Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Khatib Said Haji (14 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nianze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kunijalia leo kusimama hapa nikiwa na afya njema. Pili, niwashukuru kwa dhati sana wananchi wa Jimbo la Konde kwa kunirejesha tena hapa ili niweze kuwawakilisha.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, kwa umuhimu mkubwa sana natoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar kwa maamuzi mema na ya dhati ya kumchagua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar. Suala la Jecha kasema nini, Mwenyezi Mungu ataisimamisha haki hapa duniani na watu wote wataona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ilikuwa ni bashrafu, sasa nataka nianze kuchangia. Ukurasa wa nane wa hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyeitoa hapa alisema, naomba ninukuu:- “Eneo lingine linalolalamikiwa ni Polisi. Kuna malalamiko mengi ya wananchi
kubambikiwa kesi, upendeleo, madai ya Askari kutotimizwa, ukosefu wa nyumba za Maaskari na kadhalika”.
Mheshimiwa Naibu Spika, malalamiko ya raia wa nchi hii juu ya Polisi ni mengi sana. Wakati mwingine tunaweza kuwalaumu Polisi wakati amri hizi wanazozitekeleza Polisi zinatoka kwa viongozi wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uchaguzi mkuu ilitoka amri ya Kiongozi Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu akiwaambia ni marufuku vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara hasa kwa wale waliokuwa hawakushinda. Kiujumla tangazo lile lilihusu kutubana sisi vyama vya
upinzani kuonana na wananchi wetu kuwaeleza ukweli juu ya yaliyotokea katika uchaguzi mkuu, hii siyo sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa Katiba. Tunapoapa hapa kabla ya kuanza kazi hizi tunaapa kuilinda, kuitetea na kuiheshimu Katiba hii. Leo unapokurupuka na amri zako zilizo kinyume na Katiba hii, wewe ndiyo unayesababisha fujo, tukubaliane! Kuna mambo tunayoinishiwa kama vyama vya siasa kwa mujibu wa Katiba tuna haja ya kuyatenda. Hatulazimiki kuomba vibali kwa Polisi tunapotaka kufanya mikutano yetu ya hadhara, tunalazimika kutoa taarifa, leo imepotea hii na badala yake twende tupige magoti
kwao wao ni nani? Hilo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ukurasa wa kumi wa hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la Zanzibar kwa kifupi sana kana kwamba si jambo muhimu sana. Naomba ninukuu sehemu tu:-
“Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM, tutahakikisha majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa usalama kabisa”.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya neno hili alilolisema Rais mpaka leo hii Mheshimiwa Magufuli hajasema tena neno lingine lolote linalohusiana na Zanzibar, hajasema! Ameishia kuwaalika Ikulu baadhi ya viongozi na pale alipokuwa akitoka hakuna lolote alilolizungumza
kuweka njia ya kuonyesha kwamba analichukulia uzito suala la Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nieleze sisi ni wawakilishi wa wananchi. Mimi kabla ya kuja hapa Bungeni nilikutana na wananchi wangu wa Jimbo la Konde na kimoja walichotaka niseme nitakisema hapa bila kujali kwamba litawapendeza au litawakasirisha.
Sikuja hapa kwa mapenzi ya yeyote, nimekuja hapa kwa mapenzi ya Mungu kwa uwakala wa watu wa Konde. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnaposimama mkasema kwamba uchaguzi wa Zanzibar, wengine wamesema hapa, utarudiwa tarehe 20…
MHE. KHATIB SAID HAJI: Tulieni mgangwe maradhi si kitu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tujiulize hao waliosimamia hilo waliapa kutii Katiba wanarudia uchaguzi, Tume ya Uchaguzi, Jecha alipofuta uchaguzi ule alifuta kwa aya ya ngapi ya kanuni na sheria za nchi hii?
MHE. KHATIB SAID HAJI: Akamuulize, nitawauliza ninyi mliomuweka. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, alivunja sheria za nchi, mtu anayestahiki kuweko gerezani, Magufuli anakwenda Zanzibar kwenye sherehe za Mapinduzi anakaa ubavuni kwake, anatujojea Wazanzibari. Tunasema haki itasimama kuwa haki hata mfanye nini hamtaipinga.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, anayepigwa, anayedungwa sindano kila mmoja anahisi maumivu anayopata mdungwa sindano lakini tako linalodungwa sindano ndiyo linaloathirika zaidi na maumivu ya sindano hiyo.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, mambo ya Zanzibar yanachukuliwa kiutani, mnalifanyia jambo hili utani ndugu zangu. Ni wajibu tujue kwa mfano Jimbo langu la Konde uchaguzi uliopita CCM mlipata kura 700 mwaka huu mmepata kura 500.
Kwa mujibu wa sensa Jimbo lenye wananchi 50,000, CCM wako mia tano. Leo mnapofanya masihara ya kusema kwamba uchaguzi unarudiwa, kwa wana CCM 500 walioko kwenye Jimbo la Konde mnatutakia amani kweli ninyi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliangalia jambo hili kwa ujumla wake. CCM katika Kisiwa cha Pemba hakuna, vurugu ikianza wale watu hata tukisema nyumba kumi zizunguke nyumba moja, haiwezekani hawatafika popote. Msiweke mazingira ya kuitia nchi ile kwenye joto la uhasama na uuwaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu Nyerere aliwahi kunukuliwa katika miaka ya sitini akiwa Marekani au Uingereza, akisema kwamba: “Laiti angekuwa na uwezo angevihamisha visiwa vile vya Zanzibar vikawa mbali na Bahari ya Hindi kwa sababu anahisi vitakuja kutuletea
shida hapo baadaye”. Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo halikuwezekana. Nawauliza CCM mliobakia, nia yenu sasa ni kutuua Wazanzibar wote ili lengo lile mlilolikusudia Wazanzibar wasiwepo duniani mlitimize?
Kama lengo si hilo, kwanza kabisa nachukua nafasi hii nikiwa mwakilishi wa wananchi wa Konde na Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuziomba Jumuiya za Kimataifa, walioshuhudia ukweli na uhalali wa kazi waliyoifanya Wazanzibar ya kuchagua Rais
wanayemtaka walisimamie hili kwa nguvu zao wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Watanzania wanahukumiwa kwa kukosa msaada wa mabilioni ya shilingi kwa kuwalinda wahuni wa Zanzibar wasiozidi kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita, kuna Mheshimiwa Mbunge mmoja, alitamka yafuatayo naomba kunukuu, alisema na akamuomba Rais Kikwete, nia yake ya kuiona Zanzibar inabaki na ustawi ni wakati wa utawala wake tu. La pili..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Ole wenu…
SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha, naomba ukae.
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninamshukuru Mungu kunijalia na mimi leo kuwa mchangiaji katika hoja hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu tumekuwa tukipanga mipango kadhaa, waswahili wanasema mpango siyo matumizi, tumekuwa tukipanga lakini hatutumii, ni vema tujiulize tunapokosea ni wapi katika mipango hii, bila shaka kuna makosa tunayoyafanya ambayo yanatupelekea tunapanga vizuri lakini hakuna matokeo mazuri ya mipango yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii katika Mpango kuna jambo zito kubwa sana ambalo linajielekeza kuifanya Tanzania iwe ni nchi ya uchumi wa viwanda. Kusema tumesema sana juu ya hili na siyo mwanzo leo kusema kwamba nchi hii haiwezi kuendelea bila kuwa na mpango madhubuti wa kuendeleza viwanda vyetu. Leo hii yalaiti mimi nataka niseme wazi CCM mmemsaliti Mwalimu Nyerere, mimi siko radhi na Watanzania hawako radhi, mmemsaliti Mwalimu Nyerere kwa nini, kwa sababu Mwalimu Nyerere nchi hii alijitahidi kuwaonesha mfano, kwamba viwanda ndiyo vitakavyotutoa hapa tulipo na kwenda mbele. Matokeo yake mmekuja na sera zenu za ajabu, mmeua viwanda vyote, sasa mnafufua viwanda kwa maneno matupu, neno tupu hakuna utekelezaji unaofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani, ndugu yangu Mheshimiwa Silinde, alizungumzia habari ya kusema lengo la Wachina kujenga pale Kurasini Logistic, ni kuifanya nchi hii kuendelea kuwa madalali, dampo ni kweli! Lakini imekosolewa vikali, hata mimi nataka niseme kwamba Mheshimiwa ndugu yangu Silinde mzoea udalali hawezi kazi ya duka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukubaliane nao hivyo hivyo, kwa sababu tukisema tunakataa Wachina kujenga pale, uwezo wa kujenga viwanda kushnei, hakuna! Tutasema tumekaa humu, tutapita, watakuja na watakaopita, kwa Itikadi hii na utendaji huu wa Sera za Chama cha Mapinduzi, hebu ndugu zangu igeni yale mazuri yetu, ambayo tunawapa mawazo ninyi muyafuate, nchi hii ni yetu wote, nchi hii hakuna kitabu chochote kitakatifu kilichotaja CCM wala CUF wala CHADEMA, vitabu vyote vimewataja waja wa Mwenyezi Mungu atakao waweka sehemu moja aliyopenda yeye, tumejichagulia majina tumejiita Watanzania, wa Afrika katika dunia hii, lakini hakuna hilo andiko liko wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposhauri tuna malengo mazuri, nataka kusema kwamba ndugu zangu, tufuateni yale mawazo bila kujali anayeyatoa ni nani. Lile zuri na wewe Mheshimiwa Naibu Spika nimesikia huko, Bwana Mkubwa kamtumbua Wilson Kabwe, jamani tulisema hapa, Ezekiel Wenje alisema mpaka povu likamtoka, ninyi wenzetu huko mlifanyaje, sisi tulikuwa wabaya, leo mnatulaumu eti vyama vyetu hivi vya UKAWA vilimsimamisha Mheshimiwa Edward Lowasa kuwa mgombea wa Urais, Mheshimiwa Edward Lowasa akiwa CCM akitembea mnampokea kama malaika ninyi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi alienda Tanga nilikuwepo Katibu Mwenezi wa CCM alimpiga mtu kutaka kumuua kwa sababu kamkaripia Lowassa, kweli uongo? Mliimba nyimbo nzuri za kumpamba, mpaka mkatusadikisha kweli yaweza kuwa yale maneno yetu hatuko sawa, hebu tumuangalie. Leo tumefanya kosa kubwa, miaka yote mliokuwa naye alikuwa mzuri, mbaya kwetu, kwenu kizuri, tutakuwa naye na tutakufa naye Lowassa na Mungu akimuweka 2020 ndiye huyo huyo, mkipenda msipende dozi ni hiyo hiyo, mkinywa mkitema shauri yenu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie jambo moja lililonigusa sana. Mheshimiwa Zungu siyo mara ya kwanza, siyo mara ya pili, siyo mara ya tatu amekuwa akishauri toka Bunge lililopita. Makampuni ya simu yanaiibia nchi, hii nataka niwaulize yeye yule siyo mpinzani, Mheshimiwa Zungu ni Mbunge wa CCM. Mheshimiwa Zungu alichokisema ni kwa maslahi ya nchi hii, mlifanya yapi, mmetekeleza lipi, hamna! Tutawasifu wafanyao mazuri na tutawakosoa wanafanya mabaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliopewa jukumu la kusimamia suala hili hawajaitendea haki nchi hii, kama mu-watumbuaji wazuri wa majipu angalieni hili siyo jipu ni busha! Lazima tuangalie kile kinachokosesha mapato nchi hii, tukiangalia bila kuoneana haya, kuna tatizo gani kuandaa wataalam wetu makini, wakaona ni kwa kiasi gani Tanzania inapoteza mapato kutokana na makampuni ya simu. Yupo nani nyuma ya makampuni ya simu tuambieni, yuko nani? Siyo bure iko sababu. Siyo bure kwa sababu tafadhalini tunayoyasema hapa siyo kwa ajili ya ushabiki ni kwa ajili ya kuisaidia nchi hii, itoke ilipo iende mbele. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuzungumzia juu ya maamuzi ya kukurupuka yanayochukuliwa na watendaji wa nchi hii. Nchi hii mmeingia mkataba wa himaya moja ya forodha kufanya mizigo ya Congo sasa hivi iwe inalipiwa kwao kabla ya kutoka katika Bandari ya Dar es salaam, jambo ambalo limechangia kushuka kwa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam kufikia asilimia 50. Hebu niwaulize tumefanya yale kwa faida ipi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu nchi ya Congo, mimi niliwahi kuwa mjasiriamali nilikaa pale Congo katika Mji wa Lubumbashi, nchi ile haijasimama utawala wake sawa sawa, pale unaweza kupeleka containers akaja Kanali tu wa Jeshi akatoa amri pitisha hizo kontena tano na zinapita. Sasa wafanyabiashara wale wa Congo mnapoweka vile vikwazo ambavyo haviisaidii nchi hii, wametafuta bandari ya Beira, wametafuta bandari za nchi nyingine wameiacha Dar es Salaam imedoda, mnapata faida gani? Mambo ya Wacongo yanawahusu nini ndugu zangu, msiba wa Kichina Mmasai anaingiaje? Waacheni wenyewe sisi tukusanyeni kodi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimesoma gazeti moja, nimeona taarifa Serikali inasema kwamba imeliona hili na mnalifanyia kazi, nawaomba sana ndugu zangu shitukeni mapema, kule Beira wakizoea utamu wa kule hakuna atakayerudi hapa, anzeni sasa kuchukua hatua msisubiri kesho na kesho kutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la utawala bora. Suala la utawala bora lina mtazamo mpana sana. Mojawapo ikiwa ni wananchi wenyewe wafaidike na utawala bora wenyewe. Nasikitika kwa kituko ambacho kimefanywa na Serikali yenu ya kuzuia matangazo haya wananchi wa Tanzania wasione wawakilishi wao wanasema nini, amesema mwenzangu hapa mmoja kwamba ule umaarufu Dkt. Chegeni mliokuwa mkiupata kwenye TV sasa hamtoupata tena. Kila Mbunge aliyeingia hapa mpaka ukiitwa Mbunge tayari wewe ni maarufu tu, ukaonekana kwenye TV usionekane kwenye TV wewe tayari ni maarufu tu. Wengine tuna umaarufu wa ziada.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mwenyewe ni maarufu kwa sababu ni baba watoto nina familia na watoto wasiopungua 12, nina mke wangu ambaye naweza kumfanya Waziri Mkuu, mimi Rais wa familia na watoto wangu Baraza la Mawaziri, siyo umaarufu mdogo huo? Kila umaarufu una ngazi yake, leo umaarufu wangu siwezi kuufananisha na Mheshimiwa Magufuli lakini hata umaarufu wa Mheshimiwa Magufuli hauwezi kuwa zaidi ya Mheshimiwa Barrack Obama, hauwezi kuwa sawa! Kwa hivyo, humu hamna uwezo wa kutupunguzia umaarufu tulionao, mimi ni maarufu, mimi ni Rais kwenye familia yangu, watoto 12 ninao ni Baraza tosha kabisa la Mawaziri na mama watoto Waziri Mkuu wangu, ninataka umaarufu gani tena. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tafadhalini sana fikirieni tena kwa makini, hatutafuti umaarufu tunataka Watanzania wajue wawakilishi wao waliowachagua wanasimamia vipi yale wanayoelekeza wawakilishe kwa Serikali yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo katika utawala bora kwa masikitiko tu ni kwamba leo hii nchi inayoitwa Zanzibar, nilisema kabla ya Bunge hili, kabla ya uchaguzi haramu uliofanyika mara ya pili Zanzibar, nilisema kwamba jamani tufikirieni maneno ya nchi wahisani wanayosema juu ya kuikatia misaada nchi yetu. Hili jambo misaada hii tusikae tukisema tutakula mihogo, mihogo ipo siku zote mbona hatukushiba? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo jamani Watanzania wenzangu, Wabunge wenzangu, niwaambie wazi watu wasiozidi kumi Zanzibar wanaifanya nchi hii iingie katika historia nyingine ya kuonekana nchi isiyo na demokrasia, wakati tunajidai ni nchi ya demokrasia. Kisiwa cha Zanzibar ambacho Mheshimiwa Ally Keissy alisema ukiwaita kwa filimbi wanakusanyika tunapatikana, wanainyima mamilioni ya Watanzania misaada katika nchi hii, siyo haki na tusijidai. Tumekuwa na matatizo, madeni yameongezeka, muda wote wakati ambapo tulikuwa tukipewa misaada, kuondoka kwa misaada hii ni tatizo, fikirieni tena.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge hili, napenda kuwaambia wananchi wangu wa Jimbo la Konde, kwa sababu kule kwetu Zanzibar hata kufanya mikutano hatufanyi, ile nchi imekaa ndivyo sivyo, kile kisiwa kimekaa ndivyo sivyo, utawala bora haujulikani. Kwa mfano, leo akitokea CCM mmoja katika Jimbo akienda ku-report tu wale wana-CUF wameniangalia kwa jicho baya, kijiji kizima wanapelekwa askari wanakwenda kukisomba wanakiweka ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, siropoki! Tarehe 17 siku tatu kabla ya uchaguzi, mwana CCM mmoja katika Jimbo langu, alizua kwamba amechomewa nyumba hakikuungua hata kibakuli kimoja, walikuja kuchukuliwa wazee wa kijiji 30 wakaswekwa ndani kwa sababu tu ya amri ya kisiasa ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba. Utawala bora gani mnaoujadili nyinyi hapa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba alitoa tangazo la kupiga marufuku wananchi wa Mkoa ule wasitembee usiku, ana mamlaka gani kisheria na Kikatiba kutangaza hali ya hatari katika Mkoa? Nchi hii ina Majemedari Wakuu wa Majeshi, Amiri Jeshi Wakuu wangapi? Hebu niambieni maajabu hayo kuna Amiri Jeshi wangapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasema na ninawaambia wananchi wa Jimbo la Konde kwamba dini zote zinakataza mtu kushirikiana na dhalimu, dini zote zinakataza kabisa mtu kushirikiana na mtu aliye dhalimu kwa njia yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, nawaomba wananchi wangu kuanzia mimi mwenyewe wasishirikiane na madhalimu muda wote wa uhai wa maisha yao, wasishirikiane nao. Kama wanauza watii masharti ya leseni kwa sababu inataka lazima kuuza, lakini kununua ni hiyari yao na hakuna atakaethubutu kuwaingilia, waendelee kufanya wanaloweza kuhakikisha madhalimu hawakamatani nao, hawashirikiani nao katika lolote na hilo nawaunga mkono mia kwa mia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape mfano tu mimi mwenyewe nimeanza, Mwakilishi wa CCM haramu aliyechaguliwa tarehe 20 alinipigia simu nikamwambia ukome kama ulivyokoma kuzaliwa mara ya pili kwenye tumbo la mama yako, na nilimwambia asinisogelee na akinisogelea hamtaniona tena hapa Bungeni, tutamalizana huko huko, hamtaniona. Haiwezekani, unakaaje na watu wanaodhulumu haki za watu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii imejijengea historia sasa ya kuifanya ile Zanzibar ni kichaka, leo ninyi mnatafuta watalii wakija wakiwinda vitalu na kupiga wanyama badala yake ninyi mnachukua Jeshi lenu mnalipeleka Zanzibar kuwalinda mama zetu na baba zetu, haki iko wapi? Wameleta magari yote ya Tanzania Bara kuja katika Kisiwa cha Pemba; mnawawinda nini, mnawatakia nini mama zetu, ndugu zetu, watoto wetu, tuna lipi baya, kukataa tu kuiunga mkono CCM ndiyo kosa letu? Kama hilo ndiyo kosa niwahakikishieni hata dunia iundwe mara ya pili CCM hatutaikubali na hatuitaki!
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie katika hoja iliyoko mbele yetu inayohusu Muungano na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nami kwanza kumwomba Mwenyezi Mungu atujaalie Wabunge na Viongozi wetu afya njema na wale ambao afya zao zimetetereka miongoni mwao hata mimi, tujiombee Mungu atupe uzima ili tuweze kulijenga Taifa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti namwombea kwa dhati tu Mheshimiwa Magufuli kama anavyopenda kusema tumwombee na mimi namwombea. Pia, namwombea kipenzi cha Wazanzibari, Mheshimiwa Seif Sharrif Hamad
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mungu ampe afya njema na nawaombea hao wengine walioko huko pia Mungu awajaalie afya njema ili tutakapochukua madaraka halali Zanzibar waone namna tunavyoendesha nchi Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye maombi yangu niweke upande wa pili. Pamoja na kwamba tumejiombea dua tupate uzima, lakini ikiwa Mwenyezi Mungu mwenyewe aliowajaalia maradhi ni kwa ajili ya dua zetu tulizoomba wale tuliodhulumiwa, Mwenyezi Mungu awaongezee maradufu maradhi hayo, ili wajue kama Mwenyezi Mungu yuko na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye uwezo wa kutenda kila jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kuchangia kwa kushukuru kuniweka mtu wa tatu na kulishukuru Bunge lako leo kutupanga wa upande huu tuwe wa mwanzo kuchangia, hii ina maana kubwa, hata Rais anapolihutubia Bunge hupewa yeye nafasi kwanza halafu sisi tukaja mwisho kuchangia. Kwa hivyo, leo wale mliowaweka badala yangu wote, najua hawana la kusema watalisema baada ya nitakayoyasema mimi, kaeni wanafunzi mjifunze. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema juzi Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati anatoa mchango wake hapa alijinasibu sana na akasema mengi sana kuhusu uhalali wa kilichofanyika 20/3/2016 Zanzibar. Wanasema wajuzi wa mambo uongo unapoendelea kusemwa na usipokanushwa unaonekana ukweli. Bahati mbaya sana hayupo nilitaka niyaseme haya akiwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Kifungu cha 71 na Kifungu cha 72 ambacho kwa kuokoa muda nitasoma Kifungu cha 72. Kinasema hivi: “Mahakama Kuu ya Zanzibar ndiyo pekee yenye mamlaka na uwezo wa kusikiliza na kuamua mashauri yote yanayohusiana na uchaguzi wa Zanzibar.” Hicho ni kifungu.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona wanawashwa ujue sindano inawapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaosema hata sisi hatukwenda Mahakamani, lakini Tume ya Uchaguzi ilitakiwa izingatie Kifungu hiki. Kwa hivyo, tunachosema hapa ni kwamba, uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika mara ya pili ulikuwa ni uchaguzi wa haramu na umewapa madaraka ambao haukustahiki kuwepo, maana yetu ni Katiba hii. Sasa kama Katiba hii hamuikubali na Katiba hii ndiyo alioapia Rais wa Zanzibar na ndiye muapaji wa kwanza kushika Katiba hii, maana yake ni kwamba Katiba hii ni haramu hata kuishika. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamesemwa na tutaendelea kusema kwamba mnadhani limekwisha lakini ninalowaambia halijakwisha, la Zanzibar halijapita! Lipo na litaendelea kuwepo. Mambo ya Zanzibar ni wale wanaosema ni sawa na mchuzi wa mbwa, ukiukosa kuunywa wa moto ukipoa haunyweki tena! Utakuwa ni uvundo na subirini soon uvundo wa mambo ya Zanzibar mtaanza kuuona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru katika Mkutano wa 15, Bunge la mwaka 2010, Bunge lililopita, nilinyanyuka hapa nikasema kwamba hakuna haja kusheherekea na kutumia mabilioni ya Tanzania kwa ajili ya sherehe za Muungano, nilisema hapa ndani, mwenye kukariri Hansard iko aende akatafute najua nilisema mimi. Nilisema tunapoteza pesa nyingi kusheherekea kitu kisicho na maana yoyote. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mheshimiwa Waziri uliouremba na kuupaka kila aina ya poda, lipstick, manukato au udi, hakuna kitu!
Muungano wa Zanzibar na Tanganyika tuliungana kwa madhumuni makubwa ya kusaidiana kiuchumi, kudumisha amani na kuleta maendeleo ya nchi zetu hizi. Leo kama nchi hizi zimekuwa ni katika mstari wa mwisho kwa umaskini duniani mnajivunia nini na Muungano huu? Kipi cha kujivunia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona aibu sana kwamba Muungano huu umekuwa ni silaha tu ya kukidhi matakwa ya watawala kuendelea kuitawala Zanzibar kimabavu, hili ndilo lililoko! Nataka nikuhakikishie, Wazanzibari wamefikia mahali pamoja na unyonge wao, lakini siku ya hukumu tunaiandaa kwa ajili ya wote wanaodhulumu haki za Wazanzibari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ilikuwa ni nchi ya mstari wa mbele katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, lakini Tanzania hiyo leo imekuwa ni nchi ya mwanzo inayokandamiza washirika wa Muungano wa Zanzibar na watu wake. Hili halikubaliki, lakini tunakokwenda siyo kuzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mnajifariji hapa kwa kuona kwamba sisi hatuna uwezo wa silaha lakini tuna silaha kubwa kuliko zenu ninyi na silaha yetu ni umoja wetu na Wanzazibari kwa umoja wetu tumekubali kufanya mabadiliko ili kuviondoa visiwa hivi pale vilipo viende mbele pamoja na wale wasakatonge wenu mliowaweka Zanzibar ambao wanakuja hapa wakitetea matumbo yao na siyo kutetea maslahi ya Wazanzibari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ni aibu gani wakati Marekani wanafikiria kuondoa gereza la Guantanamo bay kule Cuba, leo Watanganyika mmeligeuza gereza la Seregea kuwa Guantanamo bay ya Wazanzibari. Mmewachukua Masheikh wa Zanzibar ndani ya miaka mitatu wako hapa kesi zao hata ushahidi tembe moja hamjapeleka wa kuthibitisha ugaidi wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Brussels pametokea ugaidi juzi, wamekufa watu within one week, yule mwanamme mmoja ameachiwa huru kwa kusema hakuna ushahidi unaoonesha alihusika vipi na ugaidi wa pale. Leo ninyi hata aibu wala haya hamna, wanazuoni wa Zanzibar three years mnawanyima kukaa na watoto wao na wake zao, mmewaweka wake wajane ilhali waume zao wako, mmewaweka watoto mayatima ilhali baba zao wako. Haki gani, Muungano gani? Alaysa-Allah biahkami lhakimina hakika Mwenyezi Mungu atalipa juu ya udhalimu wote mnaowafanyia watu wa Zanzibar. Hatuna nguvu za vifaru, lakini nguvu zetu ni umoja wetu na iko siku Mwenyezi Mungu atatusikia kilio chetu cha kuona haki iko wapi mtaifuata mtake msitake! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niseme wazi msimamo wetu wa kutoitambua Serikali ya Zanzibar. Wako wengine wanasema hapa kwamba, kama hamuitambui Zanzibar mbona mmekuja hapa? Katika busara ya kawaida unapokwenda porini ukakutana mbwa mwitu utafanya vyovyote ujinasue na mbwa mwitu, lakini ukitembea mtaani ukakutana na mbwa anakubwekea na mwenye mbwa unamuona yaani mfugaji wake, huna haja ya kuparuana naye, mtafute mwenye mbwa u-deal naye.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Utaweza kumwambia mwenye mbwa, kwa hivyo tunajua kwamba Zanzibar mpiga filimbi wake yuko hapa na tunajitahidi kusema….
MWENYEKITI: Muda wako kwanza umekwisha;
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo katika hotuba hii Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kusimama hapa. Napenda ni-declare interest mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa masikitiko, hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo naamini maneno yale mengi kama yatatekelezwa ni mwendelezo mzuri na ningependa na ningetamani sana Watanzania waisikie na pia wasikie maoni ya Kambi ya Upinzani ili kuonesha mwelekeo sahihi wa ile kauli ya Rais ya Tanzania ya Viwanda, nilitamani sana. Kwa bahati mbaya sana Bunge hili bado tumeendelea kukaa gizani, tutaambiana sisi kwa sisi, tunaendelea kuambiana haya tuliyoambiana kwenye Kamati, mengi tunayajua.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nifarijike jana tu kwa Wabunge wawili wa CCM, niwapongeze sana kwa kitendo chao kizuri sana walichoionesha jamii ya Watanzania kwamba sisi siyo wapinzani tu tunaopenda haya tunayoyasema hapa kwamba Bunge hili lionekane live. Wao walitumia jitihada ya kupigana picha za video, Mheshimiwa Abuu na Mheshimiwa Aeshi na gazeti la Nipashe likaonesha Watanzania kumbe letu ni moja, lakini tunatofautiana tu kimtazamo.
Mwimbaji mmoja kule Zanzibar aliimba nyimbo akasema kisebusebu na kiroho kiko papo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya tuendelee kuambiana katika njia za upole nadhani tutaelewana tu, hakuna haja, muone tu umuhimu wa haya mambo. Mheshimiwa Mwijage leo katika majibu yako ya maswali hapa, kuna raia wangu alinipigia akasema nilitamani nimwone Mwijage kila muda lakini wapi umeyatupa ndugu yangu hulitetei hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba Msemaji wa Kamati, Makamu Mwenyekiti alizungumzia jambo moja zuri. Alizungumzia umuhimu wa biashara na namna Serikali inavyowa-treat watu wanaoingiza bidhaa kutoka nje kutokana na ukadiriaji wa kodi ambazo wakati mwingine tunasema hazina mashiko. Kwa mfano, hivi sasa Watanzania wengi wanafilisiwa magari yao katika Bandari ya Dar es Salaam kwa tatizo moja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe hukuwepo Bunge la Kumi, nilisimama hapa wakati Waziri wa Fedha akiwa Mheshimiwa Saada Mkuya nikasema ikiwa Serikali mmeweza kuweka Maafisa wa TBS katika nchi tunazochukua bidhaa kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa ubora wa bidhaa, ni kipi kinachowashinda katika suala hili la bei? Kwa sababu nchi ambazo Watanzania tunachukua magari kubwa ni tatu tu hapa duniani, ni Uingereza, Japan na Dubai, wakaweka usahihi wa ile bei ya gari Mtanzania analonunua ili akifika hapa atozwe kodi kulingana na thamani halisi ya gari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu kauli ile ilitoka left hand ikaonekana haifai. Leo Wabunge wenyewe wameonja bakora hii, wameagiza magari, thamani ya gari anavyolinunua akija hapa TRA tayari wameweka bei yao ambayo hiyo ni bei astaghfirullah wameifanya kama bei ya Msahafu maana Msahafu na Bibilia ndiyo ambayo haipingiki. Hii inapelekea watu kuona ugumu kiasi fulani wa kufanya biashara na watu wengi kufilisiwa gari zao zinapofika pale bandarini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naweka msisitizo wa hili, gari aina ya Suzuki Carry inauzwa si zaidi ya dola 500 Japan na ukiingia kwenye mitandao utaziona hizo bei, leo inachukuliwa hata carry ni gari ya anasa? Tungeondoa kutumia wanyama huko vijijini, mkulima mdogo mdogo analima mazao yake badala ya kutumia wanyama na kuokoa muda na kufikisha bidhaa zake katika soko angeweza kununua carry kwa dola 500 akija hapa akalipishwa kwa thamani ya ununuzi na usafirishaji ambayo haizidi dola 800, dola 1500 ikapigwa thamani lakini ukifikisha hicho kigari TRA wanakuambia thamani yake ni dola 2,500. Hii si haki, ni dhuluma na ni aibu sana kwa Serikali kuwadhulumu raia wake, tuliangalieni hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwa na wigo na maneno mengi juu ya biashara ya magendo baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Yamekuwa yakisemwa njia za panya zimekithiri katika ukanda wa bahari, lakini sababu ni moja. Sababu inayochangia hili ni vikwazo vya wafanyabiashara wa Zanzibar wanapoingiza bidhaa katika soko la Tanzania Bara. Kumekuwa na vikwazo na ugumu mkubwa sana ambao unasababishwa na Mamlaka ya Bandari na TRA Dar es Salaam kuwafanya wafanyabiashara wa Zanzibar watafute njia mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika hali ya kawaida ukimziba mdomo lazima atatoa pumzi kwenye pua. Wafanyabiashara wale wa Zanzibar cha kushangaza TRA ni moja, maafisa wa TRA wanateuliwa na Kamishna Mkuu wanafanya kazi kule Zanzibar, hakuna TRA mbili. Leo hii bidhaa kutoka Zanzibar zinapofika Dar es Salaam zinatazamwa kwa mtazamo hasi na kuonekana ni bidhaa ambazo hazifai kuingia ndani ya nchi yaani zinaangaliwa kwa ukakasi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na Tume za Pamoja toka miaka ishirini ya Bunge hili kujadili kuondoa vikwazo vya wafanyabiashara wa Tanzania Bara na Zanzibar lakini hili nalo linaonekana ni jipu. Ninukuu usemi wa Mheshimiwa Nahodha, Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar namheshimu sana kwamba ni jukumu la uchumi mkubwa kusaidia uchumi mdogo. Kwa hiyo, badala ya kuitazama Zanzibar kwa jicho hasi na wafanyabiashara wake lazima sasa muwatazame kwa mtazamo wa huruma na kuwaongoza katika njia stahiki ili biashara ifanyike pasipo na vikwazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo, nilisema na ninarudia raia wa nchi yoyote jirani ana haki ya kutoka na gari lake akaingia Tanzania, akitumia ruhusa ya kibali maalum kwa kukaa ndani ya nchi karibu miezi mitatu. Hilo kwa Zanzibar limeondoka na halipo, hawezi Mzanzibar kutamani kwenda Mikumi na gari yake na watoto wake ku-enjoy akaingiza gari lile na akapewa permit ya kwamba utakaa miezi mitatu gari kwa sababu labda kodi ya Zanzibar na hapa ina tofauti ukimaliza miezi mitatu urudi Zanzibar, hilo halipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii raia wa Burundi ambaye hayupo kwenye Muungano ataingia na gari lake na ata-enjoy kukaa nchi hii anavyotaka Wakongo halikadhalika. Kwa hiyo, hili nalo ni jambo linalotakiwa liwekewe utaratibu. Wapo wanaoleta magari yao kwa biashara wapitie ule utaratibu wote wa kiforodha na kama kuna makusanyo ya kodi ni sawa lakini anayekusudia kuja kukaa na gari lake katika kipindi kifupi kuna tatizo gani kupewa temporary document ya kukaa hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbona mkitoka na gari zenu hapa mkiingia kule hakuna kikwazo hiki, kwa nini? Leo hii ukitoka na gari lako Tanzania Bara ukiingia nalo Zanzibar njoo Konde uta-enjoy utaenda kulala under water room kule Jimboni kwangu hakuna tatizo lakini hapa kwa nini? Tatizo ni kwamba …
MHE. KHATIB SAID HAJI: Hatujipambi wakati wa kuolewa twajipamba wakati wa kuachwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mwenyezi Mungu pekee kwanza dakika zenyewe ni tano.
MWENYEKITI: Mheshimiwa khatib dakika tano.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa haya yanayotukuta hapa Bungeni, nimshukuru Mungu kwa kila linalotukuta. Leo nimesikitishwa sana na kilichotokea kwa njia yote ile iliyosababisha hotuba yetu ya Kambi ya Upinzani kufanya isisomwe hapa ndani ya Bunge imenisikitisha sana. Lakini nataka nikuambie tu kwamba, mmejaribu kufunga banda farasi ameshatoka. Watanzania wanaelewa kila kilichomo kwenye hotuba ile, taarifa ziko na wote wanajua ni nini, ujumbe gani umekusudia kuwafika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niwashukuru wananchi wa Pemba hususani wa Jimbo langu la Konde kwa mapokezi makubwa waliompa kipenzi chao, Maalim Seif Sharif Hamad, jana katika ziara yake aliyofanya kule Pemba. Sasa mapokezi yale ni ishara tosha kwamba, hakika Wazanzibari nyoyo zao ziko na Maalim Seif. Kilicho chema ni chema hakibadili tabia, ni bure mngekisema na mengi kukizulia, Mungu hukipa baraka na amani kukitia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo baada ya tukio la kuzuiliwa hotuba, nilimuuliza, ninaye mtabiri wangu wa nyota na mtabiri wa ndoto, nikamuuliza hatua ya mwanzo ndani ya Bunge yamezuiliwa matangazo live ya TV, wananchi wasione tunachokisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea, leo tayari tumezuiliwa hotuba yetu isisomwe ndani ya Bunge nikamuuliza what is next? Jibu aliloniletea muda mfupi ananiambia kinachoendelea baada ya kuweka dole mtawekewa vibakuli vya gundi wapinzani tutatia gundi ndi! Tukiingia hapa kimya. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni wajibu wetu kuona tunakoelekezwa kwenda, tuna hiari sasa kuamua kukubali kila tunalofanyiwa na wenzetu kwa sababu ya wingi wao au kuangalia ni hatua gani madhubuti tunachukua tukatae dhuluma yote ndani ya Bunge hili. Tukatae kunyamazishwa kwa namna yoyote sauti yetu hata humu ndani pia zisisikike, tukatae kabisa na tukatae. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kuzungumzia suala moja ambalo linaendelea. Jeshi la Polisi, nimekereka sana na kitendo chao cha kuwashikilia watu zaidi ya muda wa kisheria ambao wanatakiwa kuwa-hold katika vituo vya polisi. Hili limesemewa na mimi nalisemea na linaniuma sana, kwa sababu ukiacha hilo kule Zanzibar, Jeshi la Polisi linatumika sana kisiasa, anaweza kutokea tu Mkuu wa Mkoa akasema wakamate hao weka ndani na wanafanya hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku kumi hili linaniumiza sana, nalisema sana. Siku kumi kabla ya uchaguzi haramu wa marudio Zanzibar, wananchi wangu wa Jimbo la Konde wasiopungua 30 walizuiliwa katika vituo vya polisi katika muda usiozidi siku 14, wakapelekwa mahakamani, mahakama wakasema hatuoni kesi hawa ya kuwafungulia tulichotegemea kirudishwe vituo vya polisi watapewa dhamana, matokeo yake imetoka amri kutoka hatujui wapi, wanaambiwa endeleeni kuwashikilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuuliza Waziri wa Mambo ya Ndani, ni yeye, ni Naibu wake au ni nani anayesimamia amri hii haramu ifanyike kwa wananchi wangu. Leo akija hapa Mheshimiwa Waziri mimi na yeye na mshahara wake mpaka tujue nani anayetoa amri haramu ya kuwazuia wananchi zaidi ya muda wa kisheria unaotakiwa uwe nao au uwe umewapeleka mahakamani kwa hatua za mbele zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa sana, hapa alinyanyuka, katika moja ya maneno mabaya aliyowahi kusema kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM ambaye sasa hivi ni Waziri, ni pale alipotamka katika mmoja wa mkutano wake akiwa ndani ya kanisa kwamba, tatizo la Zanzibar ni Uislamu, Mheshimiwa Lukuvi, alisema hayo maneno, nataka niseme tatizo la Zanzibar sio Uislamu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkutano wa Bunge la Kumi kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilianzisha kauli mbiu isemeyo; “Utalii Uanze kwa Mtanzania.” Pamoja na kauli hii kuonesha msisitizo kwa Watanzania kuweza kujivunia na kunufaika na sekta hii, bado zaidi ya robo tatu ya Watanzania hawanufaiki hata kidogo na sekta hii ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli hii iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, ni hadaa kubwa kwa Watanzania. Inajulikana bayana kwamba kima cha chini cha mshahara wa Mtanzania hakizidi shilingi 300,000. Kutembelea mbuga zetu ni lazima kila Mtanzania kuchangia kiasi cha shilingi 5,000 mpaka shilingi 15,000, lakini pamoja na mchango huu, kama Mtanzania atalazimika kulala mbugani katika hoteli kwa usiku mmoja itamlazimu kulipa gharama mara mbili zaidi ya mshahara huo kwa kima cha chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Watanzania wakafahamu kuwa Mtanzania anapotaka kwenda mbugani kwa siku mmoja tu inagharimu dola za Kimarekani takribani 145 sawa na fedha za Kitanzania shilingi 316,825 kwa exchange rate ya shilingi 2,185. Hii ni kwa hoteli yenye gharama nafuu zaidi mfano Rhino Lodge. Gharama hii haijahusisha chakula wala huduma nyingine yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayojipambanua na kauli ya Hapa Kazi Tu kwa nini isingeona umuhimu wa kuvaa viatu vya wananchi hawa wa kipato cha chini na kuona ilivyo kazi kuweza kuishi kwa kiasi hicho cha fedha kitakachomfanya Mtanzania huyu aweze na yeye kujisikia sehemu ya kulinda na kuzifahamu mbuga zetu? Ni kwa nini Serikali isifike mahali ikaona umuhimu wa dhati kuweza kumsaidia Mtanzania huyu kuweza kujisikia kuwa sehemu ya rasilimali zilizo ndani ya nchi yake kwa kuweka mazingira nafuu zaidi kwa bei ambayo Watanzania wengi wataweza kulipia na kufurahia mandhari mazuri ya mbuga zetu? Ni vyema sasa tukaaza kujivunia vya kwetu kwa vitendo ili basi Watanzania wasiwe ni watu wa kusimuliwa au kuona mandhari ya mbuga zetu kwenye runinga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali inafumbia macho malipo yanayofanywa kwa fedha za kigeni hasa kwenye sekta ya utalii? Mara nyingi tumekuwa tukilizungumzia suala la matumizi ya dola katika mzunguko wa fedha hapa nchini, lakini ni kwa nini Serikali haichukui hatua?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, Mtanzania anayeamua kufanya utalii wa ndani na kuamua kulala kwenye hoteli zilizopo ndani ya mbuga, hasa zile zilizoko kwenye Hifadhi ya Ngorongoro, Serengeti na hata hoteli kubwa za Zanzibar, ni lazima afanye malipo kwa dola. Katika hali ya kawaida, ni Watanzania wangapi wanamiliki dola katika uchumi wao? Hii ina maana kwamba ni lazima wabadili fedha zao katika maduka ya kuuza fedha ili waweze kufanya malipo. Ifike mahali hasa Serikali ijitathimini. Ukienda nchi za wenzetu walioendelea, mfano, Norway, Switzerland, German na nyingine, huwezi kununua kitu kwa fedha ya kigeni. Wanathamini fedha yao zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni aibu na ni fedheha kubwa kwa Serikali kuendelea kushiriki katika michezo ya kuua thamani ya shilingi yetu kwa kuruhusu makampuni haya kuendelea kufanya tozo mbalimbali ndani ya nchi kwa fedha za kigeni. Serikali ije na sera lazimishi ya kuhakikisha kuwa fedha yetu inatumika. Wageni waweze kununua fedha yetu ili tuwe na akiba ya dola. Tunawezaje kufikia ndoto ya kuwa na uchumi na kati wakati sisi wenyewe ndiyo tunadidimiza thamani ya shilingi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza sana kuwa booking za hoteli za kitalii kwenye hifadhi za nchi hii zinazofanywa kupitia kwa mawakala walio nje ya nchi yaani ukitaka kupata nafasi ya hoteli unapiga simu Afrika Kusini au Nairobi kwa Wakala ambaye yeye ndio atakupa nafasi au laa. Tunataka kujua ni kwa nini jambo hili linafanywa kwa namna hii? Ni kwa nini booking zote za hoteli zilizopo hapa nchini zisifanyike kupitia mawakala waliopo ndani ya nchi yetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati sasa Tanzania kuweza kuthamini vitu alivyotupa Mwenyezi Mungu. Inasikitisha sana kuona vyura wa kipekee kabisa duniani hawapewi nafasi ya kutosha kuweza kufahamika kwa wananchi wetu. Vitu hivi vya kipekee kabisa ambavyo duniani kote hakuna, mfano wa vyura hawa wa Kihansi wanaozaa na kunyonyesha, ni dhahiri kabisa tunakuwa hatuwatendei haki wananchi wetu na hata watoto wetu ambao watakuwa watu wazima na hawaifahamu nchi yetu na vivutio vyetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ije na mpango mkakati wa kuhakikisha vyura kama hawa ambao ni amphibia, pamoja na malikale nyingine zinaingizwa katika mitaala mbalimbali ili watoto wetu waweze kuvifahamu vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nikuelezee tu kwamba moyo wangu unasikia burudani sana unapokaa kwenye Kiti hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu sana kunijalia na mimi leo kusema hapa. Pia nataka nimwombee dua zaidi kiongozi wetu wa Chama cha Wananchi CUF, Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad kwa majaribu anayokumbana nayo Wazanzibari na Watanzania wapenda haki wako sambamba na yeye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kila aliaye anashika kichwa chake, hashiki kichwa cha mwenzie. Tarehe 25 Julai, kama sikosei, mwaka 2011, nilisimama kwenye Bunge hili wakati huo ikiwa Wizara ya Afrika Mashariki nikilalamikia kitendo cha Jamhuri ya Kenya wanachowafanyia wananchi wetu wa Zanzibar wanaokuwepo Kenya wakishiriki katika shughuli za kujitafutia rizki kupitia njia ya uvuvi. Nililalamika hilo na Waziri aliyekuwepo wakati ule alifuatilia kiasi chake mambo yale yalitulia kwa kiasi lakini katika miaka ya karibuni masuala ya askari wa Kenya kuwakamata wavuvi kutoka Kisiwani Pemba kule Kenya ni suala ambalo linaonekana ni jambo la kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yamekuwa yakitokea, hivi karibuni tu, nadhani miezi mitatu iliyopita, wananchi karibu 100 kutoka Visiwa vya Pemba, wengi wao wakitoka katika majimbo yetu ya Kaskazini, Wilaya ya Micheweni, Wete walishikiliwa pale na sababu za msingi za kuwashikilia watu wale hawana, tumekuwa tukilalamika sana. Balozi wetu wa Kenya, Balozi mdogo aliyeko Mombasa amekuwa akifuatilia mambo haya na wakati mwingine amekuwa akiambiwa hakuna hasa shtaka la kuwashtaki watu wale badala yake wanapigwa faini ambazo kwa bahati mbaya sana tunalazimika Wabunge sisi kutoka Zanzibar hasa kutoka Pemba, tuchangishane mifukoni mwetu kwenda kuwagomboa watu wale kwa kuwalipia faini kubwa sana, haya mambo hayafai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar tuko kwenye Muungano, hatuna Wizara wala hatuna utetezi wa moja kwa moja, lazima tupitie kwenu. Mliyafanya, mnayaweza lazima muyaweze. Kule Zanzibar asilimia 90 ya watandika vitanda kwenye hoteli za kitalii ni Wakenya, wala hawanyanyaswi. Kwa nini Wapemba wanapata tabu katika Jamhuri ya Kenya? Naomba sana, Mheshimiwa Waziri akija atuambie tumekosea nini, wavuvi wetu wanapokuwa katika Jamhuri ya Kenya wanapata matatizo makubwa na yanajirudia kila mwaka. Hili haliwezekani na hatutakubali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tufike mahali tuseme kunyanyasiwa watu wetu imetosha, raia wa Tanzania ana thamani sana. Kwa hiyo, kuwaacha Wazanzibari ambao sasa ni Watanzania wakiendelea kuteseka na Balozi yupo, Mheshimiwa Waziri afuatilie jambo hili, linatukera sana. Kama wameshindwa wafikirie upya Zanzibar kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waone tutakavyotetea haki zetu kule. Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nataka nizungumzie suala lingine la mahusiano. Tanzania imezuka aibu sana hasa kwa viongozi na watu wanaosimamia usalama wa nchi hii. Jambo dogo ugaidi, kuna ugaidi, kuna magaidi Amboni, kuna ugaidi Zanzibar, hii hatujengi! Neno ugaidi ukilitaja kwa watu wengine huko macho yao yanakaa hivi. Leo pale Zanzibar imetajwa ni kisiwa ambapo kuna magaidi yako mahakamani wakati hakuna tendo la ugaidi ambalo limewahi kufanyika Zanzibar, kama lipo litajeni!
MHE. KHATIB SAID HAJI: Sio sifa kutaja ugaidi wakati hakuna ugaidi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami kabla ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuweza kusimama hapa na pia napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwajalia Wabunge wenzangu wote ambao tuko hapa, tupo katika hali ya afya njema na salama kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kabla ya kutoa mchango wangu wa mpango huu kuitakia heri Kamati ya Uongozi ya Chama cha CUF chini ya Jenerali Julius Mtatiro. Pili nimtakie kheri kipenzi cha Wazanzibari, Maalim Seif Sharrif Hamad nikimwambia zidisha uzi huo huo na kwa niaba ya Wabunge wa Chama cha Upinzani cha CUF, wote wako pamoja na wewe na Kamati ya Uongozi wa CUF na hawatayumba na hawatayumbishwa, wale wote wenye dhana kwamba CUF itakufa, watakufa wao kabla CUF haijafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbunge mwenzangu Mheshimiwa Stanslaus Nyongo aliongelea suala la mdororo wa mizigo katika bandari yetu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Nyongo ni Mjumbe mwenzangu tuko katika Kamati moja inayoongozwa na Mwenyekiti shupavu Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango kama huu mwaka uliopita mimi ni miongoni mwa waliosimama hapa kwa mdomo huu huu, kiti hiki hiki, kipaza sauti hiki hiki nikatahadharisha juu ya mpango wa Serikali kuingia kwenye mfumo mmoja wa himaya hii ambao utawafanya Wakongo walipie mizigo yao kabla ya kuondoka katika bandari ya Dar-es-Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitahadharisha kwa kujua kwamba, athari zake wafanyabiashara wa Congo wana mbinu zao ambazo hazihusishi nchi yetu na nikatahadharisha sana kwamba, tutahadhari na mpango ule tusijiingize katika jambo lile ambalo limekuwa ni source moja kubwa ya mdororo wa mizigo katika bandari ya Dar-es-Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri sana tulipopata bahati ya kwenda katika Bandari ya Dar-es-Salaam Kamati yetu kutembelea na kuona uhalisia wa mambo ulivyo na taarifa tulizopewa na Watendaji wa Bandari, tuliporudi na kuiambia Serikali ukweli wa tulichokiona, zilikuja tafsiri tofauti tofauti ambazo tulionekana sisi ni waongo na hatuna ukweli katika tunayoyaeleza, au tumetumwa au tunatumiwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Bunge yenye mchanganyiko wa Vyama vyote inakwenda kufanya kazi kwa ajili ya maslahi ya kuisaidia nchi hii, leo tunapoeleza ukweli, tunapokuwa tofauti na Watendaji wa Serikali ambao wanaogopa kumwambia Rais ukweli, huu ni ukweli! Wanaogopa kumwambia Mheshimiwa Magufuli ukweli uko hivi, wakadharau na wakasema waliyoyasema, lakini namshukuru Mwenyezi Mungu kitu cha ukweli kitaonekana tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi Waziri wa Biashara na Viwanda, Mheshimiwa Charles Mwijage, akikutana na Taasisi ya Wafanyabiashara Wasafirishaji (TATOA), kauli aliyosema ni ushahidi Watanzania nyote mmeisikia. Amekaa na wenye ma-truck anawaambia kwa muda waliofikia mizigo katika bandari yetu imepungua na sasa kinachofuata ni malori yenu mtafute parking myaweke na ikiwezekana wekeni vilainishi (grease), ili msubiri, hatujui ni mwaka huu au mwaka ujao. Nani mkweli na nani mwongo? Kamati kweli au Waziri mwongo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mhukumuni kwa matendo yake, msimhukumu kwa dhana hafifu. Tuliyasema yale, leo Waziri amekuja kumthibitishia Rais kwa mlango wa nyuma kama ni kweli Kamati iliyoyasema, mdororo wa mizigo Bandari ya Dar-es-Salaam umekithiri na umeathiri sekta nyingi sana. Umeathiri uuzaji wa mafuta katika ma-truck, umeathiri huduma za mahoteli, umeathiri hata wale madereva, dereva yule wa truck kutoka Tanzania hadi Congo ana vituo chungu nzima, humo si ajabu wengine wameshazaa na watoto! Watu wale leo hawapiti, mashaka yameongezeka, uchumi umedorora, mahoteli yamefungwa! Sisi tunasema ukweli, ule mpango haufai na tunaiomba Serikali izingatie hili na iuondoe mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi katika huduma za mizigo ya transit ni kigezo cha pili ambacho kimesababisha wafanyabiashara wa Congo wakimbie! Naomba Mheshimiwa Waziri, jambo hili pia walizingatie kwa makini ili bandari yetu irudi katika hali yake, wafanyabiashara warudi na sekta za uchumi za nchi hii ziweze kupanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi duniani ndani ya siku 100 za utawala wao huwa wanatoa taswira ya hali za uchumi za nchi zao zinavyoendelea, leo tuna mwaka mmoja wa utawala huu wa Chama kizee bado hatujajua hasa Watanzania wanaelekea wapi katika mfumo wa uchumi wa nchi hii. Hili ni jambo la kusikitisha sana! Sasa tunapowaambia hapa siyo kwamba, tunawaambia tunawachukia, tunawaambia ili mjue kama ni wajibu wetu kuwawakilisha wananchi na kuwaambia yale yaliyo ya kweli na hakuna budi myafuate, kwa sababu, sisi pamoja na kwamba ni washauri, lakini mshauri anayemalizia na kuwa na azimio huyo ni mshauri tofauti na washauri wa ngoma za mtaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie Kituo cha Uwekezaji ambacho kimeandikwa katika taarifa ya Kamati, Kituo cha Uwekezaji cha Biashara cha Kurasini; mradi huu mkubwa wa Kituo cha Uwekezaji cha Kurasini ni jambo lililoanza mwaka 2010 na Bunge lililopita kwa mara ya mwanzo walitakiwa kulipa bilioni 45 Tanzania shillings ili kuuwezesha mradi ule mkubwa wa uwekezaji uwepo ndani ya nchi yetu. Matokeo yake mradi ule ulisuasua kutoka shilingi 45 bilioni ukaenda mpaka shilingi bilioni 60 ni mwaka wa pili, ukaenda mpaka shilingi bilioni 90 mwaka wa tatu, ukaenda mpaka shilingi bilioni 120, ndiyo matokeo yake umemaliza kulipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha leo katika taarifa hii nimeona wanasema kama wale wafadhili ambao walikusudia kuendeleza mradi ule kuutekeleza wameondoka na haijulikani hatima yake. Tukumbuke kwamba, pesa za Watanzania zilizotumika, Watanzania walioondolewa maeneo yale kupisha mradi ule ni gharama kubwa ambayo imepatikana na maslahi hayaonekani yako wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tatizo ni nini? Tatizo ni kuchelewa kwetu kufanya maamuzi katika mambo ya msingi ya nchi hii. Tunachelewa, ni hodari sana wa kuandika kwenye karatasi, lakini ni wazito sana wa kutekeleza yale ambayo tunadhani yanaleta tija kwa nchi hii. Leo mradi ule ambao ulikuwa unagombaniwa na nchi zote za Kiafrika, Tanzania ikapata bahati ikachaguliwa na China kuletewa mradi ule mkubwa tumekaa hapa tumebabaika-babaika mpaka tayari mradi ule, leo nimeona kwenye taarifa umeondolewa wakati Tanzania ikiwa imeshalipa mabilioni ya shilingi kupata lile eneo na Watanzania waliokuwa wakiendesha maisha yao pale wametupwa hata hatujui wametupwa wapi! Leo matokeo yake tunakuja kuona hapa kwenye taarifa kama wafadhili wale wamejiondoa. Hiyo ni hasara nyingine kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huku kusuasua kwa kutekeleza miradi ambayo ni fursa kwa nchi inatueletea shida sana. Leo ni mwaka karibu wa 10 tunazungumza ndani ya nchi hii kuna chuma pale Liganga na Mchuchuma na kwenye mpango huu, kila mpango unaokuja tunaambiwa, tunasadikishwa kwamba, mradi wa chuma Liganga na Mchuchuma utafanyika, lakini matokeo yake tunaishia kusoma vitabu! Laiti mradi ule ungekuwa uko Kenya au Uganda au Burundi, leo tayari nchi zile zingekuwa zinazalisha chuma kile kwa wingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana Mwenyezi Mungu akishawapa anawapa, lakini kwa ugoigoi ambao tuko nao hata kama ingekuwa Mwenyezi Mungu anafikiria kuuondoa, bora angeuondolea mbali kwa sababu anatupa riziki tuzitumie kwa niaba ya watu wetu, lakini hatuwezi kutumia zile fursa, badala yake tunaandika kwenye makaratasi tu hatuwezi kufanya chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu tena leo nimeona nia ya Serikali juu ya kufufua viwanda. Imezungumzwa hapa General Tyre ya Arusha na viwanda vingine, TEMDO na kadhalika. Mheshimiwa nyimbo hizi hebu sasa Waheshimiwa Mawaziri, Serikali, wawe tayari kile wanachotusadikisha kinaweza kufanyika waweze kukifanya kwa muda unaowezekana. Leo hakuna asiyejua kwamba nchi ina demand kubwa ya matairi ya magari, biashara ya matairi ya magari ni biashara kubwa sana duniani, leo fursa ipo, mipira ndani ya nchi hii inazalishwa, lakini bado tunaimba wimbo tunafufua General Tyre kwenye vitabu, kwenye utekelezaji hakuna kinachotekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Maprofesa wengi wabobezi wa uchumi, wabobezi wa uchumi chungu nzima kwenye nchi wa kuisaidia Serikali kuandaa mipango mizuri ya uchumi, leo badala yake kupata wachumi wakatoa ushauri wao na kukaa na Serikali, leo wachumi mnawapeleka kuzoa taka mkiwapiga picha na wheelbarrow Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachumi wa kuisaidia nchi hii mnawapiga picha wakizoa taka na ma-wheel barrow! What? Tutakwenda wapi? Wachumi wetu tunawageuza vituko tukitegemea nchi itakwenda mbele! Hasara yao. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie lile Shirika la TEMDO. TEMDO ile taasisi imeanzishwa kwa ajili ya kusaidia uvumbuzi wa viwanda vidogovidogo na mashine ambazo zinaweza kuwasaidia Watanzania kuanzia wa viwango vya chini kabisa, lakini cha kusikitisha Mheshimiwa Serikali imeanzisha taasisi ile kwa kujua umuhimu na faida zake, lakini taasisi ile imetupwa kama yatima. Wamekuwa wakilazimisha waonekane wapo kwa kutenda mambo ambayo hata Serikali haiwasaidii hata senti tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunafanyaje? tunaanzisha kitu kwa nia ya kusaidia Taifa, lakini leo mnakitelekeza mnakifanya yatima! Matatizo ni yapi, hakuna kinachofanyika pale wakati wana uwezo mkubwa wa kusaidia kama vile viwanda amesema mwenzangu, viwanda vidogo-vidogo vya soksi, viwanda vya juice, viwanda vya kuteketeza taka kwenye mahospitali, ni watu ambao wana ujuzi mkubwa na wamesomeshwa na Taifa hili, lakini badala yake wametelekezwa. Naomba Mheshimiwa Waziri waiangalie hii taasisi, hakuna nchi zilizoendelea bila kuwa na taasisi za uvumbuzi kama hizi, taasisi za utafiti kama hizi ambazo zinaweza kusaidia nchi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itakuwa ni nchi ya ajabu sana kwamba, leo tunapozungumzia suala la uimarishaji wa viwanda, lakini wawekezaji wanapotoka nje ya nchi kuja hapa kutaka kuwezeshwa kuwekeza katika maeneo wanapata usumbufu sana kuanzia kwenye ardhi na watu wa NEMC wanakuwa ni vikwazo vikubwa vya uwekezaji katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko ushahidi wamekuja wawekezaji hapa, Mwekezaji anatumia mpaka mwaka mmoja kuhangaikia vibali vya kuweza kuwekeza miradi ambayo italeta tija kwa nchi hii, italeta ajira kwa nchi hii. Wako wawekezaji wamekuja na wamehangaika mwisho wameondoka kwa kuona kwamba sisi ni Taifa ambalo hatuko tayari. Hawakufanya kosa Rais Museveni na mwenzie Rais Kagame siku zile walipoamua wakasema katika East Africa kuna nchi zilizo tayari kimaendeleo na kuna nchi kama Tanzania tuziache kwa sababu wao hawako tayari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwanza tuwe tayari kusikiliza ushauri unaotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Pili, tuwe tayari kumshauri na kumwambia ukweli Mtukufu Rais kwamba, hali halisi ilivyo ni hii. Yule tunatakiwa ni Rais wetu tumheshimu na nawaahidi watu wa CCM tunamheshimu Rais Magufuli, lakini niwaambie hatutamwogopa katika kumwambia ukweli utakaosaidia kulijenga Taifa hili. Tutamheshimu ni Rais wa Tanzania, ni Rais wetu, lakini muwe tayari kumweleza ukweli, mnapoendelea kumfichaficha hamumsaidii! Mficha maradhi kifo humuumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wa Tanzania ukikua kwa kumshauri na kumwambia ukweli Rais, sifa na maendeleo ya nchi yetu ndio itakayotufanya sisi tujione ni Wabunge bora ni Mawaziri bora ni Serikali bora, lakini kuendelea kuona kila mmoja aah! Bwana mkubwa hafikiki! Itatuletea dhara na sisi tunawaambia haya, kama sisi tungekuwa na nia mbaya sana na Chama cha Mapinduzi tusingeyasema haya, tungekaa tu kwa sababu tunajua mnaharibikiwa. Watanzania sasa hivi wote wanalia hali ilivyo! Watanzania walikuwa hawajawahi kulia kwa ukosefu wa dawa katika nchi hii, mara hii mnasikia kilio!
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wetu wanalia na mabegi barabarani wanarudishwa makwao hawana pesa katika mikopo! Leo huduma nyingine zote zimedorora, lakini akishuka hapa Mheshimiwa Waziri wa Fedha atasema uchumi wetu umekua! Uchumi umekua mabenki yanaeleza kabisa, draft imetolewa mabenki yote yame-collapse! Hasara tupu ambayo ipo katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwe pamoja katika hili, tumshauri Mheshimiwa Rais Magufuli. Mtukufu Rais sio Mungu ni mwanadamu akiambiwa atasikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nianze kwa kusema kwamba, wakati tuna msiba mkubwa uliolipata Taifa kwa kuondokewa na kipenzi chetu, nasikitika kwamba tunaletewa tena msiba mwingine ambao ni mkataba usiofaa hata kuujadili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili jambo leo nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge wenzangu, nimesimama hapa kama mzalendo wa Tanzania. Katika mambo ya kinchi, katika mambo ambayo yataleta tija au hasara kwa nchi hii, na mimi nakubaliana, lazima tuwe wamoja. Naupongeza sana uongozi wa juu wa chama changu kwa kuliona hili na kutuletea mawazo ambayo siyo lazima, lakini kutuelekeza katika njia ya kwenda katika mjadala huu ambao ni hasara kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimejaribu kutafuta nondo zangu hapa, kila nilivyoangalia sizioni, lakini nina wasiwasi ndugu yangu Mheshimiwa Zitto Kabwe kazichukua. Kwa sababu yale niliyopanga kuyasema hasa, ndiyo yale ambayo ameyawakilisha. Hongera sana Mheshimiwa Zitto Kabwe. Ametupa somo na funzo zuri ambalo tunafika mahali kama Taifa lazima tukubaliane katika mambo ya msingi kama hili ambalo tunalo sasa hivi mbele ya meza yetu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, binafsi kuna kipengele katika mkataba huu kinachosema kwamba tutakaposaini mkataba huu hatutakuwa tena na uwezo kama nchi kuwa na ushirikiano na nchi nyingine, hii ni aibu! Hii ni aibu kwa sababu Tanzania ni Taifa huru. Hautakuja mkataba wowote ambao utatuzuia kuwa na ushirikiano wa kibiashara, ya kiuchumi au ya kisiasa na nchi nyingine, mkataba huo ukawa na una manufaa kwa nchi hii, haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna kifungu kingine kinasema kwamba tukishaingia katika mkataba huu, suala la kupandisha kodi kwa bidhaa itakuwa halina tena nafasi.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu hii kila mwaka unaona kodi zetu ni hizo za sigara, bia, vilevi na kadhalika. Hizo ndiyo kodi; revenue kubwa inatokana na hayo. Leo tukisaini mkataba huu, hayo mambo yatakuwa hayapo. Kuingiliwa uhuru wa nchi yetu kwa namna yoyote ni janga ambalo mzalendo wa ukweli haifai kulishabikia.
Mheshimiwa Spika, isionekane kwamba wapinzani ni watu wa kukataa kila kitu. Niwahakikishie, likija jambo lenye maslahi tutakuwa pamoja na hatutaangalia chama, lakini niwatahadharishe wenzangu, hasa upande huo, likija jambo la ovyo ovyo kama vile ulivyokuwa Muswada wa Habari, tutaukataa mpaka mwisho wa kiama. Tuambiane ukweli, mkileta lenye manufaa ni kama mnavyotuona, lakini mkija na mambo ya ovyo hatutakuwa pamoja, lazima muone mawazo yetu na muelewe kwamba sisi tupo kwa ajili ya Tanzania yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina mashaka sana. Jamhuri ya Kenya ni watu ambao wakati mwingine sijui wanatuona sisi Watanzania tukoje. Wamekuwa ni watu wa ku-beep, beep tu. Hii Afrika Mashariki haikuja kwa lengo la kunufaisha nchi moja katika Afrika Mashariki na nchi nyingine ziwe mashahidi, haiwezekani. Leo wenzetu Kenya kwa sababu katika mauzo ya nje wana karibu asilimia 90 na kitu, kwa hiyo, wao ni haraka sana kusaini katika hili; na wamekimbilia sana katika hilo, lakini hawatuangalii sisi. Nao ni miongoni mwa zile nchi zilizojifanya wako tayari katika kila jambo. Kwa hiyo, kama hili wako tayari, watakwenda peke yao, sisi bado. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Spika; Mheshimiwa Spika, umekuwa mtoro sana siku hizi mpaka tunakusahau. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, Kenya hao hao tuliokaa nao katika makubaliano ya single custom territory, ndio hao wametuacha kwenye junction. Sisi tumekwenda, wao wamechomoa. VAT on transit goods, hao hao Wakenya tulikubaliana, wakati wa kusaini, sisi tumeingia kichwa kichwa, wao wamechomoa. Mpaka lini Kenya watatuona sisi ni watu ambao ni kama wa kututumia rubber stamp ya kuendeleza mambo yao na sisi kutuacha nyuma. Haiwezekani, lazima tujiangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii inatupa funzo moja kubwa sana. Waheshimiwa, Serikali hii ya CCM hebu sasa fikirieni, dira na sera zetu za kiuchumi zinatuelekeza vipi? Haya ndiyo matatizo makubwa tunayoyapata; kuna mjuvi wa maneno mmoja au mjuaji wa kusema mmoja, alisema kwamba nahodha bora ni yule anayejua bahari anayokwenda. Kwa nahodha asiyejua bahari anayokwenda, hakuna upepo utakaokuwa muafaka katika safari yake, hakuna. Kwamba nahodha ni yule anayejua nchi yangu hii Tanzania, Serikali yetu; sera zetu za kiuchumi zinapelekea sasa wenzetu kuweka mikataba hii na kutuletea kuona kwamba sisi kwa sababu ya dhiki zetu, kwa sababu ya njaa zetu, wao watuletee lolote na tutakubali.
Mheshimiwa Spika, sasa tunasema kwamba ni afadhali tufe na dhiki zetu kuliko kukubali mikataba ya ovyo ovyo kama hii. Hatutakuwa tayari kufungiwa ngulai na kwa sababu eti ni nchi maskini tuendelee kukubali. Sasa umaskini huu ni lazima tuwaulize watawala wa miaka 50 mlioitawala nchi hii, kwa nini nchi yetu inaendelea kuwa maskini wakati sera nzuri na mambo mazuri mnayataja kwenye mikutano, lakini kwenye utekelezaji tunakuwa zero? Why? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima sasa mtimize wajibu wenu. Nakiomba sana chama kizee cha CCM, wengine wanaposema chama kizee wanaona kama ni kejeli; uzee ni busara.
Mimi ninapokiita chama kizee, naamini kuna busara. Niliwaambia bahati nzuri sana Bunge hili asilimia karibu 60 ni vijana na wengi ni ninyi, tusifike mahali tukaona wale wazee waliokuwemo kwenye Bunge hili ni bora kuliko vijana ninyi mlio na mawazo ya kizee kupita kiasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi kwa sababu ya muda mfupi nikubaliane na kumuunga mkono dada yangu Mheshimiwa Halima kwa hapo alipofika. Nikuhakikishie kwamba na sisi tunajua kama kuna utapeli umefanyika wa kulisadikisha Bunge hili kwamba Lugumi walichokuja nacho mara ya pili ni cha ukweli wakati ukweli halisi unajulikana. Kama alivyosema ni maajabu katika muda wa mwezi mmoja kutoka vituo 14 vikaja 153. Huo ni uongo, ni uongo, ni uongo kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nataka nianze kuchangia kwa kusema kwamba nasikitika sana kwa taarifa hizi nzuri ambazo tumeletewa hapa na wenzetu wa PAC na LAAC lakini kuna upungufu na nataka nianze na hii ripoti ya LAAC.
Kamati hizi ni za Bunge na ni Kamati za mahesabu. Umuhimu wa Kamati hizi hakuna ambaye hawezi kuuona kwa vyovyote vile iwe kwa jicho la karibu au kwa mbali. Hata hivyo, malalamiko makubwa yaliyopo hapa, nataka nisome katika ukurasa wa nne wa taarifa hii ya LAAC, anasema, nanukuu:-
“Zipo namna kuu tatu za kutekeleza majukumu ya Kamati ambazo ni:-
3. Kamati kuzuru na kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika baadhi ya Halmashauri ili kujiridhisha na thamani ya fedha katika miradi hiyo (value for money).”
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha sana ni kwamba tunaletewa taarifa hizi, siyo LAAC wala PAC, wote wanasema hakuna aliyepata fungu la kwenda kujiridhisha na taarifa hizi tulizoletewa hapa. Kwa maana nyingine ni kwamba wao wamepelekewa taarifa kwenye meza na wametuletea sisi hapa bila kuthibitisha chochote, hili ni kosa moja kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni mambo ya kimahakama kosa hili linafanana na utakatishaji fedha, uhaini, ugaidi, makosa ambayo hayana dhamana, ndiyo! Kwa sababu tunakotoka tunajua mambo yaliyokuwa yanaletwa kwenye makaratasi na wanapokwenda field kwenye ukaguzi kulikuwa kunakuja manyago makubwa sana. Kulikuwa kunakuja mambo ya hatari, mtu anaoneshwa hapa imejengwa shule wakifika hata kiwanja hakuna. Leo Bunge mmeridhia tuletewe haya kwenye makaratasi badala yake tunakuja kulishwa humu na tunapiga makofi tunakubaliana nayo. Hili ni kosa moja kubwa sana ambalo Serikali haihitaji kupewa dhamana juu ya kosa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najua tunabana na kubana mimi najua kuna utamu wake, lakini na kubanua kuna raha zake. Huwezi kubana moja kwa moja ukadhani mambo yataenda, haiwezekani. Lazima sehemu nyingine ubanue kidogo ndiyo raha ipatikane. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka ninukuu usemi…
Mheshimiwa Naibu Spika, hicho ni Kiswahili cha mwambao. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka ninukuu usemi wa hekima aliosema Rais Mstaafu kipenzi cha nyoyo, Jakaya Mrisho Kikwete. Hivi karibuni alisema hivi, unapokuwa mpya watu wanataka mambo mapya, lakini yawe mapya ya kimaendeleo siyo mapya ya kuharibu kule tulikotoka. Huu ni usemi mmoja wenye hekima sana kwa Rais wetu yule mpendwa mstaafu, Mungu amjalie akae kwa amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi taarifa za CAG ndizo zilizosaidia kuonesha madudu makubwa sana yaliyofanyika ndani ya nchi hii lakini leo hata CAG amelalamika kushindwa kwenda kufanya verification kwa sababu hakupewa bajeti ya kutosha. Mnataka kuficha nini ikiwa CAG sasa hapewi uwezo wa kwenda field kuangalia uhalisia wa mambo yanayofanyika? Mmeanza kubana Bunge lisionekane live, mmeanza kubana mikutano ya vyama vya siasa, mmeanza kumbana mpaka CAG asiende kwenye kazi zake? Tunawatendeaje haki Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatari na kama huko tunakokwenda mwendo wenyewe ndiyo huu jiangalieni upya. Mliwaambia Watanzania mnaleta ajira, mnaleta maisha mazuri, mnaleta afya, Watanzania wakawaamini na kuwapa kura zao sasa fanyeni yale mliyowaahidi Watanzania msiende kinyume chake. Siku ya hukumu inakuja na haiko mbali, siku zinakwenda kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshangazwa na jambo lingine na mimi nataka niliseme kwamba Kamati ya PAC wamelalamika hapa na mchangiaji mmoja amelalamika anasema wametaka taarifa ya madeni ya TIB wamenyimwa. Hili ni kosa lingine la uhaini kabisa kwa Kamati ya Bunge kunyimwa taarifa ili wafanye kazi zao. Hili Bunge linaonekanaje sasa? Hili siyo Bunge tulilotokanalo sasa tunataka kuchezewa na sisi tumekubali kuweka videvu vichezewe, haiwezekani! Ni lazima tuoneshe wajibu wetu kama wawakilishi wa wananchi ni vipi tumeisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati yangu hatukukubaliana na hili na TIB walileta orodha yote ya waliokopa Community Import Support tukawa nayo. Kwa hiyo, haiwezekani ni lazima wakubaliane na matakwa ya Kamati za Bunge, hakuna namna nyingine, ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nimshukuru Mwenyezi Mungu kunijaalia kupata nafasi na mimi kuchangia kidogo na nikushukuru na wewe kwa kunipa nafasi hii na shukrani kwa pekee zizidi kwako na nikuhakikishie tu kwamba uwepo wako katika kiti hicho unatupa raha ndani ya roho zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka nizungumzie nikiwa nimejieleza wazi kwamba ni Mjumbe wa Kamati hii ya Viwanda na Biashara na nimpongeze kwa dhati Mwenyekiti wetu. Kati ya Wenyeviti makini wa Kamati hizi za Bunge, Mheshimiwa Dalaly Peter Kafumu naweza kusema ni nambari moja.
Sasa katika Kamati zetu siku moja, alikuja mchumi fulani akatuambia kwamba wawekezaji ni kama ndege, kule wanapokuwa wanaruka angani wanaangalia ni nchi gani inafaa kuwekeza ndipo wanaleta uwekezaji wao. Na kati ya vigezo muhimu sana vinavyowavuta wawekezaji na vivutio muhimu sana, kimojawapo ni amani na usalama katika nchi. Wawekezaji wanaangalia mazingira ya usalama ndani ya nchi, hayo yanawafanya wawe na umuhimu wa kukaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo tunaokwenda nao sasa hauashirii kuwakaribisha wawekezaji katika nchi yetu. Juzi tu hapa wakati nauliza swali nilimshukuru Mwenyezi Mungu sana kwa kuijaalia nchi yetu kuwa ni miongoni mwa nchi ambazo haziko katika janga, tishio la ugaidi, hili ni jambo la kushukuru sana na tumuombe Mungu azidishe hilo. Lakini jambo la kusikitisha, Mheshimiwa Waziri, ninaemuheshimu sana alikuja akalipinga hilo na akaona kwake yeye ni bora kusema kama nchi yetu ni miongoni mwa nchi zilizo katika tishio hilo, ni kitu cha ajabu sana. Mimi namheshimu sana Mheshimiwa Mwakyembe, lakini ningeweza nikadhani labda sijui kuna kitu kimemvuruga au vipi lakini tuyaache hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hilo dogo, leo hii tunashuhudia vitu vya aibu ambavyo vinafanyika ndani ya nchi. Leo hii mtu mmoja anayejipa madaraka ambae aliwahi kujiita Mungu wa Dar es Salaam anafikia hadi ya kutaja majina ya wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa kwamba hao ni drug dealers wakubwa sana, kitu ambacho wale wawekezaji tayari wanatafakari upya na kuendelea kuwekeza kwao, je, hawa walioko nje watajifikiriaje kuja kuwekeza katika nchi yetu? Upande mmoja tunahimiza wawekezaji waje kuweka viwanda, upande wa pili tunawa-harass wawekezaji juu ya uwekezaji wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina mfumo kamili wa ulinzi wala sidhani kama umetetereka. Kuna Jeshi la Polisi, kuna Waziri wa Mambo ya Ndani makini sana tunayemuamini, mchapa kazi, kuna vyombo vya ulinzi wa usalama makini sana, kuna Usalama wa Taifa tunaamini ni makini sana, kuna Jeshi la Ulinzi ni makini sana. Leo vyombo vyote hivi vimeonekana havina maana, father god wa Dar es Salaam aliyejiita Mungu wa Dar es Salaam ndiye amejipa jukumu la kusema kila kitu katika nchi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu wa Dar es Salaam leo anaweza kumtaja yoyote na isiwe lolote siku ya pili anatoa amri aje central police, ni nani huyu katika nchi hii?
Waheshimiwa Wabunge, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilipopewa jukumu la kusimamia mambo haya muhimu ya ulinzi na usalama, dawa za kulevya na everything vimelala wapi? Vinamuachia Makonda aliyejibatiza kujiita Mungu leo anafanya kila kitu, ni nini, what for, tunakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nataka niliseme hili kwa sababu azma ya kuwekeza kwenye viwanda haiwezi kwenda kwa matamshi ya ajabu ajabu na maamuzi yanayotolewa na mtu mmoja kwa sababu yeye kauli yake inaonekana inasikilizwa sana na Mheshimiwa Mtukufu Rais, haiwezekani. Mimi nadhani sasa kila mmoja atajua wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa la mwisho mimi nataka kumwambia ndugu yangu Waziri, Mheshimiwa Waziri nia yako nzuri ya kuimarisha viwanda na mimi nakubaliana na wewe lakini Mheshimiwa Waziri kila mchezo una sheria zake. Kwenye riadha ile kuna mbio za vijiti. Huwezi kukimbia tu ukafika…..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia leo kuwepo hapa katika hali ya uzima. Pili, nakushukuru wewe binafsi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia hotuba hii muhimu iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuchangia naomba kwa heshima kubwa tu nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu na nimwombe Mufti Bulembo kidogo ampe nafasi Mheshimiwa Waziri Mkuu ili atusikilize. Naomba tu Mufti Bulembo, tafadhali!
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nachukua nafasi hii kwa dhati ya nafsi yangu kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua Profesa Kabudi kuwa Waziri wa Sheria na Katiba. Hii inatoka ndani ya moyo wangu. Sambamba na hilo, nampongeza kwa kumwondoa Mheshimiwa Mwakyembe katika nafasi hiyo na kumpeleka katika Wizara ile ya kucheza; atacheza, sasa tunamwona anapiga makofi uwanja wa Taifa. Huu ni ujumbe tosha kwamba akufukuzaye hakwambii toka, waona nyendoze zimebadilika; waweza ukae, huwezi ondoka. (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza sana Kamati ya Katiba na Sheria. Naipongeza kwa dhati sana kwa kuacha mapenzi ya vyama na kueleza lile lililo sahihi na la ukweli kwa mustakabali wa nchi yetu. Nawapongeza kwa dhati kwa kuona umuhimu wa kumwambia na kumweleza Msajili wa Vyama vya Siasa kama yeye wajibu wake ni kuvisajili na kuvilea vyama vya siasa na siyo kuvifarakanisha vyama vya siasa. Atekeleze wajibu wake na siyo kufanya mambo kwa mapenzi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba sana utusikilize. Mheshimiwa vyama hivi, mpaka chama kinaposimama kuna mambo mengi kinayopitia. Siyo jambo rahisi; vimeundwa vyama zaidi ya 20 ndani ya nchi hii, lakini hadi leo vyama vilivyosimama ni vyama visivyozidi vinne. Leo kwa sababu tu ya ulevi wa madaraka wa mtu mmoja, anatumia nafasi yake kufanya hujuma za waziwazi kwa ajili ya kukiteketeza Chama cha Wananchi - CUF, hilo jambo siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasikitika sana kwamba amani ya nchi yetu ni miongoni mwa sekta muhimu ambayo vyama vya siasa wanabidi kuvisimamia inavyopasa. Leo hii tunaona yanayofanyika, tunaona jitihada zinazofanywa hata kumbeba yule kibaraka anayetumiwa na wanaomjua; baada ya kufanikiwa kuingia Buguruni, leo wanaandaa njama za kuvamia katika Makao Makuu ya Chama Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yanafanywa chini ya usimamizi wa watu wanaojulikana na kuna Waziri mmoja wa Zanzibar anaitwa Hamad Rashid ndiye plan master wa kuandaa mambo haya kwa kushirikiana na Makamu wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ally Iddi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema wazi haya ili dunia ijue na Watanzania waelewe. Haya yanayotokea kwetu siyo ya bure, ni mambo yamefanywa. Haiwezekani mtu anaacha chama mwenyewe zaidi ya mwaka mmoja anaenda kukaa huko, anarudi anajishauri. Hata kama ni mke, unakuta ameshaolewa na watoto ameshazaa na mume mwingine. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya yanayofanyika kwetu, leo hii nitashangaa nisikie Sofia Simba leo karudi kajitangaza tayari ni Mwenyekiti tena UWT. Hamtakubali! Kwa hiyo, kuchochea hayo katika vyama vyetu vya upinzani ni jambo la athari mbaya, jambo ambalo halitaipeleka Tanzania
katika neema ambayo tunatarajia kuipata kwa Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Naibu Spika, neema ya Mwenyezi Mungu inakuja kwenye masikilizano. Msituchochee ndani ya Vyama vya Upinzani ili mkidhi haja zenu. Haiwezekani! Mlipoomba kura kwa Watanzania, mlisema Watanzania mtawaletea maendeleo, mtaleta elimu, maji; hamkusema kama
mtafitinisha vyama vya siasa ili mambo hayo muweze kuyapata. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukae tufikirie, tunapoandaa uwanja; tunapopanda nyasi tucheze vizuri, msitupandie michongoma ili tuumie miguu yetu. Haiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ujumbe huo umeupokea, naomba tufanye kila linalowezekana lililo ndani ya uwezo wenu, Serikali isaidie kutatua migogoro hii na isiwe wao ndio sababu ya kuimarisha migogoro hii. Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, hivi karibuni katika vyombo mbalimbali vya habari ilitangazwa kwamba Watanzania tuko nafasi ya 153 kwa kukosa furaha duniani. Kwa kweli hili jambo lilinisikitisha, lakini halikunipa homa sana, lakini sasa baada ya kukosa furaha, inakuja Tanzania tunajengewa hofu ya lazima. Hili la furaha tungeliacha mbali,
lakini hofu ambayo Tanzania tunajengewa sasa ndiyo jambo ambalo linanitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo haya yanayotokea ndani ya nchi sasa hivi katika tawala zote zilizopita hatukuzoea kuyaona. Wamepita Marais kadhaa na Mawaziri Wakuu kadhaa, hatukuona matukio yanayotokea ndani ya Tanzania yetu ya leo. Leo hivyo vikosi vinavyokwenda
vinachukua watu na kuwapeleka ambako hakujulikani na bado sisi Watanzania, sisi Wawakilishi wa wananchi wa Tanzania tuliomo humu, kama hatukusemea hili na Serikali ikawajibika katika hili, itakuwa hatutendi haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kundi la swala, anaweza akanyakuliwa mmoja, wawili na swala wakaendelea na safari, lakini siyo kundi la binadamu, kundi la Watanzania. Iwezekane yafanyike hayo na bado sisi tuendelee kufanya mambo mengine; hili jambo ni la hatari. Leo Mheshimiwa Bashe amesema, kama kuna orodha ya Wabunge kumi ambao wako listed haijulikani ni nini kitakachowapata wakati wowote. Mimi nimeingiwa na homa, sijui kama na mimi nimo! Eeh, Mungu wangu, tulinde waja wako na hizi hujuma ambazo hatujui nani anayeziandaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kitu cha hatari! Mheshimiwa Bashe anasema amepata taarifa kutoka kwa baadhi ya Mawaziri wa Serikali; hili siyo jambo dogo. Nadhani leo sisi Wabunge tusingekuwa na lingine la kujadili zaidi ya kufikiria hili. Kama kuna list ya Waheshimiwa Wabunge, hao raia wadogo wao wakoje?
Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunajadili bajeti ya maendeleo, maendeleo yapi yatakayopatikana wakati tayari tumejengewa hofu ya namna hiyo? Maendeleo yanaletwa pale watu wanapokuwa na amani, wanapojadili mambo kwa uwazi, wanaposema kwa uwazi; na mambo yale wakakaa wakapata muda wa kuyafikiri. Leo ikiwa Wabunge kumi hatujui, Mheshimiwa Selasini sijui yuko, sijui nani yupo, tunakaa sasa kila mmoja ana maswali ndani ya moyo; haijulikani ni nani yumo kwenye hiyo list, hebu Serikali tutoleeni hofu juu ya haya mambo. Tutoleeni hofu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Wafanyabiashara hawana furaha, Wamachinga hawana furaha, Wanasiasa hawana furaha, bodaboda hawana furaha; sasa jamani ikiwa kila mtu hana furaha na kila mtu anaiishi kwa hofu, ni Tanzania ipi tunaipeleka na ni wapi tunaipeleka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo anayeapa nambari moja Tanzania ni Mheshimiwa Rais, anaapishwa mbele ya Watanzania wote wanaona. Leo Mheshimiwa Rais baada ya kula kiapo kulinda na kuitetea Katiba, ni wa mwanzo anayetangaza vyama vya siasa ni marufuku kufanya mikutano ya kisiasa katika nchi hii. Hebu niambieni, ni nini kinachofanyika? Vyama vya siasa mnavipa ruzuku; sasa mnavipa ruzuku waende wakale na wake zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnawapa ruzuku wajitangaze watoe elimu ya siasa, elimu ya uraia, wajipanue wapate wanachama ili siasa za ushindani zitendeke ndani ya nchi. Leo mnawaambia tunawapa ruzuku, lakini ni marufuku kufanya mikutano ya vyama vya siasa. Maana yake
nini? Sasa wataenda kuvizuia vyama vya siasa kupewa ruzuku, mnamchukua kibaraka Lipumba, mnamchotea mahela ya Serikali, anaenda kutumia anavyotaka yeye. Hiyo siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, haya mambo anayefikiria kwamba kufa kwa CUF ndiyo neema yenu Zanzibar, anajidanganya. Ziko roho zilizotangulia kwa ajili ya CUF na ziko tayari roho nyingine kuzifuata kama mtafikiria kukifuta Chama cha Wananchi – CUF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu pekee kwa sababu ni dakika tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muongeaji anasema mwanadamu uvumilivu unapomuishia anakuwa ni afadhali mnyama kuliko mwanadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukumuacha Lipumba na vibaraka wake na wanaomtumia kwa sababu

tunamuogopa, hapana. Tulimuacha kwa sababu Watanzania na dunia ijue ujinga wao na hao wanaomtumia kufanya ujinga ule. Watanzania waelewe ujinga wa Lipumba na hao wanaomtumia kudhihirisha ujinga wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa sheria. Vyama vya siasa waasisi wa kuleta vyama hivi vya siasa mmojawapo ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mnamuita Baba wa Taifa na sisi tunakubali ni Baba wa Taifa, hawezi kutokea mjanja akamuona Baba wa Taifa aliyekubali vyama vingi vije nchi hii ni mjinga yeye ndiyo mwerevu, huyo ni zumbukuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme wazi kwamba mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF)kwa kupandikizwa na watu tunaowajua, akiwemo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Mheshimiwa Hamad Yussuf Masauni. Mheshimiwa Waziri umesema maneno makubwa sana nakuheshimu na katika Mawaziri kwenye Bunge hili ninaowaheshimu ni Mheshimiwa Mwigulu, lakini msaidizi wako hafai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umesema Mheshimiwa Waziri hakuna ushirika wowote wa waovu utakaoweza kuishinda haki, nakubaliana na wewe sana. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Masauni umekuwa ukifanya mambo kadhaa kwa kushirikiana na hao mnaoona wanaweza kuiuwa CUF, lakini nikuambie hukuijua ilivyozaliwa na hutoishuhudia ikifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna matukio 13 ya utekwaji wanayofanyiwa watu wa CUF na bado watu wa CUF tumeendelea kudumisha amani na kuvumilia. Hivi niambieni yule mwendawazimu aliyetumwa na hawa akina Maftaha juzi, akapigwa pale, kama siyo uvumilivu na ukomavu wa watu wetu, angekuwa hai leo? Angekuwa hai leo kama si ustaarabu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wetu, chama chetu, viongozi wetu wameendelea kuilinda amani na kuhakikisha damu haimwagiki kama anavyotaka Mheshimiwa Masauni imwagike ili apate sababu ya kufuta chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Hamad Masauni juzi uliratibu kikao cha kuhakikisha Tanga Mwenyekiti wetu hafanyi kikao, wewe kwa kushirikiana na Mheshimiwa Maftaha pamoja na mungiki wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumevumilia vyakutosha, hatumuogopi Lipumbana ninakuambieni sasa tunamnyoosha Lipumba na watu wake…

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa kumnyoosha tunao, nia ya kumnyosha tunayo na sababu ya kumnyosha tunayo.(Makofi)

Uvumilivu umetuishia, na ninakuambia hawa mungiki kwetu hawajai kwenye mkono mmoja.

Hawa ni wadogo sana, Chama cha Wananchi ni kikubwa sana ndani ya nchi hii, tunawaambia ifike mwisho na wakome, tupo tayari kwa lolote, lakini tutamnyoosha Lipumba na watu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la mrundikano wa mahabusu mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa sana kuhusu mrundikano wa mahabusu ndani ya magereza yetu. Hivi karibuni tunakwenda kwenye mfungo wa Ramadhani ilhali Masheikh wa Uamsho bado wakiwa gerezani wanaendelea kukaa bila kufikishwa mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mungiki tutawanyoosha.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Tuko hapa kujadili Muswada wa Habari. Kabla ya yote nimkumbushe dada yangu aliyemalizia kuchangia hapa kwamba kuna methali ya Kiswahili inasema: “Ukienda kwa wenye chongo fumba lako jicho” ili ufanane nao hata kama wewe macho yako yanaona sawasawa, lakini jaribu kufumba yako ufanane nao, kwa hivyo jiangalie.
Waheshimiwa Wabunge wenzangu leo katika kituko cha karne kinachotokea ni anaponyanyuka Mbunge wa CCM ndani ya Bunge akatulaumu kwa sababu eti tunampenda Lowasa, hiki ni kituko cha karne. Waheshimiwa rudini kwenye kumbukumbu kidogo tu. Mkutano Mkuu wa CCM, jinsi kale kawimbo katamu “kweeli”...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu kati ya watu ninaowaheshimu katika Bunge hili ni Mwenyekiti wewe kwa busara zako na hekima zako, lakini Mheshimiwa inapokuja hoja kutoka upande ule na tunaijibu kwa uzito unaofanana ule, naomba utupe nafasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala uliopita ulikuwa una nyenzo zote; una dola, una vitu vyote, Ikulu ilikuwa kwao, vyombo vya mashtaka vilikuwa kwao, kila kitu uwezo, power ya dola yote ilikuwa kwao. Katika kipindi chote walishindwa nini kumshtaki na kumshughulikia Lowassa mpaka yanakuja leo? Kwa hivyo, ninachosema ni kwamba ukienda kwa wenye chongo fumba lako jicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia kwa hadithi moja ndogo pia. Mheshimiwa Rais wa kwanza wa Zanzibar baada ya uhuru, marehemu Abeid Amani Karume, Mungu amuweke anapostahiki, alipokuwa na Maswahiba zake wa karibu baada ya nchi ile kupata uhuru, baada ya mapinduzi yale matukufu, moja kati ya sheria alizoweka, Zanzibar akiwa na maswahiba wake wa karibu kabisa, aliidhinisha chakula cha gerezani, Zanzibar kule kwetu tunaita Chuo cha Mafunzo kiwe ni dona, sembe na maharage, hiyo ndiyo kanuni aliyoipitisha. Hicho ndiyo chakula cha gerezani na kwa wakati ule Zanzibar kumlisha mtu dona na maharage ilikuwa kweli ni adhabu, ilikuwa ni adhabu kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haukupita muda mrefu alikosana na baadhi ya maswahiba zake waliotunga pamoja hiyo sheria. Matokeo yake wale mabwana wakaenda gerezani, watu wawili hao sipendi niwataje ni marehemu. Walipofika gerezani walikutana na chakula dona na maharage. Wale Mabwana mmojawapo alianza kula mmoja kilimshinda hakuweza kula. Siku ya mwanzo, siku ya pili, ilipofika siku ya tatu yule mwenzake amwambia “Shekhe inabidi ule kwa sababu hii sheria tuliipitisha wenyewe, tulikuwa pamoja wakati wa kupitisha hili na hivyo leo tumekuja hapa lazima tule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo sheria hizi, Muswada huu unaoletwa leo hapa, madhumuni makubwa ikiwa kwamba wanakomolewa watu fulani na kukiwa na lengo mahususi la kulenga uchaguzi wa 2020, Mungu ni mkubwa sana hapo katikati bado kuna safari ndefu sana. Linaweza likatokea lolote la kutokea, wanaotuletea huu leo wakawa waathirika wa mwanzo na Inshallah kwa Mwenyezi Mungu awajaalie wawe waathirika wa mwanzo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo binafsi sitaki niseme sana, lakini wakati mwingine tunapotoa hoja huku zinaangaliwa wanaotoa ni Wapinzani. Tunapotoa mawazo huku yanaangaliwa wanaotoa ni Wapinzani hata mazuri yanabezwa, matokeo yake leo hii tunaathirika kwa Sheria ya Ugaidi iliyopitishwa na Bunge hili. Sheria za ugaidi za kuwakamata watu na kuwaweka makorokoroni katika muda ambao hata haupatikani ushahidi ni moja kati ya sheria ambazo zilipitishwa na Bunge hili ambazo zinawaathiri, zinawanyanyasa, zinawanyima haki watu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko ushahidi kadhaa, leo katika magereza Tanzania, kuna wafungwa wanaohusishwa na kesi za ugaidi walioko mahabusu wasiopungua 85, Masheikh wa dini ya Kiislam, ni miongoni wa zile sheria zinazopitishwa kwa uharaka ili kukidhi mahitaji ambayo wenzetu mnaona yana maana sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge hili hili lilikaa Bunge la Katiba, yakapitishwa maamuzi tukashauri vizuri, Katiba hii siyo, rasimu inayofaa kufuatwa ni hii, mkafanya mliyoyafanya, mkaona yale mawazo yetu hayana maana, matokeo yake jana mmesikia Mtukufu Rais alivyosema. Yote hayo ni kutokana na kupuuza maneno yetu ambayo wakati mwingine msipokubali leo, kesho mtakubali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kusikitisha zaidi katika hili, Waheshimiwa tunakaa hapa tunajadili hili jambo, kabla ya kujadili hili jambo ni nini kilitokea? Sote tunajua. Hawezi kutumikia mtu mabwana wawili kwa wakati mmoja. Uchague kutumikia wananchi au uchague kutumikia nguvu ya pesa. Waswahili wanasema penye udhia penyeza rupia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mtukufu Rais anasema ukiingia kesho anausaini na anao uwezo wa kusema hivyo kwa sababu anajua nini kilichotangulia, anajua, anajua nini kilichotangulia. Sasa ninachosema ni kwamba tunapoteza muda bure, leo Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi Mwenyekiti wa Kamati hii ambayo ameutetea Muswada huu na amekataa wadau wasitoe maoni yao katika muda muafaka ni sawa na mchawi aliyepewa mtoto alee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote asingekwenda vingine kwa sababu anajulikana ni mtu wa upande gani au ni mtu ana mwelekeo gani. Kwa hivyo, haya yanayotokea tunafanya kazi bure lakini kwangu mimi Muswada huu na mtayarishaji mkuu, Waziri huyu ambaye mwelekeo wake toka alfajiri alipoingia hapa tulianza kuuona, toka akiwa huko nje tulianza kumwona, mtu maarufu wa goli la mkono. Msitegemee katika maisha yake ataleta kitu cha heri katika Bunge hili hata siku moja. Msitegemee hata siku moja kama ataleta jambo lenye heri kwa Watanzania, huyu ni mchafuzi, ni mchafuzi tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naseme kwamba haya mnayoyafanya jiangalieni vizuri. Bunge lililopita tulikuwa tumeishia mstari huu hapa, Bunge hili tumebakisha ka-quarter kadogo. Mwaka ujao he! He! 2020 na matendo haya na kwa Mawaziri hawa akina Nape Nnauye, Watanzania wahukumuni Musha-Allah. (Makofi)
Waheshimiwa msihuzunike sana. Muswada huu naufananisha na utunzi wa mtunzi mmoja anaitwa Suleiman Rashid…