Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zainab Mndolwa Amir (12 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa afya njema ili na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Pili napenda kukushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia na tatu, napenda kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake pamoja na Naibu wake na pongezi nyingi ziende kwa Kamati ambayo imetoa maoni, naomba Serikali izingatie maoni hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuja na mpango wa elimu bure, lakini haikuwa na maandalizi ya kutosha. Wazazi na Taifa likahamasika kupeleka wanafunzi mashuleni, lakini katika shule zile madarasa na madawati ni machache. Serikali ikajitahidi kufanya harambee kwa taasisi mbalimbali pamoja na wadau kuleta madawati, lakini ilikuwa haifikirii kwamba yale madawati yanaenda kuwekwa wapi. Matokeo yake wanafunzi wakawa wengi kuliko madarasa yaliyopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta darasa moja kuna wanafunzi 100 mpaka 120 na natolea mfano hivi karibuni nilienda katika shule ya msingi Ungindoni iliyopo Kata ya Mjimwema, Wilaya ya Kigamboni, wanafunzi wanakaa zaidi ya 120 kiasi kwamba mwalimu anashindwa kumsaidia yule ambaye ni slow learner ili aweze kufaulu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatakiwa ijipange, isilaumu walimu kwamba hawafundishi ndiyo maana watoto wanafeli. Kuwaadhibu walimu kwa kufeli kwa watoto wetu kwa kweli wanawaonea. Kama Serikali ingekuwa ina-provide incentives zote kwa walimu, mishahara mizuri, mazingira mazuri ya kufundishia, nyumba bora na mishahara ya walimu inatakiwa iongezwe kwa kiwango cha juu ili walimu waweze kuvutiwa na fani hii. Tunaona tuna ukosefu mkubwa wa walimu kutokana na wengi hawapendi kujifunza fani hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke sote sisi tumepita kwa walimu, madaktari wamepita kwa walimu, wanasheria wamepita kwa walimu lakini walimu wamefanywa kuwa madaraja kwa taaluma nyingine, hatuwajali. Mheshimiwa Ndalichako mama yangu nakuomba sana, wewe umepitia kwa walimu mpaka umekuwa Profesa, wasaidie walimu hawa katika kuboresha maslahi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madai yao sasa hivi imekuwa kama ni wimbo wa Taifa maana yanaandikwa kwenye vitabu hayatekelezwi. Mimi naona sasa imekuwa mgomo baridi kwa wao kutojituma ili kuleta ufaulu wa hali ya juu. Shule za private zinafaulisha kwa sababu utakuta mwalimu anatoka Serikalini anakwenda kufundisha private kwa sababu ya incentive anazopata, mshahara na mazingira mazuri, kwa nini Serikali haioni haja basi na sisi kuboresha mazingira ya walimu wetu katika shule hizi za Serikali? Kwa nini sisi ambao tumepitia kwa walimu tunadharau walimu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana, nakuomba mama yangu umepitia kwa mwalimu mpaka umefikia hatua hii na angalia yule mwalimu uliyemuacha kule kijijini ulikosoma hali yake ilivyo. Nakuomba tuwaboreshee maslahi yao ili walimu hawa waweze kufanya kazi zao sawasawa ili kusaidia wanafunzi wetu kuweza kufaulu kwa kiwango cha juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitembelea shule ya msingi Yombo Dovya iliyopo Kata ya Makangarawe, Wilaya ya Temeke, shule ile kwa kweli ni mtihani. Ina wanafunzi walemavu na wa kawaida, madarasa hayatoshi. Nimejitolea pale tani moja ya mifuko ya saruji na mabati 20 lakini pia hayakidhi mahitaji. Vyoo ni vichache, walimu wanangojea wanafunzi wakajiasaidie na wao waingie katika vyoo vilevile, ofisi za walimu hawana meza za kutosha, wanatumia madawati kama meza zao, huwezi kujua kama hili ni darasa au ni ofisi ya walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwajali walimu wetu, hii ndio source ya kushuka kwa elimu yetu. Tusiwaadhibu walimu wala shule zile kuzifungia, sisi Serikali ndio wenye matatizo. Serikali inatakiwa ku-provide kila kitu ili walimu waweze kufanya kazi kwa bidii na kujituma.
Nadhani tukifanya kila kitu wanafunzi wetu watafaulu kwa kiwango cha juu na hatuwezi kumtafuta mchawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwafukuza walimu kwamba hawajafaulisha tunawaonea. Kuwasimamisha au kufungia shule kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe mimi siafiki, kwa sababu mwalimu hawezi kujenga darasa wala maabara, kwa nini unamuadhibu kwamba kasababisha wanafunzi wafeli. Inayotakiwa iadhibiwe ni Serikali ambayo haijaweka mazingira rafiki ya kufundishia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana pindi tutakapopitisha bajeti yako Mheshimiwa Waziri uwajali sana walimu ndio kila kitu, bila walimu sisi tusingefika hapa, bila walimu wewe Mheshimiwa Waziri usingekuwa Profesa.

Kwa hiyo, haya ya kujenga maabara, ukanunue vitabu bila kumwezesha mwalimu huwezi kumlazimisha ng’ombe kunywa maji kama hataki kunywa maji. Utamwekea mazingira, lakini kama mshahara yake hujamboreshea, hujamwekea nyumba bora zenye umeme, anafanya andalio la somo na azimio la kazi kwenye giza hawezi kufanya kazi vizuri. Ndiyo maana wengi hawataki kukaa vijijini wanakimbilia mjini angalau kufanya biashara huku wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa tueleze una msimamo gani kwa walimu wetu wa Tanzania kuwaboreshea maslahi yao ambayo yataleta ufaulu wa juu kwa shule zetu. Kwa sababu ukisema uwafukuze walimu unawaonea, ufungie shule zile pia unazionea kwa sababu hawana uwezo. Hata wewe mshahara wako huwezi ukasema ukajenge maabara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ishauri Serikali na Rais walimu ndiyo kila kitu katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa afya njema ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi yake nzuri anayoifanya pamoja na Naibu Mawaziri wake na wafanyakazi wa Wizara wote kwa ujumla. Nampongeza kwa sababu tunaona msongamano Mkoani Dar-es-Salaam umepungua kwa kupata mwendokasi na sasa hivi katika bajeti hii nimeona barabara mbalimbali zimetengewa bajeti ya matengenezo ili kuepuka msongamano huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuna changamoto nyingi zinajitokeza. Bajeti hii imepangwa na kwenye vitabu inaridhisha na inaonekana ni nzuri sana, Dar- es-Salaam ni uso wa nchi yetu kwa sababu watu mbalimbali wanavyotoka nchi za nje hufikia Dar-es-Salaam na baadaye ndio wanakuja mikoani, kwa hiyo, naomba bajeti iliyotengwa ifike kwa wakati. Vilevile tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri atutafutie wakandarasi ambao wana kiwango cha hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona barabara yetu ya Kilwa ilitengenezwa chini ya kiwango baada ya muda mfupi imeharibika na hapa tumeona pia itatengenezwa kwa mwendokasi. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri mkandarasi atakayempata aiboreshe ile Barabara ya Kilwa iwe yenye ubora kwa sababu ilitengenezwa mara ya mwanzo lakini haikuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia kuhusu Kivuko cha Magogoni. Ni muda mrefu sana wananchi wa Dar es Salaam, hususan waishio Kigamboni walikuwa na tatizo la kivuko na msongamano wa magari lakini tunashukuru Serikali ikatujengea Daraja la Nyerere. Napenda kueleza Bunge lako Tukufu, wananchi wa Kigamboni bado wana changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uvuke katika daraja lile kwa gari ndogo tu ni shilingi 2,000 ukizingatia wananchi wake wengi shughuli zao zote ziko ng’ambo ya bahari, lazima wavuke asubuhi wawapeleke watoto shule, ofisi nyingi ziko ng’ambo ya bahari, hospitali pia, changamoto ni nyingi na kwamba ni ghali mno kuvuka katika daraja lile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa gari ndogo ni Sh.2,000, mtu akivuka tu kwenda na kurudi Sh.4,000. Wakati mwingine watu pia wanakuwa na wagonjwa hospitalini wanaenda mara tatu kwa siku, gharama ya kivuko ni kubwa mno Mheshimiwa Waziri. Namwomba pamoja na Wizara ya TAMISEMI, ingawa nilishauliza swali hili kwamba NSSF nao walijenga lakini ninachokiona kwa Daraja la Kigamboni, wananchi wa Kigamboni wamepewa mzigo mkubwa sana. Hawana faraja na lile daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijua kwamba wananchi wa Kigamboni wamepata faraja kwa uwepo wa daraja lile angalau watavuka labda kwa bei nafuu, lakini kwa bei ya Sh.2,000 kwa gari ndogo na gari kubwa mpaka Sh.7,000 mpaka Sh.15,000 ni ghali mno. Naiomba Wizara hii kwa kushirikiana na TAMISEMI waliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi imefikia wakati wananchi wa Kigamboni ambao wanatumia vyombo vya moto, magari yao hawavuki nayo. Ukienda katika Kata ya Kigamboni utakuta watu wengi wameweka parking za magari, anaweka gari lake anavuka kwa panton kwa shilingi 200, anaenda kufanya shughuli zake mjini kisha anarudi analipa shilingi 1,000. Kwa hiyo, anakwepa kuvuka kwenye daraja kwa sababu ni ghali mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba wafanye utaratibu kabisa, Mheshimiwa Dkt. Ndugulile analifahamu hili, wananchi wa Kigamboni wanafurahia daraja, lakini daraja lile halina neema kwao. Wanasema maisha bora kwa watu wa Kigamboni kwenye daraja lile hayapo ni ghali mno. Kwa sababu, hata kama ni mshahara Sh. 4,000 mtu anavuka kila siku kwenda na kurudi, mwisho wa mwezi aki-calculate ina maana unaishia kwenye usafiri. Nadhani katika madaraja yote Tanzania ni Daraja la Kigamboni tu ambalo watu hutozwa nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea kwamba watu wa Kigamboni watapata neema kwa sababu madaraja ni huduma kama huduma nyingine. Kama ni masuala ya kukusanya kodi basi lile daraja lingejengwa Ruvu au Wami kwa sababu ni magari mengi sana yanapita maeneo hayo na Serikali ingekusanya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiomba Mheshimiwa Waziri, naona ananitazama lakini naomba aandike haya ninayozungumza na ayazingatie akishirikiana na TAMISEMI, wawaonee huruma wananchi wanaoishi Kigamboni kwa sababu daraja lile halina manufaa kwao, ni ghali mno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wapunguze na ikiwezekana wavuke hata kwa kutumia smart card, hata kama wakiambiwa shilingi 10,000 kwa mwezi au shilingi 20,000 hata mtu akivuka mara tano mara kumi lakini ana kadi maalum ili kupunguza gharama ile. Wakati mwingine wanashindwa kabisa magari yao huacha ng’ambo na kwenda kwa kutumia panton. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia kuhusu barabara zetu. Tumeona Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa na imeona jambo la muhimu barabara ya Dar es Salaam – Morogoro na sisi ni mashahidi tunapita kila siku katika barabara zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja niliuliza hapa kwamba ni lini Serikali itafanya mkakati wa kukarabati barabara zetu na mojawapo ni eneo korofi sana la Chalinze hadi Mlandizi. Nikajibiwa kwamba eneo lile ni korofi kwa sababu inapita mizigo mizito lakini mimi ninachosema siyo mizigo mizito tu pia kiwango cha barabara ni cha hali ya chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mkandarasi aliyejenga maeneo yale hakuzingatia eneo lenyewe husika labda lina maji ya aina gani ili atumie material husika. Kwa sababu kama ni mzigo mzito umetokea Kurasini bandarini, ukapita barabarani ukafika mpaka Mlandizi pale barabara angalau ni nzuri, lakini kutoka Mlandizi mpaka Chalinze ile barabara ni mbovu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo suala la mzigo mzito kwa sababu mzigo ni uleule uliotoka bandarini na ndiyo uleule uliopita katika eneo lile na ndio uliofika Chalinze na kwenda Chalinze ukaenda Morogoro au Tanga na barabara kule ni nzuri. Kwa hiyo, hapa tatizo ni wakandarasi wetu, wanajenga barabara chini ya viwango. Namwomba Mheshimiwa Waziri pindi atakapoanza kutengeneza hizi barabara atafute wakandarasi wenye viwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuwawekee masharti hawa wakandarasi, ikiwa watajenga barabara chini ya kiwango na ikifikia muda fulani na tumewalipa pesa, kwa pesa zao wenyewe waweze kugharamia barabara zile kwa maana kwamba wazitengeneze kwa fedha zao kwa sababu wanapewa fedha lakini barabara ziko chini ya kiwango na kuipa Serikali hasara kila mara kwenda kukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona katika taarifa hii kwamba barabara ya Chalinze mpaka Mlandizi kuna kilometa kama 12 zimeshaanza kukarabatiwa toka Machi lakini mimi napita mara kwa mara, ukarabati unaofanyika pale ni kuziba viraka. Kuziba viraka siyo kwamba ndiyo unatengeneza barabara, barabara ile ina mabonde kama matuta ya viazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ile barabara ijengwe kwa kiwango hata kama ni cha zege ili kuhimili mizigo mizito inayopita. Kwa sababu wanakarabati kwa kuweka viraka kusema ukweli bado tutapiga mark time, bado hatujatengeneza barabara zetu. Naiomba Serikali, kama mnavyosema Serikali hii ni sikivu, iwe sikivu kweli, haya yaliyoandikwa yatekelezwe kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara nyingi zina matatizo pia. Kuna barabara ya kutoka Magole - Gairo ni mbovu. Mnaona maeneo ya Magubike tukipita barabara ni mbovu, naomba Serikali yetu pia itengeneze barabara hizo. Barabara nyingine ziko kwenye kingo za milima angalau Serikali wakati wanajenga zile barabara kuu zile waweke pavements ili wakati wa mvua kubwa mmomonyoko usiathiri barabara zetu na kuleta matatizo.

Kwa hiyo, haya aliyoyaandika Mheshimiwa Waziri katika kitabu hiki ni mazuri lakini changamoto zinakuja utekelezaji upo? Serikali itoe fedha kwa wakati na wakandarasi wanaoomba nawaomba wazingatie ubora na viwango vyao ili waweze kutengeneza barabara zetu ziwe za viwango na siyo kutengeneza barabara ili mradi barabara tu na kuipa Serikali hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri haya yote yaliyoandikwa yawe yanatekelezeka maana nimeona Waheshimiwa Wabunge wenzangu wengi hapa wamechangia wakisema kwamba mambo mengi yalikuwepo bajeti zilizopita lakini mpaka leo ni ahadi tu kwenye vitabu lakini utekelezaji wake ni wa chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa, kama ni Serikali sikivu aishauri iweze kukarabati na kujenga barabara zetu kwenye kiwango kinachohitajika ili kuepuka ukarabati wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Mbarawa, kama ni Serikali sikivu naomba aishauri iweze kukarabati na kujenga barabara zetu kwenye kiwango kinachohitajika ili kuepuka ukarabati wa mara kwa mara. Ukarabati huu wa mara kwa mara huipa Serikali hasara pia na badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma. Badala ya kujenga barabara nyingine, tunarudi kujenga barabara ambazo zilishajengwa na zimejengwa chini ya kiwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nashukuru sana kwa mchango huu namwomba Mheshimiwa Waziri yatekelezwe kwa wakati na Serikali itoe fedha kwa wakati kama ilivyoahidi na kama ilivyoandika ili barabara zetu ziwe za kiwango.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kuchangia katika ofisi ya TAMISEMI na ofisi ya Utumishi na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kazi nzuri inayoifanya. Naipongeza kwa juhudi kubwa anazozifanya Mheshimiwa Jafo katika Wizara yake, hususani katika kazi zake zinazoonekana dhahiri katika kujenga vituo vya afya pia katika kujenga zahanati, na pia namshukuru sana kwa kupandisha Hospitali yetu ya Temeke kuwa Hospitali ya Rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokiomba na kushauri Serikali; Hospitali ya Wilaya ya Temeke imepandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa lakini hospitali ile inachukua wagonjwa kutoka Wilaya za karibu hususani Mkuranga na Wilaya ya Kigamboni.

Nakuomba Mheshimiwa Waziri, najua kuna utaratibu unafanya kuboresha zahanati zilizokuwa Mkuranga pamoja na Kigamboni; naomba wakati unafanya utaratibu huo uitupie macho Hospitali ya Temeke. Hospitali hii wodi zake zile kweli ni chakavu na ni za siku nyingi. Nakuomba sana uipe kipaumbele, uiboreshe, kwa sababu wananchi wa Mkuranga wakipata transfer ni lazima waende Tumbi na Tumbi ni mbali sana kutokana na jiografia yake kwa hiyo wanachotakiwa ni kuwaleta Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Jafo unaandaa mazingira nakuomba sana Hospitali yetu ya Wilaya ya Temeke ambayo sasa hivi ndio itakuwa ni hospitali ya rufaa iboreshwe, majengo yake yawe ya hadhi ya rufaa. Kwa sababu eneo ni dogo nashauri Wizara angalau zile wodi namba moja, namba mbili , namba tatu majengo yake yawe ya ghorofa ili iweze kukidhi idadi ya wagonjwa. Pia si majengo tu kuna vifaa muhimu pia vinatakiwa hospitali vifaa kama x- ray mmejitahidi, lakini vifaa vingine ni vile vidogo vidogo lakini tunaona si vya muhimu. Katika wodi za wagonjwa lazima kuwe na vikabati vya kuhifadhia chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa ukifika Hospitali ya Temeke sasa hivi kuna matatizo, unapompelekea mgonjwa wako chakula unaweka chini chakula hakuna vikabati vya kutosha kwa hiyo naomba sana katika kuboresha hizo hospitali na vifaa vingine ambavyo mnaviona ni vidogo vinahudumia wananchi, vinahudumia wagonjwa wote ni muhimu sana katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Ni ukweli usiopongika kwamba Hospitali ya Muhimbili inachukua wagonjwa wengi kutoka mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani. Serikali imejitahidi katika kujenga vyumba vya upasuaji na kuongeza wodi, lakini kuna changamoto moja inayoikabili hospitali ya muhimbili naona watu wengi hawaioni, lakini sisi wakazi wa mjini Dar es Salaam tunaiona. Si wagonjwa wote wanaoletwa katika Hospitali ya Muhimbili wana wenyeji katika Mkoa wa Dar es Salaam. Wanapopewa rufaa wakifika pale emergence na kukabidhi wagonjwa wao huwa wanaambiwa kwamba mgonjwa wako ameshapatiwa kitanda, kwa hiyo yeye aondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine hawana ndugu wala jamaa Dar es Salaam. Tunaiomba Wizara angalau itenge jengo maalum ambalo litasaidia wale wasindikizaji ambao wanakuja kuleta wagonjwa wao waweze kupata eneo la kijisitiri na kusubiri matokeo ya wagonjwa wao kama ni vipimo na kuwahudumia. Kuna huduma nyingine haziwezi kufanywa na daktari, haziwezi kufanywa na nesi. Nurse hawezi akamlisha mgonjwa, kufua nguo za mgonjwa na labda mgonjwa akiwa amejisaidia, ni mtu wa karibu mno anatakiwa azifanye zile huduma.

Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Jafo, Hospitali ya Muhimbli ipatiwe eneo maalum ambalo litakalokuwa na wahudumu watakaoweza kukaa na kuwaona wagonjwa wao jinsi wananvyoendelea na vipimo na kuweza kuwasaidia katika mambo mbalimbali. Kama ikiwezekana wawe na hata identy card ya kuonesha kwamba huyu mgonjwa wake yuko Sewa Haji au yuko Kibasila. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili iweze kusaidia hata wale walinzi wetu wawapo katika maeneo ya ulinzi naomba sana hospitali zetu; nitolee mfano Hospitali ya Mwananyamala; naitolea mfano; ukipeleka mgonjwa hospitali ya Mwananyamala na Mwenyezi Mungu akamtanguliza mbele ya haki akitoka wodini, anapopelekwa chumba cha maiti ili kumtoa kila siku ni 20,000. Akikaa siku 10 ni shilingi 200,000, akifia nyumbani na kuletwa ndani kwenye mortuary ya hospitali unakuta anakuwa-charged shilingi 30,000. Sisemi utofauti wa malipo ninachosema yule ni Mtanzania halisi ambaye wakati wa uhai wake alikuwa analipa kodi na kodi hiyo ilikuwa inalipwa na Serikali inakusanya, iweje Mtanzania huyu amekufa na ametibiwa na ndugu zake kwa gharama nyingi sana maiti mnaitoza malipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaombeni kama inawekana, kwa ushauri wangu nawaomba mtoe yale malipo ya maiti. Nadhani pale mimi ninatolea mfano tu, kuna hospitali nyingi naona Waheshimiwa Wabunge sidhani kama mmefanya uchunguzi, ukiweka maiti yako hospitali si kama unaweka kwa sababu hutaki kumzika, huenda unasubiri ndugu na jamaa; kwa kweli gharama ni kubwa sana. Huyu maiti wa Tanzania ni Mtanzania alikuwa analipa kodi.

Naomba sana Mheshimiwa Jafo uliangalie kwa makini katika bajeti yako, muondoe haya malipo ya kumtoa maiti wetu katika hospitali hizi za Serikali, iwe huduma kama huduma nyingine. Kwa sababu inaonekana kama tumekosa sehemu nyingine ya kukusanya mapato, tutafute eneo lingine Serikali si kwenye maiti, tuwaonee huruma wafiwa na tumuonee huruma pia marehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia pia Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Hospitali ya Mkoa wa Morogoro chumba chake cha kuhifadhia maiti kipo nje ya uzio wa hospitali na kiko karibuni sana na shule ya sekondari ya Morogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilisoma pale miaka ya 1980, ni kero sana ile mortuary, iko karibu na madarasa kiasi kwamba ndugu waliofiwa na ndugu yao wakati wanakuja kuchukua marehemu wao wanahisia mbalimbali wengine hulia, wengine huja pale labda kuaga kwa mapambio na mwalimu anapofundisha darasani hakuna usikivu. (Makofi)

Naombeni Mheshimiwa Jafo wakati unapanga bajeti yako uliangalie kwa jicho la huruma wanafunzi wa Morogoro Sekondari wanapata tabu kwa kuwepo chumba cha maiti karibu na madarasa. Naomba ulifanyie kazi kwa sababu hili ni tatizo kubwa ingawa Mheshimiwa Abdul-Azizi ataniunga mokono ni Mbunge wa Morogoro na anaona tatizo hili, yeye alisoma Forest, mimi nimesoma Morogoro miaka ya 1980 lakini tatizo ni kubwa sana. Hata wakati mnafanya mtihani mwalimu unakuta anaweka stop watch kwa sababu wangoje zile kelele zipungue, nawaombeni muhamishe ile mortuary ilipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napenda kuchangia kwenye utawala bora, muda hautoshi mambo ni mengi. Kuna baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanawaweka ndani kwa masaa 24 wananchi wetu bila sababu na wakati mwingine sababu zenyewe hazijulikani, anakuambia wewe kaa ndani. Sasa nataka Serikali inijulishe, je, kama kuna sheria hii ni makosa gani ambayo Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya anatakiwa amuweke mtu ndani kwa masaa 24?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikibainikwa kwamba amemuweka kimakosa, je, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya atachukuliwa hatua gani? Maana sasa hivi hatuelewi, hata sheria kila mtu anachukua mamlaka mikononi. (Makofi)

Nakuomba Mheshimiwa George Mkuchika unijibu swali hili, ni sheria gani inawaruhusu wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwaweka ndani wananchi na baadae anawatoa? Je, ikibainika kwamba hana kosa lolote je, Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya atachukuliwa hatua gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ndugu tuliwarudisha juzi wa darasa la saba, wengine wamefariki, je, Serikali ina mpango gani kwa wale ndugu ambao jamaa zao wamefariki; na hapa juzi tumetangaza kwamba waterejeshwa, je, stahiki zao zitakuwaje? (Makofi)

Kwa hiyo, naomba wakati wa kutoa maelezo tufahamishwe, kwamba stahiki za wela ambao wamepoteza maisha wengine kwa presha tu baada ya kusimamishwa, je, stahiki zao zitapatika vipi? Kwa sababu wameondoka mbele haki wameacha familia na juzi tumesema kwamba warudi makazini na hawapo duniani? Tunaomba Serikali itupe majibu kwa wale ambao wametangulia mbele ya haki na sheria imesema warudi kazini, walipwe mishahara yao tangu pale waliposimamishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mengi ya kuyazungumza lakini naomba sana walimu wengi wana matatizo, wengi wamezungumza, na sisi wote tumepita kwa walimu lakini sekta hii hatuipi uzito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na kuongeza mishahara nashauri walimu wawe wa kwanza, utaona, kwamba utakapowaongezea mishahara walimu wengi, hata kama mtu kapata division one atakuwa interest ya kusoma ualimu. Kama walimu wangekuwa wanalipwa mishahara kama tunayolipwa sisi, wengi na mimi pia ni mwalimu nisingekuwa hapa, lakini kutokana na ualimu kuonekana kama ni kazi dhalili watu wengine wanaacha ile kazi wanaondoka. Kwa hiyo, naomba sana tuwaboreshee walimu mishahara yao stahiki zao ili waweze kufanya kazi kwa weledi. Watakapofanya ya kazi kwa weledi wanafunzi wetu watafaulu vizuri kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru sana, naomba haya yasiishie kwenye vitabu hivi tu, mmeandika mambo mazuri lakini yasiiishie kwenye maandishi. Hii bajeti iliyopagwa itolewe kwa wakati ili muweze kufanya kazi zenu barabara, ahsanteni sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Philip Isdor Mpango (Mbunge) kwa kuwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu na maoni yangu katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/2019utakuwa katika sehemu tatu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iweke kipaumbele katika viwanda hususani kujenga, kufufua viwanda vyetu mfano, katika Mkoa wa Morogoro kuna viwanda kama vile Canvas, Polyster, Ceramic, Magunia, Tannaries (Kiwanda cha Ngozi), Moro Shoe, Moproco. Vyote hivi vipo katika Manispaa ya Morogoro, viwanda hivi vingine vinafanyakazi na vingine wawekezaji hawaviendelezi. Hivyo Serikali isimamie na kuwapa muda wawekezaji hao kuviendeleza na wakishindwa virudishwe kwa Serikali ili wapewe wawekezaji wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vikifanyakazi kama miaka ya 1980 na 1990 vitaleta ajira kwa Watanzania pia kuongeza Pato la Taifa la Tanzania, kulipa kodi ya bidhaa zinazozalishwa kutokana na ujenzi wa reli itakayojengwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro (treni ya mwendokasi itaongeza chachu ya ajira ya wananchi wa Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani na Morogoro ambao watapata ajira katika viwanda hivyo vilivyopo Mkoa wa Morogoro).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kodi, niipongeze Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kukusanya kodi kwa wafanyakazi hususani katika Miji Mikuu mfano Dar es Salaam. Nashauri katika kipaumbele kimojawapo Serikali iandae utaratibu maalum ambao utamwezesha mfanyabiashara alipe kodi kwa wakati na afurahie kuchangia Pato la Taifa na siyo Serikali iwe adui kwa mlipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iboreshe mazingira ya mwananchi wakati wa kuanza biashara. Kuna tatizo katika utaratibu uliopo, nashauri katika Mpango wa Maendeleo 2018/2019 Serikali impe muda angalau miezi mitatu (grace period) mwananchi anayeanzisha biashara na baada ya hapo ifanye makadirio kwa malipo ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa mfanyabiashara anakadiriwa malipo ya kulipa kwa mwaka kabla ya kuanza biashara na sehemu kama vile Kariakoo makadiro ni makubwa mno ambayo si chini ya milioni mbili kwa mwaka, na hii hupelekea wafanyabiashara kushindwa kulipa kodi na
hatimaye kufunga biashara. Hivyo maoni yangu Serikali ipitie tena utaratibu huu kupunguza makadirio ili mwananchi aweze kumudu kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri faini wanazotozwa wafanyabiashara ambao wanakutwa na makosa, mfano ya kutotoa risiti za EFD ni kubwa mno shilingi milioni tatu kulinganisha na bidhaa aliyouza na hii hupelekea mwananchi kushindwa kulipa faini na hatimaye kufunga biashara zao. Pia nashauri wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama wamachinga hususani waliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam (Kariakoo) Serikali iwasajili ili waweze kuwa na mchango kwa Pato la Taifa kwa kulipa kodi na kwenda sambamba na kauli mbiu ya Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli ya ukiuza toa risiti na ukinunua dai risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya Serikali imefanya jitihada kubwa katika kutatua matatizo mbalimbali yakiwemo kutoa madawa, vifaa tiba, ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Maoni yangu Hospitali ya Taifa Muhimbili ni Hospitali ya Rufaa Tanzania, wakati tunaelekea katika Mpango wa Maendeleo wa Bajeti wa mwaka 2018/2019 Serikali ijenge eneo ambalo litasaidia wananchi wanaowasindikiza wagonjwa wao kutoka katika mikoa mbalimbali Tanzania ambao hawana ndugu au jamaa Jijini Dar es Salaam, waweze kupata sehemu za kufikia baada ya kumkabidhi mgojwa wodini. Maana kuna baadhi ya wagonjwa wanahitaji huduma za karibu kutoka kwa ndugu zao ambazo wahudumu wakati mwingine ni vigumu kuzifanya. Wakati mwingine wagonjwa wanaopewa rufaa kuja Muhimbili ni watoto zaidi ya miaka 5 – 15 ambao wanahitaji huduma ya karibu ya mzazi au mlezi wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/ 2019.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa taarifa ya 2017 – 2018 Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itenge bajeti ya kutosha ili kuwezesha sekta ya utalii, maliasili na ardhi iweze kuwekeza kwa muda muafaka, hatimaye kuweza kuingizia Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe elimu ya kutosha kwa wananchi wetu ili kuweza kutunza mazingira yetu ili yasiharibike na hususan ndani ya hifadhi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iwekeze vya kutosha kutangaza vivutio tulivyonavyo nchini kwetu, si kwa mbuga za wanyama na Mlima Kilimanjaro tu bali hata vivutio vingine kama Mapango ya Amboni na kadhalika ili kuweza kuliletea pato Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge utaratibu wa kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati ili kuweza kulimaliza tatizo hili na wananchi waendelee na shughuli za uchumi na uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhakiki mashamba (makubwa) yaliyotelekezwa ili kuyabaini na Serikali kutoa ardhi hiyo kwa wananchi waliokosa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi la Wanyamapori wawe na utaratibu wa kutoa fidia kwa wananchi ambao watajeruhiwa au kuuawa na wanyamapori.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kipindi cha Januari, 2017 mpaka Januari, 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu. Ili kutekeleza kwa vitendo Maoni na Mapendekezo ya Kamati, Serikali itoe bajeti ya kutosha ili itumike kwa muda sahihi kuweza kutekeleza mambo yote yanayojadiliwa na kupendekezwa katika Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ijenge na iboreshe maghala ili kuweza kuhifadhi mazao ya nafaka sehemu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iongeze viwanda vya pembejeo za kilimo, madawa na mbolea nchini ili wakulima waweze kupata zana hizo kwa wakati na kuvitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kutoharibu vifaa vya uvuvi mfano ngalawa ambazo si zana haramu katika uvuvi; hivyo visiharibiwe.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa taarifa yake nzuri ya kipindi cha Februari, 2017 hadi Januari, 2018.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Zimamoto hususan katika Kikosi cha Zimamoto kilichopo Mkoa wa Dar es Salaam kinawalazimisha wafanyabiashara waliopo karibuni Wilaya ya Ilala kununua mitungi ya gesi (Fire extinguish) kwa lazima na kuiweka ndani ya duka la kila mfanyabiashara. Mfanyabiashara asipotekeleza hutozwa faini, badala ya mmiliki wa nyumba kununua mitungi hiyo na kuiweka pembezoni mwa jengo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza je, ikiwa moto utatokea usiku na wakati huo mfanyabiashara ameshafunga duka, amelala nyumbani kwake, je mtungi huo uliopo ndani ya duka utamsaidiaje mfanyabiashara kuokoa mali zake? Je, hatuoni kuwa huu ni mradi maalum wa Kikosi cha Zimamoto na siyo kulinda mali za wafanyabiashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu wafanyabiashara hao wanaelemewa na milolongo ya kodi nyingi na wakati mwingine kushindwa kuendesha biashara zake na kupelekea kufunga duka. Naomba Wizara husika isaidie kuondoa kero hii na kiuhalisia haina tija yoyote kwa mfanyabiashara ambaye anachangia pato la Taifa kwa kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ufinyu wa fedha hupelekea msongamano wa wafungwa magerezani na pia kuna uchakavu wa majengo ya Balozi za Tanzania. Naomba Serikali itenge fedha za kutosha na kwa wakati ili kupeleka katika Wizara husika kuondoa tatizo hilo. Mwisho nakupongeza Mheshimiwa wa Kamati Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajabu kwa taarifa yako.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naipongeza hotuba nzuri iliyotolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, naipongeza Serikali, ila nashauri kutokana na Hospitali ya Rufaa Muhimbili iliyopo Mkoa wa Dar es Salaam kupokea wagonjwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na wengi wa wagonjwa hawana ndugu Mkoa wa Dar es Salaam hivyo, naishauri Serikali ijenge eneo maalum ambalo litawasaidia ndugu waletao wagonjwa wao kuweza kukaa na kutoa huduma za dharura ambazo wauguzi hawawezi kuzifanya na itasaidia ndugu wa mgonjwa kufuatilia maendeleo ya mgonjwa wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali itafute eneo lingine la kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro maana chumba cha kuhifadhia maiti kipo karibu na Shule ya Sekondari Morogoro, hivyo kusababisha ndugu wa wafiwa wanapokuja kuchukua maiti wao hulia na kelele hizo za vilio zinasababisha wanafunzi waliopo madarasani kukosa usikivu wa kufuatilia masomo wawapo darasani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za kiuchumi, barabara zote za lami nchini zilizojengwa chini ya kiwango, mfano barabara ya Chalinze hadi Mlandizi, zifanyiwe ukarabati ili kuepusha ajali za barabarani. Barabara zilizojengwa pembezoni mwa milima, mfano Milima ya Usambara katika Mkoa wa Tanga zijengewe pavements au uoto ambao utazuia mmomonyoko wa ardhi, hususan kipindi cha mvua ambayo uharibu barabara hizo na kutopitika kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba njia ya reli ya Dar es Salaam – Tanga ikarabatiwe ili iweze kupitika na kuweza kusaidia usafirishaji wa mizigo na abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kutafuta njia mbadala ya msongamano wa magari eneo la mizani, hususan Vigwaza Mkoa wa Pwani, ukizingatia magari ya abiria yanatembea kwa ratiba maalum hivyo, husababisha usumbufu na abiria pia, hupata usumbufu kwa kusafiri kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iboreshe viwanja vya ndege. Mfano uwanja wa ndege uliopo Mkoa wa Morogoro wakati wa usiku haufanyi kazi kutokana na ukosefu wa taa uwanjani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta za uzalishaji; kilimo, wakulima wahamasishwe kulima mazao ambayo yatatumika kama malighafi katika viwanda vilivyopo nchini, mfano, kilimo cha alizeti, tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda, viwanda vipya vinavyojengwa vijengwe nje, mbali na makazi ya watu. Viwanda vinavyojengwa viwe ambavyo malighafi zake zinapatikana hapa nchini ili wakulima wetu wapate soko la kuuza bidhaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara, wafanyabiashara wakadiriwe na Mamlaka ya Mapato (TRA), kulingana na biashara wanayoifanya na si eneo wanalofanyia biashara. Mfano, maeneo ya Kariakoo katika Mkoa wa Dar es Salaam wafanyabiashara wanakadiriwa kutokana na eneo. Pia, wafanyabiashara wakati wanaanzisha biashara zao wapewe muda maalum (Grace Period) angalau wa miezi mitatu kisha ndio wafanyiwe makadirio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu; maslahi ya Walimu yaboreshwe ili wawe na utulivu wanapofundisha. Madarasa yaongezwe kuepuka msongamano wa wanafunzi katika shule zetu. Wanafunzi wapatiwe angalau mlo mmoja kwa siku wawapo shuleni.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Mbunge) pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Mbunge) kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iondoe malipo katika hospitali za Serikali kwa maiti ambazo zimehifadhi wa katika vyumba vya kuhifadhia maiti kwa kuwa wakati wa uhai wao walikuwa wanachangia Pato la Taifa kwa kulipa kodi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, watoto wote walio chini ya miaka mitano wapate huduma za afya bure kama ilivyo kwa wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, dawa za ugonjwa wa saratani ni ghali mno, hivyo nashauri Serikali ipunguze bei ya dawa hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kwa wale wagonjwa wasio na uwezo wa matibabu ya moyo hususani watoto, Serikali iweze kugharamia matibabu hayo. Kuna baadhi ya chanjo za watoto ambazo wakati wanachanjwa huwaletea homa kali sana. Nashauri Serikali ifanye maboresho kwa chanjo hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, akina mama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano waendapo kliniki kuchunguzwa afya zao nashauri Serikali itoe vyakula vya lishe kama ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya usafishaji figo ni gharama sana. Hivyo naishauri Serikali ipunguze gharama za tiba hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iweke stand by generators katika hospitali zote za Wilaya ili kuweza kusaidia wagonjwa na wauguzi umeme unapokatika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali nyingi majengo yake ni chakavu, ukarabati ufanyike katika hospitali hizo, naishauri Serikali iweke nyavu za kuzuia mbu katika wodi za Hospitali ya Muhimbili na ukarabati wa vyoo na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iboreshe miundombinu ya hospitali zetu hususani upatikanaji wa huduma ya maji katika hospitali zetu nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, madaktari na wauguzi waongezwe mishahara na posho ili waweze kufanya kazi kwa weledi na kuondoa tatizo la rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iboreshe kambi za wazee, kujenga/kukarabati nyumba zao, chakula cha kutosha na kuwapatia vifaa muhimu katika kambi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, namuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu Waheshimiwa Ummy A. Mwalimu (Waziri) na Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile (Naibu Waziri) ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika Wizara hii ambayo kimsingi
ni tegemeo la Watanzania wote hususani katika masuala ya afya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, pamoja na Naibu Mawaziri wake kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iondoe tozo, malipo kwa wananchi wa Kigamboni wanaotumia vyombo vya moto kupita katika Daraja la Kigamboni (Daraja la Nyerere), ni ghali mno na kipato cha Watanzania na hali ya uchumi ni ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakandarasi wanaojenga barabara za lami chini ya kiwango wawajibike kuzikarabati zitakapoharibika kabla ya muda maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iondoe msongamano katika mizani iliyopo Vigwaza, Mikese na Morogoro. Kwa magari ya abiria (mabasi) yawe na eneo maalum la kupima uzito maana mabasi mara nyingi huenda kwa ratiba maalum, abiria wengine ni wagonjwa, watoto na mabasi hutumia muda mwingi katika mizani hiyo. Pia nashauri barabara zote zilizopo pembezoni mwa milima zijengewe pavements ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi na ili zisiharibu miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya Dar es Salaam hadi Tanga ifufuliwe ili kuweza kusaidia mizigo mizito hususani malori kutumia reli ili kuepuka uharibifu wa barabara. Katika barabara kuu zijengwe kalvati ambazo zitakuwa na uwezo wa kuhimili wingi wa maji kipindi cha mvua za masika ili kuepuka maji kupita juu ya barabara na kuharibu miundumbinu. Mfano, barabara ya Dodoma - Morogoro eneo la Mbande hadi Kibaigwa ni eneo korofi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwanja wa ndege wa Morogoro ambao upo maeneo ya Kihonda Bima, uwanja ule uboreshwe ili ndege ziweze kutua usiku na mchana na ukizingatia Morogoro kuna Mbuga za Wanyama za Mikumi na Selous ambazo ni vivutio vikubwa vya watalii, kwa kutumia uwanja huo tutaweza kuwavutia watalii wengi kuja Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali itoe fedha kwa wakati ili kuwezesha Wizara kufanya kazi kwa muda uliopangwa kujenga miundombinu ya nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZAINABU M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu nashauri Serikali iwekeze katika mchezo wa mpira wa miguu pia isisahau kuwekeza katika michezo mingine ambayo tayari imeshiriki katika mashindano mbalimbali ndani na nje ya nchi yetu na imesajiliwa, kufuata taratibu zote za kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Roll Ball – Timu hii ya mchezo wa Roll Ball imeshindwa kushiriki kwenda kuwakilisha nchi katika nchi ya Kenya kwa sababu ya kukosa wadhamini. Hivyo Serikali ione haja ya kusaidia mchezo huu ambao utasaidia kuleta ajira pia kusaidia nchi kujitangaza Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu itolewe kwa wasanii wetu hususan wanaoimba muziki wa kizazi kipya, kuweza kutunga na kuimba nyimbo zenye maadili yanayoendana na utamaduni wa nchi yetu. Serikali itunge sheria ya kudhibiti vijana ambao wanavaa nguo fupi (nusu uchi) ambazo haziendani na maadili yetu ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali, iweke mkakati maalum wa kuhamasisha michezo mashuleni, kuanzia shule za awali, shule za msingi, sekondari hadi katika vyuo ili kuweza kuibua vipaji kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Taifa upo katika Wilaya ya Temeke, Mkoa wa Dar es Salaam, hivyo pindi mechi zinapochezwa katika uwanja huo wananchi wa Wilaya ya Temeke hawafaidiki na fedha zinazopatikana katika viingilio. Hivyo naishauri Serikali kwa kushirikiana na TFF iweze kutoa kiasi cha fedha kwa Wilaya ya Temeke ambayo itasaidia katika kuboresha miundombinu na shughuli nyingine za kijamii katika Wilaya hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mungu awape afya njema Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake ili kuweza kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Ole Nasha kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wanafunzi wawe na ufaulu wa kiwango cha juu ni lazima Serikali ifanye yafuatayo:-

(i) Iboreshe na iwaongezee walimu mishahara na posho;

(ii) Iwapandishe madaraja wale waliofundisha zaidi ya miaka mitatu;

(iii) Ijenge madarasa ya kutosha na maktaba pamoja na maabara katika shule za sekondari na shule za msingi;

(iv) Ijenge nyumba bora za walimu na ni muhimu ziwe na umeme ili walimu waweze kuandaa maazimio na maandalio ya kazi kwa masomo ambayo watayafundisha siku inayofuata darasani;

(v) Isajili shule za awali (chekechea) ili kuweza kutambulika kisheria. Pia itengeneze mitaala kwa shule hizi na ziwe na miundombinu inayolingana na uhitaji wa watoto hao wa chekechea;

(vi) Ipeleke mashuleni vitabu vya kiada na ziada kwa wakati;

(vii) Itengeneze mitaala ya sekondari inayomuandaa kijana/mwanafunzi kujiajiri. Mfano kuwe na masomo ya needle work, cookery, wood work, metal work, fine arts na kadhalika kama ilivyokuwa zamani katika shule mfano Morogoro sekondari.

(viii) Iwe na mtaala wa michezo ili kuweza kukuza vipaji kwa wanafunzi wetu;

(ix) Ijenge ofisi za walimu na kuweka samani katika ofisi hizo ili walimu waweze kuzitumia katika shughuli za kiofisi;

(x) Ijenge vyoo vya walimu na wanafunzi katika shule zetu. Mfano, katika Shule ya Msingi Yombo Dovya iliyopo Kata ya Makangarawe, Wilaya ya Temeke hakuna matundu ya vyoo vya kutosha; na

(xi) Iandae angalau mlo mmoja kwa siku katika shule zetu ili kusaidia wanafunzi waweze kuhamasika kuhudhuria masomo. Pia kupata mlo ambao utawasaidia kuwa na afya njema na kuelewa vyema masomo yao maana mwanafunzi akiwa na njaa hafundishiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namtakia Waziri wa Elimu na Naibu wake afya njema na Mwenyezi Mungu awape umri mrefu ili waweze kuyatekeleza majukumu yao ya kila siku.