwenda Zambia, nimeisoma vizuri kweli! Kwa kweli kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari, niende naye Zambia hata kwa nauli yangu. Twende ukaone kitu kinaitwa Return to School Policy. Sera ya Wanaopata Mimba Mashuleni, wananyonyesha miezi mitatu, wanarudi kusoma shuleni. Sisi hapa sijui tuna tatizo gani? Hii ndiyo tumeiona dhambi kubwa kuliko nyingine tunazozifanya. Watoto wa kike wanabeba mimba mashuleni, tunawaacha na hakuna anayefuatilia maisha yao ya baadaye! Hili nitaanza nalo mwaka huu na mpaka nitakapotoka humu, sitaliacha! (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Zambia tulipouliza, nini madhara? Yaani haliongezi kasi ya mimba? Walituambia kasi ya mimba imepungua kwa sababu wanaporudi they fill shy. Kwa hiyo, wale wenzao wana-learn through them, kwamba kumbe kubeba mimba ni tabu! Wanarudishwa mashuleni kwa lazima! Lazima urudi shule! Sasa wewe umerudi, ulishabeba mimba tena miezi kadhaa kabla ya kujifungua, ndiyo unaruhusiwa ukajifungue, wote wameiona pale shuleni inaonekana na unarudi wanajua umemaliza kunyonyesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, na wenzao wanasema haiwezekani na wao yawakute hayo. Sisi hapa tunaona kwamba ndiyo tutakuwa tumewahamasisha sasa kwamba mambo ni bomba! Naomba tuone uchungu, akinamama mwone uchungu! Nanyi msingekuwa humu! Hao 400 ambao kwa mwaka wanabeba mimba, maisha yao ya baadaye yako wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani akina mama wengi wataniunga mkono, nami katika hili nitakuwa ambassador, tuokoe hiki kizazi kinachoteketea bila elimu. Mwisho wa siku watoto hawa ndiyo wanakuwa mitaani. Yaani umaskini unatengenezwa na sera zetu wenyewe. Wanakuwa maskini, wanaishia kuwa ombaomba, wanatupa watoto, kama vile watoto wale hawakuwa na haki ya kuja duniani. Naomba hili tuendelee nalo; Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, hawa watoto watarudi kusoma? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambalo nilitaka nilizungumzie jioni ya leo ni viumbe ambavyo vipo hatarini kupotea nchini. Viumbe ambavyo viko hatarini kupotea nchini ni wanawake weusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanawake weusi wanapotea Tanzania. Katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri ameeleza ukurasa kama sabini na kidogo anavyopambana kudhibiti vipodozi visivyo salama kuingia nchini. Vile vipodozi vinaingia, halafu tunapambana kuvitafuta vilipokwenda kutumika. Badala ya kuzuia visiingie, tunasubiri viingie, kwanza, halafu tupambane na kuvitafuta vilipokwenda. Ni hatari kweli kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Tunduma ukaambiwa tafuta mwanamke mweusi utapata shida! Kwa sababu ya Carolight zilizoko pale! Carolight ni vipodozi ambavyo ni vya hatari, vimepigwa marufuku na vinaendelea kuuzwa. Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie, haya madhara wanawake wanayoyapata ya kansa za ngozi na vipodozi vinaendelea kutumika na mwisho wa siku wanawake wetu weusi wazuri wanapotea. Lazima tuchukue hatua juu ya hili! Hatuwezi kuliacha linaendelea tu; na vipodozi haramu. Unasikia zimechomwa tani na tani za vipodozi, vilipita wapi? TFDA wako wapi? Wanafanya kazi gani? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atusaidie juu ya hilo, maana tutakuja kufikia hatua ya kutafuta mwanamke mweusi, unaenda kwenye Google ndio unamwona mwanamke mweusi wa kitanzania ni yupi na alikuwa anafananaje? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hoja ndogo sana kwa wazee, Mheshimiwa Waziri atuambie kama pension kwa wazee ilishindikana, haya mambo tuyafute yaishe kuliko tubaki tunasema itakuja, itakuja. Wakati fulani tulisema tunatafuta umri wa wazee ni upi? Hivi mzee si anajulikana umri wake? Nchi hii hatujajua hata wazee ni wa umri gani? Retirement age Serikalini inajulikana 60, ukianza 60 hapo tayari wewe ni mzee. Kuna watu wame-extend wakasema twende 75. Sijui inakuwaje 75! Lengo lilikuwa ama wapungue wazee wasiwe wengi labda, tuweze kuwalipa vizuri; lakini miaka 60, huyo ni mzee. Hawa Wazee tuwape pension hata fedha kidogo, maisha yao ni magumu mno. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwelewe kwamba hawa wazee ndiyo wanaopiga kura vizuri. Yaani mngewapenda hawa, mambo yangekuwa mazuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hoja ya wazee….
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkoa wa Kigoma kitu ambacho kimeifanya Kigoma iwe hivyo ilivyo ni ukosefu wa barabara. Barabara ndizo zimetufanya tuonekane hatuna thamani yoyote, mfanyakazi akipangiwa kazi Kigoma anajiuliza mara mbili mbili niende au nisiende, akienda unamuuliza umekujaje na umefikaje hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu ambavyo mkoa wa Kigoma lazima utendewe haki ni kuufungua ule mkoa na kuutoa kwenye minyororo ya ukosefu wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Kigoma - Nyakanazi tangu nilipoanza kusikiliza na kuangalia Bunge imekuwa ikitwajwa mpaka leo na mimi na umri huu nimeingia humu naikuta barabara hiyo inaendelea kutajwa. Watakuja na wengine huenda wakaikuta tena barabara ya Nyakanazi inatajwa, kuna tatizo gani na Nyakanazi na Kigoma? Tuna dhambi gani watu wa Kigoma mpaka barabara hii inayotuunganisha na Mwanza na Kagera isifunguke, barabara hiyo moja tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia pesa zilizotengwa kwenye barabara katika vipande vile viwili ni shilingi kama shilingi bilioni 40 ambazo tuseme zinaweza zikatengeneza kilometa kama 40, lakini kuna wakandarasi wa kilometa hamsini hamsini, Kidawe – Kasulu na Kabingo – Kakonko kwennda kwenda Nyakanazi kuna shilingi bilioni 40, zitafanya kazi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine kikubwa kabisa cha kuiunganisha barabara hiyo hatuoni eneo linalotoja Kabingo, Kibondo, Kasulu, Manyovu, kilometa 258, hakuna kitu kinachozungumzwa pale. Kwa maneno mengine hii barabara bado ina safari ndefu ya kwenda. Tunaambiwa kuna fedha za ADB zimetengwa, labda Waziri akisimama atatuambia ziko sehemu gani kwasababu kwenye vitabu vyake vyote fedha hizo hazionekani, na kama hazionekani maana yake ni nini? Hiyo barabara haitatengenezwa kwa mwaka huu wala kesho wala lini. Na kwa kipande kilichopo tukikitengeneza kwa shilingi bilioni 40, sijui tunahitaji miaka mingapi kumaliza barabara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ya kuifungua Kigoma ni Kigoma – Uvinza, Kaliua – Urambo – Tabora. Hiyo isipofunguka bado tuna taabu. Sisi Kigoma ndio tunaolisha Tabora na wao wanafahamu ndiyo maana watu wa Tabora wala hawatuchokozi maana tukifunga hiyo barabara msosi Tabora itakuwa shughuli. Kwa hiyo, lazima hiyo barabara itengenezwe. Kuna pesa zimetengwa tena pale ili kukamilisha vipande vya kuanzia Uvinza kwenda Malagarasi na Kaliua hadi Urambo bado kuna shida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ambayo lazima ifunguliwe ni ya kuanzia Uvinza kwenda kwa watani wetu Mpanda hadi Sumbawanga. Barabara hizo zikifunguliwa utaona tu kwamba kila mtu anatamani kuhamia Kigoma, kwa sababu katika mikoa ambayo haijachakachuliwa ardhi ni Mkoa wa Kigoma, na barabara hizo zikishafunguka tutapata wageni wengi kuja kuwekeza katika mkoa wetu. Hatuwezi kupata wawekezaji kama hakuna barabara. Hata vile viwanda vilikuwa vinazungumzwa na Mheshimiwa yule mtani wangu, nilikuwa najiuliza wale wawekezaji watapita wapi? Na hata wakiwekeza viwanda bidhaa za viwanda wataziuzaje hakuna barabara? Ni land locked region, huwezi kutoka, ukiingia unashukuru Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuzungumzia reli hujazungumza kitu chochote katika nchi hii. Na tukitaka kujikomboa lazima hii reli tuitengeneze. Nchi makini zinatengeneza reli, nchi makini zinasafirisha bidhaa kwa kutumia treni, sisi tumerundika malori barabarani rundo. Kuna mtu mmoja aliwahi kusema haya malori ni ya nani? Mbona tukizungumzia kujenga reli hakuna ile motive ya ujenzi wa reli, kuna watu wanalinda linda haya malori haya? Maana mimi sikuona hata sababu kwa mfano Dar es Salaam – Mbeya malori yote yale ya nini wakati TAZARA iko pale na iko vizuri tu? Lakini ukizungumzia malori yale yatoke barabarani unatafuta matatizo. Mtu mmoja aliwahi kulizungumzia hili nadhani lilim-cost alipokuwa Waziri wa Uchukuzi – lilitaka kumgharimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu zangu niseme reli ya kati kwa standard gauge ni jambo ambalo haliepukiki kwa gharama yoyote. Kama tulishakopa vitu ambavyo huenda hata havikutusaidia sana tunatafuta mkopo sasa wa kujenga reli ya kati na matawi yake yote kuingia nchi zenye rasilimali Burundi, Rwanda na Congo kwa tawi litakaloishia Kalema ili tuweze kujikomboa kiuchumi. Reli hizo zitatusaidia katika maisha yetu haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata umasikini kwasababu hatuna infrastructure za uhakika. Yaani wakati fulani unaweza ukajiuliza hivi anaetufanya tuwe maskini ni nani? Tumerogwa na nani nchi hii? Kumbe ni wakati fulani inawezekana hata kufikiri kwenyewe kwetu si kuzuri zaidi. Tunahitaji kufikiri vizuri zaidi ya leo. Na ndugu zangu tunapozungumza suala la Kitaifa kama hili tunaondoa itikadi zetu, tunakomaa pamoja. Hii reli hakuna reli itakayojengwa ya UKAWA, reli ikijengwa kwa standard gauge hapa ni nchi nzima tutaona matunda yake na faida zake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie bandari. Kuna nchi ambazo zina bandari ndogo ndogo tu lakini zimetengeneza uchumi wake vizuri.
Wakati fulani ni aibu nchi kuwa maskini wakati ina bandari kubwa. Una bandari ya Dar es Salaam, una bandari ya Tanga, una bandari ya Mtwara, bandari kubwa zinazoingia na kutoka nchi nyingine za nje. Kinachotu-cost kwenye bandari yetu hii, hatujawekeza vizuri zaidi. Ushauri umetolewa kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani ukilinganisha na bandari za wenzetu wanavyo improve kuweka gat za kutosha; sisi sijui tuna politic! Wakati fulani huwa napata hata jina zuri la kutumia; lakini niwaambie kufanya biashara na bandari ya Dar es Salaam si rafiki kwa wafanyabiashara wanaopitisha mizigo pale Dar es Salaam, kuna red tapes kibao. Yaani urasimu mwingine hata usio na sababu, watu wanapoteza muda mwingi wa kutoa mizigo bandarini wakati bandari zingine mzigo unatoka kwa njia rahisi sana. Hiyo inatupotezea mapato mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na Mheshimiwa Waziri ukitaka hili likuokoe komaa na bandari, punguza urasimu pale bandarini. Yaani mimi nashindwa kuelewa bandari ya Dar es Salaam, mna-operate yaani hakuna electronic system ya kutoa mizigo na kulipia na kufanya nini. Unakuta watu wamebeba makaratasi anatoka TRA anakimbia kwingine, kwa nini usilipe TRA na karatasi lako likaonekana bandarini kwa electronic system? Tuna operate kama wakulima tu wa kijiji fulani hivi, wasomi wakubwa, maprofesa na madaktari tunashindwa kuweka system ambayo mtu akilipa TRA akienda bandarini anakuta inasomeka na inampunguzia muda. Panda, teremka, ukifika kule wanakwambia hatujapata karatasi kutoka TRA, ukienda TRA wanasema tuliyemtuma yuko njiani anapeleka hizo karatasi. Haya maisha ni ya kizamani kabisa kabisa na ni ya ujima kabisa! Sijawahi kuona kitu kama hicho katika nchi ambayo inaendelea ya sayansi na teknolojia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie simu fake. Hizi simu fake zilipongia mlichukua ushuru na mliendelea kupata kodi kwenye voucher zinazoingia kwenye simu fake. Leo mnatangaza sijui tarehe ngapi mnazizima, kwanza mmesha- calculate mtapoteza kiasi gani kwenye mapato ya nchi hii? Kwa sababu watumiaji wengi ni wale wanaosema walinunua simu fake, na aliejua simu fake ni ninyi, mliziuzaje zikiwa fake? Yaani ni kama mchezo wa kuigiza mnasema leta hizi simu mnaingiza zinauzwa halafu baadaye mnawaambia; jamani mna habari hizi zilikuwa fake? Sasa zilikuwa fake sisi tungejuaje? Mimi mnunuzi nina haja ya kuuliza hii ni fake? Na ukiuliza hii ni fake muuzaji anakwambia hii ndiyo original! Mimi natoka kijiji cha Kasuga, hivi kule Kasuga Kakonko najua original ni ipi na fake ni ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Buyungu, Wilaya ya Kakonko bado kuna migogoro midogo midogo ya wananchi wanaoingia Burundi na Warundi wanaoingia Tanzania, wanapata usumbufu wa hapa na pale hasa ule wa polisi. Wilaya imepakana na Burundi kwa eneo lote la Magharibi yaani Vijiji vya Mugunzu/Kiduduye, Katanga, Ihabiro, Gwanumpu, Bukirilo, Malenga/Kikulezo, Kiga, Kasuga, Nyakeyenzi, Muhange, Gwarama/Kabare, Nyakibuye, Rumeshi, Kinyinya na Nyanzige (Kata ya Nyamtukiza).
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi hawa wanapata usumbufu kwenda kuuza au kununua mazao/biashara Burundi. Wananchi hawa wanakamatwa na polisi na kunyanga‟anywa bidhaa na fedha bila sababu. Aidha, Warundi nao wananyanyaswa na polisi na kuibiwa/kunyang‟anywa pesa/bidhaa wanazouza au kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri yafuatayo:-
(i) Umoja wetu wa Afrika Mashariki uwanufaishe wadau wa nchi
wanachama;
(ii) Polisi wazuiliwe kuwaonea na kuwanyang‟anya Warundi bidhaa toka Burundi mfano kama bia za Primus, Amstel, sabuni na kadhalika; na
(iii) Masoko ya mipakani (Burundi/Tanzania) yasiwekewe vikwazo vya nani/nini uuze/ununue kutoka nchi zetu za Burundi na Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitaifa nina ushauri ufuatao:-
(i) Viza za nchi zote zenye Mabalozi hapa nchini zitolewe humu nchini bila urasimu kama za Uingereza zinatolewa South Africa;
(ii) Mabalozi/ofisi za Tanzania nje ya nchi watangaze vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini kama vile hoteli za kitalii, mbuga za wanyama, Mlima Kilimanjaro na kadhalika. Mfano miaka ya 2005-2008 Uingereza hapakuwa na matangazo ya kutosha kwa watalii kuja Tanzania na hata hoteli zilizoonekana ni za Kenya na Zanzibar tu. Mlima Kilimanjaro uliendelea kujulikana kama upo nchi ya Kenya; na
(iii) Afrika Mashariki haijatulia hasa viongozi wa nchi pale wanapogombania rasilimali zinazopatikana nchi moja au nyingine. Kwa mfano mafuta ya Uganda kuletwa Tanzania, Kenya haifurahi, reli kwenda Rwanda toka Tanzania baadhi ya nchi wanachama hawafurahii. Nashauri wakae na kuelewana ili chokochoko ziishe.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya maskini – Mpango ueleze namna ambavyo wilaya maskini zitasaidiwa kutoka kwenye lindi la umaskini kama ilivyotangazwa kwenye Bunge la Bajeti 2016. Wilaya ya kwanza ni Kakonko ikifuatiwa na Biharamulo. Wilaya hizi zisaidiwe kwenye kilimo (pembejeo za bei nafuu kwa wananchi wote), ufugaji, mabwawa ya samaki, viwanda, vidogo vidogo vya kuchakata mihogo, ujasiriliamali na elimu yake. Wilaya hizi zisipopata boost ya kiuchumi zitaendelea kurudisha nyuma uchumi wa nchi (overall).
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara; zipo barabara za Kidahwe hadi Nyakanazi zitengewe fedha za kutosha. Aidha, ikumbukwe Manyovu-Kasulu hadi Nyakanazi, pia barabara ya Sumbawanga-Mpanda-Nyakanazi, kwa nini zisitajwe hivi:-
(i) Manyovu-Kasulu-Kibondo-Kabingo (mpya)
(ii) Sumbawanga-Mpanda-Uvinza-Kasulu (mpya)
Mheshimiwa Naibu Spika, Nyakanazi-Kabingo inaendelea, bajeti iwepo, Kidahwe-Kasulu-Nyakanazi iendelee kutengewa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pato la Taifa; hali ya pato la Taifa kukua litafsiriwe kwenye hali nzima ya maisha ya Watanzania. Haiwezekani pato la Taifa limekua, wananchi wanabakia maskini, karibu Watanzania milioni 20 ni maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tozo na Kodi; kumekuwa na tozo nyingi kwa wajasiriamali na shughuli zao. Mfano tozo za mazao kama korosho, kahawa na kadhalika wajasiriamali wadogo kama bodaboda wametozwa ushuru wa parking; parking fee. Kodi mbalimbali za bandarini zipunguzwe ili zivutie wawekezaji wengi kuja Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyabiashara wamezuiliwa kukata leseni za biashara za halmashauri na kuamriwa wakalipe mapato TRA jambo ambalo limewafanya washindwe kufanya biashara hivyo kupotea kwa mapato ya halmashauri/Serikali Kuu. Mfano mfanyabiashara mwenye mtaji wa laki mbili anataka kufungua biashara ndogo anaenda TRA anatakiwa alipe kodi ya laki moja nukta tano kitu ambacho hakiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushuru juu ya mapato kuongezeka; mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara. Hali ya kisasa iwe nzuri isiyodhibiti demokrasia nchini. Utulivu wa kutosha usioleta shaka/hofu kwa wawekezaji. Mfano, Serikali ya CCM na kuwakataza wapinzani kufanya mikutano ya hadhara na hivyo nguvu kubwa kutumika kudai demokrasia hiyo. Hili linawaweka wawekezaji katika hofu na wasiwasi, kuleta mitaji inaleta mashaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira rafiki kibiashara zipunguzwe zinazoleta urasimu wa kusajili biashara na kufanya biashara. Mfano, Mfanyabiashara haruhusiwi kufanyabiashara kwa muda hata wa miezi mitatu ndipo aanze kulipa kodi/ushuru. Vivutio vizuri vitawezesha wafanyabiashara wengi kuingia na hivyo Serikali kupata mapato makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bandari; ni kosa kubwa kuwa na bandari tatu kubwa nchini halafu nchi inakuwa maskini. Bandari ya Dar es Salaam isiwekwe kodi nyingi zisizo na tija kwa wafanyabiashara na zinazosumbua wananchi. Bandari ifanye operations zake electronically ili kupunguza muda wa kutoa mizigo bandarini kama vile malipo all financial transactions na zionekane kila upande TRA- Bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi, Sekta iimarishwe ili kuuza samaki wengi ili kuweza kuuzwa nje na ndani ya nchi. Mfano, zinunuliwe meli za uvuvi wa baharini na maziwa kama vile Victoria na Tanganyika, meli zivue samaki wanaoshindikana kuvuliwa kwa sababu ya poor fishing gears.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo; mazao ya biashara na chakula yalimwe kitaalam kwa kutumia mbolea na mbegu bora. Kilimo cha umwagiliaji kisisitizwe ili kuepuka njaa kwa sababu ya ukame. Iteuliwe mikoa/wilaya za umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, gesi; nchi yoyote yenye gesi asilia haitakiwi kuwa maskini, tuuze gesi kwa wananchi kwa bei nzuri affordable ili kuokoa misitu yetu itakayotuletea mvua. Tuuze gesi nje ya nchi kupata fedha za kigeni tuuze umeme unaotokana na gesi kwa nchi jirani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii. Mimi najiuliza kidogo nirudi kwenye Katiba Ibara ya 63 hiyo aliyoinukuu Msemaji aliyemaliza kuongea, maneno ya kusimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano kazi ya Bunge. Sasa najiuliza ili umsimamie mtu na kumshauri lazima huyo mtu awe kwanza anakubali kushaurika, awe anakubali kusimamiwa. Kusimamiwa unaweza ukalazimisha lazimisha vyovyote, lakini habari ya kushauri ni je, huyu anashaurika? Maana kama hashauriki utapata shida sana na huyo unayetaka kumsimamia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tujiulize je, Serikali yetu inashaurika? Kama haishauriki tunafanya kazi gani Wabunge katika Bunge hili? Hakuna kwenye Katiba hii sehemu iliposemwa ukiwa na chama chako ni tawala wewe ambae ni Mbunge wa Chama Tawala huruhusiwi kuisimamia Serikali yako. Nawaombeni Wabunge tufanye kazi yetu ya kuisimamia Serikali na kuishauri bila kujali itikadi zetu, vinginenvyo hatu-play role yetu kama Wabunge. Nilikuwa nawakumbusha hicho kipengele. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa kwenye bajeti na hali ya uchumi. Bajeti yetu ya maendeleo imetekelezwa kwa asilimia 34. Hivi hili linahitaji kuwa wa chama gani na chama gani? Asilimia 34 utekelezaji na asilimia 66 haijatekelezwa kwa nini tusiisimamie Serikali? Siamini kwamba hii Serikali inazo hizi fedha halafu ina roho mbaya haikuzitoa, basi tuisimamie ipate fedha na tunapotoa ushauri wa namna ya kupata fedha, vyanzo mbalimbali vya kupata fedha Serikali itusikilize, sasa isipotusikiliza halafu baadae inakwama inakosa hela.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa donors niliwahi kuongea mwaka jana nakumbuka, donors wetu kabla ya kuleta kwenye bajeti kuu huwa tunaweka ni mkataba gani tunafunga na donors kwamba hawata default ili fedha yote tunayoipata kwenye bajeti iweze kutoka. Tunapanga bajeti kubwa halafu baadae hatupati zile fedha na tunashindwa kuitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunashindwa kuitekeleza ni kwa nini tupange nyingine kubwa zaidi, tusibaki na bajeti ile ya mwaka jana na tukaweka vipaumbele vyetu ndani ya ile bajeti ya mwaka jana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu haiingii akilini wewe ulitenga shilingi trilioni 29 halafu ikashindikana ukapanga shilingi trilioni 32, ni muujiza gani utakaofanyika tupate hizo fedha? Maana yake bajeti kama ni tegemezi inategemea wafadhili hatutafanya miujiza hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la kilimo. Suala la kilimo tumejipanga kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, bila kuimarisha sekta ya kilimo hivi viwanda vitatoka wapi? Malighafi ya viwanda hivyo itatoka wapi? Sekta kubwa kabisa ambayo inaajiri watu wengi ambao wangeweza kumaliza umaskini katika nchi hii lakini ndiyo Wizara inayopewa fedha kidogo kabisa katika nchi hii Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana pembejeo tulipata wakati mgumu wananchi wanataka kutumaliza, mifuko 30 tunapeleka Kijiji kimoja nani apate mtoto wa Katibu Kata au mtoto wa nani? Mifuko 30 hivi wanaobaki wanakuwa ni wananchi hawatakiwi kulima katika nchi hii?
Kama hawatakiwi kulima maana yake hawatainua uchumi wao. Kuna Mheshimiwa amezungumzia habari ya pembejeo, kilimo bila pembejeo ni sawa na kuvaa nguo ambayo haikufuliwa, wewe unaona uko bomba tu unatembea kumbe hakuna kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo bila pembejeo unategema tuzalishe na wananchi wanatumia jembe la mkono, hili jembe la mkono maana yake wanalima kidogo wanatarajia kuvuna sana katika kidogo wanachoweza kulima. Sasa analima kidogo halafu hana pembejeo kwa hiyo hawezi kuvuna miaka nenda rudi umaskini unajirudia rudia, tunazidi kuwa na watu maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati fulani huwa najiuliza hawa maskini wanatengenezwa ili wawe, maana yake mtu maskini kupiga kura ni lazima aelezwe namna ya kupiga. Ukiwa maskini utaambiwa tu fanya hiki, sawa, fanya na kile sawa. Kwa nini tunakubali kundi kubwa la Watanzania ambao ni wakulima waendelee kuwa ni maskini? Pembejeo haziwezi kupatikana kwa wakati kwa nini? Na pembejeo zipo humu nchini, utakuta mbolea… (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimefika kwangu kule Kakonko mwezi Disemba mbolea inakuja na mbegu inakuja tulishalima siku nyingi na tulishapanda ndiyo mbegu zinakuja. Hivi pembejeo ikija mapema ninyi mnapata hasara gani? Wakulima wakapata pembejeo mwezi wa sita, mwezi wa saba akakaa mbegu iko pale na mbolea ipo ili ajiandae kulima msimu unapoanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kuzungumza mwaka jana kwamba kuna siku tutaleta mbolea ya kuvunia sijui tutaipata wapi. Unaleta mazao karibu yanakoma kabisa wewe ndiyo unaleta mbolea, inanipa wakati mgumu sana. Wakulima hawa tuwahurumie walime kidogo, wavune sana waondoe umaskini ili wawe na uwezo wa kufikiri vizuri hata wakati wa kupiga kura. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la elimu. Upande wa elimu tumetoka kwenye semina ya TWAWEZA, hali ya elimu ni mbaya. Wanafunzi wa darasa la saba wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu ni asilimia 79 “K” tatu zile. Sasa walipewa mtihani wa darasa la pili
wakashinda kwa asilimia 79, ndugu zangu hali ya elimu ni mbaya. Walimu wana malalamiko rundo, walimu wanaidai Serikali shilingi trilioni moja, hawajalipwa na hakuna anayefikiria kuwalipa na kila wanapofikiria wafurukute ili waweze kulipwa ni vitisho vya kufanyiwa hili na lile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeongea na mwalimu mmoja ananiambia mwalimu wakati wa mitihani siku hizi kama mock na nini, hatusimamii kwa kuogopa kufelisha tunawaacha, tunakaa nje waoneshane mle ndani ili pass mark iwe ya juu Mwalimu Mkuu asihamishwe shule hiyo au
kuvuliwa madaraka, hayo ndiyo maelezo wanayoeleza shuleni. Wanachofanya tunasimamia nje kuangalia je, kuna pikipiki inakuja au gari la Afisa yeyote, tukiona ni shwari mle ndani wanaendelea kuoneshana na pass mark zinapanda, hiyo ndiyo elimu ya Tanzania tulipofika. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu tunasema, HakiElimu wamefanya utafiti juzi juu ya elimu bure, wakakuta elimu bure haijatekelezwa kikamilifu, taarifa waliyoitoa front page ya gazeti la Serikali likasema elimu bure imetekelezwa kwa asilimia 100. Hao waandishi wa habari wangekuwa wakati wa Mheshimiwa Nape Nnauye nadhani wangewajibika tu. Hivi asilimia 100 kweli ipo asilimia 100 na mwandishi yule yuko vizuri tu anamfurahisha nani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii elimu ni mali yetu, tukiongeza wajinga hapa nchini iko siku wajinga watakaa waungane wachague mjinga mwenzao awe Rais wa nchi, tufike mahali tukatae hili, tukatae kabisa, kwamba tunataka elimu iliyo bora na sio bora elimu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishakubaliana kwenye Kamati yetu, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwamba iundwe Tume ya kuchunguza elimu in totality, hali ya elimu ni mbaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hussein Bashe aliwahi kutoa hoja binafsi ya kuundwa kwa Tume, yaliyompata sijui ndiyo maana yuko kwenye orodha ile ya watu 11, hata sijui! Lakini hali ya elimu tunakwenda kule ambako Marekani walipofanya utafiti waliambiwa a nation at risk, its where we are going in this country. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi ya mazingira kampeni ya utunzaji wa mazingira; iwepo kampeni ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi wote kuanzia mashuleni, Vyuoni, Vitongoji, Kata, Vijiji, Wilaya, Mikoa na Taifa. Mkakati uwekwe wazi ili kila mwananchi ajue faida za utunzaji wa mazingira na hasara za kinyume chake mfano mito kukauka, ukosefu wa mvua na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampeni ya upandaji miti; iwekwe au iandaliwe kampeni ya upandaji miti kwa kila kaya na kuhakikisha inakua kampeni/zoezi endelevu, mfano kila kaya ipande miti 10 kila mwaka na kuhakikisha inakua. Halmashauri zihakikishe zinaandaa vitalu vya miche kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampeni ya kuzuia ukataji wa miti na uchomaji moto; kampeni hii iwe ni ya kuhakikisha miti inalindwa na wananchi wenyewe, kampeni kama “Panda Miti Kata Mti”, wavunaji halali wa miti. Halmashauri zote ziwe na Sheria ndogo za kudhibiti uchomaji moto wa misitu/mapori, hii italinda misitu yetu na miti hivyo kuokoa vyanzo vya maji. Wenzetu Burundi ni kosa kubwa kuchoma moto au kukata miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Serikali ishughulikie nishati mbadala ya mkaa ili kupunguza matumizi ya mkaa na hiyo kuokoa miti na misitu kuteketea mfano, Watanzania wanufaike na gesi ya Mtwara kutumika majumbani kwa gharama nafuu Affordable cost, haiingii akilini mtungi wa gesi kuuzwa kwa Shilingi 55,000- 60,000 kule Kakonko (Kigoma), wakati gesi ipo nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, athari ya wakimbizi kwenye mazingira, Mkoa wa Kigoma una wakimbizi wapatao laki tano kwa sasa toka Burundi na DRC wakimbizi hawa wanatumia kuni kupikia hivyo wanakata miti kila siku. Hivyo miti 500,000 inatumika kama kuni kwa siku kwa mwaka ni miti 182,500,000 kiasi ambacho hakina replacement yake kwani haipandwi miti mingine. Mapendekezo; UNHCR wahakikishe wakimbizi wanapikia gesi ili kuokoa uharibifu wa miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viroba vilivyokamatwa vilitozwa kodi na ilikuwa biashara halali, hivyo wamiliki waruhusiwe kuuza ili kulinda mitaji yao. Serikali ingezuia uzalishaji ikatoa muda wa kuvimaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za Muungano zielezwe wazi kwa wananchi wote na wananchi waelezwe kama kweli wanaridhika na jinsi Muungano unavyokwenda. Ni muda muafaka sasa wananchi waulizwe kama wanataka Muungano au la ili isionekane Serikali inawaburuza wananchi au kuwa lazimisha kuwa kwenye Muungano. Magari yaliyosajiliwa ZNZ kwa nini yakiwa bara yanatozwa ushuru tena kwa vile yanatoka nchi nyingine wakati ni nchi moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, CCM Zanzibar ikae na CUF ili kuleta muafaka juu ya maridhiano. Haileti afya ya kitaifa kuendelea kuishi kibabe hasa CCM wanapojinadi kuwa hawako tayari kukaa na CUF kutafuta muafaka au suluhu, duniani kote wagombanao ndio wapatanao.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa Mahakama ya Wilaya ya Kakonko; Wilaya ni mpya ina Mahakama za Mwanzo tatu, ambazo hata moja hakuna hakimu (aliyekuwepo yuko masomoni) kama Wilaya tuna kiwanja cha kujenga Mahakama ya Wilaya. Ombi naomba kujengewa Mahakama; na mbili naomba Mahakama ya Mwanzo Kakonko ipewe Hakimu ili kupunguza umbali kwa wananchi kufuata huduma hiyo wilaya jirani ya Kibondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Burundi kukamatwa ovyo na kufungwa bila kosa lolote. Polisi wanakuwa wakiwakamata warundi wanaokuja kufanya biashara Kokonko (Jimbo la Buyungu) kwa kukutwa sokoni kuwa ni wahamiaji haramu. Matokeo yake hata wanaokuja kulima vijiji vya jirani Burundi na kurudi jioni kwao nao hukamatwa na kufungwa vifungo bila kujadili ni nchi ya Afrika Mashariki. Wapo warundi wapatao 254 wamefungwa gereza la Nyamisinyi- Kibondo kwa makosa kama hayo. Kimsingi Burundi na raia wake pamoja na sisi tunaopakana nao hatufaidi kuwa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo, Warundi waruhusiwe kuja Wilayani Kakonko kulima na kurudi kwao (uwekwe utaratibu). Warundi wanaokuja kufanya biashara wasikamatwe na kufungwa. Sheria ya kukamata ovyo iangaliwe upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, polisi kubambikiza kesi wananchi, kesi nyingi ni za kubambikiza tu na hivyo kujaza wafungwa gerezani wasio na hatia. Polisi Kakonko wamekuwa wakiwabambikiza kesi wananchi, sheria zilizopitwa na wakati zifanyiwe marekebisho hapo Bungeni. Mfano Sheria ya Ndoa ya 1971.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashauri kuchelewa kupelekwa mahakamani. Kumekuwa na tatizo la mashauri kutopelekwa Mahakamani mapema hivyo kuwekwa polisi zaidi ya saa 24.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Kakonko kwa muda mrefu imetumia Kituo cha Afya Kakonko kama Hospitali ya Wilaya. Naomba Wizara ya Afya isaidie kusukuma Halmashauri ya Wilaya na TAMISEMI kujenga Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Watumishi wa Afya Wilayani Kakonko ni mkubwa sana. Uhaba huo ni Madaktari wa kufanya kazi katika Vituo vitatu, yaani Kakonko, Nyanzige na Gwanumpu. Aidha, kuna uhaba wa kutoa huduma kama AMO, Core Nurses.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la akinamama kutozwa fedha wanapopeleka watoto clinic kupimwa. Hali hii inajitokeza kwa mama kuwalipa wahudumu wa afya (binafsi). Kwa nini kazi hiyo isifanywe zahanati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watendaji wa Ofisi ya Maendeleo ya Jamii watoe elimu ya ujasiriamali kwa wananchi ili waanzishe vikundi vya kujitafutia kipato. Aidha, hamasa itolewe kwa wananchi kusajili vikundi kama VICOBA, SACCOS na vikundi vinginevyo vya kijasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba matibabu bure ya wazee kutolewa kama Sera ya Wazee inavyoeleza. Wazee walipwe pensheni kila mwezi kama ilivyowahi kuamuriwa na Bunge. Vile vile Vitambulisho vya Wazee vitolewe kwa muda muafaka, kwani Mheshimiwa Waziri aliagiza viwe vinatolewa kabla ya tarehe 30/12/2016, lakini hadi sasa Wilaya ya Kakonko wazee hawajapata vitambulisho, sambamba na sensa ya kuwatambua wazee wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ifanyiwe marekebisho ili kuepuka watoto (underage) kuolewa kwa kigezo cha umri wa kuolewa. Pia watoto wa kike wanaobeba mimba shuleni wapewe nafasi ya kuendelea na masomo. Wizara ishauriane na Wizara ya Elimu kuweka Sera (re-entry policy) ya wanaobeba mimba kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua. Hii itasababisha watoto hawa kupata haki ya elimu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Spika, habari; TBC mitambo iboreshwe, kuwa na uwezo wa kusikika nchi nzima hasa redio ambayo ni ya Taifa lakini haisikiki nchi nzima hasa wilaya na mikoa ya pembezoni kama Mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Kakonko.

Mheshimiwa Spika, TBC (TV) mitambo yake ni chakavu iboreshwe. Vyombo vya habari kutokuwa huru; uwepo uhuru wa vyombo vya habari kama redio TV, Magazeti na kadhalika. Kuna fununu kuwa Serikali ina mpango wa kuzuia TV na redio kusoma magazeti asubuhi kwa Watanzania (yaani tuongee magazeti). Hii itazuia Watanzania wengi sana kukosa hata ile haki ya kujua nini kiko kwenye magazeti hasa kule ambako magazeti hayafiki kama Kakonko.

Mheshimiwa Spika, mitambo ya redio Kakonko/ Kibondo kutojengwa wakati bajeti ya 2016/2017 ilipitisha bajeti ya kujenga TBC redio boster. Mitambo hiyo haijajengwa hadi sasa.

Mheshimiwa Spika, michezo; tuandae michezo kuanzia shule za msingi/awali, sekondari, vyuo, na kadhalika. Hii itatengeneza “Pool” ya wachezaji watakaounda timu za kitaifa. Serikali itenge bajeti ya michezo hasa mpira wa miguu ili timu za kitaifa kama Serengeti boys zinapofanya vizuri ziweze kupewa fedha.

Mheshimiwa Spika, sanaa; chuo cha sanaa Bagamoyo kipewe fedha za kutosha ili kujiendesha na kiboreshe miundombinu yake kama studio ya kisasa. Serikali ilinde haki za wasanii pamoja na kupewa haki miliki lakini kazi zao bado zinaibiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madini ya chokaa yaliyoko mbuga ya wanyama Moyowosi eneo la Kakonko. TCCIA na wadau wa maendeleo walileta ombi Wizarani kupitia DCC ili kuongeza eneo la kilometa 15 kuingia mbugani kusababisha eneo lenye chokaa kuwa nje ya mbuga na kuwafanya wananchi wanufaike na chokaa hiyo lakini hadi sasa hakuna majibu yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ijikite katika kutangaza utalii nje na ndani ya nchi. Kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya kutangaza utalii hasa nje ya nchi hakitoshi. Nchi ya Kenya wamefanya vizuri kwenye matangazo ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na wimbi la mauaji ya wananchi ndani ya hifadhi kana kwamba wanyama ni bora kuliko wananchi. Hali hii inatupunguzia heshima kimataifa na kitaifa. Uwekwe utaratibu mzuri wa kuhakikisha hakuna raia/mwananchi anayepoteza maisha kwa kukutwa kwenye hifadhi ya wanyama au misitu. Kuua watu marufuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mauaji ya wananchi/raia kuna mifugo inayoingia kwenye hifadhi na kuuawa/kuzuiliwa na hivyo ama kutozwa faini au kuuzwa kwa njia ya mnada ambapo fedha zinakuwa za Serikali. Huu ni wizi wa Serikali. Hata kama wamekosea kuingiza mifugo kwenye hifadhi bado mifugo ni mali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo nyingi kwenye sekta ya utalii; VAT iliyoongezwa mwaka jana kwenye utalii kwa mtalii kulipia kulichangia kupunguza idadi ya watalii waliokuja nchini kwani nchi jirani yetu hawana hiyo VAT na hivyo watalii wengi kukimbilia nchi hizo kwa sababu ya gharama nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi zinachukua eneo kubwa sana na mengine hazifanani na idadi ya wanyama waliopo. Hali hii ikilinganishwa na ongezeko la watu husababisha wananchi kukosa ardhi ya kilimo na mifugo. Nashauri ifanyike tathmini kwenye hifadhi zote kuona hali ya hifadhi na mahitaji ya ardhi kwa wananchi wanaozunguka hifadhi ili hifadhi zisogezwe ndani zaidi kuwezesha wananchi kupata ardhi. Hii itapunguza ugomvi kati ya wafugaji na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijipange vizuri katika zoezi la kuzuia matumizi ya mkaa bila kuja na nishati mbadala. Bei ya gesi na umeme viko juu kiasi kwamba mwananchi hawezi kutumia gesi/umeme kwa kupikia, hataweza kumudu gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TFS Kakonko, Jimbo la Buyungu. TFS wanatesa wananchi Wilayani Kakonko kwa kukamata wananchi wenye hata mbao moja au gunia la mkaa. Hali hii haikubaliki kwani bado wananchi wanahitaji kujenga, kutengeza samani na kadhalika. Mateso haya hayavumiliki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama huna utafiti huruhusiwi kuongea jambo ambalo hujafanyia utafiti. Hapa ndani kuna Wabunge walitembea nchi mbalimbali, kuna Wabunge walitembea nchi hii kufanya utafiti wa jinsi watoto wetu wanaobeba mimba mashuleni watarudi kusoma. (Makofi)

Sasa watu wanaposimama hapa na kueleza watoto wanaobeba mimba wasirudi mashuleni tunashindwa kuwashangaa, halafu watu hao ndiyo wanaosimama na kusema tunataka fifty fifty. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapata wapi fifty fifty wakati ndani ya fifty moja kuna watu walibeba mimba na hawakuruhusiwa kuendelea kusoma? Unataka hiyo fifty uipate wapi wakati wanaobeba mimba ndiyo fifty yako halafu hawarudi shuleni. Kila mtoto ana haki ya kupata elimu, anayebeba mimba utotoni isiwe ni laana, mimba ya utotoni siyo laana na kama mnadhani ni laana wamo Wabunge humu walibeba mimba za utotoni na leo ni Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Elimu, leta re-entry policy juu ya hili tuendelee. Nchi za jirani wamefanikiwa Zambia wanakwenda vizuri na wale watoto tumewauliza, ukiwauliza wale watoto wanasema kabla ya hii re-entry policy issue ya mimba ilikuwa kubwa baada ya re-entry policy mimba zimeshuka mashuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo nilitaka nizungumzie ni makato kwenye mishahara ya walimu bila ridhaa yao. Walimu wanakatwa mishahara yao bila ridhaa.

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe. Nilikuwa nazungumzia makato yanayotokea kwenye mishahara ya walimu bila ridhaa yao. Miongoni mwa makato hayo ni pamoja na makato ya Mwenge, pamoja na makato ya bima za maisha, kuna kitu kinaitwa National Insurance Corporation, wanakwenda mashuleni wanachukua cheque number za walimu zilizobandikwa ubaoni kwenye mbao za matangazo wanakwenda kuingiza makato bila ridhaa yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kakonko ni walimu zaidi ya 14 wanakatwa hizo fedha tena hazionekani kwenye salary slip wala haziko kwa mwajiri wao, mshahara ukiingia anaona message imeingia makato yamefanyika shilingi 56 zimetoka kwenye mshahara wako, akienda kuchukua bank statement anakuta makato yameenda NIC, akiwasiliana na watu wa NIC wanamwambia hatuna habari hiyo, akimuuliza mwajiri hana habari, sasa hili hatuwezi kulivumilia mtu anakatwa makato ambayo hayana ridhaa yake, huu ni wizi lazima ifike mahali haya makato yasimame walimu wafaidi, wanufaike na mshahara wao. Kama vile haitoshi, mwalimu akiwahi kuchukua ule mshahara, mwezi huo NIC hawakati wanashindana wanagombania mshahara nani aanze kuutumia.

Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Elimu mlisimamie hili na Shirika la Bima za Maisha waache huu ujambazi wa kukata mishahara ya walimu bila ridhaa yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la miundombinu mashuleni; tunaomba Mheshimiwa Waziri Elimu na TAMISEMI mshughulikie suala la miundombinu mashuleni. Miundombinu ni pamoja na uhaba wa walimu, tunao uhaba mkubwa sana wa walimu. Hili tunalojidanganya kwamba walimu wamezidi, walimu ni wengi siyo kweli. Tuende tukawahesabu physically mashuleni, idadi ya walimu ni ndogo kabisa ukilinganisha na enrolment ya wanafunzi iliyofanyika, hawa walimu hawatatisha mpaka maisha, tukubali walimu waajiriwe wa nchi hii ili wafundishe kizazi chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda kukimbia lakini hili mnisaidie Wabunge tulijadili kwa pamoja, mimi naangalia hili suala la vyeti fake. Suala la vyeti fake linatupeleka kugumu zaidi. Najiuliza kama mwalimu amepatikana na cheti feki, je, aliyefundishwa na mwalimu huyo naye siyo fake? Hana elimu fake? Kwa sababu tusi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya elimu ni bajeti finyu sana ambayo haiwezi kukidhi mahitaji ya elimu ya nchi hii. Angalau elimu ipangiwe asilimia tatu ya GDP kama nchi za wenzetu katika Afrika Mashariki ambapo huanzia asilimia nne hadi asilimia saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu re-entry policy; watoto wa kike wanaojifungua wakiwa shuleni wawekewe sera ya kurudi kuendelea na masomo baada ya kujifungua, sera hii itasaidia watoto hawa kupata haki ya elimu (right to education). Aidha, itapunguza idadi ya wasio na elimu nzuri nchini na pia kupunguza idadi ya wasio na ajira nchini. Nchi nyingi zimefanikiwa katika hili, mfano ni nchi ya Zambia. Wapo Wabunge waliofanya utafiti juu ya hili na wadau wa nchi hii waliafiki wanaobeba mimba warudi shuleni kuendelea na masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ubora wa elimu nchini; elimu bora hutolewa na walimu bora ambao wanalipwa vizuri na Serikali, wana mahali bora pa kuishi, wana madarasa ya kutosha na hakuna mlundikano wa wanafunzi darasani. Aidha, walimu walipwe stahili zao mapema kuondoa malalamiko ili wafanyekazi wakiwa na amani moyoni.

Aidha, miundombinu ya elimu kama uhaba wa walimu mashuleni, uhaba wa madarasa na madawati, uhaba wa vyoo, uhaba wa maji safi na salama na uhaba wa vitabu, chaki na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu makato ya mishahara bila ridhaa, walimu wamekuwa wakikatwa mishahara yao bila ridhaa yao jambo ambalo ni kinyume cha Sheria za Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2013 makato hayo ni kama vile ya kwenye ujenzi mbalimbali wa majengo ya umma; kwa mfano, maabara, madarasa na kadhalika. Makato mengine ya NIC toka mishahara ya walimu wa Wilaya ya Kakonko wanaozidi 14 bila mikataba yoyote. Makato haya ni wizi wa mishahara ya walimu kwani hata kwenye salary slip makato hayo hayaonekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kusimamisha kazi walimu kwa kigezo cha wanafunzi ku-fail. Hili halikubaliki kwani ni wahalalishaji tu. Aidha, wakuu hawa hufikia hatua ya kuwashusha vyeo Walimu Wakuu kwa kigezo cha wanafunzi ku-fail bila kujali miundombinu mashuleni.

Kuhusu kuundwa kwa TSC toka iliyokuwa TSD hakujaleta mabadiliko yaliyokusudiwa, mfano TSC ilitakiwa:-

(i) Iwe ndio mwajiri/afunge mikataba na walimu;
(ii) Ilipe mishahara;
(iii) Ipandishe madaraja;
(iv) Iadhibu walimu (nidhamu); na
(v) Itoe barua ya kustaafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake mwalimu amendelea kuhudumiwa na Wizara, Idara nyingi sana hivyo kuleta ugumu kwa walimu katika kuhudumiwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu JWTZ wanaolinda mpaka - Wilaya ya Kakonko. Wapo wanajeshi wanaolinda mipaka ya nchi yetu kufuatia ujio wa wakimbizi Wilayani Kakonko. Wanajeshi hawa husumbua raia wanaotoka Burundi kuja kwenye masoko ya ujirani mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimepata taarifa juu ya JWTZ kupiga Warundi waliokuja soko la Kabare, Kata ya Gwarama. Nashauri askari hawa watekeleze majukumu yao bila kuvunja sheria za nchi, wawe karibu na wananchi ili kujenga mahusiano mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ma-DC na RC kuvaa sare za jeshi; Wakuu wa Wilaya na Mikoa ambao ni wanajeshi wamekuwa wakivaa mavazi ya kijeshi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya Kiserikali ofisini. Jambo hili huwapa hofu sana wananchi ambao hawajazoea kuona Mkuu wa Wilaya/Mkoa akawa ndani ya vazi la kijeshi na hivyo kushindwa kupeleka shida zao kwa wakuu hao. Huu si utawala bora pale ambao mtawala anaogopwa na wale anaowaongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mchakato wa vijana kujiunga na JKT; zoezi la kusajili vijana wanaojiunga na mafunzo ya JKT linagubikwa na vitendo vya rushwa sana na hivyo zoezi zima kutokuwa huru kwa raia wote.

Mheshimiwa Mwenyeikiti, Kambi ya JKT Kamembwa bado mipaka yake haijakaa vizuri kwani raia wa Kazilamihunda wanadai eneo lao linavamiwa na jeshi na hivyo kuleta malalamiko mengi. Nashauri ufanyike upimaji rasmi wa kuweka mipaka ukishirikisha viongozi wa Kijiji cha Kazilamihunda na uongozi wa Jeshi (Kambi ya Kanembwa).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa SUMA JKT ambapo ni jeshi la uzalishaji mali lielekeze miradi yake kufanyika/kupatikana kila kambi ili JKT zote nchini ziweze kutekeleza majukumu ya mradi huo bila kutegemea toka Dar es Salaam.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwenye sekta ya viwanda kama ifuatavyo:-

(i) Serikali itafute wawekezaji wa kufufua viwanda vilivyotaifishwa na Serikali na kuwakabidhi wawekezaji wazawa ambao wameshindwa kuviendeleza.

(ii) Serikali itafute wawekezaji kwenye viwanda vidogo vya matunda, viungo (nyanya - tomato sauce), viwanda vya juisi za machungwa, maembe, nanasi (simple machines) kwenye maeneo yanayozalisha matunda ya nyanya na pilipili.

(iii) Viwanda vinahitaji umeme wa kutosha na wenye uhakika na wa gharama nafuu. Haiingii akilini kuwa na umeme wa gharama kubwa wakati tunazalisha kwa gesi ya Mtwara.

(iv) Kuimarisha sekta ya kilimo kutasaidia upatikanaji wa rasilimali/malighafi za viwanda. Hivyo basi kilimo endelevu ni cha kumwagilia na matumizi bora ya pembejeo. Agriculture - Raw materials - Industrial goods/ product.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu biashara napenda kuchangia yafuatayo:-

(i) Biashara zinafungwa nchini kwa sababu ya mazingira ya kufanya biashara kutokuwa rafiki. Serikali inawabana sana wafanyabiashara kwa kuweka kodi nyingi sana za uingizaji wa bidhaa toka nje. Hii ni hatari kwa uchumi.

(ii) Mfanyabiashara mpya na hasa wale wadogo wanawekewa makadirio makubwa ya kodi TRA hata kabla hajaanza kuzalisha. Serikali iruhusu waanze biashara kwanza kisha itoze kodi tena inayokubalika.

(iii) Leseni za biashara ndogo hazitolewi mpaka mfanyabiashara akalipe kodi TRA apewe tax clearance ndipo akakate leseni ya biashara Halmashauri. TRA hawako efficient/ available hasa vijijini kama Wilaya ya Kakonko, hawapo mpaka mfanyabiashara aende Kibondo, Mtambo wa TIN haupo Kakonko wala Kibondo mpaka Kigoma sawa na km.300. Hivyo wafanyabiashara wanashindwa kwenda Kigoma (300km) ili kupata TIN number. Nashauri wafanyabiashara hawa wakate leseni za biashara za Halmashauri ili nazo zipate fedha wakati TRA ikiweka utaratibu wa kutoa TIN vijijini.

(iv) Machinga kuuza bidhaa zao holela hasa maeneo ya Kariakoo soko la wafanyabiashara wakubwa. Hii ni kwa sababu wao hawalipi kodi hivyo huchukua bidhaa za wafanyabiashara dukani na kuziuza bila ushuru wowote. Hivyo wenye maduka Kariakoo hawalipi kodi kwani bidhaa zao zinauzwa nje na machinga, kwa sababu zina bei ndogo na wenye maduka kutotumia EFD machines.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa wawekezaji, nashauri wapewe masharti nafuu ili wahamasike kuja kuwekeza nchini. Mazingira rafiki na ya kuvutia yatawakaribisha wengi, invite more coming on board.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Mjini Kakonko ulitengewa fedha shilingi milioni 300 katika bajeti ya 2016/2017 na mradi ulishatangazwa na wazabuni kupatikana. Mradi haujaanza kwa sababu ya mikataba kutosainiwa. Nashauri kwamba mkataba usainiwe ili Mkandarasi aanze kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mkubwa wa Mto Mgembezi – Kakonko ni mpya, unahitaji nguvu ya kifedha. Intake ilishajengwa, bado kuweka mabomba na tank (reserve). Mradi ukikamilika, utanufaisha Kata za Kusuga, Kakonko, Kanyonza, Kiziguzigu na Kasanda. Ushauri wangu ni kwamba Serikali iweke kipaumbele kwa maji haya ya mteremko (gravity water).

Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya World Bank iliyopo Wilayani Kakonko yote imekwama kukamilika wakati fedha zilishatolewa. Miradi hiyo iko Vijiji vya Muhanga, Katanga, Kidudaye na Nyagwijima. Ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri afike Kakonko kukagua miradi hiyo ili atoe ushauri wa nini kifanyike ili wananchi wanufaike na miradi hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Naomba nianze kuzungumzia suala la Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mdhibiti na Mkaguzi huyu amekuwa akifanya kazi ya kukagua fedha za Serikali miaka nenda rudi, nilitaka kujua ukaguzi huu unalenga nini? Kama ukaguzi unafanyika na wanaofanya ubadhirifu wa fedha za umma hakuna hatua inayochukuliwa kuna sababu gani ya CAG kuendelea kukagua fedha. Kila mwaka tunaletewa taarifa kuna Halmashauri zenye hati chafu, sijui ripoti chafu lakini hakuna kinachofanyika. CAG ana kazi gani kama ripoti yake haiwezi kuwa na impact? Tunatenga fedha CAG afanye ukaguzi lakini akimaliza kukagua hatuoni madhara au hatuoni impact ya ukaguzi wake kwenye nchi hii. Lazima ifike hatua baada ya ukaguzi what next, nini kifanyike juu ya ripoti ile kwa ukaguzi mbovu uliopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ukurasa wa 34 ambao Waziri amesema Ofisi ya Mdhibiti ya Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali ndiye yenye jukumu la kufanya ukaguzi wa fedha wa hesabu za Serikali. Sasa nataka kuuliza, nimepata taarifa kwamba CAG anakagua fedha za vyama vya wafanyakazi. CAG ameanza kukagua Chama cha Walimu Tanzania (CWT) chama ambacho kimekuwepo tangu mwaka 1993 hakijawahi kukaguliwa na CAG na kule hakuna ruzuku ya Serikali, hakuna fedha ya Serikali yoyote iliyokwenda kule anakwenda kutafuta nini kule Chama cha Walimu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi inanipa wakati mgumu sana. Tena vyama viko zaidi ya kumi na mbili, kumi na tatu ameendaje Chama cha Walimu kukagua ambapo vyama vya wafanyakazi vinakaguliwa kwa mujibu wa sheria, vinakaguliwa na Mkaguzi wa Vyama vya Wafanyakazi anayetambulika kwa Msajili ya Vyama vya Wafanyakazi. Huyu CAG amekwenda kufanya nini, kama siyo kuna jambo fulani mtu anafikiri limefanyika anamtuma CAG kwenda kukagua fedha ambazo zimekwisha kaguliwa na ripoti ya vyama vya wafanyakazi na fedha zote zinakaguliwa mwezi wa tatu na taarifa lazima ifike kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi si zaidi ya tarehe 30 mwezi wa tatu. Leo CAG yupo Chama cha Walimu anakagua fedha. Naomba kujua hilo nipate majibu anatafuta nini kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Wazabuni kutolipwa. Serikali lazima ifike mahali ifahamu kwamba uzabuni ni biashara. Wazabuni ni wafanyabiashara! Kama Serikali inawakopa wazabuni, inashindwa kuwafanya waendelee ku-move na biashara zao ni makosa makubwa. Sambamba na hilo wapo watu wali-supply mbolea, pembejeo, waliosambaza pembejeo hapa nchini mpaka leo hajalipwa, wamefilisiwa na mabenki na wengine wamekufa kwa sababu ya kudaiwa fedha za pembejeo na benki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakopaje watu binafsi? Nani mwenye capacity kati ya Serikali na mtu binafsi? Ifike hatua Serikali iangalie nani wa kumkopa na nani isimkope. Mnarudisha nyuma uchumi wa wananchi wanaojitolea kuitumikia hii nchi kwa ku-supply kabla ya kulipwa. Kwa hiyo, Serikali ifike mahali ilipe wananchi hawa wanaotoa huduma Serikalini mapema iwezekanavyo wasiwarudishe nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kuchagua tukubaliane, Serikali inataka kodi, inapenda kodi au inapenda machinga. Tumeruhusu machinga wamemwagika Kariakoo wanauza mpaka milangoni mwa watu wanaotakiwa kutumia mashine ya EFD, matokeo yake bidhaa zinatoka kwenye maduka anapewa machinga anauza, mwenye duka hauzi kwa sababu tayari bidhaa zake ziko kwa machinga. Biashara inaendelea wala yule mtu wa dukani halalamiki kwa nini machinga yuko mlangoni kwake, kwa sababu anajua yeye inamlipa. EFD mashine haitumiki kwa sababu yeye hauzi. Bidhaa zake zinauzwa na machinga. Machinga halipi kodi. Ni nchi gani hii tunayokwenda? Halafu watu wamesimama tu wanaona machinga tunapenda machinga tunapoteza kodi za nchi hii, mwenye EFD pale Kariakoo halipi kodi, bidhaa zake dukani zinakwisha, wanapewa wamachinga….(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali ina impact gani kwa ukaguzi wa kila mwaka? Ubadhirifu unaoonekana kwenye ripoti ya CAG umefanyiwa kazi gani? Wabadhirifu kila mwaka wanapatikana lakini hakuna hatua zinazochukuliwa, hivyo ni business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG kukagua fedha za Vyama vya Wafanyakazi kama vile CWT ni halali? Sheria iliyounda vyama hivyo imetaja Mkaguzi kuwa ni yule aliyetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwepo kwa Ofisi za TRA Kakonko ni jambo linaloleta usumbufu kwa wafanyabiashara kufuata huduma kilomita 300.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgogoro wa ardhi ya vijiji-Kakonko; Vijiji vya Nyakayenzi na Kiga vina mgogoro wa mpaka wa muda mrefu kwenye bonde la Mto Ruhwiti. Mgogoro huo ulipelekea Kijiji cha Kiga kuhodhi ardhi ya Nyakayenzi kwenye mpaka wa vijiji hivyo. Mheshimiwa Waziri alipokuja Kigoma, akiwa Kibondo viongozi wa Nyakayenzi walifanikiwa kuonana na kuongea na Waziri aliagiza DC ashughulikie kutatua mgogoro huo ambao maamuzi aliyotoa hayakuwaridhisha wananchi wa Kijiji cha Nyakayenzi maana wananchi wa Kiga walipewa haki ya mashamba kwenye eneo la Nyakayenzi. Wananchi wa Nyakayenzi walitaka mashamba hayo yaendelee kutambuliwa kama ya Nyakayenzi huku yakilimwa na wananchi wa Kiga kwa mujibu wa ramani na mipaka ya vijiji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walikata rufaa kwa Waziri Bunge lililopita na kuwasilisha kwa Naibu Waziri wa Ardhi. Ushauri, naomba Serikali/Wizara isimamie na kumaliza mgogoro huo kwa kujibu au kushughulikia rufaa hiyo. Bado wananchi wa Nyakayenzi wana imani na Wizara kuwa haki itatendeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa ardhi kambi ya JKT Kanembwa na Vijiji; kumekuwepo na mgogoro kati ya eneo la Kambi ya JKT Kanembwa na Kijiji cha Kazilemihunda kwani mipaka imekuwa ikibadilika mara kwa mara kwa Kambi kuongezea eneo na kuingia katika ardhi ya Kijiji cha Kazilamihunda. Ushauri, maeneo hayo yapimwe kwa kushirikisha Serikali ya Kijiji cha Kazilamihunda na uongozi wa Kambi ya Kanembwa JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya wananchi iliyochukuliwa Kambi ya Wakimbizi-Mtendeli. Kuna wananchi wa Kasanda walionyang’anywa ardhi ili kupisha wakimbizi kwenye Kambi ya wakazi Mtendeli. Baada ya ardhi hiyo kuchukuliwa wananchi hawakupewa ardhi nyingine kwa matumizi ya kilimo na mifugo. Ushauri, wananchi hao wapewe ardhi nyingine pamoja na fidia kwa mazao yaliyoharibika hasa eneo la juu ya Kambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri juu ya bomoa bomoa, kumekuwepo na bomoa bomoa ya nyumba zilizokwishajengwa hasa zile ambazo zimekamilika ama kwa kigezo cha nyumba, kujengwa eneo lisilostahili kama vile hifadhi ya barabara, open space, hifadhi ya Mto, Ziwa, Bahari, na kadhalika. Mjenzi anakuwa na documents zote za ardhi, kama vile ramani, kiwanja na amelipia na kadhalika. Ushauri, kwa nini ardhi wasisimamie kuhakikisha hawatoi kibali cha ujenzi bila kuwasiliana na Wizara ya Miundombinu na Mazingira kujiridhisha kuwa eneo hilo linaruhusiwa kujengwa nyumba kuliko kuacha ijengwe kisha inabomolewa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya wananchi wa Mkoa wa Kigoma kushambuliwa kwa sababu ya uraia. Kumekuwa na tatizo kubwa la wananchi wa Mkoa wa Kigoma kusumbuliwa na Maafisa wa Uhamiaji juu ya kukamatwa, kusumbuliwa, kuhojiwa, kuwekwa lock up na hata kuombwa rushwa ili misukosuko hiyo iishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Kakonko, Jimbo la Buyungu kila basi linasimamishwa na abiria wote kuulizwa vitambulisho, kuvuliwa nguo za juu yaani shati au blauzi ili kuona chanjo iko mkono gani yaani kushoto au kulia. Hali hii isipodhibitiwa italeta kuzorota kwa amani ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma. Mikoa mingine ya mipakani hatuoni mambo haya yakifanyika, hii ni sambamba na raia wengi wa Kigoma kuhojiwa juu ya uraia wao, mfano; Askofu Kakobe (wa Kakonko), Abdul Nondo (wa Ujiji) na wengine wengi, hii haikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za wakimbizi-Mtendeli Kakonko; kumekuwepo na athari za mazingira kwenye Kambi ya Wakimbizi Mtendeli kwa ajili ya ukataji miti na kuni. Awali Serikali iliahidi kutoa gesi ya kupikia kuokoa miti inayoharibiwa na wakimbizi wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji jirani na kambi kunyimwa maji. TCRS/UNHCR walikaa kikao na vijiji jirani na Kambi ya Mtendeli (host community) ili watoe maeneo ya kuchimba visima virefu kwenye maeneo ya vijiji kwa makubaliano ya kuwapa maji. Vijiji hivyo ni Asanda, Nkuba, Kewe, Kazilamihunda na Juhudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maji kupatikana (visima virefu) kwenye vijiji hivyo, maji yalipelekwa kambini bila kupewa vijiji vilivyoingia mkataba na UNHCR/TCRS. Huu ni uporaji wa rasilimali za wananchi kwani kambini (Mtendeli) maji yaliisha na kambi ilikuwa ihamishwe sasa wamepata maji na kuwanyima wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki maana maji ya vijiji vyetu yakiisha wananchi watahamia wapi? Aidha, wananchi wameahidi kuharibu miundombinu ya maji hayo yanayopelekwa kambini ili wakose maji wote, yaani wananchi (host community) na wakimbizi. Serikali iingilie kati suala hili ili kupunguza hasira ya wananchi kwa kuchukua maji yao na kuyapeleka kambini (Mtendeli) kinyume na mkataba (NB: mkataba upo)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji iliyokamilika lakini haitoi maji (miradi minne). Kuna miradi ya maji chini ya NORAD iliyokamilika na kulipwa fedha zote mpaka retention fee lakini imetengenezwa chini ya kiwango hivyo haitoi maji kabisa. Miradi hiyo hewa ni:-

Nyagwijima, Kiduduye (Kata ya Mafufunzu), Katanga (Kata ya Katanga) na Muhanga (Kata ya Muhanga). Miradi hii ni kero kwa wananchi kwa sababu wanaona mabomba bila maji hata tone. Haya ni matumizi mabaya ya fedha za Serikali/mfadhili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri; wahusika kufilisi miradi hii na wakandarasi wawajibike.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Bunge lililopita nilisimama hapa na Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63(2) juu ya kazi za Mbunge, kazi ikiwa ni kuisimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana nishauri Waheshimiwa Wabunge tutimize majukumu yetu ya kikatiba. Hii habari ya kusimama Bungeni na kusifia sifia wakati mambo yanaharibika haitatusaidia kwenye Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unashangaa mtu anaunga mkono anasema asilimia mia moja halafu anaweka neno lakini sasa mimi kama mwalimu haiingii akilini; kama una mambo yameharibika ueleze yalivyoharibika tu usianze kutafuta mambo mazuri wakati hayo mazuri hayapo. Kama unaona hayapo hili Taifa ni letu wote; tuisimamie Serikali na kuishauri, ndivyo ambavyo Katiba imetuambia, hii hapa ibara ya Ibara ya 63. Sasa kuna watu humu wanaremba remba wanapamba mambo ambayo hayapo, wanaogopa kuishauri na kuisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninyi Wabunge wa CCM mlikuwa na nafasi nzuri sana ya kuisimamia Serikali yenu inayoongoza ya Chama cha Mapinduzi, maana sisi tukitoa ushauri huku bahati mbaya tunaonekana kama ushauri wetu bado hamuukubali, lakini hatutachoka kusema, tutaendelea kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati zote zimekwenda kwenye ukaguzi wa miradi, lakini fedha za miradi ya maendeleo hazikwenda/hazijapelekwa. Ilikuwa ni aibu wakati fulani mnakwenda kwenye mradi hata shilingi moja haijapelekwa, mnakwenda kukagua fedha za wafadhili wengine tu waliojitolea kuleta fedha, ninyi za kwenu nchini hazijapelekwa. Hili nalo tukishauri mnatuona wabaya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa tulisimama tukashangilia bajeti hii ya mwaka, ya karne, haijawahi kupatikana, haya ndio madhara yake sasa sisi tuliona haikubaliki ndiyo maana tulikataa kuiunga mkono. Tulikataa kuunga mkono kwa sababu tulijua ni bajeti ya mbwembwe ya maandishi mazuri kwenye karatasi utekelezaji wake haupo, tunafanyaje hii kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia miradi inatekelezwa, fedha za maendeleo kwenye wizara zinapelekwa asilimia 11, asilimia 33, kilimo wamepeleka asilimia 11, hiki kilimo tunakipeleka wapi kama kinapelekwa kwa asilimia 11 tu ya maendeleo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na bahati nzuri kuna mtu mmoja wa Hazina alikuja akatuambia akasema kwa kweli Serikali ina majukumu mengi, fedha iliyokusanywa ni kidogo na haiwezi kukidhi, hata wafadhili wenyewe waliokuwa wakituletea fedha hawaleti vizuri. Mimi nikahoji tuna mahusiano mabaya na mataifa ya nje? Kama yapo mtuambie uhusiano wetu wa kidiplomasia umekuwaje mpaka wafadhili walioahidi kuleta fedha hawaleti fedha nchi hii? Kwa hiyo, hili lazima tulione. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni Wabunge humu, tusione tu Serikali ni kuisifia, tuishauri, wapo watu hapa, mimi napongeza naliona jambo zuri la ununuaji wa ndege, lakini sio kununua ndege kwa cash. Mataifa yote hayanunui ndege kwa cash, hii cash ingeweza kufanya shughuli zingine za maendeleo tukanunua ndege kwa mkopo ndege ikawa inalipa deni la ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ndege ya mwisho iliyokuja tuliwahi sisi wapinzani kusema nje kwamba kuna ndege imeshikiliwa, lakini waliosema ndege imeshikiliwa walipata misukosuko, juzi Serikali imekiri ndege iliyokuwa imeshikiliwa Canada sasa imeletwa. Mimi napata wakati mgumu, tulipowaambia imeshikiliwa tulipata msukosko, imerudi mkakiri wenyewe iliyoshikiliwa imerudi sasa… (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndege hii imekuja kama ndege moja tumenunua ndege tatu, kuna ndege moja ya bilioni 31 ambayo ndio hii iliyokuja ikaonekana baada ya kushikiliwa muda mrefu, lakini ili itoke tumelipa bilioni 78 sawa na fedha za Kitanzania bilioni 140 na kidogo ili hiyo ndege moja ipatikane. Sasa watu tunaposhangilia ni lazima tujiulize tumeumia kwa kiasi gani? Unanunua ndege moja kwa bilioni karibu mia moja na hamsini halafu tunalishangilia hilo, hapa watu tuna matatizo ya maji na kiafya hatulioni hilo wala hatuishauri…

T A A R I F A . . .

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, umri wangu na aliyetoa taarifa haulingani, kwa hiyo, naachana nae kwa sababu ya umri nilionao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa ushauri mzuri tu ambao unaweza ukatusaidia kwa baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kwenye upande wa Wizara ya Elimu. Tunalo tatizo la uhaba wa walimu, hali ya uhaba wa walimu ni kubwa sana, tuna tatizo la upungufu wa walimu wa shule za msingi, walimu shule za msingi hawatoshi, tuna upungufu karibu wa walimu 95,000.

Vilevile bado tuna tatizo la walimu wa sayansi, walimu wa sayansi karibu 15 na point hawatoshi. Hivi viwanda tunavyohubiri katika nchi yetu bila walimu wa sayansi ni viwanda gani? Kwa sababu tunaweza kutafikia hatua; mimi sijui kama kuna kiwanda kinaendeshwa na mtu aliyesoma history na geography aka-run mitambo ya viwanda na hivyo viwanda vikawa salama na mwenyewe anayekiendesha akawa salama. (Makofi)

Tuchukue hatua za makusudi kunusuru taifa hili upande wa elimu. Walimu wamekata tamaa morali ya kufundisha imeshuka. Taarifa ya Haki Elimu inasema walimu waliobaki na morali ya kufundisha ni asilimia 37, hawa 60 na kidogo wote wamepoteza morali wa kufundisha kwa sababu tu ya kukosa motisha. Wana madai mengi hawalipwi, wamebaki kulipa wanadokoa dokoa. Mwezi wa pili tulidhani walimu watalipwa wote, walidokoa dokoa wakalipa baadhi ya walimu, hivi hii hali tunaipeleka wapi Taifa hili? Kama hatutakuwa na elimu nchini hakuna sekta ambayo itakwenda vizuri, sekta zote zinategemea elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufaulu sasa hivi division four na division zero ni asilimia 60 na point, yaani mimi hata sielewi ni ufaulu kwa sababu zero si ufaulu hata four yenyewe si ufaulu yaani waliopata four na zero ni asilimia 60 yaani tunatarajia nchi iendeshwe na asilimia 30 ndio uwezo kidogo waliofanikiwa darasani division one, two na three, where are we heading to? Halafu tunakaa humu tunasifia, tunapongeza, tupongeze lakini tuisimamie Serikali, tuinue ubora wa elimu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii tuliwahi kufikia hatua jamani tuwe na mkutano wa kitaifa wa elimu na bahati nzuri juzi alizungumza Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa akasema hali ya elimu ni mbaya tuwe na mkutano wa kitaifa kuliangalia hili.
Naomba hili tuliangalie kwa pamoja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuzungumzia suala la utawala bora. Kwenye suala la utawala bora tuzungumzie habari ya Tume Huru ya Uchaguzi, kama hatutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi hatutakuwa na utawala bora hapa nchini, na hili ndilo limetufikisha hapa. Nafurahia maoni ya Kamati yaliyosema Tume Huru ya Uchaguzi iangalie wale wasimamizi wa uchaguzi waendeshe uchaguzi kwa uadilifu. Ile habari ya kila chaguzi ndogo zinazofanyika ni mauaji, ni fujo, vurugu na uporaji wa kura na matokeo mnaambiwa nendeni mahakamani, hatutaki; uchaguzi ufanyike ulio huru tuepukane na mahakama.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ugonjwa wa tezi dume umeonekana kuongezeka sana nchini. Tatizo kubwa ni operation zinazofanyika, lazima mgonjwa afanyiwe mara mbili. Aidha, hata wanaofanyiwa operation wengi wanakufa.

Ushauri wangu madaktari waongezewe ujuzi nje ya nchi na ikibidi vifaatiba vya kisasa vipatikane kuokoa wanaume hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ajira ya watumishi sekta ya afya; Mkoa wa Kigoma una upungufu wa watumishi wa afya wapatao asilimia 70 hali ambayo inatishia uhai wa watu wa Kigoma. Aidha, nchi nzima kuna upungufu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu Serikali ichukue hatua za makusudi kuajiri watumishi hao ila kila zahanati iwe na CO/CA, vituo vya afya viwe na daktari mmoja na CO , hii itasaidia kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la matibabu ya wazee; sera ya wazee kutibiwa bure bado inasuasua sana kwani sehemu nyingi wazee hawa hawapati matibabu bure. Aidha, vitambulisho vimekuwa shida kupatikana. Ni vyema vitambulisho vikatolewa kwa wazee hawa wenye umri wa miaka 60+.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kuwa Wizara iwasiliane na TAMISEMI ili wazee wote wapewe vitambulisho ili wapate matibabu bure. NB: Vitambulisho vitolewe bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya Engender Health na Bloomberg; miradi hii iko Mkoa wa Kigoma na inatarajiwa kufikia ukomo/mwisho Aprili, 2019. Huduma nyingi zinazofanyika Mkoani na Wilaya zote ni huduma ya mama, baba na mtoto. Mfano, vituo vitano kila Wilaya vilivyojengwa vimewekewa vifaatiba vya kisasa lakini hakuna wataalam wa vituo hivyo hasa Jimbo la Buyungu (Kakonko). Ni aibu kwa Serikali yetu kupewa msaada wa majengo na mfadhili kisha Serikali inashindwa kuweka/kuajiri wataalam wenye ujuzi wa kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ushauri wangu kuwa vituo hivi vipewe vipaumbele na Wizara itafute ufadhili utakaosaidia miradi hii iendelee kutoa huduma (sustainability).

Mheshimiwa Naibu Spika, kinga ni bora kuliko tiba; Wizara ya Afya ijiimarishe kwenye kampeni ya kinga ili iepuke kutumia fedha nyingi za tiba. Kampeni ya kutumia tv, redio, michezo/maonesho/sanaa na kadhalika, vipindi kama chakula bora (kuleni chakula bora, mboga, samaki, maziwa na kadhalika), kampeni ya kunawa mikono baada ya kutoka chooni, kuchemsha maji; mabwana na mabibi afya wafanye kazi kukagua usafi majumbani (karo, vyoo safi na kadhalika).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Mto Mgembezi unalenga kutoa maji kwenye vijiji zaidi ya 15 toka chanzo chenye uhakika cha mto huu. Mradi huu ulishafanyiwa upembuzi yakinifu miaka ya nyuma na kuonekana gharama yake ni shilingi bilioni 10. Hata hivyo, mradi huu umeshajengwa intake ya zaidi ya shilingi milioni
200. Hivyo bado kazi ya kutandika mabomba na ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji. Mradi huu unaweza kufanyika kwa awamu mbili kama ifuatavyo:-

Awamu ya kwanza ni kutandika bomba hadi Kakonko Mjini na kujenga tenki kubwa kwa kuyasambaza Mjini Kakonko na awamu ya pili ni kuyasambaza kwa vijiji vya jirani vya Kata za Kanga, Kakonko, Kiziguzigu na Kasanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji ya BTC waliahidi kuweka miradi ya maji katika vijiji vya Wilaya ya Kakonko. Vijiji hivyo ni Kakonko, Mbizi, Itumbiko, Muganza, Kiziguzigu, Ruyewizi na Kabingo. Miradi hii imekwama hadi sasa haijaanza kutekelezwa. Serikali ieleze ni lini miradi hii itaanza kutekelezwa ili wananchi waliopewa matumaini waanze kunufaika?

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo miradi mitano katika Wilaya ya Kakonko ambayo imekamilika lakini haitoi maji wakati miradi ilishakabidhiwa na kulipwa fedha zote hata za retention. Miradi hiyo ni Nyagwijima, Kiduduye, Katanga, Muhange na Kiga (huu una nafuu). Miradi hii ilifanyiwa ufisadi wa hali ya juu na hivyo hakuna value for money.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba waliohusika na ubadhirifu wachukuliwe hatua yaani wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo, yaani wahandisi wa Kibondo na Kakonko, maana ilianza kabla ya kugawa Wilaya za Kakonko na Kibondo. Naomba miradi hii ifanyiwe tathmini ili kujua inahitaji nini ili iweze kuhudumia wananchi baada ya kufanyiwa marekebisho muhimu yanayohitajika.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo visima Wilaya ya Kakonko katika vijiji mbalimbali ambavyo vina maji lakini vina miundombinu mibovu ya visima kama vile pump, rubber na kadhalika. Visima hivi vinashindikana kutengenezwa kwa nguvu za wananchi kutokana na gharama za vipuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri zianzishwe Kamati za Maji za Vijiji vyote vyenye visima ili Kamati zikusanye fedha kwa watumiaji wa maji zitakazotumika kukarabati miundombinu ya visima. Pia nashauri Idara ya Maji, Wilaya ipewe uwezo kifedha ili wataalam wake wawe wanakagua visima hivyo mara kwa mara kwa kuvifanyia service.

Mheshimiwa Naibu Spika, Miradi ya Umwajiliaji ndio pekee inayoweza kulitoa Taifa hili katika uhaba wa chakula pindi ukame unapoathiri nchi hii na pia msimu wote wa mwaka yaani kiangazi na masika. Hivyo nashauri iwepo miradi mikubwa ya kitaifa kwa kanda. Kila kanda iwe na Irrigation Scheme kubwa ya mazao yanayostawi kanda hiyo. Pia kila Wilaya iwe na Irrigation Schemes zenye uwezo wa kilimo cha mwaka mzima yaani kiangazi na masika (sustainable irrigation schemes).
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la Teachers Professional Board (Bodi ya Kitaaluma ya Walimu). Bodi hii iliwahi kuandaliwa Muswada na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwenye utawala wa Awamu ya Nne na kuiwasilisha Serikalini ili iweze kufanyiwa mchakato wa kuunda chombo hiki. Mpaka sasa chombo hiki hakijaundwa pamoja na malengo yake mazuri kabisa, kusimamia taaluma ya walimu nchi hii pamoja na nidhamu ya walimu wa nchi hii. Kwa mfano, lengo lilivyokuwa zuri la Teacher’s Professional Board ikitokea mwalimu wa nchi hii amefanya makosa akafukuzwa kazi anaendelea kwenda kufundisha shule za private and nobody will ask him or her! Lakini lengo la hii Teacher’s Professional Board ilikuwa inaandaa leseni pamoja na vyeti vya ualimu unapewa leseni ya kufundishia. Uki-mess up wanakunyang’anya leseni, hautafundisha shule yoyote katika nchi hii. Kwa hiyo, nimuombe Waziri hiki chombo kiundwe kama zilivyo Bodi za Taaluma zingine kiweze kulisaidia Taifa hilika katika upande wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala la ufaulu wa wanafunzi katika Taifa hili. Kidato cha nne, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamati nilitarajia Wabunge wote wawe wamesononeka sana juu ya hali hii na ingekuwa inaruhusiwa kusimama Bungeni kama kwenye msiba kwamba tusimame kidogo kumuombea marehemu nalo tungesimama kwa suala hili kuiombea elimu nchini, lakini watu waliposoma ni data tu, wanaziona data tu, sawa tu walifaulu hawa sawa tu! Hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo hapa, shule binafsi mwaka 2016 shule 10 bora zilikuwemo asilimia 10 za Serikali. Katika shule 50 kulikuwa na asilimia sita za Serikali; shule 100 asilimia 11. Mwaka jana katika shule bora 10 zilikuwemo za Serikali asilimia sifuri. Katika shule 50 asilimia moja katika shule 50 ni za Serikali, shule 100 zilikuwemo asilimia sita. Maana yake elimu ya Taifa hili imebebwa na shule binafsi. Shule za Serikali hakuna chochote. Tungeondoa private hapa tungekuwa na wanafunzi sita mwaka jana bora ndani ya wanafunzi mia moja! Halafu tunashindwa kuisaidia Serikali na kuisimamia iboreshe elimu. Hili halikubaliki! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungewauliza watu wa shule binafsi wanafanyaje? Hii kitu Waziri mngeenda tu mkanong’ona nao, ninyi mnafanyaje mnapata performance nzuri kama hii, sisi huku tumekwama, hebu mtusaidie. Siri yao wamesema hivi, kuna motisha ya kutosha kwa walimu, Serikalini hakuna motisha. Shule za Serikali walimu hawana motisha yoyote, hata madai yao wanayodai hawalipwi kwa wakati, madaraja hayapandi hata wanaopandishwa hawarekebishiwi, wanaorekebishiwa hawalipwi arrears, mnatarajia nini? Shule binafsi wanao walimu wa kutosha, sisi kila siku hatuna walimu na tumepigia kelele ndani ya ukumbi huu, walimu hawatoshi shuleni, tunaliona jambo la kawaida! Hivi hiki kitu tunakwenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetoa walimu wa sekondari tumepeleka primary, tumeenda kuongeza frustrations kwa walimu. HakiElimu walituambia asilimia 37 ndiyo wamebaki na morale ya kufundisha, hawa 60 na kidogo hawana morale kabisa! Ualimu siyo kitu cha kusema lazima utafundisha tu, haiwezekani! Morale kwanza, itoke moyoni na kutoka moyoni lazima huo moyo uwe umetengenezwa ukubali kufundisha kwa bidii na nguvu zako zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine, shule binafsi wana kitu wanaita mfumo imara shirikishi wa udhibiti elimu, mfumo wao imara una mkakati wa kukaririsha wanafunzi wanaofanya vibaya ili wasiendelee na makapi.

Sasa nataka Waziri utakapokuja hapa utuambie ni kwa nini unazuia shule private zisikaririshe? Kwa sababu mimi ni mzazi nimeamua kumpeleka mtoto wangu private, hata angekaririshwa mara mia naendelea kulipa karo, Serikali inawahusu nini? (KIcheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niacheni na mtoto wangu nikomae naye mpaka nitakapojiridhisha kwamba viwango vyake vya elimu vimekuwa vizuri na hili mwisho wake ndilo linalosababisha, tumejiuliza kwa nini Serikali ina ugomvi na private, ni wivu tu! Wana performance nzuri, kwa hiyo, ni kama inaidhalilisha Serikali. Kwa hiyo, lazima wivu uwepo ili na wao ufaulu ushuke wote mfanane, muende mnafanana fanana. Matokeo yake sasa ufaulu ukiharibika kwenye shule za private tunaanza kupeleka watoto Uganda na Kenya wakati hii biashara ilikuwa imekwisha. Ziko shule hapa zinafanya kama Uganda kama Kenya na zaidi ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu wivu uishe, Serikali iachane na wivu, shule za private ziachwe zi-perform, wakaririshe, mwanafunzi atoke ni the best student. Sisi tunataka wote waende. Subirini muziki utakaokuja wa hii elimu bure! Matokeo ya elimu bure yatakuwa zaidi ya haya tutashangaana wote. Tumeweka elimu bure miundombinu imebaki ile ile, hatujajiandaa vizuri, maana batch ya kwanza nadhani mwaka kesho au kama mwaka huu ya kidato cha nne yenye elimu bure, tutashangaana hapa. Kwa hiyo, tusijifiche kwenye kichaka cha elimu bure tukidhani iko bomba. Tuangalie elimu bure inafanana na miundombinu tuliyonayo? Inafanana na tunachoweza kubeba kwenye elimu bure? Inaweza kutusaidia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la walimu wa sayansi, nimepata taarifa walimu waliosoma masomo ya art wamepelekwa Chuo cha Kleruu kwenda kujifunza methodology ya kufundisha shule za ufundi!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie hii, walimu waliosoma masomo ya arts baada ya kuona wamezidi kule sekondari wamewachukua wakaenda kusoma methodology ya kufundisha practical shule za ufundi. Wamekwenda Iyunga Sekondari, wame- prove failure kwenye BTP wameshindwa! Sasa niambieni hivi mimi nimesoma history, geograpghy labda HGL, HGK, mimi na metholodgy ya sayansi wapi na wapi? Nikajifunze namna ya kufundisha kutengeneza gari, namna ya ku-operate viwanda, eeh, hii kiboko! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siri nyingine masomo ya lugha, kiswahili na kiingereza Tanzania yanaanza kufundishwa darasa la tatu. Hawa shule za private wanaanza chekechea kule na wakitoka chekechea hawa walioanza la tatu wanakwenda kukutana kwenye mtihani wa darasa la nne, wale walioanza… (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, urasimu wa kupata leseni ya biashara; wafanyabiashara katika Halmashauri husika wanapata shida kupata leseni ya biashara kwa masharti ya kuwa na TIN number ya TRA. Akifika TRA anaambiwa lazima afanyiwe makadirio ya kodi ya biashara yake bila hata kuiona biashara yenyewe. TRA Officers wanakaa ofisini na kufanya makadirio ya mfanyabiashara bila kuona ukubwa wa biashara yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara akishakadiriwa kodi ya juu zaidi ya biashara yake anagoma kukata TIN, kisha anaendelea na biashara zake bila kuwa na leseni jambo linalopoteza mapato ya Halmashauri kwani leseni zinakatwa na Halmashauri baada ya kuwa mfanyabiashara amekidhi masharti ya TRA ya kuwa na TIN number.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri, TRA wasifanye makadirio ya kodi kwa wafanyabiashaa wakiwa ofisini, wafike site wakaone ili wasiwaonee au kuwapendelea wafanyabiashara. Leseni za biashara zitolewe na Halmashauri bila masharti ya kuwa na TIN number ili waendelee na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji, viwanda vikubwa na vya kati hutegemea nishati ya umeme. Kakonko hakuna umeme wa uhakika wa kuwavutia wawekezaji kuja kuweka viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hutegemea miundombinu ya barabara kwa ajili ya kusafirisha malighafi, Kakonko hadi Kigoma ni kilometa 30 na barabara ni mbovu hivyo haiwavutii wawekezaji kuwekeza Mkoa wa Kigoma na Wilaya zake kama Kakonko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliahidi kiwanda cha kuchakata mihogo tangu mwaka 2016 na kiwanda hicho kinasubiriwa Kakonko. Nashauri kiwanda hicho kipatikane ili wananchi waendelee kuwa na imani naye asije kuonekana ni muongo. Heshima ya Kiongozi ni kutekelekeza ahadi zake anazotoa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ukiukwaji wa haki za raia wa Mkoa wa Kigoma na kusumbuliwa kuwa siyo raia wa Tanzania. Kakonko kila basi linasimamishwa na kukaguliwa na Maafisa wa Uhamiaji. Abiria wanavuliwa nguo za juu, yaani t-shirt au blauzi ili kuona chanjo iko mkono gani kulia au kushoto? Huu ni udhalilishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachukua rushwa kwa kila raia atakayekosa kitambulisho na kushushwa kwenye gari la abiria. Wamekamatwa wanaodhaniwa kuwa raia na kufungwa kwenye container, barrier ya Kihomoka Kakonko. Huu ni udhalilishaji wa hali ya juu. Je kufunga binadamu kwenye container ni halali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Mtende iliishia kumaliza maji Kambini (underground water) kisha wakaja kuomba wachimbe visima vitano kwenye Vijiji vya Kasanda, Kazilamihunda, Kewe, Juhudi na Nkuba. TCRS waliomba kuchimba visima, hivyo waliweka mkataba kuwa wakipata maji lazima wapate host community kwanza (vijiji vitano) kabla hayajapelekwa kambini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maji kupatikana, TCRS walidai hawana bajeti ya kupeleka maji kwenye vijiji vitano kinyume na mkataba. Kijiji cha Kasanda walipata maji toka Water Mission Gate9 na Mkuba Gate2 tu, maji ambayo hayatoshi kabisa na ni kinyume na mkataba. Wananchi wana hasira, chuki na TCRS pamoja na wakimbizi waliochukua maji yao bila wao kupata, jambo ambalo litaleta mgogoro mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi 92 wanaodai fidia ya mazao mpaka sasa hawajalipwa. Suala hili nililifikisha Wizarani ili liweze kufanyiwa kazi, lakini hadi sasa wananchi hao hawajapata fidia yoyote wakati mazao yao yaliharibiwa. Hili linazidi kuongeza chuki kwa wakimbizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu kwenye barrier ya Kihomoka Kakonko, hutumiwa na Polisi, Uhamiaji na Maliasili. Matumizi yenye uharibifu ni rushwa kwenye magari ya mizigo, abiria wanaodhaniwa kuwa sio raia, rushwa kwa bodaboda, rushwa kwa wafanyabiashara wanaopita barrier hiyo, rushwa kwa wanaobeba mbao, mkaa na kadhalika na kupiga watu bila sababu. Nashauri barrier hii ifungwe, kwani haitendi haki bali kuwafaidisha Polisi na Uhamiaji kwa kujipatia kipato kisicho halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi Kakonko na nchini kote wanakamata bodaboda wasio na hatia na kuwaomba rushwa kila wakati na kufanya zoezi hili, ni shamba la Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wengi wa Kakonko wanaomba rushwa kwa raia wanaopatikana na tuhuma mbalimbali na hakuna dhamana bila rushwa. Kituo cha Polisi kina kesi za kubambikiza ili mtu atoe rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Polisi wengi kukaa muda mrefu Kakonko (overstay).
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 7(1)(b)(iv) - Serikali kuelekeza vyombo vya habari kuhusu jambo la kutangaza. Hii inaingilia uhuru wa habari. Serikali ingejikita kuelezea issue of National importance, ni zipi? Akija kutokea kiongozi wa nchi asiye na uadilifu, atatumia kifungu hiki vibaya. Mfano Mkuu wa nchi anaweza kusema birthday yake ni National importance. Kifungu kifutwe.
Kifungu cha 32(2)(3) kinasema, maiti anaweza kukashifiwa (defamation in print media). Kwa kawaida kashfa imemgusa mhusika mwenyewe, hivyo maiti haiwezi ku-feel kashfa au udhalilishaji. Kifungu hiki kifutwe kwa sababu maiti haikashfiki na wala haina uwezo wa kutoa ushahidi wa kashfa husika.
Kifungu cha 33(1) katuni (effigy) zinaigizwa kwenye dhana ya kashfa. Duniani kote katuni ni kiburudisho kinachowasilisha ujumbe kwa njia ya burudani na dhihaka na dhana hii imekubaliwa duniani kote. Hivyo, Tanzania itakuwa ya kwanza kuingiza katuni katika dhana ya kashfa. Hivi Watanzania hawawezi kucheka au kuendeleza utamaduni wa utani wa asili? Kifungu kitanyima haki ya watoto kupewa kusoma magazeti ya katuni, kuangalia TV zenye vipindi vya katuni. Katuni zinafundisha watoto lugha ya Kiingereza, maadili na maonyo mbalimbali? Kifungu hiki kifutwe.
Kifungu cha 50(2) - (11); vifungu hivi vinaadhibu wasomaji na wachapishaji wa magazeti. Vifungu hivi vimetishia maisha ya wasomaji na wawekezaji katika mitandao ya uchapishaji kwa kumpa ruhusa Mkuu wa Polisi au Maafisa wa Jeshi hilo kukamata na kuharibu mitambo ya uchapishaji na kukamata wananchi watakaokutwa na yanayodaiwa kuwa machapisho ya uchochezi. Hii italeta hofu na mtafaruku mkubwa nchini usio wa lazima. Kifungu hiki kifutwe.
Kifungu cha 55 kuhusu mamlaka ya Waziri kuzuia uchapishaji wa baadhi ya habari; Waziri hana haja ya kupewa mamlaka haya, kwani tayari habari zinahusu usalama wa Taifa, zinaangukia chini ya kifungu cha 72(a) (i) kinachozuia uchapishaji wa habari za aina hii na adhabu yake iko wazi katika Muswada huu. Kifungu hiki kifutwe.
Kifungu cha 56 kinatoa nguvu kwa Polisi na Mkurugenzi wa Idara za Habari, Maelezo kukamata mitambo. Dhana ya kukamata na kuharibu mitambo imetawaliwa katika kifungu cha 50. Kifungu hiki kifutwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa Walimu wa sayansi, Sekondari Kakonko. Nchi nzima ina uhaba wa Walimu wa sayansi wa sekondari zaidi ya 15,000. Kwa mantiki hiyo sera ya uchumi wa viwanda ni ndoto nchini maana wataalam watakuwa hawapo kutokana na ukosefu wa sayansi. Kakonko kuna upungufu. Ushauri ni Serikali iajiri Walimu wa sayansi nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya mashuleni; kuna uhaba mkubwa mashuleni wa miundombinu, kama ifuatavyo: Nyumba za Walimu, vyumba vya madarasa, vyoo vya wanafunzi na Walimu, madawati, maabara, viwanja vya michezo na vifaa vya michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya Walimu; Walimu wana madai mengi yasiyolipika. Hali hii inakatisha tamaa Walimu na kushusha morali ya kazi. Ushauri ni Serikali ilipe madeni yote ya Walimu ili waongeze tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa Hospitali ya Wilaya Kakonko; Wilaya ya Kakonko haina hospitali ya wilaya na sasa Kituo cha Afya cha Kakonko kimeelemewa sana. Kituo hicho kinapata dawa kwa hadhi ya kituo cha afya wakati kinahudumia wagonjwa kwa ngazi ya wilaya, hivyo kuishiwa dawa mapema. Pia, dawa muhimu zinaletwa kwa level ya kituo cha afya. Nashauri kwamba, Serikali ijenge Hospitali ya Wilaya Kakonko mwaka 2018/2019. Pia Kituo cha Afya Gwanumpu kifanyiwe ukarabati, kwani kilitengewa fedha 2017/2018 lakini fedha hazikutoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu wa Watumishi wa Afya. Kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa sekta ya afya, jambo linalotishia afya za Watanzania sambamba na vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga. Nashauri Serikali iajiri watumishi wa sekta ya afya. Ukosefu wa watumishi wa sekta ya afya kwenye vituo vilivyojengwa na Bloombergy vipatavyo vitano kwa ajili ya baba, mama na mtoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Miradi ya Maji ya World Bank iliyokwama. Kuna miradi mitano ya maji ambayo imekamilika, lakini haitoi maji. Miradi hii ilishalipiwa fedha zote mpaka za retention, lakini hakuna maji. Miradi hiyo ya World Bank ni kama ifuatavyo:-

(i) Mradi wa Maji Nyagwijima, Kata ya Mugurunza;
(ii) Mradi wa Maji Kiduduye, Kata ya Nugunza;
(iii) Mradi wa Maji Katanga, Kata ya Katanga;
(iv) Mradi wa Maji Muhange, Kata ya Muhange; na
(v) Mradi wa Maji Kiga, Kata ya Ruyeye una nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ichunguzwe haraka. Nashauri wasimamizi na wakandarasi waliohujumu miradi hii wachukuliwe hatua za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nichangie Ofisi ya Rais, Utumishi kama ifuatavyo:

Upungufu mkubwa wa watumishi; uhaba wa Walimu shule za msingi about 95,000, uhaba mkubwa wa Walimu wa Sayansi (sekondari) zaidi ya 15,000, uhaba mkubwa wa watumishi wa Sekta ya Afya. Nashauri Serikali itoe ajira Wizara ya Elimu na Afya ili kukidhi mahitaji ya watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Utawala bora; utawala wa sheria (rule of law); kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi na Katiba ya nchi kwa ujumla. Mfano, kuzuia mikutano ya hadhara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusiana na uhuru wa mawazo. Wanaoikosoa Serikali au kuishauri wanapata misukosuko na wengine kupotezwa. Mfano Azori, Ben Saanane na kadhalika; watumishi wa kiroho kupata misukosuko baada ya kuhoji kuwepo kwa Katiba mpya au Serikali kukosolewa kwa maslahi ya Taifa. Mfano, Maaskofu Niwemugizi na Kakobe kufikia kuhojiwa uraia wao kwa sababu hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu tena za kikatiba. Magazeti yanafungwa na Waandishi wa Habari kukosa uhuru wa kuandika taarifa zao; TV kutozwa faini kwa sababu ya kutoa taarifa zisizoipendeza Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosekana haki ya kuishi; tumeshuhudia wananchi wakipoteza maisha na maiti zao kuonekana zinaelea baharini na Serikali iko kimya; mauaji ya mwanafunzi Akwiline Akwilini; mauaji ya Daniel, kiongozi wa CHADEMA, Kata ya Hananasifu na maiti yake kutupwa Fukwe za Coco Beach.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka ninukuu kifungu cha Katiba Ibara ya 18(d) inayosema kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote. Naomba mpigie mstari hayo maneno „wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii‟.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tuna Katiba ambayo ni Sheria Mama, ambayo inazungumzia habari, suala la kupata habari wakati wote, lakini kwenye Muswada unaokuja unaelezea unaweza taarifa nyingine ukaipata ndani ya siku 30! Hivi siku 30 ni wakati wote? maana yake ni nini? Inaweza ikatokea move ya baadhi ya taarifa kufichwa ili mtaka taarifa asifanikiwe kwa sababu ya kuweka number of days unnecessarily tu, labda una shida ya kesi una taarifa unazihitaji zikusaidie kwenye kesi yako, una taarifa unazihitaji zikusaidie kwenye biashara yako, lakini kwa sababu tu kuna limitation ya information kutolewa katika muda fulani, tena siku 30 sielewi katika sayansi na teknolojia ya sasa kupewa taarifa ndani ya siku 30, hizo taarifa zinaenda kuchukuliwa nchi gani kama siyo hapa hapa nchini, lakini unaambiwa subiri ndani ya siku 30 ndivyo sheria inasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge niwashawishi tusikubali kupitisha sheria hii bila kuona hivyo vidude gani vinatakiwa kutolewa ndani ya siku 30, ni taarifa ipi na kwa sababu zipi itatolewa ndani ya siku 30. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la taarifa linatupa shida sana, taarifa za Kiintelijensia, Polisi wamekuwa wakitumia habari hizi kwamba wana taarifa za kintelijensia kuzuia mikutano ya Vyama vya Upinzani. Ukiuliza hiyo taarifa ya intelijensia ina nini ndani wanakwambia wanaifahamu wao wenyewe. Sasa hiyo taarifa ambayo wanaifahamu wao wenyewe maana yake yaweza kuwa kwa hila mbaya, roho mbaya, mtu akawa na taarifa ya kiintelijensia halafu anakuzuia usifanye mkutano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini taarifa isitolewe kwa upande unaohitaji kufanya mkutano ukajulikana hiyo intelijensia iliyoko humo ni nini? Na wewe uridhike kwamba kwa kweli kwa intelijensi hii sistahili kufanya huu mkutano, lakini ukiambiwa nenda tu intelijensia tuliyonayo tumezuia mkutano kwa sababu za kiintelijensia. Wakati fulani pale ambapo tumelazimishwa kufanya mikutano, wakati tumeambiwa kuna intelijensia tumekuwa tukifanikiwa mikutano hiyo haina vurugu. Pale walipong‟ang‟ania wao pana intelijensia na wakazuia sana, ndiyo panatokea vurugu, sasa tujue tuambiwe hii intelijensia ina nini ndani ili tujiridhishe wote, inawezekana tukasaidia kuzuia hiyo intelijensia wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni taarifa ambazo ni za kisayansi zaidi, ambazo zinatolewa labda na watu wa idara ya hali ya hewa. Kumekuwa kukitokea taarifa weather forecast, taarifa inatolewa ya tahadhari ya mvua nyingi, El-Nino inakuja, huku kunatokea kitu gani baadaye hiyo El-Nino wala hatuioni, matokeo yake ni vumbi tupu. Wananchi wanaambiwa hameni kuna mvua nyingi inakuja, hakuna mvua inayopatikana, taarifa hizi, kwa wananchi zinaleta usumbufu mkubwa wakati zimepatikana kisayansi. Let us be scientific!
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ingetokea hii ya juzi ya Mbarali kupatwa kwa jua, ikatokea halafu watu waende kule lisipatwe, hali ingekuwaje? Kwa hiyo, naliona hili kwamba wanaotoa taarifa za kisayansi zaidi wawe makini na utabiri wao wa kisayansi, kwamba tumepata kwenye vyanzo halisi kama mitambo imechoka ya watabiri wa hali ya hewa ibadilishwe, tutafute mitambo ya kisasa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za wenzetu wanatoa utabiri wa hali ya hewa in every hour, kila saa wanaweza wakajua kuna nini, sisi kujua tu mvua itanyesha kiasi gani mwezi wa Kumi tunasema mwezi wa Kumi kutakuwa na El-Nino halafu hatuioni! Tunaingia kwenye hasara ambazo siyo za kawaida na atafutwe huyo atakayetuingiza kwenye hasara tutafanya naye nini kwa taarifa yake hiyo isiyo na uchunguzi wa kina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni taarifa zinazotokana na vyombo vya habari, ambavyo Mheshimiwa Nape amekuwa akivifunga tu kila anaposikia kuna ukakasi mwilini mwake. Naomba tukubaliane kwamba taarifa zinaweza zikapatikana kupitia vyombo vya habari. Kama taarifa moja ina tatizo ndani ya vyombo hivyo, unafungaje chombo cha habari chote kilichoajiri watu 40, 50, 60 na hivyo kupunguza ukosefu wa ajira za Watanzania hapa nchini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Nape Waziri wa Habari tulimshauri, kama kuna gazeti linaleta tatizo kuna article whatever imeandikwa ndani ya gazeti inaleta ukakasi, sijui inaleta uchochezi, sijui kwa magnitude ipi, afungiwe Mhariri au Mwandishi wa Habari ile, watu wengine waendelee kuchapa kazi ndani ya chombo kile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii zimefungwa redio mbili juzi tu, Radio Five na Radio Magic. Wafanyakazi wangapi ambao wamepoteza ajira na Waziri wa Ajira tunaye humu ndani, hao watu walikuwa na familia, wana watoto, wana wake, wana waume, wote wamepoteza ajira halafu hakuna anayeshtuka kwa jambo la Mtangazaji mmoja au wawili waliotangaza habari hiyo wanayodhani ni ya uchochezi. Ukiadhibu mtu mmoja, chombo kikabaki hiyo ni discipline already kwa chombo hicho! Siyo habari ya kuamka asubuhi tu unafuta chombo, gazeti unalifungia watu wanaendelea kusota mtaani na wewe unaona raha tu, wanavyoteseka mtaani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa tunazipata wapi? Lazima tukubali kuna mazingira mengine kama kwetu ninakotoka Kibondo, Kakonko, Jimboni kwangu Buyungu bila taarifa kupatikana kwenye vyombo vya habari kama radio hatuwezi kusikia chochote katika nchi hii. Bahati nzuri sisi tunasikiliza radio ya Burundi ndiyo inayosikika jirani na hivyo unaweza ukakuta Watanzania wa kule wanapenda Burundi zaidi kuliko Tanzania kwa sababu ndiko wanakopata information. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo tuwe makini kabla ya kufanya maamuzi mengine, tuone Watanzania wanaathirika kwa kiasi gani na siyo chombo cha habari kile kinaathirika, ni Watanzania wanaoshughulika na kile chombo cha habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii. Kwanza naomba niseme kwamba, kama wafanyakazi wa Tanzania wangefahamu kuna mabadiliko katika Sheria hii ya Public Service Act na negotiating machinery wangejaa humu. Viwanja vya Bunge vingejaa wafanyakazi wa Tanzania, lakini kwa sababu hawafahamu kinachokwenda kufanyika wapo kimya na Watanzania wetu ni wapole kama kondoo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza bomu ambalo litalipuka kwa wafanyakazi wa nchi hii. Mabadiliko yanayokwenda kufanyika kwenye Public Service Act, yanapingana na ILO Conventions, Convention namba 98 ya mwaka 1949. Naomba niinukuu, Convention 98, article 4 inasema hivi:
“Measures appropriate to national conditions shall be taken, wherenecessary, to encourage and promote the full development and utilisation of machinery for voluntary negotiation between employers or employers‟organisations and workers‟ organisations, with a view to the regulation of terms and conditions of employment by means of collective agreements.” Naomba upigie mstari haya maneno; by means of collecting agreement.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanayotaka kuja kupewa Katibu Mkuu apange mishahara ya watumishi yanatoka wapi? Mimi sijui AG anataka ku-achieve nini katika hili. Utumishi wa umma hauwezi kuwa kama grocery ambayo mtu mmoja anaweza akapanga mishahara ya watu wote hawa. Akapanga posho za watu wote hawa, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mabadiliko haya yanapingana na CMA Commission for Mediation and Arbitration (Tume ye Usuluhishi na Uamuzi) ambapo mtumishi yoyote akiwa aggrieved, kwa mfano amefukuzwa kazi lazima awe ameripoti kwenye Tume ya Utumishii na Uamuzi ndani ya siku 30. Hii imesema twende kwa Katibu, twende kwenye Tume ya Public Service Act au twende kwa Rais; atakuwa ameshapoteza haki ya kukata rufaa na kusikilizwa na hii itapoteza haki ya watumishi wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie hii ILO Conventions, Tanzania ime-ratify tarehe 30 Januari, 1962; leo hii yote tumefunika kwa sababu ya kumfurahisha baba yetu. Tunatengeneza mabadiliko ya sheria kwa ajili ya ku-favor mtu na alisema atapunguza mishahara ya watu. He had no grounds, anatafutiwa grounds za kupunguza mishahara ya watu. Hii ni hatari katika nchi hii. Ndugu zangu nawaambia hata upande wa CCM, watumishi wapo ambao ni wana-CCM wazuri lakini hili hawatalifurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuweka maisha ya wafanyakazi rehani, mtu mmoja anakaa kuamua mambo ya watu wengi. Mabadiliko haya yanapingana na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2003 (Employment and Labor Relations Act) ya 2004. Sijui AG anatuambia nini juu ya hili? Anatueleza nini juu ya Sheria zote hizi. Anakwenda kufuta kabisa haki ya mfanyakazi kudai haki yake, haki ya mfanyakazi kujadiliana na mwajiri wake juu ya maslahi yake. Hakuna maslahi yatakayojadiliwa bila kuwa na collective bargaining. Hawezi mtu mmoja akapanga mishahara na marupurupu ya wafanyakazi? Katibu Mkuu ni nani? Hizo ni sheria tulizo-ratify sisi wenyewe, tulikubali kwamba watakuwa wanakaa watatu; mwajiri, mtumishi na Chama cha Wafanyakazi kujadili maslahi ya wafanyakazi; mishahara na hayo marupurupu yanayofanana na kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Sheria hiyo ambayo tunataka kwenda kuifanyia marekebisho, naomba niisome, inaipa mamlaka hii sheria iweze ku-prevail inapogongana na sheria zingine. Public Service Negotiating Machinery Act ya mwaka 2003 na yenyewe hii ime-prevail, ni ipi atakayochukua ndugu yangu AG, kati ya hizi mbili? Public Service Negotiating Act na yenyewe ina-prevail ambayo inazungumzia haki na maslahi ya wafanyakazi wa nchi hii. Hii nayo unataka i-prevail zote ziwe zina prevail, mtumishi atachukua ipi aache ipi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweka maslahi ya wafanyakazi rehani. Tunawaingiza kwenye mgogoro. Masuala ya utumishi yasifanywe kisiasa. Ndugu yangu Chiluba aliwahi kutunga sheria ambayo alisema atakayekuwa Rais asijihusishe na mambo ya siasa akistaafu. Alipostaafu yeye akaanza mambo ya siasa wakamchomolea waraka wa Sheria aliyotunga akiwa madarakani. Leo hii tunatunga sheria kudhibiti wafanyakazi na maslahi ya wafanyakazi kwa sababu tu ya maslahi ya mtu anataka watu waishi kama mashetani, hataki waishi kama malaika, haitawezekana. Kuna siku na yeye itakuja kula kwa watoto wake wakiwa watumishi watakapokuja kukosa haki kutokana na haya mabadiliko tunayoyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo gani juu ya utumishi wa wafanyakazi? Kwanza kupunguza mshahara wa mtu ni dhambi na ni kinyume cha sheria, alishaishi kwa standard ya mshahara fulani, leo hii tunatengeneza mazingira ambayo watu watakuwa wanapunguziwa mishahara yao. Mmoja ana-regulate, ana-harmonize remuneration, allowances and other fringe benefits, hiyo mliiona wapi AG? Nchi hii tutaonekana watu wa ajabu na hii kwenye ILO Conventions, inaruhusiwa nchi kwenye kushtakiwa kwenye Shirika la Kazi Duniani inapo-violate sheria za wafanyakazi nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ikishindikana humu ndani kwa sababu ya wingi wenu ni kuipeleka ILO na kuwaambia hawa watu wamevunja Sheria za Kazi na ita-hold water kwa sababu… muda umeisha?
kwa sababu kinachofanyika hapa ni kufurahisha mtukufu, tusitunge Sheria ya kumfurahisha mtukufu, tutunge Sheria itakayolinda maslahi ya wafanyakazi katika nchi hii na tunazo Sheria nzuri sana kama ilivyoeleza hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Sheria za utumishi ziko vizuri, tusizibadilishe kwa sababu ya kumfurahisha mtu mmoja, mtukufu. Hivyo kuliangamiza Taifa la wafanyakazi wanaokwenda kwenye hali ngumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizungumzie kwenye hizi remedies ambapo kifungu cha 32(a) A public servant shall, prior to seeking remedies provide for in labor laws, exhaust all remedies as provided for under this Act. Hii ni hatari. Wafanyakazi watafukuzwa na hawatakuwa na pa kwenda, utakuwa ukifukuzwa ukirudi kwenye chombo cha kukusaidia wewe uliyefukuzwa urudi kazini wanakwambia ulishapoteza muda, ulishachelewa na kwa sababu walisema uende ku-exhaust huku na hii haikusema utakapo-exhaust hapa unaweza ukarudi kwenye sheria zingine kama CMA ambayo ni nzuri kabisa kwa wafanyakazi na imewaokoa wafanyakazi wengi kutopoteza haki zao za utumishi. Leo hii tunatengeneza sheria ya kupoteza haki za wafanyakazi na tunashangilia kabisa na AG anakuja na nguvu zake zote, anataka kubadilisha wafanyakazi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi wanapoteza haki zao, 2020 ndiyo mtaanza kusema mnawapenda, leo mnawapenda kivipi? Wakati wa uchaguzi ndiyo mtawapenda, baada ya kuchaguliwa mnataka kuwaangamiza, itawakaanga hii, haitawasamehe, haitawaacha.
Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma wa Mwaka 2017
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwanza ni-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, kwa hiyo, nimeusoma muswada huu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote katika yote, ili tuutendee haki muswada huu ni lazima kikokotoo kiingie kwenye kanuni. Kama kikokotoo hakitaingia kwenye muswada huu kikaenda kwenye kanuni, Mheshimiwa Waziri anaweza akaja na yake ambayo hayatakuwa na maslahi kwa wafanyakazi waliokuwa wakiyapata kwenye mifuko iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kufutwa kwa full pension, ile tafsiri ya full pension ni baada ya kuona kikokotoo cha 100 kwa 580 kinapigiwa kelele hakikubaliki kubaliki. Kwa hiyo, ikaonekana kiondolewe halafu eti mtu akafanya actuarial valuation ndiyo aweze ku-determine kikokotoo, ni hatari sana. Mfanyakazi hawezi kuingia kwenye scheme; unamwingiza mfanyakazi kwenye scheme hajui mwisho wa siku atanufaikaje na scheme hii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kitu kiwe in black and white kwenye sheria. Hizi sheria tunazo-merge zote zilikuwa zina formula. Kabla hujajiunga unaangalia formula ya PSPF inanifaa kwa kiasi gani? Formula ya NSSF inanifaa kwa kiasi gani? Formula ya PPF, kwa hiyo, mfanyakazi anasema should I go to PSPF or NSSF or PPF? Baada ya kuona maslahi yanayo muhusu. Sasa tukienda kuficha kwenye kanuni, halafu sheria iwe kimya kabisa, haina mafao yoyote, haionyeshi mwisho wa siku itatusaidia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili halileti afya na kama Waziri anaona, ili kikokotoo kifahamike ni baada ya actuarial valuation, alitakiwa afanye actuarial valuation ndiyo alete hoja ya kuunganisha kwamba hawa nimewaona
wakiungana, nimeridhika kwamba watakuwa na afya ya kutosha kunufaisha wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unakuja unaunganisha ambapo hujui kwamba baada ya actuarial valuation watakuwa na afya kiasi gani? Ukikuta baada ya kuungana, hali zao ni mbovu, ni mbaya kabisa, tutarudi humu tena kuja kushughulikia hii kitu? Kwa hiyo, hilo naliomba kabisa Waheshimiwa Wabunge tukubaliane, tusipitishe sheria ambayo iko kimya, yaani hata leo tukitoka, unakwenda kumuuliza mwenzako ambaye ni mfanyakazi aliyeko nyumbani, hivi tutafaidikaje na huu mfuko? Nikistaafu nitalipwa bei gani? Huwezi kumwambia bei atakayolipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kuna hii cutoff point ambayo inataka wafanyakazi waliokuwa katika sekta fulani wabaki huko tu-board na hawa wapya kwenye mfuko huu mpya. Basi ikiwezekana, vikokotoo vyao walivyokuwa navyo vibaki. Kila watu wa board in kwenye mfuko huo na vikokotoo vyao. Kwa hiyo, waliokuwa na 540, waendelee na 540 yao mpaka watakapo-phase out, waliokuwa na 580 nao waingie humo wa-board in mpaka watakapomaliza. Kikokotoo kipya kitakachokuja kianze na wafanyakazi wapya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia njema kabisa ya kuunganisha mifuko hii, tusisahau baadhi ya benefits ambazo zilikuwa kwenye mifuko ya zamani. Mfanyakazi aliyekuwa ana-benefit kwenye mfuko aliokuwanao tusiipoteze ile benefit kwa sababu tu ya kuanzisha mfuko mpya. Mfuko mpya kama tunauanzisha na tunapoteza baadhi ya benefits, haina sababu ya kuunganishwa. Kuunganishwa kuboreshe kutoka pale tulipokuwa kwenda sehemu nyingine bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fao la elimu limeondolewa wakati mifuko mingine ilikuwa inatoa hilo fao. Fao la afya (health insurance) nalo linaondolewa wakati lilikuwepo. Sasa hivi vitu tusipoviangalia vitatuletea confusion. Sasa mtu anajiuliza, huu mfuko mpya unanifaa kweli au haunifai? Kwa sababu hata kuwa na option, yaani ni kama tunatengeneza kitu ambacho utake, usitake utaingia tu. Kwa hiyo, hiki ni kitu cha hatari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 19 ambacho kimtoza fine anayechelewesha makato, mwajiri ambaye amechelewesha makato. Tukubaliane ile fine inayotozwa imnufaishe na mfanyakazi yaani at the end of the day wanapo-calculate mafao yake, waangalie tulinufaikaje na fine? Isiwe fine tu inaunufaisha mfuko halafu member hatanufaika nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 18(2) kwenye (b) pale, kuna mahali ambapo tunazungumzia viwango vya kutoza, asilimia tano kwa mfanyakazi na asilimia 15 kwa mwajiri. Pale chini pamesema hivi, baada ya kusoma (b): “or such amount as the Minister may by order published in the Gazette determine taking into consideration of the actuarial valuation.” Maana yake nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna siku watafanya actuarial valuation waone labda mfuko una afya mbaya, Waziri akaamua kuongeza makato. Inawezekana, yaani hii inampa room Waziri kuongeza makato wakati tulishaweka kwenye sheria ni 5% by 15% ya Mwajiri. Hivi kwa nini tusiondoe hiki kifungu? Yaani kila siku akiamka tu akiona mifuko ina afya mbaya, anakwenda kuongeza makato. Mfanyakazi anaishi bila ya kuwa na uhakika atamaliza anakatwa kiasi gani? Kama ni 5% ibaki 5% na 15 ibaki 15. Kama anaiongeza, aiongeze kwa mwajiri, Mtumishi abaki na ile ile ya kwake.