Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deogratias Francis Ngalawa (7 total)

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado ulipaji wa fidia huu umeonekana kuwa ni kitendawili, kwa mara ya kwanza tuliambiwa kwamba fidia hizi zitalipwa tarehe 16 Februari, lakini sasa hivi Serikali inakuja na majibu mengine kwamba itaanza kulipa mwezi Juni. Sasa tunaomba kujua specific date ya fidia hiyo itakuwa ni lini?
Pili, kumekuwa na usumbufu mkubwa katika ulipaji wa hiyo fidia, je, kwa sababu muda utakuwa umeshapita fidia hii italipwa pamoja na fidia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli fidia ilianza kulipwa tangu mwezi Februari mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, lakini tutambue kwamba suala la ulipaji fidia ni suala endelevu, kadri tathmini inavyofanyika ndiyo fidia inavyoendelea kulipwa na ndiyo maana tunasema hata mwezi huu na mwezi ujao wataendelea kulipwa fidia. Suala kubwa Mheshimiwa Mbunge ni kwamba shughuli za ujenzi wa mradi huu zitaanza mapema tu baada ya fidia kukamilika.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kama wananchi watalipwa pia pamoja na nyongeza ya mapunjo ya awamu iliyopita.
Mheshimiwa Spika, taratibu za fidia kwa waathirika hufanyika wakati tathmini inapofanyika, kwa hiyo malipo ya fidia hulipwa kulingana na viwango wakati tathimini inafanywa na siyo vinginevyo.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na umuhimu mkubwa wa bonde hili ikiwa ni pamoja na kufua umeme ili kuweza kupeleka katika Gridi ya Taifa: Je, ni lini Serikali itaona kuna umuhimu wa kuitengea hela bila kutegemea ufadhili?
La pili; katika Wilaya ya Ludewa kuna mabonde kama ya Bonde la Mkiu na Bonde la Lifua: Je, ni lini Serikali itaiwekea mpango mkakati ili mabonde haya yaweze kutumika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya kwanza, Mheshimiwa ameshauri kwamba ni lini Serikali itaacha kutegemea wafadhili katika kutekeleza miradi yake. Nimfahamishe Mheshimiwa Ngalawa kwamba mwaka 2006/2007 tulianza programu ya utekelezaji wa maendeleo ya Sekta ya Maji kwa kushirikiana na marafiki na wadau mbalimbali wenye nia nzuri ya kutusaidia sisi Watanzania. Programu hiyo ya kwanza iliisha mwezi Desemba, 2015. Januari mwaka huu, tayari tena tumesaini memorandum ya utekelezaji wa maendeleo ya maji kwa kushirikana na wadau hao mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hatua hii, kwa sababu tuna memorandum tayari, hatuwezi kusema Watanzania tujitenge peke yetu. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana nao katika utekelezaji wa miradi ya maji ikiwemo ya umwagiliaji kwa kushirikiana na fedha ya Seikali ya Tanzania ambayo ni kodi ambazo Mheshimiwa Rais amesisitiza kwamba tulipe ili tufanye miradi ya maendeleo pamoja na wafadhili. Pia Mheshimiwa Mbunge ujue, bila wewe mwenyewe kutenga fedha, wafadhili hawawezi kukusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ni kwamba ni lini sasa? Yapo maeneo mengi yanayofaa kwa umwagiliaji, Serikali itahakikisha kwamba inajenga miundombinu. Ni kwamba nchi yetu tayari ilishafanya utafiti kwamba tuna hekta zinazofaa kwa umwagiliaji milioni 29.4 na kati ya hizo, hekta 461,000 zimeshaendelezwa na zinafanya kazi. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba hekta zote tumezikamilisha tumeziwekea miundombinu ya umwagiliaji ili tuweze kuondokana na tatizo la maji pamoja na tatizo la njaa. Katika hiki kipindi cha miaka mitano cha Awamu ya Tano, tumepanga kuhakikisha kwamba tunajenga miundombinu, tunapata hekta milioni moja kuendeleza Sekta ya Umwagiliaji.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Juu ya suala la upembuzi yakinifu wa barabara hii limeshakuwa ni la muda mrefu sana. Bahati nzuri tayari hata Mkandarasi alishapatikana na tayari hilo tangazo lilishatolewa toka Desemba, 2015. Sasa leo hii mnapozungumza kwamba, process za kumpata mkandarasi zinaendelea ni mkandarasi gani tena mwingine huyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, imeshakuwa ni kawaida kwa Serikali kuwa inatoa utaratibu wa kwamba hiki kitu kitashughulikiwa muda fulani, lakini matokeo yake muda unapita na hicho kitu kinakuwa hakijafanyika. Sasa ningependa kujua kwa sababu 2016/2017 ni muda mrefu, ni muda ambao unachukua miezi 12, wananchi wa Ludewa wangependa wajue ni lini hasa itaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa nilizonazo kama ambavyo nilisema katika jibu la msingi mkandarasi yupo katika hatua ya mwisho kupatikana. Vilevile ujenzi wa barabara hii atakumbuka kwamba, alisaidia sana Bunge limepitisha bajeti ya Wizara yetu na katika bajeti ile kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara hii, kwa hiyo, ujenzi utaanza katika mwaka ujao wa fedha unaoanza tarehe Mosi, Julai.
MHE. DEOGRATIUS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado tunauliza. Wadau mbalimbali wamekuwa wakichangia michango hii ya maji kwa karibu sana lakini Serikali imekuwa ikusuasua kupeleka hizi hela.
Je, Mheshimiwa Waziri ananithibitishiaje kwamba tutazipata fedha hizi kwa haraka?
Pili, kwa sababu wadau wa maendeleo wamekuwa wakileta ile michango na kazi inakuwa imeshafanyika, kutokana na Serikali kuchelewesha michango yao inakuta kwamba baadhi ya miundombinu inakuwa tayari imeshabomoka.
Je, Serikali inaweza ikagharamia ile miundombinu iliyobomoka kwa sababu ya kucheleweshwa kwa fedha?
NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS-TAMISEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze wazi kwa sababu Serikali kuna commitment ya shilingi milioni 50, na kwa sababu jukumu letu kubwa ni kuhakikisha miradi ya maji iliyotengwa katika kipindi hichi inaweza ikapata msaada wa haraka. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Deogratius, ofisi yetu itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tunasukuma pesa hii milioni 50, kama ni matching grands ya kuhakikisha mradi huo unatekelezeka, tutaweza kulifanya hili wala usihofu, mimi mwenyewe naomba nitoe commitment hiyo kama Serikali kuhakikisha jambo hili linakaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima kwamba miradi mingine imetekelezwa lakini mpaka imechakaa. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha miradi ile sasa inarekebishwa kuweza kufanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Deo kuwa tutakachokifanya kwanza ofisi yetu itawasiliana na Ofisi wa RAS Mkoa wa Njombe, kuangalia ni jinsi gani kama kuna miradi ambayo ina changamoto kubwa na kubainisha ni kitu gani kinatakiwa kifanyike. Kwa sababu mwisho wa siku, mradi kama umetekelezwa lakini mradi saa nyingine umeharibika kabla ya kuwapatia wananchi fursa hiyo ya maji ina maana tutakuwa hatujafikia malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Ofisi ya RAS Mkoa wa Njombe naomba niiagize kupitia mkutano huu, kwamba wahakikishe wanafanya follow up katika Jimbo hili la Ludewa kuangalia changamoto iliyokuwepo halafu tuangalie mkakati sasa, tutafanyaje ili mradi miradi hiyo iweze kufanya kazi. Lengo kubwa wananchi wako Mheshimiwa Deo waweze kupata fursa ya maji, na hiyo ndio azma ya Serikali kwamba kuhakikisha inawahudumia wananchi wake.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kuzungumza hapo kwamba tarehe 19 mwezi wa nne liliulizwa swali kwenye Bunge lako Tukufu kuwa Mradi wa Chuma, Liganga na Makaa ya Mawe Mchuchuma, utaanza lini? Majibu ya Serikali yalikuwa kwamba kwanza fidia italipwa mwezi Juni, 2016 ambayo fidia hiyo haijalipwa mpaka leo na pili miradi hii kwamba itaanza mwezi Machi, 2017.
Je, mkanganyiko huo unatokana na nini na majibu hayo yote ambayo sasa hivi inaonekana hayajitoshelezi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa anavyosema Mheshimiwa Mbunge ni sahihi. Kwenye Bunge la mwezi Aprili tulisema kwamba mradi huu utaanza mapema ifikapo mwezi Machi. Hivi sasa bado tupo Januari, hivyo Mheshimiwa Mbunge nadhani avute subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kuhusu suala la fidia; fidia inayotarajiwa kufidiwa wananchi wale inafikia takribani shilingi bilioni 13.34, ni kiasi kikubwa. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kupitia tathmini halisi ya fidia hiyo, halafu baada ya zoezi hilo kukamilika, basi wananchi watalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba yapo masuala ya kimkataba ambayo Serikali pamoja na mwekezaji inayapitia, likiwemo suala la incentives kwa maana ya vivutio, mara baada ya kukamilika, basi mradi huu utaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yetu zoezi hili likikamilika kabla ya mwezi Machi, basi kweli mradi huu utaanza mara moja.
MHE. DEO F. NGALAWA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jumuiya ya Afrika Mashariki ilivunjika mwaka 1977, mpaka
leo hii ni miaka 40. Shirika hili limekuwa likisuasua sana lakini moja kati ya vigezo inavyolifanya lisuesue ni kwamba hela yake ambayo ilitakiwa iingie kwenye operesheni ndiyo hiyo ambayo inatumika kuwalipa wale wastaafu wa Afrika Mashariki. Je, Serikali ina mpango gani sasa hivi kuanza kuwalipa wale wastaafu yenyewe moja kwa moja bila kutumia fedha za shirika? Pili, fedha hizi ambazo tayari Shirika la Posta linaidai Serikali ni lini zitakamilishwa kulipwa kwa sababu imefikia kipindi Shirika linasuasua, ikafikia kipindi hata ule mwaka 2016 Shirika hili lilifungiwa akaunti zake kwa sababu TRA ilikuwa inalidai sh. 600,000,000. Je, kulikuwa na fairness gani ya kufungia zile hela wakati shirika hilo linaidai Serikali shilingi bilioni tano?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza Serikali ina mpango gani wa
kulipa yenyewe, naomba kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali sasa hivi iko kwenye jitihada za kuhakikisha kuwa malipo haya yanalipwa na Serikali yenyewe na kwa kuwa tayari watumishi wote wa Shirika la Posta wanaendelea kuchangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wastaafu hawa wataendelea kulipwa na Mifuko hii badala ya kulipwa tena na Shirika la Posta.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni lini fedha hizi zitalipwa. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba, tutaendelea kulipa kwa kadri fedha zinapopatikana na ni jukumu la Serikali kulipa fedha hizi tunafahamu, tumejipangia mpango itakapofika Juni 30, shilingi bilioni 3.2 zote zitakuwa zimeshalipwa.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa ruhusa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto nyingi za ukaguzi kwenye shule zetu za sekondari, msingi na vyuo vya ualimu, je, Serikali haioni sasa imeshafika wakati wa kuunda mamlaka au taasisi itakayosimamia ubora wa elimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Idara zetu za Ukaguzi wa Elimu, shule za sekondari na msingi zimekuwa zikipata changamoto nyingi hasa za vyombo vya usafiri na watendaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha Idara hiyo ya Ukaguzi ili iweze kufanya kazi yake katika ubora unaotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema awali ni kweli Idara yetu ya Ukaguzi inakabiliwa na changamoto mbalimbali hususan katika ukuaji wa sekta ya elimu kama ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyemiti, mwanzo idara hii ilikuwa inakaguliwa kupitia kwenye kanda zetu, lakini kwa sasa ni kanda pamoja na Wilaya, hata hivyo tunaona kwamba kuna mapungufu kidogo katika mfumo mzima, na ndio maana kupitia mabadiliko haya ya sheria tutaangalia namna bora zaidi ya kuendesha shughuli ya ukaguzi katika shule zetu za primary, sekondari na vyuo. Hali kadhalika kwa upande wa uwezo wa Idara za Ukaguzi, ni kweli kuna mapungufu hasa yanayotokana na vifaa kama vitendea kazi kama magari, ofisi na Wizara imeshaona hilo na tayari tumeshaanza kufanyia kazi, tayari kuna magari yamekuwa yakipelekwa kwenye Wilaya na mwaka huu tumeagiza magari mengine kwa ajili ya kupeleka kwenye Wilaya nyingine na wakati huo huo tunatarajia pia kwa mwaka huu kuanza kujenga angalau ofisi 100 kwa ajili ya wakaguzi katika Wilaya zetu.