Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jaku Hashim Ayoub (9 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, unapokuta maji yakoge, mwanzo hujui mbele kama utayakuta tena.
Kwanza nichukue fursa hii kukushukuru wewe kunipa hizi dakika nne au tano hizi zilizobaki kumalizia ngwe hii iliyobaki na nitakuwa si mwingi wa fadhila kama sikumshukuru Mwenyezi Mungu, aliyeniwezesha kusimama hapa na kuvuta pumzi zake na kurudi tena kwa mara ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo Mheshimiwa Waziri kipindi kilichopita mwaka jana, nilikigusia sana na nikazuia shilingi, na hii leo hii nafikiri Mheshimiwa Waziri kuna vijana 13 kutoka Zanzibar. Nazungumza kuhusu maslahi ya Zanzibar kuhusu Wizara hii, kutokana na mambo yanayohusu masuala ya Muungano.
Kuna vijana 13 mmewasomesha Chuo cha Diplomasia, bahati mbaya mkawachukua saba, lakini kwa masikitiko makubwa na unyonge na huruma kubwa mpaka hii leo vijana hao saba hamjawaajiri. Mwaka jana nilihoji kwenye bajeti na Mwenyezi Mungu si Athumani kanirudisha tena leo hii, nipo hapa, kwa hiyo, nitahitaji maelezo ya vijana saba hawa wa Zanzibar mpaka leo hamjawaajiri na hii ilikuwa si hisani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni makubaliano katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Vijana hawa hamjawaajiri hadi hivi leo, nataka maelezo ya kina kuhusu suala hili na umri wao unakwenda, na mmechukua barua Zanzibar kama kuwaazima, si kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka hapo kwa haraka haraka nitahitaji maelezo lakini haya vilevile ni ya kusikitisha, Wizara hii huko nyuma au uzoefu unaonesha Waziri anatoka Bara, Naibu Waziri kutoka Visiwani. Lakini kwa masikitiko Wizara hii wote wazee mmekalia kiti chenu, lakini si maamuzi yangu ni maamuzi ya Mheshimiwa Rais. Lakini kama hapatoshi hapo, hata Wizara ya Fedha haya mambo ya Muungano tulikuwa tupokezane, hapatoshi hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa umakini wake na Mwenyezi Mungu ampe umri mrefu, alikuwa akijitahidi katika safari za nje, kuwachukua Mawaziri kutoka Zanzibar katika safari zake, je, mpango huu utaendelea tena vilevile au utalala?
Mheshimiwa Mwenyikiti, nitoke hapo nataka kuulizia haya maslahi ya Mabalozi wangapi wa Zanzibar waioajiriwa, huu ni wimbo wa Taifa wa muda mrefu. Wimbo huu umekuwa wa muda mrefu, kuhusu ajira katika Wizara hii nataka kujua Mabalozi kutoka Zanzibar ni wangapi wanaowakilisha hivyo? Vilevile senior officer kutoka Zanzibar, katika Mabalozi wako wangapi, wimbo huu umekuwa ni wa muda mrefu lakini hautoshi...
MWENYEKITI: Ahsante,
Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa dakika hizi za majeruhi. Mchango wangu utakuwa mdogo sana kwa hizi dakika ulizonipa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Balozi Seif Idd na Waziri Mkuu kwa jitihada alizozichukua lakini vilevile nitakuwa sijamtendea haki dada yangu Jenister Mhagama kwa suala hili. Nizipongeze kabisa Serikali mbili hizi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa kuweza kukiondoa kifungu cha 2(2). Ni jambo la kulipongeza sana tena sana kabisa kwa usikivu, vinginevyo kingepita hivi wananchi wale wa Pemba na wa Darajani wangeumia kwenye majahazi yao na wana majahazi wale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wangeshindwa kusajili hata uwakala ule ungekwenda zake, wangeumia sana sana na unajua ajira zilivyo. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri hiki kifungu kweli hamkukiona? Hii ofisi ina Wanasheria wangapi? Kuna Makatibu wangapi Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Spika, ahsante nimekusikia. Huu Muswada nathubutu kuapa kwamba Zanzibar hawakushirikishwa, lakini kuna Miswada mingine muifikirie kama wa TTCL umekuja dakika za mwisho kwenye Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo jambo hili lifikiriwe.

Mheshimiwa Spika, lakini nije katika kifungu cha sita (6), hiki kifungu kinafanana na cha 11, NASACO huyu huyu atakuwa Wakili, NASACO huyuhuyu atakuwa Jaji? Hebu iangalieni sheria hii, huyu ndio atazikagua meli huyuhuyu atakuwa wakala wa meli, patakwenda kweli, ni kitu cha kuzingatia sana, haiwezekani mtu mmoja ukampa majukumu mawili, hata kanuni zetu za uchaguzi zinasema kule kuwa mtu mmoja huwezi kumpa kazi mbili.

Mheshimiwa Spika, Zanzibar wana Zanzibar Maritime Authority ambayo imepitishwa mwaka 2006, lakini SUMATRA wana kifungu chao kinaitwa Shipping Act ya mwaka 2003, kila mmoja ana sheria yake sasa kufika mahali na hapo nakumbuka mimi, walikuwa wakishirikiana lakini cha kusikitisha cha kutia huruma hizi sheria zikifika na za Wazanzibari washirikishwe kwenye mambo ya Muungano.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo kuna suala la bandari, tumelipigia kelele humu juzi. Bado Wazanzibari wanasumbuliwa bandarini, ule mchele pale ukafika unapokewa, utafikiri unapewa heshima, pana kitu unapimiwa lakini nafikiri kipo kisheria, hebu aliangalie Mheshimiwa Waziri, mwenzetu angalau anapanda bombadier lakini pale pana usumbufu bandarini, pembeni ukifika unapewa heshima zote na wafanyakazi. Ule mzigo wako unapimiwa kisha unalipishwa, kitu cha ajabu kwelikweli.

Mheshimiwa Spika, kutengeneza jina kuna kazi, kuliharibu ni mara moja’ kutengeneza jina kuna kazi lakini
kuharibu ni mara moja. Hizi sheria tuziangalie, hapo zamani meli pale Msasani zilikuwa zikijaa kuja kwenye bandari ya Dar es Salaam, tulikuwa tuna kazi nzuri kupita kiasi lakini sasa zimeshaanza kupungua hebu tujiulize kulikoni kuna tatizo gani? Tusiwe tunatengeneza sheria tu baadaye zikaja zikatubana wenyewe, tuangalie nini athari yake na nini faida yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba kuunga hoja mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Bila kupoteza muda wala kurembaremba sana, kwanza nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na baadhi ya watendaji wake, maana wengine siwajui kwa umakini wao na utendaji wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumsifia Mheshimiwa Waziri, ikiwa yeye ana pumzi zake, na mimi nina pumzi zangu. Watu wengi baada ya mtu kuondoka ndiyo humsifu mtu kwamba alikuwa mzuri; lakini namsifu nikiwa niko hai na yeye yuko hai.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ni miongoni mwa Mawaziri wa Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa bora katika utendaji wake, bila kuficha! Mheshimiwa Waziri ni msikivu, utendaji wako tumekuwa tukiuona ambao hautaki torch. Ni Waziri unayeshindana kidogo na Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba, kwa muda mfupi amechukua Wizara mbili kuongoza na huo ni kutokana na umakini wako Mheshimimiwa Waziri. Waziri ambaye hana Jimbo, akitokea Ikulu mara nyingi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kutokana na elimu yake, utendaji wake, umakini wake na busara zake, ndiyo maana Marais wengi huvutiwa na wewe kutokana na umakini wako. Mheshimiwa kuna usemo usemao; mgema akisifiwa, tembo hutia maji, unatokea Zanzibar. Hata Mheshimiwa Kishimba anatamani kuwa Mzanzibari Mbunge wa Kahama, lakini Mungu hajamjalia. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaigusa Bandari ya Dar es Salaam na nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe kwa kazi aliyoifanya pale. Mabenki yale baada ya kuchangia kipindi cha mwaka uliopita, akafungua benki na tumeziona. Mheshimiwa Dr. Mwakyembe keep it up! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hapa, kidogo Mheshimiwa Waziri anisikilize kwa umakini kabisa; na ball pen iwe karibu kuandika; yatamgusa Engineer Kakoko wa bandari ile na Port Manager ambaye ana-act, Fredy John Liundi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyo katika bandari ya Dar es Salaam bado kuna matatizo, kauli siyo nzuri na sisi Waislamu tunasema maneno mazuri ni sadaka au methali inayosema, kauli nzuri humtoa nyoka pangoni. Sasa Mheshimiwa Waziri anza kuandika mwanzo. Customer care kwanza haipo katika bandari ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, customer care katika bandari ile haipo. Mheshimiwa Kakoko siyo kila anayepepesuka ni mlevi. Kazi zote hizi Mheshimiwa Kakoko huwezi kuzifanya peke yako. Kama yupo juu, basi nafikiri utakuwa unasikia huko. Madaraka haya lazima mgawane na wenzio, utakuja kuumia, sisi bado tunakuhitaji. Huu ni ushauri wangu, bado tunakuhitaji. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, ndungu yangu, trend ya mizigo ya miaka kumi au saba ya nyuma, mizigo iliyoingia na iliyotoka na sasa hivi, kaiangalie. Tuelezane ukweli, mizigo iliyoingia na kutoka imeshuka. Ni ushauri wangu. Kaangalie trend ile ya miaka saba au sita ya nyuma au mitano iliyotoka hivi sasa, utaona ukweli ulipo. Hali siyo nzuri kusema ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ni declare interest, mimi ni mfanyabiashara, siwezi kudharau dafu kwa embe la msimu. Hii siasa kesho Mungu akijaalia haipo, lakini dafu siku zote unaweza kulipata. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna VAT on transit hivi vitu wananchi wanalalamikia sana. Ajira mnavyotangaza, hivi juzi mmetangaza ajira, sijui kama mmezitangaza, lakini kuna watu mmewaajiri. Tuwe wawazi, tuwe wakweli katika bandari.
Mheshimiwa Naibu Spika, DG baadhi ya wafanyakazi wanamwogopa sasa hivi. Kama wanapita njia hii wafanyakazi wanamwogopa, wanapita njia nyingine. Liandike, ulifuatilie kama nasema ni ya kweli ama siyo ya kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, wafanyakazi wengine wanaomba muda wao wa kustaafu kabla haujafika, wanaogopa bandarini kutokana na matukio yanayotokea. Suala za wizi limekuwa wizi tu. Ndiyo yale niliyosema, siyo kila anayepepesuka ni mlevi. Muda wa kustaafu wafanyakazi haujafika, watu wanataka kustaafu kuondoka, wameshachoka. Tena wale wazoefu; tutakuja kutafua rasilimali hiyo wakati huo hatuna. Huu ni ushauri wangu, Mheshimiwa Waziri fuatilia niliyokwambia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije DMI (Chuo cha Baharia). Kuna eneo pale limekaa miaka nane au kumi, kibanda kimeshaanguka. Unafanya biashara; mimi mwenyewe binafsi nilishapeleka barua pale, lakini hakuna majibu, hakuna kilichofanyika. Nafikiri wenyewe wapo hapo. Imekuwa kama nyoka wa mdimu Mheshimiwa Waziri. Nyoka wa mdimu hukaa kwenye mdimu, yeye hana kazi nazo na ukienda kuchuma, anakurukia, faida iko wapi? Siyo kitu kizuri!
Kodi zingesaidia! Wengine wamekodishwa maeneo yale, wengine hawajakodishwa, wako kinyume na utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika Bandari ya Letakii, hapa pana dhambi na maonevu makubwa. Wafanyabiashara wa Zanzibar na Zanzibar tegemeo lake kubwa ni biashara. Leo viazi, cabbage, pilipili ina-megati nane inapekuliwa. Vipo hapa hapa, local food hiyo, hatutendi haki. Kama unataka, nitakutajia; kuna geti namba tatu Mheshimiwa Waziri. Malindi pana geti pale pale, mita 50 haijafika, pana mizani, halafu unakuta mizani yenyewe. Usumbufu, mnasema mnapunguza foleni, huku mnazidisha foleni. Umefunga mlango wa mbele wa nyumba wa nyuma umefungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanalipa ada za bandari pale kwa muda mrefu, lakini charge zimekuwa nyingi. Bandari zimekuwa na mapote; ikija mvua tope, likija jua, vumbi; wafanyakazi wana mazingira magumu katika kazi ile. Nampongeza sana Acting Port Manager, John Liundi, kazi anayofanya pale nitakuwa sijamtendea haki na nitakuwa mtovu wa adabu wa mwisho kama sikumshukuru kwa mazingira ya kazi anayofanya pale. Hongera Port Manager unayekaimu kwa muda. Pengine Mungu atakujalia muda siyo mrefu utatoa fupa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna yule mlinzi pale anayeshughulikia ulinzi wa bandari. Kwa muda mrefu ulinzi umeimarika bandari ya Dar es Salaam. Tuwape haki zao. Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Jamaa wa pale anaitwa Twange, amefanya kazi nzuri ya ulinzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla muda haujamalizika, nije kwenye ndege, Bombardier sasa.
Mheshimiwa Waziri chukulia mfano Pemba kule Makombeni kuna mabonde ya mpunga, umelima, umeshaotesha mpunga wako, kuna ndege wanaitwa tongwa wale, ukishauacha unakuja kuuvuna. Hawa wana malalamiko.
Mheshimiwa Naibu Spika, umenunua baiskeli, leo unashindwa kununua pump tu kujaza upepo baiskeli! Hebu waingizeni pesa tusije tukawalaumu, baadaye tukawa tunasema Tanzania wanafanya vibaya. Wanahitaji mtaji hawa. Kama hamuwezi, wakopesheni five billion. Leo tunafanya vitu vizuri, baadaye tutakuja ku-fail.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu msikivu sana yule CO hata jina lake silijui mimi. Ni rasilimali kubwa sana yule. Maneno yake tu ukisikia akizungumza utafikiri asumini zinatoka mdomoni, harufu yake. Ndiyo yale walisema, maneno mazuri ni sadaka. Ongeza mtaji wa Mtanzania. Hawawezi kufanya kazi wale bila kuwa na mtaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutoka hapo utaratibu wa Bombardier jamani, kuja usiku sisi kama walinzi tumechoka. Jaribuni kupanga utaratibu, Bunge linaanza Jumanne. Pangeni Jumatatu angalau saa 10.00 tuondoke kule. Badilisheni utaratibu huu. Halafu bei zake zikoje? Leo unanunua bei nyingine, kesho bei nyingine, kiti ndiyo kile kile. Hebu jaribuni kufanya utaratibu (format) mwingine. Bunge hapa linaanza Jumanne, Jumatatu angalau ndege ingeondoka saa 10.00 pale.
Hayo ni maoni yangu, nanyi kama hamtaki mtachangia. Kila mmoja ana uhuru wake wa kusema.
Nije kwa SUMATRA. Mheshimiwa Branch Manager, sheria hii inaumiza watu...
Mheshimiwa Branch Manager, sheria hii inaumiza (Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi bila kupoteza muda nichukue fursa hii kukupongeza wewe kwakuniruhusu kuchangia. Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa muda mfupi kuwa Waziri katika Wizara mbili tofauti, hii ni kutokana na utendaji wake na umakini wake Mheshimiwa Waziri. Nikupongeze vilevile kwa timu ya Singida United kupanda daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nimpongeze Kamishna Hamdani Omar Makame kwa kutuongoza vizuri Zanzibar katika kipindi chake na nimtakie kila la kheri na mapumziko mema ya kikazi. Nitakuwa sijamfanyia haki Kamishna Johari Masoud Sururu waImmigration Zanzibar kwa kazi anayoifanya Zanzibar, amekuwa makini katika utendaji wake bila ya kujali mvua, jua, usiku, mchana anapiga kazi, nimpongeze sana Kamishna Sururu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitakuwa sijamfanyia haki Kamishna Musa Ali wa Zanzibar, kwa kujenga vituo vingi Zanzibar vya polisi zikiwemo nyumba. Amejenga nyumba na vituo vya Polisi Paje katika Jimbo langu ninakotokea.Vilevile amejenga vituo cha polisi karibu saba kikiwemo cha Jambiani, Nungwi, Bumbwini, Kiboje, Meli Nne, Fumba, Jozani na Pemba – Chokocho. Mheshimiwa IGP huyu mtu nafikiri ni hazina kubwa sana unisikilize kwa makini Mheshimiwa IGP, amefanya kazi vizuri sana na kubwa zaidi kujenga Kituo cha Afya Ziwani katika Makao Makuu ya Polisi, kituo cha kileo kabisa, huyu ni mtendaji kazi kupita kiasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri hapa unisikilize kwa makini vinginevyo shilingi nitaizuia. Kuna mjenzi nimeshakwambia mara mbili/mara tatu, amejenga nyumba na Kituo cha Madungu anadai shilingi milioni 220, leo mwaka wa tano anahangaika,mpaka akapata maradhi anafanya mazoezi bila kutaka kupata ngazi kwenda na kushuka.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili nitakuwa mkaidi sana kama hujamlipa haki yake na Mwenyezi Mungu kamjalia kapata maradhi ya mitihani sasa hivi. Mtu anadai shilingi milioni 220; ameshajenga vituo, leo miaka mitano na baya zaidi hata kwenda kukaguliwa hazijaenda kukaguliwa, hilo ni jambo la kusikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na IGP naomba mnisikilize, kumekuwa na kilio cha Wabunge humu ndani kunyanyaswa na wanaambiwa baada ya miaka mitatu muda wao wa Ubunge umekwisha, kuna Mbunge wa Ulanga yumo ndani humu, anaonesha kitambulisho kwa traffic anaambiwa wewe baada ya miaka mitatu Ubunge wako unaisha, siyo kauli nzuri hiyo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tunalipigia kelele katika vikao vyetu siku zote. Traffic wamekuwa wameshika mpini, Mbunge hana thamani mbele ya traffic. Leo Mbunge wa Ulanga yule anaambiwa baada ya miaka mitatu na kitambulisho anatoa, hatuwezi kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kuhusu hali za uchakavu wa nyumba, Mheshimiwa Waziri ulikuwemo Ziwani umeona askari wetu wanaishi vipi, mchana haendi kujisaidia, anakaa mtu upande huo huko anamwambia nitizamie mtu anakuja huko, ili apate kwenda chooni! Hali hairidhishi, mazingira siyo mazuri wanayofanya askari, vitendea kazi havipo, tunafanya nini? Hali ya Ziwani ndiyo Makao Makuu ya Polisi hairidhishi.(Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile askari wanakaa muda mrefu kupandishwa vyeo, anafika miaka 15 mpaka mtu anakaribia kustaafu hajapanda cheo! Hii siyo halali.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya vituo vya polisi vimekuwa vichakavu sana, ulikaja Pemba, pia wale wanaojenga mbona hamuwalipi?(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo nichangie kuhusu mahabusu.Polisi wanapata shida wanatoa pesa zao mfukoni kuwahudumia mahabusu.Pia hali ya bajeti Zanzibar kupiga doria, umekuwa mtihani vilevile mafuta.

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Sitaunga hoja mkono mpaka jamaa apate haki yake.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nichukue fursa hii kukupongeza kwa dhati kwa kuniruhusu kuchangia hoja hii. Bila kuniruhusu nisingeweza kuchangia hoja hii kwa hiyo nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada anazochukua kwa wananchi wake na kwa jinsi anavyowatumikia. Nichukue fursa hii tena kuwapongeza wale Mawaziri na Naibu Mawaziri waliopanda hivi juzi kwa kupata vyeo hivi na niwape pole waliokuwa wakitegemea, lakini hawajapata nafasi hizi mpaka muda huu. Niwaombe wasikate tamaa, Mwenyezi Mungu siyo Athumani lakini niwaambie tu uteuzi wao huu wanaujua nini maana yake? Uteuzi huu Mheshimiwa Rais aliotoa Mawaziri na Naibu Mawaziri ili wamsaidie kutumikia wananchi kinyume chake Mawaziri na Naibu Mawaziri simu mnazifunga, hamuwatumikii wananchi, siyo kitu kizuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaziteua Wizara kama Wizara ya Afya wenye matatizo ya afya waende afya, Wizara ya Elimu waende wenye matatizo na elimu, Wizara ya Ardhi waende wenye matatizo ya ardhi lakini kwa masikitiko simu ukimpigia Waziri hapokei, ukimpigia Naibu Waziri hapokei, humu ndani tumo sawasawa haya mambo yanageuka. Aliyeko mbele mngoje nyuma, aliyeko juu msubiri chini atateremka tu. Hivi vyeo ni dhamana na tutakwenda kuulizwa siku ikifika tumewatumikia vipi wananchi. Kuna milango mitatu ya kuingilia humu ndani ya Bunge hili, kuna Jimbo kutoka Ikulu, kuna Viti Maalum na uchaguzi wa wananchi, hiki chombo kina uzito kutokana na wananchi. Wananchi ndiyo waliopotupa dhamana ya kuja kusema matatizo yao humu ndani. Kuna siku tutakwenda kuulizwa hizi dhamana zetu tumezitumia vipi, haya mambo ya kupita tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika mchango wangu sasa kuhusu TRA. Mheshimiwa Waziri kwa masikitiko na unyonge mkubwa sana kitendo ulichokifanya cha kutatua kero ya Kenya na Tanzania kuhusu maziwa na cigarette umechukua muda mfupi sana, lakini kero ya Zanzibar bado kila Waziri kinamshinda. Leo Muungano wetu huu tunasema kwa mdomo tu tunataka uendelee kudumu kwa vitendo. Mali inayotoka Uganda, Kenya, Burundi, Zaire, Zambia ikiingia Tanzania wala huulizwi kitu, leo mali inayotoka Zanzibar ukiingia nayo Dar es Salaam utafikiri umeleta unga, huu uonevu wa aina gani? Dkt. Mpango Wazanzibari hamtufanyii haki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mzanzibar kachukua gauni zake tatu anakuja hapo bandarini anaambiwa weka chini, tv tu moja, mbili anaonewa, hii haki ikoje? Nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Saada Mkuya, kazungumza vizuri sana lakini huu Muungano tunaosema ni wa upande mmoja tu jamani? Tunasema huu Muungano uendelee kudumu na mimi nasema uendelee kudumu, Zanzibar ukiacha zao la karafuu tegemeo kubwa ni biashara. Wenzetu Tanzania Bara Alhamdulillah, endeleeni kushukuru tuna madini, mbuga na neema nyingi tunazo lakini leo biashara ile nguo tatu au nne, miche mitatu ya sabuni unasumbuliwa pale mwisho mchele unaonunua pale bandarini unalipishwa pana kimizani kidogo kimewekwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala siyo la upande mmoja Mheshimiwa Saada kazungumza bado hujafika Zanzibar, mimi nikuombe ufike. Pindipo utakapokusanya mapato Mheshimiwa Rais atakusifu, tuangalie biashara, huku kidogo, huku kidogo, kuku anataga yai moja ukamlazimisha mayai matatu utamuua, utakosa kuku. Chukua huku kidogo, huku kidogo pishi inajaa lakini kuku yule anataga yai moja, unamlazimisha leo leo atage matatu atakwenda wapi, tutaua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu twende Kariakoo ukaangalie milango ya maduka nani anaitaka saa hizi? Samora mlango ulikuwa unakodishwa bei kubwa sasa hivi milango imefungwa. Fikiri Mheshimiwa Waziri huu ni ushauri wangu wa bure wala sitaki kulipwa mimi. Kaa na wafanyabiashara utazame nini tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Muungano Zanzibar tunauhitaji kwa kila hali miongoni mwao ni mimi kutokana na udogo wetu, lakini mzigo utoke Kenya, Rwanda, Burundi hauulizwi kitu, mzigo ukitoka Zanzibar ukifika hapa aibu. TRA ni moja, formula yake ni moja, vigezo vyake ni vimoja, Waziri nikuombe kwa masikitiko makubwa, Wanzanzibar ukiacha karafuu wanategemea biashara. Juzi umetatua tatizo la Kenya kwa muda mfupi tu, leo unatuaacha sisi ndugu zako wa damu. Umetatua juzi tu tumekupongeza lakini litatue na hili pia. Taa huwashi nje, unawasha kwanza ndani ya nyumba yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawashaje nje kabla ya kuwasha ndani huwezi kuona na sadaka sisi tunasema inaanzia nyumbani ndipo utoe nje. Kwa hii kero dada yangu kazungumza sana hapa, fanya uwaite wafanyabiashara, wanafunga milango wanaanza kuondoka. Tembea na kama uko tayari tufuatane nikakuoneshe mlango huu umefungwa, huu umefungwa utahesabu milango mingapi. Tufike wakati tupunguze, tujihurumie jamani mapato tunahitaji wewe kusanya mapato mazuri uone Mheshimiwa Rais atakavyokusifu. Nchi inataka kwenda kwa mapato lakini tukianza kubana kwa marungu, leo watu wananyang’anywa komputa zao wanavamiwa na TRA, polisi imekuwa TRA sasa hivi watu wanasumbuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri sisi sote humu ndani vyeo vyetu vimoja tunaitwa Waheshimiwa tofauti tu ni Waziri na Waheshimiwa na haya mambo yanageuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba kukaa.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo na Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017, Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nisikupotezee muda, mimi nitahitaji maelezo maana nikichangia itachukua muda mrefu, nitahitaji maelezo kwenye mambo kama manne Mheshimiwa Waziri. Nikupongeze tu juzi nilikuona katika sherehe za Siku ya Sheria Duniani na ulihimiza sana Mheshimiwa Waziri, mahabusu sheria ya kesi zao zile haraka, hebu tueleze kuna tatizo gani Arusha kule watu wana miaka sita mpaka leo wanachunguzwa nini? Kesi mpaka leo au kunatakiwa ushahidi wa Kinyamwezi mpaka ukamilike? Watu wanateseka, wana familia zao, wana watoto, wengine wanataka kuthubutu kuachwa, hebu tueleze tatizo ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kumejitokeza tatizo hivi sasa Zanzibar watu kuchukuliwa wakaja kushitakiwa huku Bara, je, Zanzibar hawana Mahakama? Hawana wanasheria? Tatizo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sheria inavyosema unapokamatwa ndipo unapohukumiwa. Leo sijaona mimi mtu kakamatwa Pakistan akaletwa Tanzania, kakamatwa Mascut akaletwa huku, hebu tueleze utaratibu gani wa sheria huu, ukoje? Mimi si mtaalamu wa sheria, lakini haya mambo yanajitokeza sasa hivi na yanazidi kuendelea, keshokutwa usije ukanichukua mimi ukanileta huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini na lingine nikuombe, hebu katika hiyo orodha ya mambo ya Muungano, na hii Mheshimiwa Chenge ulikitunga wewe kitabu hiki ukiwa Mwanasheria mwaka 2005. Kuna orodha hii ya mafuta na gesi, mali pamoja na mafuta yasiyochujwa na matokeo ya mafuta aina ya petroli na aina nyingine ya mafuta, limo humu na sheria hii ilivyoelezwa, angalia Ibara ya 64 Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba na Sheria; “Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, sheria hiyo itakuwa ni batili na itatanguka na pia endapo sheria yoyote itakayotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa ni batili na itatanguka.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni vichekesho, kwa hiyo bado tuna mtihani wa mafuta Zanzibar. Pamoja na jitihada zilizochukuliwa, niwapongeze Marais wote wawili, lakini bado, na ulijibu hapa, ulimjibu Mheshimiwa Juma Ngwali kuwa bado mafuta ni tatizo. Hebu lipate kuliondoa ili Muungano ulete sura nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na lingine, mara nyingi waislamu wamekuwa wakiahidiwa Mahakama ya Kadhi humu ndani hebu tueleze imefikia wapi? Hata katika Katiba Iliyopendekezwa na wewe ulikuwa ni Mjumbe katika Tume ya Warioba, hebu tuelezeni juu ya Mahakama ya Kadhi nayo ina mambo matatu, ndoa, mirathi na talaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamekuwa wakilalamikia suala hili, na hili Bunge hili ukifuata Hansard limezungumza ndani wakati wa Mheshimiwa Mizengo Pinda kuwa, utaratibu fulani utaletwa, lakini mpaka leo? Imekuwa kama mtoto wa kuku anayetaka kunyonya, kesho, keshokutwa mpaka anakuwa kuku, maziwa hayaoni. Hebu tuelezeni lini utaratibu huu utaletwa wa Mahakama ya Kadhi? (Kicheko)

Mheshimiwa Waziri ulikuwa Mjumbe katika Tume ya Warioba na waislamu wengi walizungumzia suala hili. Kuna mambo ya ndoa, talaka na kuna mambo ya mirathi, hebu tuendelee na utaratibu wa kulieleza suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nisikupotezee muda. Naomba nafasi hii umpe mtu mwingine achangie dakika zilizobaki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nikushukuru, ntakuwa mchoyo wa fadhila kama sikukushukuru kwa kupata nafasi hii. Niyakumbuke maneno ya Mheshimiwa Rais Mstaafu, Mheshimiwa Salmin Amour Juma, almaarufu Komando, alikuwa na maneno mawili akisema urafiki na nchi, kwanza nchi urafiki baadae.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa January Makamba, Waziri wa Wizara hii jinsi anavyojituma bila kujali mvua, jua, usiku au mchana, anapoitwa Zanzibar wakati wote anatii amri; nimpongeze sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu cha kupendeza sana Wizara hii, hasa Naibu, angetoka angalau Zanzibar, ingeleta sura nzuri sana ya Muungano, ndiyo Wizara ya Muungano, ingeleta sura ya Muungano. Hata hivyo, siwezi kuingilia mamlaka ya Mheshimiwa Rais, nataka kujua nini Muungano, nini definition ya Muungano; what is union? Umuhimu wa kuungana watu, kuwa pamoja, kushirikiana katika nyanja mbalimbali kiuchumi, ulinzi, ajira, huu ndiyo Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini Muungano, definition yake ni hii; umuhimu wa kuungana watu kushirikiana, kuwa pamoja kiuchumi, nchi, ulinzi, ajira. Hata Tume ya Mheshimiwa Jaji Warioba ilisisitiza sana umuhimu wa Muungano huu kuwepo, katika watu 1,000 labda watu wawili watakataa Muungano huu kuwepo. Lakini kuna mambo muhimu au fomula gani ya kuendesha Muungano wetu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Mheshimiwa Jaji Warioba haikukataa Muungano huu kuwepo, katika watu1,000 labda watu wawili watakataa Muungano huu. Kwa hiyo Muungano huu tunauhitaji na ukizingatia keshokutwa, Mheshimiwa Machano amezungumza, tunatimiza miaka 54 ya Muungano wetu huu. Hata hivyo, kuna baadhi ya watu mnawalea vibaya, wanachafua Muungano huu bila kuwaonya. Tatizo tutafute formula ya kuendesha Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kupoteza muda, nije kwenye changamoto za Muungano, akiwemo Mheshimiwa Keissy. Ya nini kusema … (Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila mpangilio)

T A A R I F A . . .

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, narudia yaleyale, ni mzee wangu, adabu kitu cha bure, nitaendelea kumheshimu hata tukatoka nje. Mimi ni jirani yangu, nikianguka leo ataniokota yeye na akianguka leo nitamuokota mimi, sisi sote Waislamu, sisi ndugu moja lakini ukweli utabaki ukweli; moja moja mbili mbili, kavu kavu mbichi mbichi, mimi naendelea kukuheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye changamoto mwaka jana Mheshimiwa January alizungumza zimebaki changamoto tatu, nimpongeze. Hata hivyo, changamoto hizo mpaka leo nafikiri zipo ICU, hazijapata ufumbuzi, wanakaa vikao lakini zinafika mahali zinapata kigugumizi. Angalia Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ukurasa wa sita Sura ya Saba, vifungu 133 na 134, huu ndiyo mzizi wa fitna yetu ya Muungano, ni Joint Finance Commission, ukamaliza huu Muungano umekwisha, Mungu atuweke hai. Joint Finance Commission, Jamhuri ya Muungano Katiba 1977, nafikiri ukurasa wa sita, kifungu 133 na 134, huu ndiyo mzizi wa fitna uliobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumza humu katika mahali palipokuwa nidhamu yake siwezi kusema nzuri bandarini. Watu wamekuwa wanapata mpaka maradhi. Waziri wa Fedha hayupo hapa, Naibu Waziri ampelekee salamu Mheshimiwa Waziri. Huu Muungano tumeungana kwa nia njema, isiwe kama Lugha ya Kiarabuukiandika unavutia kwako tu, maandishi ya Kiarabu ukiandika unavutia kwako tu. Naibu Waziri wa Fedha, Waziri wa Fedha hayupo hapa, lakini mahali wanapoteseka watu, Mheshimiwa Tauhida kazungumza, mtu kavunja TV kwa uchungu, ule ni uchungu, tunaumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara Rais wetu tumemuona shahidi anawatetea wanyonge, anasimamisha misafara njiani kuwasikiliza wananchi, Wamachinga kaachia huru wafanye biashara. Leo mtu katoka Zanzibar, Zanzibar uchumi wake ukiacha karafuu ni biashara, tuwe wakweli. Imefika mahali kero hizi hazijafika mahali, double standard, VAT imekuwa kupita kiasi, tutaendelea kusema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna msemo usemao asemaye hachoki…

T A A R I F A . . .

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa aliyonipa nimeipokea kwa mikono miwili. Taarifa nzuri, taarifa ambayo inaleta sura ya Muungano wetu; nimshukuru sana Mheshimiwa Mattar kwa umakini wa hali hiyo. Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukizingatia kuna mambo matatu ya uchumi haya yako Tanzania Bara, sera za kodi ziko Tanzania Bara, sera ya sarafu iko Tanzania Bara. Hebu tufike mahali haya madogomadogo wenzetu mtuachie au tubadilishane, miaka mitano mchukue ninyi, miaka miwili tupeni sisi. Sera hizi muhimu, nyenzo hizi muhimu mnazo ninyi, Sarafu ya Tanzania, Benki Kuu, kodi hizi, mna mbuga nyingi za kuendesha, mna madini mengi. Zanzibar uchumi wake ni biashara, mambo madogo madogo haya ifike mahali… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nikushukuru kwa kunipa fursa hii, jioni hii kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Hata Mheshimiwa Rais wetu amekuwa akihimiza sana viwanda na kasi yake. Tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, maneno mazuri sisi Waislam tunasema ni sadaka au maneno mazuri humtoa nyoka pangoni. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, uongozi ni dhamana, ni jambo la kupita, leo lipo kesho halipo na baada ya siasa kuna maisha nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, biashara ni nini? Biashara haifanywi na mtu mmoja, biashara lazima iwe na monopoly. Biashara haiwezi kufanywa na mtu mmoja hata kidogo. Uzuri wa Wizara ya Biashara haiwezi kwenda bila ya fedha. Fedha ndiyo biashara, biashara ndiyo fedha, kwa hiyo, hivi vitu kidogo vinaoana. Hapa kidogo Mheshimiwa Waziri nataka unisikilize kwa makini, hasa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mpango, nikuombe sana, kuomba siyo kosa, kuiba ndiyo kosa, kama kuna watu wanateseka, Benki ya FBMEwatu wanateseka, nimepiga kelele, nitaendelea kupiga kelele mpaka pumzi yangu ya mwisho. Watu wanaweka haki zao kule, wananyanyasika, wengine wameshaanza kutangulia mbele ya haki, hakuna harufu yoyote na Benki Kuu ndiyo dhamana na kama nilivyosema cheo ni dhamana na tutaenda kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu au mbele ya haki, tumetumia vipi dhamana zetu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanataka kusomesha, fedha zao zimekwama benki. Mnawaambia nini? Benki Kuu iko chini ya Wizara ya Fedha, Bureau de Change zote mna-control ninyi. Tumeona Greenland Bank imefungwa na wakati huohuo mnasema fedha za wateja ziko salama, salama iko wapi? Au Salama jina la mtu? Maana kuna jina la mtu Salama. Kuna wawekezaji Zanzibar pesa zao zimekwama, wafanyakazi wa benki pesa zao zimekwama, mishahara yao haipatikani.

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa huruma na unyenyekevu, sijawahi kukuambia hivi Mheshimiwa Dkt. Mpango. Wewe binadamu na mimi binadamu, tuwe na jicho la huruma. Je, ungefanyiwa wewe au mimi tungekubali? Tuwaonee huruma wananchi. Wananchi ndiyo walioweka Serikali hii madarakani. Mtu ana shilingi milioni 200, unampa milioni moja na laki tano ni sawasawa na kumpa peremende baadaye ukamnyang’anya, haifai hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika kero za Muungano, biashara ndogondogo bandarini. Hii tuliambiwa moja kati ya kero ya Muungano. Msijali mtu wa mbali, jirani yako ndiyo mtu wa karibu. Tumetimiza miaka 54 ya Muungano huu na tuombe uendelee kudumu. Wafanyabiashara bandarini Mheshimiwa Mwijage wanateseka na hesabu inaanza moja ndipo ije mbili na tatu. Hawa wote wafanyabiashara wameanzia biashara ndogondogo wakafika kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi wa Zanzibar amechukua TV moja, amechukua mashati yake matatu, amechukua kilo zake sita za sukari akafika pale ananyanyaswa. Imefika wakati watu wakathubutu kuvunja TV zao, huu siyo ubinadamu wala siyo uungwana. Nikuombe Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Waziri wa Biashara mliangalie hili suala. Leo imekuwa mali inayotoka Zambia, Uganda, Burundi na Kenya inaingia hapa iko salama, inayotoka kwa ndugu zetu upande wa pili utafikiri umeleta bangi au unga, kwa nini tunafanya hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema na nitaendelea kusema, baada ya siasa kuna maisha nje, haya mambo ni ya kupita na cheo ni dhamana lakini hatuwatendei haki. Zanzibar inategemea zao la karafuu, uchumi wake wa pili ni biashara. Leo bandari imezuiwa usajili wa meli, kuna matatizo hatujui kinachoendelea, lakini tusiwanyanyase wafanyabiashara. Mtu ana TV moja, mbili, atakula nini? Anakuja na boti yake asubuhi, jioni apate kuuza aondoke lakini anakuja mzigo unaoza ndani mle, ndiyo lengo hilo? Katika moja ya kero kubwa ya Muungano hili ni moja, tuwe wakweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Kiwanda cha Sukari cha Mahonda, hapa nisikilizeni vizuri. Kiwanda hiki kipo Tanzania, Tanzania hii imeitwa na Zanzibar ikiwemo. Tunalinda viwanda vya Tanzania, je, Zanzibar haipo Tanzania? That is my question. Tunalinda viwanda vya Tanzania, Zanzibar haiko Tanzania? This is my question au hailindwi Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalinda viwanda vya Tanzania Bara kwa hiyo Zanzibar haipo? Pombe, nondo, saruji, unga wa ngano unaingia Zanzibar lakini bidhaa kutoka kule kuleta huku imekuwa mtihani, tuwe wakweli. Ndiyo yale nimemwambia Mheshimiwa Keissy, moja iwe moja, mbili iwe mbili, mbichi iwe mbichi, kavu iwe kavu. Kama tunalinda tuseme tunalinda viwanda vya Tanzania Bara siyo Tanzania, tuwe na vigezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. au Prof. Mwijage maana cheo chao kikubwa, juzi ulijibu swali la 205. Mheshimiwa Spika aliona udhaifu wa swali hili, ningesema mimi ingekuwa mtihani, huku unakataa Tanzania hakuna uhaba wa sukari, huku unasema baada ya miaka mitano sukari itakuwa ya kutosha, tukamate wapi? Huku unakataa, uhaba wa sukari haupo, baada ya miaka mitano unasema uhaba wa sukari utakuwa umekwisha. Sasa tunafanya nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Waziri toka kaangalie bandarini, hiyo sukari imeshafika usije ukauziwa mbuzi kwenye gunia. Uende ukapate ushahidi, usije ukapata ushahidi wa Kinyamwezi. Nenda kaangalie hii sukari uliyowapa vibali imefika? Isije kufika Ramadhan hapa tukawasumbua au kuwatesa wananchi. Narudia tena, Serikali hii isingekuwa madarakani bila wananchi. Hata Uwaziri wako huu,Mheshimiwa Waziri ungekuwa mtihani tungetawala nini, miti au barabara? Wananchi ni kitu muhimu. Hata Mheshimiwa Rais mwenyewe anawajali wananchi, tumpongeze kwa dhati kabisa hasa wananchi wa chini, credit yake kubwa iko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isiogope kula hasara kwa mambo madogo madogo kama haya na wewe mshauri Mheshimiwa Rais usiogope kuwa hiki kiko hivi, hiki kiko hivi, mueleze tuna upungufu huu. Tuliwapa vibali vya sukari, mimi na ninyi, twende mguu kwa mguu kama sukari mliyotumbia imeshaingia tani 135,000, twende tukaiangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijamaliza lakini itabidi nishukuru hivyo hivyo kwa muda ulionipa.
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyeniwezesha kusimama hapa. Huu sio uwezo wangu wala nguvu zangu wala ubabe wangu ni neema yake hii, na pumzi alizonipa hapa za kuniazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kukushukuru wewe kwa kunipa fursa hii kuchangia muswada ulio mbele yetu, muswada muhimu na sijui niseme niilaumu Serikali kidogo kwa kuchelewa kuleta muswada huu. Muswada muhimu kwa wananchi, umechukua muda mrefu haujafika hapa, wananchi wakaendelea kuumia.
Mheshimiwa Nibu Spika, lakini vilevile nitakuwa sijamtendea haki Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Msaidizi wake Naibu Waziri, Dkt. Hamisi Kigwangalla, team captain wa timu ya Bunge kwa muswada huu.
Mheshimiwa Nibu Spika, lakini mimi ni mdau wa Kamati hii, lazima ni-declare interest. Sifa pekee za aina yake ziende kwa Mkemia Mkuu wa chombo hiki. Mkemia Mkuu amekuwa akifanya kazi katika mazingira magumu bila kujali mvua, jua, usiku mchana. Mkemia Mkuu hongera sana na usitegemee malipo kwa binadamu, tegemea malipo kwa Mwenyezi Mungu. Kazi uliyofanya Mheshimiwa Mkemia Mkuu ni kazi nzito sana katika mazingira mazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwape pole sana watendaji wa kitengo hiki, wamekuja Kamati karibu mara nne, kwenda na kurudi hawapungui watu 20. Ndipo pale Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nilipotaka Mwongozo wako kwa vitengo hivi kwenda na kurudi, gharama ya mafuta, kulala, kula, kunywa, inakuwa ni gharama kuliko Bunge likabaki pale Dar es Salaam, ndicho kilio change hiki nilikiona muda mrefu na nilikuwa na Kamati jirani palepale, Wizara ya Ulinzi walikuwa wanakuja kwa ndege, gharama ni kubwa, tulifikirie hili suala kwa ajili ya kubana matumizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa nisichangie, nimekaa sana kwa kipindi kirefu kusikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge, lakini kazi hii yote mwisho wake ingekuwa bure. Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize kwa makini hivi sasa na ukaanza ku-note hizi point ninazozungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, DNA Tanzania nzima ni moja. Tanzania na ukubwa wake tuliokuwa nao ni moja kwa utambuzi wa vipimo vya binadamu. At least Serikali itafute angalao DNA sita kwa Tanzania ili baadhi ya Kanda ziwekwe. Huwezi mtu kumtoa Mtwara kuja kufuata kipimo Dar es Salaam. Huwezi kumtoa mtu Arusha kuja kufuata kipimo Dar es Salaam! Kweli tunaitendea haki? Niliyazungumza haya Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwenye Kamati haya na yote ukayakubali kwa mdomo, si vitendo, sijui vitendo viko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na mashine moja inahitaji angalao shilingi milioni 700 kwa utafiti niliofanya, lakini Serikali isiogope hasara kwa ajili ya wananchi wake. Serikali hii isingekuwa madarakani bila kuwa wananchi, wananchi ndio Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili, kwanza Serikali ibanwe itoe fedha haraka, ije sheria maalum ya kuibana Serikali kuhusu vyombo hivi vya DNA. Hatuwezi kuja kuzungumza maneno yote hapa wakati vitendea kazi hatuna, hii ni sawa sawa na kutwanga maji kwenye kinu, kazi yote hii itakuwa bure. Kama hawajawezeshwa hawa tunapitisha muswada huu kwa malengo gani? Ndiyo yale tunayosema tuna huruma kwa mdomo, sio kwa vitendo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hapatoshi changamoto ya tatu, watumishi ni kidogo. Waliopo hivi sasa kwa mujibu wa taarifa niliyokuwa nayo kwenye Kamati ni 192, at least wapatikane watumishi 400.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndio pale niliposema nilikuwa sitaki kuchangia, lakini kama sikuzigusa changamoto hizi tukiwa tunachangia muswada huu, wale watenda kazi watafanya kazi katika mazingira gani? Watu sita watafanya kazi gani? Watu 12 watafanya kazi gani Tanzania kutokana na ukubwa wake? Hata sisi Zanzibar tunaitegemea DNA hii, ndio ukweli ulivyo; mtu avuke bahari aje apime kipimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mazingira wanayofanya kazi ukiyaona utalia. Hiyo wafanyakazi 208 wapatikane hivi sasa tukijaliwa. Hapa nitahitaji maelezo Mheshimiwa Waziri, watu 400 wanahitajika, wafanyakazi wako 192, hapa nitahitaji maelezo yakutosha, majengo ya Kanda hayapo. Kama mfano Arusha, Mwanza, Mtwara, Mbeya, huu mji mpya mnaotaka kuufanya sasa hivi, Dodoma, hatujawa tayari. Changamoto hii Mheshimiwa Waziri nitahitaji maelezo ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwa kumalizia, nimuombe Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini Waheshimiwa kama nitawakera kidogo niombe radhi hasa akinamama kuhusu nywele zetu hizi kidogo za kubandika, zina mitihani jamani, zina maradhi. Nazungumza kwa nia njema kabisa, haya mambo nimeyapata mimi kwenye Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mkemia Mkuu wa Serikali kama itawezekana kabla ya kuondoka kesho ukatupa semina bure siku ya Jumamosi kuhusu namna ya kubandika hizi nywele, zina maradhi Waheshimiwa. Niombe radhi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.