Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Zainab Mndolwa Amir (11 total)

MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi napenda kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itasitisha tozo katika Daraja la Kigamboni ili liweze kutumika kama madaraja mengine yalivyo ya Ruvu na Wami?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwanza niwashukuru Waziri wa TAMISEMI na Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Kigamboni limejengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF. Ni kivuko ambacho kinafanya kazi kama vivuko vingine tulivyonavyo nchini na vivuko vingine vilivyopo nchini pia vimeweka mfumo wa utozaji wa tozo kidogo ili kuhakikisha kwamba vivuko vile vinaendelea kulindwa na vinaendelea kukarabatiwa viweze kuendelea kufanya kazi.
Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge tozo iliyowekwa kwenye Kivuko cha Kigamboni na NSSF imefuata utaratibu wa kisheria na wa kikanuni na hivyo, itaendelea kuwepo, lakini itaendelea kuwa ikibadilishwa kulingana na mazingira na taratibu za kisheria ambazo zinaongoza tozo zote katika nchi yetu ya Tanzania katika vivuko vyote nchini.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuwapatia wanafunzi hususan wa shule za msingi angalau mlo mmoja kwa siku?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini Serikali itahakikisha kwamba wanafunzi watapata angalau mlo mmoja kwa siku, naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari kuna utaratibu unaoendelea kwenye shule nyingi nchini kuhakikisha kwamba wanafunzi wanapata uji wakiwa shuleni. Hata hivyo, katika Mpango wetu wa elimu bila malipo, tayari tunafikiria kufanya maboresho ili masuala kama haya ya mlo vilevile yaweze kuchukuliwa
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Kutokana na umuhimu wa mboga za majani kwa afya ya binadamu na ukizingatia maeneo mengi ya Dar es Salaam mboga hizo hulimwa mabondeni na kipindi cha mvua kuna mafuriko yanayoharibu mboga hizo. Je, ni lini Serikali itatenga maeneo maalum ambayo wakulima hawa watalima? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia wakulima hao mikopo ambayo itasaidia kulimo kilimo chenye tija na chenye kuzingatia afya ya mlaji? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, moja ya mikakati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inawatengea wananchi, hasa wajasiriamali wakiwemo wakulima wa mbogamboga na hili linafanywa na halmashauri au manispaa husika. Kwa hiyo ni suala zima la ufuatiliaji ili kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaweza kupata maeneo sahihi ili wananchi wa Dar es Salaam waweze kunufaika na kilimo cha mbogamboga.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu suala zima la mikopo; bila ya nyezo huwezi kutoka, kuna namna bora ya kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi wetu ili waweze kupata mikopo. Hili linatokana na halmashauri husika kwa kutenga asilimia tano za vijana na akinamama, ila kubwa sasa nimwombe Mheshimiwa Mbunge kushirikiana nao kusimamia fedha hizo ili waweze kupata na ziweze kuwasaidia wakulima wetu.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu ya Tanzania kuna baadhi ya barabara za lami zimejengwa chini ya kiwango, kwa mfano barabara ya Chalinze hadi Mlandizi.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuzikarabati barabara hizi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu barabara hii imekuwa ni barabara ya siku nyingi, barabara hii ilijengwa kwa kiwango kizuri, lakini kwa sababu haikudumu kwa muda mrefu na matumizi ya barabara yameongezeka kwa maana ya kupitisha magari mengi na mizigo, kwa hiyo barabara imechakaa. Serikali inao mpango wa kuifanyia matengenezo makubwa barabara hii ili iweze kuwa imara zaidi.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tunaona jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kudhibiti suala hili la madawa ya kulevya na wakati yanapokamatwa tunaoneshwa. Je, ni kwa nini cocaine na heroin wakati zinateketezwa hatuoneshwi tunaoneshwa bangi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwamba amekiri amekuwa akiona uteketezaji wa mashamba ya bangi ambao kwa kipindi cha Januari, 2017 mpaka Disemba, 2017 takribani ekari 542 za bangi zimeteketezwa na hii ikiwa ni kazi nzuri ambayo imefanywa na mamlaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake alitaka kujua kwa nini hatuoni uteketezwaji wa madawa mengine aina ya cocaine na heroin. Kwa nature ya madawa yenyewe namna uteketezaji wake uko tofauti na utaratibu unaotumika ni utaratibu ambao kwanza kabisa utahakikisha tunalinda afya na mazingira vilevile upo utaratibu ambao mamlaka unautumia katika uteketezaji huu ambao kwa kiwango kikubwa sana haijawa rasmi kwamba inaoneshwa kila wakati, lakini ni kweli kazi kubwa imefanyika katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka ninapozungumza hivi sasa takribani kilo 196 za heroin zimeteketezwa ikiwa ni kazi nzuri ambayo inafanywa na mamlaka. Kwa hiyo, siyo kwamba kazi hii haifanyiki inafanyika lakini kwa uangalizi mkubwa sana, inahitaji pia kuangalia na athari za mazingira.

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu lake sahihi na niunge mkono kwamba ni kweli madawa mengine yanateketezwa kwa uangalifu sana kwa sababu hata bangi tu nilienda kuteketeza nilipotoka pale ilibidi niende kwa Daktari kuangalia kama haijaniingia na Daktari aliniambia sijavuta. (Kicheko)
MHE. ZAINABU M. AMIRI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na kugundulika kwa gesi nchini mwetu, je, ni lini Serikali itasitisha uingizaji wa gesi ili tuweze kutumia gesi yetu hapa nchini?
(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pilot project iliyofanyika ni Mikocheni Dar es Salaam, je, ni vigezo gani vimezingatiwa katika project hiyo na isiwe kule ilikotoka gesi Mtwara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zainabu Mndolwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameuliza ni lini Serikali itasitisha uagizaji wa gesi kutoka nje ya nchi. Ni kweli ugunduzi wa gesi asilia iliyogunduliwa hapa nchini ni gesi zaidi ya mita za ujazo trilioni 55,000. Nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge matumizi ya gesi yapo mengi kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi ikiwemo kwenye uzalishaji wa umeme, matumizi ya viwanda na matumizi ya majumbani.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna mipango mbalimbali ambayo inafanywa na Serikali ikiwemo pia ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi asilia Mkoani Lindi. Kwa hiyo, baada ya kiwanda hiki kukamilika na hizi fursa mbalimbali za usambazaji gesi na miundombinu mbalimbali ya kusambaza gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani itakapokamilika, Serikali itatafakari kwa kina namna ambavyo inaweza kusitisha uagizaji wa gesi hiyo nchini. Kwa sasa bado tuna mahitaji na kwa kuwa mipango inaendelea, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itatafakari na kuchukua hatua pale ambapo tutakuwa tumejiridhisha na soko na uhitaji wa gesi asilia ndani ya nchi na kwa matumizi ya nchi. (Makofi)
Mheshimwia Spika, swali lake la pili alikuwa anauliza kuhusu vigezo vilivyotumika kwa maeneo ya kusambaza gesi kwa matumizi ya majumbani na ameuainisha Mkoa wa Mtwara. Nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kuna miradi na tafiti zinazoendelea katika Mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Morogoro, Dodoma, Mwanza na Tanga chini ya Mradi wa JICA ili kuona mahitaji ya matumizi ya gesi ya kupikia ili kuanza mradi wa usambazaji wa gesi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, nimthibitishie katika Mkoa wa Mtwara kwa mwaka huu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 140 zimetengwa kuendelea na study hiyo na kwamba mkoa huo utapatiwa usambazaji wa gesi kwa matumizi ya nyumbani. Nakushukuru.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti hovyo ikiwemo matumizi ya nguzo za umeme za miti. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kutumia nguzo za chuma badala ya nguzo za miti katika kusambaza umeme vijijini na mijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mndolwa. Ni kweli kuna mpango huo wa kuhama kutoka kwenye matumizi ya nguzo zinazotokana na miti, na kwenda nguzo zinazotokana na zege.
Mheshimiwa Spika, kwanza Shirika letu la TANESCO limeunda kampuni tanzu kwa ajili ya kuzalisha nguzo za zege. Pili kama Wizara pia tumehamasisha wadau wa ndani kuanzisha viwanda vya kutengeneza nguzo za zege na tayari kuna viwanda Bagamoyo, Kibaha na Mbeya na hiki nilikitembelea.
Mheshimiwa Spika, kinachofuata sasa ni taratibu za manunuzi, tumewaelekeza TANESCO kwamba miradi inayoendelea ya umeme vijijini kupitia REA na kupitia hata miradi yao, tuanze kuhama kutoka kwenye nguzo hizi za miti ambazo zinadumu kwa muda mfupi sana ndani ya miaka mitano, sita wakati hizi nguzo za zege zinaweza kudumu zaidi ya miaka 20 na kuendelea. Kwa hiyo, ni wazi tutakapotimiza azma yetu ya kutumia nguzo za zege tuta-save pesa nyingi zinazotumika kwenye ukarabati wa nguzo hizi za kawaida ambazo zinachukua muda mfupi na zinaoza. Nakushukuru.
MHE. ZAINABU AMIR MNDOLWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara itaokayo Korogwe kupitia Kwa Mndolwa - Mkaalie - Tamota hadi kuunganishwa na Kiwanda cha Chai Mponde ni takribani kilometa 40 lakini haijajengwa kwa kiwango cha lami. Hii ni barabara muhimu sana katika nchi kwa sababu mazao mengi kutoka Jimbo la Bumbuli ambayo yanasafirishwa kwenda Dar es Salaam hupita pale, lakini wakati wa mvua barabara hii haipitiki kabisa na kuna maporomoko ya mawe:-

Je, ni lini sasa Serikari itajenga hii kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza kuendelea kuwasema wananchi wa Korogwe, lakini namwomba sana kwa sababu tupo kwenye wakati wa bajeti hii aunge mkono bajeti ya TAMISEMI Jumatatu tutakapofika kwa majaliwa ya Mwenyenzi Mungu tupate fedha hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilijibu swali hapa nikasema, tuliunda timu ya wataalam, inapitia sasa namna ya ku-identify hizi barabara ili tuangalie ule Mfuko wa TANROADS na TARURA. Nimesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge kwamba TARURA inafanya kazi nzuri sana. Shida hapa ni fedha. Tukipata chanzo realible cha fedha na formula ambayo ipo sawaswa na wadau mbalimbali na bajeti ikaungwa mkono. Nia ya Serikali ni kukamilisha barabara zote ikiwezekana kwa kiwango cha lami ikiwepo hiyo ya Korogwe. Ahsante.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Hospitali ya rufaa ya Temeke haina mashine ya kufulia nguo, hadi kupelekea mashuka ya wagonjwa kupelekwa katika Hospitali ya Muhimbili ili kuweza kufuliwa. Je, Serikali itapeleka lini mashine ya kufulia nguo katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na Hospitali ya Rufaa ya Temeke kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyojua Hospitali yetu ya Rufaa ya Temeke inamashine ya kufulia, inawezekana katika kipindi hiki cha karibuni imeharibika na niombe tu baada ya kikao hiki cha Bunge nitafuatilia. Vile vile tumekuwa na utaratibu mbadala katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Muhimbili ina mashine kubwa za kuweza kufulia na mara nyingi katika Hospitali za Rufaa za Mikoa katika Mkoa wa Dar es Salaam wanapopata tatizo basi huwa tunatumia Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kama mbadala. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya kikao nitafuatilia kuhakikisha mashine hiyo inafanya kazi.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina maswali madogo ya nyongeza; kuna baadhi ya watu wanajenga katika mabonde na wengine wanajenga katika hifadhi za barabara na pia karibu kabisa na njia za reli lakini Serikali yetu kupitia halmashauri zetu kila mwaka hukusanya kodi za majengo na kodi za ardhi katika maeneo hayo. Je, Serikali inatueleza nini kuhusu kadhia hii?

Mheshimiwa Spika, Swali langu la pili ili mwananchi aweze kujenga katika eneo husika ni lazima apate kibali kutoka katika mamlaka na sasa nauliza swali langu. Je, ni nini adhabu ambazo wanapewa watendaji ambao wanatoa vibali katika maeneo ambayo ni hatarishi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli wako watu ambao wamejenga katika hifadhi za barabara, hifadhi za miundombinu mbalimbali na mabondeni lakini wamefanya hivyo kinyume cha sheria na Serikali hairuhusu na hata zoezi la urasimishaji na utoaji wa leseni za makazi hautafanyika wala hatutarasimisha makazi kwa watu ambao wamejenga katika maeneo hatarishi na maeneo ambayo yamepangwa na wapangamiji kama maeneo ya hifadhi ya barabara au maeneo ya miundombinu. Kwa hilo nakiri ni kosa wako watu wamefanya namna hiyo na sheria lazima ichukue mkondo wake kwa sababu ya kuwasaidia wao lakini kusaidia maendeleo ya miji yetu.

Mheshimiwa Spika, pia ni kweli kwamba kodi inakusanywa kwa sababu hawa watu lazima walipe kodi, kuishi kwao kule wanatumia rasilimali za Halmashauri husika, kwa hiyo halmashauri zile zinapaswa kuwatoza kodi katika maeneo yale kwa sababu na wenyewe wanatumia rasilimali na infrastructure zilizoko kule lazima wachangie, Hilo linafanyika na ni kweli lazima watoe kodi, lakini ujenzi katika maeneo hayo hairuhusiwi. Kwa hiyo huwezi kujenga tu eti kwa sababu unataka kukaa mabondeni halafu usitozwe kodi kama wanavyotozwa Watanzania wengine. Ni kweli kodi za majengo zitatozwa na kodi mbalimbali za halmashauri wanazotoza raia wengine zitazozwa, lakini hiyo haihalalishi kwamba wewe hapo umekaa kihalali. Lolote likitokea linaweza likatokea kama wapangaji na halmashauri husika wakiamua kuchukua hatua za kisheria.

Mheshimiwa Spika, la pili vibali vya ujenzi zamani vilikuwa vinatolewa zamani vilikuwa vinatolewa na Kamati ya Mipangomiji ya Madiwani lakini sasa utaratibu Serikali ya Awamu ya Tano imebadilisha kwa sababu ilikuwa inachelewesha sana na ilikuwa inachukua gharama kubwa sana, inamaliza hela nyingi kwa ajili ya posho ya vikao na kila kitu. Sasa hivi iko timu ya wataalam tu wa Serikali ambao ndiyo wanatoa vibali vya ujenzi na tumesema vibali visichukue zaidi ya siku tatu viwe vimeshatoka, kwa sababu watu wako pale wana uwezo wa kwenda kufanya ukaguzi na ni wataalam waliobobea katika kazi hiyo na vibali vya ujenzi lazima zitolewe. Kwa hiyo vibali sasa vinatolewa kwa kasi na hii imesababisha kupunguza hata gharama kwa wananchi za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ni kweli kwamba siku za nyuma ilionekana kwamba watu waliweza kutoa vibali hata kwa watu ambao wametakiwa kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa. Serikali kwa wakati tofauti imechukua hatua kali na wengine wameachishwa kazi kwa wale ambao wametoa vibali katika maeneo ambayo hayastahili. Kwa hiyo Serikali imekuwa inachukua hatua za kinidhamu mara kwa mara, lakini nataka kumhakikishia katika Awamu hii ya Tano hilo halifanyiki. Awamu ya Tano imejenga nidhamu tofauti, watu ni wale wale lakini nidhamu yao imekuwa tofauti, hawatoi vibali tena hovyo hovyo na hawatatoa tena vibali katika maeneo ambayo ni hatarishi.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna baadhi ya maeneo tunaona kwamba kuna upanuzi wa barabara nikitolea mfano barabara ya Dodoma mpaka Morogoro, maeneo ya Gairo na maeneo ya Dumila. Je, ni hatua zipi zinazochukuliwa sasa kwa wale wakandarasi ambao kazi zao hazikukidhi viwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunaendelea kupanua barabara maeneo mbalimbali. Kama nilivyozungumza jana hapa ni kwamba asilimia 90 ya fedha zinazokwenda kwenye ujenzi wa barabara ni kwa ajili ya matengenezo, kwa hiyo, zoezi linaloendelea nchi nzima kufanya maboresho ya barabara ni la kawaida kwa sababu barabara zinavyotumika zinachakaa na saa nyingine kutokana na umri, kutokana na hali ya hewa na mambo mbalimbali, kwa hiyo, matengenezo hayo ni muhimu yanaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niseme tu kwamba upanuzi huu wa barabara au kazi zinazoendelea barabarani ni kwa mujibu wa mikataba ambayo ipo na mikataba imezingatia specifications za kitaalam na mikataba pia imeweka masharti ya pande zote mbili, upande wa sisi Serikali, lakini upande wa mkandarasi na ziko hatua ambazo zinachukuliwa, tunacho chombo ambacho kinawasimamia wakandarasi, tuna Contractors Registration Board na lakini pia kuna ERB yaani Engineers Registration Board ambayo hawa wanafuatilia miradi mbalimbali kukagua kuona kama shughuli hizi zinaenda vizuri, lakini kwa kuzingatia pia mikataba.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo idadi ya makandarasi ambao wamechukuliwa hatua, wapo ambao amesimamishwa kwa muda, wapo ambao wamefutiwa usajili wao na tutaendelea kuchukua hatua kwa mtu ambaye anakiuka taratibu za ujenzi.

Kwa hiyo, nikuhakikishie tu na Bunge lako kwamba, sisi Serikali tuko makini kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika kufuatana na mikataba iliyokuwepo, kufuatana na taratibu zilizokuwepo, ili kuhakikisha kwamba kazi ambazo tumeziweka kwa ajili ya ukarabati au ujenzi zinakamilika, lengo ni wananchi waweze kupata huduma nzuri na kwa haraka inavyowezekana.