Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Godbless Jonathan Lema (8 total)

MHE. CATHERINE V. MAGIGE (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Hivi karibuni Mheshimiwa Rais ameamuru Wakuu wa Mikoa kuwakamata na kuwaweka mahabusu vijana watakaokutwa wanacheza pool table na draft mitaani kama ishara ya mizaha katika nguvukazi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza ajira ili vijana waweze kuajiriwa na kuepuka adhabu hiyo itakayotekelezwa na Wakuu wa Mikoa?
(b) Ni dhahiri kwamba Taifa letu linapita katika adhabu kubwa ya umaskini. Je, Serikali haioni kwamba Taifa linaweza kuingia katika vurugu kati ya vijana wasiokuwa na ajira na Jeshi la Polisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lema kuwa kazi si adhabu na nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi na hasa za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwezesha vijana wengi kufanya kazi Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
(i) Kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususan kilimo-biashara. Aidha, katika hili, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvukazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021)
(ii) Kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo maeneo ya kazi (apprenticeship na internship programs). Pia kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi ya ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi na ujasiriamali.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha hakuna vurugu kati ya vijana wasio na ajira na makundi mbalimbali, Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umejikita zaidi katika kukuza viwanda vidogo na vya kati ili kukuza ajira na kuondoa umaskini. Lengo la Serikali ni kuweka msisitizo wa watu kufanya kazi hususan vijana ili wachangie katika maendeleo ya nchi. Uzoefu umeonesha kwamba Taifa la wachapakazi lina utulivu na hivyo Serikali haitegemei vurugu kutoka kwa vijana wanaochapa kazi.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Mahitaji ya tairi za magari katika Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla ni makubwa. Mpango wa Serikali kufufua kiwanda cha tairi cha General Tyre unaonekana kwenda taratibu:-
(a) Je, ni lini Serikali itatambua umuhimu wa kiwanda hicho kuanza uzalishaji mapema;
(b) Wapo baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho bado hawajalipwa mafao tangu kiwanda kifungwe: Je, Serikali ina mpango gani wa kuwahakikisha wafanyakazi hao wanalipwa stahili zao?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatambua na kuthamini uwepo wa kiwanda cha kutengeneza matairi nchini. Ili kutimiza azma hiyo, Wizara yangu kama tulivyoelekeza katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017 tumeanza jukumu hilo kwa kubaini mambo ya msingi tunayopaswa kuzingatia katika kujenga kiwanda cha matairi ambacho imara na shindani. Baada ya taarifa ya kitaalam (Roadmap) ambayo itakamilika wakati wowote, kwa kushirikisha ngazi mbalimbali za maamuzi ikiwepo Kamati ya Bunge inayosimamia Viwanda, Biashara na Mazingira, uamuzi juu ya uwekezaji utafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kiwanda cha matairi ili kutekeleza dhima ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Kiwanda hiki kitatoa ajira, kitazalisha bidhaa bora, salama na imara na kwa kuzalisha tairi nyingi tutaokoa fedha za kigeni zinazotumika sana kuagiza matairi kutoka nje ya nchi. Pia uwepo wa kiwanda hicho ni kichocheo kwa soko la malighafi ya mpira ambalo tuna fursa ya kuzalisha kwa wingi hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, mtupe muda tusimamie kikamilifu utekelezaji wa jukumu hili muhimu.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Agizo la Mheshimiwa Rais la kufufua viwanda ni muhimu na la msingi kwa maendeleo ya Taifa:-
Je, Serikali haioni mradi wa Kurasini Logistic Centre unakwenda kinyume na fikra za Mheshimiwa Rais kuhusu viwanda?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimshukuru Mheshimiwa Godbless Lema kwa kutambua na kuthamini fikra za Mheshimiwa Rais juu ya azma ya kujenga Tanzania ya viwanda. Mchango wake na Wabunge wote katika kuhamasisha dhima ya Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Mradi wa Kurasini Logistic Centre tunaouhamasisha sasa ni mchango na chachu ya maendeleo ya uchumi wa viwanda. Dhamira yetu ni kuona mradi huo unaendeshwa na sekta binafsi kwa misingi ya kibiashara. Serikali imefidia eneo hilo kwa takribani shilingi bilioni 101 hivyo kiasi hicho ni mtaji wa Serikali katika mbia atakayechaguliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Kurasini Logistic Centre mwekezaji atawajibika kufanya yafuatayo:-
(i) Kujenga miundombinu ya viwanda ikiwemo ma-
godown ya viwanda, barabara, mifumo ya nishati na maji;
(ii) Kutafuta wawekezaji (operators) ambao watanunua malighafi kutoka ndani na nje ya nchi na kuzalisha bidhaa katika industrial shed nilizozitaja hapo juu;
(iii) Kuwa na mchakato wa kuzalisha bidhaa katika maeneo hayo;
(iv) Kufundisha na kuajiri vijana wa Kitanzania na kutumia Kurasini kama kituo cha mauzo ya bidhaa zinazozalishwa viwandani ambapo ni mauzo ya jumla tu yatakayofanyika katika sehemu hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huu unakwenda sawa na fikra za Mheshimiwa Rais za kujenga viwanda ili kutengeneza ajira kwa vijana na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa kukidhi mahitaji ya soko la ndani na soko la nje.
MHE. JOHN W. HECHE (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA)
aliuliza:-
Kukosekana kwa mpango madhubuti wa Mipango Miji pamoja na gharama kubwa za ujenzi zinazosababishwa na kodi kubwa katika vifaa vya ujenzi kumefanya wananchi kujenga kiholela.
• Je, ni kwa nini Serikali isiondoe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vifaa vyote vya iujenzi?
• Shirika la Nyumba la Taifa linajenga nyumba bora za makazi na bashara; je, ni kwa nini Serikali isiondoe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyumba za Shirika hilo ili ziwe za bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa fedha na mipango napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa vya ujenzi hutumika kwa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo nyumba za makazi pamoja na nyumba za biashara. Kwa kuwa matumizi ya vifaa vya ujenzi ni mtambuka, ni vigumu kutambua kama mnunuzi atatumia kwa ujenzi wa makazi binafsi, biashara au miundombinu kama vile barabara, umeme na maji. Hivyo basi, kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi kwa lengo la kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba za makazi kunaweza kabisa kuwanufaisha zaidi wafanyabiashara wachache kuliko mwananchi wa kawaida na pia kusababisha kupungua kwa mapato ya Serikali na hivyo Serikali kuwa na uwezo mdogo wa kutoa huduma muhimu kwa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika,kama ilivyo kwa bei ya bidhaa nyingine bei ya vifaa vya ujenzi haipangwi kwa kutumia kigezo cha kodi ya VAT pekee, bali hutokana na gharama mbalimbali zikiwemo za uzalishaji kama vile malighafi, umeme, maji, nguvu kazi, teknolojia pamoja na miundombinu ya usafirishaji na msukosuko wa nguvu ya soko. Hivyo basi, kuondoa VAT kwenye vifaa vya ujenzi si kigezo pekee kitakachopunguza gharama za ujenzi wa nyumba za makazi.
• Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kutoza kodi ni kuiwezesha Serikali kuwa na mapato ya kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kutoa huduma muhimu za jamii kwa wananchi wote. Nyumba zinazojengwa na kuuzwa na Shirika la Nyumba la Taifa ni mradi wa kibiashara na si huduma.
Pili, ni vema ikaeleweka kwamba, wauzaji wa nyumba hapa nchini ni wengi, hivyo uamuzi wa kuondoa kodi ya VAT kwenye nyumba zinazouzwa na Shirika la Nyumba la Taifa pekee utakuwa na sura ya ubaguzi kwa wauzaji wengine wa nyumba, ikiwa ni pamoja na kuikosesha Serikali mapato kwa manufaa ya Taifa letu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Barabara ya Mzunguko wa Afrika Mashariki (by pass) inayojengwa katika Jiji la Arusha na viunga vyake inaonekana kusuasua ingawa fedha za ujenzi zimeshapatikana.
Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi walioacha maeneo yao kwa ajili ya mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa mradi wa barabara ya mzunguko inayojengwa katika Jiji la Arusha na viunga vyake ni sehemu ya mradi wa Arusha – Holili yaani Taveta hadi Voi, ambayo ni mradi wa kikanda chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Tanzania Mradi wa Barabara ya Arusha – Holili unatekelezwa kwa awamu. Awamu ya kwanza inahusisha upanuzi wa Barabara ya Arusha kutoka Sakina hadi Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 kutoka njia mbili za sasa hadi njia nne ambayo ujenzi wake umekamilika mnamo Julai, 2017 na sasa upo katika kipindi cha uangalizi (Defects Liability Period).
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili inahusisha ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya mchepuo (Arusha by pass) yenye urefu wa kilometa 42.4 ambayo ujenzi wake ulianza tangu Februari, 2017 na unategemea kumalizika Juni, 2018. Mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wa Serikali katika kutekeleza mradi huu ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hii. Jumla ya shilingi bilioni 21.195 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi walioathirika na barabara hiyo ya mchepuo. Zoezi la kulipa fidia lilianza tarehe 22 Machi, 2016 na hadi sasa jumla ya wananchi 742 walioathirika na mradi huo wamepokea malipo yao ya jumla ya shilingi bilioni 21.195 na hakuna mwananchi anayedai fidia tena kwenye mradi huu.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Mishahara ya taasisi za umma hupangwa na Serikali. Utaratibu huo wa Serikali kupanga mishahara ya watumishi wake huathiri pia upangaji na ukadiriaji mishahara katika taasisi binafsi.
Je, Serikali haioni haja ya kuboresha mishahara yake na kuzielekeza taasisi binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha mishahara ya watumishi wake wa kada mbalimbali kila mwaka kwa kutoa nyongeza kulingana na kanuni za kiutumishi ikiwa ni pamoja na muda wa kukitumikia cheo au kupandishwa cheo mtumishi. Sambamba na utaratibu huu Serikali imeunda Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara ambayo hufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na uwezo wa kibajeti wa Serikali na kumshauri waziri mwenye dhamana na masuala ya utumishi wa umma kupanga kima cha chini cha mshahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 kama ilivyoboreshwa mwaka 2015 imeanzisha Bodi ya Mishahara ya Sekta Binafsi ambayo ina jukumu la kufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya gharama za maisha na masuala mengine ya kiuchumi na kupendekea kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi. Serikali hivi sasa ipo katika hatua za kuiwezesha bodi hiyo kufanya utafiti ili kuhakikisha utafiti huo unakidhi matakwa ya sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika hapa nchini na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi na ukuzaji wa tija na uzalishaji sehemu za kazi unaboreshwa kila mwaka, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015, imeweka utaratibu kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta binafsi kujadiliana na kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi kwa lengo la kuboresha maslahi yao ikiwemo mshahara na stahiki nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia utaratibu huu wa kisheria waajiri katika sekta binafsi wanaruhusiwa kuwalipa viwango vya mishahara hata zaidi ya kiwango kinachowekwa kama kima cha chini cha mshahara pale ambapo wanaona kwa kufanya hivyo itaongeza motisha kwa wafanyakazi wao kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa lengo la kuongeza tija katika kuzalisha mali au katika kutoa huduma.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Mishahara ya Taasisi za Umma hupangwa na Serikali. Utaratibu huo wa Serikali kupanga mishahara ya watumishi wake huathiri pia upangaji na ukadiriaji mishahara katika taasisi binafsi:-
Je, Serikali haioni haja ya kuboresha mishahara yake na kuzielekeza taasisi binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha mishahara yake na kuzielekeza taasisi binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha, Serikali imeunda Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara ambayo hufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na uwezo wa kibajeti wa Serikali na kuwashauri Mawaziri wenye dhamana na masuala ya utumishi wa umma na sekta binafsi katika kupanga kima cha chini cha mshahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya Mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015 imeanzisha Bodi ya Mishahara ya Sekta Binafsi ambayo ina jukumu la kufanya uchunguzi na kupendekeza kiwango cha kima cha chini cha mshahara na maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla. Serikali itaendelea kuiwezesha Bodi ya Mishahara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi pamoja na kuhamasisha majadiliano baina ya waajiri na vyama vya wafanyakazi katika kuboresha maslahi na kukuza tija na uzalishaji sehemu za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa sekta binafsi, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya Mwaka 2004, imeweka utaratibu kwa waajiri na wafanyakazi kujadiliana na kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi kwa lengo la kuboresha maslahi yao ikiwemo mshahara na stahiki nyingine. Kupitia utaratibu huu wa kisheria waajiri katika sekta binafsi wanaruhusiwa kuwalipa viwango vya mishahara hata zaidi ya kiwango kinachowekwa kama kima cha chini cha mshahara pale ambapo wanaona kwa kufanya hivyo itaongeza motisha kwa wafanyakazi wao kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa lengo la kuongeza tija katika kuzalisha mali au kutoa huduma.
MHE. GODBLESS J. LEMA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza kunufaika na nishati mbadala itokanayo na jua hasa, katika mikoa yenye ukame unaosababishwa na jua kali kwa kutengeneza Solar Village na kuunganisha nishati hiyo kwenye Gridi ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO inatekeleza Mradi wa Nishati Endelevu kwa Wote (Sustainable Energy for all – SE4ALL) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Kazi zilizofanyika hadi kufikia Disemba, 2018 ni pamoja na uhakiki wa kubainisha sehemu zinazofaa kwa uzalishaji wa nishati ya umeme-jua katika maeneo ya Same (Kilimanjaro) Zuzu (Dodoma) na Manyoni (Singida). Ili kuwa na uhakika wa uwezo wa kuzalisha umeme katika maeneo hayo, Serikali kupitia TANESCO imeanza kufanya upembuzi yakinifu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TANESCO imeanza kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme-jua wa MW 150 katika Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga. Gharama ya mradi ni Dola za Marekani milioni 375.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mshauri Mwelekezi anatarajia kukamilisha upembuzi yakinifu mwezi Machi, 2019. Ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2019 na kukamilika mwezi Machi, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utekelezaji wa miradi hii, Serikali kupitia TANESCO mwezi Oktoba, 2018, ilitangaza zabuni kwa ajili ya kupata wawekezaji binafsi watakaozalisha umeme. Kampuni 52 zimeonesha nia ya kuzalisha umeme kutoka chanzo hicho na hivi sasa, TANESCO wanafanya uchambuzi kwa ajili ya kupata Kampuni ya kuzalisha umeme MW 150 kutoka vyanzo mbalimbali vya nishati jadidifu pamoja na umeme wa jua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.