Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rukia Ahmed Kassim (6 total)

MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:-
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeifutia The Federal Bank of the Middle East (FBME) leseni yake ya kufanya shughuli za kibenki na kuiweka chini ya ufilisi na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kama mfilisi kuanzia tarehe 8/5/2017.
Je, ni nini hatma ya wateja ambao waliweka fedha zao katika benki yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatma ya wateja endapo benki au taasisi ya fedha itawekwa chini ya ufilisi imeainishwa katika kifungu namba 39(2) na (3) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Kifedha ya mwaka 2006. Wateja wa FBME Bank Limited ambayo sasa hivi ipo katika ufilisi watalipwa kwa utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza ni malipo ya fidia ya bima ya amana. Kwa mujibu wa sheria, mteja mwenye amana katika benki anastahili kulipwa fidia ya bima ya amana, kiasi kisichozidi shilingi za Tanzania 1,500,000 kutegemeana na kiasi cha salio la amana yake wakati benki inafungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za kulipa fidia hiyo zinatoka katika Mfuko wa Bima ya Amana (Deposit Insurance Fund) unaosimamiwa na Bodi ya Bima ya Amana. Wateja waliokuwa na amana zisizozidi kiwango cha juu cha fidia cha shilingi 1,500,000 wakati benki inafungwa watapata fedha zote. Aidha, wateja wenye amana zinazozidi kiwango cha juu cha fidia watalipwa shilingi 1,500,000 kwanza kutoka mfuko wa bima ya amana na salio litalipwa kwa mujibu wa Sheria ya Ufilisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya pili ni malipo kwa wateja ambao fidia ya bima ya amana itakuwa ndogo ikilinganishwa na salio la amana yake wakati benki inafungwa. Malipo haya yatatokana na taratibu za ufilisi ambapo mchakato wake unahusisha kukusanya madeni, fedha iliyowekezwa katika taasisi nyingine na kuuza mali na benki. Kiasi kitakacholipwa kwa kila mteja kitategemea kiasi cha fedha kitakachopatikana kutokana na mauzo ya mali, makusanyo ya madeni na fedha zilizowekezwa katika taasisi zingine.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:-
Je, Serikali imejipanga vipi kutokomeza vitendo vya udhalilishaji kwa watoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua ukubwa wa tatizo la udhalilishaji kwa watoto katika jamii na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana nalo ikiwemo kuhamasisha wananchi kutoa taarifa za matukio ya aina yoyote ya udhalilishaji kwa watoto wakiwemo watoto wa kike. Kupitia Sheria ya Mtoto Na.21 ya mwaka 2009, Serikali imekuwa ikielimisha jamii wakiwemo wazazi na walezi kuelewa wajibu wao wa kuripoti matukio ya udhalilishaji punde yanapotokea. Sheria hii imeelekeza kutolewa kwa adhabu kali kwa watuhumiwa wote wanaopatikana na hatia ya udhalilishaji wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao unaisha mwaka 2021/2022 umeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa. Kamati hizi wajumbe wake wamehusisha Idara za Mahakama, Jeshi la Polisi, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii pamoja na Idara ya Elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ni kuhakikisha kwamba tunadhibiti matukio ya udhalilishaji katika maeneo husika na kuyashughulikia kisheria. Aidha, Wizara imekwishatoa mafunzo ikiwamo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii wapatao 50 kutoka katika mikoa yote 26. Ili kuratibu uanzishwaji wa Kamati hizo, tayari mikoa tano wameshaanzisha Kamati hizo. Vilevile, Serikali imekwishaanzisha Madawati ya Jinsia na Watoto katika vituo 417 katika Jeshi la Polisi ili kuwezesha kushughulikia pamoja na masuala mengine vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitendo vya udhalilishaji watoto vinaweza kudhibitiwa pia kwa kupitia mtandao maalum wa mawasiliano kwa ajili ya kutoa taarifa mbalimbali za udhalilishaji. Namba hiyo naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge inapatikana kupitia namba 116 na Waheshimiwa Wabunge wanaweza kupiga namba hiyo na kuwajulisha wapiga kura wao kuhusiana na namba hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo ya kutumia namba hii na mtandao huu ni kwa mtoto mwenyewe au mtu mwingine kwa niaba ya mtoto kuweza kuripoti tukio lolote la udhalilishaji wa mtoto. Mtandao huu huwasilisha taarifa la tukio hilo kwenye vyombo husika ambapo mwathirika hupata huduma stahiki za kiafya na unasihi na mtuhumiwa kufikishwa katika mamlaka husika za kisheria. Katika kipindi cha Januari mpaka Disemba 2017, matukio 1,072 yaliripotiwa katika mtandao huu na kushughulikiwa.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM aliuliza:-
Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga Uchumi wa Viwanda ifikapo 2025:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwavutia Wawekezaji wa Viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025 limetafsiriwa vema katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2015/2016 - 2020/2021, wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Utekelezaji wa mpango huu unaenda sambamba na utekelezaji wa Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda (Intergratged Industrial Development Strategy) wa mwaka 2011 mpaka mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango na mikakati hiyo inalenga katika kuhakikisha uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na amani na usalama wa nchi, kuondoa vikwazo kupitia sera na sheria wezeshi, uwepo wa miundombinu wezeshi na saidizi na upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu fursa za uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza mipango na mikakati niliyoirejea hapo juu, Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kupitia TIC, EPZA, Balozi zetu nje ya nchi pamoja na Serikali ngazi za Wilaya na Mkoa. Uhamasishaji huo unaenda sambamba na kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kikodi kupitia sheria za uwekezaji pamoja na zile za uendelezaji maeneo maalum ya uwekezaji (EPZ na SEZ). Aidha, Serikali kupitia Taasisi za SIDO, NDC na EPZA inatoa ushauri wa namna ya kuanzisha viwanda vidogo sana, viwanda vya kati na kuvilea ili vikue na kuwa vikubwa.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA (K.n.y. MHE. RUKIA AHMED KASSIM) aliuliza:-

Kuna baadhi ya wanawake wameathirika sana na matumizi ya dawa za kuongeza makalio pamoja na matumizi ya kope na kucha bandia:-

Je, Serikali ipo tayari kufungia saloon zote pamoja na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaotoa huduma hii?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA (K.n.y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa imekuwa ikidhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa na vitendanishi kupitia mifumo yake ya usajili, ukaguzi na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa husika zinapokuwa kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufuatilia ubora na usalama, TFDA imeweka mfumo wa kupokea taarifa kutoka kwa watumiaji na watendaji wa afya juu ya ubora na madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa na vitendanishi. Taarifa hizo hupokelewa kupitia fomu maalum pamoja na mfumo wa kielektroniki wa upokeaji wa taarifa za madhara ya bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za ubora na madhara ya chakula, dawa, vipodozi, vifaa na vitendanishi ni muhimu kwani huzisaidia Mamlaka za Udhibiti Duniani ikiwemo TFDA katika kuchukua hatua mbalimbali kuhusiana na bidhaa inapokuwa kwenye soko mfano kuiondoa kwenye soko, kuifutia usajili au kubadili matumizi ya bidhaa husika. Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, TFDA ilipokea kutoka kwa watumiaji na watendaji wa afya taarifa 238 za madhara yaliyohisiwa kusababishwa na matumizi ya dawa ambapo tathmini zilionesha kuwa ni salama na zinafaa kuendelea kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, TFDA haijawahi kupokea taarifa za madhara kuhusiana na kucha za kubandika. Kutokana na kukosekana kwa takwimu hizo, Serikali haioni sababu ya kufunga saloon zote wala kuwachukulia hatua wanaotoa huduma hii bali Wizara kupitia TFDA itaendelea kutoa elimu kwa watumiaji pamoja na kuwahamasisha watendaji wa afya umuhimu wa kutoa taarifa za ubora na madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa za chakula, dawa, vipodozi, vifaa, vitendanishi na vipodozi zikiwemo kucha za kubandika ili kuiepusha jamii kutokana na athari za kiafya zinazoweza kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara pia inatoa wito kwa watumiaji wa vipodozi kuzingatia masharti na maelekezo ya utumiaji sahihi wa vipodozi hivyo na kutoa taarifa pindi athari za matumizi ya vipodozi na vifaa vya urembo zinapojitokeza.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED aliuliza:-

Baadhi ya magereza nchini yamejaa wafungwa na mahabusu ambao ni wakimbizi.

Je, ni lini Serikali itawarejesha wakimbizi hao makwao ili kupunguza msongamano ndani ya magereza yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba miongoni mwa wafungwa na mahabusu walioko katika magereza hapa nchini ni raia wa kigeni wakiwemo wakimbizi kutoka nchi za Burudi, DRC na nchi nyingine duniani. Magereza yenye idadi kubwa ya raia wa kigeni yapo Mkoani Kigoma ambapo yana jumla ya wakimbizi 91 kati yao wafungwa 38 na mahabusu 53. Gereza la Kibondo lina wafungwa 22 na mahabusu 31, Gereza la Kasulu lina wafungwa wawili na mahabusu 19, Gereza la Bangwe lina mfungwa mmoja na mahabusu watatu, Gereza la Ilagala lina mfungwa mmoja na Gereza la Kwitengo lina jumla ya wafungwa 12. Wakimbizi ambao wamefungwa gerezani wanarejeshwa katika nchi zao za asili baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kuwarejesha wakimbizi nchini kwao kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wahamiaji (IOM) pamoja na nchi ya Burundi. Kuanzia mwezi wa Julai, 2018 hadi Aprili, 2019 jumla ya wakimbizi 31,643 kutoka Burundi walirejeshwa nchini kwao kwa hiyari.

Mheshimiwa Naibu Spika, idadi hiyo imefanya wakimbizi waliorejeshwa nchini mwao tangu zoezi hilo lilivyoanza mwaka 2017 hadi 2019 kufikia 66,148. Aidha, zoezi la kuwarejesha wakimbizi hao nchini kwao kwa hiari ni endelevu.
MHE. RUKIA K. AHMED aliuliza:-

Mazingira ya kufanya biashara nchini ni magumu na hii ni kwa wafanyabiashara wa ndani na wa nje:-

Je, ni lini Serikali itaondoa urasimu ili wananchi waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA (k.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikibuni na kutekeleza mikakati na mipango mbalimbali kwa kuhakikisha uwepo wa mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini. Kwa mwaka 2017, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa Sekta binafsi ilifanya uchambuzi wa kina wa mazingira ya biashara nchini kwa sekta zote na kubaini changamoto mbalimbali zikiwemo mwingiliano wa sheria. Kufuatia changamoto hizo, Serikali iliandaa Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Mazingira ya Biashara Nchini (Blue Print for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment for Tanzania) ambao umeridhiwa na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango huo utasaidia kuondoa mwingiliano wa sheria na kupunguza urasimu kwa wafanyabiashara wakati wa kupata huduma katika Taasisi mbalimbali za Serikali. Mpango wa Utekelezaji wa Blue Print umekamilika. Sambamba na hilo, Serikali tayari imetekeleza baadhi ya mapendekezo ambayo ni ya kiutawala na yasiyohitaji mabadiliko ya sheria. Mfano, katika Sekta ya Kilimo na Mifugo, jumla ya tozo 114 na tano za OSHA zimeondolewa na mapendekezo ya kuondolewa tozo nyingine kupitia Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019 yameshawasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mafanikio ya jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara ni kwa Tanzania kuendelea kuongoza kwa uwezo wa kuvutia mitaji kutoka nje (Foreign Direct Investment) katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki tangu mwaka 2012.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ripoti ya Uwekezaji ya Dunia (World Investment Report) inayotolewa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) ya mwaka 2018, Tanzania imeongoza katika nchi za Afrika ya Mashariki kwa kuvutia mitaji ya jumla ya Dola za Marekani 1,180 ikifuatiwa na nchi ya Uganda kwa Dola za Marekani 700. Aidha, Serikali itaendelea kuhakikisha maboresho yanayofanyika yanadumishwa na kuendelea kubuni mikakati ya kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara nchini. (Makofi)