Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Rukia Ahmed Kassim (10 total)

MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kuuliza swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa Zanzibar Sheria ya Makosa ya Kimtandao (CyberCrime Act) bado haijapitishwa, je, inapotokea Mzanzibar kamtendea kosa Mzanzibar mwenzie yaani makosa ya mtandao, naweza kumfungulia kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, Sheria ya CyberCrime au Makosa ya Mtandao ni sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria hii inafanya kazi pande zote mbili za Muungano kwa maana ya Zanzibar au Bara. Sheria hii tayari imeshaanza kufanya kazi na tunasimamia maeneo yote ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nimuambie Mheshimiwa Rukia kwamba sheria hii ni ya Muungano na imeshapitishwa kwa taratibu zote.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Mwenyekiti,asante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inahimiza wananchi waweke fedha benki badala ya kuweka majumbani na kwa kuwa katika jibu lako la msingi umesema kwamba malipo ya wateja hawa yatatokana na mauzo ya mali, makusanyo ya madeni na fedha zilizowekezwa katika taasisi nyingine.
Je, itakapotokea fedha za wateja ni nyingi kuliko makusanyo yaliyokuswanywa, Serikali itawasaidiaje wateja hawa ambao wao hawana makosa hasa ukizingatia kwamba benki hii ina matawi katika nchi nyingi tu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Bodi ya Akiba ya Amana wamesema kwamba hata kama mteja ameweka fedha za kigeni atalipwa fedha ya kitanzania tena kwa rate ambayo ilianza ufilisi yaani tarehe 8 Mei, 2017. Je, Serikali haioni kama huu ni uonevu na ipo haja ya kuingilia kati ili dhuluma hii isitendeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema malipo ya wateja yanalipwa kutokana na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39. Kwa hiyo, kinachofanyika ni utekelezaji wa sheria hii na wala Serikali haina mpango wa kumuonea mteja yeyote. Nimesema madeni yatakusanywa na pesa hizo zitakusanywa. Serikali inasimamia hili kwa kiwango kikubwa na ndio maana mpaka leo tayari wameshaanza kulipwa wateja wote hawa zaidi ya wateja 695 wameshalipwa kiasi cha shilingi milioni 727,988,000. Ni Serikali yetu italisimamia hili kwa umakini mkubwa na kila mteja atapata amana yake kama ilivyowekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa walioweka fedha za kigeni, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi tunatekeleza kazi hii kulingana na sheria yetu ya fedha na tutalisimamia hivyo. (Makofi)
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, aliyekuwa Waziri katika Wizara ambayo ilikuwa ikishughulikia mambo ya Muungano, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ambaye sasa hivi ni Makamu wa Rais, aliwahi kutuambia kwamba kuna kikao ambacho kilikaa kati ya pande hizi mbili, Wajumbe kutoka Zanzibar na Wajumbe kutoka Tanzania Bara waliokuwa wakizungumzia kuhusu kero ambazo zinahusu mambo ya Muungano. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kutuambia ni Wajumbe gani hao ambao walikuwa wakikutana kuzungumzia kero hizi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma kumekuwa na taratibu mbalimbali za kushughulikia changamoto za Muungano hatuziiti kero ni changamoto za Muungano. Mwaka 2006 ukaanzishwa utaratibu mpya wa kikao cha Kamati ya Pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Kikao kile cha Kamati ya pamoja kilikuwa kinaongozwa na Makamu wa Rais pamoja na Watendaji Wakuu wa Serikali za pande mbili. Maana ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar au Waziri Kiongozi kabla ya mabadiliko ya Katiba ya 2010.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao kile kinajumuisha Mawaziri wote ni Mabaraza ya Mawaziri ya pande zote mbili za Muungano wetu. Kwa taarifa tu kikao cha mwisho kilikutana tarehe 13 Januari, 2017 kule Zanzibar ambapo kilijumuisha Mawaziri wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mawaziri wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao hicho kinatanguliwa na kikao cha Makatibu Wakuu wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makatibu Wakuu wote wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kabla ya hapo kinatanguliwa na kikao cha wataalam wa masuala husika yatakayozungumzwa katika kikao hicho kwa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kikao hiki na utaratibu huu ni mkubwa, ni mzuri na umetusaidia sana kupunguza changamoto za Muungano. (Makofi)
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa vitendo hivi vinapotokea mara nyingi ushahidi wa awali haupatikani. Je, Serikali imejipanga vipi kutoa taaluma kwa wananchi nini kifanyike mara tu linapotokea jambo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali inachukua hatua za kutosha dhidi ya udhalilishaji huu lakini bado vitendo hivi vinaendelea kwa kasi kubwa katika jamii zetu. Je, Serikali haioni kwamba adhabu inayotolewa ni ndogo hivyo basi ilete sheria hapa Bungeni tuipitishe yeyote atakayepatikana na hatia ya kubaka mtoto mdogo ahasiwe? (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio mengi ya udhalilishaji sasa hivi yanakuwa reported na hii inaonesha kwamba mwamko wa jamii nao umeongezeka. Tumepanua wigo sana kupitia Idara zetu za Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii pamoja na Jeshi la Polisi kwa kuanzisha Madawati ya kuweza kutoa taarifa kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini matukio mengi ya udhalilishaji dhidi ya watoto yamedhihirisha kwamba yanafanywa na watu wa karibu wa familia. Naendelea kutoa rai kwa wanajamii na familia kuyatolea taarifa punde yale matukio yanapotokea na sisi ndani ya Wizara ya Afya pamoja na Jeshi la Polisi tumejipanga vizuri kuyashughulikia kwa uharaka zaidi pindi yanapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi kwa mujibu wa sheria udhalilishaji wa mtoto adhabu yake ni faini isiyozidi shilingi milioni tano na kifungo kisichozidi miezi sita ama vyote kufanyika kwa wakati mmoja. Sambamba na hilo, Serikali itaendelea kutafakari kwa kadri inavyoona inafaa kama kuna umuhimu wa kuongeza adhabu kutokana na matukio kama hayo.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni kubwa, nzuri na ya kisasa ambayo inatumika kuwahudumia wananchi wa Dodoma, wanafunzi wa UDOM pamoja na sisi Wabunge, lakini ina tatizo kubwa sana la Madaktari pamoja na watumishi wengine. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Madaktari ni kidogo sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ambayo ndiyo mamlaka ya kusimamia Hospitali ya Benjamin Mkapa, inatambua kwamba tuna changamoto ya Madaktari Bingwa.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeweka mikakati ya kuainisha mahitaji ya Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na Hospitali zote za Rufaa za Mikoa na tutafanya mgawanyo kwa kuangalia yale maeneo ambayo yana Madaktari wa ziada na kuwapeleka katika Hospitali zote za Rufaa za Mikoa, ikiwa pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, katika mwaka huu wa fedha tumefadhili masomo ya Madaktari Bingwa 125 katika fani ambazo hatuna katika Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Benjamin Mkapa. Pindi Madaktari hao watakapomaliza watakuwa posted katika hospitali hizi.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa kuna ongezeko kubwa la maradhi ya kisukari mpaka kuna baadhi ya watoto wachanga wanazaliwa wakiwa na maradhi haya; je, Serikali inaweza kutuambia nini chanzo kinachosababisha watoto wadogo kuzaliwa wakiwa na kisukari?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika majibu yangu ya msingi nilisema kuna aina tatu za kisukari. Aina ya kwanza ni kisukari ambacho kinawapata watu katika umri mdogo na changamoto ya aina hii ni kwamba mtoto anazaliwa zile cell zake za kongosho ambazo kwa lugha ya kitaalam tunaita pancreas mwili wake wenyewe unaanza kuishambulia ikiona kwamba kile ni kitu ambacho ni kigeni ndani ya mwili. Kwa hiyo, hiyo ni aina moja ya kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya pili ya ni kisukari ambacho kinawapata watu katika umri mkubwa; na hiyo ndiyo hali ambayo ilikuwepo kutokana na jinsi tunavyokula, masuala ya uzito, matumizi ya vilevi na kutofanya mazoezi. Sasa hivi hali imeendelea kubadilika, hata watoto wadogo kwa sababu ya lishe. Mara nyingi ukiona mtoto anakuwa na uzito mkubwa na sisi kama wazazi tunaona kwamba ni faraja. Uzito uliopitiliza wa aina yoyote hauna tija na ni moja ya kitu ambacho kinapelekea sasa hivi watoto wetu kuanza kupata kisukari wakiwa na umri mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aina ya tatu ni kisukari ambacho kinatokana na ujauzito. Mama anapokuwa mjamzito kuna baadhi wanapata kisukari na mara nyingi kinaisha baada ya yule mtoto kuzaliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ombi langu na kwa kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim, ni kwamba ni lazima sisi kama wazazi tuzingatie misingi ya lishe kwa watoto wetu, tusiwalishe chakula kilichopitiliza na watoto wetu wakawa wazito na uzito mkubwa kwa sababu nayo ina mchango mkubwa sana katika kupata kisukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kikundi kidogo ambacho miili yao tangu wamezaliwa zile cells zao za kongosho sinashindwa kufanya vizuri, hazizalishi insulin ama kwa kuwa na deformity ama kwa kuwa haikuumbwa vizuri zaidi au zikawa zimeshambuliwa; hawa wako wachache na wao watakuwa wanahitaji insulin tangu wakiwa na umri mdogo. Kubwa la msingi ni kuzingatia suala la lishe hususan kwa watoto hawa wasiwe na uzito mkubwa.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.Kwa kuwa viwanda vingi vimeshindwa kujiendesha kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa, kama vile kodi kuwa nyingi pamoja na bei ya umeme kuwa ghali hata ukilinganisha na nchi jirani zetu hapa Afrika ya Mashariki. Je, Serikali iko tayari kupunguza hizi kodi pamoja na gharama za umeme ili iwe kivutio kwa wawekezaji wengine kuweza kuja kuwekeza na hivi tulivyonavyo vijiendeshe kwa faida ili vijana wetu waweze kupata ajira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili, kwa kuwa viwanda vingi ambavyo Serikali ina lengo la kuvifufua miundombinu yake ni ya kizamani. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvifufua viwanda hivi ili viende na hali tuliyonayo na vijiendeshe kwa faida na vijana wetu waweze kupata ajira.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza la kuhusu gharama za uendeshaji na mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini, nimwondoe tu hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba hata wakati wa usomaji wa bajeti wa Wizara, Mheshimiwa Waziri alieleza mipango na mikakati ya Kiserikali ya kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ya kuweza kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kufanya biashara nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya jambo kubwa ambalo linaendelea hivi sasa ni matayarisho ya mpango ambao unaitwa Blue Print to Emprove Business Environment in Tanzania ambao lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira wezeshi ya kuwafanya Wawekezaji wote wavutike na kuja kuweka katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika swali lake la pili alitaka kufahamu kuhusu ufufuaji wa viwanda kutokana na miundombinu chakavu. Wizara inaendelea na mchakato huo na kama ambavyo imekuwa ikitolewa taarifa mara kwa mara, tumepitia katika maeneo mengi ya viwanda ambavyo vilishabinafsishwa na maelekezo yalitoka ili vifufuliwe, viweze kuajiri vijana wengi zaidi, kwa sababu lengo hapa kubwa ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2025 kundi kubwa zaidi ya asilimia 40 lipate ajira kupitia viwanda.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Spika, ahsante, nami kunipa nafasi ya kuweza kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha swali la nyongeza, nilitaka kujua kwa sababu Mbunge ana haki ya kuleta gari yake kwa kupitia exemption kama Mbunge, ana haki ya kuileta Tanzania Bara au Tanzania Visiwani. Ni kwani basi anapoleta gari yake Tanzania Visiwani, akiileta Bara hawezi kupewa namba ya hapa mpaka anaambiwa ailipie difference? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimeshaeleza changamoto ya Kimfumo tuliyonayo, unapopewa namba ya Tanzania Bara, maana yake gari ile inasajiliwa kutumika Tanzania Bara, kwa hiyo, kama inasajiliwa kutumika Tanzania Bara na utofauti wa Kimfumo nilioueleza ni lazima tuweze kuthaminisha gari yako sasa inasajiliwa Tanzania Bara tukupe namba ya Tanzania Bara na uweze kulipia utofauti ule wa Kodi uliopo kwa sababu ya mfumo wetu wa utofauti kati ya Mamlaka mbili hizi ili gari lako liweze kutumika Tanzania Bara.
MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakimbizi kutoka Somalia pamoja na wakimbizi kutoka Ethiopia, hawawezi kuingia nchini mpaka wapitie nchi ya Kenya. Je, Serikali haioni kwamba ipo haja kwa kushirikiana na nchi ya Kenya kuwazuia wakimbizi hawa wasiingie katika nchi yetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa ukiacha wakimbizi walioko katika magereza, kuna wakimbizi ambao wako katika kambi za wakimbizi. Kwa mfano, Kadutu - Kigoma, Ulyankulu - Tabora pamoja na kambi nyingine. Wakimbizi hawa wana tabia ya kuzaana sana na kwa kweli idadi yake inaongezeka ukizingatia miaka 10 iliyopita sasa hivi wako mara mbili zaidi.

Je, Serikali, kwa kuwa nchi zao tayari zina amani, wana mkakati gani wa kuwarejesha wakimbizi hawa ili wasiendelee kuzaana hapa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na rai yake ya kwanza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba rai yake ambayo ameitoa tumeshaanza kuifanyia kazi. Hivi karibuni tulikuwa tuna kikao kilichoshirikisha ngazi ya Mawaziri wa Tanzania, Kenya na Ethiopia, ili kujadiliana namna ya pamoja ya kudhibiti wimbi la wahamiaji hawa hususan wanaotokea Ethiopia ambao wanaingia kwa wingi kupitia Kenya na jambo hilo limeleta mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu suala la wakimbizi kurudi makwao, kama ambavyo nimejibu swali langu la msingi kwamba kwa takwimu za mpaka Aprili, 2019 tuna zaidi ya wakimbizi 99,000 ambao wameamua kurudi kwa hiari. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba nalo hili ni jambo ambalo tumeshaanza kulifanyia kazi na tunaendelea nalo. Kwa sababu ni kweli kama alivyozungumza Mbunge kwamba hali ya amani katika nchi hizi imetulia, hakuna sababu ya wakimbizi hawa kuendelea kubaki katika nchi yetu kwa kipindi hiki.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa tatizo kubwa tulilonalo katika nchi yetu kwenye mazingira ya biashara ni mfumo wa kodi kuwa kuwa hauko wazi: Je, ni lini sasa Serikali itaandaa mfumo wa kodi ambao utakuwa wazi katika mazingira haya ya ufanyaji biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa sababu nchi yetu katika uwezeshaji ufanyaji wa biashara imeambiwa ni nchi ya 144, Rwanda ambayo ni nchi ndogo ni ya 29, Kenya ni nchi ya 40: Je, Serikali haioni kwamba tutapoteza wawekezaji katika halali hii ili tuweze kujirekebisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA): Mheshimiwa
Naibu Spika, kuhusiana na mazingira yetu ya kodi kuwa wazi, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikipitia mazingira ya kodi kila wakati na ndiyo maana hata kwenye kila Bunge, mara nyingi tumekuwa tukipata mapitio ya kodi mbalimbali ili kuendelea kuboresha mazingira yetu ya kodi yaweze kuwa ya kishindani na yaweze kurahisisha biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na changamoto ambazo bado zipo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali la pili la namna gani tunaweza tukaboresha mazingira yetu ya uwekezaji, kama nilivyosema kwenye jibu letu la msingi, Serikali imeshachukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kukaa na wafanyabiashara kujadiliana nao mazingira au changamoto wanazozipata. Ndiyo maana tumekuja na Blue Print kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kibiashara. Tutaendelea kufanya reforms; na ndiyo maana hata juzi Mheshimiwa Rais aliwaita wafanyabiashara akakaa nao mkutano wa masaa mengi akisikiliza kero zao. Lengo ni kupata changamoto na mawazo yao ili kuboresha mazingira ya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili litaendelea na baada ya muda siyo mrefu, mazingira yetu yataboreka, yatakuwa mazuri na itaendelea kuvutia wawekezaji kutoka nje.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nami naomba kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda katika swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Rukia Kassim kuhusiana na wepesi wa kufanya biashara. Kwanza kabisa nimhakikishie kwamba tutakapoenda katika mwaka ujao kwa nafasi ya Tanzania tutakuwa tumefanya vizuri zaidi. Changamoto ambayo tunayo ukizingatia na maboresho ambayo sasa hivi Serikali imeyafanya, huwa katika upimaji wa nafasi ya nchi katika wepesi wa kufanya biashara, kipimo chao deadline ni mwezi wa Tano wa kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa sasa Juni - Julai mambo mengi yamefanywa na Serikali. Juzi tu nilikuwa na mkutano pamoja na Benki ya Dunia Washington na Dar es Salaam, kuhakikisha kwamba tunawasilisha vielelezo vya kuonyesha ni namna gani kama nchi tumefanya maboresho mbalimbali na tumepiga hatua katika kuboresho viashiria vile 11 ambavyo vinatumika katika kupima wepesi wa kufanya biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba, tumepata muda wa kuongezewa mpaka Ijumaa ijayo kuweza kuwasilisha vielelezo vingine vya namna gani tumeweza kufanya makubwa na marekebisho katika mifumo yetu ya kufanya biashara, ikiwemo kuanzisha biashara, ufungaji wa biashara, taratibu za biashara mipakani pamoja na nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kwamba tumepata muda wa kuongezewa mpaka Ijumaa ijayo kuweza kuwasilisha vielelezo vingine vya namna gani tumeweza kufanya maboresho makubwa na marekebisho katika mifumo yetu ya kufanya biashara ikiwemo kuanzisha biashara, ikiwemo ufungaji wa biashara, ikiwemo taratibu za biashara mipakani pamoja na nyingine. Kwa hiyo, niwatoe hofu Watanzania niwatoe hofu Wabunge kila mmoja atimize nafasi yake tujitahidi kuona ni kwa namna gani tunaboresha huduma hizi na ninaamini itakapofika mwaka 2020/2021 ripoti yetu na nafasi ya Tanzania tutaweza kufanya vizuri zaidi.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili tumepata pia utaratibu tutawaita wataalam wa Benki ya Dunia Makao Makuu pia waweze kuja ili kuweze kutoa mafunzo na kutoa maelekezo kwa wale viungo au focal point wa mazingira ya biashara ya kila Wizara na kila Taasisi maana yake tunao watu hawa, ili waweze kuona ni kwa namna gani watapaswa kufanya maboresho zaidi. Tunaamini tulishafanya kitu kama hiki mwaka 2016 na ilitusaidia sana kama nchi tuliweza kuvuka na kuimarika nafasi takribani saba. Kwa hiyo, tunaamini kati ya mwaka huu mpaka mwaka 2021 tutaweza kufanya vizuri zaidi, muhimu kila mmoja atimize wajibu yake. (Makofi)