Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ally Mohamed Keissy (18 total)

MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwambao wa Ziwa Tanganyika wavuvi wengi wanatoka DRC-Congo. Cha ajabu wanakata leseni kwa bei kama mvuvi mwenyeji wa Ziwa Tanganyika. Je, ni lini Serikali itachukua hatua ili wavuvi kutoka nchi za jirani walipie leseni kama inavyotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Keissy kwa sababu amekuwa akifuatilia kwa karibu sana changamoto mbalimbali za uvuvi na hasa katika maeneo ya Jimbo lake. Tumepata taarifa kwamba kuna wavuvi wanaotoka nchi za jirani wanavua katika maziwa yetu. Kwa vyovyote vile, hii ni kinyume na sheria. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge taarifa kama hizi tuendelee kuzipata. Tukitoka hapa mimi mwenyewe nitachukua hatua za makusudi za kufuatilia ili tuweze kujua nani amehusika, tuwajue Maafisa wa Halmashauri wanaotoa leseni kwa watu hao ili kuweza kuchukua hatua stahiki.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pia nampongeza Mheshimiwa Sitta kwa namna anavyofuatilia tatizo la maji kwa wananchi wa Urambo. Amekuja Wizarani, tumeongea naye na kimsingi tumekubaliana kwamba maji ya wananchi wa Urambo tutayatoa Mto Ugalla. Suala la kufanya upembuzi yakinifu ni jambo la msingi katika miradi yote. Ni lazima tufanye haya maana kule Ugalla ni Hifadhi. Sasa ni lazima tufanye mawasiliano nao kwamba tutapitisha mabomba sehemu zipi na itaathiri vipi! Masuala haya ni ya msingi lakini haitazuia mradi ule kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie kwamba tutapeleka maji kupitia kwenye Hifadhi, lakini mawasiliano ya kimsingi kati ya Wizara husika; Maliasili na Utalii pamaja na Ofisi ya Rais, Mazingira, lazima tuyafanye ili tuweze kukubaliana vigezo vipi tuvifanye na mradi uweze kuwa endelevu kwa ajili ya faida ya nchi hii. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Keissy kuhusiana na matatizo ya utekelezaji wa miradi katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, nakiri kwamba tumeshawahi kuongea naye nje, amenitolea taarifa kwamba kuna miradi katika Wilaya yake ambayo haijaenda vizuri; sasa tumeanza kazi. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba sisi tunasema hapa ni kazi tu kwa kutekeleza kauli ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi, tatizo hili tunalifanyia kazi na imani yangu ni kwamba tutalipatia majibu kwa haraka sana.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimwia Spika, kwa kuwa Mkoa wa Kigoma pamoja na Wilaya zake zinaingiza gharama kubwa sana katika Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutumia majenereta, zaidi ya bilioni 160 kwa mwezi, kwa nini Serikali pamoja na Wizara ya Nishati na Madini isifanye haraka mradi huu ili kuokoa pesa kwa Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa shughuli za ugawaji wa umeme katika Mji wa Kigoma ni gharama kubwa na gharama alizozitaja Mheshimiwa Keissy kwa kweli ni kidogo siyo shilingi milioni 160 isipokuwa ni shilingi milioni 600 kila siku za mafuta tunatumia.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia uzito huo huo, ndiyo maana Serikali imesema itaanza ujenzi wa mradi huo wa Malagarasi ndani ya miezi sita kuanzia sasa, kuanzia mwezi Februari mwakani shughuli za ujenzi kwa ajili ya kuwapatia umeme wa uhakika wananchi wa Kigoma zitaanza. Kama nilivyosema shughuli hizi zitachukua miaka mitatu hivyo mwaka 2020 shughuli za ugawaji wa umeme katika Mji wa Kigoma zitakamilika na umeme utakuwa ni wa uhakika ambao haukatiki.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jiografia ya Wilaya ya Nkansi, naomba hilo swali labda angesaidia kujibu Mheshimiwa Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Elimu, Teknolojia na Elimu ya Juu. Inaonekana hilo swali halikujibiwa jinsi inavyotakiwa na aliyeandika hilo jibu, hajui Wilaya ya Nkasi ilivyo; Kipili iko wapi, Namanyere iko wapi, Kala iko wapi, Itindi iko wapi, Kabwe iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majambazi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hilo gari haliwezi kuhudumia vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, lini Serikali, itawapatia mgawo wa mafuta wa kutosha Wilaya ya Nkasi?
Mheshimiwa Naibu Spika, gari lenyewe liko Wilaya ya Nkasi, hata mafuta halina! Lini itaongeza mgao wa mafuta katika Wilaya ya Nkasi? Lini itawapatia pikipiki vijana wa Marine Kipili, ili kuondoa tatizo la usafiri ambako unatokea ujambazi katika vijiji vilivyopo jirani jirani na mwambao wa Ziwa Tanganyika ili kupunguza uharamia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwamba Wilaya ya Nkasi kijiografia imekaa na changamoto nyingi sana hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya vijiji vyake kama Kipili, Kala, Wampembe na vijiji vingine kama Samazi, vimekaa mbali kidogo, vinahitaji mwendo mrefu kuvifuata. Kwa hiyo, vinahitaji mafuta ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imefanya jitihada kubwa sana katika Mkoa wa Rukwa na Nkasi kwa ujumla. Kwanza kuna maboti ya kutosha ambayo yalipelekwa kwa ajili ya Jeshi la Wananchi ambao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana na Jeshi la Polisi.
Vilevile kuna vituo ambavyo vimeanzishwa katika maeneo hayo na hivyo, kuwezesha kuwa na urahisi wa kuwafikia wananchi wanapokuwa na tatizo, hususan katika kijiji cha Kipili. Kwa hali hiyo, naamini kwamba pamoja na jitihada ambazo zimekuwa zikiendelea kufanyika hali ya Nkasi kwa sasa ni bora kuliko ilivyokuwa hapo awali. Ahsante sana.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Kituo cha afya cha Kirando kilianzishwa miaka 42 iliyopita wakati Kirando ikiwa ni Kijiji, leo kina wakazi mara 50 zaidi kutoka miaka 42, aliyekuwa Waziri wa Afya Mheshimiwa Dkt. Seif Rashid alifika pale Kirando na akaniahidi kwamba hiki kituo kweli kimezidiwa na ninafanya mpango wa kuwa hospitali kamili.
Lini Serikali yako itaipa hadhi kituo cha afya Kirando kuwa hospitali kamili kwa kuwa kimezidiwa na wagonjwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli inawezekana kabisa kwamba katika huduma za vituo mbalimbali vya afya kumekuwa na kuzidiwa kwa sababu ya umbali kutokana na maeneo yetu kati ya kituo kimoja hadi kingine. Lakini kwa
suala la kituo cha afya ya Kirando ambacho Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba kimezidiwa na je ni lini au kuna mikakati gani ya kuimarisha ili kiweze kutoa huduma hiyo au kubadilishwa kuwa hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kikubwa hapa ni ushirikiano kati ya mamlaka ya Serikali za Mitaa ambapo Waheshimwia Wabunge ni Madiwani kule katika kupanga vipaumbele vyetu, ni vizuri mkawa mnaturahisishia kazi ya kupanga halafu mnajua kabisa kwamba hatua zile huwa ikitoka pale mnaenda kwenye Mkoa ambapo mnashauriana, katika Sekretarieti ya Mkoa kwenye kikao cha ushauri cha Mkoa pale ndipo ambao mnaweza mkaja na mapendekezo halafu Serikali Kuu tukaona tuanze na lipi katika eneo lenu.
Mheshimiwa Ally Keissy, nikuombe tu kwamba kama mtasema tukiimarishe hiki na kuwa hospitali, basi jambo hili lije kwa utaratibu wa kisheria kama ulivyoelezwa katika Sera ya Afya.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Nkasi, kuna Ranchi ya Kalambo ambayo iligawiwa kwa wafugaji block kama kumi, kila block heka 3000 mpaka 2500 kila mfugaji, block kumi. Lakini hizo block kumi hakuna ng‟ombe zilizopelekwa baadhi ya blocks na baadhi ya waliochukua hizo block ni wajanja hawana mfugo hata mmoja wanakaa wanakodishia wafugaji.
Je, Serikali iko tayari kupitia upya Ranchi ya Kalambo ili kugawa upya kwa wafugaji ili kuondoa matatizo ya wafugaji na wakulima nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba kuna changamoto kubwa sana katika ranch ya Kalambo na ranch nyingine ambazo zinamilikiwa na NAFCO, hasa zile ambazo zimegawiwa kwa Wawekezaji.
Nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa sasa Wizara inafanya tathmini ya kuangalia namna uwekezaji ule ulivyofanywa ili ikigundulika kwamba kuna wawekezaji walipewa ranchi za NAFCO lakini hawatumii ipasavyo wanyang‟anywe na kupewa kwa wafugaji na wawekezaji wengine ambao watatumia inavyotakiwa.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi leo ina miaka 40 tangu ilipoanzishwa, lakini haina hospitali ya Wilaya, wala Serikali haina mpango wa kujenga hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali yetu itakuwa na azimio la kujenga hospitali ya Wilaya hasa katika Makao Makuu ya Wilaya katika Mji wetu wa Namanyere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninamfahamu Mheshimiwa Keissy kuhusu suala la tatizo la afya. Miongoni mwa mambo ambayo ninayakumbuka Mheshimiwa Keissy alipendekeza kituo kimoja kile cha afya kukipandisha grade kuwa hospitali ya Wilaya kama sikosei. Alizungumza hapa Bungeni kwamba kituo kile cha afya licha ya kuwahudumia wananchi wa Jimbo lake, wengine wanatoka katika nchi mpaka ya Congo. Hili nilisema siku ile kwamba Mheshimiwa Keissy jambo hili tumelichukua, katika mpango wa pili wa afya kila Halmashauri kuwa na hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Keissy naomba niseme tu kwamba tutaungana pamoja katika mipango kwa sababu tunajua Wilaya yako ipo pembezoni na ina changamoto nyingi. Tutajitahidi kwanza kuhakikisha kile kituo cha afya tunakiangalia na mimi nimekiri wazi kwamba nikija kwako lazima nikitembelee kituo cha afya, tutashawishi wenzetu wa Wizara ya Afya wakiangalie kama kimefikia vigezo kipandishwe kuwa hospitali ya Wilaya, tutakuunga mkono ili wananchi wa eneo lako lazima wapate afya. Jambo hili umelipigia kelele sana toka Waziri Mkuu wa mwanzo Mheshimiwa Peter Pinda nilikusikia ukilizungumza, nasema kwamba tupo pamoja katika hili.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Waziri ametembelea mpaka Wilayani kwangu Nkasi kule na kujionea mwenyewe jinsi matatizo ya mawasiliano ya Redio TBC hayafiki kule kwetu. Ni lini sasa bataweka mkazo ili watu wanaokaa mwambao mwa Ziwa Tanganyika waache kutegemea matangazo kutoka DRC Congo?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI,SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika Mikoa michache ambayo nimeitembelea ni pamoja na Mkoa wa Rukwa na Jimboni kwake Nkasi na nimpongeze kwa juhudi walizozifanya Halmashauri ya Wilaya Nkasi kwa kuanzisha redio yao na inafanya vizuri sana. Ni kweli pia kwamba usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa kwa Wilaya ya Nkasi ni mbovu na baadhi ya maeneo yakiwemo ya Kabwe na maeneo mengine kwa kwa kweli wanasikiliza matangazo kutoka nchi jirani ya Congo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema tumeweka mkazo mkubwa kuhakikisha mikoa hii ya pembezoni tunaimarisha usikivu wa Shirika letu la Utangazaji la Taifa ili wananchi wetu waache kusikiliza redio za nchi jirani ikiwezekana watu wa nchi jirani wasikilize redio yetu na Shirika letu la Utangazaji wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie katika maeneo yote niliyotembelea kwa bahati nzuri, baada ya ziara yangu Mkurugenzi wa TBC Dkt. Rioba amekwenda huko nilikopita, na kuhakikisha kwamba yale niliyoyaagiza yanatekelezwa; na nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi wa TBC kwa kazi nzuri anayofanya, ya kulibadilisha Shirika letu la Utangazaji na mimi naamini kwamba kwa kasi yake mambo yatakwenda vizuri.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Naibu Waziri katika swali lake la kwanza alisema kwamba ana ziara ya Iringa, Mbeya na Songwe. Je, yuko tayari sasa katika hiyo ziara kuunganisha mpaka Wilaya ya Nkasi akajionee mwenyewe matatizo ya Afya, Elimu na Barabara katika Wilaya yetu ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ziara yangu inaanzia Mkoa wa Iringa, nitakwenda Mkoa wa Njombe, Mbeya, Rukwa, nikitoka hapo nitakwenda Mkoa wa Kigoma halafu namalizia Mkoa wa Tabora, hiyo ni phase namba moja. Baadaye nitakwenda Mkoa wa Mara, Geita, Mwanza, Kagera, halafu nitarudia katika Kanda ya Mashariki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Keissy mpo katika awamu ya kwanza ya ziara yetu kubaini changamoto ili kuona jinsi gani Ofisi ya Rais TAMISEMI, tutafanya kuwahudumia wananchi wa Tanzania.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hii Awamu ya Tano, kila siku namsikia Mheshimiwa Rais anazungumza haya mambo, kwamba ukinunua kitu dukani omba risiti; ukienda hotelini, omba risiti, je, Serikali imejipangaje kuhusu hawa wauza mitumba na wanaotembeza mali (machinga) na mama ntilie kwa ajili ya kutoa risiti ili tupate kodi ya Serikali yetu? Serikali imejipangaje hapo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Keissy, kwa nyakati tofauti amekuwa akihimiza sana suala la ulipaji kodi. Naomba tukiri kwamba hii nchi haitaweza kwenda bila watu kulipa kodi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, 2015 ametudokeza sehemu moja, mfanyabiashara mmoja anaingiza karibu shilingi milioni saba kila dakika. Kwa hiyo, kuna watu wakubwa wanakwepa kodi na wadogo wakati mwingine kodi hazikusanywi vizuri.
Mheshimiwa Keissy naomba nikuhakikishie, Ofisi ambayo inaongozwa na kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mpango imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba inafanya utaratibu mzuri, kila mtu atalipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisisitize tena; na sababu ni kwamba katika kada zote, kila mtu atawekewa utaratibu mzuri ilimradi kodi tupate shilingi trilioni 29.54 kutimiza matakwa ya bajeti yetu. Naomba tushirikane na Serikali kwamba wale wenye sheli za mafuta waweke mashine za mafuta na kila mtu atumie mashine za EFD katika Halmashauri zote, tutumie elektroniki na kila utaratibu, kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango ametuwekea utaratibu kuona jinsi gani tutafanya tukusanye kodi kila mtu alipe kodi bila kukwepa kodi.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kijiji cha Kipili, Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa, tulikuwa na Chuo cha Uvuvi, na kulikuwa na generator na cold room, lakini bahati mbaya awamu zilizokuja ikageuzwa ikawa secondary school na uvuvi ukaisha, na sisi watu wa mwambao tunategemea sana uvuvi, hasa mwambao wa Ziwa Tanganyika, na hakuna Chuo:-
Je, ni lini Serikali itakirudisha Chuo cha Uvuvi cha Kipili ili kusaidia wavuvi wetu wa mwambao wa Ziwa Tanganyika?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala alilolisema Mheshimiwa Keissy, Serikali ilikuwa na nia njema kufuatana na mahitaji la kupanua elimu, ikafanya mabadiliko hayo, lakini kwa kuzingatia kwamba Jimbo la Mheshimiwa Keissy wananchi wake wanategemea uchumi wa uvuvi, sisi pamoja na TAMISEMI tutashirikiana kuangalia utaratibu mpya wa kuweza kurejesha utaratibu wa kuwa na chuo ambacho kitasaidia vijana wetu kuweza kujifunza na kuweza kumudu kazi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili litaendana pia na mpango wa Wizara ya Elimu na Ufundi, ambao unahusisha vyuo vya VETA katika kila Wilaya ili tuweze kupata wanafunzi wengi ambao watafanya kazi kwa utalaam zaidi. Hili jambo linaenda sambamba na Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso wa Jimbo la Pangani ambaye alishaongelea kwamba wananchi wake pia wanahitaji sana kufufuliwa kwa chuo ambacho uchumi mkubwa wa Pangani wa vijana unategemea uvuvi.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Katika Ziwa Tanganyika tuna Halmashauri tano na kila Halmashauri ina licence yake na mvuvi anakata licence, lakini anapotaka kuhama kwenda Halmashauri nyingine hata kama licence yake haijakwisha muda lazima alipie licence upya kwenye Halmashauri anayokwenda. Je, ni lini Serikali itaondoa kero hii kwa wavuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema hapo awali kwamba ziko tozo ambazo zimekuwa ni chanzo cha mapato ya Halmashauri mbalimbali na moja ya vyanzo hivi vya mapato kwa Halmashauri zetu ni leseni. Bahati mbaya sana kwa kanuni tulizonazo na Sheria ya Uvuvi iliyopo leseni hizi za Halmashauri zimekuwa za maeneo ya Halmashauri husika yaani hazihamishiki na ndiyo maana kumekuwa na huu usumbufu kwa wavuvi kwamba leseni zinazotolewa na Halmashauri ya Sikonge haiwezi kwenda kutumika katika Halmashauri ya Urambo, hili ndilo limekuwa changamoto. Nimpe tu faraja Mheshimiwa Mbunge kwamba hili nalo liko katika mambo ambayo yanaangaliwa na hiyo Tume ya Taifa ya Makatibu Wakuu inayopitia upya hizi kodi ambazo zimekuwa kero kwa wananchi.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, Asante sana. Pamoja
na jibu zuri la Naibu Waziri. Sasa lini Serikali itatoa kero kwa hizi kodi ndogo
ndogo za akina mama hasa wakinamama wauza vitumbua, wauza mchicha,
wauza dagaa, wauza nyanya ili kutoa kero kwa wananchi wetu wasiendelee
kudhulumiwa na kuteswa na hawa wakusanya kodi na hawa Wanamgambo,
imekuwa kero na Serikali kila mara ilitangaza hapa kwamba kodi ndogondogo
hizi ni kero lini Serikali itatangaza Halmashauri zote ziache mara moja kutoza
akina mama kwenye masoko madogo madogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya rejea wakati wa kampeni ya uchaguzi ya mwaka 2015. Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akijinadi kwa wananchi ni suala zima la mchakato wa kuondoa hizi kero ndogo ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Keissy, nimefanya ziara katika maeneo mbalimbali hata pale maeneo ya Ilala pale katika soko letu la Ilala, soko la Feri, Sokola Pugu Kajungeni na maeneo mbalimbali, soko la Mwanjelwa kule Mbeya. Hizi ni miongoni kwa concern lakini siyo hivyo utakuta mtu wa kawaida analipishwa risiti isiyokuwa sawasawa ndio maana tumezielekeza Halmashauri zote. Sambamba na hilo tukaona sasa lazima tubainishe ipi ni kero ambayo itaweza sasa ikashughulikiwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana sasa kwa mujibu wa utaratibu wetu tumeandaa sheria sasa inakuja hapa Bungeni, ambayo sheria ile itaainisha sasa sheria ambayo marekebisho ya Sheria ya Mambo ya Tozo na Ushuru Sura ya namba 290 itakuja hapa na sisi Wabunge wote tutashiriki, na nina imani kwamba Mungu akijalia huenda Mkutano ujao wa Bunge inawezekana sheria hiyo itaweza kufika mara baada ya wadau wakishashiriki vya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaziagiza Halmashauri zote kwamba yale mambo ambayo unaona kwamba hili ni kero, kwa sababu hili suala Mameya wote, Wenyeviti wa Halmashauri wanajua kwamba sehemu hizo wamepewa kura na wananchi wao. Jambo ambalo naona kwamba jambo hili halina tija kwa wananchi wetu wa kawaida, naomba tulifanyie kazi, lakini jambo ambalo mmeona mmeliweka kwa mujibu wa sheria basi mlisamize kwa utaratibu bora, siyo kwenda kutoa kapu la mama anauza vitunguu barabarani au anauza nyanya barabarani hilo jambo litakuwa siyo sawasawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nazielekeza Halmashauri zote hasa Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri waweze kukaa pamoja na Kamati zao za Fedha, wabainishe ipi ni kero kwa sasa kabla sheria hii haijakuja hapa Bungeni ili mradi kuweza kuondoa kero kuwafurahisha wananchi waishi katika maisha ya utaratibu wa kujenga uchumi wa nchi yao.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Swali; je, wale Wakandarasi au Halmashauri zilizolipa pesa kwa Wakandarasi hewa, mtachukua hatua gani? Kuna miradi kadhaa katika Wilaya ya Nkasi ambayo pesa zililipwa lakini hakuna kilichofanyika.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkandarasi amelipwa lakini kazi hajafanya, maana yake huo ni wizi; jambo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie na hili tumelisema katika vipindi mbalimbali, Wakandarasi wowote ambao kwa njia moja au nyingine wamechukua fedha na kazi wametelekeza, tutahakikisha, nami nitawaomba Wakurugenzi wote waweze kuwabainisha; hasa wale Wakandarasi wa maji waliotekeleza miradi katika maeneo yao. Kwa sababu tukirejea katika Bunge lililopita, Waziri wa Maji hapa alisema wazi kwamba Wakandarasi ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao watafutiwa hata suala la kupata tenda katika nchi yetu. (Makofi)
Kwa hiyo, Mheshimiwa Keissy, naomba tukitoka hapa unipe rejea ya hao Wakandarasi ili mradi tuweze kuwafanyia kazi. Lengo kubwa ni kwamba, wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji.

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI, hoja ya Mheshimiwa Keissy ndiyo tumeshaanza kuifanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji tumeamua kuchukua hatua kwamba hatuwezi kupeleka hela kwenye Halmashauri mpaka walete certificate. Tumefikia hili kwa sababu hela zilikuwa zinapelekwa, halafu zinatumika, lakini ukienda kule hakuna kilichofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza huko nyuma katika Bunge hili, ni kwamba tunakwenda kuunda Kamati ya Wataalam. Utaleta certificate yako kabla hatujailipa, tutatuma wataalam kwenye eneo twende tukaangalie kama hiyo kazi imefanyika ili tuweze kupambana na hili suala ambalo lilitaka kutupeleka pabaya.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kama Serikali ipo tayari kupeleke pesa hizo, lakini nataka kujua ni shilingi ngapi zitapelekwa kwa ajili ya kumalizia huo mradi wa Skimu ya Lwafi? Nataka kujua kiasi cha pesa.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, fedha itakayopelekwa kule ni shilingi milioni 550 na fedha hii inatolewa na Serikali ya Japan na tayari taratibu za kuipeleka hiyo fedha zimeshafanyika ila kumekuwa na matatizo kidogo kupanua ile item ya kulipia kwa upande wa Halmashauri, ndiyo Serikali inaendelea kupanua. Fedha hiyo ipo tayari na wakati wowote itaingia.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Vituo vya Kirando na Kabwe ni majengo ambayo Wizara ya Mambo ya Ndani ilinunua kwa wananchi wa kawaida. Ni majengo yaliyojengwa kwa tofali mbichi na hata leo akienda kuyaona hayana milango, saruji na yanabomoka na baadhi ya nyumba za uani wanazolala polisi hazina milango kabisa. Je, katika hizo nyumba 4,136 vituo vya Kirando ni miongoni mwa vituo vitakavyokarabatiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufanya ziara katika Wilaya ya Nkasi kuvitembelea Vituo vya Polisi Kirando na Kabwe na vituo vya Uhamiaji vya Mwambao wa Ziwa Tanganyika ambavyo viko katika hali mbaya sana, havistahili Polisi kuishi wala kufanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa nyumba 4,136 hausiani na ukarabati wa vituo vya Kabwe na Kirando. Hata hivyo, kama nilivyozungumza katika jibu langu la msingi ni kwamba tuna program vilevile ya ujenzi wa vituo vya polisi nchi nzima. Ingawa kutokana na udharura wa vituo vya Kabwe na Kirando kwa kuwa ujenzi wa vituo na uimarishaji wa usalama katika nchi yetu unakwenda sambamba na maendeleo ya nchi hii, basi ikiwa Mheshimiwa Mbunge ataona inafaa si vibaya katika Mfuko wa Jimbo akaangalia uwezekano wa kukarabati vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na ziara, tutaangalia uwezekano huo. Kama ambavyo nimekuwa nikizungumza kila siku, wajibu wetu ni kuweza kufanya ziara nchi nzima katika maeneo yote kuangalia changamoto zinazokabili vyombo hivi ambavyo viko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Nkasi ni moja ya sehemu hizo.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa mara ya kwanza Serikali kutoa jibu zuri la kuridhisha kwa wananchi wa Nkasi.
Kwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliniahidi mimi humu Bungeni kwamba mara baada ya kukamilika ile barabara yuko tayari kutoa yale majengo kwa Chuo cha Ufundi VETA. Na sasa barabara yetu inakwenda speed ya ajabu, imebaki kilometa 10 au 12 na wakandarasi wameniahidi Januari au Disemba kipande cha barabara hiyo kitakamilika.
Je, lini sasa mazungumzo kati ya Wizara ya Elimu na Wizara ya Ujenzi yataanza haraka iwezekanavyo wananchi wapate kile chuo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wake tumeupokea, na mara baada ya kumaliza Bunge hili, tutawasiliana na wenzetu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili tuweze kuona suala hili kabla hata barabara hazijaisha.
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Jiji la Dar es Salaam linashangaza kwani wamechukua kampuni ya kutoka Kenya ili kukusanya fedha za maegesho ya magari Dar es Salaam. Vilevile hawatumii mashine za EFD kukusanya pesa na kupandisha kutoka Sh.300 kwenda Sh.500. Hivi kweli nchi nzima ya watu milioni 50 wamekosa kampuni yoyote katika nchi yetu mpaka kuchukua Kampuni ya Kenya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue concern hii ya Mheshimiwa Keissy lakini ninavyojua katika suala la ukusanyaji Manispaa za Ubungo, Ilala na Kinondoni zinakusanya zenyewe lakini kwa ukubwa wake Manispaa ya Temeke na Kigamboni, Halmashauri ya Jiji yenyewe inasimamia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la kampuni kutoka Kenya kukusanya nadhani huo ni mchakato wao lakini ninavyojua ni kwamba kuna utaratibu maalum kwa Jiji la Dar es Salaam, kila Manispaa kwa maana ya Ilala, Kinondoni na Ubungo zina utaratibu wake wa kukusanya ila Manispaa ya Temeke na Kigamboni Jiji lenyewe linasimamia kwa taarifa nilizokuwa nazo, wanasimamia kama Wakala wa Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo, Mheshimiwa Keissy kuhusu hii kampuni kutoka Kenya kukusanya fedha hizi ngoja tuzi-cross check zaidi lakini inawezekana ni taarifa za kimagazeti zaidi kuliko uhalisia wake.