Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Rashid Mohamed Chuachua (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa weledi wake katika kuhakikisha juhudi za kujenga Tanzania ya Viwanda zinafanikiwa. Kusini mwa Tanzania ni eneo ambalo viwanda vya korosho vilijengwa kwa kuwa ndiko mali ghafi hii inakozalishwa kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa juhudi za Serikali zinahitajika katika kufufua viwanda hivi kwa ajili ya kuinua uchumi wa nchi yetu pamoja na wakazi wa maeneo husika. Jimbo la Masasi lina kiwanda cha kubangua korosho ambacho hakifanyi kazi kwa muda mrefu sasa. Naomba majibu ya Serikali kuhusu mpango wa kuhakikisha kuwa kiwanda hiki kinafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakusudia kutoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri ikiwa katika majumuisho Serikali haitatoa kauli kuhusu suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOHAMED R. CHUACHUA: Microphone yangu haiwaki hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Serikali kwa mwaka 2016/2017. Kabla sijaanza kuchangia, kwa heshima kubwa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika katika Bunge hili, lakini pia nawashukuru Watanzania wote kwa kukichagua Chama cha Mapinduzi kwa kishindo kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee ninawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Masasi kwa kazi kubwa waliyofanya ya kampeni takribani miezi mitatu, minne hivi katika uchaguzi mdogo. Hawakukata tamaa walifanya kazi usiku na mchana hatimaye CCM imeshinda kwa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa namna ya kipekee, naomba nitumie fursa hii kuwaambia wananchi wa Masasi chaguo walilolifanya ni chaguo sahihi kukichagua Chama cha Mapinduzi, lakini kunichagua mimi mtoto wao ili niwapiganie na tutatekeleza tuliyo waahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Serikali iendelee kuweka nguvu kubwa katika kukusanya mapato. Iendelee kuweka nguvu kubwa katika kuhakikisha kwamba wanakusanya kodi na kuwachukulia hatua wakwepa kodi wote pamoja na kuongeza juhudi zake za kupambana na ufisadi. Haya ni mambo ambayo tukiyafanya kwa nguvu kubwa tunaimani kwamba tunaweza tukasonga mbele kiuchumi.
Vile vile niwashukuru sana wale walioandaa mapendekezo haya na niseme tu mapendekezo haya yameakisi kwa kiasi kikubwa Hotuba ya Mheshimiwa Rais, lakini pia yameakisi kwa kiasi kikubwa ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa mchango wangu katika sekta ya kilimo, kila mmoja wetu hapa anafahamu umuhimu wa sekta hii, namna ambavyo sekta hii ina uhusiano mkubwa sana na Sekta ya Viwanda. Hata hivyo, niseme tu Serikali ina mzigo mkubwa sana kuhakikisha kwamba sekta ya kilimo inasonga mbele na lazima tuelezane wazi kwamba hatuwezi kusonga mbele katika viwanda kama sekta ya kilimo haitapewa uzito mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima kubwa naomba niishauri Serikali lakini pia nimshauri Waziri mwenye dhamana kuwa ana kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba kilimo kinasonga mbele. Tunapozungumzia kilimo tunazungumzia sekta tofauti tofauti, lakini pia tunazungumzia suala la mazao ya biashara. Kwa kweli hali ya manunuzi na mauzo ya mazao yetu ya biashara haijafikia kwenye kiwango cha kutembea kifua mbele. Nasema hivi nikiwa naakisi Jimbo langu la Masasi ambapo mchakato mzima wa ununuzi wa zao la korosho kama zao kuu la biashara umegubikwa na mambo mengi ambayo yanamkandamiza mkulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa Serikali ihakikishe kwamba kama tunataka kusonga mbele katika viwanda basi ni lazima kuhakikisha kwamba tunaondoa kero zote zinazomkandamiza mkulima wa zao la korosho. Zipo kero nyingi, kuna makato yasiyo na sababu za msingi, kuna sheria ambazo kimsingi zinapaswa zifanyiwe marekebisho ili kusudi korosho imnufaishe mkulima na iwe ni zao lenye tija. Pia mchakato mzima wa pembejeo na usambazaji wake nao umegubikwa na mambo ambayo kimsingi yanamkandamiza mkulima. Wapo wanaopata pembejeo ambao hawakustahili pembejeo. Namwomba Waziri mwenye dhamana aliangalie sana eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo deni kubwa kwa Watanzania na tusingependa kusikia tena Watanzania wakiendelea kulalamika kuhusu mazao yao ya biashara. Kero hizi namwomba Waziri mwenye dhamana na Serikali ihakikishe kwamba inaziondoa na tutaisaidia Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanakiona kilimo chao kikiwa kina tija. Pamoja na mambo mengine wakati wote wakulima wetu wamekuwa hawana dhamana ya kuweza kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itoe nguvu kubwa kuhakikisha Benki ya Kilimo inawafikia wakulima, lakini tuhakikishe kwamba rasilimali zao zinarasimishwa ili waweze kupata mikopo, waweze kupata hati miliki na waweze kukopesheka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika Jimbo la Masasi tunacho Kiwanda cha Korosho, kiwanda hiki ni cha muda mrefu tungependa pia kiwanda hiki kiweze kufanya kazi ili wananchi waweze kubangua korosho zao na kuzisafirisha zikiwa zimebanguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengine ya msingi nitazungumzia kuhusu barabara, tunapozungumzia Kusini na mchango wake katika uchumi ni lazima tukumbuke kwamba wakulima wanaweza kurahisishiwa shughuli zao za kusafirisha mazao kama barabara zetu zinapitika. Tunalo tatizo kubwa tumeona katika mpango kuna kilomita kadhaa zilizotengwa kwa ajili ya barabara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningeomba Serikali safari hii iangalie Mikoa ya Kusini ambayo imekuwa ikisahaulika sana kwa ujenzi wa barabara zetu. Zipo barabara zina umuhimu mkubwa kama waliotangulia kusema wenzangu kama vile barabara ya Ulinzi inayotokea Mtwara inakwenda Tandahimba na Nanyamba - Newala inakuja kutokea Nanyumbu, hii ni barabara muhimu sana. Ipo barabara nyingine ya kutokea Mtwara unakwenda unatokea mpaka Jimbo la Lulindi unaingia Jimbo la Masasi hii ni barabara muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa namna ya kipekee tunaiomba Serikali itutengenezee barabara ya Masasi kwenda Nachingwea, tunaomba Serikali itutengenezee barabara inayotoka Jimbo la Masasi inaelekea Jimbo la Ndanda na inakwenda kukutana na Jimbo la Nanyumbu kupitia katika Kata za Mwengemtapika Kata za Mlingula, Kata zote hizo mpaka tunafika katika hayo Majimbo mawili. Hizi ni barabara muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa mazao ya wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango mwingine kwa upande wa elimu, tunalo tatizo kubwa. Katika elimu tunazo changamoto lakini pia tunakila wajibu wa kuishukuru Serikali kwa kazi kubwa iliyofanya. Sisi ambao tumeishi katika Ualimu takribani miaka 15, 16; tunajua namna ambavyo Wananchi wameguswa na suala la Serikali kufanya elimu bila malipo. Hili ni jambo la msingi sana na sote tunapasa kuipongeza Serikali kwa kazi yake kubwa iliyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Waziri mwenye dhamana pamoja na Serikali iangalie namna ambavyo tunataka kuboresha elimu isisahau elimu nje ya mfumo rasmi. Tunapotaka kuboresha elimu, tusifikirie tu kuboresha elimu kwa upande elimu iliyo rasmi, tuangalie pia elimu nje ya mfumo rasmi. Ningeiomba Serikali ifanyekazi pamoja na Wizara husika, kukaa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, ione namna ambavyo inaweza, ikatoa mchango mkubwa katika kuelimisha watu nje ya mfumo ulio rasmi wa elimu. Ni lazima tukubali kwa sasa kwamba tunao Watanzania wengi wasiojua kusoma na kuandika, tunao Watanzania wengi wenye hitaji la elimu lakini wako nje ya mfumo rasmi wa elimu; hawa wanahitaji msaada mkubwa tusije tukawasahau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo tatizo la maji, Mapendekezo ya Mpango yameonesha namna ambavyo Serikali inakwenda kulitatua tatizo la maji. Niseme tu, niishukuru Serikali kwa namna ya kipekee kwa kujumuisha mradi mkubwa wa maji wa Mbwinji na kutaka kutengeneza mipango ya kuuendeleza kwa sababu mradi huu ni muhimu sana, kwa wananchi wa Jimbo la Masasi, lakini pia ni muhimu sana kwa Watanzania. Nawashukuru sana Serikali kwa kuweka mpango huu ili kusudi maji sasa yafike katika vijiji vyote vya Jimbo la Masasi, ambavyo havina maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza kuhusu suala la barabara, lakini ni muhimu kuelewa kabisa, tunapoizungumza Mtwara na miundombinu yake lazima tuzungumzie pia uwanja wa ndege. Uwanja huu umekuwa ukiimbiwa mara nyingi kwamba unahitaji marekebisho ya kina, lakini marekebisho haya yamekuwa hayafanywi. Si jambo zuri mpaka leo tukiwa tunazungumzia uwanja ambao ni uwanja wenye sifa za kuweza pengine kuwa wa Kimataifa, lakini hauna taa. Uwanja huu haujafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu. Tunaiomba Serikali yetu sikivu ifanye kazi katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa katika huduma zetu za afya, katika Jimbo la Masasi zipo zahanati saba tu. Tunajua Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha kwamba kila Kijiji, kila Kata kinakuwa na zahanati, lakini lengo hili halijafikiwa ipasavyo katika baadhi ya maeneo. Tunaiomba Serikali wakati inataka kupiga hatua mbele kuelekea katika uchumi wa kati unaotegemea viwanda, tuangalie pia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Chuachua.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali, Ofisi ya Waziri Mkuu na Waziri Mkuu mwenyewe kwa kazi kubwa na nzuri inayopendeza ya kuandaa hotuba hii ambayo kimsingi inatafsiri kwa kina Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Maendeleo wa mwaka mmoja. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niseme tu kwamba kazi kubwa inayofanywa na Serikali iliyopo madarakani ni kazi ambayo inapaswa kuungwa mkono na sisi Wabunge. Tuiunge mkono Serikali yetu ili tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisahau kusema kwamba wakati tuna harakati za kisiasa, wananchi wangu hawakunituma ili nije kuonekana kwenye tv. Wamenituma nije kufanya kazi kwa sababu wao hawahitaji tv, wanahitaji maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda niiambie Serikali kwamba wakati tunajiondoa kwenye hali ya utegemezi lazima tufahamu kwamba maendeleo haya tunayoyataka ni vita kubwa sana. Hili ni jambo la msingi sana, maendeleo ni vita. Nachukua kauli ya Profesa wangu Mheshimiwa Norman Sigalla King ameandika maendeleo ni vita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo viongozi wengine ni waandamizi, wanazungumza kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Rais wake wanapofanya kazi kubwa ya kuwawajibisha watumishi ambao kimsingi wanatenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma wanakosea, hili ni suala la ajabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema ni suala la ajabu kwa sababu viongozi hao wanafikia hatua ya kudiriki kuzungumza kwamba wanaowajibishwa ni watu wa mkondo fulani wa kisiasa, ni jambo kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais tunamuona anavyofanya kazi na Waziri Mkuu akiwa anawawajibisha viongozi ambao kimsingi wengine ni waandamizi katika Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, lazima tuzungumze mambo ambayo hatuwapotoshi Watanzania. Tukisema hivi maana yake tunataka kuwaaminisha Watanzania kwamba hao wanaoharibu wao ndiyo wamewatuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba wakati Serikali inakwenda kwenye hatua ya maendeleo ya viwanda, naomba waendee katika hatua hiyo wakijua kwamba maendeleo haya ni vita. Unapokwenda kwenye viwanda unahitaji rasilimali kubwa inayozalishwa nchini iende kwenye processing industry, lakini wakati huo huo tunawakwaza Watanzania wenzetu ambao kimsingi tuliwategemea watusaidie, wao kazi yao ilikuwa ni kusafirisha malighafi, wanakwazika na kitendo cha Tanzania kutaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kwenda kwenye uchumi wa viwanda na kuziwezesha sekta zinazotegemea viwanda, wapo Watanzania wenzetu wanaishi hapahapa, wanakwazika na ununuzi wa ndege kwa sababu wana hisa kwenye makampuni mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kuboresha reli tunawakwaza Watanzania wenzetu kwa sababu wengine wana malori, wanataka bidhaa zisafirishwe kwa malori wapate faida hata kama tunadidimia katika uchumi wetu. Maendeleo ni vita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ikaze buti kuhakikisha kwamba inasimamia yale ambayo wameyasema na sisi tutawaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, niseme tu kwamba wakati tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda tunategemea sana kilimo lakini mipango yetu inaonyesha wazi kabisa kwamba mchango wa sekta ya kilimo ni asilimia 25 tu katika Pato la Taifa wakati nguvu kazi iliyopo katika kilimo ni zaidi ya asilimia 74.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ina maana kwamba kiasi kikubwa cha nguvu kazi kipo kwenye kilimo lakini tija ya kilimo bado haiwezi ku-support uchumi wa viwanda. (Makofi)
Naiomba Serikali iliangalie hili na ihakikishe kilimo kinatengewa pesa za kutosha. Wakati wa kuondoa kero kwa wakulima wetu ni sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali kwa kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, alipotembelea maeneo ya Kusini. Amefanya uamuzi mkubwa wa kufuta baadhi ya makato ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa wakulima. Huu ni uamuzi mkubwa sana. Wakulima wetu wamelalamika kwa miaka mingi na tunaendelea kuitia moyo Serikali kwamba iendelee kuona namna ambavyo inaweza kuondoa kero kwa wakulima wa mazao yote yanayotegemewa kukuza uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, tunategemea pia Serikali sasa itoe kipaumbele katika suala zima la pembejeo. Katika bajeti iliyopita, Serikali ilitoa voucher za pembejeo kwa takribani voucher milioni tatu. Mkoa wa Mtwara peke yake ulipata voucher 10,000 tu na Jimbo la Wilaya ya Masasi lilipata voucher 3000. Hili ni jambo ambalo linaweza kuwakatisha tamaa wakulima kwa sababu voucher hizi hazikutosha. Naiomba Serikali iongeze mkazo mkubwa sana katika kuhakikisha kwamba voucher zinatoka za kutosha ili wakulima wetu wapate pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze haraka haraka kwenye suala la elimu. Tunazo changamoto kubwa na Serikali imefanya juhudi kubwa. Mimi naamini kwamba changamoto hizi ni sehemu ya maendeleo. Kwa hiyo, niendelee kuiomba Serikali iendelee kufanya juhudi kubwa, lakini naiomba Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi, iweke msisitizo mkubwa sana kwenye suala la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi. Ukiangalia historia ya elimu ya nchi hii, toka Serikali ya awamu ya kwanza, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa, alifanya kazi kubwa katika eneo la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwa sababu tunahitaji nguvukazi kwenye Sekta ya Viwanda, hatuwezi kuhakikisha kwamba tunawaelimisha Watanzania wengi kwa wakati mmoja kwa kutegemea waingie madarasani. Pia naiomba Serikali ifahamu kwamba kiwango cha Watanzania kutokujua kusoma na kuandika kinaongezeka na vijana wetu wengi hawana elimu ya kutosha. Kwa hiyo, tunaweza tukawa na viwanda vya kutosha lakini tukaishia kwenye kuwa wabeba mizigo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba sana, Serikali yangu ihakikishe kwamba inapanua wigo wa elimu ili wale ambao hawana uwezo wa kwenda kwenye sekta rasmi ya elimu waweze pia kupata elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo changamoto kubwa katika ardhi, lakini juhudi za Serikali za kutaka kuwapimia wananchi tunazipongeza ila tunamwomba kwa heshima kubwa Waziri wa Ardhi afike Jimbo la Masasi ili atatue kero za wananchi wa Masasi. Wananchi wa Masasi wana matatizo mengi katika ardhi na bahati nzuri tumezungumza na Waziri, amesema atapanga muda. Naomba baadaye atuambie ni lini atakwenda ili kusudi wananchi waweze kutatuliwa matatizo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo matatizo katika eneo la afya, lakini pia Serikali imepiga hatua katika kutatua kero za afya kwa wananchi wetu, isipokuwa katika Jimbo la Masasi matatizo bado yapo. Tunaiomba Serikali ihakikishe kwamba katika bajeti ya mwaka huu inatoa pesa za kutosha ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanapata huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze tu suala la ulinzi na usalama. Tunaishukuru Serikali kwa juhudi zake, tunashukuru Serikali kwa kuhakikisha kwamba inawajali Askari Polisi. Isipokuwa katika Jimbo la Masasi, kuna tatizo kubwa. Jeshi la Polisi wanaishi katika maeneo ambayo hayana nyumba. Tunaomba Serikali iangalie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nizungumze tu kwamba Askari wetu wa Jeshi la Kujenga Taifa, tunaomba wapatiwe Bima ya Afya. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Maana naona Walimu tuko wengi sana, nami nimefundisha zaidi ya miaka 15, ni muhimu sana kutoacha bajeti hii ipite hivi hivi bila ya kuwasemea Walimu na elimu kwa ujumla. Kwa nini? Kwa sababu, kimsingi elimu ndiyo injini ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la kwanza ni kuzungumzia maslahi na madai ya Walimu. Tulitoa ahadi na tunaendelea kuitoa ahadi hiyo kwamba tutawatetea Watumishi wa Umma na hili ni jambo la msingi ambalo ni lazima tulifanye. Tumewaahidi tutawatetea na sisi tutafanya kazi hiyo, ila Serikali nayo itimize wajibu wake katika kuhakikisha inatimiza ahadi inazozitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Walimu wana changamoto kubwa. Wapo Walimu ambao wanadai kupandishwa mishahara katika maeneo mbalimbali nchi nzima. Kwa mfano, tu katika Jimbo langu la Masasi Walimu zaidi ya 50 bado wanadai kupandishwa mishahara. Hili ni jambo la msingi na ni lazima Serikali iwajibike kuhakikisha kwamba watu hawa wanapata fursa ya kulipwa mahitaji yao ili waweze kufundisha vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jambo hilo, kimekuwa kilio cha Walimu cha muda mrefu cha kupata posho ya madaraka (responsibility allowances). Tunao waraka ambao umetolewa na utumishi, Waraka Na. 3 wa mwaka 2014, unaotoa maelekezo, toka mwaka 2015/2016 maelekezo hayo yalipaswa kutimizwa kwa bajeti iliyopita, kwamba Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi alipaswa kulipwa shilingi 200,000/= kila mwezi kama posho ya madaraka; Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari shilingi 250,000/=, Mkaguzi wa Elimu Kata ni shilingi 250,000/= lakini Mkuu wa Chuo cha Ualimu ni shilingi 300,000/= kwa mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maneno mazuri tu, tumwambie Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atupe mkakati ukoje katika kutekeleza mahitaji ya waraka huu unaotaka Walimu walipwe responsibility allowances.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, ni muhimu tuliweke wazi suala ambalo kimsingi nchi yetu imepita katika mtikisiko wa kutoka kufanya mabadiliko makubwa ya namna ya kutoa vyeti vyetu kwa wanafunzi wetu wa Kidato cha Nne. Hili ni jambo la msingi sana! Sasa hivi tunao vijana wetu ambao tumeshatikisa standard ya vyeti vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali, sasa iandae utaratibu na Waziri atuambie utaratibu anaokuja nao, tufute vyeti vyote vyenye GPA, badala yake watoto hawa wapewe vyeti ambavyo vina division.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tumeamua kufanya mabadiliko, tumetoka tena kwenye GPA tunakwenda kwenye division, tayari tumeshaathiri watu katika kundi kubwa sana ambao mpaka sasa hivi wanashindwa kutambulika wana standard gani ya elimu katika vyeti vyao. Naomba tuliangalie sana hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo kuhusu Elimu Maalum. Kama kuna eneo ambalo limesahaulika katika nchi hii, ni Elimu Maalum. Ninajua tukisema Shule za Sekondari na Shule za Msingi tutasema ziko katika eneo la TAMISEMI, lakini acha tu tuseme, nami ninaishauri Serikali, iangalie uwezekano wa kuchukua shule hizi za Elimu Maalum na kuzipeleka kwenye Wizara badala ya TAMISEMI ili ziweze kupata jicho maalum la kuziangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukifika katika hizi Shule za Msingi na Shule za Sekondari ambazo zinawasaidia vijana wetu wenye mahitaji maalum, unaweza ukatokwa na machozi. Vijana hawa wanasoma katika mazingira magumu sana. Nadhani hata kama tukienda kwenye theories of learning tunajua kabisa miongoni mwa shule ambazo zilitakiwa ziwe na mazingira rafiki na ya kuvutia ni hizi zenye mahitaji maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu kuna shule mbili za msingi; Shule ya Msingi Masasi na Shule ya Msingi Migongo. Watoto hawa wamesahaulika! Naomba Serikali iangalie namna invyoweza kuziboresha shule hili ili na hawa wenye mahitaji maalum wajione ni sehemu ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mambo hayo, napenda tu kuelezea jambo la msingi kwamba tunaposhughulikia elimu katika nchi yetu, hatuwezi kuweka mkazo moja kwa moja kwenye formal education pekee, yaani kwenye elimu ndani ya mfumo rasmi. Hili nimekuwa nikilisema na leo nalirudia tena. Ninaposoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri sioni inapojitokeza non formal education.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo takwimu kwamba kama asilimia 50 ya Watanzania ni watoto; na kama asilimia 50 ni watoto, maana yake ni takriban milioni ishirini na kitu. Kama waliopo katika mfumo rasmi wa elimu ni milioni 12 tu, ni wazi kabisa kuna kundi kubwa la watu ambalo haliwezi kufikiwa bila ya kushiriki nje ya mfumo rasmi wa elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie, hatuwezi kutumia madarasa yetu pekee kutoa elimu ya sekondari. Naiomba Wizara iangalie namna ambavyo inaweza ikazitumia taasisi zake kama vile Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuhakikisha kwamba watoto wengi ambao wanakosa kuingia katika elimu rasmi, waende nje ya mfumo rasmi wa elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ya kuyaangalia katika hilo. Nimekuwa nikisema, Waziri naye sasa hivi atakuwa na dhamana kubwa ya kuhakikisha tunakuja na mikakati ya kupunguza kiwango cha watu ambao wako nje ya mfumo wa elimu, wasiojua kusoma wala kuandika, wengine ni watu wazima; nao pia tuwaelimishe, tusizingatie tu elimu rasmi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ya kuzungumza, lakini niseme tu kwamba hali ya elimu tunaendelea kujikokota, tunakwenda, lakini yako mambo ambayo bado ni changamoto. Katika Jimbo la Masasi tuna tatizo kubwa la Walimu wa Shule za Msingi. Tunahitaji Walimu takriban 252; hatuna hata Mwalimu mmoja wa kufundisha Shule ya Awali, katika Walimu wa sayansi kiwango cha sekondari tuna matatizo makubwa. Tunapungukiwa Walimu zaidi ya 60, haya ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto tulizonazo, pamoja na juhudi kubwa tunazofanya za kutoa elimu bila malipo, lakini pia tuongeze nguvu katika kutatua changamoto zinazotukabili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi, huo ndiyo mchango wangu. Naunga mkono hoja. Naomba Mheshimiwa Waziri aje na majibu ambayo yatatupa imani. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia kwenye Wizara hii adhimu kwa mustakabali wa afya za Watanzania. Nitumie pia fursa hii kumpongeza Waziri na timu yake kwa hotuba nzuri waliyoitoa, inayoonesha mwelekeo wa suala zima la utekelezaji wa sera ya afya katika awamu hii.
Mheshimiwa Spika, ninapoiangalia Wizara ya Afya, nashindwa kabisa kutenganisha majukumu yake na TAMISEMI na kwa maana hiyo basi kama majukumu hayo tunaweza tukayatenganisha katika actual practice, acha tuseme katika kiwango hiki cha kuchangia, ili tuweze kueleza matatizo na changamoto zilizopo katika Wizara ya Afya, halafu hao wenyewe kwa sababu Serikali ipo, watagawana, watajua hiki ni cha TAMISEMI na hiki ni cha Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema maneno haya, niseme tu kwamba kama ningekuwa napata fursa ya kuangalia changamoto za Wizara zote, basi Wizara ya Afya ningesema namba moja, inawezekana katika Majimbo mengine ni tofauti, lakini katika Jimbo langu Wizara ya Afya ni Wizara ambayo ina changamoto kubwa sana kuliko Wizara nyingine zote.
Mheshimiwa Spika, jambo hili kwanza linatupeleka katika kuhakikisha kwamba, fedha wanazoomba zinapatikana na zinafika kwa wakati. Pili, ni jambo ambalo nadhani linatakiwa liwekewe msisitizo maalum na Serikali ili kila mwaka tusiendelee kuimba changamoto za Watanzania katika eneo hili la afya.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwa kuakisi moja kwa moja Jimbo la Masasi ambalo kimsingi Jimbo hili kabla halijagawanywa na hata kabla ya Wilaya haijagawanywa tulikuwa tuna Hospitali moja tu ya Wilaya inaitwa Hospitali ya Mkomaindo. Tumegawanya Wilaya na sasa tuna Wilaya ya Nanyumbu, Hospitali kubwa ni ile ile. Tumegawanya Majimbo, lakini bado tunategemea hospitali moja. Hospitali ambayo inahudumia watu wa Wilaya takribani mbili, pamoja na watu wanaotoka nje ya nchi ya Tanzania kwa upande wa Msumbiji. Ni hospitali iliyoelemewa sana.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tunapozungumza, hospitali hii ina changamoto kubwa ya dawa, hospitali hii ina changamoto kubwa ya vifaa tiba na hospitali hii ina changamoto kubwa ya majengo. Labda tu nitoe mfano, tunayo wodi ya wazazi ambayo kwa mwaka hospitali hii inapokea takriban wazazi 4,200, ina vitanda 10 tu. Hii ni changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, nina imani kwamba, mwanamke ndiye kiumbe anayekwenda hospitali mara nyingi zaidi kuliko mtu yeyote. Kama hatutaangalia kwa jicho la kipekee huduma zinazowagusa wanawake, hatuwezi kusema tumepiga hatua katika sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali liwe suala hili linahusu TAMISEMI au liwe linahusu Wizara ya Afya, waje na majibu, ni lini upanuzi wa wodi ya akinamama katika Hospitali ya Mkomaindo utafanyika ili kusudi akinamama hawa wasilale chini au wasilale wawili wawili? Mheshimiwa Ummy amefika Hospitali ya Mkomaindo ameiona. Mheshimiwa Jafo pia amefika, ameiona na changamoto zake. Tunaomba tupate majibu ya Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba huduma zinasogea karibu na wananchi, tunaiomba Serikali izipandishe hadhi baadhi ya zahanati zinazozunguka Jimbo la Masasi ili kusudi kuisaidia Hospitali ya Mkomaindo. Naomba ipandishwe hadhi zahanati ya Mwengemtapika, zahanati ya Mombaka na zahanati nyingine ya Chisegwe, tuwe na vituo vya afya. Wenyewe mtagawana majukumu mjue ni nani ambaye anahusika na kupandisha zahanati hadhi na nani anahusika na kuwepo kwa zahanati hizo. Naiomba Serikali iangalie eneo hili.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza hapa, Jimbo la Masasi lina takribani ya mitaa na vijiji 60 na zaidi, lakini tunazo zahanati tano tu. Tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi wa afya, tunapungukiwa na watumishi 400 na kibaya zaidi kama wiki mbili zilizopita watumishi 19 tena wamesimamishwa kazi kwa kosa la kughushi vyeti na kwa maana hiyo, hatuna kabisa watumishi. Naomba Serikali iliangalie hili na ilifanye kama jambo la dharura, hali sio nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na haya yote niliyoyaeleza, lakini tuna magari mawili tu kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa. Haiwezekani, mambo hayawezi kwenda. Tunaiomba Serikali na hili nalo iliangalie.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 kuna ubadhirifu wa fedha ulifanyika na baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Mkomaindo, fedha za dawa. Naiomba nayo Serikali itoe majibu, hatua gani mpaka sasa zimeshachukuliwa? Shilingi milioni 29 hazijulikani zilitumika vipi. Naomba Serikali itoe majibu hatua ambazo imezichukua ili wale wanyonge waendelee kupata matibabu.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala la utekelezaji wa huduma za afya bure kwa wazee, nalo jambo hili ni zito na gumu sana katika Jimbo langu. Hapa ninapozungumza toka mwezi wa Kwanza hakuna hata shilingi iliyopelekwa kwa ajili ya kuwahudumia wazee katika Jimbo la Masasi. Wazee hawa wanapata shida, wanawaona madaktari kwa shida na wakiwaona hawapati dawa. Kwa hiyo, tunakosa kuona umuhimu wa kuwepo hilo Dirisha la Wazee. Naomba pia Serikali iliangalie hili kama ni suala la Serikali Kuu au kama ni suala la Serikali za Mitaa, lakini sisi shida yetu watu wa Masasi, wazee wapate huduma zao.
Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi katika Wizara hii hatuwezi kuyamaliza yote, lakini kimsingi na kwa namna ya kipekee tuone namna ambavyo Serikali inatoa msisitizo maalum katika kuboresha vyuo vyetu vya maendeleo. Tunavyo vyuo takribani 55 ni vyuo vichache nchi nzima, tunahitaji vyuo hivi viongezwe, lakini kikubwa zaidi vyuo hivi havina wataalam na havina vifaa vya kutosha.
Mheshimiwa Spika, nadhani umefika wakati sasa pamoja na pendekezo la vyuo hivi kwenda Wizara ya Elimu, lakini lazima utoke msisitizo maalum kuhakikisha kwamba vyuo hivi ndivyo ambavyo tutakuja kuvitegemea kwa ajili ya kutengeneza vijana watakaoingia kwenye soko la ajira tunapokwenda kwenye uchumi wa viwanda. Vyuo vilivyopo chini ya mamlaka ya VETA havitoshi na kwa maana hiyo, vyuo hivi vina nafasi kubwa sana. Naomba Serikali itazame vyuo hivi, kikiwemo chuo kilichopo katika Jimbo langu cha Masasi FDC. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema yako mambo mengi, nimeongea kwa kifupi. Naunga mkono hoja, lakini naiomba sana Serikali ije na majibu ya maswali niliyoyauliza. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. RASHIDI M. CHUACHUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa na nzuri ya kusambaza na kusimamia nishati ya umeme. Hata hivyo, naomba ufafanuzi Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa chanzo cha nishati ya umeme wa gesi katika Mkoa wa Mtwara, hali ya usambazaji wa umeme hairidhishi. Pale ambapo umeme umefika hali ya kukatikakatika kwa umeme inaendelea kuwakatisha tamaa wananchi wa Mikoa ya Kusini hususani Wilaya ya Masasi. Kwa kweli ikiwa nishati ya mwanga wa kibatari inayoweza kuzimika kwa upepo wakati wowote inapaswa iwe tofauti na ile ya umeme. Kwa sisi watu wa Masasi inatuwia vigumu kutofautisha kutokana na kukatikakatika kila wakati bila ya taarifa yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atueleze hali hii itakwisha lini? Je, Serikali haioni sababu ya kuwa na njia mbadala ya umeme ambayo kwa sasa umeme unaokuja Masasi unapitia Tandahimba, Newala - Masasi kuelekea Nanyumbu? Matatizo yoyote ya umeme katika maeneo hayo yanatuathiri mara kwa mara wananchi wa Masasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo tatizo kubwa la kutofanyiwa marekebisho au matengenezo ya nyumba za wafanyakazi wa TANESCO zilizopo katika Kata ya Migongo, Jimbo la Masasi. Nyumba hizi zinageuka kuwa magofu wakati watumishi wanahangaika mahali pa kukaa. Naomba nijue mkakati wa Serikali kuhusu nyumba hizi ?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakushukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia leo tarehe 21 Mei kwenye hotuba ya Wizara ya Ardhi, inayoongozwa na Mheshimiwa William Lukuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 143. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake anaonyesha kwamba maeneo ya ardhi yaliyonunuliwa na Shirika la Nyumba la Taifa hadi Aprili, 2016 katika Wilaya mbalimbali nchini, Jimbo langu linajitokeza katika Wilaya ya Masasi ambapo Shirika la Nyumba limejenga nyumba chache pale na inaonekana eneo hili ni la ekari 16 na kwamba walilinunua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho, aweke sawa taarifa hizi, kama kulipa fidia ya shilingi milioni 22 katika eneo la ekari 16 ndio kununua eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, naomba pia Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake, atuambie ni vigezo gani Shirika la Nyumba wanavitumia katika kulipa fidia ya eneo lililopo katika mji kwa shilingi 22,500,000 kwa eneo la ekari 16 za wananchi ambao wamehamishwa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lililopita, Mheshimiwa Waziri alituelekeza tuorodheshe migogoro iliyopo katika maeneo yetu. Mimi binafsi niliunda kikosi kazi na tukaorodhesha migogoro mbalimbali iliyopo katika maeneo ya Mji wa Masasi wakati wananchi wa eneo la Kata ya Mtandi, Migongo, Napupa, Mkomaindo, Jida, Mkuti na Mwenge Mtapika, wamekuja wakaleta malalamiko yao mengi, tukapata orodha ya wananchi takribani 1,123. Kwa pamoja wananchi hawa wanadai fidia ya zaidi ya shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha migogoro, jambo hili halipo. Sasa naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni mgogoro mkubwa kwa kiwango gani unatakiwa uoneshwe kwamba ni mgogoro ambao umedumu kwa takribani miaka kumi kwa sasa, wananchi hawa wanaendelea kuhangaika, wamehamishwa kwenye maeneo yao na hawajapewa fidia?
Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu ametupa documents za kusoma, nataka pia tujaribu kuangalia hizo sheria ambazo zinawaruhusu watumishi wa Idara ya Ardhi kupima maeneo ya wananchi, kuwahamisha maeneo hayo, kuyauza kwa watu wengine na kujenga nyumba zao, halafu wananchi hawa wanaendelea kuidai Serikali fidia. Hizi ni sheria za kutoka wapi? Tunaomba pia Mheshimiwa Waziri aweze kutupatia ufafanuzi wa jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Masasi wanakusubiri. Sisi Wabunge tunapofikia hatua ya kuleta migogoro kwako, maana yake migogoro hii imekuwa ni sugu na viongozi waliopo katika Halmashauri zetu wameshindwa kuishughulikia, ndiyo maana yake! Kwa sababu hatuwezi kuwa na migogoro miaka kumi, kila siku tunazungumza haya haya, mpaka leo hayajapatiwa ufumbuzi.
Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufanya hitimisho, utuambie utakuja Masasi lini ukae na wananchi wa hizi Kata nilizozizungumza hapa waweze kulipwa mahitaji yao? Hali yao siyo nzuri na wanasubiri kauli yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Masasi limepitiwa na barabara ya kutoka Masasi kuelekea Nachingwea. Pambezoni mwa barabara hii ambayo kwa sasa inasubiri upanuzi, wapo wananchi ambao tayari wameshafanyiwa tathmini ya eneo hili. Kwa maana hiyo, wanatakiwa kupisha upanuzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini hii imefanywa muda mrefu na sasa ni miaka mingi imepita, wananchi hawa wameambiwa watalipwa fidia zao ili watafute maeneo mengine ya kukaa, lakini mpaka sasa hivi wananchi hawa wapo stranded hawajui wafanye nini kwa sababu hawajalipwa fidia zao. Mheshimiwa Waziri kwa sababu eneo la fidia linakuhusu wewe, naomba utoe ufafanuzi, ni lini Serikali itawalipa fidia zao wananchi hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nilipokuwa napitia makabrasha ya Wizara ya Ardhi, sijaona mipango ya upimaji wa miji hususan Mji wa wa Masasi. Naamini kwamba harakati za upimaji wa mji na kuyarasimisha makazi ni jambo muhimu sana kwa sababu kadri tunavyozidi kusonga mbele ndivyo wananchi wetu wanavyozidi kujenga kwenye makazi holela na kwa maana hiyo, hatua zetu za upangaji wa miji zinazidi kuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atoe pia ufafanuzi, mpango huu hasa ukoje? Ni maeneo yapi na ni lini Mji wa Masasi nao utaingia katika mpango huu wa upimaji ili kusudi wananchi wakae katika maeneo yaliyorasimishwa waweze kupata umiliki wa maeneo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya machache, namuomba Waziri akija hapa atoe ufafanuzi wa maeneo hayo niliyoyaeleza na mimi naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kusema kwa kifupi ili nitoe mchango wangu kwenye mapendekezo ya mpango. Kwanza kabisa tuipongeze Serikali kwa sababu kilicholetwa hapa ni mapendekezo na kama tukitoa mapendekezo mazuri yatafanya mpango wetu uwe bora zaidi kwa ajili ya bajeti ya mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumza katika maeneo mawili; kwanza nitazungumzia suala la kilimo, katika kuzungumzia suala la kilimo nitajikita kwenye miradi ya kimkakati. Katika ukurasa wa 43 tumeelezwa kwamba mradi namba saba utakuwa ni kuimarisha kilimo cha mazao ya chakula na malighafi nakadhalika. Mimi ninaomba niishauri Serikali eneo hili lisomeke kuimarisha ushirika na kilimo, tusiache ushirika, nikiangalia mpango huu sioni namna unavyozungumzia kwa kina suala la ushirika. Katika kipindi kifupi na uzoefu tulioupata wa kuwatetea wananchi katika majimbo yetu tunaona kwa kiwango kikubwa kabisa wakulima wanategemea ushirika, lakini ushirika lazima uimarishwe na usimamiwe vizuri ili kusudi wakulima wetu waweze kupata tija ya mazao wanayolima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa kusimamia vema suala la kilimo, mauzo na manunuzi ya zao la korosho kwa msimu wa mwaka huu, hili ni jambo kubwa kwa sababu bei ya korosho imepanda lakini bado kuna changamoto za hapa na pale ambazo kimsingi tunapenda Serikali iziangalie kwa kina. Nitazisema kwa kifupi, jambo la kwanza katika msimu wa korosho uliopita wananchi wa Mikoa ya Kusini wamepata shida kubwa baada ya vyama vya msingi kukata fedha kwa wakulima wetu. Fedha hizi ni nyingi na tunaomba Serikali ichukue hatua ya haraka ili wakulima walipwe fedha zao ambazo zilikuwa zimekatwa katika msimu uliopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ripoti iliyoandaliwa na TAKUKURU inaonyesha kwamba takribani shilingi bilioni 30 hazijulikani zilipokwenda, lakini bodi ya korosho imeeleza takribani shilingi bilioni 11 hazijulikani zilipokwenda katika Mikoa ya Kusini. Cha kushangaza bado wale wale waliohusika na wizi wa namna hii wanaendelea tena kusimamia mfumo wa mwaka huu. Wakulima wanaendelea kuuza korosho zao, lakini jicho lao lipo kwa Serikali ni namna gani watu hawa watachukuliwa hatua ili fedha zao zirudishwe na hatua zichukuliwe kwa ajili ya ubadhilifu mkubwa uliofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala lingine la msingi ambalo linapaswa kuangaliwa katika ushirika, katika msimu wa mwaka huu mazao mchanganyiko yameuzwa kwa bei holela mno. Tunaiomba sasa Serikali ije na mpango madhubuti wa kuona namna gani mazao mchanganyiko kama vile mbaazi, ufuta, choroko zitauzwa kwa bei inayofaa na kwa utaratibu unaoeleweka ili wakulima wetu waweze kupata manufaa makubwa, tunaiomba Serikali ilisimamie jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi ninapochangia katika eneo la elimu nimekuwa nikisema jambo ambalo na leo nitalisema, nina imani Serikali yangu sikivu italisikia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoiangalia elimu tunapaswa kuiangalia elimu kwa jicho pana sana tusiiangalie elimu kwa mtazamo wa elimu rasmi peke yake. Nimekuwa nikilisema hili mara nyingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia utaratibu wenyewe wote wa kuendesha elimu rasmi uliowekwa katika mpango wetu unaonesha wazi kabisa kuna kundi kubwa la watu tunaowaacha, ambao kwa msingi huo hawatapata elimu kwa muda mrefu sana na baadaye tutakuwa na kundi kubwa la watu ambao hawajaelimika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia sensa ya watu ya mwaka 2012 tunaona kwamba takribani watu wazima milioni 5.5 hawawezi kusoma na kuandika. Lakini pamoja na hilo tukiangalia tena idadi ya watu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, wa Mwaka 2016
MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kupata fursa hii na mimi nichangie kidogo kwenye Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo. Ni imani yangu kwamba tukiwa na good legal framework na good institution framework kwa pamoja tunaweza tukafikia malengo yetu. Kwa maana hiyo basi, lazima sheria zetu zitupeleke katika kujenga msingi mzuri wa namna ya kuziendesha taasisi zetu. Nasema hivi nikiwa na maana kwamba sheria hii inapaswa ituongoze katika kuzisimamia pia taasisi zetu na kuzijengea misingi imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sheria hii tunaambiwa kabisa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kumteua Mwenyekiti wa Bodi. Kuwa na mamlaka ya kumteua Mwenyekiti wa Bodi siyo tatizo, lakini tatizo linatokea pale ambapo sheria haoinyeshi sifa za Mwenyekiti wa Bodi. Nimesoma sheria mbalimbali zinaonesha wazi vigezo ambavyo Mwenyekiti wa Bodi anatakiwa awe navyo ili aweze kuchaguliwa hususani tunapowaweka Wenyeviti wa Bodi ambao wanakwenda kuongoza Bodi zinazolenga weledi wa namna fulani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo basi, ni muhimu sheria yetu ifikirie Mwenyekiti wa Bodi awe na sifa zipi ili awe Mwenyekiti wa Bodi husika. Nitaleta schedule of amendment mezani na nina imani Wabunge wataunga mkono namna ambavyo tunatakiwa tuangalie vigezo vya kuwateua Wenyeviti wa Bodi kwa sababu wana mamlaka makubwa ya ku-influence maamuzi ya Bodi hizi. Kwa hiyo, ni vyema wakawa na weledi wa eneo ambalo wanaliongoza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, Kamati husika imeeleza namna ambavyo kuna mgongano wa kimajukumu kati ya Tume ya Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi hii tunayoitengenezea sheria. Kwa maana hiyo basi, napenda kama kuna uwezekano sheria hii itambue kuwepo kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma sheria yetu hii hakuna mahali ambapo Tume ya Sayansi na Teknolojia inatambuliwa. Ni lazima tujiulize, je, kuna umuhimu wowote wa taasisi hii ya utafiti katika kilimo kutoa taarifa angalau za mwaka au kila mwaka kwa Tume kuhusiana na tafiti inazofanya au inazozisimamia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo lingine la msingi, kuna taasisi hii ambayo ina vituo vya utafiti. Vituo hivi vya utafiti vimetajwa kwenye sheria lakini havijawekewa majukumu yake ya msingi. Nimesoma sheria ya Uganda, Kenya, Malaysia na nchi nyingine vituo vya utafiti vya namna hii majukumu yake yamekuwa stipulated kwenye sheria husika. Jambo hili limesaidia sana kuhakikisha kwamba vituo hivi vinakuwa na majukumu yaliyoko kwenye sheria hata kama wanatekeleza majukumu mengine wanayopewa na Bodi au Director General lakini wakati huo huo wanayo majukumu yao ya msingi. Ni muhimu tuyataje katika sheria ili vituo hivi viweze kufanya kazi zake kwa weledi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo lipo tatizo kubwa la kutopelekwa kwa taarifa za matokeo ya utafiti kwenye grass roots, hili nalo ni jambo la msingi sana. Sheria yetu haioneshi ni wakati gani vituo hivi vya utafiti vinalazimika kupeleka matokeo ya utafiti walioufanya kwa wananchi ambao kimsingi ndiyo consumer wa matokeo yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo manne nadhani kama yatazingatiwa tutakuwa katika mstari mzuri wa kuendelea kuiboresha sheria yetu. Ahsante sana.