Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jerome Dismas Bwanausi (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hoja hii ya Waziri wa Fedha.
Kwanza, niwashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Lulindi ambapo katika uchaguzi uliopita nilishinda Ubunge kwa asilimia 87. Siri kubwa ya ushindi katika uwakilishi kwa wananchi ni kupunguza maneno na kufanya kazi na kuondoa kero kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua zote anazoanza katika kuhakikisha Taifa hili linaelekea kwenye uchumi wa kati, nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapa pole sana wapiga kura wangu kwa maafa waliyopata kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika vijiji vya Matogoro kule Msanga, Mkangaula, Lupaso na maeneo mengine ambayo sikuyataja, nawapa pole sana na nataka kuwahakikishia kwamba nipo pamoja nao katika mkasa huu uliowapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda moja kwa moja katika hoja, nianze kuzungumzia kuhusu mapato. Kwanza, nimpongeze sana Waziri wa Fedha na Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa jinsi ambavyo imejipanga kuhakikisha kwamba tunakusanya mapato ya kutosha ili tuweze kwenda kuondoa kero za wananchi ambapo kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri huduma kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Wizara ya Fedha na watendaji, baadhi ya watendaji wengi hapa nchini wanashindwa kuwa wabunifu wa vyanzo ni kwa sababu wenyewe wanaendelea kupata riziki yao kwa maana ya mshahara na wanaendelea kupata pensheni baada ya kustaafu, wako tofauti kabisa na taasisi za binafsi ambapo wenzetu wamekuwa wabunifu sana. Mimi naomba sana tuhakikishe tunakuwa wabunifu na kupata vyanzo vipya vya mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunacho chanzo kikubwa sana cha mapato ambacho hatukitumii cha property tax. Mheshimiwa Mnyika atakubali kule Dar es Salaam tunazo nyumba nyingi sana kama zingeweza kulipa property tax vizuri na tukawaweka katika makundi mawili, wale ambao tunaweza kutathmini nyumba zao lakini wale ambao tunaweza kuwaweka katika kundi la ukadiriaji na tukakadiria katika kiwango ambacho mwananchi anaweza akalipa, ni chanzo kikubwa sana cha mapato. Naomba Wizara na Halmashauri ziweze kuona ni jinsi gani tunaweza tukakusanya mapato kutoka kwenye chanzo hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuziwezesha halmashauri zetu kuweza kukusanya mapato ni jambo lingine. Kwa mfano, Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi, tarehe 23 Januari, 2013 nilipata janga kubwa sana la watu waliovamia Halmashauri na kuchoma magari 11 lakini pia kuchoma ofisi tano. Serikali ilituahidi kwamba halmashauri yetu ingeweza kupata fidia ya shilingi 1,337,000,000/= lakini tangu mwaka 2013 hadi sasa Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu sana. Kwa hiyo, hata viwango tunavyopangiwa kukusanya tunapata ugumu mkubwa sana. Namwomba Waziri wa Fedha, namuona Naibu yupo, hebu chukueni jambo hili ili kuhakikisha kwamba Halmashauri hii inapata fidia ili tuweze kununua magari, tuweze kutengeneza majengo yale ili ifanye kazi yake inavyostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye suala zima la barabara. Barabara ni jambo muhimu sana na sisi wote tunajua. Kwa mikoa ya Kusini sisi ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho na moja ya barabara ambayo ni ya kiuchumi ni ile inayotoka Mtwara – Newala - Tandahimba - Masasi kupitia Lulindi. Barabara hii imeahidiwa na Mheshimiwa Rais na ipo kwenye Ilani na tayari kuna dalili za kuanza kujenga barabara hii.
Naiomba sana Wizara ya Fedha na Wizara ya Miundombinu kuhakikisha katika miaka mitano barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingine ni barabara ya Ulinzi. Katika miaka mitano iliyopita tumezungumza sana juu ya barabara ya Ulinzi ambayo inapita kwenye zaidi ya Majimbo manne. Jimbo Mtwara Vijijini kwa Mheshimiwa Hawa Ghasia, kwa Mheshimiwa Mkuchika, kwa Mheshimiwa Katani kule Tandahimbi, kwangu kwenye Jimbo la Lulindi na kwa Mheshimiwa Dua kule kwenye Jimbo la Nanyumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ilikuwa na madhumuni makubwa mawili, kwanza ilikuwa ni barabara ya ulinzi. Wakati ule tunapigana na Mreno kule Msumbiji barabara hii ndiyo ilitumika vizuri sana kuhakikisha kwamba tunapambana naye. Pia tulianzisha vijiji vya ulinzi katika barabara yote hii lakini vijiji vile vyote havipati huduma ya barabara kwa sababu tuliiombea iingizwe kwenye TANROADS lakini hadi sasa Wizara haijakubali. Namuomba sana Waziri anayeshughulika na Wizara hii ya Miundombinu tuhakikishe kwamba barabara ile tunaiweka TANROADS ili iweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka nilieleze ni suala zima la umeme. Nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Muhongo, tulikuwa wote kwenye Kamati ya Nishati na Madini, kwa kweli kazi yake kila mmoja wetu hapa tunakiri ni kazi iliyotukuka, hongera sana Mheshimiwa Profesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Profesa ameeleza hapa kwamba wanatagemea kwenda Mtera kufanya tathmini ya REA I na REA II, yako mambo ambayo ningeomba mkayazungumzie. Kwanza, ni kwamba kwenye REA I na REA II idadi ya wananchi wanaotakiwa kupewa umeme kwa bei ya shilingi 27,000/= ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji. Kwa hiyo, jambo hili ni muhimu sana mkalizungumzie ili kuhakikisha kwamba idadi ile inaongezeka kulingana na hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ambalo limejitokeza ni kwamba wakati vijiji vinavyowekwa kwenye mradi wale wanaokwenda kufanya survey wanaacha vijiji vya katikati bila kuviingiza kwenye mpango, jambo ambalo linatusumbua sana wakati mpango ukiendelea. Ningeomba sana Profesa hili mkalishughulike kwa nguvu zenu zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari kengele ya kwanza imeshagongwa, nichukue fursa hii kuzungumzia suala la viwanda. Kule Kusini zao letu la korosho linahitaji kuongezewa value lakini itategemea na jinsi ambavyo tutaanzisha viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri mwenye dhamana afanye juhudi katika miaka mitano hii kuhakikisha kwamba viwanda vya korosho vinafufuliwa katika Mikoa ya Kusini ili korosho ipewe thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuokoa muda, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu. Nianze tu kwa kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nianze kwenye sekta ya kilimo ambayo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imo kuanzia ukurasa wa 26 hadi 32. Nijikite kwenye zao la korosho. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, ndugu yangu Majaliwa Kassim, kwa kazi kubwa sana aliyoifanya wakati alipofanya ziara kule Ruangwa na kutoa tamko la Serikali la kuondoa tozo tano ambazo zilikuwa ni kero za wananchi, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tatizo la korosho ambalo ni zao la pili kwa kuiingizia pato Serikali yetu, ukiacha tumbaku ambayo ni ya kwanza. Lakini hali ya wakulima wetu Mheshimiwa Waziri Mkuu anajua, hali za wakulima wetu ni hali mbaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna sakata linaloendelea katika Wilaya ya Masasi ambalo wakulima hawajalipwa fedha zao kati ya shilingi 200 hadi shilingi 400 kwa kila kilo, lakini hadi sasa kuna wingu ambalo halieleweki wakulima wale watalipwa lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linawafanya wakulima wetu wawe katika mazingira magumu sana. Wanahangaika, wanapalilia, wanapulizia, wanakwenda kuokota korosho zao, wanapeleka kwenye Vyama vya Msingi, vinakwenda kwenye Vyama Vikuu na hadi pale kupata soko, lakini baadhi ya wachache wakiwemo baadhi ya Maafisa Ushirika ambao siyo waaminifu wanashirikiana na baadhi ya Viongozi wa Bodi za Wakulima wa Vyama vya Msingi kuwaibia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa Wilaya ya Masasi safari hii tumesema tunahitaji fedha walipwe wakulima, nani amechukua, ameziweka wapi, hiyo siyo hoja yetu! Ninamshukuru sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Mwigulu baada ya mazungumzo naye amekubali kufanya ziara kwenda Masasi kujionea hali halisi na ninaamini kabisa kwa utendaji wake mzuri ataweza kuwaridhisha wakulima wale na kuwapa matarajio na mategemeo makubwa jinsi ambavyo Serikali inajitahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ili kuwasaidia wakulima wa korosho katika mikoa yote ambayo inalima korosho ni lazima kufanya reshuffle ya Maafisa wa Ushirika. Maafisa wa Ushirika waliokaa katika Mkoa wa Mtwara sasa wamekaa wengine zaidi ya miaka 10 wengine miaka 15, katika mazingira hayo wanatengeneza mtandao wa kutengeneza hata Bodi za Wakulima kule kwenye Vyama vya Msingi na kuhakikisha wanajipatia kipato kutokana na hali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanyie kazi hili kwa nguvu zake zote ili kumfanya mkulima sasa ajengewe matumaini kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ni Serikali inayowajali wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sekta ya afya. Nimesoma kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, amesisitiza sana jinsi ambavyo Serikali itajitahidi sana kuhakikisha kwamba inaboresha sekta ya afya, nimueleze tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, sasa hivi ameelekeza kwenye ukurasa wa 55 kwamba tujitahidi sana tuhakikishe tunawahamasisha wananchi waweze kujiunga na Bima ya Afya. nimthibitishie tu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo zimeshaanza kufanywa na wananchi wamehamasika lakini nina mashaka juu ya jambo hilo, kukakatishwa tamaa wananchi kwa sababu wamekata Bima, lakini wanapokwenda kwenye zahanati zetu hakuna dawa! hivyo hawaoni umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kama hawapati dawa kwenye zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ijikite kuhakikisha kwamba haya yote yanakwenda sambamba, tunahamasisha suala la Bima ya Afya, lakini tunaongeza dawa kwenye zahanati zetu na watendaji wetu ili wananchi wawe na uhakika kwamba wakienda zahanati wanapata dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka niliseme ni juu ya suala la barabara. Mheshimiwa Waziri Mkuu umeelezea juu ya jitihada ya Serikali jinsi ambavyo itaimarisha sekta ya barabara lakini nataka tu nikuhakikishie Mheshimiwa kwamba wananchi wanaimani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano sana, haya yote mnayoyasema na mnayotuambia tunakubali kwamba awamu hii mambo mengi yatatekelezwa, lakini nasisitiza suala la barabara kutoka Mtwara - Newala - Tandahimba hadi Masasi ambayo ni barabara ya uchumi. Napenda Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ujenzi atekeleze agizo la Mheshimiwa Rais alilolisema ataweka wakandarasi wanne ili kuhakikisha barabara hiyo inamalizika kwa haraka ili kutatua tatizo lililoko pale. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu katika maelezo hayo ambayo umetupa matumaini lakini kuna suala la barabara ya kutoka Masasi kwenda Nachingwea ambayo inaunganisha hadi Ruangwa hadi Nanganga kwenye Jimbo la Mheshimiwa Waziri Mkuu. Barabara hii tumeisemea muda mrefu, kwa kweli kuna kila sababu barabara hii ijengwe. Ni barabara muhimu inaunganisha mikoa miwili, ni barabara ya uchumi na kwa hakika wewe mwenyewe huwezi kujisemea, sisi lazima tuseme kwamba barabara hii sasa tunataka ijengwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nijikite katika eneo hilo lakini pia nimalizie kwenye sekta ya elimu. Mimi niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu bahati nzuri alikuwa mwalimu. Naamini kilio cha walimu sasa kitapewa kipaumbele. Kilio kile ambacho kwa kweli muda mrefu wao wamekuwa wakilalamikia kuhusu marupurupu yao, kuhusu nyumba, kuhusu stahili zao nyingine, hatutegemei Serikali ya Awamu ya Tano walimu wawe ni sehemu ya manung’uniko kama ilivyokuwa miaka mingine.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hili lipewe kipaumbele ili Walimu waweze kupewa umuhimu katika jamii na ndiyo sekta ambayo inaajira pekee kuliko sekta nyingine na Walimu ni wengi naamini kabisa Serikali hii na Walimu wameshaanza kuwa na imani, tuendelee kuwapa imani zaidi ili wafanye kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hotuba ya Waziri Mkuu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru kunipa nafasi na mimi ili ukayasikie tena mambo ya korosho.
Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, lakini pia Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo na Watendaji wa Wizara kwa jinsi ambavyo mmejipanga kurudisha imani katika Wizara hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua juhudi za Mheshimiwa Waziri Mwigulu ambazo anazifanya na wananchi wana imani kubwa sana kwa jinsi ambavyo ameonyesha njia na mipango thabiti ya kuhakikisha kwamba wakulima na wavuvi wanaanza kuneemeka kwa kupata kipato kizuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sakata la korosho Masasi. Mheshimiwa Waziri, mimi niendelee kukushukuru na ninamshukuru sana Mrajisi, namshukuru sana Katibu Mkuu wa Wizara, ndugu yangu Turuka kwa kuanza kulichukulia kwa umakini mkubwa suala la sakata la korosho katika Wilaya Masasi. Mheshimiwa Waziri, sakata hili ambalo wewe mwenyewe umeahidi kwenda kulisikiliza kule, takriban zaidi ya shilingi bilioni tatu, wakulima wale hawajuwi watazipata lini. Mchezo huu wa kuwadhalilisha wakulima na kuwanyima haki zao haujaanza leo. Ni wa miaka mingi, lakini mwaka huu Mheshimiwa Waziri wamekufuru kuchukuwa hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa umakini wa Serikali ya Awamu hii ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye amesema Serikali hii ni ya kuwajali wanyonge na watu ambao wako kule chini, ninao uhakika kabisa kwamba Serikali itaingilia kati suala hili na kuhakikisha wakulima wale wote ambao wanaelekea kudhulumiwa wanalipwa stahili zao inavyostahili! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelipokea sana kwa shangwe kubwa tamko la Waziri Mkuu juu ya kupunguza zile tozo, lakini nataka kutoa angalizo, wananchi wamefurahi sana kuona jinsi ambavyo korosho sasa zitaweza kuuzwa kwenye maghala yao. Kama hatukujipanga vizuri kuhakikisha bodi inaweka watalaam wa korosho kule katika kila ghala kuangalia ubora wa korosho kwa kuziweka katika grade zinazostahili na kuhakikisha zinawekwa vizuri, tutajikuta baadaye tunakwama katika suala zima la soko la korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni imani yangu katika miezi hii michache iliyobaki, Bodi ya Korosho kwa kushirikiana na Mfuko, lakini pia kwa kushirikiana na Wizara, ijipange vizuri. Umebaki muda mfupi, tujipange vizuri ili azma ya Serikali ya kumfanya mkulima wa korosho apate bei nzuri mwaka huu iweze kutimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana Wizara hii ijielekeze sana katika kuhakikisha kwamba Mfuko wa Wakulima wa Korosho unajielekeza kutumia zaidi kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya korosho kuliko matumizi ya kawaida. Ingewezekana kabisa, bodi kwa kushirikiana na Mfuko ikaongeza fedha kwenye ruzuku ya mbolea na kuwafanya wakulima wengi zaidi wapate punguzo la bei ya pembejeo kuliko ilivyo sasa. Na mimi naomba sana Mfuko wa Wakulima wa Korosho ni lazima ufanye kazi yake kwa uwazi zaidi kuliko ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotolewa kupelekwa kwenye Mfuko wa Wakulima wa Korosho ambayo inatokana na export levy ni fedha nyingi sana, lakini sijuwi kama Serikali inaziangaliaje fedha zile tunazozipeleka kule kwa maana ya kuzikagua, lakini kuhakikisha kwamba matumizi yasiyo ya lazima yanaepukwa ili ule Mfuko ufanye kazi yake ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nielekee kwenye suala zima la kilimo katika Bonde la Mto Ruvuma. Kama kuna maji ambayo hatuyatumii mpaka yanaelekea baharini ni maji ya Mto Ruvuma. Yale maji tungeweza kuyatumia kwa kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili bonde lile litumike kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya chakula, lakini yale maji yote yanatiririka kwenye bahari na wala hatuna mpango wala scheme kubwa ya kuhakikisha kwamba maji yale tunayatumia. Naomba sana Mheshimiwa Waziri katika mipango yako hebu tujaribu kuangalia uwezekano huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumzie kuhusu Maafisa Ugani. Katika kipindi changu cha siasa nimefanya kazi kwenye ngazi za chini, kuanzia chini kabisa; Mwenyekiti wa Mtaa, Diwani, Meya hadi sasa. Nilichobaini ni kwamba Maafisa Ugani wengi tunawalipa mishahara bila kufanya kazi. Ni lazima wale Maafisa Ugani tunaowapeleka kwenye Kata, Maafisa Kilimo na Maafisa Mifugo, waonyeshe mpango wa kazi. Unamkuta wakati mwingine baadhi ya maeneo, siku Mheshimiwa Mbunge unakwenda ndiyo na yeye anajitambulisha mbele ya wananchi. Wananchi hawamjui! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima Wizara isimamie kuhakikisha wale Maafisa Ugani kule chini kwa kweli wanafanya kazi, lakini kuwe na utarabu hata wa kwenda kuwakagua shughuli gani ambazo wanazifanya za kila siku katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hakika wananchi wangependa sana kuendelea na mfumo huu ambao hivi sasa upo wa pembejeo za ruzuku. Naiomba Wizara, kama haijajipanga vizuri, utaratibu huu wa kusambaza pembejeo za kilimo kwa maana ya ruzuku usitishwe mpaka mtakapojipanga vizuri! Hakuna sababu Serikali inapeleka fedha kwa ajili ya kuwapa wachache wanaoweza kutumia zile fedha kwa njia za udanganyifu! Hakuna sababu! (Makifi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mawakala wengi sio waaminifu hata kidogo! Wenyewe wanashirikiana na baadhi ya wachache ambao sio waaminifu katika vijiji kusaini kwamba wamepokea mbegu pamoja, ambapo hawakufanya hivyo, yaani hawapokei! Wanakwenda kuziuza tena zile pembejeo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia. Wizara ya Kilimo kama haijajipanga vizuri kwa muda huu mfupi kabla ya msimu ujao wa kilimo, iache, isubiri mwakani ikijipanga vizuri! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja Masasi. Naomba katika mahitimisho yake atuthibitishie Wanamasasi kwamba lini tunakwenda ili kukutana na wananchi wale ili tuwaondelee matatizo waliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kukushukuru nami kuwa miongoni mwa Wabunge ambao wanachangia hotuba hii ya Waziri wa Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Maji, Naibu wake na watendaji wa Wizara ya Maji kwa jinsi ambavyo mnafanya kazi sasa kwa kujituma ili Watanzania waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wengine wanaosema kwamba tatizo siyo Waziri, tatizo ni upatikanaji wa fedha katika Wizara hii. Katika bajeti ya mwaka jana 2015/2016 ni asilimia 19 tu ya fedha ambazo zilipangwa kwenda Wizara hii zilipelekwa. Niwaeleze Waheshimiwa Wabuge kwamba hata hizi fedha mnazoziona sasa hazitokani na fedha za miradi ya maendeleo zilizopangwa, hizi ni fedha zinazotokana na Mfuko wa Maji ambao Waheshimiwa Wabunge tuliopita tuliuanzisha mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge kama kweli tunataka maji yapatikane na tuweze kupata fedha zetu kutoka Wizara ya Fedha bila vikwazo ni lazima tuongeze fedha kwenye Mfuko wa Maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetoa ushauri na mapendekezo kwamba angalau mwaka huu tozo ya kwenye mafuta kutoka shilingi 50 iwe shilingi 100, kwa hakika Waheshimiwa Wabunge, tuunge mkono hili ili tuhakikishe Mfuko wa Maji unapata fedha za kutosha, hizi ndiyo fedha za uhakika ambazo zinaweza kututoa na kutuhakikishia kwamba tunapata maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyejua umuhimu wa maji katika Taifa letu, maji ni muhimu na hapa Mheshimiwa Gekul amesema maji kwanza na kwa vyovyote vile lazima tuhakikishe kwenye bajeti hii tunapata fedha za kutosha ili fedha zipelekwe kwenye miradi na tunapata maji katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Jimbo langu la Lulindi, kwanza ninaishukuru sana Wizara kwa kuutengea fedha mradi wa Chiwambo, ambao upo kwenye Jimbo langu la Lulindi kule Masasi, bahati mbaya mradi huu hii ni bajeti ya tatu mradi haujakamilika, ni imani yangu Serikali hasa Wizara kwa kipindi kilichobaki cha miezi miwili kuelekea mwisho wa bajeti na ziko kila aina ya dalili kwamba Wizara ya Fedha huenda ikakusanya kufikia asilimia 100 kwa fedha za ndani. Ningeomba mradi huu sasa ukamilike ili wananchi wa Kata saba na vijiji zaidi ya 30 waweze kupata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya vijiji kumi ambapo kila Jimbo tunalo, kila Mkoa ipo. Katika Jimbo langu kuna mradi wa Chipingo, mradi wa Shaurimoyo, mradi wa Mkululu, ningependa kuona miradi hii Wizara inaitekeleza ili kuhakikisha kwamba wimbo wa vijiji kumi au mradi wa vijiji kumi sasa unakwisha ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona kwenye miradi ya umwagiliaji katika Mkoa wetu wa Mtwara, nina uhakika hata Mkoa wa Lindi, ningeomba tuhakikishe kwamba tunakuwa na scheme za umwagiliaji kandokando mwa Mto Ruvuma, maji ni mengi, yote yanaingia baharini, ni imani yangu kabisa kwamba Wizara tukijipanga vizuri kwenye suala la umwagiliaji, kilimo kinaweza kukuzwa kandokando ya Mto Ruvuma na kuwafanya wananchi wanaoishi katika Mikoa hii hasa kandokando ya Mto Ruvuma wanufaike na kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie kwamba wote tunakuombea na Wizara tunaiombea ili ikamilishe azma ya kuhakikisha kwamba kila eneo ambalo linahitaji maji liweze kupatiwa maji. Hata tunapozungumzia suala la viwanda, maendeleo ya kilimo, suala la maji ni la kipaumbele cha kwanza. Kwa hiyo, Wizara ijipange upya ihakikishe kwamba inakuwa na usimamizi bora wa fedha zinazopelekwa kwenye Halmashauri. Hivi sasa miradi ile inasimamiwa na Halmashauri kwa asilimia kubwa zaidi kuliko Wizara, ninaomba Wizara iweke kitengo cha usimamizi wa miradi ya maji katika Halmashauri zetu, isisitize suala la ubora wa vifaa vinavyonunuliwa kwenye suala zima la maji. Kwa sababu yako maeneo, miradi imefanyika, lakini inadumu kwa muda mfupi kwa sababu vifaa vilivyotumika, mabomba, viunganishi na mambo mengine yanakuwa hayako katika kiwango kinachostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na fedha hizi zinazotengwa tunapeleka kule safari hii zaidi ya shilingi bilioni 900, lakini kama hakuna usimamizi, na hakuna uangalifu kuhakikisha kwamba vifaa vinavyonunuliwa vinakuwa kwenye kiwango kinachostahili, hakika hatuwezi kupata mafanikio kama tunavyotarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie pia mradi mkubwa ulioko Masasi, mradi wa Mbwinji. Mradi huu umeigharimu Serikali zaidi ya shilingi bilioni 51, ningeomba shilingi bilioni moja iliyotengwa kila mwaka ihakikishe ile shilingi bilioni moja ipelekwe, tunataka tuone kwamba katika bajeti hii inayoishia ya 2015/2016 kiasi kile cha shilingi bilioni moja kilichopangwa kiende ili kiweze kufanya kazi ya kusambaza maji vijijini.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niyaeleze hayo lakini msisitizo mkubwa ni kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwa kauli moja tuhakikishe tunaunga mkono, suala la kuongeza shilingi 100 ili iwe tozo ya kuhakikisha kwamba tunapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kutoa shukrani kwa kupata fursa hii kama mchangiaji wa kwanza kwenye hotuba ya Waziri Mkuu.
Nianze tu kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa anayoifanya na kuonesha uzalendo wa hali ya juu katika kuhudumia Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, la pili, namshukuru sana mtoa hoja, Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa jinsi alivyotoa hotuba yake na jinsi alivyojaribu kuchambua maeneo mbalimbali yanayohusiana na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, labda niende moja kwa moja, lakini pia bila kuwasahau Waziri anayeshughulikia Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama pamoja na Naibu wake, ndugu yangu pale Mheshimiwa…
SPIKA: Mavunde!
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mavunde kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara hiyo.
Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye kilimo na hasa kwenye ukurasa wa 23 wa kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu, alipozungumzia zaidi suala la stakabadhi ghalani. Nianze tu kwa kusema, kwa kweli Sheria ya Ushirika inabidi tuombe mamlaka zinazohusika zilete sheria ile tena, tuifanyie marekebisho kwa sababu sheria ya ushirika ina upungufu mwingi sana na kusababisha wananchi wetu
kupata athari mbalimbali katika kupata haki zao katika mazao yao.
Mheshimiwa Spika, nakubaliana kabisa na hoja ya Waziri Mkuu kwamba maeneo mengi, stakabadhi ghalani imeonekana moja kwa moja kuwa ndiyo ufumbuzi wa matatizo ya masoko katika mazao yetu mbalimbali, ikiwemo kahawa, chai, tumbaku, pareto, korosho na mengineyo.
Nitolee mfano zao la korosho; tatizo kubwa lililojitokeza kufanya wakulima wetu wasipate haki vizuri ni tatizo la vyama vya msingi na vyama vikuu wakati mwingine kufanya kwa makusudi kabisa hujuma ya kuiba fedha za wakulima.
Mheshimiwa Spika, nikitolea mfano, wananchi walipeleka zao lao la korosho kwenye maghala tangu Septemba mwaka 2016, lakini ninavyosema hivi sasa, kwenye Halmashauri yangu ya Wilaya ya Masasi kiasi cha zaidi ya sh. 1,200,000,000/= hazijalipwa kwa wakulima.
Mheshimiwa Spika, jambo hili linawakatisha tamaa wananchi na ndiyo maana nimesema ile Sheria ya Ushirika inabidi tuitazame upya, kwa sababu wenzetu wanaopata mamlaka kwenye vyama vya msingi na vyama vikuu wamegeuka kuwa miungu watu na kuona kwamba wao
wana uhuru uliopitiliza kana kwamba wanaishi kwenye himaya tofauti na Watanzania wengine.
Kwa hiyo, ombi langu kwa Ofisi ya Waziri Mkuu ni kwamba hebu iingilie kati kuona jinsi gani wananchi hawa wanavyoweza kupata haki zao, kwa sababu kwa kweli ni jambo ambalo wananchi hawalielewi, kwa sababu hakuna korosho zilizopo kwenye maghala lakini fedha zao
hazionekani zipo wapi.
Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la tozo kama alivyozungumzia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Serikali mwaka huu imepania kuhakikisha kwamba inaondoa baadhi ya tozo kwenye mazao mbalimbali ya biashara yakiwemo tumbaku, chai, kahawa pamoja na korosho.
Bahati nzuri mimi ni miongoni mwa wanaotoka kwenye maeneo yanayolima zao la korosho; Masasi ni Wilaya ya pili kwa uzalishaji ukiachia Tandahimba. Kwa kweli tunampongeza sana Rais pamoja na Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo wameshiriki katika kufanya zao la korosho kwa
mwaka huu liweze kufikia kilo moja sh.3,800/=. Naamini kabisa Serikali ikiendelea kukaza uzi korosho zinaweza kuwa na uwezo wa kuuzwa sh. 5,000/= kwa kilo katika misimu ijayo.
Mheshimiwa Spika, naomba sana katika tozo zile ambazo Mheshimiwa Waziri Mkuu amezisema, lakini napenda kwa mfano tozo ya magunia ambayo kwa kweli inatozwa kwa wakulima, nadhani iondolewe pamoja na zile nyingine ili kumfanya mkulima aweze kupata unafuu zaidi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningetaka niliseme, ni juu ya masuala ya umeme. Bahati nzuri ameelezea Mheshimiwa Waziri Mkuu katika hotuba yake kwamba Serikali ina nia nzuri ya kusambaza umeme, lakini napenda sana ieleweke kwamba wananchi wa Mikoa ya Mtwara na Lindi kwa sababu ambazo hata Mawaziri wanazijua kwamba maeneo haya yaliachwa kupewa huduma za umeme tangu mwanzo kwa sababu kulikuwa na tetesi kwamba Mkoa huu wa Mtwara na Lindi ulikuwa uhudumiwe na kampuni ambayo ilianza pale kusambaza gesi. Kwa hiyo, baadaye Serikali iliamua kusitisha makubliano yale na TANESCO kuendelea kuhudumia mikoa hii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tatizo ambalo lipo ni kwamba maeneo, vituo au Wilaya za Mkoa wa Mtwara na Lindi hazina magari. Hata magari yaliyoletwa hivi karibuni, hayakusambazwa tena katika mikoa hii vizuri na kufanya utendaji wa kazi katika Mkoa wa Mtwara na Lindi hasa Wilaya ya Masasi kuwa mgumu sana kiutendaji kwa sababu hawana usafiri. (Makofi) Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali
ione kwamba eneo hili linahitajika kutazamwa vizuri zaidi. Naipongeza suala la REA Awamu ya Tatu, kwamba linazinduliwa katika mikoa, lakini nataka tu nitoe angalizo kwa Serikali kwamba kama Mkoa wa Mtwara na Lindi haukutazamwa vizuri, unaweza ukajikuta maeneo mengine
yote nchini yamemaliza vijiji vyake, lakini Mtwara na Lindi vikabaki kwa sababu kule hatukuwahi kupata ile phase one
na wala zile fedha za MCC kwa ajili ya umeme hazikupatikana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tukienda kwa uwiano ulio sawa, basi mikoa hii bado itabaki nyuma. Kwa hiyo, naomba sana hata katika usambazaji umeme, katika maeneo ambayo umeme ulipita muda mrefu, utakuta maeneo ya Mkoa wa Mtwara na Lindi bado maeneo mengi
sana umeme umepita lakini wananchi hawajanufaika.
Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la reli. Naomba sana hii reli ya kutoka Mtwara kwenda Mchuchuma na kama Mheshimiwa Nape alivyokuwa analalamika kwamba maeneo mengi yamewekwa ‘x’ lakini hatuoni zile juhudi za hasa za kuhakikisha kwamba kweli reli hii inataka ijengwe
hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Maliasii na Utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumpongeza sana Profesa Maghembe; Naibu Waziri, Injinia Makani; Katibu Mkuu na Watendaji wa Wizara kwa kuanza kuonesha sura mpya ya Wizara na kuanza kuleta matumaini mapya kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Wizara, Mheshimiwa Waziri Profesa Maghembe na wenzake kwamba juhudi zinazoendelea hivi sasa za kutatua migogoro walioyoikuta ziongezwe kasi ili kuwe na mahusiano mema kati ya Wizara na wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Pia niitahadharishe Wizara siyo vema kuanza kutafuta migogoro mipya kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakala wanaoshughulika na mambo ya misitu wamepewa jukumu la kwenda kutathmini mipaka ya hifadhi za misitu, lakini nimwombe na kumkumbusha tu Mheshimiwa Waziri kwamba zoezi hili halikuwa limefanyika kwa zaidi ya takribani miaka 20 iliyopita,
kinachotokea hivi sasa ni baadhi ya maeneo kuanza kuzalisha migogoro kutokana na zoezi hili. Mheshimiwa Waziri nitolee mfano tu kwenye Jimbo langu la Lulindi tunayo hifadhi ya msitu ya Njawala, lakini tunavyo vijiji vinavyozunguka katika eneo hili, ambavyo Vijiji hivi vya Njawala, Mchoti na Mtona ni vijiji ambavyo vipo tangu miaka 20 iliyopita, katika zoezi hili vijiji vile vinaambiwa vimo ndani ya msitu, sasa inaleta kero kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha basi ni vizuri kueleza wataalam wetu wasiende kuanzisha migogoro mipya. Nilipokuja katika Bunge hili nimemletea Mheshimiwa Waziri barua na wamenituma nimwombe Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge atembelee maeneo ya Jimbo la Lulindi ili akajionee hali halisi katika maeneo haya, naamini atanikubalia ili tukayasikilize na kuyatatua matatizo haya tukiwa kule site. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kulichangia ni tatizo kubwa sana la wanyama hatarishi na wanyama ambao wanawadhuru wananchi. Tangu niingie katika Bunge hili 2010 nimekuwa nikilalamika sana juu ya Wizara kutotilia maanani matatizo yanayotokana na mamba wanaoshambulia wananchi katika Jimbo langu la Lulindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuliwahi kufanyika utafiti kama miaka minne iliyopita na utafiti ulifanywa na wenzetu wa Wizara ya Maliasili, wakabaini kwamba katika Mto Ruvuma hasa eneo langu la Jimbo la Lulindi, mamba ni wengi zaidi ya 300 wapo katika eneo lile. Kulitolewa ahadi, ya kuwapunguza mamba wale lakini kwa masikitiko makubwa katika miaka minne tu wananchi wa Jimbo langu na Watanzania 35 wameshapoteza maisha na zaidi ya watu 50 wamekwishajeruhiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua tunayo Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), nichukue fursa hii kuilalamikia sana TAWIRI, najiuliza labda makao makuu yapo mbali sana na Mtwara yako Arusha, katika kipindi chote cha Ubunge wangu sijawahi kuwaona TAWIRI wakija kutembelea maeneo yaliyoathirika katika Majimbo yetu. Kikubwa ambacho wanakatisha tamaa ni kwamba sisi tunasikiliza maelekezo yanayotolewa na Shirika la Wanyama Duniani kwamba lazima tuwalinde wanyama wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwombe Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha hebu awape matumaini wananchi wale ambao wanaishi kandokando ya Mto Ruvuma, vijiji hivi ni vijiji vya ulinzi, kuna Vijiji vya Mapili, Mduhe, Maparawe, Mkoo, Sindano na Mgwagule wananchi hawa katika kipindi chote hiki wameishi kwa maisha ya shida mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshafika ofisini kwa Mheshimiwa Waziri mara nyingi na tumezungumza, kwamba moja ya suluhisho la kuwasaidia wananchi wale ili wasiathirike na tatizo la mamba ni kupunguza idadi ya wananchi wanaokwenda kuchota maji na huduma zote za maji kutoka kwenye mto ule. Tunao mfuko hapa unaoshughulika na wanyama pori, tunayo mifuko mingi inayoshughulika na wanyama pori, inazo fedha, kwa nini Wizara isihakikishe kwamba inasaidia vijiji vile kupata maji ili tupunguze idadi ya watu wanaokwenda kutumia maji kutoka Mto Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namfahamu Mheshimiwa Profesa Maghembe, Naibu Waziri Engineer Makani na Katibu Mkuu kwamba ni wasikivu sana, naamini atakapokuwa anahitimisha kwenye hotuba yake atawaambia ndugu zangu wale Lulindi ni jinsi gani Wizara yake itakavyolichukulia suala hili kwa uzito mkubwa na kuhakikisha katika bajeti hii ya 2017/2018, tunatenga fedha kwa ajili yakuchimba visima vinane kwenye vijiji hivi ili kuwasaidia wananchi wale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaacha kusema aliyosema aliyetangulia kutoa maoni yake. Mheshimiwa Waziri hili tamko tunalotaka kuendelea kupewa msisitizo la kuzuia mkaa kutoka eneo moja kwenda lingine ni lazima litazamwe upya. Bado hatujafika wakati ambapo nishati mbadala zinaweza kutosheleza badala ya mkaa. Namwomba sana hili jambo la kuhifadhi misitu ni jambo muhimu sana, nakubaliana nalo sana kwa asilimia mia moja, lakini twende taratibu, kuagiza tu mamlaka zote zianze kuzuia mikaa kuingia mijini kwenda wapi, wakati mitandao ya gesi hatujaikamilisha, ni jambo ambalo hapana, hili jambo tutaonekana tunakurupuka na litaleta athari kubwa sana kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana kwa sababu hili jambo linagusa maisha ya wananchi wetu wengi wa vijijini na maisha ya wengi wa mijini, jambo hili lisitishwe mpaka pale ambapo tayari tutakuwa na nishati nyingine ambayo wananchi hawa wanaweza wakatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa sina tabia ya kupenda kugongewa kengele, naamini haya ambayo nimeiambia Wizara, nimeiambia Serikali na hasa kwa wananchi wale ambao wanapoteza maisha, yatazamwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki cha mvua huwa hakuna matukio makubwa ya mamba kuwavamia wananchi, kwa sababu maji yamejaa, wako katikati ya maji marefu, lakini kuanzia Julai hadi Desemba kila siku tunapokea taarifa ya vifo vya wananchi. Mheshimiwa Waziri wale ni Watanzania sasa nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kuwaambia Watendaji kwamba, wakiwa wanang’ang’ania taarifa zinazotolewa na jumuiya ya Kimataifa… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Serikali. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Mpango na Dada yangu Mheshimiwa Dkt. Kijaji kwa kazi nzuri wanazozifanya na kutuletea bajeti ambayo imejenga matumaini makubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano kwa jinsi anavyofanya kazi. Nami nataka niseme tu, hii ni zawadi kwa Watanzania. Kama ambavyo nchi nyingine wanatamani Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awe Rais katika nchi nyingine, sisi wote kwa pamoja tunatakiwa tuienzi hii tunu ambayo tumepata kutoka kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoeleza Mjumbe aliyetangulia kusema hapa Mheshimiwa Bura, kwamba ziko taarifa kwamba yako matumaini makubwa ya kupata zile fedha ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anazisema, nashauri hizi fedha zikipatikana, basi baadhi ya sehemu kubwa ya fedha hizi zielekezwe kwenye mradi wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huwezi kuzungumzia suala la uchumi bila kuhusisha suala la upatikanaji wa maji kwa wananchi wetu. Tulipendekeza kuanzia kwenye Kamati ya Bajeti lakini pia kwa Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba tungeweza kupata Sh.50/= kwa kila lita ya mafuta ili iende kwenye maji, lakini bahati nzuri imetengwa Sh.40/= kwa kila lita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa hizi fedha sasa zielekezwe kwenye maji ili ziweze kwenda kutusaidia kuwafanya Watanzania waweze kufanya kazi nyingine na kuhakikisha kwamba maji yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye uti wa mgongo wa Taifa letu ambao ni kilimo. Naishukuru Serikali kwamba imefanya juhudi sana za kuondoa tozo na kwenye korosho Serikali imeamua kwa mara ya kwanza kabisa kutoa sulphur bure kama ruzuku kwa wakulima wa korosho. Sasa isiishie tu kwenye kuondoa tozo, ni lazima tuelekee pia kwenye kuwatafutia masoko bora wakulima wetu ili waweze kupata masoko mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitembelewa na viongozi wengi hapa nchini akiwemo Waziri Mkuu wa India; na alipokuja alizungumza na Serikali na alizungumza na Mheshimiwa Rais, akatoa matumaini kwamba Serikali ya India iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kununua aina zote za Kunde kwa maana ya choroko, kunde na mbaazi. Naomba Serikali iharakishe suala la mazungumzo na Serikali ya India. Hivi sasa Wakulima wa Wilaya ya Masasi na Mkoa mzima wa Mtwara kwa ujumla, waliitikia wito wa kulima mazao haya na choroko sasa ndiyo zinavunwa lakini bei imeshuka kutoka Sh.1,200/= hadi Sh. 400/= kwa kilo. Kwa hiyo, naiomba Serikali, pamoja na juhudi ya kuondoa tozo kwenye mazao, lakini ihakikishe tunapata soko zuri la mazao yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine ninaotaka kuutoa kwa Serikali; hivi karibuni Kamati ya Bajeti ilipata nafasi ya kuzungumza na wenzetu ambao wanatusaidia misaada kutoka nje. Jambo ambalo limeonekana kuchelewa kupata misaada ya nje ni kwamba tunawatoza VAT, fedha zinazoletwa hapa nchini kwa misaada ya maendeleo, jambo ambalo Mataifa yanayotoa misaada yanakataa, kwamba sisi tunatoa misaada kuwaleteeni ninyi kwa maendeleo, kwa nini mtukate VAT? Kwa hiyo, naiomba Serikali hili suala liondolewe ili kuwafanya wafadhili wetu walete zile fedha zao bila vikwazo. Sasa tunalalamika kwamba fedha haziji kumbe tatizo ni kwamba Serikali zile wamesita kuleta kwa sababu sisi tunawatoza VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nichangie ni juu ya Serikali kuona umuhimu wa kupeleka milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizi zinahitajika sana kule, lakini iko haja ya kutazama pia upya jinsi ya kuzipeleka fedha zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri badala ya kwenda kuwagawia mmoja mmoja kwa ajili ya miradi midogo midogo, ni vizuri kuchagua mradi mmoja katika Kijiji na zile fedha zikatumika shilingi milioni 50 kwa ajili ya kusaidia kwenye maendeleo ya kile kijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilitaka nichangie kwenye bajeti hii, lakini kabla sijamaliza kuchangia nirudi kwenye kilimo kuwapongeza sana Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Ole Nasha, wanafanya kazi kubwa sana na Watanzania wana imani nao sana kwenye Sekta ya Kilimo. Naamini kabisa wataongeza bidii ili kuhakikisha wakulima wanaweza kufanya kazi yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye Sekta ya Viwanda. Ni lazima Serikali sasa tujielekeze kwenye suala la viwanda kwa moyo wa dhati kabisa na dhamira ya kweli. Tunavyo viwanda ambavyo kama tungevifufua tungeweza kuongeza uchumi wetu kwa kiasi kikubwa sana likiwemo zao la korosho. Tunavyo viwanda ambavyo vilijengwa, viwanda vile vikachukuliwa na baadhi ya watu wakisema watavifufua, lakini hadi sasa hawajafufua. Ni vizuri tukavifufua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naipongeza Serikali kwa kuwasaidia wakulima wa zao la tumbaku ambao kwa muda mrefu walikuwa wanalia, lakini naamini sasa wale wa Urambo, wale wa maeneo yote yanayolima tumbaku sasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)