Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deogratias Francis Ngalawa (5 total)

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Wananchi wa Ludewa wamekuwa wakisikiliza mipango ya Serikali juu ya miradi mikubwa ya Makaa ya Mawe, Mchuchuma na Liganga ambapo kumekuwa na mipango mingi ambayo kwa sasa inaonekana kutekelezwa:-
(a) Je, ni lini wananchi walioachia ardhi yao kupisha miradi hiyo watalipwa fidia?
(b) Je, ni lini miradi hiyo inatarajiwa kuanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga inasimamiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji lakini inafanywa hivyo kwa kupita Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Miradi hii inaendelezwa kwa pamoja kwa maana ya (Intergrated Projects) kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) lenye asilimia 20 ya hisa na Kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Company Limited ya China yenye hisa asilimia 80 kupitia kampuni ya ubia Tanzania China International Mineral Resources Limited (TCIMRL).
Mheshimiwa Spika, Serikali ilitoa leseni za uchimbaji mkubwa SML namba 533/2014 ya tarehe 09/10/2014 katika eneo la Liganga lenye ukubwa wa kilomita za mraba 30.41. Lakini SML ya pili namba 534/2014 ya tarehe 9/10/2014 katika eneo la Mchuchuma lenye ukubwa wa kilomita za mraba 25.46. Leseni hizi zilitolewa kwa kipindi cha miaka 25 na zitaisha muda wake tarehe 08/10/2039.
Mheshimiwa Spika, Kampuni ilifanya uthamini wa mali za wananchi walioko ndani ya maeneo ya miradi ambao walitakiwa kupisha shughuli za utekelezaji wa miradi mwezi Agosti, 2015 na kuridhiwa na Mthamini Mkuu wa Serikali mwezi Agosti, mwaka huo huo. Mpango wa kulipa fidia unatarajiwa kuanza mwezi Juni, mwaka huu chini ya usimamizi wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
(b) Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza Machi, 2017 na kukamilika mwezi Julai, 2020 na utafanywa hivyo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Bonde la Mto Ruhuhu lililopo katika Kata ya Ruhuhu Wilaya ya Ludewa ni eneo muhimu sana, linaweza kuzalisha mazao mengi na kupunguza uhaba wa chakula Tanzania:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza bonde hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deo Francis Ngalawa, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Ruhuhu linalojumuisha Kata ya Manda, Wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe na Kata ya Lituhi Wilayani Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma kwa kilimo cha mazao ya aina mbalimbali yakiwemo mpunga, mahindi, mihugo na mboga mboga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maandalizi ya uendelezaji wa bonde hilo, upembuzi wa awali ulifanyika kati ya mwaka 2013 na 2014 na kubaini uwezekano wa kujenga bwawa kubwa katika eneo la Kikonge kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo kudhibiti mafuriko katika Bonde la Mto Ruhuhu, kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa eneo la takriban hekta 4,000 na kufua umeme mkubwa utakaounganishwa kwenye Gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika ipo katika hatua ya kutafuta fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa eneo hili pamoja na kuweka miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. DEOGATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Serikali ilitoa ahadi ya kutengeneza barabara ya lami toka Itoni – Njombe – Manda na upembuzi yakinifu tayari umeshafanyika.
Je, ni lini ujenzi huo utaanza hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo imekuwa kero kubwa hasa kipindi cha masika lakini pia ni muhimu kwa sababu ya ujiio wa miradi ya makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Itoni – Ludewa hadi Manda yenye urefu wa kilometa 211.4 kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Maandalizi kwa ajili ya ujenzi wa barabara yameshaanza ambapo kwa sasa barabara inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, usanifu wa kina kwa sehemu ya barabara yenye urefu wa kilometa 50 kuanzia Kijiji cha Lusitu hadi Kijiji cha Mawengi umekamilika na taratibu za kumpata mkandarasi wa kujenga sehemu hii ya barabara zipo katika hatua za mwisho. Ujenzi wa kiwango cha zege wa sehemu ya Lusitu hadi Mawengi umepangwa kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa kina wa sehemu ya barabara iliyobaki, unatarajiwa kukamilika Julai, 2016. Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DEOGRATIUS F. NGALAWA aliuliza:-
Pamoja na kwamba Jimbo la Ludewa lina vyanzo vingi vya maji, lakini kuna matatizo makubwa sana ya maji na wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kusaidia tatizo hili lakini Serikali na Halmashauri zimekuwa hazitoi ushirikiano kwa kurudi nyuma katika kuchangia sehemu yao kwa kigezo cha kutokuwa na fedha. Mfano vijiji vya Maholongwa, Mlangali, Mavanga, Manda, Nkomang’ombe na Lwela.
(a) Je, Serikali iko tayari kuweka kipaumbele katika kusaidia pale inapohitajika kuchangia?
(b) Je, nini kauli ya Serikali katika kushughulikia tatizo la maji Jimboni Ludewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deogratius Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya maendeleo unafanyika kwa njia shirikishi yaani Serikali, wadau wa maendeleo na wananchi kupitia mpango wa fursa na vikwazo kwa maendeleo. Kwa utaratibu huo mafanikio makubwa yamepatikana katika kuboresha huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imeweka kipaumbele na kutenga shilingi milioni 861 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji katika Kijiji cha Lugarawa, ukarabati wa miradi ya maji Lifua/Manda na Kijiji cha Ludewa K. Vilevile Serikali inashirikiana na taasisi isiyo ya Kiserikali ya Lusala Development Association kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji katika vijiji vya Mlangali, Mavanga na Nkomang’ombe utakaogharimu shilingi milioni 250 ambapo mchango wa Serikali ni shilingi milioni 50.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapongeza mchango mkubwa wa wadau mbalimbali kushirikiana na wadau wa maendeleo katika sekta za maji zikiwemo taasisi za dini. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na kuhakikisha bajeti inatengwa kila mwaka kwa ajili ya kutatua tatizo la maji kwa wananchi wa Ludewa na maeneo mengine hapa nchi.
MHE. DEO F. NGALAWA Aliuliza:-
Shirika la Posta Tanzania lilitumia fedha zake kuwalipa Wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kulirejeshea Shirika hilo fedha hizo ili kulinusuru?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Shirika la Posta Tanzania lilitumia fedha zake kuwalipa wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki na kuwasilisha madai Serikalini ili lipate kurejeshewa fedha zake. Hadi sasa Shirika limelipa shilingi bilioni 5.9 na Serikali imesharejesha shilingi bilioni 2.7 kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, Novemba, 2016 Serikali ilirejesha Shilingi milioni 700; Desemba, 2016 Shilingi 1,000,000,000; na Januari, 2017, Serikali ilirejesha Shilingi 1,000,000,000. Aidha, Serikali itaendelea kurejesha kiasi kilichobaki cha Shilingi 3,200,000,000 kwa kadri fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Msajili wa Hazina inaendelea na jukumu la kuwalipa pensheni ya kila mwezi wastaafu wa lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki wapatao 292.