Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Godfrey William Mgimwa (4 total)

Kuwawezesha Wananchi Kupata Umeme wa Bei Nafuu
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-
Licha ya Serikali kupeleka umeme vijijini kwa kasi kupitia mradi wa REA, bado kuna changamoto za kuunganisha umeme kwa wananchi.
(a) Je, Serikali ina mpango gani kuwawezesha wananchi kupata umeme kwa bei nafuu?
(b) Nguzo za umeme zinasimikwa kwenye njia kuu tu; je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha nguzo hizi zinapelekwa kwenye vitongoji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwezesha wananchi kupata umeme kwa gharama nafuu, Serikali kupitia mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini (REA) inaunganisha umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu na hii ikiwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) imepunguza gharama za umeme kwa kuondoa gharama za malipo ya maombi ya kufungiwa umeme yaani shilingi 5,000 pamoja na malipo ya huduma ya kila mwezi (service charge) ambayo ni shilingi 5,520 kwa wateja wote wa majumbani; hatua hii imeanza tangu tarehe 1 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo vya gesi asilia, joto-ardhi, jua, maji na makaa ya mawe pamoja na tungamotaka, ili kupunguza gharama za umeme zaidi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, nguzo nyingi zimesimikwa kwenye njia kuu, hata hivyo katika Mpango wa REA Awamu ya Tatu utakaoanza bada ya bajeti yetu kupita mwezi Julai mwaka huu, maeneo mengi ya vitongoji yatafikiwa kwa kupewa huduma ya umeme, ili kurahisisha shughuli za uchumi za wananchi wa maeneo ya Kalenga.
MHE. GODFREY W. MGIMWA aliuliza:-
Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa.
Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning‟ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua ukubwa wa tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga. Kwa kulitambua hilo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iliainisha vijiiji vya Kata ya Wasa kikiwemo kijiji cha Ikungwe na kuviingiza katika Mradi wa Awamu ya Kwanza (A). Mradi huu unatekelezwa na Kampuni ya Simu ya TTCL kwa ruzuku ya dola za Kimarekani 107,968 ambapo mpaka sasa mnara tayari umeshajengwa. TTCL itaanza kutoa huduma za mawasiliano huko Kalenga mwishoni mwa mwezi Juni, 2016 baada ya kukamilisha ufungaji wa vifaa vya mawasiliano katika mnara uliojengwa.
Aidha, vijiji vya Igunda na Lyamgungwe kutoka katika Kata ya Lyamgungwe vimeingizwa katika utekelezaji wa miradi ya mawasialiano ya Viettel katika awamu ya pili na awamu ya tatu iliyoanza Novemba, 2015 na kutarajiwa kukamilika Novemba, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kijiji cha Kaning‟ombe katika kata ya Mseke na kijiji cha Ikuvilo katika kata ya Luhota vitaingizwa katika miradi ya mwaka wa fedha 2016/2017 kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. GODFREY W. MGIMWA Aliuliza:-
Tatizo la mawasiliano ya simu katika Jimbo la Kalenga bado ni kubwa:-
Je, ni lini Serikali itapeleka minara ya simu kwenye vijiji vya Kaning’ombe, Ikungwe, Lyamgungwe, Igunda na Ikuvilo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote iliainisha maeneo mbalimbali katika Jimbo la Kalenga na kuyaingiza katika miradi mbalimbali ya utekelezaji. Vijiji vya Igunda na Lyamgungwe kutoka katika Kata ya Lyamgungwe vimo katika utekelezaji wa mradi wa Viettel. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 2017. Aidha, Vijiji vya Ikungwe na Kaning’ombe vimeingizwa katika orodha ya miradi inayosubiri fedha ili kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y. MHE. GODFREY MGIMWA) aliuliza:-
Tatizo la umeme bado ni kubwa licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali.
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili na hatimaye kuvipatia umeme Vijiji vya Kipera, Lupalama, Itagutwa na Lyamgungwe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali Mheshimiwa Godfrey William Mgimwa, Mbunge wa Kalenga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatarajia kuvipatia umeme Vijiji vya Kipela, Lupalama, Itagutwa, Ikongwe na Lyamgungwe katika Awamu ya Tatu ya uetekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA III) inayoendelea kwa sasa. Aidha, kwa Mkoa wa Iringa miradi hiyo inatekelezwa na mkandarasi Kampuni ya Sengerema Engineering Group na tayari yupo katika eneo (site) akifanya upimaji wa awali kwenye vijiji tajwa pamoja na vijiji vingine 145 vya Mkoa wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo tajwa inajumuisha ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kilovolti 33 na 11 zenye urefu wa kilometa 22; msongo wa kilovolti 0.4 yenye urefu wa kilometa 18; na uwekaji wa transfoma tisa pamoja na kuwaunganisha umeme wateja 215. Gharama ya kutekeleza miradi hiyo ni jumla ya shilingi bilioni 2.3.