Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Jerome Dismas Bwanausi (15 total)

MHE. RASHID M. CHUACHUA (K.n.y. MHE. JEROME D. BWANAUSI) aliuliza:-
Kulikuwa na ahadi ya Serikali ya kujenga minara ya mawasiliano katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji (a) Je, ni lini wananchi wa Kata ya Mchauro, Mkundi na Sindano watajengewa minara ili kurahisisha mawasiliano?
(b) Je, ni utaratibu gani unaotumika ili waliotoa maeneo yao na kijiji husika wapate ushuru kutoka kwenye Kampuni iliyojenga mnara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Rivango kutoka katika Kata ya Mchauro, pamoja na Kijiji cha Luatala kutoka katika Kata ya Sindano na Vijiji vya Chipango, Mkoropola, Nakachindu na Kijiji cha Nakalola kutoka katika Kata ya Mikundi vimeshapata huduma ya mawasiliano kupitia utekelezaji wa Awamu ya kwanza ya mradi wa Kampuni ya Simu ya Viettel.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vya Lichehe, Sindano kutoka katika Kata ya Sindano na vijiji vya Maparawe, Mkowo Mwitika na Nangomwa kutoka katika Kata ya Mchauro vipo katika orodha ya miradi ya Viettel inayotegemewa kutekelezwa katika Awamu ya Pili na ya Tatu iliyoanza Novemba, 2015 na kutarajiwa kukamilika Novemba, 2017. (Kicheko/Makofi)
Aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imevijumuisha Vijiji vya Mchauro, Mhata, Mirewe na Namwombe katika orodha ya miradi ya siku za usoni itakayotekelezwa na mfuko katika mwaka wa fedha 2016/2017 kulingana na upatikanaji wa fedha. (Kicheko/Makofi)
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kiutaratibu kampuni inayotaka kujenga mnara huingia mkataba na mwananchi mwenye eneo husika na hukubaliana kiasi cha malipo kwa mwezi kwa muda wa mkataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna wananchi walitoa maeneo yao kwa makubaliano ya kulipwa, basi wafatilie utekelezaji wa mkataba wao na kampuni husika.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Barabara ya ulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji ni muhimu sana kwa ulinzi na kiuchumi.
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa hasa ikizingatiwa kuwa imekuwa ikiahidiwa kwa miaka mitano sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya – Mnongodi – Mapili hadi Mitemaupinde ni barabara ya ulinzi inayounganisha Wilaya za Mtwara Vijijini, Newala na Nanyumbu. Barabara hii inayoambaa na mpaka wa Tanzania na Msumbiji ilikuwa inatumiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa ajili ya ulinzi wa mpakani. Kipande cha barabara hii kati ya Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya hadi Mnongodi chenye urefu wa kilometa 108 kinahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Sehemu inayobaki yenye urefu wa kilometa 250 haiko chini ya milki ya mamlaka yoyote, hivyo imekuwa pori baada ya kukosa matengenezo kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania, imefanya na kukamilisha usanifu wa kipande cha barabara chenye urefu wa kilometa 120 kati ya Mapili na Mtemaupinde pamoja na daraja la Lukwamba na usanifu kukamilika mwaka 2007. Kwa kuanzia Serikali ilianza kazi ya ujenzi wa daraja hili mwaka 2013 na kazi zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na ufunguzi wa sehemu Mapili hadi Mitemaupinde na hadi sasa jumla ya kilometa 25 zimefunguliwa. Aidha, Wizara yangu imetenga fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya kuendelea kuifungua barabara hii na barabara nyingine za ulinzi zilizopo katika Mkoa jirani wa Ruvuma.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali iliwaahidi wakulima wa korosho kupata malipo halali ya mauzo ya korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
(a) Je, ni lini Serikali itawahakikishia wakulima wa korosho wa Wilaya ya Masasi wanalipwa malipo yao ya mwisho wanayostahili?
(b) Je, Serikali imekuchukua hatua gani kwa Vyama vya Ushirika ambavyo haviwapi wakulima wa korosho fedha zao kama korosho zilivyouzwa kwenye mnada?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna baadhi ya wakulima wa korosho katika baadhi ya vyama vya msingi ambao hawakulipwa bonus baada ya kuuza korosho zao kama ilivyostahili. Hii ilisababishwa na baadhi ya vyama hivyo kukiuka taratibu za makato ya korosho kama ilivyokubaliwa katika Mkutano Mkuu wa wadau uliofanyika mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha suala la bonus, wakulima wote walilipwa malipo ya awali ya korosho kwa bei elekezi ya shilingi 1,200 na waliongezewa malipo ya pili kutegemeana na bei iliyopatikana sokoni. Nyongeza ya malipo ya pili yalianzia shilingi 800 kwa kilo na kufanya malipo ya chini aliyopata mkulima kuwa shilingi 2,000 kwa kilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la bonus Serikali inafuatilia kuona kama kuna ubadhirifu uliofanyika katika Vyama vya Ushirika kwa kufanya ukaguzi na iwapo itadhihirika, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa waliohusika ikiwa ni pamoja na kuamuru wahusika kurudisha fedha hizo na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa mapunjo ya malipo ya ziada hayatokei tena, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imejipanga kuendelea kuvihamasisha na kuvielimisha vyama vya msingi umuhimu wa kukusanya korosho kutoka kwa wanachama wake na kuziuza badala ya kuchukua mikopo yenye riba kubwa kutoka kwenye mabenki na kununua korosho hali inayosababisha malipo ya awamu yasiyokuwa na tija kwa mkulima. Vilevile wakulima wote wa korosho wanashauriwa kufungua akaunti benki kwa lengo la kukabiliana na ubadhirifu wa fedha unaochangiwa na zoezi la usafirishaji wa fedha kutoka benki kwenda kwa wakulima.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali kupitia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ililihakikishia Bunge kuwa madaraja ya Mto Mresi katika barabara ya Ulinzi na Shaurimoyo na Nachalolo katika Mto Mwiti yalizolewa na mafuriko na yatajengwa kwa dharura:-
(a) Je, ni maandalizi gani yamefanyika ili madaraja hayo yajengwe kwa haraka?
(b) Je, madaraja hayo yataanza kujengwa lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Ulinzi ya kutoka Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya – Mnongodi – Mapili hadi Mitema Upinde inaunganisha Wilaya za Mtwara Vijijini, Newala na Nanyumbu. Sehemu ya barabara hii, yaani Mangamba – Madimba – Tangazo – Kitaya - Mnongodi hadi Namikupa yenye urefu wa kilomita 108 inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Mheshimiwa Mwenyekiti, TANROADS imekamilisha usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha changarawe wa sehemu ya barabara hii yenye urefu wa kilomita 120 unaojumuisha madaraja ya Mbangara, Miesi na Kigwe yaliyopo katika barabara hii ya Ulinzi. Serikali kwa sasa inatafuta fedha ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, madaraja ya Shaurimoyo na Nakalola yaliyopo katika barabara za Mpindimbi hadi Shaurimoyo na Mpindimbi hadi Nakalola zinahudumiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ambapo fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo bado zinatafutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali itaendelea kuifanyia barabara hii matengenezo ya kawaida, matengenezo ya muda maalum na matengenezo ya sehemu korofi. Aidha, kuhusu sehemu ya barabara ya Ulinzi iliyobaki kuanzia Mapili hadi Mitema Upinde yenye urefu wa kilomita 250, Serikali imetenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya kuifungua.
MHE. JEROME D. BWANAUSI Aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga madaraja ya Shaurimoyo, Nakalolo na Miesi.
Je, ni lini madaraja hayo yatajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kwa msaada wa Wakala wa Barabara (TANROADS) imekamilisha usanifu wa madaraja yanayohitajika kujengwa katika mito ya Mpindimbi - Shaurimoyo - Nakanyimbi mpaka Nakalolo. Gharama za awali za ujenzi wa madaraja hayo
zimebainika kuwa ni shilingi bilioni tatu. Kutokana na ufinyu wa bajeti ya Halmashauri, Wakala wa Barabara (TANROADS) imekubali kutenga fedha hizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali iliahidi kuweka minara katika Kata ya Sindano, Mchauru, Lipumbiru na Lupaso.
Je, ni lini minara hiyo itajengwa ili kuondoa tatizo la kutokuwa na mawasiliano katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliingia mkataba na Kampuni ya TTCL kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata za Lupaso na Lipumbiru kwa ruzuku ya dola za Kimarekani 94,000. Ujenzi wa mnara huo ulikamilika tangu mwezi Machi, 2015 na kuanza kutoa huduma. Hata hivyo, baada ya mnara huo kuwaka Kampuni ya TTCL inaendelea na taratibu a kubadilisha masafa kutoka teknolojia ya CDMA 800 Mhz kwa lengo la kukabiliana na changamoto iliyopo katika teknolojia hiyo ya CDMA katika kutoa huduma za ziada kwa wateja, ikiwa ni pamoja na huduma za mobile money, mobile banking, na kadhalika. Kampuni ya TTCL inaendelea kuboresha upatikanaji wa mawasiliano kwenye eneo la Lipumbiru na Lupaso na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Simu za Mkononi
ya Viettel itafikisha huduma ya mawasiliano katika kata za Sindano na Mchauru, kwa mujibu wa makubaliano baina ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Kampuni hiyo. Kwa upande wa kata ya Mchauru yenye vijiji vya Mchauru, Mhata, Mirewe na Namombwe iliingizwa katika zabubi ya mfuko ya kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipaka iliyofunguliwa tarehe 27 Aprili, 2017 ambapo kampuni itakayopewa jukumu la kufikisha mwasiliano kwenye kata hiyo ya Mchauru itajulikana mara tu baada ya taratibu za tathmini kukamilika.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-
Serikali iliahidi kuanzisha mfumo wa commodity exchange ili kuwasaidia wananchi wanaolima korosho kupata bei nzuri katika msimu husika
– Je, Serikali ina kauli gani huu ya kuanza kwa mfumo huo?
– Je, Serikali itatatua vipi suala la kodi nyingi kwa wakulima wa korosho inayosababisha kupata bei ndogo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya soko la bidhaa (commodity exchange) yalianza mwaka 2011 kwa lengo la kufanya biashara ya mazao kuwa ya wazi na yenye ushindani kulingana na nguvu ya soko. Aidha, mfumo huu umelenga kupunguza gharama za uendeshaji wa masoko yote ya mazao yote ya chakula na biashara ili kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri na yenye tija.
Mheshimiwa Spika, hatua ambazo zimeshachukuliwa hadi sasa ni pamoja na kupitishwa kwa waraka wa soko hilo, kuundwa kwa bodi ya soko, kutungwa kwa sheria ya mwaka 2015 ya soko la bidhaa pamoja na kanuni zake, kufanya uzinduzi wa kuanzisha soko hili, kutoa mafunzo kwa madalali watakaoendesha soko hilo na kutoa mafunzo kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na sekta binafsi ili kujenga uelewa wa pamoja. Vilevile ofisi na jukwaa la soko hilo vimefunguliwa kwenye jengo la LAPF lililo kijito nyama Jijini Dar es Salaam. Kazi za uwekaji wa vifaa katika ofisi na jukwaa zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, elimu ya soko la bidhaa inaendelea kutolewa kwa baadhi ya viongozi wa ngazi za Mkoa na Wilaya na maafisa kilimo, ushirika, biashara na maendeleo ya jamii katika Mikoa ya Lindi, Mtwara, Morogoro, Dodoma na Singida. Aidha, elimu hiyo imeshatolewa kwa viongozi wa vyama vikuu vya ushirika na viongozi wa vya msingi na vyama visivyokuwa vya kiserikali ili kujenga uelewa wa somo hili. Pia elimu itaendelea kutolewa kwa wakulima na wananchi wka ujumla ili wadau waufahamu mfumo huo wa soko.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imeondoa ushuru na tozo an kubakiza makato ya usafirishajia korosho kulingana na umbali halisi. Mchango wa kuendeleza zao na ushirika na kuondoa shilingi 50 kwa kila kilo zilizokuwa zinatozwa kwa ajili ya kufungashia korosho. Aidha, Serikali imepunguza ushuru wa Halmashauri za wilaya kutoka asilimia tano hadi tatu.
MHE. JEROME D BWANAUSI aliuliza:-
Wakati Serikali inafanya juhudi za kuongeza idadi ya Walimu na kulipa stahiki zao:-
(a) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kurudisha Chuo cha Ualimu Ndwika badala ya sekondari kama ilivyo sasa?
(b) Je, ni lini Serikali italipa madeni hayo?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1999, Serikali iliamua kuvibadilisha baadhi ya Vyuo Vya Ualimu kuwa shule za sekondari, Ndwika kikiwa kimojawapo. Uamuzi huo ulifikiwa baada ya utafiti uliofanyika kubaini kuwa vyuo hivi vilikuwa na uwezo mdogo wa kudahili wanachuo kiasi cha kutokuwa na tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uamuzi huo wa Serikali Chuo cha Ualimu Ndwika kilibadilishwa na kuwa na shule ya sekondari ya wasichana ya bweni kutokana na mahitaji makubwa ya shule za bweni kwa wasichana. Aidha, uamuzi huo ulitokana na changamoto mbalimbali yanayopata wanafunzi wa kike zikiwemo umbali mrefu wa kwenda shule na kurudi nyumbani, baadhi ya jamii ya kutowapa fursa ya kwenda shule na pia vishawishi mbalimbali vinavyopelekea kupata mimba wakiwa masomoni. Hivyo, shule hii ina umuhimu mkubwa katika kumkomboa mwanafunzi wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina jumla ya Vyuo vya Ualimu 35 ambavyo vimekuwa vikidahili wanachuo kutoka nchi nzima. Kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imefanyia upanuzi na ukarabati mkubwa vyuo 24; na katika mwaka wa fedha 2014/2019 vyuo vingine kumi vitapanuliwa kwa lengo la kuongeza nafasi za udahili hivyo kutosheleza mahitaji ya Walimu. Kwa hiyo Serikali itaendelea kuyatumia majengo ya kilichokuwa Chuo cha Ualimu Ndwika kutoa elimu ya sekondari kama ilivyo sasa.
Mhehsimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imelipa madeni ya Walimu 86,234 yenye jumla ya shilingi bilioni 33,804,082,905 katika kipindi cha mwaka wa 2015/2016 na 2017/2018. Serikali kwa sasa inahakikisha kuwa hakuna madeni yatakayolimbikizwa kwa kulipa stahiki za Walimu kwa wakati.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA - (K.n.y. MHE. JEROME D. BWANAUSI) aliuliza:-
Madaraja ya Mwitika – Maparawe, Mipande – Mtengula na Mbangara – Mbuyuni yalisombwa na maji wakati wa mafuriko miaka mitano iliyopita na kusababisha matatizo makubwa ya usafiri:-
Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo ili kuondoa adha ya usafiri inayowakabili wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismasi Bwanausi Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba madaraja ya Mwitika, Maparawe, Mputeni, Mtengula na Mbangala, Mbuyuni yalisombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha mwaka 2015/2016. Kwa kutambua umuhimu wa barabara hii Serikali ilifanya tathmini juu ya gharama za ujenzi wa madaraja hayo, ilibainika kuwa kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zinahitajika kukamilisha ujenzi wa madaraja hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kiasi hicho cha fedha ni kikubwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeweka kwenye maombi maalumu, hivyo ujenzi wake utategemea kuanza pindi fedha hiyo iliyoombwa itakapopatikana. Madaraja hayo yatahudumiwa na Wakala wa Huduma za Barabara Vijijini yaani TARURA.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-

Wananchi wengi wameendelea kupoteza maisha na kujeruhiwa na mamba katika Mto Ruvuma:-

Je, ni lini wananchi walioathirika na mamba katika Vijiji vya Miesi Utimbe, Naliongolo, Mtolya, Geuza na Mchoti watalipwa fidia zao kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikilipa kifuta machozi kwa wananchi ambao wameshambuliwa na wanyamapori wakali kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta Jasho na Machozi za Mwaka 2011. Kuanzia mwaka 2013 mpaka 2018 jumla ya Sh.37,300,000/= zimelipwa kwa wananchi 65 waliopatwa na madhara kutokana na wanyamapori wakali, hususan mamba, katika Wilaya ya Masasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kupunguza matukio ya wananchi kuendelea kupoteza maisha na kujeruhiwa na mamba, hasa wanapokwenda kuchota maji mtoni, Wizara kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) imechimba visima vya maji tisa katika vijiji vilivyo kandokando ya Mto Ruvuma. Vijiji hivyo, ni chipingo, Nalimbudi, Chikolopora, Maparawe, Mbangala, Geuza na Mkowo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika kukabiliana na changamoto za athari zilizosababishwa na mamba, mwezi Julai, 2016, Wizara ilitoa kibali kwa Kampuni ya Ontour Tanzania Limited ambayo ilivuna mamba nane katika Mto Ruvuma na kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya wananchi kujeruhiwa na kuuawa na mamba. Mfano katika kipindi cha Februari, 2018 mpaka sasa Wizara yetu haijapokea taarifa yoyote kuhusu wananchi waliouawa na kujeruhiwa na mamba katika eneo hilo. Ahsante.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-

Serikali iliahidi kujenga minara ya simu katika Kata za Sindano, Lipumburu, Namtona, Mcharu, Chikolopola na Mkundi.

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote iliviainisha Vijiji vya Kata za Sindano, Lipumburu, Namtona, Mchauru, Chikolopola na Mkundi kwa ajili ya tathmini kuangalia mahitaji halisi ya Mawasiliano kwenye eneo hilo. Baada ya tathmini husika kukamilika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote iliviingiza Vijiji vya Kata za Mchauru katika mradi wa mpakani na kanda maalum unaotekelezwa na Kampuni ya Simu ya Tigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari vibali vya ujenzi kutoka NEMC vimeshapatikana, hivyo Kampuni ya simu ya Tigo inategemea kuanza ujenzi wa mnara sambasamba na kufunga vifaa vya mawasiliano mara moja. Aidha, ujenzi wa mnara huu unatarajiwa kukamilika mwezi Januari, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Sindano na Lipumburu ziliingizwa katika mradi wa awamu ya tatu ambao ulitiwa saini tarehe 13 Desemba, mwaka 2018 na utekelezaji wake unategemewa kukamilika mnamo mwezi Septemba, 2019. Kata ya Sindano itafikishiwa huduma ya mawasiliano na Kampuni ya Vodacom na Kata ya Lipumburu itafikishiwa huduma ya mawasiliano na Kampuni ya TTCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Kata za Namtona, Chikolopola na Mkundi vitaingizwa katika orodha ya miradi ya zabuni zinazotangazwa katika siku za usoni kulingana na upatikanaji wa fedha hususan katika mwaka huu wa fedha 2019/2020.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-

Wananchi wa Mipande – Mtengula na Mwitika Maparawe wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa madaraja na Rais wa Awamu ya Tano aliwaahidi Wananchi hao kuwajengea madaraja:-

Je, ni lini ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza usanifu wa Daraja la Mwitika hadi Maparawe linalounganisha barabara yenye urefu wa kilomita 4 na daraja la Mputeni-Mtengula linalounganisha barabara yenye urefu wa kilomita 3.06. Lengo la usanifu huo ni kubaini gharama zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa madaraja yote mawili. Hivyo, naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati Serikali inakamilisha kazi hiyo ya usanifu ili kuanza shughuli za ujenzi.
MHE. JEROME D. BWANAUSI Aliuliza:-

Serikali iliahidi kujenga minara ya mawasiliano ya simu katika Kata za Sindano, Lupaso, Lipumburu, Mchauru na Mapili (Chikolopola) ambazo zipo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi, Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliviainisha vijiji vya Kata ya Sindano, Lipumburu, Namtona, Mchauru na Chikolopola (Mapili) na kuviiingiza vijiji vya Kata za Mchauru katika mradi uonatekelezwa na Kampuni ya Simu ya MIC (Tigo) ambapo vibali vya ujenzi kutoka NEMC vimekwisha patikana. Kata za Sindano na Lipumburu ziliingizwa katika mradi wa awamu ya tatu ambayo ilitiwa saini tarehe 15 Desemba, 2018 ambapo utekelezaji wake unategemewa kukamilika mnamo mwezi Desemba, 2019 ambapo Kata ya Sindano inafikishiwa huduma na Kampuni ya Vodacom wakati Lipumburu itafikishiwa huduma na TTCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vijiji vya Kata za Lupaso na Chikolopola vimeingizwa katika orodha ya miradi ya zabuni iliyotengwa mwezi Julai, 2019. Utekelezaji wa mradi unategemea kuanza mwezi Oktoba, 2019.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-

Wananchi wengi wa Vijiji vya Mieji, Utimbe, Naliongolo, Mtolya, Geuza na Mchoti wamekuwa wakiliwa na mamba na wengine kujeruhiwa vibaya hasa wanapokwenda kuchota maji katika Mto Ruvuma kutokana na ukosefu wa maji katika maeneo yao.

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kuchimba visima vya maji katika vijiji hivyo ili kunusuru wananchi wanaouawa na kujeruhiwa na mambo wnapofuata maji katika mto huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi Mbunge wa Lulindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi wa vijiji vya Miesi, Utimbe, Naliongolo, Mtolya, Geuza na Mchoti wana shida ya kupata majisafi na salama na sehemu pekee ya kupata maji ya matumizi ya nyumbani ni kutoka Mto Ruvuma. Hata hivyo kutokana na umbali uliopo kati ya vijiji hivyo inapelekea gharama ya kuchukua maji katika Mto Ruvuma kuwa kubwa ukilinganisha na gharama ya kuchimba visima.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Masasi inategemea kuingia mkataba wa kuchimba visima na Wakala wa uchimbaji visima na ujenzi wa mabwawa (DDCA) katika vijiji 26 kwa gharama ya shilingi milioni 579.

Mheshimiwa Spika, rasimu ya Mkataba wa uchimbaji wa visima katika vijiji 26 umewasilishwa Wizarani na tayari kibali kimetolewa kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huo.
MHE. JEROME D. BWANAUSI aliuliza:-

Serikali iliahidi kusambaza umeme katika Vijiji vya Matogolo na Nagaga.

(a) Je, ni lini vijiji hivyo vitasambaziwa umeme?

(b) Je, ni lini umeme jazilizi katika Jimbo la Lulindi utasambazwa?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jerome Dismas Bwanausi Mbunge wa Lulindi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kusambaza umeme vijiini katika vijiji vyote vya Tanzania Bara. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwenzi Juni, 2021. Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea utapeleka umeme katika vijiji 67 katika Wilaya ya Masasi kupitia Mkandarasi JV Radi Services Ltd., Njarita Contractors Ltd na Anguila Contractors Ltd.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Matogolo na Nagaga vimeshapatiwa huduma ya umeme kupitia Shirika la Umeme nchini - TANESCO mwezi Februari, 2020. Kazi zinazoendelea kwa sasa ni maandalizi ya kusambaza umeme katika vitongoji vyote vya vijiji hivyo na kuunganishia umeme wateja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Ujazilizi katika Jimbo la Lulindi Mkoani Mtwara utaanza kutekelezwa kupitia Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili (IIB) ambapo jumla ya Mikoa 16 itanufaika ikiwamo Mtwara. Miradi ya Ujazilizi IIB itawezesha kupeleka umeme katika vitongoji 2,400 na kuunganishiwa umeme wateja wa awali 95,000. Gharama na mradi ni Dola za Marekani milioni 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu utaanza mwezi Mei, 2020 na kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 9.