Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. George Mcheche Masaju (6 total)

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kati ya mwaka 2011/2012 mpaka mwaka 2015/2016, jumla ya fedha amba zo Serikali ilizikopa nje kwa mfumo wa namna hii ni shilingi trilioni 6.8. Katika taarifa ya hukumu ambayo Mheshimiwa Waziri amei-refer kwenye statements of facts ukurasa wa 17 aya ya 113 inaonesha kwamba mtindo huu wa kutumia vikampuni kwa ajili ya kuweza kupata mikopo umekuwa ukitumika na benki nyingi za biashara hapa nchini.
Serikali haioni kwamba imefikia wakati Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aweze kufanya ukaguzi maalum wa mikopo yote ya kibiashara ambayo Serikali imeichukua kati ya 2011/2012 mpaka 2015/2016 ili kuweza kujua kama pia kulikuwa kuna aina za rushwa za namna hii ambazo zilikuwa zinafanyika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwamba DFA ambayo ndiyo hiyo hukumu ya Uingereza ilikuwa ina lengo la kuilinda Benki ya Uingereza ambayo ndiyo iliyotoa hongo kwa maafisa wetu ili iweze kupata biashara. Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa Serikali ifungue kesi dhidi ya benki hii ya Uingereza ili iwe ni fundisho kwa makampuni ya nje yanayohonga kupata biashara katika nchi za Kiafrika?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwanza, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali anayo majukumu ya Kikatiba ya kufanya kazi hiyo. Kwa hiyo, naomba kushauri tu kwamba hili ni jukumu lake anaweza akalitekeleza wakati wowote ili kujiridhisha kama mikopo hii ambayo imekuwa ikipatikana imekuwa ikipatikana kwa namna ambayo inaifanya nchi iingie kwenye hasara.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili nirejee tu pia kwenye jibu zuri la Naibu Waziri wa Fedha, kwamba kama Mheshimiwa anazo taarifa zozote zinazoweza kutusaidia sisi, ama kufungua shauri la madai au kufungua shauri la jinai, basi ashirikiane na vyombo vinavyofanya. Kwa mfano, hili shauri la madai sisi tukiletewa litaletwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, tutaliangalia tuone kama linakidhi sifa na sheria na kwa kuzingatia pia mahusiano tuliyonayo na nchi kama ya Uingereza tuone kama tunaweza, moja, kufungua kesi ya jinai au pili, tulifanye kwa namna ambayo tunaweza tukafungua kesi ya madai. Lakini mpaka sasa kilichopo ni kwamba hii benki iliingia makubaliano na Serious Fraud Office ya Uingereza kwa kitu kinachoitwa deferred prosecution agreement, ambayo pamoja na mengine walitakiwa walipe hizi dola kama Naibu Waziri wa Fedha alivyosema. Wakishindwa Serikali ya Uingereza itawachukulia hatua ya kesi ya jinai hii benki na sisi huku kama alivyosema Naibu Waziri wa Fedha, Benki Kuu imewataka Stanbic Tanzania nao walipe hiyo faini na muda huu ambao walipaswa wawe wametoa jibu ilikuwa ni tarehe thelathini. Kwa hiyo, tuupokee tu ushauri wa Mheshimiwa Zitto, Serikali itaufanyia kazi kwa kuzingatia sheria za ndani ya nchi na mahusiano yetu ya kisheria katika Jumuiya ya Kimataifa. Ahsante sana.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tarehe 25 Septemba, 2015, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilitoa tathmini iliyoonesha kwamba vyombo vya dola vina asilimia 60 ya uvunjaji wa haki za binadamu katika nchi hii na asilimia 40 inafanywa na raia wa kawaida. Hivi Watanzania wamtegemee nani ikiwa vyombo vya dola vilivyopewa jukumu la kulinda usalama wa mali na raia ndiyo vinaongoza katika ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hii? Wamtegemee nani?
Swali la pili, dogo tu. Mheshimiwa Waziri, kule Zanzibar, takribani ni wiki ya pili sasa, kumekuwa na matukio ya maharamia wanaojifunika soksi kwenye nyuso wakisimamiwa na vikosi vya SMZ kufanya uharamia mbalimbali katika Mji wa Zanzibar. Mheshimiwa Waziri, jana alisema hapa hana taarifa, tunamwomba atoe tamko, wananchi wawashughulikie kwa mujibu itakavyofaa kwa sababu ni maharamia ambao huna taarifa kama wanafanya uharamia katika Visiwa vya Zanzibar. Atoe awaambie wananchi wawapige mawe na wachome gari zao moto ili tupate suluhu ya uharamia unaofanywa Zanzibar. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulishauri Bunge hili Tukufu kwamba, sisi Wabunge hapa tumeapa kuitii Katiba na sheria za nchi. Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kabisa kwamba kila mtu lazima aitii Katiba na kufuata sheria za nchi. Sasa hoja anayozungumza Mheshimiwa Mbunge kuhamasisha sheria za nchi zivunjwe siyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri hawezi akatamka kwamba watu wavunje sheria na sisi Wabunge ndiyo tunaozitunga hizi sheria tunapaswa tuwe wa kwanza kusimamia utekelezaji wake. Kwa hiyo, nashauri kwamba, Mheshimiwa Mbunge hilo tamko analotaka kutoka kwa Mheshimiwa Waziri haliwezekani kwa sababu Waziri hawezi kusimama mbele ya Bunge akahamasisha watu wavunje sheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kuhusiana na hoja yake kwamba, vyombo vya dola vinakiuka haki za binadamu, niseme tu kwamba, kwa kweli vyombo vya dola vimekuwa vikifanya kazi nzuri katika kuhakikisha kunakuwa na amani na utulivu na vinahakikisha kwamba vinafanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo anayo malalamiko au uthibitisho, akayawasilishe katika Tume ya Haki za Binadamu na upo mchakato wa namna ya kuwasilisha malalamiko hayo. (Makofi)
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba wastaafu wa Afrika Mashariki hakuna tena na Serikali haidaiwi tena lakini mimi nasema Serikali inadaiwa, wako wengi. Mimi mwenyewe nina ushahidi, kuna mzee mmoja kule Pemba alikuwa anafanya kazi Custom, anaitwa Mzee Mohamed Kombo Maalim, alikuwa Askari wa Custom, mpaka kafariki hajalipwa mafao yake, ni mzee wetu kabisa. Sasa naomba kusema kwamba Mheshimiwa Waziri asitudanganye, aseme ukweli na sisi atujibu hapa, hawa waliobakia watalipwa lini? Wapo, hawajalipwa, nina ushahidi kamili!
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, hawa ambao hawakuridhika walienda tena Mahakamani wakafungua kesi, Shauri la Rufaa Na. 73 la 2013. Mahakama ya Rufaa imeamua tarehe 29 Januari, 2016, mwaka huu, kwamba madai hayo waliyokuwa wanadai kwamba wamepunjwa hayakuwa halali na hayapo tena. Kwa hiyo, ile ndiyo mwisho wa safariā€¦
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Sasa hii ni Mahakama ya Rufaa, ndiyo mwisho wake pale.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Naomba nirudie hapo hapo aliposema Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Waziri, tarehe 08/07/2016 Majaji wawili; Jaji Lila na Jaji Munisi walitoa hukumu in favour ya Rebecca Gyumi kuhusiana na suala la vifungu vya 13 na 17 kwenye suala la Sheria ya Ndoa. Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza agizo la Mahakama Kuu ili kufuta vifungu vya 13 na 17?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maamuzi yale Serikali imekata rufaa. Kwa mujibu wa sheria ya Basic Rights and Duties Enforcement Act, kama ni kesi ya kikatiba, unapowasilisha notice ya kukata rufaa inasimamisha utekelezaji moja kwa moja wa maamuzi ya Mahakama. Kesi ile haikuwa na mambo haya ya ndoa tu, kuna mambo mengi yalijitokeza na hayo yote lazima tupate mwongozo wa Mahakama ya Rufaa. Kwa hiyo, naomba kuwasihi Waheshimiwa Wabunge wawe na subira hadi hapo Mahakama itakapotoa maamuzi.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika siku za karibuni kumekuwa na harakati nyingi zinazoonesha kutaka kuleta haki na kuondoa ukandamizaji wanawake na watoto, ni jambo jema. Kwa mujibu wa kitabu chetu cha Qurani waislamu, ni kitabu kisicho shaka ndani yake. Kwa sisi waislamu huu mjadala tu wa kukitilia shaka kitabu cha Qurani, pia tunaingia katika makosa. (Makofi)
Je, Serikali itakuwa tayari kiasi gani katika marekebisho ambayo yanatakiwa sana kuhakikisha hayaingilii imani yetu na kutuendesha, kutupeleka katika dhambi kubwa ya kukitilia shaka Kitabu cha Quran na Sheria zake? Ahsante Sana. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri amejitahidi sana kujibu swali hili. Masuala haya ya imani Serikali imeyazingatia sana. Serikali haina dini lakini inaheshimu sana imani za dini. Ndiyo maana tulipotunga Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 zoezi la kuitunga ile sheria lilikuwa shirikishi, watu walishirikishwa wakitoa maoni yao ndiyo ikaja ile sheria. Ndiyo maana hata pamoja na changamoto za wanaharakati kutaka turekebishe ile sheria, tumesema hapana, lazima tuwashirikishe wananchi kwa upana wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kuchukua nafasi hii kuwashauri Waheshimiwa Wabunge na wananchi wanaosikiliza kwamba Serikali haitakaa iingilie mambo ya dini. Hili suala linahitaji muafaka. Hata tulipoleta Sheria ya Kadhi hapa, mwaka juzi, hatukuendelea nayo kwa sababu ni masuala yanahitaji muafaka mpana. Kwa hiyo, wananchi muwe na amani. Hili zoezi litafanyika kwa kuwashirikisha. Hatuwezi tukawalazimisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwa mustakabali wa elimu, bahati nzuri Waislamu wanatambua umuhimu wa elimu, maana hata Mtume alisema kama inawezekana kuifuata huko chini, akaifuate. Ndiyo maana tulitunga ile Sheria ya Elimu mwaka 2016, tukaweka kulinda wanawake hawa wasiolewe waweze kusoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ukijaribu kuangalia suala hilo jinsi lilivyo, hawa wote walikuwa wanastahili kulipwa lakini kilichotokea ni kwamba wenzao walikuwa na uwezo wakaajiri advocate na kwenda mahakamani.
Je, Serikali haioni busara kwa sababu kesi hiyo ni kama inawahusisha wote isipokuwa tu hawa wengine hawakuwa na uwezo wa kumpata advocate kwamba hata hawa wakienda mahakamani watalipwa sawa na kama ambavyo wenzao wamelipwa?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ngalawa kwamba majibu ya Naibu Waziri katika swali lake la msingi amesema msingi wa malipo yale na hawawezi wakalipa kwa madai ambayo hayajathibitishwa kisheria. Natambua pia kwamba hawa wafanyakazi wamemuomba Waziri wa Katiba na Sheria kusudi wapate fursa ya kufungua mashauri. Kama wanataka kufanya ambavyo wenzao walifanya basi wafungue kesi, lakini Serikali haiwezi kulipa tu madai ambayo hayajathibitishwa kisheria.