Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Augustino Manyanda Masele (24 total)

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
(i) Naomba niiulize Serikali ni lini sasa madai ya hawa watumishi 65 waliosalia yatalipwa?
(ii) Kwa kuwa posho za kujikimu na posho ya usumbufu ni halali ya mtumishi, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuwa inawalipa watumishi inapowahamisha malipo hayo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni lini fedha hizi zitalipwa, nimesema katika jibu langu la msingi, kwamba ni kweli pale kuna watumishi ambao wamehamia katika Halmashauri mpya. Katika kuliona hilo sasa tukaona ni vema sasa hii fedha itengwe katika bajeti ya mwaka wa fedha huu ili watumishi waweze kulipwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndungu yangu Masele naomba uwe na subira tu, kwa sababu katika Bajeti yetu tulivyopitisha tulizungumza mchakato mkubwa katika suala zima la Halmashauri mpya kwa hiyo katika suala hili la ujenzi wa miundombinu lazima uende sambamba na malipo ya madeni ya watumishi mbalimbali. Kwa hiyo, jambo hili tutakwenda kulifanya kwa kadri iwezekanavyo ili watumishi wale wapate utulivu, wafanye kazi yao kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Spika, ni jinsi gani tutafanya Halmashauri zinapoanzishwa madai ya watumishi yaweze kulipwa kwanza, hili tutaliwekea maanani. Lakini Waheshimiwa Wabunge tukumbuke kwamba sasa hivi kuna Halmashauri mpya nyingi sana, ofisini kwangu mpaka sasa hivi nimeaandaa matrix form ya kuona Halmashauri ina Wilaya mpya ambazo Wabunge mbalimbali wameenda kupeleka maombi Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuweza kuanzishwa. Kwa hiyo, jukumu letu kubwa tutakuwanalo ni kuona ni jinsi gani haya matakwa ya wananchi katika maeneo husika yaweze kufikiwa, lakini hatuwezi kuzuia Halmashauri kuanzishwa kwa sababu posho bado hazijapatikana.
Mheshimiwa Spika, tukifanya hivyo tutakuwa tumezuia maendeleo ya wananchi katika maeneo husika, hata ninyi Wabunge hamtoridhika katika hilo. Kwa hiyo, tumechukua ushauri huo wote, lengo kubwa ni mipango yote iende sambamba, Halmashauri zinapoanzishwa na fedha ziweze kulipwa.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri nazoendelea kuzifanya za Taifa letu. (Makofi)
Swali la kwanza kutokana na umuhimu wa barabara hii katika Mkoa wa Geita; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutembelea katika Mkoa wa Geita na kuipitia hii barabara ili aone uwezekano wa kuiingiza barabara hii katika kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili hatimaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?
Swali la pili, Mheshimwia Rais wetu kwa nyakati tofauti akiwa Waziri wa Ujenzi na alipoteuliwa kuwa mgombea wa Chama chetu cha Mapinduzi, aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilometa tatu katika Mji wa Masumbwi; je, Serikali ina mpango gani sasa kutimiza ahadi hizi za Mheshimiwa Rais wetu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mheshimiwa Masele amenialika nitembelee katika mkoa wake, nataka kumuhakikisha nitatembelea nitatembelea mkoa huo na kuangalia barabara anayoisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kipindi kifupi nilichoingia kwenye Wizara hii, tumetembelea takribani mikoa kama 23 ya Tanzania Bara kuangalia barabara mbalimbali. Tunaamini baada ya miezi miwili inayokuja tutatembelea mikao yote ya Tanzania na kuangalia barabara zetu kuhakikisha kwamba tunazitengeneza kama tunavyopanga mikakati yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, alitaka kufahamu Mheshimiwa Rais, aliahidi kujenga kilometa tatu (3). Ni kweli Mheshimiwa Rais ameahidi maeneo mbalimbali kujenga, kwingine kilometa tatu (3), kwingine kilometa tano (5); sisi kama Wizara tumezichukua ahadi zote hizo za Mheshimiwa Rais na tumeziweka kwenye mpango wetu na tunahakikisha kwamba barabara hizo tutazijenga kwa awamu, itategemea upatikanaji wa fedha.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze na mimi kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimwia Naibu Spika, kwa kuwa changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo la Magu zinafanana sana na changamoto zinazolikabili Jimbo la Mbogwe, ambapo wananchi katika Kata za Ikunguigazi, Lolangulu, Ikobe na Bukwande wamejenga majengo yao ya maboma kwa ajili ya vituo vya afya lakini nguvu zao zikawa zimepelea. Je, Serikali iko tayari sasa kuwaunga mkono ili kuweza kukamlisha vituo hivyo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele mjukuu wa Mzee Ulega kuwa tumeliongelea suala la zahanati na tukiwa pale Geita wakati Mheshimiwa Mama Suluhu Hassan alipokuwa akizindua hospitali kubwa ya Geita. Nimesema hapa katika majibu yangu ya msingi, kwamba mambo makubwa tunaenda kuyafanya. Sasa hivi tunafanya tathimini ili tuangalie jinsi ya gani ya kufanya.
Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Augustino kwamba tutakupa kipaumbele kikubwa zaidi na kwa sababu katika ratiba ambayo nimeitengeneza leo, katika ziara yangu miongoni mwa maeneo nitakayopita Jimbo lako nimeliweka kutokana na kunisukumasukuma sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tukifika kule tunaweza kuangali hata structure ya majengo yenyewe na kukupa kipaumbe ili wanchi wako wa Jimbo la Mbogwe kupata huduma ya afya.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuuliza swali moja dogo la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo ya nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui yanafanana kabisa na yale matatizo ya watumishi wa Wilaya ya Mbogwe na tayari Serikali imeshatoa shilingi milioni 45 kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi lakini nyumba hizo mpaka sasa hivi hazijakamilika. Je, Serikali iko tayari sasa kuongezea pesa ili nyumba za watumishi hao ziweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la Mbogwe alilolisema, nadhani wiki iliyopita nilikuwa natoa tathmini ya Halmashauri mbalimbali mpya zilizopatiwa mgao wa shilingi bilioni mbili, milioni mia moja na arobaini kila moja, zingine zilipatiwa kati ya shilingi milioni mia tano mpaka shilingi milioni mia nane na hamsini na katika mchakato ule Mbogwe ipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kubwa ni nini? Kwa sababu bajeti imeshatengwa, jukumu la Serikali katika mwaka huu wa fedha ni kuhakikisha kwamba tunakusanya mapato ya kutosha kama tunavyofanya sasa ili mradi bajeti tulizozitenga tuweze kuzielekeza maeneo husika ili maeneo hayo ujenzi uweze kufanyika na likiwemo eneo lake la Mbogwe. Kwa hiyo, eneo lake la Mbogwe tumelishalizungumza katika bajeti yetu ya mwaka huu wa fedha.
AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kumuuliza Naibu Waziri maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mapori ya akiba mengi yamegawanywa kwa leseni za uwindaji na uwindaji huu umekuwa unachangia katika kupunguza wanyama kwa maana ya kwamba wanyama wale wanauawa na ipo siku wanyama hawa wanaweza wakatoweka kabisa. Je, Serikali ina mpango gani wa kulitenga Pori la Akiba la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ili wale wanyama ambao wamekuwa wakipunguzwa sehemu nyingine wawe wanapata eneo ambalo watapata ulinzi wazaliane na kuongezeka ili waweze kusogea tena sehemu zile ambapo kuna leseni za uwindaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia Pori la Akiba ya Selous ipo Udzungwa National Park, ukienda Ruaha kuna Ruaha National Park na kuna Ruaha Game Reserve. Kwa maana hiyo, mimi nilikuwa nashauri kwamba ikiwezekana haya Mapori ya Kigosi/Moyowosi iwepo na sehemu nyingine ambayo itakuwa ni Hifadhi ya Taifa ambapo hawa wanyama watapata nafasi ya kuwa wanakwenda kuzaliana na kwenda kuongezeka kwa wepesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Masele, naomba ufupishe tafadhali, naona swali la kwanza ushauri wako umekuwa mrefu, swali la pili nenda straight kwenye swali.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, katika jibu lake la msingi amesema kwamba kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021, Serikali ina mpango wa kuimarisha miundmbinu. Je, Wizara yake itakuwa tayari sasa kutengeneza ile barabara ya kutoka Masumbwe kuelekea Kifura katika Wilaya ya Kibondo ili kuweza kurahisisha utalii wa ndani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza la utaratibu wa uvunaji na namna ya kuhakikisha kwamba uvunaji huu unakuwa endelevu ili usiathiri idadi ya wanyamapori kwa maana ya kufikia kiwango cha kumaliza baadhi ya aina (species) za wanyamapori, jibu lake ni kwamba utaratibu huo upo na ndiyo utaratibu unaotumika kitaalam. Utaratibu huo unaitwa quota, kwanza kuna aina maalum ya wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa lakini pia kuna idadi maalum ya wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa katika kipindi kinachotajwa kwa mujibu wa kanuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kigosi/ Moyowosi, nimesema kwenye jibu la msingi kwamba tunalo eneo tunafanya utalii wa uwindaji lakini eneo lingine ni kwa ajili ya utalii wa picha. Sasa kule ambako tunafanya utalii wa picha ndiko maeneo ambayo tunatarajia kwamba kwa kutowawinda wanyama basi wataendelea kuzaana kama Mheshimiwa anavyoshauri lakini kwa ujumla ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi vizuri zaidi ili kuweza kuboresha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la barabara aliyoitaja, labda niseme tu kwa ujumla kwamba tunapozungumzia miundombinu hasa miundombinu ya barabara kwa upande wa hifadhi, ziko barabara ambazo zinashughulikiwa moja kwa moja na Wizara ya Maliasili na Utalii na hizi ni zile ambazo ziko ndani ya maeneo ya hifadhi. Ukishatoka nje ya maeneo ya hifadhi unakutana na mfumo wa kawaida wa barabara Kitaifa ambapo utakutana na barabara zinazopaswa kutengezwa na Halmashauri za Wilaya husika lakini pia utakutana na barabara kuu. Miundombinu yote hiyo ni ya muhimu kwa sababu watalii hawawezi kufika kwenye hifadhi bila kusafiri umbali mrefu pengine wanatoka Dar es Salaam na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu kama ya barabara, zile barabara kuu kupitia utaratibu wake wa kawaida wa Kiserikali wa kutengeneza na kuimarisha barabara hizo pamoja na zile za Halmashauri vilevile mpaka utakapofika ndani ya hifadhi. Zile za ndani ya hifadhi tunaendelea kuziboresha taratibu kadri fedha zinavyoweza kupatikana.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona na napenda niulize swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa kikao cha Bodi ya Barabara katika Mkoa wa Geita kiliazimia kuipandisha barabara ya Geita, Mbogwe mpaka Ushirombo kuwa barabara ya TANROAD, ni lini sasa Serikali itakuwa tayari kuipandisha barabara hiyo ili iweze kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Mbogwe na Mkoa mzima wa Geita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa huyu ndiyo unatusukuma, unatufanya tusilale usingizi lakini nadhani unavyofanya ni
kwa manufaa ya wananchi wa Mbogwe. Nikupongeze sana kwa kazi hiyo kubwa unayofanya ya kufuatilia masuala ya watu wako wa Mbogwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Geita, Mbogwe, hadi Ushirombo, kama ambavyo amesema imeombwa na TANROAD Mkoa ichukuliwe na mkoa itoke katika halmashauri. Nadhani utakumbuka nimejibu mara nyingi maswali ya aina hii hapa kwamba maombi yote ya barabara sehemu zote nchini yako zaidi ya 3000 yatafanyiwa kazi kwa pamoja na tutaleta Muswada Bungeni ili tugawane sasa barabara zipi zipande hadhi na zipi zibakie katika halmashauri na tukifanya hivyo lazima tuangalie vilevile na resources; mgawanyo tuliopanga sasa ni kwamba, asilimia 30 iwe halmashauri na asilimia 70 iwe TANROAD.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na hilo nalo tutatakiwa tulipitie ili kadri barabara nyingi tunapozipeleka TANROAD na fedha nyingi nazo tunatakiwa tuzipeleke TANROAD. Namhakikishia hilo litafanyika na Muswada utaletwa hapa Bungeni kwa ajili ya kuzigawanya hizo barabara.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kumuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Kwa kuwa kampuni ya Resolute imekuwa ikifanya utafiti kwa muda mrefu ni lini sasa Serikali itaitaka kampuni hii iweze kufungua mgodi kwa ajili ya manufaa ya Wilaya hii ya Mbogwe?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, yapo mazungumzo baina ya Serikali pamoja na kampuni yanayoendelea kuhakikisha kwamba kampuni hii inaachia eneo la Kanegere ili kusudi wananchi waweze kupata maeneo ya kuchimba dhahabu. Ni lini sasa Mheshimiwa Naibu Waziri atatembelea Mbogwe kuweza kuhakikisha kwamba jambo hili linaafikiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kampuni ya Resolute imekuwa ikifanya utafiti kwa muda mrefu na sasa hivi shughuli za utafiti kimsingi zimekamilika na hatua inayofata sasa ni kufungua mgodi. Kulingana sasa na taratibu za ufunguaji mgodi kampuni iko tayari kuanza kufungua mgodi miezi sita ijayo kutegemea sasa na bei ya soko la dhahabu pamoja na upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kutembelea eneo, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Masele anavyowatafutia maeneo wachimbaji wadogo. Hivi sasa katika eneo la jimbo la Mbogwe, Wizara imeshatenga maeneo yanayoitwa Shenda Kaskazini ambayo yana ukubwa wa hekta 990.99 na eneo hilo litapatiwa leseni 100 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa Mbogwe.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hatua hiyo bado Wizara pia imezungumza na mwekezaji na kupata eneo lingine la Kanegere namba mbili ambalo litakuwa na ukubwa wa hekta 177 ambazo pia zitapatikana leseni 18.
Lakini kadhalika eneo la Bukandwe ambalo Mheshimiwa amelizungumzia pia kampuni imeachia eneo la ukubwa wa hekta 300 ambapo pia zinapatikana leseni kama 10.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Masele nimshukuru sana kwamba, wachimbaji wake watapata maeneo mengi na nitatembelea huko mara baada ya Bunge hili kuahirishwa.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali hata hivyo nina maswali
mawili kama ifuatavyo:-
(a) Serikali kupitia kwa Naibu Waziri imekiri kwamba ni asilimia 23 tu ya zoezi zima la ujenzi wa nyumba za Wakuu
wa Wilaya na Mikoa ndizo zilizokuwa zimetekelezwa. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba hizi nyumba zinakamilika kwa wakati katika mwaka wa fedha ujao?
(b) Je, Serikali imepanga kiasi gani cha fedha kwa Wilaya ya Mbogwe katika mwaka ujao wa fedha? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika
jibu la swali la msingi kwamba kuna kiwango cha fedha ambazo TBA wanahitaji kuzipata ili waweze kukamilisha zoezi hili la ujenzi. Naomba tu kama nilivyosema kwamba fedha zimetengwa katika mwaka huu wa 2017/2018 na niombe radhi sina kile kiwango kamili kilichotengwa chini ya TAMISEMI tutaweza kukupa hizo taarifa baadaye baada ya kuwasiliana na watu wa TAMISEMI kujua kiasi gani kimetengwa. Lakini nina uhakika na nimepata taarifa kutoka TBA kwamba mwaka huu wa fedha unaokuja wanaanza kujenga nyumba hizo hadi kuzikamilisha kwa sababu wameahidiwa kupata fedha zilizobakia zote.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri sana ambayo imefanyika katika Jimbo la Mbogwe la kusambaza umeme maeneo mengi. Sasa naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme katika Kata Nyasato, Bunigonzi na Vijiji vyote vya Jimbo la Mbogwe ambavyo bado havijapa huduma hii ya umeme?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini sasa mradi wa REA awamu ya tatu utaanza katika Mkoa wa Geita na Wilaya ya Mbogwe in particular? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Masele kwa sababu ameshughulikia sana masuala ya umeme katika jimbo lake ambapo kati ya vijiji 72, vijiji 44 vyote vimeshapatiwa umeme. Hongera sana Mheshimiwa Masele.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie vijiji vyote vilivyobaki, ameuliza suala la msingi sana ni lini sasa umeme utapelekwa katika Kata za Nyasato pamoja na Budigonzi. Nimhakikishie Mheshimiwa Masele kwa niaba ya wananchi wa Mbogwe, ni vijiji vyote 28 sasa tunavipelekea, Vijiji hivyo ni pamoja na Budigonzi, Buzigozigo, Mtakuja, Budura pamoja na maeneo mengine ya Kashenda na Nyashimba, yote yatapelekewa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tunazindua Mkoa wa Geita? Nipende kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba tumeanza kuzindua utekelezaji wa mradi wa awamu ya tatu tangu tarehe 24 mwezi huu na tumeanza na Mkoa wa Manyara. Katika Mkoa wa Manyara tumefanya katika Jimbo la Babati na mengine. Tarehe saba na nane tunazindua katika Mkoa wa Kagera, tutakwenda katika Wilaya ya Karagwe. Tarehe 10 tutazindua katika Mkoa wa Geita Mheshimiwa Mbunge; na maeneo ya kuzindua ni maeneo ya Nyangh’wale pamoja na maeneo ya Mbogwe. Kwa hiyo niwahakikishie wananchi wa Mbogwe, wananchi wa Mkoa wa Geita na Wabunge wote wa Mkoa wa Geita basi tushirikiane wote tarehe 8 na 10 tutakapokuwa tunazindua katika Mkoa wa Geita.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kumuuliza swali Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwanza, kwa sababu Kampuni ya Resolute imeamua kuachia leseni zake tisa, je, Serikali itakuwa tayari sasa kuzigawa hizo sasa leseni kwa wachimbaji wadogo Wilayani Mbogwe ili waweze kunufaika na dhahabu iliyopo katika eneo hilo? (Makofi)
Swali la pili, dawa ya deni ni kulipa. Kampuni hii ya Resolute inadaiwa sasa shilingi bilioni 143 na Serikali. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba deni hili linalipwa kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Masele nakupongeza sana, najua juhudi zako na wananchi wako wanatambua jinsi unavyoshughulikia maslahi ya wananchi hasa wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kweli kabisa tumejadiliana sana na kampuni hii, kampuni hii ina leseni 22 na maeneo mengi haiyafanyii kazi, kwa hiyo tumekubaliana na Kampuni hiyo sasa imeamua kuya-surrender maeneo tisa na maeneo hayo tunagawa sasa kwa wananchi wa Mbogwe, Mheshimiwa Mbunge ninakushauri sana sasa wananchi wako waanze kuunda vikundi ili sasa waweze kurasimishwa, mpango wa kuwagawia ifikapo mwezi wa Julai na Agosti, tutawamilikisha rasmi.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na deni, ni kweli kabisa dawa ya deni ni kulipa. Kampuni hii imekuwa ikidaiwa shilingi bilioni 143.007 na kwa sababu ilitaka kuhamisha umiliki wake sisi Serikali tulikataa mpaka deni litakapolipwa.
Mheshimiwa Spika, sasa hatua inayofanyika wamekubaliana na TRA na Kampuni imekubali kulipa, kwa hiyo kuja kufika mwezi wa Julai, kampuni imeahidi kulipa deni hilo. Baada ya kulipa sasa taratibu za umilikishaji zitaendelea rasmi.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hiki kitalu kimetolewa kwa ajili mambo ya utafiti wa madini lakini kwa mujibu wa Sheria Na. 5 ya mwaka 2009 ya Wanyamapori inazuia kufanyika kwa utafiti katika maeneo ya hifadhi. Je, ni taratibu zipi ambazo Serikali imetumia kukigawa hiki kitalu ili kifanyiwe mambo ya utafiti wakati sheria hairuhusu?
Swali la pili, kwa kuwa mapori haya yana changamoto mbalimbali, je, Naibu Waziri atakuwa tayari kuambatana na mimi pindi Bunge litakapomaliza shughuli zake ili aweze kuja kuziona hizo changamoto zinazoyakabili haya mapori na kuweza kuzitatua?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mbunge kwa kazi kubwa amekuwa akifanya katika kuwatetea wananchi wake wa Jimbo la Mbogwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TANZAM ambaye alipewa kitalu hicho, kwa mujibu wa Sheria Na. 5 ya mwaka 2009 kifungu cha 20(2)kinazuia kabisa shughuli zote za utafiti wa madini ya aina zote kufanyika katika maeneo ya hifadhi. Hata hivyo, kifungu hicho cha 20(3)kinatoa mamlaka kwamba ni aina tatu tu za madini zinaruhusiwa kufanyiwa utafiti, madini hayo ni uranium, gesi na mafuta. Kufuatana na mwekezaji aliyekuwa amepewa hiki kitalu yeye alikuwa anafanya utafiti wa madini ya dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba pamoja na leseni ya huyu mwekezaji ilimalizika tereha 31 Desember 2014, baada ya kumalizika, tarehe 1 Juni, 2016 Serikali ilimuandikia barua ya kumuomba aondoke katika eneo na aondoe vitu vyote lakini hadi leo bado mwekezaji yule yupo opale na ameweka vifaa vyake wakati hana leseni na ilishapita. Tarehe 28 Aprili, 2017 alikumbushwa juu ya suala hili na mpaka sasa hivi bado hajasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kutoa siku saba, yule mwekezaji aondoe hivyo vitu vyote, kwa sababu viko pale kinyume na taratibu na sheria iliyopo. (Makofi)
Baada ya kumalizika, tarehe 1 Juni, 2016 Serikali ilimuandikia barua ya kumuomba aondoke katika eneo na aondoe vitu vyote lakini hadi leo bado mwekezaji yule yupo opale na ameweka vifaa vyake wakati hana leseni na ilishapita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 28 Aprili, 2017 alikumbushwa juu ya hili suala na mpaka sasa hivi bado hajasema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kutoa siku saba, yule mwekezaji aondoe hivyo vitu vyote kwa sababu viko pale kinyume na taratibu na Sheria iliyopo. (Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwanza naipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuongeza pesa katika Sekta ya Afya na kuwezesha ujenzi huu na upanuzi wa vituo viwili hivi vya Iboya na Masumbwe. Je, Serikali sasa itakuwa tayari kuruhusu bajeti ya mwaka huu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe uanze baada ya mwaka huu kuiondoa hiyo bajeti kutokana na ukomo wa bajeti kwa maana ya ceiling. Ceiling ili-burst kwa hiyo, ile hela ambayo tulikuwa tumepanga kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya iliondolewa. Je, Mwaka huu wa Fedha itaruhusiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, yamekuwepo madai ya muda mrefu ya watumishi ya uhamisho kutoka katika Wilaya mama ya Bukombe kuja Wilaya ya Mbogwe wakiwemo Watumishi wa Idara ya Afya hawajalipwa. Je, malipo haya yatafanyika lini ili kuondoa usumbufu kwa watumishi hawa ambao wamekuwa wakidai kwa muda mrefu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa niaba ya Serikali tunazipokea pongezi zake za dhati maana yeye mwenyewe anakiri kwamba vituo viwili kwanza kujengwa kwa milioni 400, jumla milioni 800 siyo haba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kujua je, Serikali itaruhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya baada ya kwamba haikuwezekana kutokana na ufinyu wa bajeti. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote Wilaya zote 64 na jana nilijibu, ambazo hatuna Hospitali za Wilaya, hospitali zinajengwa. Ninachoomba kwa kupitia Halmashauri yake ni vizuri wakatenga eneo na wao wakaanza ujenzi ili Serikali ije kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anauliza kuhusiana na suala la kuwalipa Watumishi ambao walihamishwa kutoka maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wilayani kwake, lini watalipwa. Mara baada ya uhakiki kukamilika na Mheshimiwa Rais alilisema, kati ya madeni ambayo yanatakiwa kulipwa ni pamoja na madeni ya Walimu pamoja na Watumishi wa Afya. Zoezi hili litakamilika muda si mrefu.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwanza naipongeza Serikali kwa kuhakikisha kwamba miradi ya Kayenze, Kakora, Ikangala, Nyamtukuza na Kharumwa inakamilika, hongera sana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Sasa napenda kuuliza, je, Serikali inaweza ikawaambia watu wa Nyang’hwale ni lini sasa huu mradi mkubwa wa vijiji tisa utakamilika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Mbogwe ipo jirani kabisa na Wilaya ya Kahama ambako kuna mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria, je, Serikali haioni kwamba ni wakati sasa umefika kuiweka Wilaya yetu ya Mbogwe katika programu ya kuweza kupata maji haya kutoka Kahama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tuwahakikishie wananchi kwamba mradi huu utakamilika. Mradi huu wa Nyang’hwale umepata shida kidogo ya kiutendaji na shida yenyewe ni kwamba Halmashauri ilitafuta mkandarasi mwingine wa kuleta mabomba na mkandarasi mwingine wa kujenga. Sasa yule mkandarasi wa kujenga hawezi kufanya kazi kama wa kuleta mabomba hajaleta na yule wa kuleta mabomba inaonekana kwamba ni kama kidogo yupo dhaifu kwa sababu hadi leo hajaleta mabomba na mkataba ni wa tangu mwaka 2014 mwezi wa pili. Hivi tunavyoongea sasa hivi ni kwamba tayari yapo mazungumzo kati ya Wizara yangu na Halmashauri ya Nyang’hwale kuhusiana na huyu mkandarasi ambaye ameshindwa kutekeleza majukumu yake na mkataba wake ulikuwa ni wa shilingi bilioni tano. Yule mkandarasi wa kujenga tayari ameshakamilisha matenki, anachosubiri ni mabomba aweze kuyalaza ili wananchi wapate maji.
Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Mbunge tunalishughulikia na mara tutakapomaliza nitakupatia majibu ili wananchi sasa waweze kuwa na uhakika ni lini hayo maji yatapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Mbogwe, kwa sasa tunaendelea, tayari kuna visima ambavyo tumechimba na kwa sasa Halmashauri imesaini mkataba wa visima sita ili tunaposubiri mradi mkubwa na kwa kuwa Geita ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata msaada wa hizi fedha kutoka Serikali ya India, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia fedha hiyo basi tutaendelea kuhakikisha pia na Mbogwe inapata maji kutoka Ziwa Victoria.
Pia unayo fursa nyingine kupitia bomba la Lake Victoria linalokwenda Solwa, napo tayari tunaanza kuangalia kama tunaweza tukachukua maji kutoka Kahama pale kwenda kwenye ile milima kilometa 40 na baadaye tukayashusha kwenda Mbogwe. Wataalam wanafanyia kazi kama hilo litakuwa limekaa vizuri basi pia unaweza ukapata maji kutoka bomba la KASHWASA. (Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa nimuulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tatizo kubwa hapa ni uhaba wa wataalam. Naomba kujua sasa Serikali itatupatia lini wataalam wa kuweza kutusaidia katika kurahisisha ukamilishaji wa hii miradi ya maji inayoendelea huko Mbogwe? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, naomba sasa kujua time frame, ni lini miradi hii itakamilishwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowatetea wananchi wake lakini kikubwa maji hayana mbadala na uhitaji wa maji ni mkubwa sana. Sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo, kubwa nimwombe Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane ili tuwape watalaam wetu wa Wizara waweze kumsaidia katika kuhakikisha wananchi wake wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala zima la fedha na ni lini miradi hii itakamilika, kikubwa nimwombe sasa Mhandisi wa Maji katika Jimbo lake ahakikishe kwamba anatengeneza certificate ili sisi kama Wizara tutawalipa kwa wakati ili wananchi wake waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa eneo hili la Nyakafuru limekuwa chini ya utafiti kwa muda mrefu na tayari wachimbaji wadogo wameshalivamia. Je, Serikali iko tayari sasa kuwamilikisha wachimbaji hao wadogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, eneo pia la Nakanegere Mlimani nalo limekuwa chini ya utafiti kwa muda mrefu. Serikali inasemaje juu ya uwezekano wa kuwapatia wananchi kuchimba kwa leseni za wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuwamilikisha wananchi kwenye eneo hilo, nieleze tu kwamba Mheshimiwa Mbunge anafahamu wananchi wa Nyakafuru ndiyo wao wako pale wanaendelea na shughuli. Kwa kuwa wanaendelea na shughuli pale na kwa maelekezo tuliyopewa kazi yetu ni kuwasaidia wachimbaji wadogo, wale ambao hawako rasmi tuwarasimishe ili waweze kupata vibali halisi waweze kuchimba kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo la Nakanegere, eneo hili lote linamilikiwa na kampuni moja na lenyewe utaratibu wake utakuwa kama ule wa Nyakafuru.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, Wilaya ya Mbogwe pamoja na Mikoa ya Kanda ya Ziwa tuna matatizo makubwa sana ya huduma za afya, matokeo yake wananchi walio wengi wanategemea sana huduma za waganga wa jadi na huko wakati mwingine wanapata uchonganishi na kuuana. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kuwajengea wananchi wa Mbogwe Hospitali yao ya Wilaya? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na kuipongeza Serikali kutupatia shilingi milioni 800 kwa ajili ya vituo vya Afya vya Iboya na Masumbwe. Je, Serikali iko tayari sasa kutupatia wataalam zaidi pamoja na vifaatiba? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Mikoa ya Kanda ya Ziwa pale ambapo huduma ya hospitali inakosekana wamekuwa wakitumia tiba mbadala na kwa Mheshimiwa Mbunge imekuwa ni jambo la kawaida. Hata hivyo, sasa hivi tangu Serikali kwa kushirikiana na wananchi wameanza zimeanza kujengwa zahanati pamoja na vituo vya afya, naamini mentality imeenda iki-change.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilienda Jimbo la Itilima kwa Mheshimiwa Silanga nikakuta kuna zahanati nyingi sana ambazo zimejengwa kwa kushirikisha wananchi na mwitikio ni mkubwa sana. Naomba hiyo kazi nzuri ambayo wameanza wenzetu wa kule ni vizuri na Mheshimiwa Mbogwe na yeye akaiga mfano mzuri ili wananchi wetu wahame katika tiba mbadala ambayo imekuwa ikisababisha mpaka watu kuuana kwa sababu ya masuala mazima ya kupiga ramli.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili juu ya suala zima la kupeleka wataalam, naomba nimhakikishie kwamba baada ya mchakato kukamilika wameajiriwa wataalam hakika na yeye mwenyewe anakiri kwamba tumempelekea vituo viwili vya afya. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba na wataalam wanapelekwa ili vituo vya afya vifanye kazi iliyokusudiwa.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana. Kwanza niishukuru Serikali kwa kutengeneza hilo greda ambalo sasa kwa kweli litasaidia sana katika utengenezaji wa barabara kule kwenye Mapori yetu ya Akiba ya Kigosi Moyowosi. Sasa niombe kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia mapori haya ya akiba pesa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya barabara katika mwaka ujao wa fedha ujao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa kuwa gari la Grand Tiger sasa hivi limeharibika na mapori haya mawili ni makubwa sana, je, Serikali iko tayari sasa kuyapatia haya mapori magari mawili kwa ajili ya kufanya doria na utawala katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa kazi kubwa ambayo umekuwa ukiifanya. Nakumbuka mwaka jana swali hilihili aliuliza na amekuwa akilifuatilia kwa karibu sana, hongera sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu tumeshalitengeneza lile greda sasa hivi tumeshatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kukarabati na kutengeneza miundombinu mbalimbali katika ile hifadhi. Kwa hiyo, pale bajeti itakapowasilishwa ataona ni kiasi gani tutakuwa tumetenga katika hilo eneo kwa ajili ya kufanya hiyo kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusu maombi ya gari; ni kweli kabisa hili gari ambalo nimesema kwamba tunaendelea kulitengeneza bado lina changamoto na tutalifufua. Lakini kwa nyongeza zaidi naomba nikuahidi kwamba tutakuongezea gari lingine moja ili yakiwa hayo mawili basi yataweza kufanya kazi nzuri sana katika hilo eneo. (Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Wilaya yetu ya Mbogwe kuna madini ya dhahabu na kumekuwa na mgogoro kati ya wananchi wa Nyakafuru pamoja na wawekezaji ambao wamekuja hapo. Sasa ninataka kujua msimamo wa Wizara uko vipi katika kuhakikisha kwamba leseni inatolewa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wanaochimba Nyakafuru wanachimba chini ya leseni ya mtu mwingine, wanachimba bila kuwa na leseni, ni kama vile wachimbaji waliovamia leseni ya mtu mwingine. Sisi kama Wizara hatuchochei wachimbaji wadogo kwenda kuvamia leseni ya mtu mwingine, huo siyo utaratibu. Lakini sisi kama Wizara ya Madini tuna mpango na mkakati wa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Spika, tuna maeneo zaidi ya 44, tuna heka zaidi ya 238,000 kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tunaomba ushirikiane na wananchi wako kwa kuwapa elimu ya kutosha kwamba tunakwenda kuwagawia maeneo ambayo ni halali, wachimbaji wadogo wachimbe kwa uhalali ili waweze kujipatia kipato chao, lakini wasiendelee kuvamia leseni za watu wengine. Ahsante.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Hadi sasa Wilaya ya Mbogwe ni vijiji 28 tu ambavyo tayari vina umeme na REA awamu ya tatu inajumuisha vijiji 28 pia. Sasa hapa nataka kuuliza Serikali kama vile vijiji vya REA awamu ya tatu na vyenyewe vitahusishwa katika hii Densification?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, vijiji 31 haviko kabisa katika mpango wa REA awamu ya tatu: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba vijiji 31 vya Wilaya ya Mbogwe ambavyo havijapata umeme vinapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali ya nyogeza ya Mheshimiwa Masele. Maswali yake mawili yalijielekeza kwanza kwenye mradi unaendelea wa REA awamu ya tatu katika vijiji 28. Alikuwa anauliza je, huu mradi wa ujazilizi utafika katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaja kwamba katika Jimbo lake kuna vijiji 28 vina umeme na anaamini katika vijiji hivyo vipo Vitongoji ambavyo havikuguswa katika miradi ya REA awamu ya kwanza na awamu ya pili. Kwa hiyo, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi wa ujazilizi utaelekea kwenye maeneo yale ya vijiji 28 ambapo kuna Vitongoji havikufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameulizia vijiji 31 katika Jimbo lake ambavyo havina umeme. Nataka nilitaarifu Bunge lako Tukufu na wananchi wa Jimbo la Mbogwe ambapo Mheshimiwa Mbunge anafanyia kazi nzuri kwamba vijiji 31 vitaingia kwenye mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili na sasa kazi hiyo imeanza na ameshapokea hiyo orodha na mchakato unaendelea na mradi huu unatarajia kuanza mwezi Julai, 2019 ahsante.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba Wilaya ya Mbogwe ni Wilaya mpya na katika Mkoa wa Geita, ni Wilaya pekee ambayo kwa kweli ina watumishi wachache sana wa Idara ya Afya: Je, Serikali ina mpango gani wa kutuongezea watumishi hao?

Swali la pili ni kwamba Serikali imejitahidi kutupatia vituo viwili vya afya na huduma mojawapo ni ya mortuary; lakini kuna shida ya mortuary cabinets, yale mafriji ya kuhifadhia maiti hayajaletwa na watu MSD. Sasa Serikali ina mpango gani kupitia MSD kutuletea hiyo huduma mara moja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza Mheshimiwa Masele anaongelea upungufu wa watumishi wa Kada ya Afya katika Wilaya yake ambayo ni miongoni mwa Wilaya mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika na wewe umekuwa shuhuda kwamba wakati mwingi zinapoanzishwa Halmashauri mpya kumekuwa na nakutopata watumishi wa kutosha. Kwa hiyo, naomba kwanza niagize Ofisi ya RAS wahakikishe kwanza ndani ya Mkoa watazame ikama ilivyo ili katika maeneo ambayo yana upungufu mkubwa kama eneo la Mheshimiwa Mbunge waweze ku-balance.

Mheshimiwa Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati nafasi nyingine zikitoka kwa ajili ya kuajiri, tutahakikisha kwamba tunazingatia maeneo yenye upungufu ikiwa ni pamoja na eneo lake kuwapeleka watumishi wale.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni juu ya kupatikana kwa friji kwa ajili ya kutunza maiti. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azima ya Serikali kuhakikisha maeneo yote ambayo mortuary zimejengwa, friji zinapelekwa. Naomba tuwasilaine na Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi cha maswali na majibu ili tujue MSD lini watapeleka hayo masanduku.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo :-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kuwa uharibifu wa mazingira umekuwa ni mkubwa sana katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa pamoja na Mkoa wa Geita kwa maana ya kwamba hifadhi za misitu zinatoweka kwa haraka sana kwa mfano Hifadhi ya Msitu ya Geita, Rwamgasa, Rwande na Miyenze inatoweka kwa haraka. Sasa je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuweza kudhibiti hali ya uharibifu wa mazingira na utowekaji wa misitu unaofanyika kwa sasa katika mkoa huo wa Geita.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe haina maafisa wanyamapori, je, Serikali ipo tayari sasa kutupatia maafisa wanyamapori ili huduma yao iweze kuonekana kwa wananchi wa Wilaya ya Mbogwe, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amekuwa akiwasiliana na mimi kuhusu uharibifu wa misitu aliyoitaja; Misitu ya Rwamgasa na Rwande ambayo kwa ujumla imevamiwa sana na wachimbaji wadogowadogo na wakataji wa kuni na mkaa lakini tumeshirikiana nae kutoa maelekezo ili kuilinda. Kwa hiyo, naomba nimpongeze sana kwa juhudi hizo ambazo ameendelea kuzionesha.

Mheshimiwa Spika, uharibifu wa misitu ambao unaendelea karibu nchi nzima ni tatizo ambalo ningependa kulitolea maelekezo. Imekuwepo tabia ya Halmashauri nyingi kufikiri jukumu la kulinda misitu ni la TFS au Wizara lakini misitu hii mingi ipo kwenye maeneo ya Halmashauri na mingi ni misitu ya vijiji na Halmashauri na misitu michache inayosimamiwa na TFS inalinda vizuri. Kwa hiyo, nizielekeze tu Halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinashirikiana vizuri na maafisa wetu wa TFS kulinda na kudhibiti wanaoharibu misitu hii kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili la nyongeza amesema Halmashauri ya Mbogwe haina afisa wa wanyamapori. Na naomba tu nitumie nafasi hii pia kuwaambia Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kwamba katika maombi yao ya watumishi tunawaelekeza Halmashauri zote ambazo zinapakana na hifadhi ambazo zimekuwa na historia ya migogoro ya wanyama na binadamu kuhakikisha kwamba wanaomba kuwa na maafisa wa wanyamapori katika halmashauri hizo kwa sababu hawa ni watu wa kwanza ku-respond na matukio ya wanyama waharibifu wanaoenda kwenye maeneo ya makazi ya watu.

Kwa hiyo, naelekeza halmashauri hiyo katika maombi yao ya watumishi ya mwaka huu waweze kuomba afisa wa wanyamapori.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ni kwamba, mkandarasi wa Awamu hii ya III wa REA katika Mkoa wa Geita anaonekana anaenda anasuasua katika utekelezaji wake. Sasa ni nini hatua zinazochukuliwa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba, maeneo ya utekelezaji wa mradi huu REA III unakamilika kwa mujibu wa ratiba?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Wilaya ya Mbogwe kuna vijiji vilivyoachwa kwenye Awamu hii ya REA Phase III ikiwemo Kata Mpya ya Bonigonzi. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, vijiji vyote vya Wilaya ya Mbogwe vinapatiwa nishati hii ya umeme? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Masele, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya mzingi:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Masele katika kuliza swali la msingi. Kwanza ni kweli Jimbo la Mbogwe lina vijiji 86 na kati ya vijiji hivyo ni vijiji 23 havijapata umeme, ikiwemo Kata Mpya ya Bonigonze. Lakini pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Masele na ufuatiliaji wake Kata Mpya ya Nyabunigonza ambayo inapitia Kijiji cha Lunguya kwenda Kijiji cha Chibutwe, umbali wa kilomate mbili na iko katikati imeshaanza kushushiwa umeme tangu jana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba, kata nzima na vijiji vyake vitano itapelekewa umeme kuanzia mwezi huu hadi mwezi Septemba mwaka huu.

Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, nimefuatilia kazi hizi na kumpongeza sana kwenye wilaya yake itabakiza vijiji vitano ambavyo tunaanza kuvipelekea umeme kuanzia mwezi ujao na vitakamilika mwezi Disemba mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini mkandarasi, White City, atamaliza kazi katika Mkoa mzima wa Geita:-

Mheshimiwa Spika, kwanza mkandarasi huyu ameshafikia average ya asilimia 52 na muda wake wa kumaliza kazi kimsingi ni mwezi Juni mwakani, lakini tunamtaka amalize kazi mwezi Disemba mwaka huu, ilibaki kazi ndogondogo za kuunga wateja, hasa ambao watachelewa kulipa. Kwa hiyo, nimpe taarifa na kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maendeleo ya mkandarasi katika Mkoa mzima wa Geita, lakini nimhakikishie kwamba, utakamilika ndani ya muda. (Makofi)
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Naibu Spika,asante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba leseni ya utafiti ya hao watu wa Mabangu imeisha muda wake na imerudishwa Serikalini. Sasa je, Serikali ipo tayari kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Mbogwe ili kusudi na wao waweze kufaidika na madini yanayopatikana katika eneo lao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, endapo Serikali itakuwa tayari kugawa hayo maeneo, je, Serikali itakuwa tayari pia kuwapatia vifaa na utaalam ili wananchi waweze kuchimba kwa kufuata kanuni na taratibu za uchimbaji wa kisasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunavyoongea sasa hivi ni kwamba tayari kuna wachimbaji wadogo wapo katika leseni hiyo wanachimba na Mheshimiwa Mbunge hilo unalifahamu. Lakini tu nipende kusema kwamba kampuni hii iliomba leseni ya kufanya utafiti na wamefanya utafiti na kawaida mtu ukimpa leseni ya kufanya utafiti, hatua inayofuata kama ameridhika na utafiti huo na akaona kwamba anaweza akafanya biashara au kwa maana anaweza akachimba kibiashara, katika hali ya kawaida ni kwamba akishafanya upembuzi yakinifu, anaomba tunampatia leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu leseni hiyo imesharudishwa Serikalini na tunadhani kwamba huyu mwekezaji atakuja na maombi yake sasa baada ya kufanya upembuzi yakinifu, hatuoni haja ya kumnyima leseni hiyo kwa sababu tayari ameshaingia gharama ya kufanya upembuzi yakinifu. Lakini kama atasema kwamba hakuna biashara, haiwezekani akachimba kibiashara, basi sisi Serikali hatusiti na tumekwishakuanza kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo mbalimbali ili waweze kuendesha shughuli zao na hilo tunalifanya kwa kweli na wachimbaji wengi wamepata maeneo mengi ya kuchimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, Mbunge ametaka kujua kama Serikali tukishawapa hilo eneo basi na vifaa tutawapa? Mimi nipende tu kusema kwamba Wizara yetu hapo awali ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo ili waweze kununua vifaa, kufanya tafiti, lakini vilevile katika ruzuku hiyo tuliona kabisa kulikuwa kuna ubadhilifu unafanyika, watu walikuwa wakipewa fedha hizo wanazitumia katika matumizi mengine, tumesitisha na sasa hivi tunaangalia namna bora ya kuwasaidia wachimbaji wadogo, lakini ikiwa ni pamoja na kuwafanyia tafiti ndogo ndogo kwa maana ya kufanya drilling kwenye maeneo ambayo yanaashiria uwepo wa dhahabu. Tumeshanunua rig machine kupitia STAMICO imekwisha kuanza kutoa huduma hiyo kwa wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kama ana wachimbaji wadogo ambao wanataka kupata huduma ya hiyo rig machine basi aje STAMICO anaweza akapata huduma hiyo.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa uendeshaji wa mashauri yaliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bukombe kutokea Wilaya ya Mbogwe yanakuwa yakikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mashahidi kutofika kutoa ushahidi kutokana na umbali, je, Serikali inaonaje ikianzisha Chamber Court Wilayani Mbogwe ili kukabiliana na changamoto hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Masumbwe na Ilolangulu na kuifanyia ukarabati Mahakama ya Mwanzo Mbogwe?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama yalivyo majibu yangu kwenye swali la msingi, ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya 33 nchini umepangwa kukamilika ndani ya miezi sita, kuanzia mwezi Juni na kukamilika mwezi Disemba, 2020. Hivyo, naendelea kumwomba Mheshimiwa Mbunge kuwa na uvumilivu ili jengo hili likamilike ambalo litatatua changamoto alizozitaja kwenye swali lake la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania imejiwekea Mpango wa kujenga na kukarabati majengo ya Mahakama kwa awamu. Aidha, Ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo katika Tarafa za Masumbwe na Ilolangulu utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Ujenzi wa Majengo ya Mahakama 33 za Wilaya nchini utajumuisha Mahakama za Mwanzo katika jengo moja. Kwa mpango huo, Mahakama ya Mwanzo Mbogwe itakuwa ni sehemu ya Jengo la Mahakama ya Wilaya Mbogwe.