Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rashid Mohamed Chuachua (16 total)

MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ili usambaze maji katika vijiji vyote vya Jimbo la Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Safi wa Masasi – Nachingwea kutoka chanzo cha Mbwinji unahudumia wakazi wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya Vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Nachingwea na Ruangwa. Jumla ya wakazi wapatao 188,250 wanahudumiwa. Mradi huo uliojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 40 na kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, tarehe 24 Julai, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma za maji katika Wilaya ya Masasi, Mradi wa Masasi – Nachingwea unakusudiwa kuendelea kufanyiwa upanuzi wa miundombinu ili kuunganisha vijiji vingi zaidi na huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Masasi inaendelea na kazi ya kuunganisha maji katika vijiji vilivyo katika Jimbo la Masasi ambavyo viko mbali na bomba kuu linalopeleka maji katika Mji wa Masasi ili kuongeza upatikanaji wa maji kupitia mradi wa Masasi – Nachingwea. Kwa sasa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa miundombinu ya maji katika Vijiji vya Nangaya, Nangose, Temeke na Marokopareni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwenye Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) ili vijiji vingi zaidi ya Jimbo la Masasi vipate maji.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Kumekuwepo malalamiko kwa upande wa huduma za afya kwa wanajeshi wetu ambao kimsingi hawana Bima ya Afya kwa sababu Jeshi lina zahanati na hospitali.
Je, Serikali haioni haja ya kuwapatia wanajeshi Bima ya Afya?
SPIKA: Naomba tuendelee kwa sababu kwa kweli Mheshimiwa Naibu Waziri ameshajibu na swali hili pia katika majibu yake swali la 10 limeshapata majibu. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, swali la Mheshimiwa Juma Kombo Hamad, Mbunge wa Wingwi.
Hitaji la Shule za Kidato cha Tano na Sita Jimbo la Masasi

Jimbo la Masasi lina shule moja tu ya sekondari kwa kiwango cha kidato cha tano na sita, ambayo ni Sekondari ya Wasichana Masasi, ambayo imekuwa haitoshelezi kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaofaulu:-
(a) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi shule za sekondari za Mwenge Mtapika na Sekondari ya Anna Abdallah ili ziweze kupokea wanafunzi wa kidato cha tano na sita?
(b) Je, ni lini Serikali itaajiri walimu katika Jimbo la Masasi ikiwa Ikama ya walimu wa sayansi katika shule za sekondari tisa zilizopo ni walimu 84 lakini waliopo ni 24 tu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashidi Mohamed Chuachau, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuwa na shule za sekondari ya kidato cha tano na sita kila tarafa. Halmashauri ya Mji wa Masasi imeteua shule mbili za sekondari, ambazo ni Anna Abdallah na Mwenge Mtapila ili ziweze kuboreshwa na kuwa za kidato cha tano na cha sita. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri imetenga shilingi milioni 140 ili kuanza upanuzi wa miundombinu ya majengo ya shule hizo ikiwemo bwalo la chakula, jiko na huduma za maji na umeme. Aidha, Halmashauri imewasilisha andiko katika Mamlaka ya Elimu Tanzania yaani TEA kwa ajili ya maombi ya fedha shilingi milioni 125 za kukamilisha ukarabati wa miundombinu hiyo ya shule.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi katika Halmashauri ya Mji wa Masasi ni walimu 60. Serikali imeendelea kuwapangia vituo walimu wa masomo ya sayansi kadri wanavyohitimu na kufaulu mafunzo yao katika vyuo ili kukabiliana na upungufu huo. Mkakati tulionao kama Serikali ni kuongeza udahili wa walimu wa masomo ya sayansi katika vyuo ili kukidhi mahitaji kwa nchi nzima. Halmashauri ya Mji wa Masasi itapangiwa walimu wa sayansi na kila mara tutakapo kuwa tunaajiri walimu hao ili kupunguza pengo lililopo hivi sasa.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Sera ya Serikali ya kujenga zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata haijatekelezwa vyema katika Jimbo la Masasi ambapo hakuna kata yenye kituo cha afya cha Serikali na zahanati zilizopo ni saba tu:-
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa zahanati na vituo vya afya katika kata 14 za Jimbo la Masasi?
(b) Je, Serikali inaweza kukiri kuwa kuna haja ya kuzipandisha hadhi Zahanati za Chisegu, Mumbaka na Mwenge Mtapika ili ziwe na vituo vya afya na hatimaye kuipunguzia mzigo Hospitali ya Mkomaindo pamoja na kusogeza huduma kwa jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa zahanati kila kijiji, vituo vya afya kila kata na hospitali kila wilaya unafanywa na Halmashauri kwa kushirikisha nguvu za wananchi kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD - Opportunity and Obstacle to Development). Kazi hii inafanyika kwa awamu katika Halmashauri zote, kulingana na bajeti iliyotengwa kila mwaka. Halmashauri ya Wilaya ya Masasi katika mwaka wa fedha 2015/2016 imeweka kipaumbele katika ujenzi wa zahanati ya Namatunu, Makarango, Mtaa wa Silabu ambao unaendelea. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 70 kwa ajili ya umaliziaji wa zahanati hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, inafanya tathmini ya miradi ya zahanati na vituo vya afya ambavyo havijakamilika pamoja ili kubaini vijiji na hata ambazo hazina miundombinu hiyo ili kujua gharama halisi zinazohitajika kumaliza miradi hiyo au kuanza ujenzi mpya.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kupandisha zahanati kuwa vituo vya afya, Halmashauri imeshauriwa kuanzisha mchakato huo kupitia vikao na kuwasilisha mapendekezo hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kupata kibali.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na uchakavu wa vitendea kazi pamoja na kukosekana kwa magari ya kutosha:-
(a) Je, ni lini Serikali itawapatia magari Askari Polisi wa Wilaya ya Masasi ili kupunguza ugumu wa mazingira ya kazi?
(b) Je, ni lini Serikali itarekebisha utaratibu uliopo ambapo inafikia wakati askari wanalazimika kutoa pesa zao mfukoni ili kuwapa chakula mahabusu?
(c) Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za askari katika Wilaya ya Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Wilaya ya Masasi kina magari mawili yanayohudumia Wilaya nzima. Hata hivyo, Serikali inatambua kuwa magari hayo hayatoshelezi mahitaji ya Wilaya. Aidha, Serikali inatarajia kupokea magari kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi wakati wowote kuanzia sasa na mara magari hayo yatakapowasili, Wilaya ya Masasi itakuwa miongoni mwa Wilaya zitakazogawiwa magari hayo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia mahabusu wanapokuwa mikononi mwa polisi ili kupata huduma muhimu za kijamii. Mathalani katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuhudumia mahabusu walioko vituo vya polisi, mwaka wa 2016/2017, Serikali ilitenga zaidi ya shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuhudumia mahabusu walioko Vituo vya Polisi Tanzania Bara na Zanzibar.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua tatizo la ukosefu wa nyumba za askari hapa nchini. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali ina mpango wa ujenzi wa nyumba kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha. Ndiyo maana Serikali inao mpango wa kujenga nyumba 4,136 kwa kupitia mkopo wa bei nafuu kutoka Serikali ya China kupitia Kampuni ya Polytech utakaogharimu dola za Kimarekani milioni 500.
MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. RASHID M. CHUACHUA) Aliuliza:-
Mfumo mzima wa ununuzi wa zao la korosho kuanzia kwenye ngazi ya Vyama vya Msingi umegubikwa na dhuluma na ukandamizaji mkubwa wa haki za mkulima kwa kila hatua. Hali hiyo imesababisha malalamiko yasiyokwisha ya wakulima wa korosho kila mwaka. Malalamiko ya wakulima ni uwepo wa makato yanayomuumiza mkulima, kutokuwepo kwa uwazi katika kumpata mshindi wa tender, kujitoa kiholela kwa makampuni yanayosababisha kushuka kwa bei ya korosho, kutolipwa kwa bei halali inayouzwa mnadani kwa Vyama vya Msingi, rushwa katika kila ngazi, pamoja na njama kati ya benki na kampuni zinazonunua korosho.
(a) Je, ni lini Serikali itaondoa na kushughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho?
(b) Je, ni lini Serikali itadhibiti usambazaji wa pembejeo za ruzuku kwa watu ambao sio wakulima wa korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUZI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na
(b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshashughulikia malalamiko ya wakulima wa korosho kwa kuondoa makato yasiyokuwa muhimu kama vile kufutwa kwa ushuru wa shilingi 20 kwa kilo kwa ajili ya Chama Kikuu cha Ushirika; shilingi 50 za usafirishaji wa korosho; shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya mtunza ghala na shilingi 10 kwa kilo kwa ajili ya kikosi kazi cha masoko. Aidha, tasnia ya korosho ina utaratibu maalum wa kupanga bei dira kwa kutumia vigezo vinavyokubaliwa kwa wadau wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu manunuzi ya pembejeo za korosho hufanywa kwa pamoja na vyombo rasmi ndani ya tasnia, awali ilikuwa ikisimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Korosho na sasa Bodi ya Korosho Tanzania. Kuhusu changamoto za namna ya kufikisha pembejeo hizo kwa wakulima wa korosho, hatua zimechukuliwa kwa kushirikisha Vyama vya Ushirika ili kudhibiti mianya ya pembejeo kwenda kwa wasio walengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu usambazaji wa pembejeo za korosho ambazo ni sulphur ya unga na dawa za wadudu, Serikali imeweka mfumo wa usambazaji wa pembejeo wenye lengo la kuhakikisha kwamba pembejeo hizo zinawafikia walengwa pekee. Utaratibu huo unazingatia kutambua wakulima wenye uhitaji wa pembejeo na hununuliwa kwa kutumia utaratibu wa ununuzi wa pamoja (bulk purchase system) na kusambazwa kwa wakulima kwa kutumia wakala walioteuliwa na kuthibitishwa na Halmashauri husika ambazo huwa zimeandaa orodha ya wanufaika.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zinazopoteza fedha nyingi kwa ajili ya misamaha ya kodi ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki kwa kigezo cha kuvutia wawekezaji na katika hotuba ya Bajeti 2013/2014 ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Mheshimiwa William Mgimwa alisema misamaha ya kodi kwa mwaka 2011/2012 ilifikia asilimia 4.3 ya pato la Taifa:-
(a) Je, hali ya misamaha ya kodi ikoje kwa sasa ikilinganishwa na ile ya mwaka 2011/2012?
(b) Kwa mujibu wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Mwaka 2009/2010 Tanzania ilipoteza asilimia 15 ya pato lililotarajiwa kukusanywa iwapo misamaha isingetolewa, 2010/2011 asilimia nane na kwa mwaka wa 2011/2012 asilimia 27; je hali ya misamaha ikoje kuanzia mwaka 2013/2014 hadi sasa.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi inayotolewa na Serikali hutolewa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi zilizopo. Baadhi ya huduma zinazotolewa katika jamii hazistahili kulipiwa kodi kwa sababu hazina manufaa ya kibiashara.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Mashirika ya Dini yanapata misamaha ya kodi kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) 2014, sehemu ya pili ya jedwali kifungu cha nane (8), kwa sababu huduma zinazotolewa na taasisi hizo hazina faida ya kibiashara kama ilivyo kwa kampuni za kibiashara. Pamoja na hatua nzuri zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza misamaha ya kodi, ni vyema ikafahamika kwamba si kila msamaha wa kodi una madhara hasi katika jamii na uchumi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, misamaha ya kodi kama sehemu
ya asilimia ya Pato la Taifa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013/2014 hadi sasa imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka. Misamaha hiyo ilikuwa asilimia 2.2 ya Pato la Taifa mwaka 2013/2014; asilimia 1.9 ya Pato la Taifa mwaka wa 2014/15; na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa katika mwaka wa 2015/16. Aidha, misamaha ya kodi ikilinganishwa na mapato ya kodi imepungua kutoka asilimia 18 ya mwaka 2013/2014 hadi kufikia asilimia 8.6 ya mapato yote ya kodi katika mwaka 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inaendelea kupitia Sheria, Kanuni na Taratibu za misamaha ya kodi mwaka hadi mwaka ili kuhakikisha kuwa misamaha yote isiyokuwa na tija inafutwa na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza mapato kwa ajili ya kupeleka huduma za maendeleo kwa wananchi wetu.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Katika Jimbo la Masasi, Kata za Marika, Mumbaka, Matawale, Sululu, Mwenge, Mtapika, Temeke na Chanikanguo, kuna tatizo kubwa la maji wakati eneo la katikati ya mji linanufaika na maji ya mradi wa Mbwinji.
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa maji wa Mbwinji ili usambaze maji katika vijiji vya Jimbo la Masasi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Jimbo la Masasi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Safi wa Masasi, Nachingwea kutoka chanzo cha Mbwinji unahudumia wakazi wa Miji ya Masasi na Nachingwea pamoja na baadhi ya vijiji vya Halmashauri za Wilaya ya Masasi Nachingwea na Ruangwa. Jumla ya wakazi wapatao 188,250 wanahudumiwa na mradi huo uliojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 31 na kuzinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 24 Julai, 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kuunganisha vijiji zaidi ili kuongeza upatikanaji wa maji kupitia mradi huo. Kwa sasa baadhi ya vijiji katika Kata za Marika, Mumbaka, Matawale, Sululu, Mwenge, Mtapika, Temeke na Chanikanguo, vimeanza kupata maji na vijiji vilivyobaki katika Kata hizo vitaendelea kuunganishwa kutoka kwenye mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuendelea kuunganisha vijiji vilivyobaki na katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali imetenga shilingi bilioni moja ambapo hadi sasa shilingi milioni 370 zimeshatolewa kwa ajili ya kuendelea kuunganisha vijiji vilivyobaki kwenye Mradi wa Masasi, Nachingwea.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiahidi kusimamia Sera ya Viwanda ili Tanzania iwe na uchumi wa kati, lakini hakuna jitihada za wazi za kufufua viwanda vya korosho ili kuongeza thamani halisi ya zao hilo na kutengeneza ajira.
(a) Je, ni lini Serikali itahakikisha Kiwanda cha Korosho cha Masasi kinafanya kazi?
(b) Kwa kuwa utaratibu wa ununuzi wa korosho hauruhusu viwanda kununua korosho kutoka kwa wakulima; je, ni lini Serikali itafungua mlango ili kukuza viwanda hivyo ili vipate fursa ya kununua malighafi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Korosho cha Masasi ni moja ya viwanda vilivyobinafsishwa na kuuzwa kwa Kampuni ya BUCCO Investments Holdings Limited ambayo ilishindwa kukiendesha kutokana na benki ya CRDB kuzuia mali za kiwanda baada ya kiwanda kushindwa kurejesha mkopo waliokopa. Hatimaye kiwanda kiliuzwa na CRDB kwa Kampuni ya Micronix Export Trading Co. Ltd., kwa njia ya mnada. Kwa kuwa BUCCO hawakuridhika na utaratibu uliotumika kuuza kiwanda hicho, walifungua kesi mahakamani na kuishtaki benki ya CRDB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kesi iliyopo mahakamani uendelezaji wa kiwanda hicho umeshindikana hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi wa kesi husika. Serikali inaandaa mazungumzo na wadau wa viwanda vyote ambavyo vina kesi mahakamani kikiwemo Kiwanda cha Korosho Masasi ili kuharakisha utatuzi wa migogoro iliyopo na hatimaye kuwezesha uwekezaji kuendelea ili vianze uzalishaji haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijakataza viwanda kununua korosho kutoka kwa wakulima, bali imekataza ununuzi wa korosho kufanyika kiholela kutoka kwa wakulima. Kwa kuwa lengo ni kusimamia maslahi ya wakulima na wadau wengine wa zao la korosho, Serikali ilianzisha utaratibu wa kuuza korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Mfumo huo haulengi kuvififisha viwanda bali kuwanufaisha wakulima na wadau wengine ikiwa ni pamoja na wenye viwanda. Kutokana na mfumo huo, korosho zilizohifadhiwa kwenye maghala huweza kutumika kama malighafi ya viwanda kwa mwaka mzima. Aidha, wakulima wanafaidika na bei shindani na udhibiti katika ubora wa korosho unakuwa ni wa uhakika.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
• Je, ni lini Serikali itaondoa kabisa malalamiko yanayotokana na makato, rushwa, uwazi na matatizo mengine yaliyopo katika mfumo mzima wa ununuzi wa zao la korosho?
• Je, ni lini Serikali itaondoa utaratibu wa wakulima kulipwa mara mbili na badala yake walipwe pesa zao mara moja na wasubiri bonus baadae?
• Ni lini Serikali itadhibiti usambazaji wa pembejeo kwa watu ambao siyo wakulima wa korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, makato yanayotokana na biashara ya zao la korosho yapo kwa mujibu wa sheria na mjengeko wa bei ambayo huamuliwa na wadau wa zao la korosho. Aidha, makato mengine ni kwa ajili ya maendeleo ya Mikoa na Halmashauri za Wilaya zao la korosho linakozalishwa.
Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilifuta tozo tano na katika bajeti ya mwaka 2017/2018 Serikali imefuta tozo mbili zilizokuwa zinatozwa kwenye biashara ya zao la korosho. Vilevile Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria Namba. 6 ya Vyama vya Ushirika ya mwaka 2013 pamoja na sheria nyingine za nchi ikiwemo kuwavua madaraka na kuwachukulia hatua za kisheria viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika wanaotuhumiwa kushiriki katika vitendo vya ubadhirifu, rushwa na ukiukwaji mwingine wa sheria, kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa malipo kwa wakulima wa zao la korosho kwa sasa hivi hufanyika mara moja tu. Aidha, malipo kwa wakulima waliouza korosho hulipwa kwenye akaunti za vyama vikuu vya ushirika kutoka kwa makampuni yanayonunua korosho kupitia minada. Baadae fedha hutumwa kwenye akaunti za benki za vyama vya ushirika vya msingi na hatimae kulipwa kwa mkulima mmoja mmoja kupitia akaunti yake ya benki.
Mheshimiwa Spika, Serikali inadhibiti usambazaji wa pembejo za zao la korosho kwa watu ambao sio wakulima wa korosho kwa kutumia sensa ya wakulima wa zao la korosho (wanachama na wasio wanachama wa vyama vya ushirika). Sensa hii inawezesha kujua mahitaji halisi ya pembejeo kwa wakulima wa korosho.
Aidha, pembejeo inayoonekana kwa watu ambao sio wakulima wa korosho, inatokana na wakulima wa zao la korosho ambao siyo waaminifu.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Jimbo la Masasi lina shule moja tu ya sekondari kwa kiwango cha Kidato cha Tano na Sita ambayo ni Sekondari ya Wasichana Masasi nayo imekuwa haitoshelezi kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaofaulu:-
(a) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi Shule za Sekondari za Mwenge Mtapika na Anna Abdallah ili ziweze kupokea wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita?
(b) Je, ni lini Serikali itaajiri Walimu katika Jimbo la Masasi ikiwa ikama ya Walimu wa Sayansi katika Shule za Sekondari tisa zilizopo ni Walimu 84 lakini waliopo ni 24 tu?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mji wa Masasi inazo shule tisa za sekondari. Kati ya hizo, ni shule moja tu ya Masasi wasichana ndiyo ya Kidato cha Tano na Sita. Katika jitihada za kutatua changamoto hiyo, Halmashauri ya Mji wa Masasi imeteua shule mbili za sekondari za Anna Abdallah na Mwenge Mtapika kwa ajili ya upanuzi na kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo bwalo la chakula, mabweni na jiko ili kuwezesha shule hiyo kuanza kuchukua wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri imewasilisha andiko la mradi wa kukamilisha miundombinu hiyo kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ajili ya maombi ya fedha za kukamilisha miundominu ya shule hizo. Mara baada ya kukamilika kwa miundombinu hiyo, taratibu nyingine za kuziwezesha shule hizo kuanza kuchukua wanafunzi wa Kidato cha Tano na Sita zitakamilishwa.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutatua changamoto ya Walimu wa Sayansi, Serikali imepeleka Walimu tisa wa masomo ya sayansi katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mwaka 2017 ili kupunguza uhaba wa Walimu wa Sayansi. Serikali iko kwenye mchakato wa kuajiri Walimu 5,870 wa Shule za Sekondari na watapangwa kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Masasi.
MHE. HAWA A. GHASIA (K.n.y. MHE. RASHIDI M. CHUACHUA) aliuliza:-
Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Masasi halina nyumba za makazi na usafiri kwa muda mrefu sana:-
a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea askari hao nyumba za kuishi kwa sababu nyumba wanazoishi sasa zimechakaa sana na pia hazitoshelezi mahitaji yao?
b) Je, ni lini Serikali itawapatia usafiri wa uhakika Askari hao ili waweze kusimamia usalama wa raia na mali zao kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la uhaba wa nyumba za makazi kwa Askari wa Jeshi la Polisi nchini ikiwemo Wilaya ya Masasi. Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kupunguza tatizo la makazi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wananchi na wadau kujenga nyumba kwa ajili ya makazi ya Askari.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itajenga nyumba za kuishi Askari kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Wilaya ya Masasi ina magari matatu ambapo kati ya hayo magari mawili ni mabovu. Jeshi la Polisi hugawa magari kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo hali ya uhalifu, sababu za kiutawala na jiografia ya mahali husika. Kwa kuzingatia vigezo hivyo hususani jiografia yake, Wilaya ya Masasi itapewa kipaumbele katika mgao wa magari mara yatakapopatikana.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Jeshi la Polisi limekuwa likifanya kazi katika mazingira magumu sana kutokana na uchakavu wa vitendea kazi pamoja na kukosekana kwa magari ya kutosha:-

(a) Je, ni lini Serikali itawapatia magari Askari Polisi wa Wilaya ya Masasi kutokana na kutokuwa na magari ya kutosha?

(b) Je, ni lini Serikali itarekebisha utaratibu uliopo ambapo askari wanalazimika kutoa pesa zao za mfukoni kuwapa chakula mahabusu?

(c) Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za askari katika Wilaya ya Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uhaba wa vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na uchache wa magari. Kwa sasa Wilaya ya Masasi imeshapatiwa gari moja aina ya Leyland Ashok, hivyo kufanya kuwepo kwa magari matatu ambayo ni PT 1865, Toyota Landcruiser, PT 4011 Grand Tiger na Leyland Ashok. Gari hili jipya litatumika kwa shughuli mbalimbali kama doria na operesheni kubwa. Aidha, kutokana na jiografia ya Wilaya ya Masasi, Jeshi la Polisi litaiongezea Wilaya ya Masasi magari kwa kadri yatakavyopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna utaratibu waAskari Polisi kutoa pesa zao mfukoni kwa ajili ya chakula cha mahabusu, bali utaratibu uliopo ni kwamba Serikali kupitia Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuwapatia chakula mahabusu waliopokorokoroni ingawa pia ndugu za mahabusu wanaruhusiwa kuwapelekea chakula jamaa zao walioko korokoroni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Masasi ina nyumba za makazi ya askari zipatazo 15 ambazo zinaishi familia za askari 30, ingawa ni kweli askari wengine wapatao 154 bado wanaishi uraiani. Hata hivyo, Serikali itaendelea kujenga nyumba za makazi ya Askari kwa awamu kwa kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Mkoa wa Mtwara una jumla ya Vijiji 869 na Vitongoji 1,826 na jumla ya Vijiji 372 vimethibitishwa kupatiwa umeme ikijumuishwa kufanya Vijiji vitakavyosalia kuwa 497 na hii ni sawa na wastani wa 23.6% ya utekelezaji wa huduma kwa kila Wilaya ndani ya Mkoa.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza miradi ya REA katika mkoa huu?

(b) Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Mji wa Masasi ilitengewa Vijiji saba tu kati ya Vijiji 31, je, ni lini vijiji vilivyobaki vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini katika vijiji vyote vya Tanzania Bara. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2021. Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unaoendelea unapeleka umeme katika vijiji 167 vya Mkoa wa Mtwara.

(b) Mheshimiwa Spika, katika Halmashauri ya Mji wa Masasi mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza unatekelezwa katika vijiji saba ambapo hadi kufika Januari, 2020 vijiji vitatu vya Mumbaka, Mlundelunde na Chanikanguo vimewashiwa umeme. Aidha, mkandarasi anaendelea na kazi za mradi katika Vijiji vya Mayula, Minazini, Mtakuja na Nangose A na B. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi zitakamilika mwezi Aprili, 2020. Gharama za kupeleka umeme katika Wilaya ya Masasi ni shilingi milioni 658.

Mheshimiwa Spika, vijiji 20 vilivyobaki katika Wilaya ya Masasi vinatarajia kupelekewa umeme kupitia mradi wa REA III Mzunguko wa pili unaotarajiwa kuanza mwezi Februari, 2020. Mradi huu utakamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Jimbo la Masasi lina Shule moja tu ya Sekondari ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita ambayo ni ya Kitaifa ingawa mahitaji ya Wanafunzi wanaofaulu kwenda Kidato cha Tano na Kidato cha Sita yameongezeka sana, Shule pekee ya Kidato cha Tano na Kidato cha Sita iliyopo Masasi ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Masasi:-

(a) Je, ni lini Serikali itazipandisha hadhi Shule za Sekondari za Mwenge Mtapika na Anna Abdallah ili ziweze kupokea Wanafunzi wa Kidato cha 5 na 6;

(b) Jimbo la Masasi linahitaji vyumba 27 vya maabara ambapo hadi sasa vyumba Saba tu ndiyo vina vifaa vya maabara katika shule Nne; Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa vya maabara katika Shule zote za Sekondari?

(c) Ikama ya Walimu wa Sayansi katika shule za Sekondari Tisa zilizopo Jimbo la Masasi ni Walimu 84 japokuwa waliopo ni 24 tu; Je, Serikali inaweza kulifanya jambo hili kama dharura inayohitaji utatuzi wa haraka kwa kutuletea Walimu 60 wa Sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi Mjini, lenye sehemu (a), (b), na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Masasi Mji inafanya jitihada kuziwezesha shule tatu za Sekondari ambazo ni Sululu, Mtapika na Anna Abdallah ili ziweze kupandishwa hadhi na kuanza kutoa elimu ya Kidato cha Tano na cha Sita. Tayari shule hizo zilishakaguliwa na wadhibiti ubora wa shule na kukutwa na mapungufu kadhaa, hasa ya miundombinu ya maji, umeme na mabweni na hivyo kukosa sifa. Halmashauri kwa kushirikiana na wadau inafanyia kazi mapungufu hayo ili shule hizo ziweze kupandishwa hadhi na kutoa elimu tarajiwa.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya shule za sekondari 1,800 zilizokamilisha ujenzi wa maabara zilipelekewa vifaa vya maabara, na kati ya hizo shule sita ni za Halmashauri ya Mji wa Masasi. Vilevile katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, jumla ya shule 1,258 zilizokamilisha ujenzi wa maabara zitapelekewa vifaa vya maabara na taratibu za manunuzi zinaendelea ambapo shule tatu kati ya shule zitakazopatiwa vifaa hivyo zipo katika Halmashauri ya Mji wa Masasi.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2018/2019, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 7,515 katika shule za sekondari nchini. Kati yaoWalimu ni 7,218 na Fundi Sanifu Maabara ni 297. Kati ya walimu walioajiriwa walimu wenye mahitaji maalum ni 29, walimu wenye elimu maalum ni 50, walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni 7,089 na walimu wa lugha (Literature in English) ni 100. Ambapo walimu 15 wa sayansi walipangwa katika Halmashauri ya Mji wa Masasi. Ahsante.
MHE. DKT. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-

Mwaka 2017/2018 kulitokea mauaji ya vijana wa bodaboda katika Wilaya ya Masasi ambapo vijana wanaokaribia kuwa zaidi ya kumi wameuwawa kikatili na kunyang’anywa pikipiki:-

Je, nini kauli ya Serikali kuhusu matukio haya katika Wilaya ya Masasi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kuwa kulikuwa na mauaji ya vijana zaidi ya 10 katika Wilaya Masasi. Kwa mwaka 2017/2018 kulikuwa na matukio manne ya mauaji yaliyotokea na kuripotiwa katika vituo vya Polisi Wilaya ya Masasi. Hata hivyo, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kutokomeza uhalifu huo kwa kuwakamata watuhumiwa wote ambao wamekuwa wakijihusisha na uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo mauaji. Hatua hizi ni pamoja na kufanya doria na misako ya mara kwa mara katika maeneo tofauti katika Wilaya ya Masasi kutoa elimu kwa waendesha bodaboda juu ya tahadhari ya kuwabeba abiria usiku na kushirikisha jamii yote katika kuwafichua wahalifu walio kati yao ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.